Sura 4 · dakika 6 za kusoma

Unyenyekevu Katika Mafundisho ya Yesu

“Mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo” Mathayo 11:29. “Na mtu atakaye kuwa wa kwanza kwenu, na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika” Mathayo 20:27.

Tumeuona unyenyekevu katika maisha ya Kristo; basi, kwa kuwa ameufunua moyo wake kwetu, na tuyasikilize mafundisho yake. Hapo tutasikia jinsi anenavyo juu yake, na kadiri gani anatarajia wanadamu, na hasa wanafunzi wake, kuwa wanyenyekevu kama alivyokuwa. Na tuyachunguze kwa uangalifu mafungu haya, ambayo siwezi kufanya zaidi ya kuyanukuu, ili tupate kuvutiwa kikamilifu na jinsi alivyoyafundisha mara nyingi na kwa bidii. Hili litatusaidia kutambua atakalo kwetu.

Tazama mwanzo wa huduma yake. Katika Heri ambazo kwazo Mahubiri ya Mlimani hufunguliwa, anena: “Heri walio maskini wa roho; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri wenye upole; maana hao watairithi nchi.” (Mathayo 5:3, 5). Maneno ya kwanza kabisa ya tangazo lake la ufalme wa mbinguni yalifunua lango wazi ambalo kwalo peke yake twaingia.

Maskini, ambao wameacha kila kitu kwa ajili ya Kristo, kwao ufalme huja. Mtu aweza kusema: “Lakini baadhi ya Wakristo ni matajiri kweli, wana ardhi, magari, na biashara nyingi.”

Naam, laweza kuwezekana kabisa, hasa wakiwa watoto wa Aliye Juu Sana; lakini wakiihesabu kuwa ubatili, waweza kwa urahisi kuitoa kwa ajili ya injili; wao ni maskini wa Roho. Wenye upole, wasiojitafutia kitu ndani yao, nchi itakuwa yao. Baraka za mbinguni na za duniani ni za wanyenyekevu.

Kwa maisha ya mbinguni na ya duniani, unyenyekevu ndiyo siri ya baraka.

“Mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.” (Mathayo 11:29). Yesu hujitoa mwenyewe kuwa Mwalimu. Huieleza roho ile tutakayoikuta ndani yake akiwa Mwalimu, na tuwezayo kujifunza na kuipokea kwake. Upole na unyenyekevu ndicho kitu kimoja atupacho, na ndani yake tutapata raha kamili ya nafsi.

Katika Agano Jipya, twawaona wanafunzi wakibishana ni nani mkuu katika ufalme, nao wakakubaliana kumwuliza Bwana wao (Luka 9:46, Mathayo 18:3-5). Akaweka mtoto katikati yao, akasema, “Ye yote ajinyenyekeshaye kama mtoto huyu, atakwezwa.” “Ni nani aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni?” Mathayo 18:1. Swali hilo kwa kweli ni la kufikia mbali. Nini kitakuwa tofauti kuu katika ufalme wa mbinguni? Jibu, hakuna ila Yesu angelitoa. Utukufu mkuu wa mbinguni, nia ya kweli ya mbinguni, neema kuu kuliko zote, ni unyenyekevu. “Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu, anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi, ampokea yeye aliyenituma.

Kwa kuwa aliye mdogo kwenu nyote ndiye aliye mkubwa.” Luka 9:48 .

Wana wa Zebedayo walikuwa wamemwuliza Yesu ni nani atakayeketi mkono wake wa kuume na wa kushoto, mahali pa juu kabisa katika ufalme. Yesu akasema si kwake kutoa, bali ni kwa Baba, atakayewapa waliowekewa tayari. Hawana budi kutokutazamia wala kuomba hivyo. Fikira yao yapaswa kuwa juu ya kikombe na ubatizo wa kufedheheshwa. Ndipo akaongeza , “Na mtu atakaye kuwa wa kwanza kwenu, na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika” Mathayo 20:27 . Unyenyekevu, ukiwa alama ya Kristo aliye wa mbinguni, utakuwa kipimo pekee cha utukufu mbinguni. Aliye mnyenyekevu zaidi ndiye aliye karibu zaidi na Mungu.

Ukuu Kanisani umeahidiwa kwa aliye mnyenyekevu kuliko wote. Akinena na makutano na wanafunzi juu ya Mafarisayo na kupenda kwao viti vya mbele, Kristo alisema tena (Mathayo 23:11), “Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu.” Kufedheheshwa ndiyo ngazi pekee ya heshima katika ufalme wa Mungu.

Wakati mwingine, katika nyumba ya Farisayo, alinena mfano wa mgeni ambaye angealikwa kupanda juu zaidi (Luka 14:1-11), akaongeza, “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajinyenyekeshaye atakwezwa.” Luka 14:11. Dai hilo halikwepeki; hakuna njia nyingine. Ni kujishusha peke yake kutakakokwezwa.

Baada ya mfano wa Farisayo na Mtoza ushuru, Kristo alinena tena (Luka 18:14), “Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajinyenyekeshaye atakwezwa.” Katika hekalu na mbele za Mungu na katika ibada yake, kila kitu hakina thamani kisipojaa unyenyekevu wa ndani na wa kweli kwa Mungu na wanadamu.

Baada ya kuwatawadha wanafunzi miguu, Yesu alisema (Yohana 13:14), “Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.” Mamlaka ya amri na ya mfano, kila wazo la utii au la kufuata, huufanya unyenyekevu kipengele cha kwanza na cha lazima kabisa cha uanafunzi. Mezani pa Chakula Kitakatifu, wanafunzi walikuwa bado wakibishana ni nani mkuu (Luka 22:26). Yesu akasema, “Aliye mkuu kwenu na awe kama aliye mdogo; naye aliye kiongozi na awe kama yule atumikaye. Mimi kati yenu ni kama atumikaye.”

Njia aliyoiendea Yesu, na aliyotufungulia, nguvu na roho ambayo kwayo aliufanya wokovu wetu na kwayo hutuokoa, ni daima ule unyenyekevu unifanyao mtumishi wa wote. Hili linahubiriwa kidogo kiasi gani! Linatendwa kidogo kiasi gani! Upungufu wake unahisiwa au kuungamwa kidogo kiasi gani! Sisemi ni wachache kiasi gani waufikiao, kwa kipimo fulani cha kufanana na Yesu katika unyenyekevu wake. Bali ni wachache kiasi gani wafikiriao kuufanya kuwa shabaha ya wazi ya shauku au maombi ya daima. Ulimwengu umeuona kidogo kiasi gani. Umeonekana kidogo kiasi gani hata ndani ya duara la ndani la Kanisa? “Aliye mkuu kwenu na awe kama aliye mdogo; naye aliye kiongozi na awe kama yule atumikaye.” Sote twajua hulka ya mtumishi mwaminifu au mtumwa yamaanisha nini: kujitoa kwa mambo ya bwana wake, kuchunguza kwa fikira na kujali ili kumpendeza, kufurahia kufanikiwa kwake, heshima yake na furaha yake. Wako watumishi duniani ambao hulka hizi zimeonekana ndani yao, ambao kwao jina la mtumishi halijapata kuwa kitu ila utukufu.

Ni kwa wangapi kati yetu ambao haijakuwa furaha mpya katika maisha ya Kikristo kujua kwamba twaweza kujitoa kuwa watumishi, watumwa wa Mungu, na kukuta kwamba utumishi wake ndio uhuru wetu ulio juu kabisa? Uhuru kutoka dhambi na nafsi? Sasa twahitaji kujifunza funzo jingine: kwamba Yesu hutuita tuwe watumishi wa mmoja na mwenzake, na kwamba, tukiukubali kwa moyo, utumishi huu pia utakuwa uliobarikiwa mno, uhuru mpya na mkamilifu zaidi kutoka dhambi na nafsi.

Mwanzoni, laweza kuonekana gumu, lakini ni kwa sababu tu ya kiburi kijihesabucho bado kuwa kitu.

Tukishajifunza mara moja kwamba kutokuwa kitu mbele za Mungu ndio utukufu wa kiumbe, ndiyo roho ya Yesu, ndiyo furaha ya mbinguni, tutaikaribisha kwa moyo wetu wote ile nidhamu tuwezayo kuipata katika kuwatumikia hata wale wanaotaka kutuudhi. Moyo wetu ukishakaza juu ya hili, ndio utakaso wa kweli, tutalichunguza kwa hamu mpya kila neno la Yesu juu ya kujishusha, wala hapatakuwa mahali palipo chini mno, wala kuinama kulikokithiri, wala utumishi ulio duni mno au wa muda mrefu mno, ikiwa tu twaweza kushiriki na kuthibitisha ushirika naye aliyesema, “Mimi kati yenu ni kama atumikaye.” (Luka 22:27).

Ndugu, hii hapa njia ya maisha ya juu zaidi. Chini, chini zaidi! Hili ndilo Yesu aliwaambia daima wanafunzi waliowaza kuwa wakuu katika ufalme, na kuketi mkono wake wa kuume na wa kushoto. Msitafute wala msiombe kukwezwa; hiyo ni kazi ya Mungu. Angalieni mwe na msingi na kujinyenyekesha, wala msichukue nafasi mbele za Mungu au mwanadamu ila ile ya mtumishi; hiyo ndiyo kazi yenu; hilo na liwe kusudi lenu moja na ombi lenu. Mungu ni mwaminifu. Kama vile maji yatafutavyo daima na kupajaza mahali palipo chini kabisa, ndivyo mara Mungu akikikuta kiumbe kimeshushwa na kitupu, utukufu na nguvu zake hutiririka ndani ili kukikweza na kukibariki. Ajinyenyekeshaye, hiyo lazima iwe tunza yetu moja, atakwezwa; hiyo ni tunza ya Mungu; kwa uweza wake mkuu na upendo wake mkuu atalifanya.

Watu husema mara nyingine kana kwamba unyenyekevu na upole vingetunyang’anya kilicho bora, chenye ujasiri na cha kiume. Laiti wote wangeamini kwamba huu ndio ubora wa ufalme wa mbinguni, kwamba hii ndiyo roho ya kifalme aliyoidhihirisha Mfalme wa mbinguni, kwamba huku ndiko kufanana na Mungu: kujinyenyekesha, kuwa mtumishi wa wote! Hii ndiyo njia ya furaha na utukufu wa uwepo wa Kristo daima ndani yetu, na nguvu zake zikitukalia daima. Yesu, yule mpole na mnyenyekevu, hutuita tujifunze kwake njia ya kumfikia Mungu.

Na tuyachunguze maneno tuliyokuwa tukiyasoma hata moyo wetu ujae wazo hili: Hitaji langu moja ni unyenyekevu. Na tuamini kwamba akionyeshacho hukitoa; alicho, hukishirikisha. Akiwa yule mpole na mnyenyekevu, ataingia na kukaa katika moyo utamanio.

Ukurasa 1 / 5 · 6 dakika zimebaki katika sura