Sura 2 · dakika 7 za kusoma
Siri ya Ukombozi
Kuweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu, ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu. Tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina, “Wafilipi 2:5-9.
Hakuna mti uwezao kukua ila juu ya mzizi ulioumea. Katika kuwako kwake kote, waweza kuishi tu kwa uzima uliokuwamo katika mbegu iliyoutokeza. Kuifahamu kweli hii kikamilifu, katika utumizi wake kwa Adamu wa kwanza na Adamu wa Pili, kwatusaidia kuelewa hitaji na asili ya ukombozi ulio ndani ya Yesu. Yule Nyoka wa Zamani, aliyetupwa nje ya mbinguni kwa ajili ya kiburi chake, ambaye asili yake yote akiwa ibilisi ilikuwa kiburi, aliponena maneno yake ya kishawishi sikioni mwa Hawa, maneno hayo yalichukua nayo sumu yenyewe ya jehanamu.
Aliposikiliza, akaitoa shauku yake na mapenzi yake kwa tumaini la kuwa kama Mungu, akijua mema na mabaya, sumu ile iliingia nafsini mwake, damuni mwake, na uzimani mwake, ikiuharibu milele ule unyenyekevu uliobarikiwa na kumtegemea Mungu ambako kungalikuwa furaha yetu ya milele. Kwa hiyo maisha yake na ya jamii iliyotoka kwake yakaharibika hata mzizi kwa kiburi chake Shetani, dhambi na laana mbaya kuliko zote.
Taabu yote ambayo ulimwengu huu umekuwa uwanja wake, vita vyake vyote na damu kumwagwa kati ya mataifa, ubinafsi wake na mateso, tamaa zake na wivu, mioyo iliyovunjika na maisha yaliyotiwa uchungu, pamoja na huzuni yake ya kila siku, vyote vyatokana na kile kiburi hiki cha laana, cha kijehanamu, chetu au cha wengine, kilichotuletea. Ni kiburi kifanyacho ukombozi kuwa wa lazima; ni kutoka kiburi chetu tunachohitaji kukombolewa. Ufahamu wetu wa hitaji hilo wategemea sana maarifa ya asili ya kutisha ya nguvu iliyoingia ndani yetu. Nguvu Shetani aliyoileta kutoka jehanamu na kuitupa katika maisha ya mwanadamu inatenda kazi kila siku, kila saa, kwa uweza mkuu duniani kote. Watu huteswa nayo, huiogopa, huipiga vita na kuikimbia, lakini hawajui ijapo, wala iwapo na ukuu wake wa kutisha.
Si ajabu hawajui wapi wala jinsi gani kinaweza kushindwa. Kiburi kina mzizi na nguvu zake katika uwezo wa kiroho wa kutisha, ulio nje yetu na pia ndani yetu; kama ilivyo lazima tukiungame na kukililia kuwa ni chetu wenyewe, lazima pia tukijue katika chanzo chake cha kishetani. Kama hili likitupeleka kwenye kukata tamaa kabisa juu ya kukishinda au kukitupa nje, litatupeleka upesi zaidi kwenye ile nguvu ipitayo asili ambamo peke yake ukombozi wetu wapatikana: ukombozi wa Mwana-Kondoo wa Mungu. Vita visivyo na tumaini dhidi ya utendaji wa nafsi na kiburi ndani yetu vyaweza kuzidi kukosa tumaini tufikiriapo nguvu ya giza iliyo nyuma ya yote; lakini kukata tamaa huko kutatuandaa vema zaidi kutambua na kukubali nguvu na uzima ulio nje yetu pia, naam, unyenyekevu wa mbinguni ulioshushwa na kuletwa karibu na Mwana-Kondoo wa Mungu, ili kumtupa nje Shetani na kiburi chake.
Hakuna mti ukuao ila juu ya mzizi ulioumea. Kama tunavyohitaji kumwangalia Adamu wa kwanza na anguko lake ili tujue nguvu ya dhambi ndani yetu, ndivyo tunavyohitaji kumjua Adamu wa Pili na uweza wake wa kutoa ndani yetu uzima wa unyenyekevu ulio halisi, udumuo na utawalao kama ulivyokuwa wa kiburi. Uzima wetu watoka kwa Kristo na umo ndani yake, kwa kweli, naam, kwa kweli zaidi, kuliko kwa Adamu. Twapaswa kwenda “tukiwa wenye shina na mzizi ndani yake,” tukishikamana na Kichwa ambaye kwa yeye mwili wote hukua kwa maongeo ya Mungu.
Uzima wa Mungu, ulioingia katika asili ya kibinadamu kwa kufanyika mwili, ndio mzizi ambamo twapaswa kusimama na kukua; ni uweza ule ule wa Mwenyezi uliotenda kazi hapo, na tangu hapo hata ufufuo, ndio utendao kazi ndani yetu kila siku. Hitaji letu moja ni kujifunza, kujua, na kuutumaini uzima uliofunuliwa katika Kristo kuwa ndio uzima wetu sasa, nao wangoja kibali chetu ili uumiliki na kuutawala utu wetu wote.
Kwa hili, ni jambo la umuhimu usioelezeka kuwa na mawazo sahihi juu ya Kristo alivyo, juu ya kimfanyacho kuwa Kristo, na hasa juu ya kiwezacho kuhesabiwa sifa yake kuu, mzizi na kiini cha hulka yake yote akiwa Mkombozi wetu. Jibu ni moja tu: unyenyekevu wake. Kufanyika mwili ni nini ila unyenyekevu wake wa mbinguni, kujifanya kuwa hana utukufu na kuwa mwanadamu? Maisha yake duniani ni nini ila unyenyekevu, kutwaa namna ya mtumwa? Na upatanisho wake ni nini ila unyenyekevu? “Alijinyenyekeza akawa mtii” (Wafilipi 2:8). Na kupaa na utukufu wake ni nini ila unyenyekevu uliokwezwa kitini cha enzi na kuvikwa taji ya utukufu? “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno” (Wafilipi 2:9). Mbinguni pamoja na Baba, katika kuzaliwa kwake, maisha yake, mauti yake, na kuketi kwake kitini cha enzi, yote si kitu ila unyenyekevu.
Kristo ni unyenyekevu wa Mungu uliovaa asili ya kibinadamu, Upendo wa Milele ukijinyenyekeza, ukijivika vazi la upole na wema ili kutushinda, kututumikia, na kutuokoa. Kama upendo na kujishusha kwa Mungu kumfanyavyo mtenda wema, msaidizi, na mtumishi wa wote, ndivyo Yesu kwa lazima alivyokuwa Unyenyekevu uliofanyika mwili. Hivyo, angali katikati ya kiti cha enzi, Mwana-Kondoo wa Mungu mpole na mnyenyekevu. Kama huu ndio mzizi wa mti, asili yake lazima ionekane katika kila tawi, jani, na tunda.
Kama unyenyekevu ndio neema ya kwanza, ijumuishayo yote, ya maisha ya Yesu, kama ndiyo siri ya upatanisho wake, basi afya na nguvu za maisha yetu ya kiroho zitategemea kabisa kuiweka neema hii kwanza sisi pia, na kuufanya unyenyekevu jambo kuu tulistaajabialo ndani yake, jambo kuu tuliombalo kwake, jambo moja tudhabihulo mengine yote kwa ajili yake. Je, ni ajabu kwamba maisha ya Kikristo mara nyingi ni dhaifu na yasiyozaa matunda, wakati mzizi wenyewe wa uzima wa Kristo umepuuzwa, haujulikani? Je, ni ajabu kwamba furaha ya wokovu inahisiwa kidogo hivyo, wakati kile Kristo alichokipata na kukileta kinatafutwa kidogo hivyo? Hata unyenyekevu utakaokaa katika mwisho na mauti ya nafsi, uachao heshima yote ya wanadamu kama Yesu alivyofanya ili kutafuta heshima itokayo kwa Mungu peke yake, ujihesabuo kuwa si kitu kabisa, ili Mungu awe yote, ili Bwana peke yake atukuzwe, hata unyenyekevu wa namna hiyo uwe ndicho tukitafutacho ndani ya Kristo kuliko furaha yetu kuu, na tukikaribishe kwa gharama yoyote, kuna tumaini dogo sana la dini itakayoushinda ulimwengu.
Siwezi kumsihi msomaji wangu kwa bidii kupita kiasi, ikiwa huenda uangalifu wake haujawahi kuelekezwa hasa kwenye upungufu wa unyenyekevu ulio ndani yake au unaomzunguka, kwamba asimame na kujiuliza kama anaiona sana roho ya Mwana-Kondoo wa Mungu aliye mpole na mnyenyekevu ndani ya wale waitwao kwa jina lake.
Na afikiri jinsi ukosefu wote wa upendo, kutojali mahitaji, hisia na udhaifu wa wengine, hukumu na maneno yote makali na ya haraka, yanayotetewa mara nyingi kwa kisingizio cha uwazi na ukweli.
Madhihirisho yote ya hasira, uchokozi na ukero, hisia zote za uchungu na kutengana, vyote vina mzizi katika kiburi kijitafutacho chenyewe daima. Macho yake yatafumbuliwa kuona jinsi kiburi cheusi, cha kishetani, kinavyojiingiza karibu kila mahali, hata katika makusanyiko ya watakatifu. Na aanze kuuliza matokeo yangekuwaje kama, ndani yake na kumzunguka, kuelekea watakatifu wenzake na ulimwengu, waamini wangeongozwa kwa kweli na daima na unyenyekevu wa Yesu. Na aseme kama kilio cha moyo wetu wote, usiku na mchana, hakipaswi kuwa: Ee, unyenyekevu wa Yesu uwe ndani yangu na katika wote wanaonizunguka!
Na akaze moyo wake kwa unyofu juu ya upungufu wake wa unyenyekevu uliofunuliwa katika mfano wa maisha ya Kristo na katika hulka yote ya ukombozi wake, naye ataanza kuhisi kana kwamba hajapata kujua Kristo na wokovu wake ni nini. Ewe mwamini! Jifunze unyenyekevu wa Yesu. Hii ndiyo siri, ndio mzizi uliofichwa wa ukombozi wako. Zama ndani yake zaidi siku kwa siku.
Amini kwa moyo wako wote kwamba Kristo huyu, ambaye Mungu amekupa, kama unyenyekevu wake wa Kimungu ulivyoifanya kazi kwa ajili yako, ataingia akae na kutenda kazi ndani yako pia, na kukufanya uwe kile Baba atakacho.
MAELEZO B Twahitaji kujua mambo mawili: moja ni kwamba wokovu wetu wote wakaa katika kuokolewa kutoka nafsi zetu, kutoka kile tulicho kwa asili; na jingine ni kwamba, katika asili yote ya mambo, hakuna kingeweza kuwa wokovu huu au mwokozi kwetu ila unyenyekevu wa Mungu upitao maelezo yote.
Kwa hiyo, sharti la kwanza lisilobadilika la Mwokozi kwa mwanadamu aliyeanguka: Mtu asipojikana mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu (Mathayo 16:24). Nafsi ndio uovu wote wa asili iliyoanguka, hali kujikana ndio uwezo wetu wa kuokolewa. Unyenyekevu ndiye mwokozi wetu, hali nafsi ndio mzizi, matawi na mti wa uovu wote wa hali yetu iliyoanguka. Maovu yote ya malaika na wanadamu walioanguka yamezaliwa katika kiburi cha nafsi. Kwa upande mwingine, wema wote wa maisha ya mbinguni ni wema wa unyenyekevu.
Ni unyenyekevu peke yake ufanyao shimo lisilovukika kati ya mbingu na jehanamu.
Basi ni nini kilichomo katika vita kuu vya uzima wa milele? Yote yamo katika mapambano kati ya kiburi na unyenyekevu. Kiburi na unyenyekevu ndizo nguvu mbili kuu, falme mbili zipiganazo ili kumiliki mwanadamu milele. Haukuwahi kuwako, wala hautakuwako, unyenyekevu ila mmoja: unyenyekevu wa Kristo. Kiburi na nafsi ndivyo vyote alivyo mwanadamu, hata apate vyote kutoka kwa Kristo. Kwa hiyo apiganaye vita vile vizuri ni yule tu ambaye mapambano yake ni kwamba ile asili ijiabuduyo nafsi aliyo nayo kwa Adamu ifishwe kwa unyenyekevu upitao asili wa Kristo uliohuishwa ndani yake.