Sura 9 · dakika 4 za kusoma

Nuhu

“Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi ya utauwa aliitengeneza safina, ili kuokoa nyumba yake; na kwa hiyo aliuhukumu ulimwengu, akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani” (Waebrania 11:7).

Habari ya Nuhu na safina yapatikana katika Mwanzo 6:5-7:24. Hapa tunapata mfano wa mtu aliyepata neema machoni pa Bwana. Alikuwa mtu mwenye haki, mkamilifu katika kizazi chake, aliyekwenda pamoja na Mungu (Mwanzo 6:9).

Katika Mwanzo 6:13, Mungu alisema na Nuhu. Si vigumu kujua Bwana anataka nini kwako anapoongea nawe.

Haikuwa vigumu kumwamini Mungu, lakini Nuhu alifanya zaidi ya kuamini tu; alitii, akifanya yote Mungu aliyomwamuru. Hii ndiyo imani! Kuamini kunakodhihirishwa kwa tendo la utii.

Maagizo aliyopewa Nuhu yalikuwa ya ajabu sana, lakini bado aliyatii yote. Alikuwa hajapata kuona gharika wala mashua, lakini kwa amri ya Mungu, alianza kazi wala hakupumzika mpaka kazi ilipokamilika. Hatusomi juu ya mtu yeyote, wakiwemo wanawe, waliomsaidia Nuhu katika mradi huu mkubwa, lakini wao na wake zao wangefaidika kwa utii wa Nuhu. Kwa jumla, uhai wa watu wanane ungetegemea neema ya Mungu na utii wa Nuhu.

Ni kanuni gani ya Kibiblia tunayoweza kujifunza kutokana na mfano huu wa imani?

Jibu moja lililo wazi latolewa na Yesu Mwenyewe katika Mathayo 24:37-39, ambapo anawafundisha Wayahudi kuhusu kurudi kwake ili kuuanzisha ufalme wake wa Kimasihi.

Kama ilivyokuwa siku za Nuhu ndivyo kutakavyokuwa wakati wa kuja kwake Mwana wa Adamu. Katika siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila, wakinywa, na kuoana, hata siku ile Nuhu alipoingia katika safina. Hawakujua sababu mpaka gharika ilipokuja ikawachukua wote; ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

Watu watakuwa hawayajali mambo ya Mungu, kwa hiyo hukumu kuu itawajia. Ni wachache tu – mabaki – watakaookolewa.

Ipo kanuni ya uhakika wa hukumu inayokuja juu ya ulimwengu huu; lakini, kweli nyingine yaonekana katika maandalizi Mungu aliyotuandalia kupitia Mwanawe, Yesu. Ameandaa njia ambayo kwayo tunaweza kuokolewa kutoka katika hukumu inayowajia wote wanaokataa kwenda pamoja Naye.

Safina imeandaliwa ndani ya Yesu, na mwaliko umetolewa kwa yeyote atakayeingia! Tunamshukuru Bwana kwamba alikuwa mtii kwa mapenzi ya Baba, ijapokuwa ilimaanisha uchungu wa Gethsemane na msalaba juu ya kilima cha Golgotha. Kwa sababu ya neema ya Baba na utii wa Mwana, wote waingiao wanapata wokovu.

Kama vile Mungu alivyoufunga mlango wa safina ya Nuhu wakati wote wanane walipokuwa ndani (Mwanzo 7:16), ndivyo alivyotutia ‘muhuri’ ndani ya Mwanawe kwa Roho Mtakatifu (Waefeso 1:13). Si tu kwamba kuna usalama ndani ya safina yetu Yesu, bali humo tunabarikiwa kwa kila baraka ya rohoni (Waefeso 1:3). Naam, sura yote ya Waefeso 1 inazungumzia baraka kama hizo.

Ndani Yake: ● Tunafanywa watakatifu wasio na hatia (mstari 4).

● Tunafanywa watoto wa Mungu (mstari 5).

● Tunapokea neema tele ya Mungu (mstari 6).

● Tuna ukombozi (kununuliwa tena kutoka utumwani) na tuna msamaha wa dhambi zetu (mstari 7).

● Mungu anatuonyesha siri ya mapenzi yake (mstari 9).

● Mungu atavikusanya pamoja viumbe vyote (mstari 10).

● Tumewekwa ili tuishi kwa sifa ya utukufu wake (mstari 11).

● Tumetiwa muhuri kwa Roho wake Mtakatifu (mstari 13).

Kisha katika Waefeso 2:6, Paulo anaandika kwamba tumefufuliwa ili tuketishwe pamoja katika ulimwengu wa mbinguni ndani Yake, ili Mungu apate kuonyesha wingi wa neema yake usiopimika katika wema wake kwetu ndani ya Kristo Yesu.

Usalama wetu haupo katika uwezo wetu wa kujenga safina yetu wenyewe, wala katika matendo yetu mema. Haki yetu wenyewe haitatufaa. Hatuwezi kuponyoka kwa mbinu au hila zetu wenyewe; bali, yote ni kwa neema, kwa njia ya imani. Mungu amepanga na kuandaa njia ya wokovu. Anatualika tuingie ndani. Twaweza kuamini, lakini kama hatutii mwaliko wake, hatutaokolewa. Imani iokoayo yahitaji jibu la utii.

Zaidi ya hayo, kila mtu aliyeishi karibu na Nuhu angekitambua chombo hiki cha ajabu alichokuwa akijenga. Wote wangejua alichohubiri, lakini hakuna aliyekuwa tayari kuitikia mwaliko wake.

Watu walihukumiwa kwa kukataa kwao kukubali kile kilichokuwa dhahiri mbele ya macho yao. Vivyo hivyo, habari njema ya wokovu ndani ya Yesu haijafichwa kutoka ulimwenguni leo, lakini watu wanachagua kutoitikia mwaliko; hivyo uwepo wa kanisa bado ni hukumu kwa ulimwengu.

Muhtasari Habari ya Nuhu kama mfano wa imani inatufundisha kanuni zifuatazo: 1. Kuna hukumu inayokuja juu ya ulimwengu.

2. Mungu, kwa neema, amefanya njia ya kuponyoka ndani ya Mwanawe, Yesu, na wokovu haupatikani katika mwingine yeyote.

3. Neema ni sifa ya msingi ya Mungu.

4. Wokovu unadai jibu la utii kwa mwaliko wa Mungu.

Hiyo, ndiyo imani iokoayo.

Ukurasa 1 / 3 · 4 dakika zimebaki katika sura
Ochorus

Kuwawezesha watu vitabu vya Kikristo vya kale — bila malipo, kwa lugha yako.

Chunguza

Dhamira Yetu

Vitabu vya Kikristo vya kale bila malipo mtandaoni — na vitabu vilivyochapishwa tunavyogawa kwenye makongamano, makanisa, shule na magereza kote Afrika Mashariki.

Faragha na Masharti

Huduma tangu 2021 · Victoria BC, Kanada · Kampala, Uganda