Sura 10 · dakika 6 za kusoma
Ibrahimu
“Kwa imani Ibrahimu alipoitwa alitii, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile; kwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu” (Waebrania 11:8-10).
Mfano wa hali ya juu wa maisha ya imani, uliotumiwa na Paulo, Yakobo, na mwandishi wa kitabu cha Waebrania, ni yule msafiri Ibrahimu, na habari yake imeandikwa katika Mwanzo 11-25. Mwandishi wa Waebrania anakazia hapa imani aliyoionyesha Ibrahimu akiwa mgeni, mtu asiye na vifungo vyovyote na mali zake mwenyewe.
Tunapolinganisha mistari ya Waebrania hapo juu na habari ya kihistoria ipatikanayo katika Mwanzo 11:31, tunaona kwamba, ijapokuwa Mungu alikuwa akimwita Abramu (baadaye Ibrahimu) kwenda nchi ya ahadi ya Kanaani, ni kupitia baba yake Tera ndipo alipotoka Uru wa Wakaldayo. Mara nyingi Mungu huwaongoza watoto wake kupitia maamuzi ya wengine. Ilikuwa hata baada ya kutoka Harani ndipo Mungu aliposema na Abramu moja kwa moja. Yeye alikuwa chombo kilichochaguliwa ambacho kwacho Mungu angeliwaimarisha watu wake na nchi yao.
Tofauti na Nuhu, Abramu hakuchaguliwa kwa sababu alikuwa mwenye haki; kwa hakika aliishi katika nchi ya kuabudu sanamu akiwa na ufahamu mdogo wa Mungu. Miongoni mwa watu waliomtangulia walikuwapo wengi waliomwabudu Mungu, lakini hakuna hata mmoja wao aliyechaguliwa kuwa Baba wa taifa kuu la watu wa Mungu.
Habili alikuwa mwema, alitoa dhabihu kulingana na mapenzi ya Mungu, lakini alitoa kwa ajili yake mwenyewe tu. Hakuchaguliwa kwa namna ya pekee.
Henoko na Nuhu pia walikuwa watu binafsi katika kwenda kwao pamoja na Mungu.
Wote watatu walimwabudu Mungu wa kweli, lakini hakuna hata mmoja wao aliyechaguliwa kwa namna ya pekee kuanza kurudisha kile kilichopotea kwa njia ya Adamu.
Ni Abramu ambaye Mungu alimchagua, naye alikuwa mwabudu-sanamu (Yoshua 24:2)! Mungu alimwita Abramu kwa sababu alikuwa na kusudi la pekee – Abramu angekuwa mwanzo wa kurejeshwa kwa kimungu kutoka katika anguko. Tunapogeukia Agano Jipya, maneno ya kwanza tuyasomayo ni, “Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu” (Mathayo 1:1). Mungu anaanza habari yake njema (Injili) na Ibrahimu!
Mungu aliposema, Abramu alitii. Hakuelewa, wala hakusimama kujadili mipango na Mungu. Alitii tu na ‘akatoka.’ Angaliweza kulalamika kwamba tayari alikuwa na umri wa miaka 75 na mzee mno kuanza kutangatanga, lakini hakufanya hivyo. Alitoka asijue aendako. Alikuwa amesikia habari za nchi, ufalme uliokuwa urithi wake. Alikuwa amesikia ahadi kwamba jina lake litakuwa kuu na kwamba angekuwa baraka kwa mataifa yote ya dunia.
Ingawa hakuwa amemjua Mungu kabla ya wakati huu, kulikuwa na uhakika uliopandwa ndani yake wa kuamini kwamba ahadi za Mungu ni za hakika. Hivyo, akatoka… Mungu leo anawatafuta wanaume na wanawake ambao macho yao yameelekezwa kwenye ufalme wake na si kwenye masoko ya ubatili ya ulimwengu huu. Mtunzi wa wimbo wa 695 wa Trinity Hymnal asema, “Mimi ni mgeni hapa katika nchi ya kigeni, nyumbani kwangu ni mbali sana juu ya ufuo wa dhahabu.
Mimi ni balozi wa mambo yaliyo ng’ambo ya anga, nipo hapa kwa shughuli za Mfalme wangu.”
A.P. Carter, ameeleza hivi katika wimbo wake, “Ulimwengu Huu si Nyumbani Kwangu:” “Ulimwengu huu si nyumbani kwangu, mimi ni mpita njia tu.
Hazina zangu zimewekwa mahali fulani ng’ambo ya buluu.
Malaika wananiita kutoka mlango wa Mbinguni ulio wazi, wala siwezi kujisikia kuwa nyumbani katika ulimwengu huu tena!”
Mtume Yohana anatuonya tusiupende ulimwengu, wala vitu vilivyomo ndani ya ulimwengu (1 Yohana 2:15). Bila shaka, twapaswa kuwapenda watu wa ulimwengu huu na uzuri wake unaotufanya kumwabudu Mungu, lakini Yohana anazungumzia mifumo iliyotengenezwa na wanadamu: siasa zake na hila zake, ubinadamu wake wa kidunia na maridhiano yake, na ubatili wake na uroho wa mali. Ibrahimu hakuwa na hamu na mambo kama hayo kwa maana alikuwa mgeni, mpita njia, na kwenda kwake kulikuwa ni kwenda pamoja na Mungu, kwenda kwa imani.
Nakumbushwa juu ya yule mwana mpotevu katika mfano uliohubiriwa na Yesu katika Luka 15. Alitoka na kutapanya sehemu yake ya urithi katika anasa za ulimwengu. Aliporudiwa na fahamu zake, alirudi nyumbani kwa toba akisema, “Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako. Sistahili tena kuitwa mwana wako. Nifanye kama mmoja wa vibarua wako” (Luka 15:18-19). Hata hivyo, baba yake anampokea kwa uchangamfu, akimvika mavazi bora zaidi, akimtia viatu miguuni, na kumwandalia karamu – jambo lililomhuzunisha sana ndugu yake mkubwa. Ingawa najitambua mwenyewe katika yule mpotevu, nikijua hatia yangu na kuukiri upendo wa Baba anayeniendelea kunikubali kuwa mwana wake, naona kidogo ndani yake cha kumsifu, hata nilinganishe na yule mwana mkubwa!
Yule mwana mkubwa analalamika kwa baba juu ya jinsi mpotevu alivyotendewa. “Ameleta aibu kwetu, ameutapanya urithi wake akitamani ulimwengu huu, hali mimi nimebaki mwaminifu nyumbani. Kwa nini umemchinjia ndama aliyenona? Wewe hujanitendea hivyo kamwe!” (Luka 15:28-30). Unafiki ulioje wa kujiona bora! Baba anajibu, “Mwanangu, ndama wote walionona ni wako! Kila kilichobaki ni urithi wako!” (Luka 15:31). Yule mpotevu alikuwa ametamani anasa za ulimwengu huu, lakini sasa alikuwa amerudiwa na fahamu zake kwa majuto ya toba.
Yule mwana mkubwa naye alitamani vitu vya ulimwengu huu – si mvinyo, wanawake, na nyimbo – bali mali zake. Alimiliki shamba wala hakutaka chochote kimnyang’anye urithi wake. Kwa kweli, shamba lilimmiliki yeye!
Si kosa kuwa na mali katika ulimwengu huu, lakini kwenda kwa imani kunadai kwamba, kama Ibrahimu, mali hizo zisitumiliki! Zishikilie kwa wepesi ili, Bwana atakapokuita uende, hakuna kitakachokuzuia. Hii ndiyo hakika sababu ambayo waaminio hawapaswi kamwe kuwa na madeni. Tunapomdai mtu fedha na kushindwa kutimiza wajibu huo wakati wowote tunapoitwa, tuko utumwani kwa mtu huyo, wala hatuko huru kuitika Bwana anapotuita ‘tutoke tuende.’ Kwa kweli tunamtumikia Mamona, na si Mungu, wakati huo. Ningependekeza kwamba jambo hili ni zito kiasi kwa Bwana kiasi kwamba hatupaswi hata kuleta zaka na sadaka zetu madhabahuni pake ikiwa mwingine ana neno juu yetu, yaani, tuna deni kwake.
Twapaswa kutoka katika deni kabla hata ya kutoa zaka zetu kwa Mungu (Mathayo 5:23-26).
Labda hivi ndivyo Bwana alivyomaanisha aliposema, “aliye mkuu kwenu na awe kama aliye mdogo; naye aliye kiongozi na awe kama yule atumikaye” (Luka 22:26). Tofauti kati ya ndugu hao ilikuwa mitazamo yao juu ya vitu vya ulimwengu. Ndugu mkubwa alikuwa na wasiwasi urithi wake usije ukatapanywa katika karamu ya yule mpotevu aliyerudi. Hakutaka mtu yeyote atikise mashua yake, aliridhika na hali ilivyokuwa. Vivyo hivyo, Esau angeuza haki yake ya uzaliwa wa kwanza kwa ajili ya kuridhika kwa sasa, kwa muda, hali ndugu yake mdogo Yakobo, ingawa alikuwa mdanganyifu, alikuwa msafiri aliyekwenda – na kushindana mieleka – pamoja na Mungu.
Kama yule mpotevu, Yakobo aliletwa katika toba, lakini si Esau. Mmoja alikuwa na urithi wake katika Mungu; mwingine katika ‘sahani ya dengu.’ Ni jambo la kushangaza kwamba Mungu angetamka, “Nimempenda Yakobo, lakini nimemchukia Esau” (Malaki 1:3). Tena ni jambo la kuzingatiwa kwamba ahadi zilizopewa yule mwabudu-sanamu Abramu zilirudiwa kwa yule mdanganyifu Yakobo, naye pia, angekuwa mmoja wa wale mababu watatu wakuu wa watu wa Kiyahudi, Ibrahimu, Isaka, na Yakobo.
Mungu anawatafuta wanaume na wanawake kama Ibrahimu. Watu walio tayari kuongozwa na Bwana hasa wakati na mahali anapotaka kuwaongoza. Kwetu bado anasema, “Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake” (Mathayo 6:33).
Tutamzingatia Ibrahimu tena katika sura ya baadaye ambapo tutaona ushahidi zaidi wa kwenda kwake kwa imani pamoja na Mungu, ushahidi ulioitwa pia na Yakobo na Paulo mitume, katika maandiko yao.
Muhtasari Ibrahimu ametolewa kwetu katika Waebrania 11 ili kutufundisha kanuni hizi: 1. Mungu hamchagui mtu kwa sababu ya jambo lolote adaialo kuwa. Badala yake huvichagua vitu vilivyo dhaifu na vipumbavu, vitu vilivyo dhalili na vinavyodharauliwa, ili mtu yeyote asije akajivuna (1 Wakorintho 1:27-29).
2. Watu wa imani ni wale ambao macho na mioyo yao imeelekezwa kwenye ufalme wa mbinguni; ambao mtazamo wao ni ule wa ‘mdogo,’ wakiwa na vifungo vyepesi na ulimwengu huu.
3. Mungu alianza kazi ya ukombozi katika mtu ambaye angekuwa mfano bora wa kwenda kwa imani, uliodhihirishwa katika kutumaini kwa utii.