Sura 8 · dakika 6 za kusoma
Henoko
“Kwa imani Henoko alihamishwa ili asione mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mungu alikuwa amemtwaa. Basi kabla ya kutwaliwa alishuhudiwa kwamba amempendeza Mungu.”
(Waebrania 11:5).
Habari ya Henoko imeandikwa kwa kifupi sana katika Mwanzo 5:18-24.
Swali jingine la mashindano ya Biblia ya watoto lauliza, “Ni nani mtu aliyeishi zaidi ya wote?” Methusela, mwana wa Henoko!
Henoko aliishi duniani miaka 365, akienda pamoja na Mungu kabla ya ‘Mungu kumtwaa.’ Kuenda huku pamoja na Mungu kulikuwa mwendo wa imani, ambao pasipo huo haiwezekani kumpendeza Mungu (Waebrania 11:16).
Alijua ni nini kuwa na ushirika wa karibu na Muumba wake, kuisikia sauti yake na kujua uongozi wake.
Ni tamu kama nini ushirika huo lazima ulikuwa! Ijapokuwa Henoko alionyesha dalili za anguko la Adamu na Hawa, bado alifurahia uwepo wa Mungu. Leo pia, wakati kila kitu kinachotuzunguka chaweza kuonekana kimeharibika, na uovu waonekana kushinda, mtoto wa Mungu aendaye kwa imani angali aweza kuwa na ushirika mtamu na Bwana wake.
Historia imejaa habari za waaminio ambao hali zao zilikuwa ngumu sana, lakini ambao ushuhuda wao uling’aa kwa sababu walijua uwepo wa Kimungu.
“Kwa imani Henoko alihamishwa” (Waebrania 11:5).
Maana yake nini? Bila shaka si kwamba Henoko aliamini sana kwamba angehamishwa, hata Mungu akamtendea hivyo!
Badala yake, lilikuwa tendo la Mungu la enzi lililomhamisha, ili kutufundisha kweli kuu!
Tumaini la Ufufuo Ni kanuni gani ya kimaandiko tuwezayo kujifunza kutokana na habari hii fupi yenye maana kwetu leo?
Ni wazi, kuna kanuni ya uzima wa milele.
Kwa wale waendao pamoja na Mungu kwa imani, kuna ahadi ya Ufufuo, au unyakuo wakati wa kuja kwake mara ya pili, kuingia katika uzima wa milele. Paulo na Petro wote wawili, waliposimama mbele ya watu, walitangaza kwamba hili ndilo tumaini la waaminio wote. Naam, Paulo alijua kwamba hii ndiyo iliyokuwa sababu kuu ya kuteswa kwake. “Mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini na ufufuo wa wafu” (Matendo 23:6). Dini nyingine zaweza kufundisha kuzaliwa upya mara kwa mara, au wokovu unaotegemea matendo ya haki; lakini, ujumbe wetu hautikisiki katika tangazo lake la Ufufuo uingiao katika uzima wa milele kwa wote waendao kwa imani pamoja na Mungu.
Tumaini hili ambalo kwa ajili yake Paulo na Petro, na mitume wote, walikuwa tayari kufa, limejengwa juu ya jambo la hakika - kama ilivyo kila tumaini la Kikristo, tofauti na matumaini ya ulimwengu. Niwakumbushe kwamba tumaini la Kikristo hufafanuliwa vyema kuwa “kutarajia kwa shauku kile kilicho hakika.” Tumaini letu la Ufufuo limejengwa juu ya tukio tukufu kuliko yote katika historia yote; ufufuo wa Yesu kutoka kwa wafu.
Mtu anapoyaangalia kwa haki habari zote, nadharia, na maoni juu ya Jumapili ile ya kwanza ya Pasaka, sharti afikie hitimisho kwamba jambo lililoshuhudiwa zaidi ya yote katika historia yote ni kwamba Yesu wa Nazareti, akiisha kusulubiwa juu ya msalaba wa Kirumi, na kuzikwa katika kaburi la kuazima, alifufuka kutoka kwa wafu, na kufufuliwa katika uzima mpya.
Aliwatokea wanafunzi na wengine wengi. Mtume Paulo aandika kwamba zaidi ya ndugu 500 walikuwa mashahidi wa macho wa uzima wake mpya, ambao karibu wote walikuwa bado hai kuushuhudia ukweli huo wakati mtume alipoandika miaka mingi baadaye. Watu hawa hawakuwa na faida yoyote kwa kueneza uongo na wangepoteza kila kitu kwa kushikilia ukweli. Kulikuwa na mateso makuu dhidi ya waaminio, ambao wengi wao walipoteza maisha yao kwa sababu hawakukubali kukana kile kilichokuwa kwao ni jambo la hakika.
Mapokeo yatuambia kwamba kila mmoja wa mitume, isipokuwa Yohana, waliuawa kishahidi kwa ajili ya kile walichokijua - kwamba Yesu alifufuka kutoka kwa wafu!
Sasa walielewa alichokusudia alipowafundisha, “Bado kitambo kidogo na ulimwengu hautaniona tena; bali ninyi mnaniona. Kwa sababu mimi ni hai, ninyi nao mtakuwa hai” (Yohana 14:19). Hili ndilo lililokuwa tumaini lao - kutarajia kwa shauku kile kilicho hakika - na ahadi iliyodhihirishwa katika ushuhuda wa Henoko.
Ufufuo wa Yesu ndio hoja ya msingi ya imani yetu ya Kikristo. Pasipo huo, hakuna Ukristo. Dini kama hiyo isingekuwa tofauti na nyingine zote kwa kuwa haiwezi kutoa tumaini. Pia ni wa maana kwa sababu zifuatazo: 1. Waonyesha haki ya Mungu aliyemtukuza Kristo mpaka uzima wa utukufu, kama vile Kristo alivyojinyenyekesha hata mauti (Wafilipi 2:8-9).
2. Ufufuo ulikamilisha siri ya wokovu wetu na ukombozi wetu. Kwa kifo chake, Kristo alituweka huru kutoka katika adhabu ya dhambi (Warumi 5:8), kwa mateso yake alituweka huru kutoka katika laana ya Sheria (Wagalatia 3:13), na kwa Ufufuo wake aliturudishia mapendeleo ya maana zaidi yaliyopotea kwa dhambi (Warumi 4:25).
3. Kwa Ufufuo wake twamkiri Kristo kuwa Mungu asiyekufa, chanzo chenye nguvu na cha mfano cha ufufuo wetu wenyewe (1 Wakorintho 15:21 na Wafilipi 3:20-21) na kama kielelezo na chanzo cha maisha yetu mapya ya neema (Warumi 6:4-6 na Warumi 9-11).
Ushuhuda wa Paulo Ni kwa sababu ya tumaini lao la Ufufuo uingiao katika uzima wa milele ndipo waaminio wa kwanza waliteswa. Maandiko yatuandikia ushuhuda wa mtume Paulo aliposimama mbele ya wakuu wa makuhani na Baraza akihukumiwa. “Ni kwa habari ya tumaini na ufufuo wa wafu mimi ninahukumiwa” (Matendo 23:6).
Baraza lilikuwa na vikundi viwili vikuu: Mafarisayo wa kidini, walioamini Ufufuo wa wale washikao sheria, na Masadukayo wa kisiasa, wasioamini. Kwa kawaida, palikuwa na mafarakano kwa maneno ya Paulo, hivyo askari waliamriwa kumrudisha Paulo katika chumba chake cha gerezani.
Sasa ikazuka njama ya kisiasa yenye kusudi la kumwua mtume, lakini jemadari wa Kirumi alijulishwa juu ya njama hiyo, hivyo akaamuru Paulo apelekwe Antipatri ambako Feliki, liwali wa Kirumi, alikuwa na jumba lake la kifalme.
Mbele ya liwali, Paulo anarudia tumaini lake katika Ufufuo, wa wenye haki kuingia uzimani, na waovu kuingia hukumuni (Matendo 24:15,21).
Kwa kutojua la kumtendea Paulo wala jinsi ya kuwaridhisha washtaki wake, Feliki alimweka gerezani mpaka, miaka miwili baadaye, aliporithiwa na liwali mpya, Festo. Mtume alifanywa kuwa tamasha, akiitwa aseme juu ya imani yake ya ‘kipumbavu’ mbele ya Festo na wageni wake, Mfalme Agripa na mkewe Bernike. Paulo hakati tamaa mbele ya wasikilizaji hawa. Tena anasisitiza, “Ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini hili kuu, Ee Mfalme. Mbona mnaona kwamba ni neno lisiloweza kusadikiwa, ya kwamba Mungu huwafufua wafu?” (Matendo 26:7-8). Baadaye angesimama mbele ya Kaisari ambako tunaweza kuwa na hakika, hakusita kutoa ushuhuda uleule, ijapokuwa ulisababisha kifo chake. Lakini kwa nini aogope kifo? Alikuwa amekwisha kuandika: “Angalieni, nawaambia siri. Hatutalala sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika. Maana sharti kitu hiki kiharibikacho kivae kutokuharibika, nacho kifacho kivae kutokufa. Basi kitu hiki kiharibikacho kikiisha kuvaa kutokuharibika, na kitu hiki kifacho kikiisha kuvaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, ‘Mauti imemezwa kwa kushinda.’ ‘Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?’ Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo” (1 Wakorintho 15:51-57).
Hii si kweli mpya, bali ni siri. Kila mara Paulo anapoandika juu ya siri, anamaanisha kweli iliyokuwako sikuzote, lakini ambayo sasa tu inafunuliwa (Warumi 16:25-26).
Ni Yesu aliyekuwa wa kwanza kunena juu ya siri ya ufalme (Marko 13:11), lakini Paulo pia alitumia usemi huu mara nyingi.
Kichwa kizuri cha Kujifunza Biblia binafsi kingekuwa kuchunguza marejeo yafuatayo: siri ya Mataifa ‘kupandikizwa ndani’ (Warumi 11:25), siri ya mapenzi yake (Waefeso 1:9), siri ya Mataifa (Waefeso 3:3), siri ya ndoa (Waefeso 5:32), siri ya Injili (Waefeso 6:19), siri ya Kristo ndani yenu (Wakolosai 1:26-27), siri ya Kristo mwenyewe (Wakolosai 2:2), siri ya uasi (2 Wathesalonike 2:7), siri ya imani (1 Timotheo 3:9), na siri ya utauwa (1 Timotheo 3:16).
Siri hii, kweli hii, tumaini hili tukufu la ufufuo uingiao katika uzima wa milele, lilifunuliwa kwetu kwanza katika ushuhuda wa Henoko.
Muhtasari “Kwa imani, Henoko alihamishwa” (Waebrania 11:5), ili tupate kujua kwamba tuna tumaini tukufu; lile la uzima wa milele.
Hii si fundisho la Agano Jipya, bali sikuzote imekuwa sehemu ya makusudi ya Mungu kwa watu wake.