Sura 7 · dakika 9 za kusoma
Kaini na Abeli
“Kwa imani Abeli alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini, ambayo kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki, Mungu akizishuhudia sadaka zake; na kwa imani hiyo, ingawa amekufa, angali akinena” (Waebrania 11:4).
Habari ya asili ya Kaini na Abeli yaweza kupatikana katika Mwanzo 4:1-8.
Swali linaloulizwa mara kwa mara katika mashindano ya Shule ya Jumapili ni, “Ni nani mtu wa kwanza kumwaga damu?” Hakuna sababu ya kutosha ya kuamini kwamba Adamu hakuwahi kumchinja mnyama kwa ajili ya chakula, lakini kumwagwa kwa damu kwa kwanza kunakoandikwa ni kule kwa Abeli alipomwaga damu ya mwana-kondoo. Wanafunzi, katika shauku yao ya kujibu, mara nyingi husema kwamba wa kwanza alikuwa Kaini aliyemwaga damu ya ndugu yake katika tendo la uuaji.
Kaini alikuwa mwana wa kwanza kuzaliwa kwa Adamu na Hawa. Mama yake alifurahi mno. Bila shaka huyu ndiye ‘mzao’ aliyeahidiwa na Mungu katika tangazo lake la vita dhidi ya yule nyoka aliyemdanganya (Mwanzo 3:15). Akamwita jina lake Kaini - maana yake “mkuki” - akisema “Nimepata mtu kwa Bwana.” Punde si punde anatambua kosa lake alipokua akiwa na tabia zote za mtoto mwingine yeyote azaliwaye; yamkini alikuwa mtundu vivyo hivyo!
Anazaliwa mwana mwingine ambaye anamwita Abeli - maana yake “ubatili” - akitambua kwamba vita havitakwisha upesi kama alivyodhani. Tumaini kama hilo lilikuwa bure. Ni dhahiri kwamba kungekuwa na ‘wazao’ wengine, basi ni yupi kati yao angekuwa yule wa kumjeruhi nyoka kichwa?
Miaka inapita, na wakati huo hakukuwa na ushirika na Mungu, wala ibada, ila hisia nzito ya hatia kwa wazazi na kuongezeka kwa maswali na hamu ndani ya wale wana wawili. Naweza kuwaza maisha yao katika siku zile za mwanzo, nje kidogo ya kuta, na kuwaona wakiwauliza wazazi wao habari za bustani na wale makerubi waliolinda lango lake. Najiuliza kama Adamu au Hawa waliweza kamwe kuwaeleza wana wao yaliyotukia ndani ya kuta zile - halingekuwa jambo ambalo wangependa kulikumbuka! Lakini, sikuzote kumekuwako ndani ya mwanadamu hamu ya kuabudu, ikiwa ni Mungu Aliye Hai au mmojawapo wa miungu isiyo na idadi inayowakilishwa katika dini mbalimbali za ulimwengu. Kaini na Abeli wasingekuwa tofauti.
Wale wavulana walipokua, walijipatia mapendezi tofauti. Kaini alilima ardhi akawa mkulima wa nchi, akizalisha maua mazuri, mboga, matunda, na mimea. Alimfuata baba yake aliyetaabika mashambani siku zote za maisha yake. Yule mwana mdogo, Abeli, akawa mchungaji, akizunguka na wanyama walipotafuta malisho mema.
Kaini ndiye aliyewaza kwanza kumletea Mungu zawadi. Hatujui kusudi lake, lakini hakuna sababu ya kuamini kwamba hii ilikuwa kitu kidogo kuliko sadaka ya kweli, ya shukrani, (lugha ya Kiebrania kwa hakika yaonyesha hivyo). Huenda kulikuwa na tumaini kwamba Mungu angemwonyesha upendeleo na kumruhusu kurudi ndani ya bustani. Angepeleka wapi kikapu cha mazao aliyoyaosha, akayang’arisha, na kuyapanga kwa uangalifu mwingi? Yamkini kwenye lango lililolindwa na makerubi. Kikapu kilionekana kizuri sana na rangi zake mbalimbali na harufu nzuri. Aliweka kikapu mbele ya malaika huku ndugu yake akitazama.
Ndugu Abeli anajiuliza ni nini awezacho kuleta kuwa sadaka kwa Mungu.
Hataki kuachwa nyuma ikiwa kuna nafasi yoyote ya kumridhisha Mungu, lakini hana mazao mazuri ya kuleta. Naam, hana kitu chochote alichokipata kwa jasho la uso wake. Alichonacho ni ng’ombe, mbuzi na kondoo tu.
Kwa imani alitoa dhabihu iliyo bora zaidi. Maana yake nini?
Twasoma kwamba “Imani ni kwa kusikia; na kusikia huja kwa neno la Mungu” (Warumi 10:17). Ni dhahiri kwamba Mungu alisema na Abeli. Nakumbushwa maneno ya Yesu kwa Petro juu ya Mlima Hermoni, yaliyoandikwa kwa ajili yetu katika Mathayo 16:17 yasemayo, “Heri wewe… kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.”
Sauti ya Mungu haikuwa sauti ya radi, wala sauti itambulikanayo kwa hisi za mwili, bali ni ile sauti ya ndani isikiwayo na nafsi na mara nyingi isiyotambulika kuwa ni yake.
Abeli, akiitikia ile sauti ya ndani, aliamua, “Nitaleta mwana-kondoo. Mwana-kondoo mchanga, mzaliwa wa kwanza. Nitamchinja, nimtayarishe, na kumleta pamoja na mafuta yake.” Basi, anatoa sadaka yake mbele ya malaika langoni. Imani yake ilidhihirika katika utii wake kwa ile sauti ya ndani.
Tendo lifuatalo ni la Mungu. Ndiye aliyewaongoza watu wote wawili hapa kwa kuwa anataka kuwafundisha - na kutufundisha sisi - kanuni kadhaa za lazima za maisha ya haki. “Bwana akamtakabali Abeli na sadaka yake; bali Kaini na sadaka yake hakuitakabali” (Mwanzo 4:4).
Nguvu Iharibuyo ya Chukizo Watu wenyewe ni wa maana kama vile sadaka zao. Mungu aujua moyo wa mwanadamu na amjua mtu ambaye aweza kumwamini ufunuo wake na uchochezi wake.
Alimwambia Musa kwamba alijua jina lake (tabia yake) na kwa hiyo angemfunulia jina lake (tabia yake), na utukufu wake kwa Musa (Kutoka 33:12-34:8). Simoni alipotangaza kwamba Yesu ndiye Masihi, bwana wake alitambua kwamba ujuzi kama huo ulikuwa umekuja kwa ufunuo kutoka kwa Mungu. Ingawa mara nyingi alinena pasipo wakati wake na alikuwa na elimu ndogo, moyo wake ulikuwa sawa, hivyo Mungu akampa ufunuo.
Akijua kwamba hii ilikuwa ushuhuda wa tabia yake, Yesu alimpa jina jipya Petro - maana yake, “mwamba.” Mungu aiona vipi mioyo yetu? Je, aiona tabia itakayompendeza?
Angekupa jina gani? Je, aona mtu ambaye aweza kumfunulia utukufu wake, akijua kwamba hutajitwalia sehemu ya utukufu huo kwa nafsi yako? Je, aona mtu ambaye moyo wake ni safi, mtu ambaye aweza kujifunua kwake (Mathayo 5:8)? Moyo safi umekaza nia moja, haujachanganywa na upendo wa vitu vya ulimwengu.
Kaini hakukosa kwa kuleta sadaka yake kwa Mungu. Kwa kweli anastahili kusifiwa kwa matendo yake; lakini, Mungu alijua kwamba ndani ya Kaini kulikuwa na uwezekano wa chukizo lipelekealo dhambini.
Chukizo lenyewe si dhambi. Yesu aliwachukiza Mafarisayo, waandishi, na hata baadhi ya rafiki zake, lakini pasipo dhambi. Hata hivyo, ni silaha itumiwayo sana na Shetani kuwanyang’anya waaminio ushindi wao, nayo imekuwa chanzo cha migawanyiko ya makanisa kuliko kitu kingine chochote katika ghala lake la silaha. Cha kusikitisha, watu wanazidi kuuacha uwanja wa vita vya kiroho kwa sababu wanachukizwa. Sababu kuu iwafanyayo wamisionari kuuacha uwanja na wachungaji kuacha mimbari zao si fedha, wala magonjwa, wala shida za viza au lugha, bali ni kwa sababu wao, au mtu wanayefanya kazi naye, wamechukizwa.
Huu hapa ni muhtasari mfupi wa mifano mitano ya kimaandiko ya watu waliochukizwa na iliyowagharimu nini.
1. Katika Mathayo 13:20-21 mtu anachukizwa na Neno. Kwa mfano, hawapendi wito wake wa kujitoa, na matokeo yake, hapakuwa na tunda la kiroho (Wagalatia 5:22-23).
2. Katika Mathayo 13:53-58 kuzoeana kwazaa dharau: walichukizwa (Mathayo 13:57)! Matokeo yake, hapakuwa na huduma ya kimuujiza. Hakuna majibu ya maombi, wala ufunuo.
3. Katika Mathayo 26:6-10 wanafunzi (hasa Yuda) wanachukizwa (Yohana 12:14 na Mathayo 26:8). Matokeo yake, hapakuwa na uthabiti, na Yuda anatoka kwenda kumsaliti Bwana wake (Mathayo 26:14).
4. Katika Mathayo 26:31-35 wanafunzi wanachukizwa kwa sababu hawaelewi. Matokeo yake, hapakuwa na ushuhuda.
Petro, “yule mwamba,” anabomoka mbele ya msichana mdogo.
5. Katika Yohana 6:51-61 wanafunzi wanachukizwa kwa wito wa Yesu wa kujitoa. Matokeo yake hapakuwa na ushirika wala urafiki. “Kwa ajili ya hayo wengi katika wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena” (Yohana 6:66).
Mungu angemtahini Kaini kama vile Yesu alivyowatahini wale aliowapenda. Yohana Mbatizaji alichukizwa na Yesu alipokuwa hakumtembelea gerezani, na Mariamu alichukizwa naye kwa sababu hakuharakisha kuzuia kifo cha Lazaro (Mathayo 11:2-6 na Yohana 11:1-35). Naam, ningependekeza kwamba sababu iliyomfanya Yesu alie ni jinsi alivyosema naye hatimaye alipokuja kumwona nje ya Bethania. Alitumia maneno yale yale kama dada yake Martha, “Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa” (Yohana 11:32), lakini itikio la Yesu lilikuwa tofauti sana. Bila shaka, hakumlilia Lazaro, wala waombolezaji wa kuajiriwa, kwa maana alikuwa akijua hali yao tangu alipoamua asije walipomwita mara ya kwanza. Pia alijua kwamba baada ya dakika chache wote wangefurahi kwa ajili ya Ufufuo.
Bwana huruhusu machukizo yaje katika maisha yetu ili kutufundisha jambo fulani juu yetu wenyewe, juu ya hali ya mioyo yetu.
Tunaporuhusu chukizo kuwa dhambi twadhihirisha tabia ambayo Mungu hatampa ufunuo, wala uchochezi wa imani.
Nguvu ya Upatanisho ya Damu Pili, Mungu aliitakabali sadaka ya Abeli, lakini si ile ya Kaini. Wengine wamesema kwamba hii ni kwa sababu Kaini angalipaswa kujua kwamba ili kumkaribia Mungu, ilimpasa amwage damu ya mwana-kondoo, lakini angalijuaje jambo hilo? Zaidi ya hayo, hakuwa na kondoo - walikuwa mali ya Abeli. Naamini kwamba hoja ya namna hiyo ni kupindua utaratibu wa mambo. Mungu aliichagua sadaka ya Abeli ili kuwafundisha wao, na sisi, jambo lililokuwa halijulikani hapo awali. Njia pekee ambayo mwanadamu aweza kumkaribia Mungu ni kwa damu ya mwana-kondoo iliyomwagwa. Hapakuwa na kosa lolote katika sadaka ya Kaini, lakini Mungu aliichagua ya Abeli. Naam, baadaye, Mungu alipoweka aina mbalimbali za sadaka kwa ajili ya siku za sikukuu za watu wake, mazao ya shamba yalikuwa sadaka iliyokubalika sana (Mambo ya Walawi 6:14-23).
Katika Agano la Kale lote, twasoma juu ya Mungu akiunyoshea mkono uumbaji wake akitaka kuwarudisha katika ushirika naye mwenyewe. Anakuta wachache ambao mioyo yao ni safi mbele zake mpaka, wakati wa gharika, anafuta wote isipokuwa jamaa moja ya watu wanane katika uso wa dunia. Baadaye anajitwalia watu wa pekee na kuwafunulia mapenzi yake katika zile Amri Kumi. Wanajionyesha kuwa hawawezi kuitimiza haki iliyodaiwa na Sheria ile, hivyo anafunua jinsi atakavyoshughulika na dhambi yao.
Kwa kila aina ya uchafu, ilibidi damu imwagwe. Hili lilikuwa kweli hasa kwa ile Siku kuu ya Upatanisho ya kila mwaka wakati dhambi za watu na taifa zilipopaswa kufunikwa kwa mwaka mwingine. Katikati ya sherehe na taratibu nyingi, mwana-kondoo alichukuliwa. Ilibidi awe ‘asiye na waa,’ dume la umri wa mwaka mmoja. Damu yake ilimiminwa katika bakuli na kuchukuliwa na Kuhani Mkuu mpaka mahali patakatifu pa patakatifu ndani ya hema au hekalu, ambapo ingetolewa mbele za Mungu. Taifa lote lingesubiri kwa hofu wakitumaini kwamba Mungu angeikubali dhabihu hii kwa mwaka mwingine. Furaha ingekuwa kubwa Kuhani Mkuu aliporudi kwao bila kudhurika. Mungu amependezwa tena kuwakubali kuwa watu wake!
Taratibu hizi za Agano la Kale zilikuwa kivuli tu cha kile kilichotimizwa katika kifo cha Yesu, Mwana-Kondoo wa Mungu, msalabani pale Kalvari; lakini, hakuimwaga damu yake ili dhambi zetu zifunikwe kwa mwaka mwingine. Kifo cha mwana-kondoo mkamilifu kilikuwa cha kuziondoa dhambi zetu kabisa, mbali kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, hata katika vilindi vya bahari (Zaburi 103:12). Kwa wale walioweka tumaini lao katika kazi iliyokamilika ya Kalvari, hakuna tena hukumu bali njia ya kuingia katika uwepo na ushirika wa Mungu. Paradiso imepatikana tena!
Itikio la Kaini Moyo wa Kaini ulifunuliwa. Alighadhibika sana, na uso wake ukakunjamana. Bwana akamwuliza kwa nini amekasirika na akamwuliza swali la kupendeza. “Kama ukitenda vyema, hutakubaliwa? Na kama usipotenda vyema, dhambi inakuotea mlangoni; nayo inakutamani wewe, lakini yakupasa kuishinda” (Mwanzo 4:7).
Ni dhahiri kwamba Kaini alikuwa bado hajatenda dhambi! Hapakuwa na dhambi katika kumkaribia kwake Mungu wala katika sadaka yake. Mtazamo wa Kaini ulikuwa mbaya, kuchukizwa kwake kulikuwa kubaya, lakini tunda la dhambi lilikuwa bado halijaja.
Ilimpasa kuishinda jaribu la dhambi na kutenda vyema; lakini, anashindwa. Abeli anauawa na Kaini anatupwa nje, walakini akiwa na alama ya Mungu ya ulinzi juu yake.
Katika kuizingatia habari hii, wafafanuzi wa Kiyahudi wana uelewa wa kupendeza wa lile swali alilouliza Mungu. Wanaliona kuwa taswira ya awali ya kutoa zaka! Sadaka ya Kaini haikukubalika kwa sababu hakuwa ‘amegawanya vyema’ mazao yake.
Wanaifasiri Mwanzo 4:7 hivi, “Kama ungaligawanya vyema, je, sadaka yako isingalikubaliwa?”
Muhtasari Ninaposoma habari ya Kaini na Abeli katika muktadha wa imani, namwona Bwana akitufundisha kanuni zifuatazo: 1. Kumkaribia Mungu Aliye Mtakatifu ni kwa njia ya damu ya mwana-kondoo iliyomwagwa tu, ambaye ni mfano mkamilifu wa Mwana-Kondoo wa Mungu ajaye, Yesu.
2. Mungu aujua moyo wa mwanadamu na atajifunua tu kwa wale walio safi wa moyo.
3. Mungu huruhusu machukizo yaje ili kutufundisha juu ya uwezekano wa moyo wetu wa kutenda dhambi.