Sura 5 · dakika 16 za kusoma
Kuisikia Sauti ya Mungu
Ingawa kuisikia sauti ya Mungu ni rahisi kwa baadhi ya watu, kwa wengine ni hisi ambayo ni lazima iimarishwe!
Kilikuwa kitu cha ajabu kilichouvutia macho ya Musa alipokuwa akichunga kondoo wa baba mkwe wake. Kichaka kilikuwa kikiwaka moto kwa nguvu, lakini hakikuteketea! Majani yalibaki mabichi, ingawa miali ya moto ilikuwa ikiyalamba (Kutoka 3:2). Hakuwahi kuona jambo lolote kama muujiza huu katika muda wake wote huko Misri akiwa mwana wa Farao, wala katika miaka mingi aliyoishi kama mchungaji katika nchi ya Midiani. Akasogea karibu kidogo ili achunguze.
Ghafla sauti ikapaza sauti, “Musa!”
Je, waweza kuuwazia mshangao wake, hasa ilipoonekana kwamba sauti hiyo ilikuwa ikitoka ndani ya kile kichaka kilichokuwa kikiwaka moto!?
Sauti ikaendelea, “Vua viatu vyako miguuni mwako, kwa maana mahali unaposimama ni nchi takatifu!” (Kutoka 3:5). Nina hakika alifanya haraka kutii kwa sababu ya jinsi tukio lilivyokuwa - ni lazima aliogopa!
Hivyo ukaanza wakati mrefu wa ushirika kati ya Mungu na Musa. Tangu hapo walizungumza pamoja mara kwa mara, huku Bwana akimwongoza mtumishi wake katika kuwaongoza Waisraeli kutoka katika utumwa wao huko Misri, akatoa maagizo ya kujenga hema la kukutania, na akaamuru sheria kadhaa kwa ajili ya watu wake wa agano.
Naam, twasoma kwamba walinena “uso kwa uso, kama mtu asemavyo na rafiki yake” (Kutoka 33:11). Haishangazi kwamba uso wa Musa uling’aa!
Je, humwonei wivu Musa kwa kuweza kuzungumza na Mungu kwa namna hiyo?
Mimi bila shaka namwonea.
Mtu aweza kukisia ni nini hasa Musa alichokiona, na kusikia Mungu alipomwambia. Sauti ya Mungu ilikuwaje?
Je, ilikuwa sauti nzito, yenye mvumo kama ya mwigizaji stadi wa michezo ya Shakespeare?
Je, ilikuwa na mahadhi au lafudhi fulani? (Labda ya Kiwelisi, kama yangu, kwa kuwa ni dhahiri kwamba hufurahia kuitembelea nchi yangu mara kwa mara, katika mafuriko makubwa ya uamsho?!) Alisema lugha gani - ile ya Misri ambako Musa alikuwa amesomeshwa au ile ya Wamidiani ambako Musa alikuwa ameishi kwa miaka arobaini iliyopita?
Yote tuwezayo kusema kwa hakika ni kwamba ilikuwa lugha ambayo Musa aliielewa.
Je, ilikuwa sauti ya mwanadamu au ilisikika kama ‘maji mengi’ kama Ezekieli alivyoieleza sauti ya Mwenyezi (Ezekieli 43:2)?
Nabii Eliya alimsikia akinena kwa sauti ndogo ya utulivu, hali Isaya aliandika kwamba alinena sikioni mwake (1 Wafalme 19:12 na Isaya 50:5).
Hakika, ni lazima iwe rahisi kuenenda katika mapenzi ya Mungu anapokusemesha kwa sauti isikikayo, kama alivyofanya kwa Musa na wengine wa siku za Agano la Kale. Ingekuwa rahisi kuenenda mwenendo wa imani katika hali kama hizo!
Je, ingekuwa hivyo kweli?
Labda ndipo Mungu angetutaka mengi zaidi kama tungeweza kuisikia sauti yake waziwazi. Tusingekuwa na udhuru wa kutotii, na utii wetu usingekuwa imani. Watumwa huwatii mabwana zao, lakini mara nyingi ni kwa sababu ya hofu. Huo si aina ya utii ambao Bwana anaudai.
Yeye anatafuta watu ambao wamejiandaa kuisikia sauti yake rohoni na ambao asili yao yenyewe imekuwa utii.
Si utii utokanao na hofu, bali utii utokanao na tabia. Haijawahi kuwa katika asili yake kuwalazimisha au kuwashawishi watu wake watende mapenzi yake au waenende sawasawa na makusudi yake. Sikuzote amewapa uhuru wa kuitikia kwa upendo na utii wa hiari. Imani impendezayo Mungu haionekani katika utii wa hofu, bali katika utii wa upendo na hiari.
Tommy mdogo alikuwa hana utulivu mezani wakati wa chakula cha jioni kwa kuwa alitaka kurudi nje kwa rafiki zake waliokuwa wakimngoja. “Huwezi kuondoka mezani mpaka umalize chakula chako,” mama yake akasema.
Tommy akameza chakula chake haraka. “Na uketi kitini pako unapokula,” baba yake akaongeza. Tommy alikuwa mzito kutii, hivyo baba yake akayarudia maagizo kwa sauti, iliyokuwa ya taratibu kidogo na ya juu kidogo. Bado Tommy aliegemea kando ya kiti chake, macho yake yakikaza kuwatazama rafiki zake nje ya dirisha, huku akijaza mdomoni mwake uma mwingine uliojaa spageti.
Sauti ya baba yake ikawa kali zaidi, akanena kwa msisitizo. “Nimekuambia uketi unapokula! Fanya nikuambiavyo sasa hivi!”
Tommy akaketi, akiwa na sura ya kununa juu ya uso wake uliochafuliwa na nyanya. Mdomo wake ulikuwa umejaa hivyo hakuweza kusema, lakini ndani ya kichwa chake sauti ikapaza, “Huenda nimeketi kwa nje, lakini kwa ndani nimesimama!” Bila shaka si mtazamo wa utii ungeompendeza baba!
Sauti Ndogo ya Utulivu Nabii Eliya alikuwa amemwona Mungu akifanya muujiza mkuu mbele ya manabii wote wa Baali. Alikuwa hodari katika kuwaua viongozi hawa wote wa uongo, na “mkono wa Bwana ulikuwa juu yake” (1 Wafalme 18:46). Lakini, aliposikia kwamba Yezebeli, yule malkia mwovu, alikuwa akitafuta kuutoa uhai wake, alikimbilia jangwani ili kujificha na kuomboleza. “Yatosha, Bwana,” akalia. “Uniondolee uhai wangu!” Bila shaka si jambo ambalo mtu angelitegemea kutoka kwa ‘mtu wa imani’! Kwanza, malaika anatumwa kuuliza kwa nini yumo katika hali hii, kisha Bwana Mwenyewe anena na Eliya - si katika ule upepo mkuu uliopasua mlima, wala katika tetemeko la nchi, au moto, bali katika sauti ndogo ya utulivu. Hakika, matukio hayo matatu ya kwanza yangalimtia hofu kubwa naye angeitika haraka kama Mungu angalinena, lakini sauti ndogo ya utulivu haitishi. Anaamriwa arudi Dameski na kumtia mafuta mrithi wake, Elisha. Hivyo, Eliya anaurudisha bidii yake kwa Bwana, kwa maana ameisikia sauti yake. Utii wake ni ule wa imani.
Nakumbushwa juu ya ‘Tomaso mwenye shaka,’ yule mtume ambaye hakutaka kuamini kwamba Bwana amefufuka kutoka kwa wafu mpaka aweze kumwona na kutia vidole vyake katika alama za misumari za mikono iliyojeruhiwa. Yesu alipotokea mbele yake, Tomaso hatimaye aliamini, naye Yesu akamwambia, “Tomaso, kwa sababu umeniona, umesadiki; heri wale wasioona, wakasadiki.”
Angeweza pia kusema, “Heri wale ambao hawajaisikia sauti isikikayo ya Mungu, na bado wametii!”
Mwenendo na maisha ya imani impendezayo Mungu huonekana katika mwanamume au mwanamke ambaye, ‘hakusikia’ (kwa sikio) na bado ametii.
Je, twapaswa kutazamia kuisikia sauti ya Bwana? Bila shaka twapaswa! Ni Yesu Mwenyewe aliyesema kwamba “kondoo wangu waisikia sauti yangu” (Yohana 10:27).
Bwana anapotaka kuwasiliana nasi, kutufundisha mapenzi yake, kutuongoza katika njia zake, huchagua kutofanya hivyo kwa sauti kuu, bali kwa sauti ndogo ya utulivu, isikikayo tu na nafsi iliyopatana naye. Anataka kuwasemesha kondoo wake na wengi wao, nina hakika, wanataka kuisikia sauti yake.
Mawasiliano sikuzote ni jukumu la yule anayewasilisha ikiwa yule anayepokea yu tayari kusikia. Ndiyo maana mwalimu mzuri sikuzote atatafuta kujua kama wanafunzi wake wameelewa aliyojaribu kuwafundisha.
Basi, je, Mungu anatusemesha sisi, kondoo wake? Kama ndivyo, kwa nini hatusikii asemayo?
Kujifunza Kuitambua Sauti Yake Naamini ananisemesha kila siku, lakini mara nyingi sauti yake huzamishwa katika mvurugano wa sauti nyingine zipitazo kasi kichwani mwangu.
Nahitaji kujifunza siri ile ambayo Mababa wa Jangwani waliinena na kuiandika, fumbo lililoeleweka na wanaume na wanawake wale wa historia ya Kanisa, ambao maisha yao yametugusa kwa kuwa katika ushirika wa kina na Mungu; wale walioitwa, mara nyingi kwa dhihaka, wafumbo.
Mababa (na Mama) wa Jangwani walikuwa wanaume na wanawake wa Karne ya Nne. Wakati ambao Ukristo ulikuwa umekubaliwa na wafalme wa Kirumi na Jumuiya ya Kikristo kama mfumo wa kisiasa na wa kidunia ilikuwa imezaliwa. Ili kuwa watiifu kwa maelewano yao ya amri ya Bwana ya “kujitwika msalaba wake,” (Luka 9:23) walikuwa wamejitenga na ulimwengu na sauti zake zote ili kutafuta upweke katika jangwa la Misri. Kwao, upweke haukuwa kuwa peke yao, bali kuweza kumkaribia Mungu kiasi kwamba wangekuwa hawawatambui watu wengine wote waliowazunguka. Walijifunza kutulia, kukuza ukimya wa ndani, kumtafakari na kuisikia sauti yake.
Nina hakika hatuhitaji kujitenga katika maisha ya kimonaki, lakini twahitaji kutumia wakati wa maana ikiwa tutajifunza kuitambua sauti yake. Hatuhitaji akili kubwa ielewayo theolojia yote, wala hatuhitaji diploma ya Chuo cha Biblia au shahada ya Seminari. Anena, si kwa akili na fikira, bali kwa roho ambako Roho wake huwasiliana na roho zetu.
Ili Kuisikia Sauti Yake, Twahitaji 1. Njaa - shauku - ya mapenzi yake.
2. Moyo uliokusudia kuwa mtiifu kwa lolote alitakalo.
3. Wakati wa kutumia katika Neno lake.
4. Mahali tulivu pa kutafakari.
5. Ukimya wa ndani na upweke.
“Bwana Aliniambia…” Hakuna kitu kinachomsumbua mchungaji kama kuwa na mtu anayekujia, eti kwa ushauri, ambaye anaanza mazungumzo kwa kusema, “Bwana aliniambia…” mwisho wa mazungumzo!
Kwa kawaida hujaribu kuwauliza jinsi Bwana alivyowaambia, ili tu kugundua kwamba, kwa maoni yangu, halikuwa zaidi ya wazo walilokuwa nalo, huenda likitokana na hisia za mkutano fulani au mazungumzo na rafiki, lakini mara chache likitokana na Bwana. Laiti tungekuwa wepesi zaidi kuuliza swali kama hilo kila watu wasemapo, “Bwana aliniambia,” huenda tungewazuia watu wasiwe wepesi hivyo katika kutumia maneno hayo.
Kwa miaka minne, mimi na mke wangu tulipata pendeleo kubwa la kufanya kazi katika Meli ya Rehema iliyosafiri kati ya Ulaya na Afrika Magharibi. Ndani ya meli walikuwepo madaktari, wapasuaji, na wauguzi waliojitolea ujuzi wao katika kufanya upasuaji uliobadilisha maisha kwa mamia ya watu wasiobahatika ambao hawakuweza kumudu gharama kubwa za upasuaji ambazo maradhi yao yalihitaji. Ingawa ulikuwa wakati wa kuridhisha sana, kulikuwa na siku nyingi za msongo mkubwa na uchovu, lakini kwa wale wa mataifa yaliyoendelea waliopokea taarifa za kazi iliyokuwa ikifanywa na wafanyakazi wa afya na wafanyakazi wengine wa meli, ni lazima ilionekana kuwa huduma yenye mvuto sana.
Nawakumbuka wengi sana waliokuja kufanya kazi katika meli ambao walisema kwamba walikuwepo kwa sababu Bwana alikuwa amewaambia waje.
Sikuzote ilinishangaza ni wangapi kati yao waligundua, muda mfupi tu baadaye, kwamba hapo hapakuwa mahali walipotaka kweli kuwa.
Ni dhahiri kwamba, ama Bwana alikuwa amefanya kosa fulani, au walikuwa wameichanganya sauti yake na nyingine.
Nimekuwa na wengine walioniambia kwamba Bwana alikuwa amewaambia wafanye jambo lililokuwa kinyume cha Maandiko! Mimi binafsi nawajua wanawake wawili walioachana na waume zao kwa sababu “Bwana aliniambia,” ingawa hakukuwa na ushahidi wowote wa uzinzi au ukatili. Mume mmoja alikuwa mwamini, lakini alikuwa ameingia katika mpango wa kibiashara (uliokuwa halali kabisa) pamoja na asiyeamini. Mke alidai kwamba Bwana alikuwa amemwambia amwache mume wake kwa sababu alikuwa “ameungwa nira isivyo sawa” na asiyeamini! Ni matumizi mabaya ya Maandiko kama nini, na bila shaka si mapenzi ya Bwana kwa ndoa yoyote!
Waamini wengi hutumia maneno haya kwa unyoofu, wakiamini kwamba wameongozwa na Mungu. Huenda ikawa kupitia ndoto, kutiwa moyo na rafiki, mazingira, mstari wa Maandiko kujitokeza waziwazi, ‘sadfa,’ au tu shauku ya ndani ya binafsi inayozidi kukua.
Njia hizi zote ni za kweli, ikiwezekana kwa pamoja, ambazo Bwana aweza kutuongoza kuenenda katika mapenzi yake; hata hivyo, ingekuwa vema kusema “Naamini Bwana angependa nifanye hivi…” badala ya maneno yale ya ‘kiroho,’ “Bwana aliniambia…” ambayo huenda yakaufanyia mengi ubinafsi, lakini mara nyingi ni yenye kuharibu sana ushuhuda wa Kikristo.
Nafasi hiyo adimu ni ushuhuda wa binafsi.
Katika maisha yangu, nimekuwa na mfululizo wa matukio ambapo niliutambua uwepo wake kwa namna ya zaidi ya kawaida. Niruhusu nisisitize kwamba ni adimu, si jambo la kawaida. Mara mbili nimemsikia akinisemesha kwa sauti isikikayo. Sijaribu kuyaeleza haya, na kwa hakika si kwa sababu mimi ni wa kiroho zaidi nyakati hizo kuliko nyakati nyingine.
Kwa kweli, nyakati zote mbili zilikuwa nilipokuwa na moyo mzito. Nitakuelezea juu ya mojawapo yao.
Ilikuwa mwaka wa 1983 nami nilikuwa mchungaji wa kanisa dogo la Christian and Missionary Alliance huko Sidney katika Kisiwa cha Vancouver, British Columbia, kwa muda wa chini ya mwaka mmoja. Walikuwa kusanyiko lenye uchangamfu na upendo, nasi tulikuwa tumejenga uhusiano wa kina na wengi wao. Lakini, matarajio ya kanisa kukua kwa idadi hayakuwa mazuri, kwa kuwa kulikuwa na ‘kizuizi’ juu ya uendelezaji wa ardhi ya eneo hilo na majengo yaliyofaa yalikuwa machache.
Kwa kweli, tulikuwa tukikutana katika makao makuu ya wenyeji ya Free Masons! Sikuwa nikipokea mshahara mkubwa, lakini ilikuwa dhahiri kwamba karibuni, matumizi machache ya kanisa yangezidi mapato yao yaliyokuwa machache hata zaidi. Kusanyiko hili dogo lilikuwa tawi lililotokana na kanisa kubwa zaidi la mji jirani wa Victoria, mji mkuu wa jimbo, lakini sasa kulikuwa na uhusiano mdogo kati ya makanisa hayo mawili, achilia mbali ahadi yoyote ya kanisa mama kugharamia matumizi ya kanisa binti.
Ilikuwa jioni ya Jumapili yenye manyunyu mwishoni mwa Novemba. Anne alikuwa amewapeleka binti zetu watatu kwenye mkutano katika kanisa mama huku mimi nikaamua kutembea na kuzungumza na Bwana kuhusu uzito uliokuwa ukizidi kuongezeka moyoni mwangu. Je, nirudi kwenye ualimu?
Labda kwa muda usiokamili ili kuongeza kipato changu kusudi kisiwe mzigo mkubwa hivyo kwa kanisa? Je, nijiuzulu na kutafuta nafasi nyingine, nikiliambia kanisa kwamba, kwa wakati huu, hawangeweza kumudu mchungaji wa muda wote? Je, niweke ‘ngozi ya kondoo’ ili kujaribu kuyatambua mapenzi ya Mungu? Akili yangu ilikuwa imejaa maswali, lakini sikuwa nikipokea jibu lolote!
Hatua zangu zilinipeleka hadi kileleni pa mahali pazuri pa eneo hilo ambapo mtu angeweza kutazama nje juu ya nchi yote iliyozunguka.
Kilima cha Bear Hill kilikuwa kimekuwa mahali petu pendwa pa kujitenga, na ilikuwa juu ya kilele chake nilipopumzika. Hapo, nilikuta ‘kichaka changu kilichokuwa kikiwaka moto.’ Nilisikia sauti isikikayo!
Maneno yake yalikuwa wazi na yalirudiwa ili niweze kuyaelewa waziwazi.
Ingawa roho yangu ilishuhudia kwamba huu ulikuwa wakati wa Kimungu, nilitazama huku na huku kuona kama kulikuwa na mtu mwingine yeyote juu ya kilima pamoja nami. Hakukuwa na mtu mwingine yeyote. Bwana alikuwa akinena, na maneno yake yalikuwa wazi.
“Utachunga Kanisa la Victoria Alliance!”
Hakukuwa na maelezo jinsi jambo hili lingetokea. Wakati huo, Kanisa la Victoria Alliance lilikuwa na wachungaji watatu na yule mkuu alikuwa amekaa hapo kwa muda wa mwaka mmoja hivi. Yeye alikuwa na shahada ya uzamili katika theolojia hali mimi sikuwahi kwenda seminari na nilikuwa nimetawazwa hivi karibuni tu. Labda Mungu hakuwa akinena juu ya wakati wa sasa na maneno yake yalihusu tu wakati ujao? Jambo hilo lingeyajibuje maswali yangu ya sasa?
Labda alimaanisha kwamba nilipaswa kumwendea yule mchungaji mkuu na kupendekeza kwamba kanisa mama lichukue tena kanisa binti, na kwamba mimi nipokelewe kuwa mchungaji wao wa nne? Hivyo ndivyo mawazo yaliyokuwa yakipita kasi akilini mwangu niliporudi nyumbani.
Nilimwambia Anne juu ya tukio langu nasi tukaamua kunyamaza juu ya jambo hili, tukiamini kwamba kama Bwana alikuwa amenena kweli, aliweza kabisa kutimiza makusudi yake bila kuingilia kwetu. Wazia mshangao wetu majuma machache tu baadaye, kusikia kwamba yule mchungaji mkuu alikuwa ametangaza kujiuzulu kwake katika kanisa la Victoria!
Tulishawishika kumpigia simu kila mtu katika kanisa hilo ili kuwaambia kwamba tulijua ni nani angekuwa mchungaji wao ajaye, lakini tukaamua kwamba busara ilikuwa chaguo bora zaidi na hivyo tukabaki kimya. Kama tahadhari ya ziada, tulijiepusha na kanisa hilo katika miezi iliyofuata, ili tusije tukashawishika kuyaendesha hali yao kwa kuleta ‘mapenzi ya Mungu’ kwa ajili yao.
Ilikuwa miezi kadhaa baadaye ambapo Msimamizi wa Wilaya alipiga simu kunialika kuchunga Kanisa la Victoria Alliance. Mara moja nikaitikia kwa ndiyo, jambo lililomfanya aseme, “Hilo lilikuwa haraka!”
“Ndugu,” nikasema, “nilijua miezi minne iliyopita!”
Katika miaka yangu saba katika Kanisa la Victoria Alliance, kulikuwa na nyakati nyingi ambazo nilishawishika kuondoka, lakini nilibaki kwa sababu nilijua kwamba Bwana alikuwa ameniita hapo na niliamini kwamba angeniita nitoke wakati wa kuondoka ukifika. Hatuna shaka kwamba, mwaliko ulipokuja mwaka wa 1990 wa kutumika ndani ya Meli ya Rehema, ulikuwa wakati wake wa kusonga mbele.
Kwa nini Mungu alinena kwa sauti isikikayo? Kwa hakika haikuwa kwa sababu mimi nilikuwa wa kiroho zaidi ya wengine wala kwa sababu ndipo tu aligundua uhitaji wangu! Labda, labda tu, ilikuwa kwa sababu uzito wangu ulikuwa halisi kiasi kwamba ulikuwa umenifikisha mahali pa upweke nilipohitaji; mahali pa utupu wa ndani na ukimya ambapo ningeweza kumsikia akinena. Labda, ulikuwa tu tendo lake huru la kunena ndani ya maumivu yangu kutokana na upendo wake mkuu.
Kusimulia hadithi hii kunanikumbusha maneno niliyowahi kuyasikia yakinenwa na Floyd McClung, ambaye zamani alikuwa mwalimu mashuhuri katika Youth With A Mission. Alikuwa akinena juu ya somo la unabii, lakini maneno yake yangeweza kabisa kuhusika na hali yangu ya kuisikia sauti ya Mungu.
Alisema kwamba kila upokeapo neno la unabii, liweke katika droo ya chini na uifunge droo hiyo! Halikutolewa kwako kwa ajili ya mwongozo, lilitolewa kwako ili kuijenga imani yako.
Utafika wakati ambapo utahitaji kukumbuka, huenda katika hali ngumu, kwamba Mungu alitoa neno hilo. Ndipo waweza kuwa na uhakika kwamba amekuleta mahali hapa, na kwa hakika kabisa aweza kukupitisha salama.
Naamini haya kuwa maneno yenye hekima sana, yanayohitajika mno katika siku hizi za unabii mwingi wa binafsi unaotolewa kutoka kwenye mimbari za hadhara. Kuna waamini wengi sana waliochanganyikiwa sana na maneno ya maarifa na unabii yaliyonenwa juu yao, yakiwa na ushahidi mdogo wa kutimia kwake, na uwajibikaji mdogo kwa upande wa watoaji wake. Kipawa cha kiroho kinachohitajika kweli leo ni kile cha ufahamu wa kupambanua.
Tumaini langu katika Bwana halijajengwa juu ya matukio haya adimu sana, badala yake, limejengwa juu ya uhakika kwamba ananiongoza kila siku ninaposhikilia mkono wake. Silazimiki kuisikia sauti yake kwa masikio, lakini ni jambo la muhimu kwamba roho yangu ipatane na yake ili aweze kuniongoza.
Maombi ya Pamoja Mojawapo ya baraka kubwa nilizozipokea ni katika eneo la maombi ya pamoja. Nilipokuwa mwamini kijana, niliona mikutano mingi ya maombi kuwa yenye kuchosha kwani mara nyingi kulikuwa na sala za kujirudia na ushahidi mdogo wa Mungu kujibu. Mambo yalibadilika Bwana alipoanza kufanya kazi ya ajabu miongoni mwa vijana wa kanisa letu. Wanaume na wanawake hawa vijana walianza kuombeana kwa namna ya kushangaza. Ilipodhihirika, walikuwa wakisikia msukumo wa ndani wa Bwana katika mambo waliyopaswa kuyaombea. Nilianza kutambua nguvu iliyomo katika maombi ya pamoja wakati wale wanaoomba wanaisikia kwa pamoja sauti ya Mchungaji.
Nilikuwa nikiongoza Shule ya Missions Bridge, ambapo lengo letu lilikuwa kuwafanya wanafunzi waamini wenye shauku na kuwapa ‘uzoefu’ wa umisheni katika taifa linaloendelea, au la ulimwengu wa tatu. Jioni moja mada yetu ilikuwa maombi ya pamoja, hivyo niliwafundisha wanafunzi kumi na wawili zoezi nililokuwa nimejifunza katika kanisa langu la kwanza. Tulinyamazisha mioyo yetu katika sala tulivu kisha nikasoma zaburi ya kutafakari.
Kisha wanafunzi waliagizwa kutafakari kwa ukimya kwa muda wa dakika kumi na tano zilizofuata wakiitumia zaburi kama msingi wa kutafakari kwao. Baada ya kumalizika kwa dakika kumi na tano - muda mrefu sana kwa wengi wetu tusiozoea zoezi kama hilo - nilimwomba kila mtu atueleze mawazo yake. Walipaswa kuelezea picha zozote, kusimulia hadithi zozote, au kunukuu Maandiko yoyote waliyokuwa wamepokea, bila kujaribu kutafsiri mawazo yao kwa namna yoyote.
Kila mmoja alipoeleza mawazo yake, nilianza kutafuta mtindo fulani.
Mke wangu, Anne, alikuwa wa mwisho kunena. Yeye hana mazoea ya matukio ya kiroho ya kimuujiza, lakini jioni ile alieleza juu ya kuona maono ya meli nyeupe ikisafiri juu ya maji meusi karibu na pwani ya Victoria, nami nilikuwa nimeona wingu jeusi likiondoka juu ya mji likidhihirisha meli nyeupe juu ya maji yake!
Nilifupisha mawazo yao kwa maneno kama haya: “Inaonekana kwamba tuna dhamira nne zipitazo katika kutafakari kwetu. Baadhi yenu mmenena juu ya serikali zetu, za shirikisho na za jimbo, watu wetu wenyeji na meli hii; najiuliza tutaombaje.”
Jioni ile marafiki wawili wapendwa walikuwa wamekuja bila kutazamiwa kututembelea mimi na Anne na sasa hivi walikuwa wameketi pembeni ya darasa. Robin na Anne Jones waliishi upande wa juu wa kisiwa, lakini walikuwa wakitumia jioni hiyo huko Victoria, wakihudhuria darasa hili la Mission Bridge, ingawa si kama wanafunzi. Anne akasema, “Gareth, tafadhali nisamehe kwa kuingilia, lakini nadhani Robin ana jambo la kuvutia sana la kushiriki.”
Nilimwalika Robin anene hivyo akatuambia sababu yao ya kuwepo Victoria jioni ile. “Usiku wa manane, nitakuwa katika uwanja wa ndege wa Victoria pamoja na wanasiasa wawili wa eneo hili (wa jimbo), tukiwapokea wanasiasa wawili wa shirikisho wanaokuja kujadili ununuzi wa meli. Hii itatumika kuendeleza huduma kwa watu wenyeji ambao wapo chini ya mahakama. Badala ya kuwapeleka gerezani wakosaji wa mara ya kwanza, twataka kuanzisha huduma ya Kikristo ya kuwapeleka baharini kwa muda wa majuma matatu, tukiwafunza ujuzi wa ubaharia na kuwafundisha kanuni za Kikristo. Hii itagharamiwa kwa pamoja na serikali za jimbo na za shirikisho.”
Tulikuwa tumesikia kutoka kwa Mungu! Alikuwa ametufunulia moyo wake, nasi tukajua jinsi ya kuomba. Darasa lile la Mission Bridge liliiombea huduma hiyo hata ikawepo, kwa maana alikuwa ametupa imani iliyolingana na uhitaji.