Sura 16 · dakika 9 za kusoma
Musa
«Kwa imani Musa alipozaliwa alifichwa miezi mitatu na wazazi wake, kwa sababu waliona ya kuwa ni mtoto mzuri; wala hawakuiogopa amri ya mfalme. Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.
Kwa imani akatoka Misri, hakuiogopa hasira ya mfalme; kwa maana alistahimili kama amwonaye yeye asiyeonekana. Kwa imani aliiweka Pasaka, na kuinyunyiza ile damu, ili yeye aangamizaye wazaliwa wa kwanza asiwaguse. Kwa imani wakavuka bahari ya Shamu kama katika nchi kavu; ambayo Wamisri walipoijaribu kuivuka wakamezwa (Waebrania 11:23-29).
Hapa panaanza muhtasari wa maisha ya Musa, rafiki wa Mungu.
Habari kamili inayogusiwa na Maandiko mafupi hapo juu inapatikana katika Kutoka 2-14.
Baada ya kuzaliwa kwake katika Misri, Farao aliyekuwa akitawala nchi ile alitoa amri ya kuwa watoto wote wachanga wa kiume wauawe, kwa kuogopa ya kwamba huenda siku moja Wayahudi wangezidi kuwa wengi mno na kuinuka kwa nguvu juu ya Misri. Lakini wakunga walimwogopa Mungu, hivyo hawakufanya kama Farao alivyowaamuru. Mungu aliwabariki kwa tendo hili, na watu wa Kiyahudi wakaongezeka nguvu sana.
Jamaa moja ya Kiebrania iliyokuwa na mwana mchanga ilimficha katika manyasi kwa imani mpaka wakati ambapo Mungu alimdhihirisha yule mtoto aliyefichwa kwa binti wa Farao (Kutoka 1-2). Ni Mungu aliyemwongoza huyu Mlawi na mkewe wamfiche mtoto wao mahali ambapo Mungu angepaamuru; angepatikana na yule binti mfalme.
Imani yao inadhihirishwa katika jinsi walivyoutii msukumo huu wa ndani.
Musa alipokuwa mtu mzima, aliongozwa na Mungu kuwa mchungaji katika nchi ya Midiani (Waebrania 11:27). Huko alikaa mpaka umri wa miaka themanini, akichunga kondoo wa baba mkwe wake, Yethro (Kutoka 2:11-3:1). Habari ya kawaida ya matukio inatuambia ya kuwa Musa alikimbia kwa hofu kutoka kwa Farao kwa sababu alikuwa amemwua mtu! Ingawa alilelewa nyumbani mwa Farao, alikuwa amefundishwa na watumishi wa Kiebrania - mama yake mwenyewe akiwa miongoni mwao - naye alijijua kuwa mtoto wa watu wa Kiebrania. Alihisi kuvutwa kwa ndani kuelekea watu wa uzazi wake ijapokuwa alizungukwa na fahari na utajiri wa Misri. Shauku ya namna hiyo ililipuka kuwa jeuri ya kuua, na upweke wa kukimbia.
Siamini ya kuwa Maandiko yanapingana, hivyo ni lazima tuisome habari iliyomo katika Waebrania 11 kama inayoonyesha uongozi wa Mungu katika maisha ya Musa ili asije akaonja ghadhabu ya Farao. 'Kuogopa,' maana yake kuonja ghadhabu ya Farao.
Mwandishi wa Waebrania anayaangalia matukio hayo kwa kutazama nyuma, naye aweza kuona, katika matukio yote ya maisha ya Musa, mkono ulio dhahiri wa Mungu ukiongoza. Anamwandaa mtu kwa ajili ya utume.
Historia iliyofuata inaonyesha kwa nini Mungu alimtoa kutoka nyumbani mwa Farao, ijapokuwa tendo lililosababisha hilo lilikuwa jeuri ya Musa mwenyewe.
«Maisha yaliyopotea bure kama nini!» huenda tukasema tunapomtazama mtu huyu, aliyefunzwa katika nyumba ya Farao, mwenye ustadi wa kujimudu katika kundi lolote la watu wenye vyeo. Badala yake, twamkuta akifanya kazi kama mchungaji, akichunga kondoo. Hili alilifanya kwa miaka 40 'iliyopotea bure'!
Lakini hakuna kinachopotea bure Mungu anapokuwa ndiye mtawala. Ni mafunzo gani yaliyo bora zaidi ambayo yangeweza kuwapo kwa ajili ya utume ambao Mungu alikuwa akiuandaa?!
Alitaka mtu aliyezijua njia za nyua za Farao na ambaye angeweza kuwaongoza mamilioni ya kondoo wenye miguu miwili wanaolia kwa miaka arobaini jangwani!
Kila badiliko la mwelekeo katika maisha ya Musa lilikuwa limeamriwa na Mungu; alikuwa akimwandaa mtu maalumu kwa kusudi maalumu, naye alikuwa amemchagua mtu sahihi, kwa maana aliujua moyo wa mtu huyu na ya kuwa angeweza kuaminiwa kuufuata uongozi wake kwa imani.
Lakini kwanza, ilipasa kuwepo kile kijiti kilichokuwa kikiwaka moto (Kutoka 3:2), ambapo Mungu alipata shida kubwa ya kumshawishi mtumishi wake awe na ujasiri zaidi katika uwezo na uongozi wake (Kutoka 3:11; 4:1, 10, 13 na zaidi). Angalia Kutoka 4:14, Mungu alikasirika kwa sababu ya Musa kukosa 'kuamini'!
Katika mstari wa 28 Musa alitii alipoamriwa kuiadhimisha Pasaka kwa kunyunyiza damu juu ya miimo ya milango ya kila nyumba ya Kiebrania katika Misri (Kutoka 12). Angeweza kumhoji Mungu juu ya amri hii isiyo na maana, lakini hakufanya hivyo.
Hii ndiyo imani.
Sasa katika mstari wa 29 anaanza kuonyesha ujasiri na kumtumaini Mungu zaidi (Kutoka 14:13), lakini msisitizo wa mstari huo ni ya kwamba Mungu aliifungua bahari na kuwafanya Wamisri wazame, si kwa sababu Musa aliuamini jambo hilo hata likawa. Yeye alitii tu alipoambiwa la kufanya, baada ya kumlilia Mungu katika kukata tamaa kwake. Aliuweka ufito wake katika maji ya Bahari ya Shamu hata maji yakagawanyika na Waebrania wakaweza kuvuka katika nchi kavu (Kutoka 14).
Angeweza kumhoji Mungu juu ya amri hii isiyo na maana, lakini hakufanya hivyo. Hii ndiyo imani.
Haishangazi Musa aliitwa «rafiki wa Mungu» (Kutoka 33:11). Maisha yake yote ni mfano wa kwenda kwa imani.
Ni kanuni gani tuwezayo kujifunza kutokana na mfano wa Musa?
Bila shaka, ni kwamba Bwana anatembea mbele ya watu wake wanapotembea katika imani. Anawaongoza ili apate kuwatumia kwa sifa ya utukufu wake. Atawaleta mpaka mahali pa hatima aliyowapangia. Nyakati nyingine anaongoza kupitia mang'amuzi ya bondeni, nyakati nyingine njia zake si za kupendeza na hazina sababu, lakini anaijua njia tuiendeayo.
«Mungu anapotaka kummudu mtu na kumsisimua mtu na kumstadishi mtu; Mungu anapotaka kumfinyanga mtu acheze fungu lililo tukufu kuliko yote; Anapotamani kwa moyo wake wote kumuumba mtu mkuu na jasiri kiasi hata ulimwengu wote utashangaa, Tazama mbinu zake! Tazama njia zake!
Jinsi anavyowakamilisha bila huruma - wale awachaguao kifalme; jinsi anavyompiga nyundo na kumuumiza na kwa mapigo makuu kumgeuza kuwa mabonge ya udongo wa mfinyanzi ambao Mungu peke yake ndiye awezaye kuuelewa!
Wakati moyo wake uliochoka mateso unalia, naye ananyosha mikono ya kusihi!
Jinsi anavyowapinda, lakini kamwe hawavunji wale ambao wema wao anaushughulikia; jinsi anavyowatumia wale awachaguao na kwa kusudi la upendo anawayeyusha, huishawishi nafsi yake iliyolemewa ijaribu utajiri wa Mungu.
Mungu anajua analolifanya!»
(Mwandishi hajulikani) Miamba Miwili Tendo pekee lililoandikwa katika maisha ya Musa ambalo hakuitii amri ya Mungu linapatikana katika Hesabu 20. Tendo hili la kutotii lilimgharimu tamaa yake iliyo kuu kuliko zote - kuingia katika nchi ya ahadi. Yafaa kulifikiri hili kwa undani zaidi, kwa kuwa kwa mtazamo wa kwanza linaonekana kuwa tendo dogo sana kutoka kwa Mungu ajiitaye rafiki ya Musa!
Katika Kutoka 17, muda mfupi baada ya Waisraeli kutoka Misri, walianza kunung'unika ya kuwa hawakuwa na maji ya kutosha ya kunywa. Mungu akamwambia Musa, «Tazama, nitasimama mbele yako pale juu ya mwamba katika Horebu; nawe utaupiga mwamba, na maji yatatoka ndani yake, ili watu wapate kunywa» (Kutoka 17:6). Musa akatii, na watu wakaweza kunywa.
Karibu miaka arobaini baadaye kwenye lango la kuingilia Kanaani, tukio kama hilo linatokea likiwa na matokeo ya aibu na maumivu kwa Musa.
Katika Hesabu 20, watu wananung'unika tena ya kuwa hawana maji. Maagizo ya Mungu kwa Musa wakati huu ni ya kwamba «Kitwae kile kijiti, ukakusanye mkutano pamoja, wewe na Haruni ndugu yako, mkauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake» (Hesabu 20:8). Badala yake, Musa kwanza aliwakemea watu kwa manung'uniko yao, kisha, akaugeukia mwamba, akaupiga kwa ufito. Hapana maji yaliyotoka! Katika aibu yake, akaupiga tena, na Mungu akaonyesha neema kwa kuyaruhusu maji yatiririke; lakini tendo hili la kutotii lilimfanya atangaze, «Kwa sababu hamkuniamini, hata kunitakasa mbele ya macho ya wana wa Israeli, kwa hiyo hamtaukusanya mkutano huu na kuuingiza katika nchi niliyowapa» (Hesabu 20:12). Ingawa Musa angemsihi Mungu ili apate kusamehewa na kuwa na furaha ya kuingia Kanaani, haikuwa hivyo (Kumbukumbu la Torati 3:23-26).
Wengine wangesema ya kuwa Musa alihukumiwa kwa sababu alikasirika na watu. Mimi siamini hivyo. Mungu ni mkuu mno kiasi cha kutomhukumu rafiki yake kwa jambo hilo! Ni tunapochunguza kwa kina zaidi kidogo ndipo tunapogundua ile kweli ya ajabu ambayo Bwana alitaka Musa aituonyeshe kwetu - picha aliyoiharibu kwa kutotii kwake.
Yatupasa kuifikiri ile miamba miwili na ile mifito miwili katika marejeo yaliyo hapo juu. Katika rejeo la Kutoka, neno la Kiebrania kwa mwamba ni “tsoor,” ambao ni jiwe lililo kali au la kukata. Ulikuwa kama mwamba wa jiwe gumu, kipande kidogo chake kingeweza kunolewa kuwa kisu. Jiwe la namna hiyo lingetumika kuua na kuwagawa wanyama wa dhabihu. Mungu alipofanya agano lake na Ibrahimu, ilikuwa kwa kuwakata wanyama vipande viwili, akiwatenga ili mwenge wa moto wa Mungu upite kati yao (Mwanzo 15). Hata leo, baadhi ya makabila ya Kiafrika yanapofanya mapatano ya kikabila, hutumia msemo «kukata agano.» Picha ya Kutoka 17 ni ya Mungu akisimama mahali pa lile jiwe kali akivumilia mapigo ya ufito wa Musa juu ya mwili wake.
Ni kivuli cha kupendeza kama nini kinachoashiria ile siku ambapo Mungu Mwokozi wetu angekata agano la milele kwa ajili yetu kwa kuvumilia mapigo ya Sheria katika mwili wake mwenyewe juu ya mti wa Kalvari! Maji ya uzima yalitiririka kutoka katika mwili ule uliovunjika; maji yawafanyayo wale wanywao «wasione kiu tena milele» (Yohana 4:14).
Katika rejeo la Hesabu, neno la Kiebrania kwa mwamba ni “selah,” ambao ni ngome, jabali refu, au boma imara. Ufito huu utakuwa ufito wa Haruni - ufito wa Kuhani Mkuu. Mfano wakati huu ni wa Mwokozi, aliye juu na aliyeinuliwa, ambaye twamwendea kwa mamlaka ya makuhani. Twanena na mwamba katika maombi na maombezi, shukrani na ibada, na maji yanatiririka.
Ni picha hii ambayo Musa alishindwa kuidhihirisha kwa kutotii kwake.
Mtume Petro aliandika, «Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki... [na sasa yeye yuko] mkono wa kuume wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake» (1 Petro 3:18,22).
Msifuni Mungu kwa kuwa kazi ya msalaba ni kazi kamili. Yesu hahitaji kuuawa tena. Sasa anatawala juu, na sisi twamwendea kwa macho yaliyoinuliwa, kuabudu kama wafalme na makuhani mbele za Mungu wetu - naye anaendelea kuyamwaga maji yake ya uzima.
Tuangalie kwa kupita ya kuwa Musa aliingia katika Nchi ya Ahadi, si katika maisha ya mwili bali katika maisha yaliyotukuzwa ya rafiki wa Mungu (Marko 9). Mwisho wa safari kwa wote watembeao kwa imani, ni kwamba watakuwa pamoja na Mwokozi wao, wakitukuzwa katika uwepo wake. Ijapokuwa Bwana aweza kuturudi, ni kwa kitambo tu ili apate kutufinyanga tuwe sura yake. Utukufu ujao ni hakika, kwa maana hukumu yote na laana vimepitishwa kutoka kwetu kwenda kwa Mwokozi!
Muhtasari Ni katika maisha ya Musa ndipo ninapoona mfano ulio dhahiri zaidi wa maisha ya imani. Katika maisha yake yote Mungu alikuwa amezielekeza hali zote zilizomfinyanga mtu apatane na moyo wake mwenyewe na kwa makusudi yake mwenyewe. Huyu kwa hakika ni mtu ambaye angekuwa «kuwa sifa ya utukufu wake» (Waefeso 1:12).
1. Mambo yote hufanya kazi pamoja kwa wema kwa wale watembeao kwa imani.
2. Rafiki za Mungu ni wale watembeao kwa imani.
3. Mungu anatafuta wanaume na wanawake awezao kuwafinyanga wawe vyombo vya utukufu wake.
4. Mchakato wa kufinyanga ni kazi ya imani.
5. Imani haituokoi kutoka patasi au nyundo ya yule Mchongaji wa Kimungu.