Sura 14 · dakika 6 za kusoma
Isaka na Yakobo
“Kwa imani Isaka alimbariki Yakobo na Esau kwa habari ya mambo yatakayokuja.
Kwa imani Yakobo alipokuwa akifa aliwabariki kila mmoja wa wana wa Yusufu; akasujudu, hali akiiegemea ncha ya fimbo yake” (Waebrania 11:20-21).
Nimewaleta hawa wawili pamoja kwa sababu wanatufundisha kanuni ileile.
Hadithi ya Isaka kumbariki Yakobo na Esau inapatikana katika Mwanzo 27 huku ile ya Yakobo kuwabariki wana wa Yusufu ikiwa katika Mwanzo 48.
Kuna kidogo cha kumsifu Yakobo. Alikuwa mdanganyifu na mwizi. Ilikuwa uamuzi wa Esau kuuza haki yake ya uzaliwa wa kwanza kwa bakuli la mchuzi, lakini ilikuwa hila ya Yakobo, aliyeshawishiwa na mama yake, iliyoiba baraka ambayo mtu angetegemea kupewa mzaliwa wa kwanza. Nina hakika hakuelewa kanuni ya Kibiblia ambayo Mungu alikuwa akienda kufundisha kupitia udanganyifu wake. Naiita “kanuni ya mzaliwa wa pili.”
Nusu karne baadaye, Yakobo anahusika tena anapowabariki wana wawili wa Yusufu. Yusufu anawaongoza wanawe wawili kuelekea kwa baba yake aliye kipofu, akihakikisha kwamba mvulana mkubwa, Manase, yuko mbele ya mkono wa kuume wa Yakobo, mkono wa baraka kuu, na mwana yule mwingine, Efraimu, yuko upande wa kushoto wa Yakobo. Hata hivyo mzee huyo, ingawa kwa nje ni kipofu, ana nuru ya ndani inayomwelekeza kuvipisha mikono yake na kutamka baraka iliyo kuu zaidi juu ya mzaliwa wa pili.
Kwa sababu fulani, Mungu anamwelekeza mzee huyo kufanya jambo lisilosikika kama hilo. Yusufu anapinga, lakini bila mafanikio. Yakobo atatii mwelekezo wa ndani. Narudia kwamba hakuna kitu kinachoonyesha kwamba anaelewa ni kwa nini avipishe mikono yake - hili linatangazwa kufanywa “kwa imani.”
Ni ipi kanuni ya mzaliwa wa pili?
Na tuwazingatie wale ambao Biblia inawaandika: Kaini alikuwa mkubwa, Habili mdogo. Mungu alimheshimu huyu wa mwisho kuliko yule wa kwanza.
Esau alikuwa mkubwa, Yakobo mdogo. Mungu alisema, “Esau nalimchukia bali Yakobo nalimpenda!”
Manase alikuwa mkubwa, Efraimu mdogo, lakini Efraimu alipokea baraka iliyo kuu zaidi.
Adamu ndiye mtu wa kwanza kuumbwa, na Yesu alikuja kama ‘Adamu wa pili,’ yaani mzaliwa wa pili.
“Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika kiama cha wafu kilikuja kwa njia ya mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa” (1 Wakorintho 15:21-22).
Hata katika siku za Agano la Kale, Mungu anaonyesha kimbele siku ambayo ‘Adamu wake wa pili’ atakuja kupinga mauti iliyowajia watu wote kwa sababu ya kutotii kwa Adamu wa kwanza.
Yeye, ‘mwana wa ahadi’ atashinda mauti kwa utii wake kwa mapenzi ya mwelekezo wa Mungu. Atakuwa mzazi wa taifa jipya la watu, wale “waliozaliwa mara mbili.” Kwanza kwa maji (kuzaliwa kwa asili), na pili kwa Roho (kuzaliwa upya). Imesemwa kwa kweli kwamba “ukizaliwa mara moja, utakufa mara mbili (yaani; mauti ya asili na ya milele), lakini ukizaliwa mara mbili, utakufa mara moja tu” (haijulikani).
Baraka za Mungu zinatamkwa juu ya wana wa mzaliwa wa pili.
Basi hapa kuna kanuni ya kuzaliwa upya ambayo pasipo hiyo “haiwezekani kuuona ufalme wa Mungu,” (Yohana 3:3) sembuse kuuingia. Adamu, mtu wa kwanza, ni mzazi wa wale “waliozaliwa kwa mwili” (Yohana 3:6). Yesu, mtu wa pili, ni mzazi wa wale “waliozaliwa kwa Roho” (Yohana 3:6).
Kwa maana mmezaliwa mara ya pili, si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, yaani, kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo (1 Petro 1:23).
Katika sura ya awali tuliona kwamba ukuu katika ufalme wa Mbinguni unatolewa kwa wale walio kama ‘aliye mdogo’ (Luka 22:26). Hivyo, katika matendo ya Isaka na Yakobo wote wawili ya kumbariki mzaliwa wa pili, Mungu anawasilisha tena kanuni iliyofundishwa baadaye na Yesu. Matendo yao ya ‘imani’ yalikusudiwa kutuonyesha aina ya watu tunayopaswa kuwa kama ‘waliozaliwa upya.’
Na tuangalie zaidi sifa za mzaliwa wa pili au aliye mdogo. Mtoto mdogo hana madai juu ya urithi kutoka kwa baba yake wa duniani. Cheo chake ni cha umaarufu na heshima kidogo. Yeye ni mtoto wa ‘kupewa vilivyotumika’ akipokea nguo na vitu vya kuchezea vilivyotupwa na ndugu yake mkubwa.
Shuleni wanaweza kujulikana kama ndugu wa “fulani,” bila utambulisho wao wenyewe. Mafanikio yao yanapimwa kwa kulinganishwa na ndugu mkubwa. Kama mtoto mpotevu, wanaweza kuondoka nyumbani na mali zao zote za duniani katika mfuko uliotundikwa begani mwao, huku ndugu yao mkubwa akibaki kutunza urithi wao, shamba.
Mtoto mdogo havutiwi na hali iliyopo, wala hafanyi kazi kisiasa kudumisha mali zao. Wao ni waasi kwa habari ya mifumo ya ulimwengu huu. Nakumbuka wakati Biblia ya Living Bible ilipokuwa ikitengenezwa. Kila kitabu cha Biblia kilichapishwa kando, kila kimoja na kichwa chake cha pekee.
Injili ya Marko, kuhusu Yesu kama mtumishi, ilipewa kichwa, “Yesu - Mwasi Mwenye Sababu.” Mama yake alitangaza kinabii, kwamba “angewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao, angewaangusha wenye enzi katika viti vyao vya enzi, na kuwakweza walio wanyonge. Angewashibisha wenye njaa kwa mema, na matajiri angewaondoa mikono mitupu” (Wimbo wa Mariamu - Luka 1:52-53). Hilo ni tangazo la vita kwa mifumo ya ulimwengu huu! Amekuja kuusimika ufalme wake, naye anawaita watu wake, waliozaliwa mara mbili, wasiridhike na jamii ya ulimwengu huu, bali kuishi Ukristo unaokwenda kinyume na utamaduni.
Ninapowazingatia wahusika wengine wa Kibiblia waliojulikana kwa kuwa aliye mdogo, wa chini kabisa, au wa mwisho, ninavutwa kwa mvulana mchungaji, Daudi.
Alikuwa mdogo kuliko wote kati ya wana wanane wa Yese (1 Samweli 16). Ni nani angeweza kuona kimbele hatima kama hiyo kwake wakati nabii Samweli alipokuja kumtia mafuta awe mfalme juu ya Israeli? Uzoefu pekee aliokuwa nao ulikuwa kuchunga kondoo, lakini hakuwa akipoteza wakati wake! Alikuwa akijizoeza kwa kombeo, akifanya kazi yake kwa uaminifu, na kulinda kondoo wa baba yake dhidi ya simba na dubu.
Ingawa alikuwa wa mwisho katika mstari wa kupewa vilivyotumika kamwe hakuonyesha kinyongo. Badala yake, alijifunza kukubali cheo chake na kungoja zamu yake. Bwana alimchagua awe mfalme kwa sababu alijua moyo wake. Kwa Samweli, Mungu alikuwa amesema, “Kwa kuwa BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana binadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo” (1 Samweli 16:7).
Daudi alikuwa amejifunza kumtumaini Mungu, hata wakati mazingira yalipoonekana kama majitu mbele yake. Kamwe hakukaza macho yake juu ya matatizo bali aliyaweka macho yake juu ya Bwana. Tumaini lake lilikuwa katika Bwana na katika kombeo, si katika silaha za Sauli ambazo hakuwa amezijaribu. Wewe umejaribu nini?
Neno la Mungu? Jina lake? Yatavumilia jaribu.
Daudi alipoingia katika jumba la Sauli, hakutaka kulazimisha ratiba ya Mungu. Alikuwa amejifunza kungoja! Usikimbie mbele ya Mungu; utatembea tu katika kivuli chako mwenyewe! Ingawa kulikuwa na fursa wakati ilipoonekana kwamba Mungu alikuwa akiweka kiti cha enzi mbele yake, Daudi bado angengoja, akisema, “Sitanyosha mkono wangu juu ya mteule wa Bwana” (1 Samweli 24:6). Hakukuwa na siasa kwake. Hiyo ndiyo njia ya ulimwengu - si njia ya watu wa Ufalme, na Mungu alijua moyo wa Daudi!
Muhtasari Kwa mwandishi wa Waebrania 11, wazee wa ukoo Isaka na Yakobo waliongozwa na Mungu kutamka baraka juu ya mzaliwa wa pili, hata kupitia udanganyifu wa Yakobo. Kanuni za Kibiblia ambazo Bwana angependa kutufundisha ni: 1. Amebarikiwa mtu aliyezaliwa mara mbili.
2. Baraka zetu ni kupitia Adamu wa pili aliyetukomboa kutoka laana ya Adamu wa kwanza.
3. Wana wa mzaliwa wa pili wanapaswa kuwa Wakristo wanaokwenda kinyume na utamaduni, wasioipenda mifumo ya ulimwengu huu na kuonyesha sifa za ‘aliye mdogo.’