Sura 12 · dakika 5 za kusoma
Ungamo la Imani
“Hawa wote walikufa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni na wasafiri juu ya nchi. Maana wao wasemao maneno kama hayo waonyesha wazi ya kuwa wanaitafuta nchi yao wenyewe. Na kama wangaliikumbuka ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurudi. Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao, kwa maana amewatengenezea mji” (Waebrania 11:13-16).
Yaonekana kwamba mwandishi wa kitabu hiki anawarejea wale ‘wengi’ wa mstari wa 12, wazao wa Ibrahimu na Sara waliokufa kabla ya kuja kwa Yesu, Masihi wao. Katika nyakati zao za imani na kumtumaini Yehova, walikiri uhitaji wao kwake, “wakikiri kwamba walikuwa wageni na wasafiri juu ya nchi” (Waebrania 11:13). Ikiwa walikuwa Misri, jangwani, au Babeli, wana wa Israeli walikuwa na shauku kubwa mioyoni mwao ya kurejea nyumbani, mahali pale walipoahidiwa katika maneno ya Mungu kwa Ibrahimu, lakini ni wachache tu kati yao ambao wangeweza kupata makao ya kudumu mahali pengine popote isipokuwa Kanaani au Palestina.
“Kando ya mito ya Babeli, ndiko tulikoketi, tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti ya mierebi iliyokuwako kati yake tuliitundika vinubi vyetu, kwa maana huko wale waliotuteka nyara walitutaka tuwaimbie nyimbo, nao waliotutesa walitutaka furaha, wakisema, ‘Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.’
Tuiimbeje wimbo wa Bwana katika nchi ya ugeni?” (Zaburi 137:1-4).
Wangaliweza kukaa katika nchi walimozaliwa, lakini moyo wa msafiri ulikuwa ndani yao. Hii ndiyo tabia ya wazao wote wa kweli wa Ibrahimu: kwamba hawajisikii kuwa nyumbani katika ulimwengu huu. Kumezaliwa ndani yao njaa ya mambo ya juu zaidi, mji wa mbinguni ambao mbunifu na mfanyaji wake ni Mungu.
Ni Mungu aliyeweka shauku hii ndani yao kwa tendo lake la kwanza la imani. Watu wa imani sikuzote wataitikia hamu hiyo.
Katika mafundisho yake juu ya imani yanayopatikana katika Warumi 4:1-12, mtume Paulo asema, “Tuseme nini juu ya Ibrahimu?” Alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki. Kwa yule asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye humhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake yahesabiwa kuwa haki.
Wakati huo, Ibrahimu hakuwa Myahudi aliyetahiriwa, hivyo alihesabiwa kuwa na haki hata kabla hajawa mwana wa agano (la Kiyahudi). Hii ilikuwa ili awe Baba, si wa waliotahiriwa (Wayahudi) tu, bali pia wa wale wote wanaohesabiwa haki nje ya agano (la Kiyahudi). Si kuishika Sheria (wala matendo yoyote mema) kunakomfanya mtu kuwa na haki: ni kwa imani tu. Kwa hiyo Ibrahimu anahesabiwa kuwa baba wa wote wanaohesabiwa haki kwa imani. Hivyo, hata kwetu sisi Watu wa Mataifa tunaoenenda kwa imani, ahadi ya Mungu iliyo msingi wake ni neema ni ya hakika. Tutairithi nchi!
“Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; kwa maana amewatengenezea mji” (Waebrania 11:16).
Umeshikamana kiasi gani na ulimwengu huu? Je, unapata thamani yako katika kiasi cha utajiri au ummaarufu wake unaoweza kukusanya? Je, unahitaji sifa na uthibitisho wake ili kukupa kujistahi? Au wewe ni mmoja wa wale ambao Yesu angemwita ‘mkuu’ katika ufalme wake?
Pindi moja wanafunzi wa Yesu walikuwa wakifanya jambo ambalo wengi wetu hufurahia. Walikuwa na mazungumzo ya kuvutia. Mtu angependa kudhani yalihusu jambo la maana kama vile usalama wa milele au unyakuo kabla ya dhiki, lakini hilo lingekuwa ni kuwapa sifa zaidi ya wanavyostahili. Kwa kweli, walikuwa wakigombana ni nani kati yao aliyekuwa mkuu zaidi (Marko 9:33-34)! Kwa sababu ya hili, Yesu alianza kuwafundisha maana ya kuwa mkuu katika ufalme wake, hapa duniani, na katika mji ule aliowatengenezea.
1. Wanapaswa kuwa watumishi, hata watumwa (Marko 10:42-45).
2. Ni lazima wawe tayari kuwa wa mwisho na wa chini kabisa (Marko 9:35 na Luka 9:48).
3. Ni lazima wajinyenyekeze kama mtoto mdogo (Mathayo 18:4).
4. Ni lazima wawe na moyo wa yule aliye mdogo (Luka 22:26).
Fundisho hili ni kinyume kabisa na miundo ya mamlaka ya ulimwengu huu na, kwa masikitiko, kinyume na mengi ya tunayoyaona katika uongozi wa kanisa leo. Wako wapi viongozi watumishi, wasiotafuta umaarufu au heshima kwa nafsi zao bali badala yake wanafurahia kuwa wa mwisho na wa chini kabisa wakati wengine wanapopokea sifa na shangwe? Wako wapi waaminio ambao, kama mtoto mdogo, ni wazi, hawawezi kudanganya kwa muda mrefu, hawana kinyongo, na hawachukizwi? Wako wapi walio wadogo ambao ulimwengu hauna vifungo juu yao na hawana hamu ya kudai haki zao au kudumisha msingi wa nguvu zao?
Wako wapi watu wanaoenenda kwa imani, wale ambao yeye haoni haya juu yao?
Ingawa watu hawa walihesabiwa kuwa wasafiri katika ulimwengu huu, walijua mambo matatu: 1. Walijua kwamba Mungu alikuwa amemwahidi Ibrahimu.
2. Walijua kwamba Yesu angeitimiza ahadi hiyo.
3. Walijua kwamba walikuwa na hatima tukufu - kukaa katika mji wa Mungu.
Nakumbushwa Yohana 13:3 ambapo Yesu, “akijua ya kuwa Baba amempa vitu vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye alikuwa akienda kwa Mungu” kisha aliondoka akawaosha wanafunzi wake miguu (Yohana 13:1-20)! Kuwa mtumishi hurahisika tu wakati mtu anapojua msimamo wake mbele za Mungu.
Je, unaweza kutazama nyuma mahali ambapo Mungu alianza kazi yake ya imani ndani yako alipokuleta msalabani? Je, unatazama mbele ukijua kwamba atakuleta katika hatima tukufu aliyokupangia?
Je, unaenenda katika imani inayoongoza kwenye hatima hiyo? Kuenenda si kwa nguvu zako mwenyewe, bali kwa msukumo wake ndani yako?
Imani hudai kwamba tuwe na maono ya ahadi za Mungu na shauku ya uwepo wake.
Muhtasari 1. Watu wa imani kamwe hawatajisikia kuwa nyumbani katika ulimwengu huu. Wao ni wasafiri, na kwa hiyo wataishi kwa kadiri hiyo.
2. Kamwe hawataki kurejea katika njia za ulimwengu, hila na siasa zake, mbinu na tuzo zake, au anasa na ahadi zake.
3. Mfalme anatangaza kwamba ili uwe mkuu ni lazima uwe na moyo wa mtumishi, wa mtoto, wa mwisho, wa chini kabisa, na wa yule aliye mdogo.
4. Kama wazao wa kiroho wa Ibrahimu - baba wa wana wa imani - tuna hatima kuu. Tutairithi nchi.
5. Ahadi kuu za Mungu huwafikia tu wale waliojifisha wenyewe.
6. Mungu haoni haya juu yetu!