Sura 15 · dakika 4 za kusoma
Hotuba ya Tatu
Kuna wingi mkubwa wa kwenda mikutanoni na kupata baraka humo, kisha kuondoka na kuishi vilevile kama zamani, hata mara nyingine sisi, ambao daima tumejishughulisha katika kujaribu kuwaleta watu karibu zaidi na Mungu, huondoka tukiwa tumevunjika moyo kiasi kwamba mioyo yetu inakaribia kupasuka.
Twahisi kwamba watu wanarudi tena kutoka mahali tulipowaongoza, badala ya kupiga hatua kwenda mahali ambapo Mungu anawaita. Wanakuja tena na tena, nasi tunakuwa kwao, kama vile Nabii asemavyo, chombo cha kupendeza sana, au kisichopendeza kabisa, kadiri iwavyo; na hivyo wanaondoka bila kupata cho chote. Hawapigi hatua yo yote ya hakika. Hatujawapatia karama yo yote ya kiroho. Hisia zao tu ndizo zimechochewa, na kwa sababu hiyo, wanaishi juma lijalo vilevile kama walivyoishi juma lililopita, na kushindwa na majaribu kama walivyofanya awali.
Je, ungeweza kudhani hata kidogo, kutokana na kusoma Agano Jipya, kwamba hiki ndicho kitu ambacho Mungu alikusudia katika maandalizi yake ya neema na wokovu? Je, hakuna lengo la hakika katika kila ahadi, onyo, na amri? Mungu ni wa hakika kabisa katika matakwa yake na ahadi zake, na katika maandalizi aliyoyafanya; hata hivyo wengi wa watu wa Bwana ni watu wasio na hakika daima na kwa kudumu. Wanakwenda huku na huku, kama mlango ulioning'inia kwenye bawaba zake, wala hawapati cho chote kutoka kwa Bwana.
Tunataka kabisa upate kitu kutoka kwa Bwana, nasi tuna hakika kabisa kwamba unaweza na utapata, ikiwa utatimiza sharti hilo. Bwana yu tayari kukupa kipimo hicho hasa cha neema, nguvu, na wokovu unachohitaji. Sasa kwa kuwa umefika kizingiti cha nchi ile njema, kuna kitu kimoja tu kinachoweza kukuzuia usiingie, ikiwa umeshafanya kujiweka wakfu kunakohitajika. Bila shaka, kama unashikilia jambo lo lote nyuma, basi huwezi kamwe kuingia mpaka uliache. Kama unang'ang'ania kitu fulani chenye shaka, wala humpi Mungu nafasi ya shaka hiyo, huwezi kamwe kuingia; lakini, kama unaliona hili, na kufanya kujiweka wakfu kunakohitajika, kama unaitamani kweli baraka hii, kuna kitu kimoja tu kinachoweza kukuzuia usiifurahie, nacho ni—kutokuamini.
Itasemwa juu yako, katika miaka ijayo, kama ilivyosemwa juu ya baadhi ya watu nyakati za kale, Waebrania 3:19: "Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini." Umefika kabisa kizingitini, na baadhi yenu mmekuwapo hapo mara nyingi. Ee! ni mvuto gani wa neema mliouonja.
Umeona ng'ambo ya pazia! Umeugusa mkono wake! Umeweka miguu yako kizingitini!
Umekaribia kuingia, kisha ukarudi nyuma kwa sababu ya kutokuamini. Je, itakuwa hivyo tena usiku huu? La hasha! Je, utavuka? Utathubutu? Utaamini? Je, utaruka juu ya uaminifu wake? Je, utajitupa mikononi mwa Upendo Mwenyezi, na kumkabidhi yeye matokeo yote? Usijali hata kama utakufa, au kama likikupata jambo ambalo halijampata mtu ye yote mwingine katika historia ya ulimwengu; Mungu atakutunza. Usijali hata kama Ibilisi akija na kukuchunguza, kama alivyomchunguza Ayubu, na kukutesa kwa majipu, na kukuweka juu ya jaa la majivu—utakuwa na furaha zaidi hapo pamoja na Yesu kuliko katika kasri bila yeye. Ee! wasiwasi huu juu ya matokeo! Ibilisi anazijua fursa kuu zilizo wazi kwa wengi wenu; anajua si tu kile mnachoweza kupokea na kufurahia ndani yenu, bali pia kile mnachoweza kutimiza kwa ajili ya Mungu iwapo tu mngeingia na kuimiliki baraka hii; na hivyo anawatia hofu kwa matokeo. Anajua kile mnachoweza kufanya, na ni nani mnaoweza kutumiwa kuwaokoa!
Ni nani ajuaye ni wangapi kati ya wapendwa hawa wanaokusanyika kukuzunguka, ambao waweza kutumiwa kuwaongoza kwenye jukwaa hili la juu zaidi—mahali hapa patukufu pa manufaa pa uzoefu wa Kikristo? na, kupitia wao, ni wangapi zaidi? na jinsi gani, kwa njia hii, baraka hiyo tukufu ingeenea? Kumbuka pia, kwamba kila mara unapokaribia na kurudi nyuma, uwezekano wa wewe kuingia kabisa unapungua; na kadiri unavyokaribia zaidi na kisha kurudi nyuma, ndivyo uwezekano wa wewe kufika karibu hivyo tena unavyopungua.
Unamhuzunisha Roho. Wako watu ambao wamekuwa wakikaribia kwa miaka mingi, na sasa wamerudi nyuma kabisa, nami naogopa hawatakuja tena kamwe. Wewe utafanyaje?
Sheria ya ufalme, tangu mwanzo hata mwisho, ni Mathayo 9:29: "...Kwa kadiri ya imani yenu mpate," na, Marko 11:24: "Kwa sababu hiyo nawaambia, yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu." Kweli ya milele imeinena—"yatakuwa yenu." Basi sasa, je, utafanya hivyo? Je, umeachilia kila kitu? Je, u huru kabisa? Je, unaacha kila kitu nyuma yako? Je, umeazimia tangu usiku huu kukata uhusiano na yaliyopita, na kutokujiandalia tena mwili ili kutimiza tamaa zake, bali kwamba utayaaga kwaheri ya mwisho yale yaliyo nyuma, kuyafumbia macho yako, na kuyakaza macho yako kwenye tuzo la mwito wako wa juu, na kukaza mwendo kila saa ifuatayo ya maisha yako mpaka uifikie? Je, utafanya hivyo? Ukifanya, Mungu atakupa baraka hii. Anangoja kuifanya; yupo hapa. Roho Mtakatifu yupo hapa: anawaongoza juu wengi wenu; anawasihi; anayaimarisha ninayoyasema ndani ya mioyo yenu; anasema, "Njoo, mpendwa; ingia katika ukumbi wa karamu;" anataka kuwabariki na kuwajaza Roho wake. Basi sasa, je, utakuja? Ee! Bwana akusaidie usirudi nyuma, bali ukaze mwendo, kaza mwendo, kaza mwendo, bila kujali matokeo.