Sura 7 · dakika 30 za kusoma
Tafsiri ya AI — inasubiri mapitio ya mzawa
Mwezi wa Juni
Juni 1
AHADI YA MUNGU HUDUMU
"Utupe mkate wako juu ya maji, kwa maana utauona baada ya siku nyingi." Mhu. 11:1
Haitupasi kutazamia kuona thawabu mara moja kwa mema yote tuyatendayo; wala haituwajibu sikuzote kuziwekea juhudi zetu mipaka ya mahali na watu wale wanaoonekana kuwa watatuzawadia kwa taabu zetu. Mmisri hutupa mbegu yake juu ya maji ya Nile, ambapo yaweza kuonekana ni kupoteza nafaka bure kabisa. Lakini kwa wakati wake gharika hupungua, mchele au nafaka nyingine huzama katika matope yenye rutuba, na mavuno hutokea kwa haraka. Na tuwatendee mema leo wasio na shukrani na wabaya. Na tuwafundishe wazembe na wakaidi. Maji yasiyotarajiwa yaweza kufunika udongo wenye matumaini. Mahali popote kazi yetu haitakuwa bure katika Bwana.
Ni juu yetu kuutupa mkate wetu juu ya maji; yabaki kwa Mungu kuitimiza ahadi, "Utauona." Hataiacha ahadi yake ianguke. Neno lake jema tulilolinena litaishi, litaonekana, litaonekana na sisi. Labda si sasa hivi, lakini siku moja tutavuna tulichokipanda. Yatupasa kuutumia uvumilivu wetu; kwa maana labda Bwana ataujaribu. "Baada ya siku nyingi," lasema Andiko, na katika hali nyingi siku hizo huingia miezi na miaka, na bado Neno lasimama kuwa kweli. Ahadi ya Mungu itadumu; na tuangalie sisi tuishike ile amri, na kuishika siku hii.
Juni 2
UHURU WA MARA MOJA
"Na sasa nitaivunja nira yake iliyo juu yako, nami nitavipasua vifungo vyako." Nahumu 1:13
Mwashuru aliruhusiwa kwa muda kuwaonea watu wa Bwana, lakini ukafika wakati wa nguvu zake kuvunjwa. Vivyo hivyo, moyo mwingi hushikwa katika utumwa na Shetani, nao huhangaika sana chini ya nira. Laiti kwa wafungwa kama hao wa tumaini neno la Bwana lingewafikia mara moja, sawasawa na maandiko, "Na sasa nitaivunja nira yake iliyo juu yako, nami nitavipasua vifungo vyako"!
Tazama! Bwana anaahidi wokovu wa sasa: "Na sasa nitaivunja nira yake iliyo juu yako." Amini kwa ajili ya uhuru wa mara moja, na kwa kadiri ya imani yako ndivyo itakavyokuwa kwako saa hii hasa. Mungu asemapo "sasa," mtu ye yote asiseme "kesho."
Tazama jinsi ukombozi utakavyokuwa kamili; kwa maana nira haitaondolewa tu, bali itavunjwa; na vifungo havitafunguliwa tu, bali vitapasuliwa. Hapa pana udhihirisho wa nguvu za Kimungu uhakikishao ya kwamba mtesi hatarudi tena. Nira yake imevunjika, hatuwezi tena kuinamishwa chini na uzito wake. Vifungo vyake vimepasuliwa, haviwezi tena kutushika. Laiti tungemwamini Yesu kwa ajili ya ukombozi kamili na wa milele! "Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli." Njoo, Bwana, ukawaache huru mateka wako, sawasawa na neno lako.
Juni 3
MIGUU ISIYOTELEZA
"Bwana MUNGU ndiye nguvu zangu, naye huifanya miguu yangu kuwa kama miguu ya kulungu, naye ataniendesha juu ya mahali pangu palipoinuka." Hab. 3:19
Ujasiri huu wa mtu wa Mungu ni sawa na ahadi; kwa maana lile ambalo imani imesadikishwa nalo ndilo kusudi la Mungu. Nabii alilazimika kupita mahali pa chini pa umaskini na njaa, lakini alishuka mlimani pasipo kuteleza, kwa kuwa Bwana alimpa kusimama. Baadaye kidogo aliitwa kwenda mahali pa juu pa vilima vya mapigano; wala hakuogopa kupanda kuliko kushuka.
Tazama! Bwana alimwazima nguvu. La, Yehova mwenyewe ndiye alikuwa nguvu zake. Fikiri jambo hilo: Mungu Mwenyezi mwenyewe huwa nguvu zetu!
Angalia, ya kwamba Bwana pia alimpa hatua thabiti. Kulungu huruka juu ya mwamba na jabali, wala hawakosi kamwe pa kukanyaga. Bwana wetu atatupa neema kuzifuata njia ngumu kabisa za wajibu pasipo kujikwaa. Aweza kuufaa mguu wetu kwa majabali, hata tutakuwa kama nyumbani mahali ambapo pasipo Mungu tungeangamia.
Siku mojawapo tutaitwa kwenda mahali pa juu zaidi. Huko juu tutapanda, hata mlima wa Mungu, mahali pa juu ambapo wenye kung'aa wamekusanyika. Lo, miguu ilioje miguu ya imani, ambayo kwayo, tukimfuata Kulungu wa Asubuhi, tutapanda katika mlima wa Bwana!
Juni 4
YA THAMANI MNO
"Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile nitakapowakusanya hazina zangu za thamani." Mal. 3:17
Siku yaja ambayo vito vya taji ya Mfalme wetu mkuu vitahesabiwa, ili ionekane kama vyapatana na orodha ile Baba yake aliyompa. Ee nafsi yangu, je! utakuwa miongoni mwa vitu vya thamani vya Yesu? U wa thamani kwake kama yeye ni wa thamani kwako, nawe utakuwa wake "katika siku ile," kama yeye ni wako siku hii.
Katika siku za Malaki, wateule wa Bwana walikuwa na desturi ya kuzungumza wao kwa wao hata Mungu wao mwenyewe akayasikiliza maongezi yao. Aliyapenda sana hata akayaandika; naam, akayafanya kuwa kitabu, alichokiweka katika Nyumba yake ya Kumbukumbu. Akipendezwa na maongezi yao, alipendezwa pia nao. Simama, ee nafsi yangu, ukajiulize: Kama Yesu angeyasikiliza maongezi yako je! angependezwa nayo? Je! ni kwa utukufu wake na kwa kuwajenga ndugu? Sema, ee nafsi yangu, ukahakikishe wasema kweli.
Lakini heshima itakuwaje kwetu sisi viumbe maskini kuhesabiwa na Bwana kuwa vito vya taji yake! Heshima hii wanayo watakatifu wote. Yesu hasemi tu, "Ni wangu," bali, "Watakuwa wangu." Alitununua, akatutafuta, akatuingiza ndani, na amekwisha kutufinyanga hata mfano wake, hata tutapiganiwa naye kwa nguvu zake zote.
Juni 5
JE! KUNA TOFAUTI?
"Bali juu ya wana wa Israeli hapana mbwa atakayeusogeza ulimi wake, juu ya mwanadamu wala mnyama; ili mpate kujua jinsi Bwana awafanyiavyo tofauti Wamisri na Israeli." Kut. 11:7
Je! Mungu ana uwezo juu ya ndimi za mbwa? Aweza kuwazuia mbwa wasibweke? Naam, ni vivyo hivyo. Aweza hata kumzuia mbwa wa Kimisri asimtaabishe mmoja wa wana-kondoo wa kundi la Israeli. Je! Mungu huwanyamazisha mbwa, na wale walio kama mbwa miongoni mwa watu, na yule mbwa mkubwa aliye langoni pa kuzimu? Basi na tuiendee njia yetu bila hofu.
Akiwaacha mbwa waisogeze ndimi zao, hata hivyo aweza kuyazuia meno yao. Waweza kupiga kelele za kutisha, na bado wasitudhuru kwa kweli. Lakini, utamu ulioje wa kunyamaza! Furaha iliyoje kutembea kati ya adui, na kuona ya kuwa Mungu awafanya kuwa na amani nasi! Kama Danieli katika tundu la simba, sisi hatudhuriwi kati ya waharibifu.
Laiti leo, neno hili la Bwana kwa Israeli lingekuwa kweli kwangu! Je! yule mbwa ananitaabisha? Nitamwambia Bwana wangu habari zake. Bwana, yeye hajali maombi yangu; wewe unene neno la uweza, naye sharti alale chini. Nipe amani, Ee Mungu wangu, unijalie kuuona mkono wako wazi ndani yake hata niitambue kwa uwazi kabisa ile tofauti ambayo neema yako imeifanya kati yangu na wasiomcha Mungu!
Juni 6
HUSIKIA SIKUZOTE
"Bwana amesikia dua yangu; Bwana ataipokea sala yangu." Zab. 6:9
Uzoefu ulioandikwa hapa ni wangu. Naweza kutia muhuri wangu ya kwamba Mungu ni kweli. Kwa njia za ajabu sana amezijibu sala za mtumishi wake mara nyingi mno. Naam, na anasikia dua yangu ya sasa, wala hageuzi sikio lake mbali nami. Na libarikiwe jina lake takatifu!
Basi, je? Bila shaka ile ahadi iliyolala ndani ya ujasiri wa kuamini wa Mtunga-Zaburi ni yangu pia. Na niishike kwa mkono wa imani: "Bwana ataipokea sala yangu." Ataikubali, ataifikiria, na kuijalia kwa njia na kwa wakati ambao hekima yake ya upendo iona kuwa ni bora. Naileta sala yangu maskini mkononi mwangu kwa Mfalme mkuu, naye ananipa nafasi ya kusikilizwa, na kuipokea kwa neema haja yangu. Adui zangu hawatanisikiliza, lakini Bwana wangu atanisikiliza. Wao huzidhihaki sala zangu za machozi, lakini Bwana wangu hafanyi hivyo; huipokea sala yangu sikioni mwake na moyoni mwake.
Mapokezi yalioje haya kwa mwenye dhambi maskini! Sisi twampokea Yesu, kisha Bwana atupokea sisi na sala zetu kwa ajili ya Mwanawe. Na libarikiwe jina lile lipendwalo litoalo ruhusa sala zetu zipate kupita kwa uhuru hata ndani ya malango ya dhahabu. Bwana, nifundishe kusali, kwa kuwa wewe wazisikia sala zangu.
Juni 7
MAHALI SALAMA KABISA
"Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu." Yohana 10:28
Twaamini usalama wa milele wa watakatifu. Kwanza, kwa sababu wao ni wa Kristo, naye hatawapoteza kamwe kondoo aliowanunua kwa damu yake, na kuwapokea kwa Baba yake.
Tena, kwa sababu awapa uzima wa milele, na kama ni wa milele, basi, ni wa milele, wala hauwezi kuwa na mwisho, isipokuwa kama kuzimu, na Mbingu, na Mungu kunaweza kuwa na mwisho. Kama uzima wa kiroho waweza kuzimika, ni dhahiri si uzima wa milele, bali uzima wa muda. Lakini Bwana anena habari za uzima wa milele, na jambo hilo lafunga kabisa uwezekano wa mwisho.
Angalia, tena, ya kwamba Bwana asema waziwazi, "Hawatapotea kamwe." Maadamu maneno yana maana, jambo hili huwahifadhi waaminio wasipotee. Kutokuamini kulikokaidi kupita yote hakuwezi kuitoa maana hii katika sentensi hii.
Kisha, ili kulikamilisha jambo, atangaza ya kwamba watu wake wamo mkononi mwake, naye awapinga adui zao wote wawapokonye humo. Hakika ni jambo lisilowezekana hata kwa yule shetani wa kuzimu. Sharti tuwe salama katika mkono wa Mwokozi Mwenyezi.
Na iwe yetu kuiondoa hofu ya kimwili pamoja na ujasiri wa kimwili, na kupumzika kwa amani katika kiganja cha mkono wa Mkombozi.
Juni 8
HEKIMA KWA KUIOMBA
"Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa." Yakobo 1:5
"Mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima." Hapana "kama" katika jambo hili, kwa maana nina hakika napungukiwa nayo. Najua nini? Nawezaje kuiongoza njia yangu mwenyewe? Nawezaje kuwaongoza wengine? Bwana, mimi ni chungu la upumbavu, wala hekima sina hata kidogo.
Wewe wasema, "Na aombe dua kwa Mungu." Bwana, sasa naomba. Hapa penye kiti cha miguu yako naomba nijaliwe hekima ya mbinguni kwa mataabu ya siku hii, naam, na kwa mambo rahisi ya siku hii; kwa maana najua naweza kutenda mambo ya kipumbavu sana, hata katika mambo yaliyo dhahiri, usiponilinda nisiingie mashakani.
Nakushukuru kwa kuwa yote yanipasayo ni kuomba tu. Neema iliyoje hii kwa upande wako, kwamba nina budi tu kusali kwa imani, nawe utanipa hekima! Wewe waniahidi hapa elimu ya ukarimu, na hiyo, tena, pasipo mwalimu mkali, wala mchunga-chuo mkemeaji. Hii, pia, utaitoa pasipo ada -- kumtolea mpumbavu apungukiwaye na hekima. Ee Bwana, nakushukuru kwa lile neno lililo hakika na dhahiri, "Naye atapewa." Nalisadiki. Wewe utamfanya siku hii mtoto wako mchanga aijue hekima iliyofichwa ambayo wenye busara za kimwili hawaijui kamwe. Wewe utaniongoza kwa shauri lako, na baadaye utanikaribisha katika utukufu.
Juni 9
JINA LA KUTUMAINIKA
"Nami nitasaza kati yako watu walioteswa na maskini, nao watalitumaini jina la Bwana." Sef. 3:12
Dini ya kweli inapokaribia kutoweka miongoni mwa matajiri hujipatia makao miongoni mwa maskini wa dunia hii, walio matajiri katika imani. Bwana anao hata sasa mabaki yake waaminifu. Je! mimi ni mmoja wao?
Labda ni kwa sababu watu wameteswa na maskini ndiyo maana hujifunza kulitumaini jina la Bwana. Yeye asiye na fedha sharti ajaribu awezalo kufanya kwa kuaminiana. Yeye ambaye jina lake mwenyewe halifai kitu machoni pake, hutenda kwa hekima kuegemea juu ya jina lingine, naam, jina lile lililo bora kuliko yote, jina la Yehova. Mungu daima atakuwa na watu wamtumainio, nao hawa watakuwa watu walioteswa na maskini. Ijapokuwa dunia haiwathamini, kule kusaziwa kwao kati ya taifa ni mfereji wa baraka zisizohesabika kwake. Hapa tunayo chumvi ihifadhio izuiayo uharibifu ulio duniani kwa sababu ya tamaa.
Tena swali laturudia kila mmoja wetu, Je! mimi ni mmoja wao? Je! nimeteswa na dhambi iliyo ndani yangu na inayonizunguka? Je! mimi ni maskini wa roho, maskini kiroho kwa hukumu yangu mwenyewe? Je! namtumaini Bwana? Hilo ndilo jambo kuu. Yesu hulifunua jina, tabia, nafsi ya Mungu; je! mimi namtumaini yeye? Kama ni hivyo, nimesaziwa katika ulimwengu huu kwa kusudi. Bwana, nisaidie kulitimiza.
Juni 10
MCHUNGAJI HUWAKINGA
"Watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewatia hofu." Sef. 3:13
Jana tulifikiri juu ya watu walioteswa na maskini ambao Bwana aliwasaza kuwa mbegu iliyo hai katika ulimwengu uliokufa. Nabii asema juu yao ya kwamba hawatatenda uovu wala hawatasema uongo. Hivyo, wakati ambapo hawakuwa na cheo wala mali za kuwalinda, walikuwa pia hawawezi kabisa kuyatumia yale silaha ambayo wabaya huyategemea sana: hawakuweza kujilinda kwa dhambi wala kwa hila.
Basi, je? Je! wataangamizwa? La, hasha! Watakula na kupumzika, wala hawatakuwa salama na hatari tu, bali watatulia hata na hofu ya mabaya. Kondoo ni viumbe dhaifu sana, na mbwa-mwitu ni adui wa kutisha; lakini saa hii kondoo ni wengi kuliko mbwa-mwitu, na shauri la kondoo daima lashinda, hali shauri la mbwa-mwitu daima lapungua. Siku moja makundi ya kondoo yatafunika nyika, wala hapatakuwa na mbwa-mwitu hata mmoja aliyesalia. Ukweli ni kwamba kondoo wana mchungaji, na jambo hili huwapa chakula, ulinzi, na amani. "Hapana" -- maana yake hata mmoja, akiwa katika mfano wa kibinadamu au wa kishetani -- "atakayewatia hofu." Ni nani atakayelitisha kundi la Bwana wakati yeye yu karibu? Twalala katika malisho ya majani mabichi, kwa maana Yesu mwenyewe ni chakula na pumziko kwa nafsi zetu.
Juni 11
HAKUNA SABABU YA KUONA HAYA
"Usiogope; kwa maana hutaona haya." Isa. 54:4
Hatutaona haya kwa ajili ya imani yetu. Wachambuzi wenye kunung'unika waweza kuyashambulia Maandiko ambayo juu yake twaisimika imani yetu, lakini kila mwaka Bwana atazidi kulidhihirisha ya kuwa katika Kitabu chake hamna kosa, wala ziada, wala upungufu. Si aibu kuwa mwaminifu mnyenyekevu; imani imtazamayo Yesu peke yake ni taji ya heshima juu ya kichwa cha mtu ye yote, na bora kuliko nyota kifuani pake.
Hatutaona haya kwa ajili ya tumaini letu. Litakuwa sawasawa na Bwana alivyosema. Tutalishwa, tutaongozwa, tutabarikiwa na kupumzishwa. Bwana wetu atakuja, ndipo siku za maombolezo yetu zitakapokoma. Jinsi tutakavyojisifu katika Bwana aliyetupa kwanza tumaini lililo hai, kisha akatupa kile tulichokitumaini!
Hatutaona haya kwa ajili ya upendo wetu. Yesu kwetu ni mpendezi wa moyo wote, wala kamwe, kamwe, hatutalazimika kuona haya kwa sababu tumeitoa mioyo yetu kwake. Kumwona Mpendwa wetu mtukufu kutauhalalisha ushikamano wenye shauku kubwa naye. Hakuna atakayewalaumu mashahidi kwa kufa kwa ajili yake. Adui za Kristo watakapovikwa dharau ya milele, wapendao Yesu watajiona wameheshimiwa na viumbe vyote vitakatifu, kwa sababu walichagua shutuma ya Kristo kuliko hazina za Misri.
Juni 12
KUKAA SALAMA PEKE YAKO
"Israeli hukaa salama, chemchemi ya Yakobo peke yake, katika nchi ya nafaka na divai; naam, mbingu zake hudondoza umande." Kum. 33:28
Kadiri tunavyokaa peke yetu, ndivyo tutakavyozidi kuwa salama. Mungu apenda watu wake watengwe na wenye dhambi. Wito wake kwao ni, "Tokeni kati yao." Ulimwengu wa Kikristo ni jambo la kutisha ambalo Maandiko hayakuliwaza kamwe. Mkristo wa kilimwengu ni mgonjwa kiroho. Wale wanaopatana kwa maafikiano na adui za Kristo waweza kuhesabiwa pamoja nao.
Usalama wetu haumo katika kuafikiana na adui bali katika kukaa peke yetu na Rafiki yetu aliye bora. Tukifanya hivi, tutakaa salama, ijapokuwa dhihaka, na masingizio, na kejeli za ulimwengu. Tutakuwa salama na nguvu mbaya ya kutokuamini kwake, na kiburi chake, na ubatili wake, na uchafu wake.
Mungu pia atatufanya tukae salama peke yetu katika siku ile ambapo dhambi itapatilizwa juu ya mataifa kwa vita na njaa.
Bwana alimtoa Abramu kutoka Uru wa Wakaldayo, lakini alisimama katikati ya njia. Hakuwa na baraka hata, alipokwisha kuanza safari ya kwenda nchi ya Kanaani, akaifikia nchi ya Kanaani. Alikuwa salama peke yake hata kati ya adui. Lutu hakuwa salama katika Sodoma ijapokuwa alikuwa katika mzunguko wa rafiki. Usalama wetu u katika kukaa peke yetu pamoja na Mungu.
Juni 13
KILIMO CHA KIMUNGU
"Mimi, Bwana, ndimi nilindaye; nitakinywesha maji kila dakika; asije mtu akakidhuru, nitakilinda usiku na mchana." Isa. 27:3
Bwana mwenyewe anenapo kwa nafsi yake mwenyewe badala ya kwa kinywa cha nabii, neno lile lina uzito wa pekee kwa nia za kuamini. Ni Yehova mwenyewe aliye mlinzi wa shamba lake mwenyewe la mizabibu; hakabidhi kwa mtu mwingine ye yote, bali hulifanya kuwa jukumu lake binafsi. Je! hawalindwi vyema hao ambao Mungu mwenyewe huwalinda?
Twapaswa kupokea kunyweshwa maji kwa neema, si kila siku na kila saa tu, "bali kila dakika." Jinsi itupasavyo kukua! Jinsi kila mche upasavyo kuwa mbichi na wenye kuzaa! Vishada vinono vilioje vipasavyo mizabibu kuzaa!
Lakini wenye kusumbua huja; mbweha wadogo na nguruwe-mwitu. Kwa hiyo, Bwana mwenyewe ndiye Mlezi wetu, na hivyo saa zote, "usiku na mchana." Basi, ni nini kiwezacho kutudhuru? Kwa nini twaogopa? Yeye hutunza, hunywesha maji, hulinda; twahitaji nini zaidi?
Mara mbili katika mstari huu Bwana asema, "Nitafanya." Kweli iliyoje, uweza ulioje, upendo ulioje, kutobadilika kulioje tunakoona katika lile kuu "Nitafanya" la Yehova! Ni nani awezaye kupinga mapenzi yake? Akisema "Nitafanya," pana nafasi gani ya shaka? Kwa "Nitafanya" la Mungu twaweza kuyakabili majeshi yote ya dhambi, na mauti, na kuzimu. Ee Bwana, kwa kuwa wasema, "Nitakulinda wewe," najibu, "Nitakusifu wewe!"
Juni 14
YEYE HUKAA SIKUZOTE
"Kwa maana Bwana hatawaacha watu wake, kwa ajili ya jina lake kuu; kwa sababu Bwana ameona vema kuwafanya ninyi kuwa watu wake." 1 Sam. 12:22
Kule Mungu kuwachagua watu wake ndiyo sababu ya yeye kukaa nao, wala kutowaacha. Aliwachagua kwa sababu ya upendo wake, naye awapenda kwa sababu ya kuwachagua kwake. Radhi yake mwenyewe njema ndiyo chanzo cha kuteuliwa kwao, na kuteua kwake ndiyo sababu ya kudumu kwa radhi yake juu yao. Ingelivunja heshima ya jina lake kuu yeye kuwaacha, kwa kuwa jambo hilo lingeonyesha ama kwamba alikosea katika kuchagua kwake, au kwamba alikuwa mgeugeu katika upendo wake. Upendo wa Mungu una utukufu huu, ya kwamba haubadiliki kamwe, na utukufu huu hataunajisi kamwe.
Kwa kumbukumbu zote za fadhili za Bwana za zamani na tuwe na hakika ya kuwa hatatuacha. Yeye aliyefika mbali hata kutufanya kuwa watu wake, hatavunja kazi ya kuumba ya neema yake. Hakututendea maajabu makuu namna hii ili apate kutuacha mwishoni. Mwanawe Yesu amekufa kwa ajili yetu, nasi twaweza kuwa na hakika ya kwamba hakufa bure. Je! aweza kuwaacha wale aliowamwagia damu yake? Kwa sababu hata sasa amependezwa kutuchagua na kutuokoa, itakuwa radhi yake bado kutubariki. Bwana wetu Yesu si Mpenzi anayebadilika. Akiisha kuwapenda walio wake, huwapenda hata mwisho.
Juni 15
BARAKA ZA NYUMBANI ZAONGEZEKA
"Bwana atakubariki toka Sayuni; nawe utauona wema wa Yerusalemu siku zote za maisha yako." Zab. 128:5
Hii ni ahadi kwa mtu amchaye Mungu aendaye katika njia za utakatifu kwa uangalifu mkubwa. Atakuwa na heri ya nyumbani; mkewe na watoto wake watakuwa chemchemi ya furaha kubwa ya nyumbani. Lakini tena kama mshiriki wa kanisa hutamani kuiona kazi ikisitawi, kwa maana hujali nyumba ya Bwana kama ajalivyo nyumba yake mwenyewe. Bwana ajengapo nyumba yetu, ni haki tu sisi kutamani kuiona nyumba ya Bwana ikijengwa. Mali zetu si njema kweli kweli tusipoyaendeleza kwazo mema ya kanisa teule la Bwana.
Naam, utapata baraka utakapopanda kwenda mikutano ya Sayuni; utafundishwa, utahuishwa, na kufarijiwa, mahali ambapo sala na sifa hupanda juu, na ushuhuda hutolewa juu ya ile Dhabihu Kuu. "Bwana atakubariki toka Sayuni."
Wala si wewe peke yako utakayefaidika; kanisa lenyewe litasitawi; waaminio wataongezeka, na kazi yao takatifu itavikwa taji ya mafanikio. Watu fulani wenye neema huitimiziwa ahadi hii maadamu wanaishi. Ole! Wafapo, mara nyingi kazi hulegea. Na tuwe miongoni mwa wale waletao mema Yerusalemu siku zao zote. Bwana, kwa rehema zako utufanye kuwa hivyo! Amina.
Juni 16
MILIKI, SI KUKIRI TU
"Kwa maana yeyote aliye na kitu atapewa, naye atazidishiwa tele." Mt. 13:12
Bwana ampapo mtu neema nyingi atampa zaidi. Imani kidogo ni yai la kutamania; imani zaidi itaijilia. Lakini basi haipasi kuwa imani ya kuonekana tu, bali iliyo halisi na ya kweli. Ni lazima gani iliyowekwa juu yetu ya kufanya kazi ya hakika katika dini, wala tusikiri mengi, hali tusimiliki kitu! Kwa maana siku mojawapo kule kukiri kwenyewe kutatwaliwa kwetu, kama ndiyo yote tuliyo nayo. Kitisho ni cha kweli kama ilivyo ahadi.
Na abarikiwe Bwana, ni desturi yake akiisha kuanza kuendelea kuzitoa neema za Roho wake, hata yeye aliyekuwa na kidogo tu, na bado kwa kweli alikuwa na kidogo kile, afanywa kuwa na wingi. Lo, kwa ajili ya wingi ule! Wingi wa neema ni kitu cha kutamaniwa. Ingekuwa vyema kujua mengi, lakini bora zaidi kupenda mengi. Ingependeza kuwa na wingi wa ustadi wa kumtumikia Mungu, lakini bora zaidi kuwa na wingi wa imani ya kumtumaini Bwana kwa ustadi na kwa kila kitu.
Bwana, kwa kuwa umenipa hisia ya dhambi, ukizidishe chuki yangu ya uovu. Kwa kuwa umenifanya nimtumaini Yesu, uiinue imani yangu hata uhakika kamili. Kwa kuwa umenifanya nikupende Wewe, unifanye nichukuliwe mbali na mapenzi yenye nguvu kwako Wewe!
Juni 17
UWANJA WETU WA VITA
"Kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye aendaye pamoja nanyi, kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa." Kum. 20:4
Hatuna adui ila adui za Mungu. Mapigano yetu si juu ya wanadamu, bali juu ya maovu ya kiroho. Twapigana na Ibilisi, na kufuru, na upotovu, na kukata tamaa, ambavyo yeye huvileta uwanjani pa vita. Twapigana na majeshi yote ya dhambi -- uchafu, ulevi, uonevu, ukafiri, na kutokumcha Mungu. Na hivi twashindana kwa bidii, lakini si kwa upanga wala mkuki; silaha za vita vyetu si za mwili.
Yehova, Mungu wetu, huchukia kila kilicho kiovu, na, kwa hiyo, huenda pamoja nasi kutupigania katika vita hivi vitakatifu. Atatuokoa, naye atatupa neema tupigane vita vizuri, na kuushinda ushindi. Twaweza kulitegemea jambo hili ya kuwa tukiwa upande wa Mungu, Mungu yu upande wetu. Kwa mshirika mtukufu namna hii vita havina shaka hata kidogo. Si kwamba kweli ina nguvu na sharti ishinde, bali kwamba nguvu iko kwa Baba aliye Mwenyezi, na kwa Yesu aliye na uwezo wote Mbinguni na duniani, na kwa Roho Mtakatifu atendaye mapenzi yake kati ya wanadamu.
Enyi askari wa Kristo, jifungeni silaha zenu. Pigeni kwa nguvu katika jina la Mungu wa utakatifu, na kwa imani ushikeni wokovu wake. Siku hii isipite bila kupiga pigo kwa ajili ya Yesu na utakatifu.
Juni 18
MUNGU MWENYEWE ATATENDA
"Sasa nitainuka, asema Bwana; sasa nitajitukuza; sasa nitajiinua." Isa. 33:10
Watekaji walipoifanya nchi kuwa ukiwa kana kwamba imeliwa na nzige, na mashujaa waliokuwa wameilinda nchi wakaketi na kulia kama wanawake, ndipo Bwana alipokuja kuokoa. Wasafiri walipokoma katika njia za kwenda Sayuni, na Bashani na Karmeli zikawa kama mashamba ya mizabibu ambayo matunda yake yamepungua, ndipo Bwana aliposimama. Mungu hutukuzwa kati ya watu walioteswa, kwa maana hutafuta uso wake na kumtumaini. Hutukuzwa zaidi tena atakapojiinua, kwa kuitikia vilio vyao, ili kuwaokoa na kuwaangusha adui zao.
Je! ni siku ya huzuni kwetu? Na tutazamie kumwona Bwana akitukuzwa katika wokovu wetu. Je! twavutwa kusali kwa juhudi? Je! twamlilia yeye usiku na mchana? Basi wakati uliowekwa wa neema yake u karibu. Mungu atajiinua kwa majira yaliyofaa. Atasimama wakati ambao utakuwa bora zaidi kwa kuudhihirisha utukufu wake. Twautamani utukufu wake kuliko tunavyoutamani wokovu wetu wenyewe. Bwana na atukuzwe, na haja yetu kuu imepatikana.
Bwana, utusaidie kwa namna ambayo tupate kuona ya kwamba wewe mwenyewe wafanya kazi. Tupate kukutukuza katika nafsi zetu za ndani kabisa. Uwafanye wote wanaotuzunguka waone jinsi ulivyo Mungu mwema na mkuu.
Juni 19
MOYO MKAMILIFU
"Moyo wangu na uwe mkamilifu katika sheria zako, nisije nikaona haya." Zab. 119:80
Twaweza kuiona sala hii iliyovuviwa kuwa ina ndani yake uhakika ya kwamba wale wanaokaa karibu na Neno la Mungu hawatakuwa na sababu kamwe ya kuona haya kwa kufanya hivyo.
Tazama, sala ni kwa ajili ya ukamilifu wa moyo. Imani iliyo kamili ni njema, hukumu iliyo kamili juu yake ni bora, lakini moyo mkamilifu kuielekea kweli ndiyo bora kuliko yote. Sharti tuipende kweli, tuisikie kweli, na kuitii kweli, ama sivyo si wakamilifu kweli kweli katika sheria za Mungu. Je! wako wengi katika siku hizi mbaya walio wakamilifu? Laiti mwandishi na msomaji wangekuwa wawili wa aina hii!
Wengi wataona haya katika siku ile kuu ya mwisho, ambapo mashindano yote yataamuliwa. Ndipo watakapouona upumbavu wa mavumbuo yao, na kujawa na majuto kwa sababu ya ukafiri wao wa kiburi na ukaidi wao wa makusudi juu ya Bwana; lakini yeye aliyeamini yale Bwana aliyoyafundisha, na kufanya yale Bwana aliyoyaamuru, atasimama akihesabiwa haki katika yale aliyoyafanya. Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua. Watu walisingiziwa sana na kudhulumiwa watakuta aibu yao imegeuzwa kuwa utukufu katika siku ile.
Na tuiombe sala ya andiko letu, nasi twaweza kuwa na hakika ya kwamba ahadi yake itatimizwa kwetu. Bwana akitufanya wakamilifu, atatulinda salama.
Juni 20
BWANA MWENZI WETU
"Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanifariji." Zab. 23:4
Ni matamu maneno haya katika kuuelezea uhakika wa kitandani pa kufa. Ni wangapi walioyarudia katika saa zao za mwisho kwa furaha kubwa!
Lakini mstari huu wafaa vivyo hivyo kwa maumivu makali ya roho katikati ya maisha. Baadhi yetu, kama Paulo, twakufa kila siku kwa sababu ya mwelekeo wa huzuni ya nafsi. Bunyan huliweka Bonde la Uvuli wa Mauti mapema zaidi katika safari ya hija kuliko ule mto uendao chini ya vilima vya mbinguni. Baadhi yetu tumepita katika lile korongo lenye giza na la kutisha la "uvuli wa mauti" mara kadha, nasi twaweza kushuhudia ya kuwa Bwana peke yake ndiye alituwezesha kuvumilia kati ya mawazo yake ya kutisha, na hofu zake za fumbo, na mfadhaiko wake mbaya. Bwana ametutegemeza, na kutulinda juu ya hofu yote halisi ya mabaya, hata roho zetu zilipokuwa zimelemewa. Tumesongwa na kuonewa, lakini bado tumeishi, kwa maana tumehisi uwepo wa Mchungaji Mkuu, na tumekuwa na hakika ya kwamba gongo lake litamzuia adui asitutie jeraha lo lote la mauti.
Kama wakati huu wa sasa ni uliotiwa giza na mbawa za kunguru za huzuni kubwa, na tumtukuze Mungu kwa kumtumaini kwa amani.
Juni 21
VITA VYA MWANAMKE
"Bwana atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke." Waamuzi 4:9
Ni andiko lisilo la kawaida, lakini yaweza kuwapo nafsi duniani zenye imani ya kutosha kulishika. Baraka, yule mtu, ijapokuwa aliitwa vitani, alikuwa na hamu ndogo ya kupigana isipokuwa Debora aende pamoja naye, na hivyo Bwana akaazimu kuvifanya kuwa vita vya mwanamke. Kwa njia hii aliukemea uzembe wa yule mtu, na kujipatia sifa kubwa zaidi, na kuwaaibisha zaidi adui za watu wake.
Bwana angali aweza kutumia vyombo dhaifu. Kwa nini si mimi? Aweza kutumia watu wasioitwa kwa kawaida kwenye shughuli kubwa za hadhara. Kwa nini si wewe? Yule mwanamke aliyemwua adui wa Israeli hakuwa shujaa wa kike, bali mke aliyekaa hemani mwake. Hakuwa mnenaji, bali mwanamke aliyekamua ng'ombe na kutengeneza siagi. Je! Bwana hawezi kumtumia ye yote miongoni mwetu kulitimiza kusudi lake? Mtu fulani aweza kuja nyumbani leo, kama vile Sisera alivyokuja hemani mwa Yaeli. Na iwe yetu, si kumwua, bali kumwokoa. Na tumpokee kwa fadhili nyingi, kisha tuidhihirishe ile kweli iliyobarikiwa ya wokovu kwa Bwana Yesu, Mbadala wetu mkuu, na kuisisitiza ile amri, "Amini ukaishi." Ni nani ajuaye kama mwenye dhambi fulani mwenye moyo mgumu aweza kuuawa na injili leo?
Juni 22
YEYE PAMOJA NASI; SISI PAMOJA NAYE
"Kumcha Bwana huongeza siku; bali miaka ya wabaya itafupizwa." Mit. 10:27
Hapana shaka juu ya jambo hili. Kumcha Bwana huongoza kwenye tabia njema, nazo huzuia ule upotevu wa uhai utokao katika dhambi na maovu. Pia lile pumziko takatifu lichipukalo katika imani ya Bwana Yesu humsaidia sana mtu awapo mgonjwa. Kila tabibu hufurahi kuwa na mgonjwa ambaye nia yake imetulia kabisa. Wasiwasi huua, lakini kumtumaini Mungu ni kama dawa iponyayo.
Kwa hiyo tunazo taratibu zote za uhai mrefu, na kama kwa kweli ni kwa manufaa yetu, tutauona uzee mwema, na kuzifikia kaburi zetu kama miganda ya nafaka kwa majira yake. Tusishindwe na kutazamia mauti kwa ghafula wakati tuumwapo kidole tu, bali tutazamie kwamba yatupasa kuendelea kufanya kazi kwa muda mrefu wa kutosha wa siku.
Na itakuwaje kama tungeitwa hivi karibuni kwenda ulimwengu wa juu zaidi? Bila shaka hapangekuwa na jambo lo lote la kuhuzunika kwa wito huo, bali kila kitu cha kufurahia. Tukiishi au tukifa sisi ni wa Bwana. Tukiishi, Yesu atakuwa pamoja nasi; tukifa, tutakuwa pamoja na Yesu.
Kule kuongeza uhai kwa kweli kabisa ni kuishi tunapoishi, tusipoteze wakati, bali tuitumie kila saa kwa makusudi yaliyo bora zaidi. Na iwe hivyo siku hii.
Juni 23
ADUI ANA KWA ANA
"Kwa hiyo Bwana asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Hataingia mjini humu, wala hatapiga mshale huko, wala hatakuja mbele yake na ngao, wala hatafanya boma juu yake." 2 Fal. 19:32
Wala Senakeribu hakuutaabisha mji. Alikuwa amejisifu kwa sauti kuu, lakini hakuweza kuyatimiza matisho yake. Bwana aweza kuwazuia adui za watu wake katika tendo lenyewe. Simba awapo na mwana-kondoo kati ya mataya yake, Mchungaji mkuu wa kondoo aweza kumpokonya mawindo yake. Shida yetu kubwa hutoa nafasi tu ya udhihirisho mkuu zaidi wa uweza na hekima ya Kimungu.
Katika habari iliyo mbele yetu, yule adui mkali hakutokea mbele ya mji ambao aliutamani kuuangamiza. Hakuweza kupiga mshale wo wote wa kuudhi juu ya kuta, wala hakuweza kufanya kazi mitambo yo yote ya kuuzingira ili kubomoa ngome, wala hakuweza kufukia maboma yo yote ili kuwafungia wenyeji ndani. Labda katika habari yetu pia Bwana atawazuia adui zetu wasitutendee hata dhara dogo. Bila shaka aweza kubadili nia zao, au kuyafanya makusudi yao yashindwe kabisa hata watayaacha kwa furaha. Na tumtumaini Bwana na kuishika njia yake, naye atatuangalia. Naam, atatujaza sifa za mshangao tuonapo ukamilifu wa wokovu wake.
Tusimwogope adui hata atakapokuja kweli, na ndipo tumtumaini Bwana.
Juni 24
BWANA "AZIDISHAVYO"
"Amazia akamwambia mtu wa Mungu, Lakini tutafanyaje kwa habari ya zile talanta mia nilizowapa jeshi la Israeli? Mtu wa Mungu akajibu, Bwana aweza kukupa wewe zaidi ya hizi." 2 Nya. 25:9
Kama umefanya kosa, ustahimili hasara yake; lakini usitende kinyume cha mapenzi ya Bwana. Bwana aweza kukupa zaidi sana ya vile utakavyoweza kupoteza; na kama hafanyi hivyo, je! utaanza kupatana bei na kubishana na Mungu? Mfalme wa Yuda amekodi jeshi kutoka Israeli waabuduo sanamu, naye akaamriwa kuwarudisha kwao watu wa vita kwa sababu Bwana hakuwa pamoja nao. Alikuwa radhi kuliondoa jeshi, ila alihuzunika kulipa talanta mia bila faida. Ole, aibu iliyoje! Kama Bwana atatoa ushindi bila hao vibarua, hakika ilikuwa biashara njema kuwalipa mishahara yao na kuwaondokana.
Uwe radhi kupoteza fedha kwa ajili ya dhamiri, kwa ajili ya amani, kwa ajili ya Kristo. Uwe na hakika ya kwamba hasara kwa ajili ya Bwana si hasara. Hata katika maisha haya hulipwa kwa wingi zaidi: katika hali fulani Bwana huzuia hasara yo yote isitokee. Kwa habari ya uhai wetu usiokufa, kile tunachokipoteza kwa ajili ya Yesu kimewekwa akiba Mbinguni. Usisononeke kwa msiba unaoonekana bali sikiliza ule mnong'ono, "Bwana aweza kukupa wewe zaidi ya hizi."
Juni 25
NGAZI YA KWENDA MBINGUNI
"Akamwambia, Amin, amin, nawaambieni, Tangu sasa mtaziona mbingu zimefunuka, na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu." Yohana 1:51
Naam, kwa imani yetu maono haya ni dhahiri hata siku hii. Twaziona Mbingu zimefunuka. Yesu mwenyewe ameufungua ufalme ule kwa waaminio wote. Twachungulia mahali pa fumbo na utukufu, kwa maana ametufunulia. Tutapaingia karibuni, kwa maana yeye ndiye njia.
Sasa twaona maelezo ya ngazi ya Yakobo. Kati ya nchi na Mbingu pana biashara takatifu; sala hupanda, na majibu hushuka, kwa njia ya Yesu, Mpatanishi. Twaiona ngazi hii tunapomwona Bwana wetu. Ndani yake ngazi ya nuru sasa hutoa njia iliyo wazi kwenda kiti cha enzi cha Aliye juu. Na tuitumie, na kupandisha kwayo wajumbe wa sala zetu. Sisi wenyewe tutaishi maisha ya kimalaika kama tukikimbia kwenda Mbinguni katika maombezi, na kuzishika baraka za agano, kisha kushuka tena ili kuzitawanya karama hizo kati ya wanadamu.
Maono haya bora ambayo Yakobo aliyaona katika ndoto tu tutayageuza kuwa uhalisi ung'aao. Siku hii hasa tutakuwa juu na chini ya ngazi kila saa; tukipanda katika ushirika, na kushuka katika kazi ya kuwaokoa wenzetu wanadamu. Hii ni ahadi yako, Ee Bwana Yesu, na tuione ikitimizwa kwa furaha.
Juni 26
HAITAKAWIA
"Nanyi vumilieni; ithibitisheni mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia." Yakobo 5:8
Neno la mwisho katika Wimbo wa upendo ni, "Fanya haraka, mpenzi wangu," na kati ya maneno ya mwisho ya Ufunuo twasoma, "Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo"; ambaye Bwana-arusi wa mbinguni hujibu, "Naam, naja upesi." Upendo hutamani kudhihirika kwa utukufu kwa Bwana, na hufurahia ahadi hii tamu -- "Kuja kwake Bwana kunakaribia." Jambo hili hutuliza nia zetu kwa habari ya wakati ujao. Twachungulia nje kwa tumaini kupitia dirisha hili.
Hili "dirisha la akiki" takatifu huingiza mafuriko ya nuru juu ya wakati wa sasa, na kutuweka katika hali njema kwa kazi au mateso ya papo hapo. Je! twajaribiwa? Basi ukaribu wa furaha yetu hunong'ona uvumilivu. Je! twachoka kwa sababu hatuyaoni mavuno ya kupanda kwetu mbegu? Tena kweli hii tukufu hutulilia, "Vumilieni." Je! majaribu yetu yaliyoongezeka yatufanya tuyumbe hata kidogo? Basi ule uhakika, ya kwamba baada ya muda mfupi Bwana atakuwa hapa, hutuhubiria kutoka andiko hili, "Ithibitisheni mioyo yenu." Kuweni imara, kuweni thabiti, kuweni wa kudumu, "thabiti, msitikisike, sikuzote mkizidi sana katika kazi ya Bwana." Karibuni utazisikia tarumbeta za fedha zitangazazo kuja kwa Mfalme wako. Usiogope hata kidogo. Ushike ngome, kwa maana anakuja; naam, aweza kutokea siku hii hasa.
Juni 27
MSHUKURU; UKAE UKUBALIKE
"Hakika wenye haki watalishukuru jina lako; wanyofu watakaa mbele za uso wako." Zab. 140:13
Lo, laiti moyo wangu ungekuwa mnyofu, ili nipate kulibariki jina la Bwana sikuzote! Yeye ni mwema hivi kwa walio wema, hata ningependa kuwa miongoni mwao, na kujiona nimejaa shukrani kila siku. Labda, kwa kitambo, wenye haki hushtuka wakati unyofu wao huleta jaribu kali; lakini kwa hakika itakuja siku watakapombariki Mungu wao kwa kuwa hawakukubali mashawishi ya uovu na kuufuata mwenendo wa udanganyifu. Hatimaye watu wa kweli watamshukuru Mungu wa haki kwa kuwaongoza katika njia iliyo sawa. Lo, laiti ningekuwa miongoni mwao!
Ahadi iliyoje inayodokezwa katika kifungu hiki cha pili, "Wanyofu watakaa mbele za uso wako!" Watasimama wakikubaliwa mahali ambapo wengine hutokea ili kuhukumiwa tu. Watakuwa waheshimiwa wa Mfalme mkuu, wakiruhusiwa kusikilizwa wakati wo wote watakapotaka. Watakuwa wapendwa ambao juu yao Yehova hutabasamu, na ambao pamoja nao husemezana kwa neema. Bwana, natamani heshima hii kuu, upendeleo huu wa thamani: itakuwa Mbingu duniani kwangu kuufurahia. Nifanye mnyofu katika mambo yote, ili nipate leo, na kesho, na kila siku kusimama mbele za uso wako wa mbinguni. Ndipo nitakapolishukuru jina lako milele. Amina.
Juni 28
KUTAZAMA KUMOJA KWA BWANA
"Bwana akamgeukia, akasema, Enenda kwa nguvu zako hizi, ukawaokoe Israeli na mikono ya Wamidiani; je! si mimi niliyekutuma?" Waamuzi 6:14
Kutazama kulioje kule ambako Bwana alimtazama Gideoni! Alimtazama kutoka katika kukata tamaa kwake mpaka katika ushujaa mtakatifu. Kama kule kumtazama kwetu Bwana kwatuokoa, je! kule kutuangalia kwake kutafanya nini? Bwana, unitazame siku hii, ukanitie nguvu kwa wajibu na mapigano yake.
Neno lilioje hili Yehova alilomwambia Gideoni! "Enenda." Haikumpasa kusita. Angeliweza kujibu, "Je, niende katika udhaifu wote huu!" Lakini Bwana akalitupilia mbali neno lile kwa kusema, "Enenda kwa nguvu zako hizi." Bwana alikuwa amemtazamia nguvu ndani yake, wala sasa hakuwa na neno la kufanya ila kuzitumia, na kuwaokoa Israeli kwa kuwapiga Wamidiani. Yamkini Bwana ana mengi zaidi ya kufanya kwa mkono wangu kuliko nilivyowahi kuwaza. Kama amenitazama amenifanya kuwa hodari. Na nitumie kwa imani nguvu ile aliyonikabidhi. Kamwe haniambii "nipoteze wakati wangu bure katika nguvu zangu hizi." Sivyo kabisa. Sharti "niende," kwa sababu yeye ananitia nguvu.
Swali lilioje hili Bwana analoniuliza kama vile alivyomuuliza Gideoni! "Je! si mimi niliyekutuma?" Naam, Bwana, wewe umenituma, nami nitakwenda kwa nguvu zako. Kwa amri yako naenda, na, nikienda, nina hakika ya kwamba utashinda kwa mkono wangu.
Juni 29
MWALIKO WA KUSALI
"Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua." Yer. 33:3
Mungu hututia moyo tusali. Wao hutuambia ya kwamba sala ni zoezi la kicho lisilokuwa na nguvu ila juu ya nia inayoshughulika nayo. Sisi twajua vyema zaidi. Uzoefu wetu huukanusha uongo huu wa kikafiri mara elfu. Hapa Yehova, Mungu aliye hai, huahidi waziwazi kuijibu sala ya mtumishi wake. Na tumwite tena, wala tusikubali shaka yo yote juu ya swali la yeye kutusikia na kutujibu. Yeye aliyelifanya sikio, je! hatasikia? Yeye aliyewapa wazazi upendo kwa watoto wao, je! hatavisikiliza vilio vya wanawe na binti zake mwenyewe?
Mungu atawajibu watu wake wanaosihi katika dhiki yao. Anazo ajabu zilizowekwa akiba kwa ajili yao. Kile ambacho hawajapata kuona, kusikia habari zake, au kukiota, atawatendea. Atavumbua baraka mpya kama itahitajika. Ataipekua bahari na nchi ili kuwalisha: atamtuma kila malaika kutoka Mbinguni ili kuwasaidia, kama dhiki yao yaidai. Atatushangaza kwa neema yake, na kutufanya tuhisi ya kwamba haikutendeka namna hii kamwe kabla ya hapa. Yote atuombayo ni kwamba tumwite. Hawezi kutuomba lililo dogo kuliko hilo. Na tumtolee sala zetu kwa furaha mara moja.
Juni 30
NYUMA KISHA MBELE
"Lakini nitalikumbuka agano langu nililofanya nawe katika siku za ujana wako, nami nitathibitisha kwako agano la milele." Eze. 16:60
Ijapokuwa dhambi zetu, Bwana angali mwaminifu katika upendo wake kwetu. Hutazama nyuma. Tazama jinsi anavyozikumbuka siku zetu zile za kwanza alipotuingiza katika agano naye mwenyewe, nasi tukajitoa kwake. Siku za furaha zile! Bwana hatutukanyagii nazo, wala hatutushtaki kwa kuwa wanafiki. La, hutazama agano lake nasi zaidi kuliko agano letu naye. Hapakuwa na unafiki katika mapatano yale matakatifu, kwa upande wake, hata kidogo. Jinsi alivyo mwenye neema Bwana hivyo kutazama nyuma kwa upendo!
Hutazama mbele pia. Amekusudia ya kwamba agano halitaanguka. Kama sisi hatulisimamii, yeye hulisimamia. Hutangaza kwa dhati, "Nami nitathibitisha kwako agano la milele." Hana nia ya kurudi nyuma kutoka ahadi zake. Na libarikiwe jina lake, huuona ule muhuri mtakatifu, "damu ya agano la milele," na humkumbuka Mdhamini wetu, ambaye ndani yake alilithibitisha agano lile, naam, Mwanawe mpendwa mwenyewe; na kwa hiyo hupumzika katika ahadi zake za agano. "Yeye hudumu kuwa mwaminifu; hawezi kujikana mwenyewe."
Ee Bwana, liweke neno hili la thamani juu ya moyo wangu, ukanisaidie kulila siku hii yote!