Sura 10 · dakika 31 za kusoma
Tafsiri ya AI — inasubiri mapitio ya mzawa
Mwezi wa Septemba
Septemba 1
KUKAA KATIKA UTII, KATIKA UPENDO
"Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu" Yohana 15:10
Mambo haya hayawezi kutenganishwa -- kukaa katika utii, na kukaa katika pendo la Yesu. Ni maisha yaliyo chini ya utawala wa Kristo peke yake yawezayo kuthibitisha ya kuwa sisi ni vitu vya furaha ya Bwana wetu. Ni lazima tuishike amri ya Bwana wetu ikiwa twataka kufurahia pendo lake. Tukiishi katika dhambi hatuwezi kuishi katika pendo la Kristo. Pasipo utakatifu umpendezao Mungu, hatuwezi kumpendeza Yesu. Yeye asiyejali utakatifu hajui neno lo lote juu ya pendo la Yesu.
Kufurahia kwa moyo pendo la Bwana wetu ni jambo jepesi kuathirika. Huathirika na dhambi na utakatifu kuliko zebaki iathirikavyo na baridi na joto. Tunapokuwa wapole wa moyo, na waangalifu katika fikira, na midomo, na maisha ili kumheshimu Bwana wetu Yesu, ndipo tunapopokea alama za pendo lake zisizohesabika. Tukitaka kuudumisha ufurahi kama huo, ni lazima tuudumishe utakatifu. Bwana Yesu hatatuficha uso wake sisi, isipokuwa tukimficha sisi uso wetu. Dhambi hufanya lile wingu litialo giza Jua letu; lakini tukiwa watii kwa kuangalia na waliojiweka wakfu kabisa, twaweza kuenenda nuruni, kama Mungu alivyo nuruni, na kuwa na kukaa katika pendo la Yesu kwa uhakika kama vile Yesu akaavyo katika pendo la Baba. Hii ndiyo ahadi tamu yenye "kama" la kutisha. Bwana, unipe "kama" hili mkononi mwangu; kwa maana kama ufunguo lafungua kijaluba hiki.
Septemba 2
FUATA ILI UJUE
"Ndipo tutakapojua, tukiendelea kumjua Bwana" Hosea 6:3
Si mara moja, bali kwa hatua kwa hatua tutakavyoufikia ujuzi mtakatifu, na kazi yetu ni kuvumilia na kujifunza kidogo kidogo. Haituhitaji kukata tamaa, ijapokuwa maendeleo yetu ni ya polepole, kwa maana tutajua bado. Bwana, aliyekuwa Mwalimu wetu, hatatuacha, hata tukiwa wazito wa kufahamu kadiri gani; kwa kuwa si heshima yake kwamba kiasi cho chote cha upumbavu wa kibinadamu kishinde ustadi wake. Bwana hupendezwa kuwafanya wajinga kuwa wenye hekima.
Wajibu wetu ni kushikamana na kiini cha shughuli yetu, na kuendelea kujua, si fundisho hili la peke yake wala lile, bali Yehova Mwenyewe. Kumjua Baba, na Mwana, na Roho, Mungu wa Utatu, huu ndio uzima wa milele; na tushikamane na hili, kwa maana kwa njia hii tutapata mafundisho makamilifu. Kwa kuendelea kumjua Bwana, twajifunza kuponywa baada ya kuraruliwa, na kufungwa baada ya kupigwa, na uzima baada ya mauti. Yale tuyaonayo huwa na kazi yake kamili moyo ufuatapo njia ya Bwana Mwenyezi.
Ee nafsi yangu, ushikamane na Yesu, uendelee kumjua Mungu ndani ya Yesu, na hivyo utaufikia ujuzi wa Kristo, ulio bora kuliko elimu zote. Roho Mtakatifu atakuongoza uingie katika kweli yote. Je, hii siyo kazi yake ya neema? Umtegemee yeye aitimize.
Septemba 3
KUTOKA KATIKA MAUTI YA KIROHO
"Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka makaburini mwenu, enyi watu wangu" Ezekieli 37:13
Naam, ni lazima iwe hivyo; wale wapokeao uzima kutoka kwa wafu ni hakika watautambua mkono wa Bwana katika ufufuo kama huo. Huu ndio ubadiliko mkuu na wa ajabu kupita yote awezayo mtu kupata -- kutolewa kaburini mwa mauti ya kiroho, na kufanywa kuufurahia mwanga na uhuru wa uzima wa kiroho. Hakuna awezaye kutenda hili ila Mungu aliye hai, Bwana na mtoaji wa uzima.
Ee mimi! Nakumbuka vyema jinsi nilivyokuwa nikilala bondeni palipojaa mifupa mikavu, mkavu kama mmojawapo wao! Ilikuwa heri siku ile neema huru na kuu ilipomtuma mtu wa Mungu kutabiri juu yangu! Utukufu na uwe kwa Mungu kwa mtetemeko ule lile neno la imani lililoleta kati ya ile mifupa mikavu. Heri zaidi ni ule pumzi wa mbinguni utokao pande zote nne za pepo uliyonifanya niwe hai! Sasa naijua Roho ihuishayo ya Yehova aishiye milele. Kweli Yehova ndiye Mungu aliye hai, kwa maana amenifanya niishi. Uzima wangu mpya, hata katika kuugua na kuhuzunika kwake, ni ushuhuda dhahiri kwangu ya kuwa Bwana aweza kuua na kuhuisha. Yeye ndiye Mungu peke yake. Yeye ndiye kila kilicho kikuu, na chenye neema, na chenye utukufu, na nafsi yangu iliyohuishwa yamsujudia kama yule MIMI NIKO mkuu. Utukufu wote na uwe kwa jina lake takatifu! Maadamu ni hai nitamsifu.
Septemba 4
USHINDI PASIPO VITA
"Lakini nitawahurumia nyumba ya Yuda, nami nitawaokoa kwa Bwana, Mungu wao, wala sitawaokoa kwa upinde, wala kwa upanga, wala kwa vita, wala kwa farasi, wala kwa wapanda farasi" Hosea 1:7
Neno la thamani! Yehova Mwenyewe atawaokoa watu wake katika ukuu wa rehema yake, lakini hatalitenda hilo kwa njia za kawaida. Watu ni wazito kumpa Mungu utukufu uupasao jina lake. Wakienda vitani kwa upanga na upinde, na kuushinda, wangempasa kumsifu Mungu wao; lakini hawafanyi hivyo, bali huanza kuutukuza mkono wao wa kuume wenyewe, na kujisifu kwa farasi zao na wapanda farasi wao. Kwa sababu hii Yehova wetu mara nyingi hukusudia kuwaokoa watu wake pasipo njia za pili, ili heshima yote iwe kwake yeye peke yake.
Basi, ee moyo wangu, umtazame Bwana peke yake, wala si mwanadamu. Utazamie kumwona Mungu kwa uwazi zaidi wakati hakuna mwingine wa kumtazama. Nisipokuwa na rafiki, wala mshauri, wala mtu wa kuniunga mkono, nisiwe na tumaini pungufu ikiwa naweza kuhisi kwamba Bwana Mwenyewe yu upande wangu; naam, na nifurahi akinipa ushindi pasipo vita, kama vile andiko laonekana kudokeza. Kwa nini niombe farasi na wapanda farasi ikiwa Yehova Mwenyewe ananihurumia, na kuuinua mkono wake kwa ulinzi wangu? Kwa nini nihitaji upinde wala upanga ikiwa Mungu ataokoa? Na nitumaini, wala nisiogope, tangu leo na hata milele. Amina.
Septemba 5
PAMOJA NAMI KOKOTE NILIPO
"Bwana atakuwa pamoja nanyi" 2 Mambo ya Nyakati 20:17
Hii ilikuwa rehema kuu kwa Yehoshafati, kwa maana mkutano mkubwa ulikuwa umetoka kupigana naye; nayo itakuwa rehema kuu kwangu, kwa maana nina uhitaji mkubwa, wala sina nguvu wala hekima. Bwana akiwa pamoja nami, si kitu ni nani atakayeniacha. Bwana akiwa pamoja nami, nitashinda katika vita vya maisha, na kadiri majaribu yangu yatakavyokuwa makubwa, ndivyo ushindi wangu utakavyokuwa wa utukufu zaidi. Nitajuaje kwa hakika ya kuwa Bwana yu pamoja nami?
Kwa hakika yu pamoja nami ikiwa mimi ni pamoja naye. Nikiitumaini uaminifu wake, na kuyaamini maneno yake, na kuzitii amri zake, yeye yu pamoja nami bila shaka. Nikiwa upande wa Shetani Mungu yu kinyume changu, wala haiwezi kuwa vinginevyo; lakini nikiishi ili kumheshimu Mungu naweza kuwa na hakika ya kuwa atanheshimu mimi.
Nina hakika kabisa ya kuwa Mungu yu pamoja nami ikiwa Yesu ndiye Mwokozi wangu wa pekee na wa peke yake. Ikiwa nimeiweka nafsi yangu mikononi mwa Mwana pekee wa Mungu, ndipo naweza kuwa na hakika ya kuwa Baba atazitumia nguvu zake zote kunihifadhi, ili Mwana wake asivunjiwe heshima.
Laiti ningekuwa na imani ya kulishika andiko fupi lakini tamu la leo! Ee Bwana, litimize neno hili kwa mtumishi wako! Uwe pamoja nami nyumbani, njiani, shambani, dukani, katika kundi la watu, na peke yangu. Uwe pia pamoja na watu wako wote.
Septemba 6
MOYO WENYE NGUVU
"Umngoje Bwana; uwe hodari, naye atautia nguvu moyo wako; naam, umngoje Bwana" Zaburi 27:14
Ngoja! Ngoja! Kungoja kwako na kuwe kwa Bwana! Yeye anastahili kungojewa. Yeye hamwangushi kamwe nafsi ingojayo.
Wakati wa kungoja, uutunze moyo wako. Utazamie wokovu mkuu, na uwe tayari kumsifu Mungu kwa ajili yake.
Ahadi ikupasayo kukutia moyo i katikati ya mstari -- "naye atautia nguvu moyo wako." Hili laenda mara moja mahali unapohitaji msaada. Moyo ukiwa mzima, viungo vingine vyote vya mwili vitatenda kazi vema. Moyo wahitaji kutulizwa na kutiwa moyo; na yote mawili haya yatakuja moyo ukitiwa nguvu. Moyo wenye nguvu hupumzika na kufurahi, na kusukuma nguvu ndani ya mtu mzima.
Hakuna mwingine awezaye kuifikia ile chombo ya siri ya uzima, yaani moyo, hata kuumiminia nguvu. Yeye peke yake aliyeuumba ndiye awezaye kuufanya wenye nguvu. Mungu amejaa nguvu, na kwa hiyo, aweza kuwapa wale wanaozihitaji. Basi, uwe hodari; kwa maana Bwana atakupa nguvu zake, nawe utakuwa mtulivu wakati wa dhoruba, na mwenye furaha wakati wa huzuni.
Yeye aliyeandika maneno haya aweza kuandika kama Daudi alivyoandika--"naam, umngoje Bwana." Nasema, kwa kweli, hivyo. Najua kwa uzoefu wa muda mrefu na wa kina ya kuwa ni vema kwangu kumngoja Bwana.
Septemba 7
UFIKIO WA NEEMA YA MWENYEZI
"Itakuwa, mahali pale walipoambiwa, Ninyi si watu wangu, huko wataambiwa, Ninyi ni wana wa Mungu aliye hai" Hosea 1:10
Neema kuu yaweza kuwafanya wageni kuwa wana, na Bwana hapa atangaza kusudi lake la kuwatendea waasi hivyo, na kuwafanya wajue alilolitenda. Ee msomaji mpendwa, Bwana amelitenda hili kwangu; je, amekutendea vivyo hivyo? Basi na tuunganishe mikono na mioyo katika kulisifu jina lake linalostahili kuabudiwa.
Baadhi yetu tulikuwa wasiomcha Mungu kabisa hata Neno la Bwana lilisema kwa kweli kabisa katika dhamiri na moyo wetu, "Ninyi si watu wangu." Katika nyumba ya Mungu, na katika nyumba zetu wenyewe, tulipoisoma Biblia, hii ilikuwa sauti ya Roho wa Mungu ndani ya nafsi zetu, "Ninyi si watu wangu." Kweli ilikuwa sauti ya huzuni ihukumuyo. Lakini sasa, mahali pale pale, kutoka huduma ile ile na Andiko lile lile, twasikia sauti isemayo, "Ninyi ni wana wa Mungu aliye hai." Je, twaweza kushukuru vya kutosha kwa ajili ya hili? Je, si jambo la ajabu? Je, halitupi tumaini kwa ajili ya wengine? Ni nani aliye nje ya ufikio wa neema ya Mwenyezi? Twawezaje kukata tamaa juu ya ye yote, kwa kuwa Bwana ametenda badiliko la ajabu namna hii ndani yetu?
Yeye aliyeishika ahadi hii moja kuu ataishika kila ahadi nyingine; kwa hiyo, na tusonge mbele kwa nyimbo za kuabudu na za tumaini.
Septemba 8
ULIOPONDEKA NA UTOAO MOSHI
"Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima" Isaya 42:3
Basi naweza kutumaini kutendewa kwa upole na Bwana wangu. Naam, najihisi kuwa, hata katika hali yangu iliyo bora, dhaifu, na mwepesi kuinama, na duni kama unyasi. Mtu mmoja alisema, "Sikuthamini wewe hata kama unyasi," na usemi huo, ujapokuwa si wa fadhili, haukuwa wa uongo. Ole wangu! Mimi ni mbaya kuliko unyasi ukuapo kando ya mto, kwa maana huo waweza angalau kukiinua kichwa chake. Mimi nimepondeka, vibaya, kwa huzuni nimepondeka. Hakuna muziki ndani yangu sasa; kuna ufa uruhusuo sauti yote nzuri kutoka. Ole wangu! Lakini Yesu hatanivunja mimi; na kama hatafanya hivyo, basi sijali sana wale wengine wajaribuo kufanya nini. Ee Bwana mwenye utamu na huruma, najibanza chini ya ulinzi wako, na kuzisahau michubuko yangu!
Kweli mimi pia nastahili kufananishwa na "utambi utokao moshi," ambao nuru yake imekwisha, na moshi wake tu ndio uliobaki. Nachelea kuwa mimi ni kero kuliko faida. Hofu zangu zaniambia kwamba ibilisi ameuzima mwanga wangu, na kuniacha moshi wa kuchukiza, na kwamba Bwana wangu karibu atanizimisha kabisa. Lakini natambua ya kuwa ijapokuwa palikuwa na mikasi chini ya sheria, hapakuwa na vizimisha moto; naye Yesu hatanizima mimi; kwa hiyo, nina tumaini. Bwana, uniwashe upya, na kunifanya niangaze kwa utukufu wako, na kwa kuutukuza wororo wako.
Septemba 9
HOFU INA NAFASI YAKE
"Heri mtu yule aogopaye sikuzote" Mithali 28:14
Kumcha Bwana ndio mwanzo na msingi wa dini yote ya kweli. Pasipo kicho kitakatifu na heshima kwa Mungu hakuna pahali pa kukanyaga kwa fadhila zilizo bora zaidi. Yeye ambaye nafsi yake haiabudu hataishi kamwe katika utakatifu.
Ana furaha yeye ahisiye hofu ya wivu ya kutenda mabaya. Hofu takatifu haitazami kabla ya kuruka tu, bali hata kabla ya kunyanyuka. Yaogopa kosa, yaogopa kupuuza wajibu, yaogopa kutenda dhambi. Yaogopa marafiki wabaya, na maongezi ya upuuzi, na siasa ya mashaka. Hili halimfanyi mtu kuwa mnyonge, bali humletea furaha. Mngoji aliye macho ana furaha kuliko askari alalaye kituoni pake. Yeye aonaye mbele uovu na kuukimbia ana furaha kuliko yeye aendaye bila kujali na kuangamizwa.
Kumcha Mungu ni neema ya utulivu imwongozayo mtu katika njia iliyo bora, ambayo juu yake imeandikwa, "Hakuna simba atakayekuwako huko, wala mnyama mkali hatapanda hapo." Kuogopa hata sura ya uovu ni kanuni itakasayo, imwezeshayo mtu, kwa nguvu za Roho Mtakatifu, kuyaweka mavazi yake bila kutiwa doa na ulimwengu. Kwa maana zote mbili yeye "aogopaye sikuzote" hufanywa mwenye furaha. Sulemani alikuwa amejaribu yote mawili, mambo ya kidunia na hofu takatifu; katika lile aliona ubatili, na katika hili furaha. Tusiyarudie majaribu yake, bali na tushike hukumu yake.
Septemba 10
KUINGIA; KUTOKA
"Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo" Kumbukumbu 28:6
Baraka za sheria hazikufutwa. Yesu aliithibitisha ahadi alipoichukua adhabu. Nikizishika amri za Bwana wangu, naweza kuitwaa ahadi hii bila shaka.
Siku hii nitaingia nyumbani mwangu bila kuogopa habari mbaya, nami nitaingia chumbani mwangu cha faragha nikitazamia kusikia habari njema kutoka kwa Bwana wangu. Sitaogopa kuingia ndani ya nafsi yangu kwa kujichunguza, wala kuingia katika mambo yangu kwa kuyakagua kwa bidii shughuli zangu. Nina kazi nyingi ya kufanya ndani, ndani ya nafsi yangu mwenyewe; laiti ningepata baraka juu ya yote hayo, baraka ya Bwana Yesu, aliyeahidi kukaa pamoja nami.
Ni lazima pia nitoke. Uoga wanifanya nitamani ningeweza kukaa ndani, wala nisiingie tena katika ulimwengu wenye dhambi. Lakini ni lazima nitoke katika wito wangu, na ni lazima nitoke ili niwe na faida kwa ndugu zangu, na wa manufaa kwa wasiomcha Mungu. Ni lazima niwe mtetezi wa imani na mshambulizi wa uovu. Laiti ningepata baraka juu ya kutoka kwangu siku hii! Bwana, na niende uongozako, katika shughuli zako, chini ya amri yako, na katika nguvu za Roho wako.
Bwana Yesu, ingia pamoja nami uwe mgeni wangu; kisha utoke pamoja nami, na kuufanya moyo wangu uwake wakati unaposema nami njiani.
Septemba 11
WATESWAO HUWA WAAMINI IMARA
"Ni vyema mtu kuuchukua nira wakati wa ujana wake" Maombolezo 3:27
Hili ni sawa na ahadi. Imekuwa vyema, ni vyema, na itakuwa vyema kwangu kuuchukua nira.
Mapema maishani ilinipasa kuuhisi uzito wa kushtakiwa dhamiri, na tangu hapo umethibitika kuwa mzigo uitajirishao nafsi. Je, ningeipenda injili kiasi hiki kama nisingejifunza kwa uzoefu wa kina uhitaji wa wokovu kwa neema? Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko ndugu zake kwa sababu mama yake alimzaa kwa huzuni, na wale wanaoteseka sana katika kuzaliwa kwa Mungu huwa waamini imara wa neema kuu.
Nira ya lawama ni ya kuchosha, lakini humwandaa mtu kwa heshima ijayo. Hafai kuwa kiongozi yeye asiyepita katika dharau. Sifa hulevya kama haikutanguliwa na matukano. Watu wapandao kwenye ukuu bila kujitaabisha kwa kawaida huanguka katika aibu.
Nira ya mateso, na kukata tamaa, na kazi iliyopita kiasi kamwe haipaswi kutafutwa; lakini Bwana anapoiweka juu yetu katika ujana wetu mara nyingi hukuza tabia imtukuzayo Mungu na kuibariki Kanisa.
Njoo, ee nafsi yangu, inama shingo yako; jitwike msalaba wako. Ilikuwa vyema kwako ulipokuwa kijana, haitakudhuru sasa. Kwa ajili ya Yesu, ujibebe mabegani kwa furaha.
Septemba 12
NA NYUMBA YANGU JE?
"Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka, wewe na nyumba yako" Matendo 16:31
Injili hii kwa mtu aliye na upanga kooni mwake ndiyo injili kwangu mimi. Hii ingenifaa kama ningekuwa nakufa, nayo ndiyo yote niitakayo maadamu ni hai. Naugeuza uso wangu mbali na nafsi, na dhambi, na wazo lo lote la ustahili wangu binafsi, nami namtumaini Bwana Yesu kuwa Mwokozi ambaye Mungu amemtoa. Namwamini yeye, napumzika juu yake, namkubali kuwa vyangu vyote. Bwana, nimeokoka, nami nitaokolewa hata milele yote, kwa maana namwamini Yesu. Libarikiwe jina lako kwa ajili ya hili. Na nithibitishe kila siku kwa maisha yangu ya kuwa nimeokolewa na ubinafsi, na mambo ya kidunia, na kila namna ya uovu.
Lakini yale maneno ya mwisho juu ya "nyumba" yangu: Bwana, sitaki kukimbia na nusu ya ahadi wewe utoapo ahadi nzima. Nakusihi, uwaokoe jamaa yangu wote. Waokoe walio karibu na wapendwa zaidi. Waongoe watoto, na wajukuu, kama ninao. Uwe na neema kwa watumishi wangu, na wote wakaao chini ya dari yangu, au wanaonifanyia kazi. Wewe waniahidia ahadi hii mimi binafsi ikiwa namwamini Bwana Yesu; nakusihi ufanye kama ulivyosema.
Ningeyapitia katika sala yangu kila siku majina ya ndugu zangu wote wanaume na wanawake, na wazazi, na watoto, na rafiki, na jamaa, na watumishi, wala nisikupe pumziko hata neno lile litimizwe, "na nyumba yako."
Septemba 13
UMANDE WA MBINGUNI
"Naam, mbingu zake zitadondoza umande" Kumbukumbu 33:28
Kama vile umande wa Mashariki ulivyo kwa ulimwengu wa asili, ndivyo ulivyo uvutano wa Roho katika ufalme wa neema. Jinsi ninavyouhitaji sana! Pasipo Roho wa Mungu mimi ni kitu kikavu kilichonyauka. Nasinyaa, nafifia, nafa. Jinsi umande huu unavyoniburudisha kwa utamu! Nikipata kupewa fadhili yake nahisi furaha, na uhai, na nguvu, na kuinuliwa. Sitaki kitu zaidi. Roho Mtakatifu huniletea uzima, na yote uzima unayohitaji. Kila kitu kingine pasipo umande wa Roho ni pungufu ya bure kwangu: nasikia, nasoma, nasali, naimba, naenda mezani pa ushirika, wala sioni baraka yo yote huko hata Roho Mtakatifu anipojia. Lakini anaponinyunyizia umande, kila njia ya neema ni tamu na yenye faida.
Ni ahadi iliyoje hii kwangu! "Mbingu zake zitadondoza umande." Nitajiliwa na neema. Sitaachwa katika ukame wangu wa asili, wala katika joto liunguzalo la ulimwengu, wala katika upepo mkali wa jaribu la Kishetani. Laiti saa hii hasa ningeuhisi umande wa Bwana ulio mpole, kimya, uzamiao ndani! Kwa nini nisiuhisi? Yeye aliyenifanya niishi kama nyasi iishivyo malishoni, atanitendea kama awatendeavyo nyasi; ataniburudisha kutoka juu. Nyasi haiwezi kuuomba umande kama niuombavyo. Hakika, Bwana ajiaye mmea usiosali atamjibu mtoto wake amsihiye.
Septemba 14
ALAMA YA KIBALI CHA MUNGU
"Heri mtu yule astahimiliye majaribu; kwa maana akiisha kukubaliwa, atapokea taji ya uzima ambayo Mungu amewaahidia wale wampendao" Yakobo 1:12
Naam, ana heri wakati anapohimili jaribu. Hakuna jicho liwezalo kuona hili hata liwe limepakwa mafuta ya macho ya mbinguni. Lakini yampasa alihimili, wala asimwasi Mungu, wala asigeuke kando na uadilifu wake. Ana heri yeye aliyepita katika moto, wala hakuteketezwa kama bidhaa bandia.
Jaribu likiisha, ndipo huja alama ya kibali cha Mungu -- "taji ya uzima." Kana kwamba Bwana alisema, "Na aishi; amepimwa katika mizani, wala hakuonekana kuwa pungufu." Uzima ndiyo thawabu: si kuwako tu; bali kuwako kutakatifu, kwenye furaha, kwa kweli, yaani kutimizwa kwa kusudi la Mungu juu yetu. Tayari namna ya juu zaidi ya uzima wa kiroho na furaha huwavika taji wale waliopita salama katika majaribu makali sana ya imani na upendo.
Bwana amewaahidia taji ya uzima wale wampendao. Ni wampendao Bwana peke yao watakaovumilia katika saa ya jaribu; wengine watazama au watanuna, au watajiondoa kwa siri warudi ulimwenguni. Njoo, ee moyo wangu, je, wampenda Bwana wako? Kweli? Kwa kina? Kwa ukamilifu? Basi upendo huo utajaribiwa; lakini maji mengi hayatauzima, wala mafuriko hayatauzamisha. Bwana, upendo wako na uulishe wangu hata mwisho.
Septemba 15
KIMBILIO SALAMA KULIKO YOTE
"Na mtu atakuwa kama mahali pa kujificha na upepo, na mahali pa kujisitiri na dhoruba." Isaya 32:2
Ni nani MTU huyu sote twamjua. Angekuwa nani ila Mtu wa Pili, Bwana atokaye Mbinguni, Mtu wa huzuni, Mwana wa Adamu? Ni mahali pa kujificha palivyoje amekuwa kwa watu wake! Yeye Mwenyewe hustahimili nguvu kamili ya upepo, na hivyo huwakinga wale wajifichao ndani yake. Hivyo tumeokoka ghadhabu ya Mungu, na hivyo tutaokoka hasira ya wanadamu, na masumbufu ya maisha haya, na hofu ya mauti. Kwa nini tusimame katika upepo hali twaweza kwa wepesi na kwa uhakika kutoka humo kwa kujificha nyuma ya Bwana wetu? Siku hii na tumkimbilie yeye, tupate amani.
Mara nyingi upepo wa kawaida wa taabu huongezeka nguvu na kuwa dhoruba, ukifagia kila kitu mbele yake. Vitu vilivyoonekana imara na thabiti hutikisika katika kishindo, na maanguko ni mengi na makuu kati ya matumaini yetu ya kimwili. Bwana wetu Yesu, yule Mtu wa utukufu, ni sitara isiyoangushwa kamwe. Ndani yake twaiona dhoruba ikipita kando, lakini sisi wenyewe twapumzika katika utulivu wa kupendeza.
Siku hii na tujifiche tu katika mahali petu pa kujificha, na kuketi na kuimba chini ya ulinzi wa Sitara yetu. Ee Yesu mbarikiwa! Ee Yesu mbarikiwa! Jinsi tunavyokupenda! Twastahili kufanya hivyo, kwa maana wewe kwetu ni kimbilio wakati wa dhoruba.
Septemba 16
THAWABU NI YA HAKIKA
"Na ye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ombe la maji ya baridi tu, kwa jina la mwanafunzi, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake kamwe" Mathayo 10:42
Basi, naweza kufanya kadiri hiyo. Naweza kutenda tendo la fadhili kwa mtumishi wa Bwana. Bwana anajua nawapenda wote, na ningehesabu kuwa heshima kuwaosha miguu yao. Kwa ajili ya Bwana wao nawapenda wanafunzi.
Ni neema iliyoje ya Bwana kutaja tendo dogo namna hii -- "kumnywesha ombe la maji ya baridi tu"! Hili naweza kulitenda, hata niwe maskini kadiri gani: hili naweza kulitenda, hata niwe mnyonge kadiri gani: hili nitalitenda kwa furaha kabisa. Hili, lionekanalo dogo namna hii, Bwana alitambua -- alitambua litendwapo kwa aliye mdogo kuliko wote wa wafuasi wake. Ni dhahiri si gharama, wala ustadi, wala wingi, aliuangaliao yeye, bali nia: kile tumfanyiacho mwanafunzi, kwa sababu yeye ni mwanafunzi, Bwana wake huona, na kulipa. Hatulipi kwa ustahili wa kile tukitendacho, bali kwa kadiri ya utajiri wa neema yake.
Nampa ombe la maji ya baridi, naye hunifanya ninywe maji yaliyo hai. Nampa mmoja wa wadogo wake, naye hunitendea kama mmoja wao. Yesu hupata sababu ya ukarimu wake katika kile ambacho neema yake imeniongoza kutenda, naye asema, "Hatakosa thawabu yake kamwe."
Septemba 17
KAMA MTENDE NA MWEREZI
"Mwenye haki atasitawi kama mtende; atakua kama mwerezi wa Lebanoni" Zaburi 92:12
Miti hii haifundishwi wala kupogolewa na mwanadamu: mitende na mierezi ni "miti ya Bwana," na ni kwa uangalizi wake ndipo isitawipo; vivyo hivyo ilivyo kwa watakatifu wa Bwana, wao ni uangalizi wake mwenyewe. Miti hii ni ya kijani kibichi sikuzote na ni vitu vizuri katika majira yote ya mwaka. Waaminio si watakatifu mara nyingine na wasiomcha Mungu mara nyingine: husimama katika uzuri wa Bwana chini ya hali zote za hewa. Kila mahali miti hii huvutia macho: hakuna awezaye kutazama mandhari yenye mitende au mierezi bila fikira zake kukazwa juu ya mimea hii ya kifalme. Wafuasi wa Yesu ni wale watazamwao na watazamaji wote: kama mji uliowekwa juu ya mlima hawawezi kusitirika.
Mtoto wa Mungu husitawi kama mtende, usukumao nguvu zake zote juu katika nguzo moja iliyonyooka bila tawi hata moja. Ni nguzo yenye kilele cha utukufu. Hauna ukuaji kwenda kuume wala kushoto, bali hupeleka nguvu zake zote kuelekea mbinguni, na huzaa matunda yake karibu na mbingu kadiri iwezekanavyo. Bwana, itimize ishara hii ndani yangu.
Mwerezi hustahimili dhoruba zote, na hukua karibu na theluji za milele, Bwana Mwenyewe akiujaza utomvu uufanyao moyo wake wenye joto na matawi yake yenye nguvu. Bwana, na iwe hivyo kwangu, nakuomba. Amina.
Septemba 18
USALAMA KAMILI
"Katika habari za Benyamini akasema, Mpendwa wa Bwana atakaa salama karibu naye; Bwana atamsitiri mchana kutwa, naye atakaa katikati ya mabega yake" Kumbukumbu 33:12
Naam, hakuna usalama kama ule utokao katika kukaa karibu na Mungu. Kwa mpendwa wake aliye bora Bwana hawezi kupata mahali paliyo hakika au salama zaidi. Ee Bwana, na nikae daima chini ya kivuli chako, karibu na ubavu wako uliojeruhiwa. Karibu zaidi na zaidi ningekuja kwako, Bwana wangu; na nikiisha kuwa karibu nawe hasa, ningekaa hapo milele.
Ni kifuniko kilichoje kile Bwana awapacho wateule wake! Si dari nzuri itakayomsitiri, wala dirisha lisilopenywa na mizinga, wala hata bawa la malaika, bali Yehova Mwenyewe. Hakuna kiwezacho kutufikia tunapokuwa tumefunikwa hivyo. Kifuniko hiki Bwana atatupa mchana kutwa, hata siku iwe ndefu kadiri gani. Bwana, na nikae siku hii nikijua chini ya kibanda hiki cha upendo, hema hii ya nguvu kuu.
Je, kifungu cha tatu chamaanisha kwamba Bwana katika hekalu lake angekaa kati ya milima ya Benyamini, au kwamba Bwana angekuwa mahali mzigo wa Benyamini ungewekwa, au chamaanisha kwamba sisi twachukuliwa juu ya mabega ya Yeye wa Milele? Vyo vyote iwavyo, Bwana ndiye tegemeo na nguvu za watakatifu wake. Bwana, na niufurahie daima msaada wako na ndipo mikono yangu itakapotosha kwangu.
Septemba 19
SABABU YA KUIMBA
"Bwana, Mungu wako, aliye katikati yako, ni mwenye nguvu, atakuokoa; atakufurahia kwa furaha, atakutuliza katika pendo lake, atakushangilia kwa kuimba" Sefania 3:17
Ni neno lililoje hili! Yehova Mungu katikati ya watu wake katika fahari yote ya nguvu zake! Uwepo huu peke yake watosha kututia amani na tumaini. Hazina za uweza usio na mpaka zimehifadhiwa ndani ya Yehova wetu, naye akaa katika kanisa lake, kwa hiyo watu wake na wapige kelele kwa furaha.
Hatuna uwepo wake tu, bali yu katika kazi yake iliyo bora ya wokovu. "Atakuokoa." Yeye huokoa daima: hulitwaa jina lake la Yesu kutoka humo. Tusiogope hatari yo yote, kwa maana yeye ni hodari wa kuokoa.
Wala si hivi tu. Yeye hukaa yeye yule sikuzote; hupenda, hupata pumziko katika kupenda, hataacha kupenda. Upendo wake humpa furaha. Hata hupata kiini cha wimbo katika mpendwa wake. Hili ni la ajabu mno. Mungu alipoiumba dunia hakuimba, bali alisema tu, "Ni chema sana"; lakini alipoujia ukombozi, ndipo Utatu Mtakatifu ulipohisi furaha ipasayo kuelezwa kwa wimbo. Lifikirie hilo, ukastaajabu! Yehova Yesu huimba wimbo wa arusi juu ya bibi arusi wake mteule. Yeye kwake ni upendo wake, na furaha yake, na pumziko lake, na wimbo wake. Ee Bwana Yesu, kwa upendo wako usiopimika kwetu utufundishe kukupenda wewe, na kukufurahia wewe, na kukuimbia wewe zaburi ya maisha yetu.
Septemba 20
UTAYARI KAMILI
"Watu wako watajitolea kwa hiari siku ya nguvu zako" Zaburi 110:3
Abarikiwe Mungu wa neema kwa kuwa ni hivyo! Anao watu aliowachagua tangu zamani wawe fungu lake la pekee. Hawa kwa asili wana nia zilizo ngumu kama wana wengine wakaidi wa Adamu; lakini siku ya nguvu zake ifikapo, na neema idhihirishapo uweza wake wote, huwa tayari kutubu, na kumwamini Yesu. Hakuna aokolewaye pasipo hiari yake, bali nia hufanywa kwa utamu ijitoe yenyewe. Ni nguvu ya ajabu iliyoje hii, isiyoihalifu nia kamwe, na hata hivyo huitawala! Mungu haivunji kufuli, bali huifungua kwa ufunguo mkuu ambao yeye peke yake awezaye kuutumia.
Sasa tu tayari kuwa, na kutenda, au kuteseka kama Bwana apendavyo. Wakati wo wote tukiwa waasi, yampasa tu atujie kwa nguvu, na mara hiyo twapiga mbio katika njia ya amri zake kwa mioyo yetu yote. Siku hii na iwe siku ya nguvu kwangu katika jitihada fulani tukufu kwa utukufu wa Mungu na wema wa wenzangu! Bwana, mimi ni tayari; je, sipati kutumaini ya kuwa hii ni siku ya nguvu zako? Nimo mikononi mwako kabisa; tayari, naam, na shauku, kutumiwa nawe kwa makusudi yako matakatifu. Ee Bwana, nisije nikalazimika kulia, "Kutaka nataka, lakini kutenda lile nilitakalo, sipati," bali nipe nguvu kama unipavyo nia.
Septemba 21
MAJARIBU NA YABARIKI
"Tukijua ya kuwa dhiki huleta saburi" Warumi 5:3
Hii ni ahadi kwa hakika, ijapokuwa si kwa umbo. Twahitaji saburi, na hapa twaiona njia ya kuipata. Ni kwa kuvumilia tu ndipo tujifunzapo kuvumilia, kama vile kwa kuogelea watu wajifunzavyo kuogelea. Hungeweza kujifunza ustadi huo katika nchi kavu, wala kujifunza saburi pasipo taabu. Je, si jambo la faida kupatwa na dhiki kwa ajili ya kupata utulivu ule mzuri wa akili ukubaliyo kimya mapenzi yote ya Mungu?
Lakini andiko letu laonyesha jambo la pekee, lisilo kwa kadiri ya asili, bali ni la kimuujiza. Dhiki yenyewe kwa nafsi yake huleta ukorofi, na kutokuamini, na uasi. Ni kwa uganga mtakatifu wa neema tu ndipo ifanywapo kutenda saburi ndani yetu. Hatupigi ngano ili kutuliza vumbi: lakini fimbo ya dhiki hufanya hivyo juu ya sakafu ya Mungu. Hatumrushi mtu huku na huku ili kumpa pumziko, na hata hivyo ndivyo Bwana awatendeavyo watoto wake. Kweli hii si desturi ya mwanadamu, bali huleta sana utukufu kwa Mungu wetu mwenye hekima yote.
Laiti ningepata neema ya kuyaacha majaribu yangu yanibariki! Kwa nini nitamani kuizuia kazi yake ya neema? Bwana, nakuomba uniondolee dhiki yangu, lakini nakusihi mara kumi zaidi uniondolee kukosa saburi kwangu. Ee Bwana Yesu wa thamani, kwa msalaba wako uchore sura ya saburi yako juu ya moyo wangu.
Septemba 22
MITO MIPANA PASIPO MASHUA
"Bali huko Bwana atakuwa pamoja nasi katika utukufu wake, mahali pa mito mipana na vijito; ambapo hapatapita mashua yenye makasia, wala merikebu nzuri haitapita huko" Isaya 33:21
Bwana atakuwa kwetu wema mkuu kupita yote pasipo hasara zo zote zionekanazo kwa lazima kuandamana na vitu vya duniani vilivyo bora. Mji ukipata baraka ya mito mipana, waweza kushambuliwa na mashua zenye makasia, na merikebu nyingine za vita. Lakini Bwana afananishapo wingi wa ukarimu wake kwa mfano huu, huchunga waziwazi kuiondoa hofu ambayo fumbo laweza kuidokeza. Ubarikiwe upendo wake ulio kamili!
Bwana, ukiniletea utajiri kama mito mipana, usiiache mashua yenye makasia ipande katika sura ya mambo ya kidunia au kiburi. Ukinipa afya tele na moyo wa furaha, usiiache "merikebu nzuri" ya raha ya kimwili ije ikisafiri juu ya mafuriko yatiririkayo. Nikipata ufanisi katika utumishi mtakatifu, mpana kama mto Rhine wa Ujerumani, hata hivyo nisiiona kamwe mashua ya majivuno na kujiamini nafsi ikielea juu ya mawimbi ya manufaa yangu. Kama ningekuwa na furaha kuu namna hii hata niufurahie mwanga wa uso wako mwaka baada ya mwaka, hata hivyo nisiwadharau kamwe watakatifu wako walio dhaifu, wala nisiiache dhana ya bure ya ukamilifu wangu mwenyewe isafiri juu ya mito mipana ya uhakika wangu ulio kamili. Bwana, nipe baraka ile itajirishayo, isiyoongeza huzuni, wala isiyoongeza dhambi.
Septemba 23
WOKOVU KUTOKA MAVUMBI NA MAKAPI
"Kwa maana, tazama, nitatoa amri, nami nitaipepeta nyumba ya Israeli kati ya mataifa yote, kama vile nafaka ipepetwavyo katika ungo, wala hapana chembe hata moja itakayoanguka chini!" Amosi 9:9
Kazi ya kupepeta bado inaendelea. Kokote twendako, tungali tukipepetwa na kuchekechwa. Katika nchi zote watu wa Mungu wanajaribiwa "kama vile nafaka ipepetwavyo katika ungo." Wakati mwingine ibilisi hushika ungo, na kututupa juu na chini kwa kasi kuu, kwa hamu kubwa ya kutuondoa milele. Kutokuamini si kwepesi kuutia moyo na akili yetu machafuko kwa hofu zake zisizotulia. Ulimwengu hutoa mkono wa hiari katika kazi ile ile, na kututikisa kwenda kuume na kushoto kwa nguvu nyingi. Baya kuliko yote, kanisa, lililo na uasi kwa wingi namna hivi, huja kutia nguvu kali zaidi katika kazi ya kupepeta.
Vema, vema! Na iendelee. Hivyo makapi hutengwa na ngano. Hivyo ngano huokolewa na mavumbi na makapi. Na ni kubwa jinsi gani rehema itujiayo katika andiko, "wala hapana chembe hata moja itakayoanguka chini"! Yote yaliyo mema, ya kweli, ya neema, yatahifadhiwa. Hakuna hata mmoja wa waaminio walio wadogo atakayepotea, wala hakuna mwamini atakayepoteza kitu cho chote kistahilicho kuitwa hasara. Tutalindwa hivyo katika kupepetwa hata kutakuwa faida ya kweli kwetu kwa njia ya Kristo Yesu.
Septemba 24
MTO UTOAO UZIMA
"Tena itakuwa, kila kilicho hai, kiendacho, kila mahali ile mito ifikapo, kitakuwa hai" Ezekieli 47:9
Maji yale yaliyo hai, katika maono ya nabii, yalitiririka kuingia Bahari ya Chumvi, na kuchukua uzima pamoja nayo, hata katika ziwa lile lililotuama. Neema iendako, uzima wa kiroho ndio tokeo la papo hapo na la milele. Neema huenda kwa ukuu kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu, kama vile mto katika mizunguko yake yote ufuatavyo hiari yake mwenyewe; na kokote uendako hausubiri uzima uje kwake, bali huuumba uzima kwa mtiririko wake wenyewe uhuishao. Laiti ungemwagika katika njia zetu, na kufurikisha vitongoji vyetu duni! Laiti sasa ungeingia nyumbani mwangu, na kupanda hata kila chumba kifanywe kuogelea ndani yake! Bwana, maji yaliyo hai na yamtiririkie jamaa yangu na rafiki zangu, wala yasinipite mimi. Nataraji nimekwisha kuyanywa; lakini natamani kuoga ndani yake, naam, kuogelea ndani yake. Ee Mwokozi wangu, nahitaji uzima kwa wingi zaidi. Njoo kwangu, nakuomba, hata kila sehemu ya asili yangu iwe na uchangamfu ulio hai na bidii kubwa. Ee Mungu aliye hai, nakuomba, unijaze uzima wako mwenyewe. Mimi ni kijiti maskini, kikavu; njoo unifanye niishi hivyo hata, kama fimbo ya Haruni, nichipue na kutoa maua na kuzaa matunda kwa utukufu wako. Unihuishe, kwa ajili ya Bwana wangu Yesu. Amina.
Septemba 25
DHABIHU IMEKUBALIWA
"Kama Bwana angependa kutuua, asingelipokea sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya unga mikononi mwetu, wala asingelituonyesha mambo haya yote" Waamuzi 13:23
Hii ni namna ya ahadi ipatikanayo kwa mantiki. Ni hitimisho lililotolewa kwa haki kutokana na mambo yaliyothibitika. Haikuwa yamkini kwamba Bwana alikuwa amewafunulia Manoa na mkewe kwamba mtoto wa kiume angezaliwa kwao, na hata hivyo awe na nia moyoni mwake ya kuwaangamiza. Yule mke alifikiri vema, nasi tutafanya vema tukifuata mwendo wa hoja yake.
Baba ameikubali dhabihu kuu ya Kalvari, naye amejitangaza kuwa amependezwa nayo; awezaje sasa kupendezwa kutuua? Kwa nini badala ikiwa mwenye dhambi hana budi kuangamia bado? Dhabihu ya Yesu iliyokubaliwa huikomesha hofu.
Bwana ametuonyesha kuchaguliwa kwetu, na kufanywa wana kwetu, na muungano wetu na Kristo, na ndoa yetu na yule Mpendwa: awezaje sasa kutuangamiza? Ahadi zimejaa baraka, zilazimuzo tuhifadhiwe hata uzima wa milele. Haiwezekani kwa Bwana kututupa mbali, na hata hivyo aitimize agano lake. Yaliyopita hutuhakikishia, na yajayo hutuhakikishia tena. Hatutakufa, bali tutaishi; kwa maana tumemwona Yesu, na ndani yake tumemwona Baba kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu. Kwa sababu ya kuona huku kuletako uzima ni lazima tuishi milele.
Septemba 26
MIONGONI MWA WALIOKOMBOLEWA
"Tazama, ni watu watakaokaa peke yao, wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa" Hesabu 23:9
Ni nani angetaka kukaa kati ya mataifa, na kuhesabiwa pamoja nao? Naam, hata kanisa lidaialo imani ni la namna hii hata kumfuata Bwana kwa ukamilifu ndani ya mipaka yake ni vigumu sana. Kuna kuchanganyika na kuchanganya namna hii hata mtu mara nyingi hutamani "makao katika jangwa kubwa fulani."
Ni hakika kwamba Bwana angependa watu wake wafuate njia iliyotengwa kuhusu ulimwengu, na kutoka humo waziwazi na dhahiri. Tumetengwa kwa amri ya Mungu, na ununuzi, na wito, na uzoefu wetu wa ndani umetufanya kuwa tofauti sana na watu wa ulimwengu; na kwa hiyo mahali petu si katika Soko lao la Ubatili, wala katika Mji wao wa Uangamivu, bali katika njia nyembamba ambako wasafiri wote wa kweli hawana budi kumfuata Bwana wao.
Hili laweza si kutufanya tu tuyakubali baridi na dhihaka za ulimwengu, bali hata kutufanya tuyakubali kwa furaha kuwa ni sehemu ya fungu letu la agano. Majina yetu hayamo katika kitabu kile kile, sisi si wa mbegu ile ile, hatuelekei mahali pale pale, wala hatumtumaini kiongozi yule yule, kwa hiyo ni vema kwamba sisi si wa hesabu yao. Ila na tuonekane tu katika hesabu ya waliokombolewa, nasi twaridhika kuwa wa peke yetu na wapweke hata mwisho wa jambo.
Septemba 27
NURU YA MUNGU GIZANI
"Maana wewe utaiwasha taa yangu" Zaburi 18:28
Yamkini nafsi yangu yaketi gizani; na ikiwa hili ni la aina ya kiroho, hakuna nguvu ya kibinadamu iwezayo kuniletea nuru. Abarikiwe Mungu! Aweza kulitia nuru giza langu, na mara moja kuiwasha taa yangu. Hata nikiwa nimezungukwa na "giza liwezalo kushikika," lakini yeye aweza kulivunja giza, na mara hiyo kufanya kung'ae pande zote zangu.
Rehema ni hii, ya kwamba akiiwasha taa hakuna awezaye kuizima, wala haitazimika kwa kukosa mafuta, wala haitajiteketeza yenyewe kwa kupita kwa saa. Zile nuru Bwana alizoziwasha hapo mwanzo zingali zikiangaza. Taa za Bwana zaweza kuhitaji kupunguzwa utambi, lakini yeye hazizimishi.
Basi na niimbe, kama ndege mwimbaji usiku, gizani. Kutumaini kutanipa muziki, na tumaini litapanga wimbo. Karibu nitafurahi katika taa iwashwayo na Mungu. Sasa hivi mimi ni mzito na mwenye huzuni. Labda ni hali ya hewa, au udhaifu wa mwili, au mshtuko wa taabu ya ghafula; lakini kizalicho giza kiwe nini, ni Mungu peke yake atakayeleta nuru. Macho yangu yamwelekea yeye peke yake. Karibu nitakuwa na taa za Bwana zikiangaza pande zangu; na, mbele zaidi katika wakati wake mwema, nitakuwa mahali pasipohitaji taa, wala mwanga wa jua. Haleluya!
Septemba 28
KAZI IMEKWISHA; PUMZIKA NDANI YAKE
"Basi, imesalia raha kwa watu wa Mungu" Waebrania 4:9
Mungu ameandaa Sabato, na wengine hawana budi kuingia ndani yake. Wale walioihubiriwa kwanza hawakuingia kwa sababu ya kutokuamini; kwa hiyo, Sabato ile imesalia kwa watu wa Mungu. Daudi aliiimba; lakini ilimpasa kugusa sauti ya huzuni, kwa maana Israeli waliikataa raha ya Mungu. Yoshua hakuweza kuitoa, wala Kanaani haikuitoa: imesalia kwa waaminio.
Njoo, basi, na tujitahidi kuingia katika raha hii. Na tuache taabu ya kuchosha ya dhambi na nafsi. Na tuache matumaini yote, hata katika kazi zile ambazo zaweza kusemwa juu yake, "Ni njema sana." Je, tunazo zo zote namna hiyo? Hata hivyo, na tuache kazi zetu wenyewe, kama Mungu alivyoacha zake. Sasa na tupate faraja katika kazi iliyokwisha ya Bwana wetu Yesu. Kila kitu kimefanywa kabisa: haki haidai zaidi. Amani kuu ni fungu letu katika Kristo Yesu.
Kuhusu mambo ya maongozi, na kazi ya neema katika nafsi, na kazi ya Bwana katika nafsi za wengine, na tuitupe mizigo hii juu ya Bwana, na kupumzika ndani yake. Bwana atupapo nira ya kuchukua, hufanya hivyo ili kwa kuichukua tupate raha. Kwa imani twajitahidi kuingia katika raha ya Mungu, nasi twakataa raha yote iliyomo katika kuridhika nafsi au uvivu. Yesu Mwenyewe ndiye raha kamili nasi tumejazwa hata ukingoni ndani yake.
Septemba 29
KUMTUKUZA KRISTO YESU
"Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasha ninyi habari." Yohana 16:14
Roho Mtakatifu Mwenyewe hawezi kumtukuza Bwana Yesu vema zaidi kuliko kwa kutuonyesha vitu vya Kristo mwenyewe. Yesu ndiye sifa yake mwenyewe iliyo bora. Hakuna kumpamba ila kwa dhahabu yake mwenyewe.
Yule Msaidizi hutuonyesha kile alichokipokea kwa Bwana wetu Yesu. Hatuoni kamwe kitu kwa usahihi hata yeye akifunue. Anayo njia ya kuzifungua akili zetu, na ya kuyafungua Maandiko, na kwa kazi hii ya namna mbili humwonyesha Bwana wetu kwetu. Kuna ustadi mwingi katika kulieleza jambo, na ustadi huo ni wa Roho wa kweli kwa kiwango cha juu kabisa. Hutuonyesha vitu vyenyewe. Hii ni fadhili kubwa, kama wajuavyo wale walioyafurahia maono matakatifu.
Na tuutafute mwangaza wa Roho; si kwa kukidhi udadisi wetu, wala hata kwa kutuletea faraja binafsi, kadiri ya kumtukuza Bwana Yesu. Laiti tungekuwa na mawazo yanayomstahili yeye! Mawazo ya kunyata huvunja heshima ya Bwana wetu wa thamani. Laiti tungekuwa na hisia zilizo dhahiri namna hiyo za nafsi yake, na kazi yake, na utukufu wake, hata tuweze kwa moyo na roho kupaza sauti kwa sifa yake! Palipo na moyo uliotajirishwa na mafundisho ya Roho Mtakatifu patakuwa na Mwokozi aliyetukuzwa kupita maelezo. Njoo, Roho Mtakatifu, nuru ya mbinguni, ukatuonyeshe Yesu Bwana wetu!
Septemba 30
MAHITAJI HUTUFANYA TUPANUE VINYWA
"Fumbua kinywa chako, nami nitakijaza" Zaburi 81:10
Ni kitia-moyo kilichoje cha kusali! Mawazo yetu ya kibinadamu yangetuongoza kuomba vitu vidogo kwa sababu ustahili wetu ni mdogo mno; lakini Bwana angependa tuombe baraka kubwa. Sala yapasa kuwa jambo jepesi kama kufumbua kinywa; yapasa kuwa usemi wa asili, usiolazimishwa. Mtu akiwa na bidii hufumbua kinywa chake sana, na andiko letu latusihi tuwe na juhudi katika maombi yetu.
Lakini pia yamaanisha ya kwamba twaweza kuthubutu mbele za Mungu, na kuomba baraka nyingi na kubwa mikononi mwake. Usome mstari mzima, ukaione hoja: "Mimi ni Yehova, Mungu wako, niliyekupandisha kutoka nchi ya Misri; fumbua kinywa chako sana, nami nitakijaza." Kwa kuwa Bwana ametupa vingi hivyo hutualika tuombe zaidi, naam, kutazamia zaidi.
Tazama jinsi ndege wadogo katika viota vyao waonekanavyo kuwa vinywa vitupu mama ajapo kuwalisha. Na iwe hivyo kwetu. Na tuipokee neema katika kila mlango. Na tuinywe kama sifongo unyonyavyo maji uliyomo. Mungu yu tayari kutujaza kama sisi tu tayari kujazwa. Mahitaji yetu na yatufanye tufumbue vinywa vyetu; udhaifu wetu na utufanye tufumbue vinywa vyetu na kutweta; naam, hofu yetu na itufanye tufumbue vinywa vyetu kwa kilio cha mtoto. Kinywa kilichofumbuliwa kitajazwa na Bwana Mwenyewe. Na iwe hivyo kwetu, Ee Bwana, siku hii.