Njia ya Kuingia Patakatifu pa Patakatifu ·Mwanadamu Ni Nini?

Sura 6 · dakika 10 za kusoma

Mwanadamu Ni Nini?

"Twamwona Yesu,...aliyevikwa taji ya utukufu na heshima." {WAEBRANIA 2:5-9.

KATIKA sehemu ile ya kwanza kuu ya risala hii, tumeona ubora usio na kifani wa Bwana Yesu juu ya malaika, na malaika wakuu, na jeshi lote la mbinguni. Lakini sasa lainuka pingamizi lililotambuliwa kwa uchungu mkubwa na hawa Wakristo Waebrania; nalo, kwa kadiri fulani, latulemea sisi sote; Kwa nini Mwana wa Mungu alifanyika mwanadamu? Huzuni, mateso, na mauti ya Mtu wa Nazareti vipatanaje na utukufu mtukufu wa Mwana wa Mungu, aliye sawa na mwenzi wa Yeye aliye wa Milele?

Maswali haya yanajibiwa katika sehemu iliyobaki ya sura hii, nayo yaweza kukusanywa katika sentensi moja: yeye aliyekuwa juu ya malaika wote alifanyika chini ya malaika kwa kitambo kidogo; ili awainue wanadamu kutoka katika unyonge wao, na kuwaweka katika kiwango chake mwenyewe cha utukufu katika ufalme wa Baba yake wa mbinguni; na ili awe Kuhani Mkuu mwaminifu na mwenye rehema kwa ajili ya wenye huzuni na wanaojaribiwa na wanaokufa. Hili ni tendo linalomstahili Mungu Haya ni maelezo yaliyo zaidi ya kutosha kujibu lile swali la zamani, ambalo kwa ajili yake Anselm alitayarisha jibu la kina kirefu katika kitabu chake, "Cur Deus Homo?"

"Mwanadamu ni kitu gani?" Maneno hayo matatu katika mstari wa 6 ndiyo mahali panapofaa kuanzia hoja hii. Twahitaji siyo tu falsafa ya kweli juu ya Mungu, bali pia falsafa ya kweli juu ya mwanadamu, ili tuwaze sawasawa juu ya Injili. Mwabudu-sanamu humdhania mwanadamu kuwa duni kuliko ndege na wanyama na vitambaavyo, ambavyo hujisujudia mbele yavyo. Mtu wa fikira za maada humhesabu kuwa ni zao la bahati la nguvu za asili zilizomsitawisha; na ambazo mbele yazo yeye yaelekea atatoweka. Sayansi bandia ya nyakati hizi humfanya kuwa wa damu moja na nyani na sokwe-mtu, na kumpa asili moja na wanyama. Tazama ni mifumo mikubwa namna gani ya upotovu iliyositawi kutokana na mawazo yaliyopotoka juu ya asili ya kweli na heshima ya mwanadamu!

Kutoka katika hayo yote twageukia ile fikira tukufu ya heshima ya msingi ya mwanadamu, iliyotolewa katika fungu hili tukufu, ambalo hurekebisha mawazo yetu yaliyopotoka; nalo, hali likitupa maelezo yanayopatana na uzoefu wetu wote na uchunguzi wetu, hutufungulia mandhari za fikira zinazomstahili Mungu.

MWANADAMU KAMA MUNGU ALIVYOMWUMBA. Maelezo yaliyotolewa hapa juu ya asili na heshima ya mwanadamu yametwaliwa kutoka Zaburi 8, ambayo bila shaka ni ukumbusho wa siku zile Daudi alipochunga kondoo za baba yake; hata kama haikutungwa mahali pale pale ambapo miaka ya baadaye makwaya ya mbinguni yaliwatokea ghafula wachungaji waliostaajabu "waliokaa makondeni wakilinda kundi lao usiku."

Igeukie Zaburi hiyo, uone jinsi inavyoelezea vyema hisia zile ambazo lazima zibubujike katika mioyo ya wacha-Mungu kumwelekea Mungu tunapotafakari mbingu za usiku wa manane, kazi ya vidole vyake kama nakshi, na tufe zinazoangazwa na mwezi na nyota, alizoziamuru. Jinsi isivyowezekana kwa wale walioelekea kutafakari kwa uchaji kukutana na umbo lolote kati ya maumbo makuu zaidi ya uzuri wa asili, upana ulioenea sana wa bahari, chore za milima, fahari ibadilikayo ya anga bila kugeuka kutoka kazi ya mikono kumwelekea Fundi mkuu, kwa usemi kama ule wa mshangao ambao kwa huo Zaburi hufunguka na kufungika: " BWANA, Bwana wetu, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!"

Kwa mtazamo wa kwanza, mwanadamu hastahili kabisa kulinganishwa na mandhari zile kubwa na za ajabu zilizofunuliwa kwetu kwa kufichwa kwa jua. Uhai wake si kitu ila ni kama pumzi; kama kivuli kipitacho kasi juu ya ubavu wa mlima; kama kuwako kwa vidukari juu ya jani katika misitu mikubwa ya viumbe. Ni nini kiwezacho kusemwa juu ya tabia yake, iliyotiwa doa la dhambi na kuchafuliwa, ikilinganishwa na vilele ambavyo theluji zake bikira hazijawahi kunajisiwa; na mandhari za misitu, ambazo amani yake haijawahi kutibuliwa; na tufe za fedha, ambazo milio yake ya upatano mkamilifu haijawahi kuvunjwa na ugomvi? Mara nne swali hili laulizwa katika kurasa za Maandiko, "Mwanadamu ni kitu gani hata umkumbuke?" (Zaburi 144:3; Ayubu 7:17, 20; Zaburi 8:4; Waebrania 2:6.)

Lakini ni jambo lisilokanika kwamba Mungu humkumbuka mwanadamu, na kwamba yeye humjilia. "Humkumbuka!" Hakuna dakika katika kuwako kwa Mungu ambayo yeye haukumbuki ulimwengu huu wa wanadamu kama vile mama amkumbukavyo mtoto wake mchanga aliyemwacha kwa dakika katika chumba cha jirani, lakini ambaye kilio chake kidogo au kuugua kwake huikamata upesi. "Mimi ni maskini na mhitaji; lakini Bwana ananifikiria." "Mawazo yako ni ya thamani mno kwangu, Ee Mungu!" "Kumjilia!" Hakuna kitanda kilicho duni hivyo, wala moyo ulio mkaidi hivyo, wala uhai ulio wa upweke hivyo, ila Mungu huujia. Hakuna atakayesoma mistari hii, ambaye njia kuizunguka mlango wa moyo wake haijakanyagwa sana na nyayo za yule ajaye mara nyingi na kusimama na kubisha. Twanena kana kwamba huzuni zetu tu ndizo majilio ya Mungu. Ole wetu, kama ingekuwa hivyo tu! Kila mpwito wa shauku takatifu, kila rehema ya upole, kila kipawa cha Majaliwa, ni jilio la Mungu.

Lakini lazima liwepo sababu fulani kubwa na ya kutosha kwa nini Muumba wa ulimwengu apaswe kuwa na hamu kubwa hivyo juu ya mwanadamu. Ni dhahiri kwamba ukubwa siyo ukuu; mtoto mchanga mdogo ana thamani kuliko mlima mrefu kupita yote; na malkia-mama atakawia katika kile chumba kimoja ambako mtoto wake ni mgonjwa, ijapokuwa aiache sehemu iliyobaki ya milki yake isiyo na mpaka karibu. Itakuwaje kama dunia itakuwa ndiyo kitalu cha ulimwengu! Lakini dokezo la kweli kwa kila kisio lapatikana katika tangazo la Mtunga-Zaburi juu ya kusudi la awali la Mungu katika kumwumba mwanadamu: "Ulimvika taji. ...Ulimfanya awe na mamlaka. . . . Umeweka vitu vyote chini ya miguu yake " (Zaburi 8:5, 6, R.v.). Wala fikira hii tukufu haikutolewa kwanza kwa maono ya kishairi ya Mtunga-Zaburi. Ilikuwa na asili ya awali zaidi. Ni kipande cha ile hati kuu ya wanadamu, ambayo Mungu aliwapa wazazi wetu wa kwanza Paradiso.

Igeukie ile kumbukumbu tukufu ya kale, Mwanzo 1:26-28, ambayo huzipita fikira za sayansi ya kisasa kadiri izipitavyo zile hadithi za uumbaji zinazofanya maandiko ya kipagani yaliyochanganywa nazo kuwa yasiyoaminika. Wepesi wake, utukufu wake, ufaafu wake, hushuhudia kwamba asili yake na mamlaka yake ni ya Kimungu. Tu tayari kukiri kwamba kazi ya Mungu katika uumbaji ilikuwa yenye ulinganifu na utaratibu, na kwamba alilitimiza kusudi lake kwa kufuata mpango unaozidi kujifunua daima. Lakini sayansi haijagundua neno lolote hata sasa la kupinga maneno ya wazi ya Maandiko, kwamba mwanadamu wa kwanza hakuwa duni hata kidogo kuliko sisi katika vipawa vile vya akili na maadili ambavyo ndivyo urithi bora kabisa wa wanadamu.

"Mungu akamwumba mtu kwa mfano wake" (Mwanzo 1:27). -Hapo twapata mfano wa Kimungu. Asili yetu ya akili na maadili imeumbwa kwa mpango ule ule kama wa Mungu: Kimungu kwa kadiri ndogo. Kweli, upendo, na usafi, kama kanuni za hesabu, ni vile vile ndani yetu kama vilivyo ndani yake. Kama isingekuwa hivyo, tusingeweza kumjua wala kumfahamu. Lakini kwa kuwa ndivyo ilivyo, imewezekana kwake kuitwaa asili yetu-tena imewezekana kwamba siku moja tutabadilishwa kuwa mfano mkamilifu wa uzuri wake.

"Na Mungu akasema, Tawaleni" (Mwanzo 1:28). -Hapo wapata ukuu wa kifalme. Mwanadamu alikusudiwa kuwa naibu wa Mungu na mwakilishi wake. Mfalme katika jumba lililojaa kila kitu cha kumpendeza: mtawala na mkuu wa daraja zote za chini za viumbe. Jua limtumikie kama Herkulesi hasa; mwezi uangaze usiku wake, au uongoze maji kuzunguka dunia katika mawimbi, ukisafisha pwani zake; vitu vya asili viwe watumwa na wajumbe wake; maua yanukize njia yake; matunda yapendeze ladha yake; ndege wamwimbie; samaki wamlishe; wanyama wamfanyie kazi na kumbeba. Si mtumwa anayenyenyekea, bali mfalme aliyevikwa taji ya utukufu wa kutawala, na heshima ya ukuu wa ulimwengu wote. Chini kidogo tu kuliko malaika; kwa sababu wao, kama yeye, hawalemewi na nyama na damu. Huyu ndiye mwanadamu kama Mungu alivyomwumba awe.

MWANADAMU KAMA DHAMBI ILIVYOMFANYA. "Bado hatuvioni vitu vyote vikitiishwa chini yake" (Waebrania 2:8, R.v.). Taji yake imevingirishwa mavumbini, heshima yake imekwaruzwa na kutiwa doa. Ukuu wake wapingwa vikali na daraja za chini za viumbe. Kama miti yamlisha, ni baada ya utunzaji wa juhudi, nayo mara nyingi humkatisha tamaa. Kama dunia yampa chakula, ni kwa kuchelewa kuitikia taabu ichoshayo Kama wanyama wamtumikia, ni kwa sababu wamefugwa na kuzoezwa kwa juhudi; hali idadi kubwa hutanga-tanga katika vichaka vya msitu, wakimpinga. Kama akikamata samaki wa bahari, au ndege wa angani, lazima angoje muda mrefu katika maficho ya werevu.

Baadhi ya mabaki ya ule ubwana wa kale bado yaonekana katika hofu ambayo sauti ya mwanadamu na mtazamo wa jicho bado huvitia viumbe vya chini, kama katika maonyesho ya mfugaji-simba au mchezeshaji-nyoka. Lakini kwa sehemu kubwa fujo na uasi vimeuharibu ufalme mzuri wa mwanadamu.

Amedhalilika hivyo, hata amesujudu mbele ya vile vitu alivyopaswa kuviamuru; na ameinamisha umbo lake la kifalme katika mahekalu yaliyowekwa wakfu kwa ndege, na wanyama wenye miguu minne, na vitambaavyo. Ni desturi ya siku hizi kuisifu falsafa ya kipagani; lakini twawezaje kuilinganisha hata kwa dakika moja na dini ya Biblia, wakati piramidi zake zimejaa maiti zilizohifadhiwa za wanyama waliofanywa miungu, na mahekalu yake yamejaa fahali mtakatifu!

Uko wapi ukuu wa mwanadamu? Si katika mshenzi anayejikunyata mbele ya wanyama wa msitu; wala katika mataifa yaliyostaarabika ambayo ni watumwa wa tamaa na ufisadi na ulafi wa kinguruwe; wala katika wale ambao, wakikataa kutambua mamlaka ya Mungu, hushindwa kutumia mamlaka yoyote wao wenyewe. "Dhambi ilitawala," kama Mtume asemavyo kwa kweli kabisa (Warumi 5:21). Na wote wainamishao shingo zao chini ya nira yake ni watumwa na vibarua na raia wanaojikunyata, wakilinganishwa na vile Mungu alivyowaumba na kuwakusudia wawe.

Usiielekeze mikono makundi yale yenye taabu yanayozunguka milango ya nyumba za ulevi katika jiji kuu la watu walio Wakristo kuliko wote ulimwenguni, na kuihesabu hali yao kuwa doa juu ya upendo au uweza wa Mungu. Hii siyo kazi yake. Haya ni mazao ya dhambi. Adui ndiye aliyetenda hivi. Kama ungependa kumwona mwanadamu kama Mungu alivyomkusudia awe, huna budi kurudi Edeni, au kwenda mbele hata Yerusalemu Mpya. Dhambi hunajisi, hushusha, huharibu sura, na huteketeza kila kitu inachokigusa. Nasi twaweza kutetemeka kufikiri kwamba sumu yake yafanya kazi kupitia mwili wetu, tunapogundua matokeo ya uharibifu wake juu ya maelfu wanaotuzunguka.

MWANADAMU KAMA KRISTO AWEZAVYO KUMFANYA. " Twamwona Yesu aliyevikwa taji ya utukufu na heshima" (mst. 9). "Msaada gani huo?" apiga kelele mpingaji; "bila shaka amevikwa taji ya utukufu na heshima, kwa kuwa yeye ni Mwana wa Mungu." Lakini angalia, utukufu na heshima vilivyotajwa hapa ni tofauti kabisa na ule utukufu wa Waebrania 1:3. Ule ulikuwa utukufu usiohamishika wa Uungu wake. Huu ni utukufu uliopatikana wa ubinadamu wake.

Katika Yohana 17 Bwana wetu mwenyewe hutofautisha kati ya hivyo viwili. Katika mstari wa 5, ni utukufu aliokuwa nao pamoja na Baba kama haki yake kabla ya ulimwengu wote. Katika mstari wa 24, ni utukufu aliopewa kama thawabu ya mateso yake, ambao asingeweza kuwa nao asingejitwika mwenyewe umbo la mtumishi, na kufanywa katika mfano wa mwanadamu, akijinyenyekeza mwenyewe, na kuwa mtii hata mauti ya msalaba, "aliyefanywa chini kidogo ya malaika, kwa sababu ya kupatikana na mauti; aliyevikwa taji ya utukufu na heshima: ili yeye, kwa neema ya Mungu, aionje mauti kwa ajili ya kila mtu" (Wafilipi 2:7, 8; Waebrania 2:10).

Hii ndiyo taji ambayo Baba yake alimvika katika siku ya furaha ya moyo wake, alipotoka, akiwa mwanadamu, mshindi kutoka mieleka ile ya mwisho na Mkuu wa jehanamu. Katika maisha yake yote ya duniani aliitimiza ile fikira ya kale ya mwanadamu. Alikuwa mfano wa Mungu; na wale waliomwona walimwona Baba. Alikuwa Mtawala katika amri zake. Pepo na mawimbi yalitii neno lake. Miti ilinyauka alipoigusa. Samaki kwa makundi walitii mapenzi yake. Makundi ya ng'ombe yalikimbia mbele ya mjeledi wake wa kamba ndogo. Magonjwa na mauti na pepo wachafu vilikubali utawala wake. Lakini yote yalitimizwa kwa ukamilifu zaidi alipokuwa karibu kurudi kwa Baba yake, akasema, kwa mlipuko mtukufu wa ukuu aliokuwa akiujua, "Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani."

"Twamwona yeye." Mwone yeye, msomaji Mkristo! Mataji ya milki yako juu ya paji la uso wake. Funguo za mauti na Kuzimu zaning'inia kiunoni mwake. Wale wenye uhai wa fumbo, wawakilishi wa uumbaji uliokombolewa, hushuhudia kwamba yeye anastahili. Vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani, na chini ya dunia, na baharini, humwabudu; kadhalika na makundi ya malaika, ambao chini yao alijishusha kwa kitambo kidogo, kwa ajili yetu.

Na kama alivyo yeye, na sisi pia tutakuwa. Yeye yuko huko kama kielelezo na sampuli na mwakilishi wa watu waliokombolewa. Tumeunganishwa naye katika muungano usiovunjika. Kwa yeye tutairudisha milki yetu iliyopotea. Sisi pia tutavikwa taji ya utukufu na heshima. Siku haiko mbali tutakapoketi kando yake-warithi pamoja naye katika milki yake; wenzake katika utukufu wake, kama tulivyokuwa wenzake katika huzuni zake; chini ya miguu yetu vitu vyote vionekanavyo na visivyoonekana, viti vya enzi na falme na mamlaka; hali juu yetu patakuwa na anga isiyo na mawingu ya upendo wa Baba yetu, milele na milele. Ee, kusudio la furaha ipitayo yote! Ee, shangwe ya mioyo ya watakatifu! Ee, muujiza wa uweza wote wa Kimungu!

Yaliyomo

Njia ya Kuingia Patakatifu pa Patakatifu F. B. Meyer

Ukurasa 1 / 1 · 10 dakika zimebaki katika sura