Sura 21 · dakika 10 za kusoma
Vitu vya Mbinguni Vyenyewe
Kwa maana palifanywa hema."WAEBRANIA 9:2.
JICHO ni jepesi kuliko sikio. Kwa hiyo hakuna lugha yenye kueleza wazi kama lugha ya mifano. Umati utaielewa maana yako vizuri zaidi kwa mfano mmoja unaofaa kuliko kwa maneno elfu. Akili hujiepusha na juhudi ya kifikra ya kukabiliana na asili tete za mambo, nayo hupenda kuipata kweli imefungwa katika umbo linaloweza kupokewa kwa urahisi na jicho, na sikio, na hisia ya kugusa.
Jambo hili laeleza kwa nini kuna mwelekeo mkubwa kiasi kile kwenye ibada za taratibu za nje katika Kanisa la Kirumi na la Kianglikana. Pale ambapo uzima wa kiroho wa mtu una nguvu, haujali umbo la nje; lakini uzima huo ukiwa dhaifu, hujiegemeza kwa unyonge juu ya misaada ya nje. Na ni kwa sababu wana wa Israeli walikuwa katika hali ya kitoto kiasi kile ndipo Mungu akayaweka mawazo yake ya ndani na matakatifu katika maumbo ya nje na vivuli vya kimwili. Watu wasiofundishwa hawana budi kupewa kweli ya kiroho ikielezwa kwa mifano, iliyowavutia hata waliokuwa wazito kabisa wa akili. Kwa hiyo, kwa muda wa miaka elfu na mia tano, ibada ya Kiyahudi ilikusanyika kuizunguka taratibu ya fahari kuliko zote ambazo ulimwengu umepata kuziona
taratibu ambayo Wakristo hawa Waebrania waliikosa kwa masikitiko walipoingia katika kanuni sahili za chumba fulani kisicho na pambo cha juu ghorofani.
Na tuutafakari kwa kitambo mifano ile ya kale.
Chagua eneo la mchanga; chora nafasi ya mstatili yenye urefu wa futi arobaini na tano kwa upana wa futi kumi na tano. Weka kotekote juu ya mistari yako mkanda usiokatika wa vitako vya fedha, vilivyochongwa ili kushika ncha za mbao zinazounda kuta za Hema. Sasa lete mbao zenyewe, boriti za mti wa mshita zenye kimo cha futi kumi na tano, zilizofunikwa kwa dhahabu iliyo bora kuliko zote, na kufungwa pamoja kwa vipingo vitatu virefu vya dhahabu, vinavyopita toka ncha hata ncha. Mlango wa kuingilia lazima uelekee mashariki, ukiwa na nguzo tano za dhahabu, ambazo juu yake huanguka mikunjo ya pazia zito na la thamani. Kisha pima futi thelathini toka hapa, na pazia jingine litenganishe mahali patakatifu na mahali patakatifu pa patakatifu. Sasa lete mapazia zaidi ya kufanya dari, na ya kuning'inia pande zote mbili juu ya boriti za mshita zilizofunikwa dhahabu zinazounda kuta za nje; kwanza, pazia zuri sana lililofumwa kwa rangi zenye kung'aa, na kufunikwa kwa maumbo ya makerubi; kisha, pazia la kitani safi cheupe; tatu, pazia imara la ngozi za kondoo waume, zilizotiwa rangi nyekundu; na, mwisho, ili kulikinga na hali ya hewa, kifuniko cha kawaida na kikakamavu cha ngozi za pomboo. Ua hufanywa kwa mapazia mazito yanayoning'inia pande zote na kuficha mienendo ya makuhani walio ndani.
Na tukitupie jicho kwa kifupi kila kitu tunapopita kwa haraka toka patakatifu pa nje hata pa ndani.
MADHABAHU YA SHABA, pamoja na pembe zake zilizojitokeza, ambazo kwazo wanyama waliochaguliwa kwa dhabihu walifungwa (Zaburi 118:27), au ambazo mkimbizi aliziishika kwa ajili ya usalama na hifadhi (Kutoka 21:14), ilisimama katika ua wa nje. Hapo palitolewa sadaka ya dhambi, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya amani. Ilihesabiwa kuwa takatifu sana (Kutoka 29:37.) Nayo ilistahili kuwa hivyo; kwa maana ilikuwa mfano wa msalaba wa Kalvari, msalaba ule wa ajabu ambapo Yesu alijitoa mwenyewe kuwa dhabihu kwa ajili ya dhambi; yeye mwenyewe akiwa kuhani na mnyama wa dhabihu na madhabahu pia.
Hakuna aliyeweza kuingia mahali patakatifu, ila kwa kupita alama hii takatifu, kama vile tusingaliweza kamwe kuingia katika ushirika na Mungu, kama isingalitendeka kwa ajili yetu pale msalabani ile dhabihu moja itoshayo yote na toleo kwa ajili ya dhambi, litakasalo moyo wetu na dhamiri mbaya. Kadiri tuishivyo muda mrefu zaidi, na kadiri tumjuavyo Mungu zaidi, ndivyo msalaba ule uonekanavyo wa thamani zaidi na usioweza kupitwa: tumaini letu katika huzuni, mwanga wetu gizani, hifadhi yetu katika dhoruba, kimbilio letu katika saa za kutiwa hatiani, mahali petu pa kukutana na Mungu, fahari yetu na furaha yetu.
Ubarikiwe msalaba! ubarikiwe kaburi! au afadhali abarikiwe
Mtu yule aliyeuawa pale kwa ajili yangu."
Na ikiwa madhabahu ya shaba yanena juu ya dhabihu ile moja, mara moja kwa ajili ya wote, ya Kalvari, birika lanena juu ya kuoshwa kwa kila siku kwa madoa ya safari zetu za jangwani, kama Yesu alivyowaosha wanafunzi wake miguu (Yohana 13).
KINARA CHA TAA CHENYE MATAWI SABA, ambacho kutoka humo uliangaza mwanga uliopaangaza mahali patakatifu, ndicho kingaliliteka kwanza jicho la kuhani, ambaye angaliweza kuvuka kizingiti kwa mara ya kwanza. Umbo lake latujulikana kwetu kutokana na nakshi iliyochongwa juu ya Tao la Tito. Jinsi kinenavyo kwa ufasaha juu ya Kristo! Muundo wa dhahabu iliyofuliwa, ambayo kila sehemu yake ilipigwa mapigo ya nyundo, wanena juu ya kuchubuliwa kwake kwa ajili yetu (Kutoka 25:36). Muungano wa taa sita ndogo, na ile moja ndefu ya katikati, waonyesha siri ya muungano ule katika kutoa mwanga uufanyao Kanisa kuwa kimoja na Bwana wake milele katika kuuangaza ulimwengu wenye giza. Mafuta ya dhahabu, yaingiayo taratibu kupitia mirija ya dhahabu iliyohitaji kutunzwa safi na isiyozibwa, yaonyesha kutegemea kwetu juu yake kwa mahitaji ya neema ya kila siku ya Roho Mtakatifu (Zekaria 4:2). Na hata mikasi ya kupunguzia utambi, yote ya dhahabu, iliyotumiwa kwa hekima na kuhani mkuu kusawazisha mwali, yamaanisha njia zile ambazo kwazo Bwana wetu mpendwa mara nyingi hulazimika kukatilia mbali kutokusawazika kwa utambi, na kutusababishia kufifia kwa mwanga kwa kitambo ili baadaye tuwake kwa uangavu na uthabiti zaidi. Uzima wake ndio nuru ya watu. Katika nuru yake twaona nuru. Yeye humwaga nuru juu ya mioyo na nyumba na siri na anga; na baadaye Mwana-Kondoo atakuwa nuru ya mbinguni.
MEZA YA DHAHABU YA MIKATE YA WONYESHO haipasi kupuuzwa, pamoja na mpangilio wake wa mikate kumi na miwili ya unga mwembamba, iliyonyunyiziwa ubani wenye harufu nzuri, na iliyoliwa na makuhani peke yao, ilipobadilishwa siku ya saba kwa ugavi mpya. Hapa tena, kama katika mfano uliopita, kuna mchanganyiko ule wa ajabu wa Kristo na watu wake. Kristo ndiye mkate wa kweli wa uwepo. Yeye ni mkate wa Mungu. Yehova huona katika utii wake na uzima wake na mauti yake utoshelevu mkamilifu; na sisi nasi twamla yeye. Mwili wake ni chakula kweli. Twaula mwili wake na kuishi kwa yeye. Meza ile ilikuwa yaweza kuchukulika, ili ichukuliwe katika safari za watu; nasi hatuwezi kamwe kufanikiwa bila kumchukua yeye pamoja nasi kokote tuendako. Hii ndiyo mana ya mbinguni; mkate wetu wa kila siku; sehemu yetu ya kikuhani. Lakini watu nao waliwakilishwa katika mikate ile kumi na miwili, kama walivyowakilishwa katika vito kumi na viwili vya kifuko cha kifuani. Na bila shaka kuna maana ambayo kwayo waaminio wote bado husimama daima mbele za Mungu katika usafi na utamu wa Kristo; "kwa maana sisi tulio wengi tu mkate mmoja na mwili mmoja, kwa kuwa sisi sote twashiriki mkate ule mmoja." Aa, je, yawezekana mimi kumpa Mungu kitu chochote cha kumridhisha? Kuamini jambo hili bila shaka kungetia maana mpya katika matendo madogo kabisa ya maisha. Lakini yaweza kuwa hivyo.
CHETEZO, AU MADHABAHU YA UVUMBA, chahesabiwa pamoja na mahali patakatifu pa patakatifu; si kwa sababu kilisimama ndani ya pazia, bali kwa sababu kilihusiana kwa ukaribu sana na ibada iliyotolewa humo. Kilikuwa karibu kadiri iwezekanavyo na sanduku (Kutoka 30:6). Chatukumbusha madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya kiti cha enzi (Ufunuo 8:3). Hakuna damu iliyopata kufifisha mng'ao wa dhahabu; majivu yaliyowaka humo yaliletwa kutoka madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa; na juu yake ulinyunyiziwa uvumba, uliokuwa umeandaliwa kwa ustadi wa pekee sana (Kutoka 30:34-38). Uvumba ule wa thamani, ambao kuuiga ilikuwa mauti, wanena juu ya ustahili wake mwingi, ambao kwa uwezo wake maombi yetu na sifa zetu hupata kukubaliwa. Je, hii siyo kazi yake ya daima kwa ajili yetu, akisimama mbinguni kama Kuhani wetu Mkuu? akiishi daima ili kufanya maombezi, akiyapokea maombi yetu maskini, na kuyaleta kwa Baba yake, yakiwa yenye harufu nzuri ya neema yake na uzuri wake na ustahili wake?
PAZIA, lililopitwa mara moja tu kwa mwaka na kuhani mkuu, akiwa amechukua damu, liliwakumbusha waabuduo kwamba njia ya kuingia patakatifu pa patakatifu ilikuwa bado haijakamilika. Kulikuwa na daraja za ushirika na Mungu ambazo taratibu zile hazingeweza kuzitanguliza. "Njia ya kuingia patakatifu pa patakatifu ilikuwa bado haijadhihirishwa." "Pazia, yaani, mwili wake" (Waebrania 10:20). Aa, kitani safi kilichosokotwa, katika usafi wako, hukupata kamwe kuwa safi kama mwili ule uliochukuliwa mimba pasipo dhambi! Aa, kazi bora ya nakshi za ajabu, huwezi kushindana na siri za ajabu zinazokusanyika katika umbo lile la kibinadamu! Lakini, hata Yesu alipokufa, kulikuwa na kizuizi, na pingamizi, na pazia. Lilikuwa limenyunyiziwa damu, lakini lilikuwa pazia bado. Lakini katika saa ile alipoitoa roho yake katika mauti, pazia lilipasuliwa kwa mikono yenye nguvu isiyoonekana toka juu hata chini, likifunua siri zote takatifu zilizo mbele huko machoni pasipozoea pa makuhani wowote ambao wakati ule huenda walikuwa wakifukiza uvumba saa ya kuomba, hali umati wote ukisimama nje (Luka 1:9). Sasa ni pazia lililopasuka, nayo njia ya kuingia patakatifu pa patakatifu iko wazi. Ni njia mpya na iliyo hai na yenye alama ya damu; kwa hiyo twaweza kuikanyaga bila hofu wala kosa, na kuingia kwa ujasiri mtakatifu ili kusimama pale ambapo malaika hufunika nyuso zao kwa mbawa zao katika kuabudu kusikokoma (10:19, 20).
SANDUKU. Kisanduku, chenye umbo la mstatili, chenye urefu wa futi 4 na inchi 6, kwa upana na kimo cha futi 2 na inchi 8; kilichofanywa kwa mti wa mshita, kilichofunikwa kwa dhahabu; kifuniko chake, kibao cha dhahabu, kiitwacho kiti cha rehema, ambacho juu yake maumbo ya makerubi yalisimama au kupiga magoti, macho yao yakikaziwa kile kibao cha dhahabu kilichotiwa madoa ya damu kilichokuwa katikati yao; kwa maana ni juu ya kiti cha rehema ambapo damu ilinyunyiziwa kwa wingi mwaka baada ya mwaka, na hapo nuru ya Shekina iliangaza daima. Katika kutangatanga jangwani sanduku lilikuwa na mbao za mawe, si zilizovunjika bali nzima, na mana, na ile fimbo. Lakini lilipofika mahali pa kupumzika, na miti ile ya kubebea ilipotolewa, mana, chakula cha wasafiri, na ile fimbo, iliyofananisha nguvu ya uzima, vilikuwa vimekwenda zao; sheria peke yake ndiyo iliyobaki.
Sheria haiwezi kamwe kubatilishwa. Ni takatifu, na ya haki, na njema. Hakuna nukta wala herufi moja iwezayo kuipita. Iko katikati ya vitu vyote. Chini ya nyuso zote, chini ya vifuniko vyote, ndani zaidi ya povu na ghasia na mapinduzi ya ulimwengu, hukaa sheria yenye haki isiyoshindika. Sisi sote hatuna budi kunyenyekea mamlaka yake ya kifalme. Hata asiyeamini kuwako kwa Mungu hana budi kuzijenga kuta zake kwa kadiri ya maagizo ya timazi, la sivyo hakika zitabomoka na kuwa magofu.
Lakini sheria iko chini ya upendo. Kiti cha rehema cha dhahabu kilizifunika na kuzificha kabisa mbao zile, kwa kuwa hazikurukaruka tena toka jabali hata jabali, bali zililala kwa utulivu chini yake. Sanduku pasipo kifuniko, ambalo ndani yake mbao za sheria ya mawe zingemtazama mtu, lingekuwa la kutisha kweli. Lakini haipasi kuwe na hofu kwa wale wajuao ya kwamba Mungu atazungumza nao toka juu ya kiti cha rehema kinachokidhi jambo kabisa nacho kimenyunyiziwa damu. Twaambiwa na Mtume, aliyekuwa amesoma vema maana iliyo ndani kabisa ya mifano hii, kwamba "Mungu amekwisha mweka Kristo Yesu awe kiti cha rehema, kwa njia ya imani katika damu yake" (Warumi 3:24, 25). Yesu ameyatimiza matakwa ya sheria kwa uzima wake wa dhahabu na mauti yake ya damu; nasi twaweza kuipata haki ya Mungu ndani yake. Haki yetu wenyewe ingekuwa kifuniko kisichotosha, chembamba mno na kifupi mno; lakini Mbadala wetu ameyatimiza kila takwa liwezekanalo. "Ni nani atakayehukumu? Ni Kristo aliyekufa." Neema hutawala kwa njia ya haki hata uzima wa milele.
Lakini ee, hakuna damu ya mbuzi wala ya ndama iwezayo kunena thamani isiyo na kifani ya damu yake, ambayo kwayo tunao uwezo wa kuingia patakatifu pa patakatifu. Ee, damu ya thamani! inenayo juu ya moyo unaovunjika kwa upendo na huzuni; idhihirishayo uzima uliomwagwa kama maji juu ya nchi katika uchungu uliopita kiasi; ikusanyayo maana yote ya Mambo ya Walawi na dhabihu zake nyingi za wanyama; ahadi ya urafiki ulio mwororo kupita yote, fedha ya ununuzi wa ukombozi wetu, divai ya uzima: uzi wako mwekundu watunena toka madirisha ya wakati uliopita kwa mifano ya furaha na tumaini na amani na upendo usioweza kufa. Damu ya thamani ya Kristo!