Sura 20 · dakika 9 za kusoma
Maagano Mawili
"Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu." WAEBRANIA 8:10.
NENO jipya linaingia katika kitabu hiki cha ajabu, ambalo laweza kuwakwaza baadhi, kwa kuwa lina sauti ya kitheolojia; na hata hivyo lina vilindi vipya vya maana na fungu kwa ajili yetu sote. Ni neno Agano. Sote twaelewa waziwazi kabisa maagano ambayo watu huingia wao kwa wao kuhusu mali, au mambo mengine ya biashara ya kila siku. Mtu mmoja hujitwika kufanya mambo fulani, kwa sharti kwamba mwingine hujifunga kufanya mambo fulani mengine. Maafikiano hayo yanapokwisha kuwekwa, huandikwa juu ya ngozi, hutiwa sahihi, na kutiwa muhuri; na tangu wakati huo kila mmoja hufungwa kwa heshima kutimiza sehemu yake katika shughuli hiyo.
Kwa namna kama hiyo, akijilinganisha na namna zetu za kufikiri na kutenda, Mungu wa milele ameingia agano na roho waaminifu na watiifu. Wala haiwezekani kukadiria kupita kiasi unyenyekevu wake, wala heshima na faida iliyowekwa mkononi mwetu kwa uhusiano wa namna hiyo. Laonekana la ajabu mno lisiweze kuwa kweli; lakini ni lazima liwe kweli, kwa maana isipokuwa kwa msingi wa ukweli wake uliofunuliwa, kamwe lisingaliweza kuwa jambo la kunenwa au kubishaniwa na wanadamu. Agano kati ya mkuu na mwombaji, au kati ya mtu kama William Penn na wenyeji wa asili wa Amerika, hupungua kuwa jambo dogo na duni kabisa likitajwa siku moja pamoja na agano kati ya Mungu na nafsi ya mwanadamu.
Wanatheolojia wameona aina mbalimbali za agano katika mkondo wa historia ya wanadamu, na kama zinavyoonyeshwa katika Biblia. Lakini yatutosha kuyaangalia maagano mawili, la Kale na Jipya, yaliyotajwa katika fungu hili. Na msingi wa hoja yote umo katika Yeremia 31:31-34, ambamo mna tofauti kati ya agano lililofanywa na baba zetu-Mungu alipowatoa katika nchi ya Misri, na lile agano jipya, ambalo katika siku za Yeremia, lilikuwa bado lijalo. Musa alikuwa mpatanishi wa la kwanza, kama Yesu alivyo wa la pili.
AGANO LA MUSA. Lilirudiwarudiwa mara nyingi kwa sauti za neema na za kuchunguza sana. Chukua, kwa mfano, tukio lile lililotokea jeshi kubwa lilipoingia tambarare chini ya kilele cha Sinai, katika mwezi wa tatu wa Kutoka. Hata wakati huo hapakuwa na wingu wala moto juu ya kilele cha Sinai; lakini pendekezo lilitolewa kwa watu na Musa, kwamba wao, kwa upande wao, wakiitii sauti ya Mungu na kulishika neno lake, Mungu, kwa upande wake, angefanya mambo mawili: angewahesabu kuwa hazina yake ya pekee kuliko watu wote; na angewatwaa kuwa ufalme wa makuhani, na taifa takatifu (Kutoka 19:5, 6). Nao watu, wasiohesabu gharama, wala kutambua yote yaliyohusika, wakalia kwa sauti moja, nyepesi, ya pamoja, "Yote aliyoyanena Bwana tutayatenda." Hivyo wakaingia agano.
Muda mfupi baadaye, Amri Kumi zilipokwisha kutolewa, masharti ya agano kwa upande wa Mungu yaliongezwa sana. Kwa kutimizwa, kwa upande wa watu, kwa sharti la kale la utii, Mungu alikwenda mbali zaidi kuliko wakati wowote kabla katika ahadi zake, zilizojumuisha mahitaji ya namna nyingi, na zilizokuwa na sehemu nyingi (Kutoka 23:22-31). Na tena watu wakatoa kelele moja kuu, ya pamoja, ya kukubali (24:3).
Wala haya hayakuwa yote; kwa maana yalipoandikwa, kwa nia ya kuyaweka kumbukumbu maagano haya mazito, katika Kitabu cha Agano, na kusomwa mbele ya watu, katikati ya uthibitisho mzito wa damu iliyonyunyizwa, watu wakasema tena, "Yote aliyoyasema Bwana tutayatenda, nasi tutatii" (24:7). Lakini walijijua kidogo kama nini! Ndani ya juma moja au mawili walikuwa wakicheza kwa fujo kulizunguka ndama wa dhahabu; na ndani ya miezi michache hapakuwa na hata mmoja aliyethubutu kudai kwamba alikuwa amelishika agano kwa kila herufi na nukta. La, kinyume chake: "ambalo agano langu walilivunja, asema Bwana." Ni nini kingine kingeweza kutazamiwa kwao! ijapokuwa Musa aliwaandikia maelezo ya pili na ya kina ya masharti ya agano katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati, pamoja na dai lililorudiwarudiwa, litokealo kama kiitikio, "Mtaangalia kuyatenda."
Kulikuwa na kasoro mbili kubwa katika agano lile la kale, zilizotokana na udhaifu wa asili duni ya mwanadamu; kwanza, halikutoa nguvu, wala uwezo wo wote wa kimaadili, wa kuwawezesha wale walioingia agano kufanya yale waliyoyaahidi; na, pili, halikuweza kuandaa njia ya kuziondoa kabisa dhambi zile zilizotokana na kushindwa kwao kutimiza nadhiri zao za agano (Waebrania 9:9).
Bila shaka wingi wa watu, wakikusudia maisha ya kidini, hupitia jaribio kama hili. Tunapokombolewa kwanza kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kutolewa katika maisha mapya, twaonekana kusimama tena chini ya Mlima Sinai; au, afadhali zaidi, dhamiri yetu huwa Sinai yetu, na kutoka kilele chake cha juu twaonekana kuisikia sauti ya Mungu, akijifunga kuwa Mungu wetu tukikubali katika mambo yote kuitii sauti yake. Na jambo hili mara moja twajifunga kulifanya. Hatuna unafiki, kwa kweli twanuia kulitimiza; twapendezwa na taswira ya maisha iliyowekwa mbele yetu. Si ya kutamanika tu kama sharti la baraka, bali ni ya kuvutia sana na ya kupendeza.
Lakini twakosea kosa kubwa kwa kujifunga wenyewe; kwa maana twajitwika jambo lililo mbali kabisa na uwezo wetu. Kama vile mtu aliyepooza angeweza kujitwika kupanda Mlima Blanc, au mtu aliyefilisika kulipa madeni yake. Karibuni twajifunza kwamba dhambi imeipooza mishipa yetu yote ya kimaadili itendayo kazi. Wema tuutakao, hatuutendi; ubaya tusioutaka, ndio tuutendao. Twaingizwa katika utumwa wa sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyetu, ipiganayo na sheria ya akili zetu. Twatoka nje kujitikisa, kama nyakati nyingine; lakini hatujui ya kuwa wembe umepita juu ya nywele zetu za nguvu, ukituacha bila uwezo na wanyonge.
Yaonekana ni jambo la kusikitisha kwamba kila mmoja ni lazima ajifunze mwenyewe ubatili wa jitihada hizi, badala ya kunufaika kwa jaribio la wengine na kumbukumbu za zamani. Lakini ndivyo ilivyo. Mmoja baada ya mwingine huanza kuchuma haki ya uwepo wa Mungu na tabasamu lake na baraka yake kwa kuwa mwema na mtiifu na mwangalifu katika kutimiza kanuni na taratibu na masharti. Huendelea vizuri kwa muda kidogo, lakini karibuni huvunjika kabisa. Twatatanishwa na kushindwa, kama ndege wa baharini wajigongao juu ya mnara wa taa wakati wa dhoruba, kisha huanguka wamejeruhiwa katika povu la mawimbi chini yake. Sisi ni wazito kujifunza kwamba, kama tunavyopokea kuhesabiwa haki, ndivyo ni lazima tupokee utakaso, kutoka mikononi mwa Mungu kuwa kipawa chake cha bure.
Kama msomaji ye yote wa mistari hii anajaribu kudumisha uhusiano wa kirafiki na Mungu kwa kanuni hii ya kujaribu na kutenda na kushika, kadiri nafsi hiyo itakavyotambua upesi hakika ya kushindwa, si kwa kukosa nia, bali kwa udhaifu wa asili ya kimaadili, na kujisalimisha kwa neema iliyofunuliwa katika agano la pili lililo bora, ndivyo itakavyopata upesi zaidi mahali pa kupumzikia palipo salama na pa furaha, ambapo haitasumbuliwa wala kufukuzwa, milele na milele.
AGANO BORA. Ni bora sana kuliko lile la Musa, kwa namna hii: ijapokuwa lamfunga Mungu kwa ahadi zilizo bora zaidi (mstari 6) kuliko zile za agano la awali, ahadi ambazo kwa kitambo kidogo zadai fikira zetu, hakuna ahadi wala jukumu la namna yo yote litakalodaiwa kutoka kwetu. Hakuna kama; hakuna maagizo ya angalia kutenda; hakuna masharti ya utii ya kutimizwa. Tangu mwanzo hata mwisho lina matakwa ya Aliye Juu. Yahesabu katika orodha hii ya ajabu (mistari 10, 11, 12), kisha uthubutu kudai kwamba kila moja litimizwe katika jaribio lako binafsi; kwa sababu hili ndilo agano ambalo chini yake twaishi, na ambalo kwalo twapata njia ya kumfikia Mungu.
"Nitaziandika sheria zangu katika nia zao." Hilo lahusu kipawa cha akili, kifikirikacho, kikumbukacho, kibishanacho. Litakuwa la thamani isiyokadirika kuwa nazo hapo kwa marejeo ya daima; ili sikuzote zisimame zikiandikwa juu ya miimo na vizingiti vya maisha ya ndani, zikidai heshima, na kulazimisha uangalifu wa kila siku.
"Nitaziandika juu ya mioyo yao." Hapo ndipo makao ya maisha ya hisia na ya mapenzi. Zikiandikwa hapo, ni lazima ziyavute mapenzi yetu. Na kile mtu akipendacho, ni hakika kabisa atakifuata na kukitii. "Chini kidogo," alisema yule askari mkongwe aliyekuwa akifa, walipokuwa wakiipeleleza risasi, iliyokuwa imezama chini sana kifuani mwake, "nanyi mtamkuta Mfalme"; na kwa habari ya Mkristo aliyetwaliwa katika agano na Mungu, sheria imeandikwa juu ya mapenzi ya ndani kabisa ya nafsi yake. Yeye hutii kwa sababu hupenda kutii. Hukaa katika utumishi wa Bwana wake, si kwa sababu ni lazima, bali kwa sababu ameuchagua mwenyewe, akisema, sikio lake linapotobolewa mlangoni, "Nampenda bwana wangu, sitatoka kwenda zangu huru."
"Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu." Kifungu cha mwisho ni bora hata kuliko cha kwanza, kwa sababu chaonyesha nguvu ya Mungu ya kutulinda. Watu wake wateule walimtoka hata akawaita mara moja "Lo-ammi" Si watu wangu (Hosea 1). Lakini kama tutakuwa watu wake milele; watu wa milki yake ya pekee basi jambo hilo laweza kutokea tu kwa kazi ya Roho wake mwenye neema, atulindaye, kama vile jua liwazuiavyo sayari zisikimbie mbali angani na kuwa nyota zitangatangazo.
"Wote watanijua." Ee, furaha kuu kuliko furaha zote! yaweza kuwa? Kumjua Mungu! Kuyajua mambo ya ndani ya Mungu. Kumjua yeye, au kujulikana naye. Kumjua kama Ibrahimu alivyomjua, ambaye alimwambia siri zake; kama Musa alivyomjua, aliyezungumza naye uso kwa uso; au kama Mtume Yohana alivyomjua, alipomwona katika maono ya Ufunuo. Na kwamba haki hii iwe mkononi hata mwa aliye mdogo kuliko wote!
"Nitawarehemu udhalimu wao." Katika agano la kale hapakuwa na nafasi kubwa ya rehema. Lilikuwa jambo la maafikiano ya hiari; kama mmoja wa waliofanya agano akishindwa katika jambo dogo kabisa, hapakuwa na wajibu kwa mwenzake kudumu mwaminifu kwa maafikiano yao. Kushindwa kwa upande mmoja kulilibatilisha agano lote. Lakini hapa hapana ukali wa namna hiyo. Kinyume chake, rehema huingizwa katika uhusiano huo, na hutumia mamlaka yake ya neema.
"Wala sitazikumbuka dhambi zao na maovu yao tena." Kama vile hesabu isahauliwavyo ifutwapo katika kibao, ndivyo itakavyokuwa dhambi, kana kwamba imefutwa katika kumbukumbu ya Mungu. Itasahauliwa, kama deni lililolipwa miaka mingi iliyopita. Itaondolewa akilini kabisa hata itakuwa kana kwamba haikuwako kamwe. Ikitafutwa, haitaonekana. Hati iliyopigiliwa misumari. Jiwe lililotupwa katika vilindi vya bahari. Wingu lililomezwa na joto la kiangazi, kama linavyofifia kutoka mbingu ya buluu iliyokolea. Ndugu zake Yusufu, katika kumkaribia kwao mara ya mwisho Yusufu, baada ya kufa kwa baba yao, walidhihirisha hofu kwamba ijapokuwa chuki yake ilikuwa imefichwa, haikuwa imeachwa kabisa. Lakini hofu zao hazikuwa na msingi wo wote. Waligundua kwamba kosa lile lilikuwa limetoweka kabisa katika wazo la ndugu yao, na Yusufu akalia hapo waliponena naye." Kwa namna kama hii Mungu huacha kuzifikiria dhambi zetu, na huhuzunika tusipoamini ukamilifu wa msamaha wake mwingi.
Je, wafurahia masharti ya agano hili katika jaribio lako la kila siku? Mungu yu tayari kuyatimiza kwa herufi. Mtegemee kufanya kama alivyoahidi. Uhesabu juu ya uaminifu wake. Dai kwamba kila ahadi itatimizwa ndani yako kwa mipaka yote ya utajiri wake, na uhitaji wako. Usijaribu kubuni masharti au maagano asiyoyaweka yeye; bali ukubali kwa furaha hali ya kutofanya lo lote la kuchuma au kushinda, na ya kuyakubali yote atoayo Mungu, pasipo fedha na pasipo thamani.
Je, wauliza jinsi Mungu awezavyo kuliita hili agano, ambamo hamna upande wa pili uliofanya agano? Jibu ni rahisi: Yesu Kristo amesimama badala yetu, na si kwamba amelipatanisha agano hili tu, bali ametimiza kwa jina letu, na kwa niaba yetu, masharti yote yaliyokuwa ya lazima na ya haki. Ameichukua adhabu ya udhaifu na uovu wa mwanadamu. Ameyatimiza madai yote ya utii mkamilifu usiovunjika. Amejifunga kupata, kwa kipawa cha Roho Mtakatifu, utakatifu ndani yetu ambao kamwe usingaliweza kupatikana kwa jitihada zetu wenyewe. Na kwa kuwa amekuwa Mdhamini na Mwenye dhamana yetu, ndivyo Mungu awezavyo kuingia masharti haya ya ukarimu pamoja nasi, bila kusema lo lote juu ya gharama yote kwa Mwanawe, bali akituruhusu kushiriki faida zote; kwa sharti hili tu, kwamba tujitambulishe pamoja naye kwa imani iliyo hai, tukikabidhi shughuli zote za kiroho mikononi mwake, na kukaa katika maamuzi ya mapenzi yake. Hili ndilo agano jipya lililo bora, lililoshika mahali pa lile la kale.