Sura 3 · dakika 1 za kusoma
Jina la Kitabu
“Wimbo ulio bora, ambao ni wa Sulemani.”
Ipasavyo kitabu hiki chaweza kuitwa ule Wimbo Ulio Bora! Hakuna wimbo kama huo. Ukisomwa ipasavyo, huleta moyoni furaha ipitayo mno furaha ya vitu vya dunia, kama vile mbingu zilivyo juu kuliko nchi. Imesemwa vyema kwamba huu ni wimbo ambao neema peke yake yaweza kuufundisha, na uzoefu peke yake waweza kuujifunza. Mwokozi wetu, akinena juu ya muungano wa tawi na mzabibu, aongeza, “Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe” (Yohana 15:11). Na yule mwanafunzi mpendwa, akiandika juu yake yeye ambaye “alikuwapo tangu mwanzo,” ambaye “alikuwa pamoja na Baba, akadhihirishwa kwetu,” ili tupate kushiriki ushirika aliokuwa nao, naye asema pia, “Haya twawaandikia, ili furaha yenu itimizwe.” Muungano na Kristo, na kukaa ndani ya Kristo, je, ni nini wasichokihakikisha? Amani, amani kamili; raha, raha idumuyo; majibu ya maombi yetu yote; ushindi juu ya adui zetu wote; maisha safi, matakatifu; kuzaa matunda kuzidiko siku hata siku. Yote, yote haya ni tunda la furaha la kukaa ndani ya Kristo. Kuuzidisha muungano huu, na kukifanya kukaa huku kudumu zaidi, ndiyo faida ya vitendo ya Kitabu hiki chenye thamani.