Sura 5 · dakika 14 za kusoma
Mei
Mei 1
Wewe ndiwe Mungu wangu; nitakutafuta mapema. Zaburi 63:1.
Katika ulimwengu ambamo mna mengi ya kutibua utulivu wa roho, jinsi ilivyo lazima kuingia katika siri ya hema la Mungu, ambalo peke yake litairudisha katika shwari na amani! Katika ulimwengu ambamo mna mengi ya kuhuzunisha na kukandamiza, jinsi ilivyo baraka kuwa na ushirika naye ambaye ndani yake mna chemchemi ya pekee ya kweli na chanzo cha furaha yote ya kweli na shangwe idumuyo! Katika ulimwengu ambamo mengi yanatafuta daima kuinajisi roho zetu, kuzifanya za kawaida na za kidunia, jinsi kilivyo cheo kikuu cha kuziweka wakfu upya katika maombi kwa utakatifu na kwa Mungu.—Archbishop Trench.
Mei 2
Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Yohana 1:4. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mathayo 5:14.
Katika nuru twaweza kutembea na kutenda kazi. Twatembea katika nuru na kuwa kabisa watoto wa nuru. Twaiacha nuru yetu, nuru ya Mungu, ing’ae, ili watu wapate kuona matendo yetu mema, na kumtukuza Baba yetu aliye mbinguni. Kwa upole, kwa kimya, kwa upendo, bila kukoma, twajitoa kuipitisha nuru na upendo ambao Mungu huutia ndani yetu bila kukoma. Kazi yetu moja ni kungoja, na kupokea, kisha kupitisha nuru ya Mungu iliyo katika Kristo.—Andrew Murray.
Mei 3
Iweni imara, msitikisike, sikuzote mkizidi sana katika kazi ya Bwana. 1 Wakorintho 15:58.
Kutenda mema kwa bidii ni dawa mojawapo ya kuwa Wakristo wenye furaha; ni kama mazoezi kwa mwili, nako huihifadhi nafsi katika afya.—Bishop Ryle.
Mei 4
Akatazama juu mbinguni, akaugua. Marko 7:34.
Mara nyingi mno twaugua na kutazama ndani yetu; Yesu aliugua akatazama nje. Twaugua, na kutazama chini; Yesu aliugua, akatazama juu. Twaugua, na kuitazama nchi; Yesu aliugua, akatazama mbinguni. Twaugua, na kumtazama mwanadamu; Yesu aliugua, akamtazama Mungu.—Stork.
Mei 5
Twajivuna katika dhiki. Warumi 5:3.
Je, umewahi kufikiri kwamba siku moja hutakuwa tena na jambo lolote la kukujaribu wala mtu yeyote wa kukukasirisha?—A. B. Simpson.
Mei 6
Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Wakolosai 3:2.
Yeye ambaye ameyaelekeza mapenzi yake kwa yaliyo juu ni kama mtu ashikiliaye mbinguni; naye, akiwa ameshika hayo kwa uthabiti, angeweza kusema, hata angeuona ulimwengu ukiviringika mbali kutoka chini ya miguu yake, “Moyo wangu u thabiti; moyo wangu u thabiti; Ee Bwana, nitaimba na kutoa sifa!”—Guthrie.
Mei 7
Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni. Luka 24:34. Nao . . . wakalipokea neno lake (Petro) kwa furaha; siku ile ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Matendo 2:41.
Kabla Bwana hajaweza kututumia katika utumishi wake, ni lazima tuwe na mashughuliko ya karibu, ya binafsi, naye mwenyewe. Sikuzote atakuwa na shughuli katika siri na ile nafsi anayokusudia kuitumia kuwabariki wengine.
Je, wataka kunena kwa ajili ya Yesu kwa wale walio karibu nawe? Basi ni lazima uende kwa Yesu mwenyewe kwa ajili ya ujumbe wako. Yale usemayo kwa ajili ya Yesu ni lazima yapatikane kutoka kwa Yesu.
Lo, ni pumzi ngapi zianguka bila nguvu kila upande kwa sababu hazikuvutwa ndani katika patakatifu! Twahitaji shughuli zaidi za siri na Mungu aliye hai. Twakimbia bila kutumwa; twanena kabla Mungu hajanena nasi; si ajabu kwamba mara nyingi twashindwa. Lo, ni maombi ya siri kiasi gani na nidhamu ya kuupekua moyo ambayo moyo wauhitaji kabla Mungu hajauweza kuutumia!—F. Whitfield.
Mei 8
Mwenye haki hula hata nafsi yake ikatosheka. Mithali 13:25.
Kristo ni lazima atosheleze; basi, kama hatujatosheka, ni lazima iwe ni kwa sababu hatujilishi kwake yeye kabisa na yeye peke yake. Kosa haliko katika riziki iliyoandaliwa.—Frances Ridley Havergal.
Mei 9
Maana yeye ambaye Bwana ampenda humrudi. Waebrania 12:6.
Imenenwa vema kwamba “mashaka ya kidunia ni nidhamu ya mbinguni,” lakini ni kitu bora hata kuliko nidhamu; ni magari ya Mungu, yaliyotumwa kuipeleka nafsi mahali pake pa juu pa ushindi. Katika Wimbo Ulio Bora twaambiwa juu ya “gari lililotandikwa kwa upendo.” Hatuwezi sikuzote kuuona utando wa upendo ndani ya gari letu wenyewe—mara nyingi laonekana lisilopendeza kamwe; lakini kila gari lililotumwa na Mungu ni lazima litandikwe kwa upendo, kwa kuwa Mungu ni upendo. Kwa hakika ni upendo wake ndio ulitumaye gari.
Basi yatazame marudi yako, hata yawe machungu kiasi gani kwa sasa, kama magari ya Mungu, yaliyotumwa kuzichukua nafsi zenu hata “mahali pa juu” pa ufanisi wa kiroho na kuinuliwa, nawe utaona ya kwamba, baada ya yote, “yametandikwa kwa upendo.”—Smith.
Mei 10
Damu yake Yesu Kristo, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. 1 Yohana 1:7.
Jifunze somo kutoka kwa jicho la mchimbaji, ambaye mchana kutwa hufanya kazi katikati ya vumbi la makaa lirukalo. Atokapo katika mwanga wa mchana uso wake waweza kuwa mchafu vya kutosha; lakini macho yake ni safi na yenye kung’aa, kwa sababu chemchemi ya machozi katika tezi ya machozi humimina daima mafuriko yake ya upole juu ya jicho, ikisafisha kila chembe ya vumbi mara ikaapo.
Je, huu si muujiza wa kusafisha ambao roho zetu zauhitaji katika ulimwengu kama huu? Na hivi ndivyo Bwana wetu mbarikiwa alivyo tayari kututendea kwa damu yake isafishayo, ikiwa tu tutamwamini.—F. B. Meyer.
Mei 11
Lo lote atakalowaambia, litendeni. Yohana 2:5.
Florence Nightingale alisema: “Kama ningeweza kukupa habari za maisha yangu, ingekuwa ni kuonyesha jinsi mwanamke wa uwezo wa kawaida kabisa alivyoongozwa na Mungu katika njia za ajabu na zisizozoeleka kutenda katika utumishi wake yale aliyoyatenda ndani yake. Na kama ningeweza kukueleza yote, ungeona jinsi Mungu alivyotenda yote, nami sikutenda lolote. Nimefanya kazi kwa bidii, kwa bidii sana, ndiyo yote; wala sijamnyima Mungu kitu chochote.”
Mei 12
Najua kuwa na vingi. Wafilipi 4:12.
Ni jambo la hatari kufanikiwa. Tanuru ya mateso ni jaribu jepesi kwa Mkristo kuliko kalibu ya ufanisi. Yahitaji ustadi upitao wa kibinadamu kukichukua kikombe cha furaha ya kufa kilichojaa pomoni kwa mkono thabiti; lakini Paulo alikuwa amejifunza ustadi huo, kwa maana atangaza, “Katika mambo yote nimefundishwa kushiba na kuona njaa.” Tupatapo mengi ya rehema za maongozi ya Mungu mara nyingi hutokea kwamba twapata kidogo tu cha neema ya Mungu; tukiridhika na nchi, twatosheka kuishi bila mbingu. Uwe na hakika, ni vigumu zaidi kujua jinsi ya kushiba kuliko kujua jinsi ya kuona njaa, ndivyo ulivyo mkubwa mwelekeo wa asili ya kibinadamu wa kiburi na kumsahau Mungu. Jihadhari kwamba uombe katika maombi yako kwamba Mungu akufundishe “jinsi ya kushiba.”—Spurgeon.
Mei 13
Kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. Luka 14:11.
. . . Kama wauliza njia ya kuufikia taji—ni kwa njia ya msalaba; ya kuufikia mlima—ni kwa njia ya bonde; ya kufikia kukwezwa—ni yeye ajidhiliye.—J. H. Evans.
Mei 14
Nami kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili wao nao wapate kuwekwa wakfu katika kweli. Yohana 17:19.
Je, wakumbuka, Yesu alipokuwa ameketi na wanafunzi wake katika karamu ya mwisho, jinsi alivyopaza sauti yake na kuomba, na katikati ya maombi yake yakaja maneno haya ya ajabu: “Nami kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili wao nao wapate kuwekwa wakfu”? Je, kuna jambo lolote katika mafundisho yote ambayo mwanadamu ameyapata kutoka vinywani mwa Mungu lililo tukufu zaidi, lililo na mtazamo mpana zaidi kuliko hilo—kuwa bora wangu si kwa ajili yangu mwenyewe tu, bali kwa ajili ya ulimwengu? Waweza kuwasaidia wanadamu wenzako—ni lazima uwasaidie wanadamu wenzako; lakini njia pekee uwezayo kuwasaidia ni kwa kuwa mtu aliye mtukufu na bora zaidi iwezekanavyo kwako.—Phillips Brooks.
Mei 15
Asiye mwepesi wa hasira ni bora kuliko shujaa, naye autawalaye moyo wake kuliko mtekaji wa mji. Mithali 16:32.
Cha thamani zaidi machoni pa Mungu na malaika zake kuliko ushindi mwingine wowote ni ushindi wa nafsi, ambao kila mtu, kwa msaada wa mbingu, aweza kujipatia mwenyewe.—Dean Stanley.
Mei 16
Kwa ajili ya mtoto huyu naliomba, naye Bwana amenijalia haja yangu niliyomwomba; kwa hiyo nami nimemwazima Bwana; maadamu yu hai amekwisha kuazimwa kwa Bwana. 1 Samweli 1:27, 28.
Mungu wakati mwingine hutoa vipawa ili tu upendo upate kitu cha kukiacha. Vitu avitiavyo mikononi mwetu yamkini vimewekwa hapo ili tupate nafasi ya kuonyesha kilichomo mioyoni mwetu. Lo, laiti kungekuwa ndani yetu bidii ya upendo ambayo ingetuongoza kukichunguza kila kitu kilicho chetu, ili kujua jinsi kingeweza kufanywa njia ya kuonyesha upendo wetu kwa Kristo!—George Bowen.
Mei 17
Utafuteni kwanza ufalme wa Mungu, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Mathayo 6:33.
Twahitaji kuwa na shughuli moja tu, ya kwamba tuweke kitu cha kwanza kwanza—uaminifu kwa Mungu. Ndipo yote mengine tuyahitajiyo kwa ajili ya ulimwengu wote miwili yatapewa. Mungu hatatuangusha kamwe; lakini twasahau, wakati mwingine, katika kufurahi kwetu juu ya uhakika kama huo, kwamba ni lazima tuitimize sehemu yetu kama twataka kudai ahadi ya Mungu.
Haitakuwa rahisi sikuzote. Kesho yaweza kumaanisha kazi isiyopendeza, wajibu usiofurahisha, dhabihu ya gharama kwa ajili ya mtu asiyeonekana kustahili. Maisha yamejaa majaribu makali ya utayari wetu wa kumfuata Mchungaji Mwema. Hatuna haki hata kidogo ya kuudai uhakika huu isipokuwa tumemchukua Kristo kuwa kiongozi wa maisha yetu.—J. R. Miller.
Mei 18
Sifa zake zitakuwa kinywani mwangu daima. Zaburi 34:1.
Sifa zako zisiwe za kupita—wimbo wa kitambo, kisha chombo kikaanikwa ukutani hata siku nyingine ya fahari ya maongozi fulani ya ajabu ikufanye ukishushe. Mungu haji kwa watakatifu wake kama mgeni, bali kukaa nao. Daudi alilichukua hili kuwa kazi ya maisha: “Maadamu ni hai, nitakusifu.”—Gurnall.
Mei 19
Siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa sababu ni mzigo mzito kwangu. Hesabu 11:14.
Ni jambo la lazima sana kwa watumishi wote wa Kristo kukumbuka kwamba kila Bwana amwekapo mtu mahali pa madaraka, atamfanya afae kwa hayo na kumtegemeza katika hayo.
Bila shaka ni jambo tofauti kabisa kama mtu atakimbilia bila kutumwa katika uwanja wowote wa kazi, au cheo chochote cha ugumu au hatari. Katika hali kama hiyo bila shaka twaweza kutazamia kushindwa kabisa, mapema au baadaye. Lakini Mungu amwitapo mtu kwa cheo fulani, atamjalia neema iliyohitajiwa ili akikalie.
Hili ni kweli katika kila hali. Hatuwezi kushindwa kamwe ikiwa tu twang’ang’ania Mungu aliye hai. Hatuwezi kukauka kamwe ikiwa twateka kutoka katika chemchemi. Chemchemi zetu ndogo zitakauka upesi; lakini Bwana wetu Yesu Kristo atangaza, “Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.”—C. H. M.
Mei 20
Ndipo niliposema, Ole wangu! kwa kuwa nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami nakaa kati ya watu wenye midomo michafu; kwa maana macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi. Isaya 6:5.
Si kuuona moyo wetu wenye dhambi ndiko kutunyenyekezacho; ni kumwona Yesu Kristo. Nimepotea kwa sababu macho yangu yamemwona Mfalme.—Andrew A. Bonar.
Mei 21
Nilipokuwa nikitafakari moto uliwaka. Zaburi 39:3.
Ee nafsi yangu, kama ungetafakari zaidi, moto ungewaka zaidi. Kwa nini hujitengi mara nyingi zaidi peke yako? Ungefaa zaidi kwa ulimwengu kama ungekuwa mtu wa kidunia kidogo. Kama ungekuwa na moto zaidi wa mbinguni ungekuwa na nguvu zaidi za kidunia.
Je, hakuna hema la siri uwezalo kuingia na kujiota? Je, hakuna patakatifu pa patakatifu ambapo waweza kupata mwako wa msukumo utakaokufanya uwe na nguvu? Je, haikuandikwa juu ya Mwana wa Adamu kwamba “aliposali sura ya uso wake ilibadilika”? Naam; ni kutoka katika maombi yake ndiko utukufu wake uliobadilika ulikotoka. Ni kutoka katika mwako wa moyo wake ndiko ulikotoka mwako wa uso wake. Ni alipokuwa akitafakari ndipo moto uliposhika.
Ee nafsi yangu, je, ungependa maisha yako yatukuzwe, yapambwe, yabadilishwe machoni pa wanadamu? Panda uende mahali pa siri pa hema la Mungu, ambapo mioto ya upendo inawaka. Maisha yako yatang’aa kwa utukufu kwa wakaao tambarare. Maombi yako yatakuwa yenye nuru; yatauangaza uso wako kama uso wa Musa alipokuwa hajui kwamba unang’aa. Maneno yako yatakuwa yawakayo; yataiwasha mioyo mingi isafiriyo njiani kuelekea Emau. Njia yako itameremeta; ukiisha kusali katika upweke wa Eliya utakuwa na gari la moto la Eliya.—George Matheson.
Mei 22
Ye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa hata kikombe cha maji baridi tu, kwa jina la mwanafunzi, amin nawaambia, hatakosa thawabu yake kamwe. Mathayo 10:42.
Twako hatarini kutafuta mbali mno nafasi za kutenda mema na za kushirikiana. Katika kunyoosha mkono kuyafikia maua makubwa yenye fahari twayakanyaga madaisi madogo.—Selected.
Mei 23
Jificha kando ya kijito. 1 Wafalme 17:3.
Si kando ya mto, bali kando ya kijito. Mto ungekuwa daima na akiba tele, lakini kijito chaweza kukauka wakati wowote.
Je, hili latufundisha nini? Mungu hawaweki watu wake katika wingi hapa. Wingi wa ulimwengu ungeweza kuyavuta mapenzi yao mbali naye. Hawapi mto, bali kijito. Kijito chaweza kuwa kikitiririka leo, kesho chaweza kuwa kimekauka.
Na kwa nini Mungu hutenda hivi? Kutufundisha kwamba hatupaswi kupumzika katika vipawa na baraka zake, bali ndani yake mwenyewe. Hivi ndivyo mioyo yetu ifanyavyo daima—kupumzika katika kipawa, badala ya Mpaji. Kwa hiyo Mungu hawezi kutuamini kando ya mto, kwa maana bila kujua wachukua nafasi yake moyoni. Imenenwa juu ya Israeli kwamba walipokuwa wameshiba walimsahau Mungu.—F. Whitfield.
Mei 24
Ufalme wake unatawala juu ya vyote. Zaburi 103:19.
Ufalme wake unatawala juu ya vyote—kwa hiyo huwezi kupata kitu chochote kisichokuwa sababu ya kusifu, kwa kuwa hakuna kitu kisichokuwa jambo la ruhusa ya Bwana wako yenye neema, au mpango wake, au usimamizi wake. Juu ya vyote—hapana mahali uwezapo kukanyaga nje ya ufalme wake, wala katika jambo lolote kuvuka mbali na uangalizi na utawala wake. Juu ya vyote—kwa hiyo yapokee yote kama yatokayo kwa Mungu; yashike yote kama yatokayo kwa Mungu; na kwa shukrani yako uyarudishe yote kwa Mungu tena, na hivyo kuukamilisha mzunguko, ukimfanya kuwa Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho wa vitu vyote.—Mark Guy Pearse.
Mei 25
Kama tukistahimili, tutamiliki pia pamoja naye. 2 Timotheo 2:12.
Mtoaji wa bei ya juu zaidi kwa taji la utukufu ndiye avaaye kwa unyenyekevu zaidi msalaba wa kujikana nafsi.—A. J. Gordon.
Mei 26
Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo, kwa maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. Mithali 4:23.
Yeye atakaye kuulinda moyo wake safi na mtakatifu, ni lazima aweke mlinzi katika kila njia ambayo kwayo dhambi yaweza kuingia humo, akijilinda dhidi ya zile nyingine kama vile zile dhambi “ndogo,” kama zionekanavyo.
Mtu wa Mungu ana macho yake ya kuyalinda, na hivyo Ayubu alisema, “Nimefanya agano na macho yangu”—ulimi wake, na hapo ndipo lile onyo, “Zuia ulimi wako usinene mabaya, na midomo yako isiseme hila”—masikio yake, na hapo ndipo lile onyo, “Mwanangu, acha kusikiliza mafundisho yakupotoshayo”—miguu yake, na hapo ndipo Daudi asema, “Nimeizuia miguu yangu isiende katika kila njia mbaya, ili nipate kulishika neno lako.” Na kwa kuwa hakuna lango la hisi tano ambalo kwalo adui hawezi kuingia kama gharika, isipokuwa Roho ainue bendera dhidi yake, twahitaji kulinda kila bandari, na kuandika juu ya kila kizingiti, “Hapa hakiingii kitu cha kudhuru wala cha kunajisi.”—Guthrie.
Mei 27
Lo lote mfanyalo, . . . fanyeni yote kwa jina la Bwana Yesu. Wakolosai 3:17.
Fanya mambo madogo kana kwamba ni makubwa, kwa sababu ya utukufu wa Bwana Yesu Kristo, akaaye ndani yako; na fanya mambo makubwa kana kwamba ni madogo na mepesi, kwa sababu ya uweza wake wote.—Pascal.
Mei 28
Wakamlazimisha auchukue msalaba wake. Mathayo 27:32.
Kuna Wakristo wengi ambao hili ni kweli kwao. Wanalazimishwa kuuchukua msalaba, lakini yaje jinsi gani? Yaja kwa kuukimbia. Wanaamua kwamba hawataubeba msalaba wa Kristo; nao waona msalaba ujapo kwamba waja kwa namna ya kutisha zaidi, kwa uzito ukandamizao zaidi kuliko ambavyo ungewahi kuja kama wangeridhika tu kujitiisha chini ya mwongozo wa Mungu; kwa maana ni lazima msalaba uje kwa wote watakaotayarishwa kwa utukufu ujao.—W. Hay Aitken.
Mei 29
Bwana wetu Yesu Kristo . . . alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu wa sasa ulio mbaya. Wagalatia 1:4.
Kushikamana na Kristo ndiyo siri pekee ya kujitenga na ulimwengu.—A. J. Gordon.
Mei 30
Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Mathayo 5:14.
Taa hazisemi, lakini zinang’aa. Mnara wa taa haupigi ngoma, wala hauchezeshi upatu; walakini mbali sana juu ya maji cheche yake ya kirafiki huonwa na baharia. Basi na matendo yako yaing’aze dini yako. Na mahubiri makuu ya maisha yako yaonyeshwe kwa mwenendo wako wote.—Spurgeon.
Mei 31
Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. Yohana 15:5. Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu, Kristo. Wafilipi 4:13.
Mbali naye hatuwezi kufanya lolote. Wakati tunapokaa ndani yake hakuna lisilowezekana. Kwa hiyo kusudi moja la maisha yetu lipasa kuwa kubaki katika muungano ulio hai na wenye nguvu na Kristo, tukijilinda dhidi ya kila kitu kingeuvunja, tukitumia kila njia ya kuuimarisha na kuupanua. Na kwa kadiri tufanyavyo hivyo, tutaona nguvu zake zikitiririka ndani yetu kwa kila dharura iwezekanayo. Yamkini hatutahisi uwepo wake; lakini tutaukuta ukiwapo kila tuanzapo kuutegemea. Hakuna jaribu tusiloweza kulishinda; hakuna dhiki tusiyoweza kuistahimili kwa saburi; hakuna ugumu tusioweza kukabiliana nao; hakuna kazi tusiyoweza kuifanya; hakuna kiri wala ushuhuda tusioweza kuutoa, ikiwa tu nafsi zetu zinaishi katika muungano wenye afya na Yesu Kristo; kwa maana kama siku yetu au saa yetu, ndivyo zitakavyokuwa nguvu zetu.—F. B. Meyer.
Sura ya 5 imekamilika
Mei