Mawazo kwa Saa ya Utulivu
Aprili

Sura 4 · dakika 12 za kusoma

Aprili

Aprili 1

Asubuhi neno la Bwana likanijia. Ezekieli 12:8.

Saa ya utulivu inayotumika peke yako na Mungu mwanzoni mwa siku ndio mwanzo bora kabisa kwa taabu na masumbufu ya shughuli zinazoendelea. Kipindi kifupi cha maombi, tukitazama juu kwa ajili ya hekima na neema na nguvu, na kutafuta kumwagwa kwa Roho Mtakatifu, hutusaidia kuchukua dini yetu katika shughuli za siku. Huleta furaha na amani ndani ya moyo. Na tunapoweka mahangaiko yetu yote katika uangalizi na ulinzi wa Bwana, tukijitahidi kwa uaminifu kufanya mapenzi yake, twapata tumaini la furaha kwamba hata matukio yakionekana kuwa ya giza au ya kukatisha tamaa kadiri gani, mkono wa Baba yetu unaongoza kila kitu, nao utatoa mwelekeo wenye hekima zaidi kwa taabu zetu zote.—Selected.

Aprili 2

Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Mwanzo 2:7.

Basi nafsi yangu hii ni mchanganyiko wa dunia mbili—mavumbi na Uungu! Yaigusa mistari ya mpaka ya dunia mbili. Kwa upande mmoja imeungana na Uungu; kwa upande mwingine, na mnyama wa kondeni. Mwanzo wake ni kutoka chini, lakini kilele chake ni kutoka juu; imeanzishwa kutoka mavumbi ya ardhi, lakini imekamilishwa katika pumzi ya Mungu.

Ee nafsi yangu, je, waishi kulingana na asili yako ya namna mbili? Je, waikumbuka nasaba yako maradufu, na hivyo wajibu wako maradufu? Una wajibu kwa Mungu wako, kwa maana pumzi yake i ndani yako; una wajibu kwa nchi, kwa maana ulitwaliwa kutoka kwayo.—George Matheson.

Aprili 3

Siku zote tukifurahi. 2 Wakorintho 6:10.

Hakuna Mkristo awezaye kujua kamwe maana ya yale maneno mawili madogo, “siku zote tukifurahi,” isipokuwa Mkristo yule auchukuaye msalaba wake na kumfuata Yesu.—W. Hay Aitken.

Aprili 4

Nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe, na uzao wako milele. Mwanzo 13:15.

Ahadi za Mungu sikuzote zapanda ngazi kwenda juu. Moja huongoza kwenye nyingine, iliyojaa zaidi na yenye baraka zaidi kuliko yenyewe. Huko Mesopotamia Mungu alisema, “Nitakuonyesha nchi.” Huko Betheli, “Hii ndiyo nchi.” Hapa, “Nitakupa nchi yote, na watoto wasiohesabika kama chembe za mchanga.” Nasi tutaona hata hizi zikizidiwa.

Ni kwa jinsi hii Mungu hutuvutia kwenye utakatifu. Bila kutoa kitu chochote hata tuwe tumethubutu kutenda—ili apate kutujaribu. Bila kutoa kila kitu mwanzoni—ili asije akatuzidi nguvu. Naye sikuzote hushika mkononi akiba ya baraka isiyo na mwisho. Ee, mabaki ya Mungu ambayo hayajachunguzwa! Ni nani aliyepata kuiona nyota yake ya mwisho?—F. B. Meyer.

Aprili 5

Usiku ule hawakupata kitu. Yohana 21:3.

Mungu aweza kuiacha dunia yenye dhambi ifanikiwe katika mipango yao iliyokatazwa, lakini, jina lake libarikiwe, hawaachi wateule wake wafanikiwe katika njia iwatoayo nje ya mapenzi yake matakatifu! Ana dhoruba ya kumpeleka kila Yona, na wavu mtupu kwa kila Simoni asiyeamini na asiyethabiti.—A. B. Simpson.

Aprili 6

Walinifanya mlinzi wa mashamba ya mizabibu; lakini shamba langu mwenyewe la mizabibu sikulilinda. Wimbo Ulio Bora 1:6.

Fikira zetu hapa zavutwa kwenye hatari ambayo hasa ni ya siku hizi: shughuli nyingi za nyakati zetu zaweza kuongoza kwenye bidii katika utumishi kwa kuupuuza ushirika wa binafsi; lakini kupuuza huku hakutapunguza tu thamani ya utumishi, bali kutaelekea kutufanya tusiweze kwa utumishi ulio bora zaidi.—J. Hudson Taylor.

Aprili 7

Tulifika nchi ile uliyotutuma . . . tukawaona wana wa Anaki huko. Hesabu 13:27, 28.

Ni tukiwa katika njia ya wajibu ndipo tuwaonapo majitu. Ilikuwa Israeli walipokuwa wakienda mbele ndipo majitu yalipotokea. Waliporudi nyuma jangwani hawakuona hata moja.—Selected.

Aprili 8

Kila mmoja alifanana na wana wa mfalme. Waamuzi 8:18.

Frances Ridley Havergal asema: “Kama Mfalme kweli ni jamaa yetu wa karibu, mfano wake wa kifalme utatambulika.”

Aprili 9

Katika malisho ya majani mabichi hunilaza; kando ya maji ya utulivu huniongoza. Zaburi 23:2.

Hili laonyesha pumziko ambalo Mchungaji wetu Mwema hulipeleka kundi lake. Uzima si taabu tupu. Mungu hutupa mahali pengi pa utulivu pa kupumzika katika njia yetu ya usafiri.

Usiku ni mojawapo ya haya, ambapo, baada ya taabu ya siku, mapambano, na uchovu, twaongozwa kando, na mapazia yavutwa ili kuzuia kelele, naye humpa mpendwa wake usingizi, katika usingizi akitoa baraka za ajabu za kufanywa upya. Sabato ni mahali pengine pa utulivu pa kupumzika. Mungu angependa tuache kazi zetu za kidunia, na kuwa na siku ya kuuburudisha mwili na nafsi pia. . . . Miadi ya urafiki pia ni mahali pa utulivu pa kupumzika, ambapo moyo waweza kuchangamana na moyo, ambapo Yesu pia huja, bila kuonekana, naye hutoa baraka yake. Amri zote za ibada ya Kikristo—nyakati za maombi na ibada, saa za ushirika na Mungu—ni mahali pa utulivu pa kupumzika.

Zaidi sana kuliko tuwezavyo kutambua twahitaji nyakati hizi za kimya katika maisha yetu yenye shughuli nyingi, tukizihitaji zaidi kadiri maisha yanavyokuwa na shughuli nyingi.—J. R. Miller.

Aprili 10

Kiasi cha kila siku kwa kila siku. 2 Wafalme 25:30.

Fimbo moja humsaidia msafiri, lakini mzigo wa fimbo ni mzigo mzito.—Spurgeon.

Aprili 11

Chukulianeni mizigo, na hivyo mkaitimize sheria ya Kristo. Wagalatia 6:2.

Hata uwe umefadhaika kadiri gani saa yoyote juu ya swali fulani la kweli, kimbilio moja na msaada sikuzote uko karibu: waweza kumfanyia mtu fulani jambo fulani asiyekuwa wewe mwenyewe. Katika nyakati usizoweza kumwona Mungu, bado wafunguliwa uwezekano huu mtakatifu, wa kumwonyesha Mungu: kwa maana ni upendo na fadhili za mioyo ya wanadamu ndizo ambazo kwazo uhalisi wa kimungu huwafikia wanadamu, wauite jina hilo au wasiuite. Basi wazo hili na likae nawe: zaweza kuwapo nyakati usizoweza kupata msaada, lakini hakuna wakati usioweza kutoa msaada.—George Merriam.

Aprili 12

Utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka: kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. Wafilipi 2:12, 13.

Si shughuli yako wala yangu kutafakari kama je, tutafika mbinguni, wala hata kutafakari kama tutakuwa watu wema; shughuli yetu ni kutafakari jinsi tutakavyoingia katikati ya makusudi ya Mungu na kuwa na pendeleo lisiloelezeka katika miaka hii michache la kufanya jambo fulani la kazi yake.—Phillips Brooks.

Aprili 13

Mungu . . . ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo. 2 Wakorintho 4:6.

Ee Mkristo! usipumzike hata utakapokijua kung’aa kamili, kusikokatika, kwa Mungu moyoni mwako. Kwa kusudi hili, jitolee kwa kila msukumo wake unaokuonyesha uovu fulani usioshindwa na labda usiowezekana kushindwa. Ulete tu nuruni; iache nuru ing’ae juu yake, na kuutoa nje. Umngoje Bwana kuliko wangojeao asubuhi, kwa maana “njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, ikizidi kung’aa hata mchana mkamilifu.” Uwe na hakika kwamba Mungu ataka kukujaza nuru ya utukufu wake: umngoje kuliko wangojeao asubuhi. “Umngoje Bwana, nasema.”—Andrew Murray.

Aprili 14

Ee nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake. Zaburi 62:5.

Je, imepata kukujia akilini kwamba kama husikii jibu la Mungu kwa maombi, yaweza kuwa si kwa sababu yeye ni bubu, bali kwa sababu wewe ni kiziwi; si kwa sababu hana jibu la kutoa, bali kwa sababu hukuwa ukilisikiliza? Twashughulishwa sana na utumishi wetu, na kazi yetu, na wakati mwingine na maombi yetu, hata haitujii akilini kukoma kuzungumza kwetu wenyewe na kusikiliza kama Mungu ana jibu fulani la kutupa kwa “sauti ndogo, ya utulivu”; kuwa watulivu, kuwa kimya, kutofanya kitu, kutosema kitu, kwa maana fulani ya kweli kutowaza kitu; ila tu kuwa tayari kupokea na kuisubiri sauti. “Umngoje Mungu peke yake,” asema mtunga-Zaburi; na tena “Umngoje Bwana.”—Selected.

Aprili 15

Je, hamkuweza kukesha nami saa moja? Mathayo 26:40.

Enyi mnaougua na kudhoofika, na kuomboleza ukosefu wenu wa nguvu,
Sikilizeni mnong’ono huu mpole, “Je, hamkuweza kukesha saa moja?”
Kwa kuzaa matunda na baraka, hakuna “njia ya kifalme”;
Nguvu kwa utumishi mtakatifu ni kuchangamana na Mungu.
—Selected.

Aprili 16

Chakula changu ndicho hiki, niyafanye mapenzi yake aliyenituma. Yohana 4:34.

Tafuta lishe ya maisha yako katika kazi ya maisha yako.—Phillips Brooks.

Aprili 17

Ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. Wafilipi 2:13.

Wokovu kamili ni kutambua kwamba kila kitu tuonacho katika Kristo, Kielelezo chetu, chaweza kuwa chetu, si kwa kuiga, bali kwa kuzalishwa upya.—Selected.

Aprili 18

Tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote. Mathayo 28:20. (R. V., pambizoni.)

“Siku zote”—katika siku za baridi, wakati furaha zimekimbia; katika siku zisizo na jua, wakati mawingu yarudipo tena na tena baada ya mvua; katika siku za ugonjwa na maumivu; katika siku za majaribu na fadhaa, kadiri ile ile kama katika siku ambapo moyo umejaa furaha kama vile misitu wakati wa masika ilivyojaa nyimbo. Siku ile haiji kamwe ambapo Bwana Yesu hayupo kando ya watakatifu wake. Mpenzi na rafiki waweza kusimama mbali, lakini yeye hutembea nao katikati ya moto; huvuka nao mito; husimama nao wanapokabiliana uso kwa uso na simba. Hatuwezi kamwe kuwa peke yetu. Ni lazima sikuzote tuongeze rasilimali zake kwa zetu wenyewe tukiwa tunafanya mahesabu yetu.—F. B. Meyer.

Aprili 19

Tukiwa na . . . ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu . . . na tukaribie wenye moyo wa kweli. Waebrania 10:19, 22.

Ee, utukufu wa ujumbe! Kwa karne kumi na tano Israeli walikuwa na patakatifu penye Patakatifu pa Patakatifu, ambapo, kwa adhabu ya kifo, hakuna aliyeruhusiwa kuingia. Ushuhuda wake mmoja ulikuwa: Mtu hawezi kukaa katika uwepo wa Mungu; hawezi kudumu katika ushirika wake. Na sasa jinsi vyote vilivyobadilika! Kama vile wakati ule onyo lilivyolia: “Hakuna kuingia! usiingie!” ndivyo sasa mwito uendavyo mbele: “Ingia ndani! pazia limeraruliwa; Patakatifu pamefunguliwa; Mungu angoja kukukaribisha kifuani mwake; tangu sasa utaishi pamoja naye.” Huu ndio ujumbe. Ee mwana! Baba yako akutamani uingie, ukae, na usitoke tena milele.—Andrew Murray.

Aprili 20

Usiku huu alisimama karibu nami malaika wa Mungu . . . akisema, Usiogope, Paulo. . . . Mungu amekupa wote wanaosafiri pamoja nawe. Kwa hiyo . . . changamkeni: kwa maana namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vilevile kama nilivyoambiwa. Matendo 27:23, 24, 25.

Imani iliyo hai yaweza kutoa shukrani kwa ahadi, ijapokuwa bado haijatimizwa; ikijua kwamba dhamana za Mungu ni bora kama fedha taslimu.—Matthew Henry.

Aprili 21

Katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Wafilipi 4:6.

Jaribu la kawaida katika kila shida ni kulipangia, kuliondoa njiani wewe mwenyewe; lakini simama ghafula na mipango yako yote, mawazo yako, mahangaiko yako, ukazungumze naye! “Umtwike Bwana mzigo wako, naye atakutegemeza.” Huenda usiweze sikuzote kufanya hivi katika dakika moja au mbili. Basi endelea kuomba hata ujue amekwisha kuupokea, na maombi yakawa sifa. Pumzika, uamini, na ungoje, ukaone jinsi afanyavyo lile ulilotaka kufanya, na uliokuwa na uangalifu mwingi hivyo juu yake. “Simameni imara mkauone wokovu wa Bwana.”—A. E. Funk.

Aprili 22

Wale wamngojao Bwana . . . watapanda juu kwa mbawa kama tai. Isaya 40:31.

Viumbe vyote vyenye mbawa vyaweza kuponyoka kutoka kila mtego uliotegwa kwa ajili yao, ikiwa tu vitaruka juu vya kutosha; na nafsi itumiayo mbawa zake yaweza sikuzote kupata “njia ya kutokea” iliyo hakika kutoka katika yote yawezayo kuidhuru au kuitaabisha.—Smith.

Aprili 23

Upendo ulio kamili huufukuza uoga. 1 Yohana 4:18.

Uoga na upendo huinuka katika upinzani mmoja dhidi ya mwingine kama vichocheo vya maisha, kama vile milima ile miwili ambako kwayo baraka na laana za sheria ya kale zilitangazwa—Mlima wa Laana wote ukiwa ukiwa, wenye mawe, usio na majani mabichi wala maji; Mlima wa Baraka ukiwa mbichi na mng’aavu wenye maua mengi, na uliobarikiwa kwa vijito vingi vitiririkavyo. Uoga ni tasa. Upendo huzaa matunda. Mmoja ni mtumwa, na kazi yake ni ya thamani ndogo. Mwingine ni huru, na matendo yake ni makuu na ya thamani. Kutoka kilele kilichoharibiwa cha mlima uzaao utumwa yaweza kusikika maneno ya sheria; lakini nguvu ya kuzishika sheria hizi zote ni lazima itafutwe juu ya kilima chenye jua ambapo uhuru hukaa katika upendo na kutia nguvu utii. Kwa hiyo, kama ungependa kutumia katika maisha yako mwenyewe nguvu iliyo juu zaidi ambayo Mungu ametupa kwa ukuaji wetu katika neema, chukua hoja zako, si kutoka uoga, bali kutoka upendo.—Alex. McLaren.

Aprili 24

Upendo wa Kristo watubidisha. 2 Wakorintho 5:14.

Upendo wa Kristo ni mkubwa mno kiasi kwamba hakuna moyo uwezao kuutunza. Utafurika ndani ya mioyo ya wengine: utajitoa nje, utajitoa mwenyewe, kwa ajili ya kutajirisha maisha ya wengine. Moyo wa Kristo ni kitu cha gharama kubwa kwa mtu yeyote kuwa nao. Utawaongoza wale walio nao mpaka mahali ulipomwongoza yeye. Kama ulimgharimu yeye msalaba, utawagharimu wao vivyo hivyo.—J. M. Campbell.

Aprili 25

Mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope, mimi nitakusaidia. Isaya 41:13.

Usijaribu kuushika mkono wa Mungu; mwache yeye aushike wako. Mwache yeye afanye kushika, nawe ufanye kuamini.—H. W. Webb Peploe.

Aprili 26

Fikirini mambo makuu aliyowatendea. 1 Samweli 12:24.

Tazama nyuma katika njia yote ambayo Bwana Mungu wako amekuongoza. Je, huioni ikiwa imenakshiwa kwa baraka elfu kumi zilizojificha? Kumbuka msaada uliohitajiwa uliotumwa wakati wa hatari; njia sahihi iliyochaguliwa kwa ajili yako, badala ya njia isiyo sahihi uliyokuwa umejichagulia mwenyewe; kile kitu chenye kudhuru ambacho moyo wako ulishikamana nacho kwa upendo mwingi, kilichoondolewa njiani mwako; nafasi ya kupumua uliyopewa, ambayo roho yako iliyojaribiwa na kutaabika ilihitaji wakati ule ule. Ee, je, Yesu hakusimama kando yako ulipokuwa hujui? Je, Upendo Usio na Mwisho haukuzunguka kila tukio kwa mikono yake ya milele, na kupamba kila wingu kwa utando wake wa rehema? Ee, fuatilia hatua zako, ukaione alama ya nyayo yake katika kila moja! Mshukuru kwa ajili ya hizo zote, na ujifunze somo lililohitajiwa la kumtegemea Yesu kwa unyofu zaidi.—F. Whitfield.

Aprili 27

Yeye . . . akasema . . . mimi . . . nikaificha talanta yako katika ardhi. . . . Bwana wake akajibu, akamwambia, Ewe mtumwa mbaya na mvivu. Mathayo 25:24-26.

Kati ya mambo makuu tusiyoweza kuyafanya na mambo madogo tusiyotaka kuyafanya, hatari ni kwamba hatutafanya kitu chochote.—Monod.

Aprili 28

Utukufu una yeye sasa na hata milele. 2 Petro 3:18.

Ee mwamini, wautazamia wakati ambapo utaungana na watakatifu walio juu katika kumhusisha Yesu utukufu wote; lakini je, wamtukuza sasa? Maneno ya mtume ni, “Utukufu una yeye sasa na hata milele.”—C. H. Spurgeon.

Aprili 29

Nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; kwa maana hawataaibika wanaoningoja. Isaya 49:23.

J. Hudson Taylor asema: “Kungoja kwa utulivu mbele za Mungu kwaweza kuokoa kutokana na makosa mengi na kutokana na huzuni nyingi.”

Aprili 30

Na iwe kwako kama utakavyo. Mathayo 15:28.

Ee, ushindi wa maombi! Ndivyo vilele vya milima vya Biblia. Vyatuchukua kurudi kwenye tambarare za Mamre, kwenye vivuko vya Penieli, kwenye gereza la Yusufu, kwenye ushindi wa Musa, kwenye ushindi mkuu wa Yoshua, kwenye wokovu wa Daudi, kwenye miujiza ya Eliya na Elisha, kwenye hadithi yote ya maisha ya Bwana, kwenye siri ya Pentekoste, kwenye kiini cha huduma ya Paulo isiyo na kifani, kwenye maisha ya watakatifu na vifo vya mashahidi, kwenye yote yaliyo matakatifu na matamu zaidi katika historia ya Kanisa na uzoefu wa watoto wa Mungu. Na wakati, kwa ajili yetu, pambano la mwisho litakapokuwa limepita, na kiti cha miguu cha maombi kitakapokuwa kimetoa nafasi kwa kinubi cha sifa, mahali pale pa wakati patakapopambwa kwa mng’ao wa kimbingu na wa milele zaidi, patakuwa pale, ambapo mara nyingi pameunganishwa na huzuni iliyo kuu zaidi na usiku ulio giza zaidi, ambapo juu yake tuna maandishi, “Yehova-Shama: Bwana alikuwa hapo!”—A. B. Simpson.

Ukurasa 1 / 1 · 12 dakika zimebaki katika sura