Mawazo kwa Saa ya Utulivu
Juni

Sura 6 · dakika 14 za kusoma

Juni

Juni 1

Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawapeleka ninyi. Yohana 20:21.

Kamwe tusiondoke chumbani mwetu hata tuwe tumeuona uso wa Bwana wetu mpenzi, Kristo, na kutambua ya kuwa tunatumwa naye kufanya mapenzi yake, na kuikamilisha kazi aliyotupa tuifanye. Yeye aliyewaambia wafuasi wake wa karibu, “Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawapeleka ninyi,” anatuambia vivyo hivyo kila mmoja wetu, mapambazuko yanapotuita tuishi siku nyingine. Yatupasa kutambua ya kuwa tunatumwa naye kama vile malaika ambao “hufanya maagizo yake, wakiisikiliza sauti ya neno lake.” Kuna mpango fulani kwa kazi ya kila siku, ambao atatufunulia, tukimtazamia tu afanye hivyo; utume fulani wa kutimiza; huduma fulani ya kufanya; somo fulani la kujifunza kwa saburi, ili tupate kuwa na uwezo wa “kuwafikia wengine pia.” Kuhusu mipango yetu hatuna haja ya kufadhaika; kwa sababu yeye anayetutuma ana wajibu wa kuutunga mpango, kwa kadiri ya hekima yake isiyo na mwisho; na kutufunulia, hata kama akili zetu ni butu na dhaifu kiasi gani. Na kuhusu utoshelevu wetu, tuna hakika ya kupata neema yote itupasayo; kwa sababu kamwe hatutumwi ila kwanza atupulizie na kusema, “Pokeeni Roho Mtakatifu.” Sikuzote kuna kipawa maalumu kwa nguvu maalumu.—F. B. Meyer.

Juni 2

Chemchemi . . . kwa ajili ya dhambi na kwa ajili ya uchafu. Zekaria 13:1.

Wewe uliye na imani katika hiyo Chemchemi, ifikie mara kwa mara. Jihadhari na makosa mawili yaliyo ya kawaida sana na ya hatari sana. Jihadhari na kudhani dhambi yoyote kuwa kubwa mno kwa ajili yake; jihadhari na kudhani dhambi yoyote kuwa ndogo mno. Hakuna dhambi ndogo kiasi, ambayo isiweze kuwa chembe ya upotevu wa milele; hakuna dhambi kubwa kiasi, ambayo tone la damu ya upatanisho lisiweze kuiosha kabisa kana kwamba imezama vilindini vya bahari.—James Hamilton.

Juni 3

Mimi ni mweusi . . . kama hema za Kedari. Wimbo Ulio Bora 1:5. Mimi ni wa mpenzi wangu, na shauku yake ni juu yangu. Wimbo Ulio Bora 7:10.

Hakuna kitu kinachoinyenyekeza nafsi kama ushirika mtakatifu na wa ndani pamoja na Bwana; walakini kuna furaha tamu katika kuhisi kwamba Yeye anajua yote, na, pamoja na hayo, angali anatupenda.—J. Hudson Taylor.

Juni 4

Daudi akamwuliza Bwana. 2 Samweli 5:19.

Mkristo, kama ukitaka kuijua njia ya wajibu, mfanye Mungu dira yako; kama ukitaka kuiongoza merikebu yako katikati ya mawimbi ya giza, itie usukani mkononi mwa Mwenyezi. Mwamba mwingi ungeepukwa kama tungemwacha Baba yetu ashike usukani; fungu jingi la mchanga au tope tungeliweza kuliepuka kama tungeliacha mapenzi yake makuu yachague na kuamuru. Mpuritani mmoja alisema, “Ni hakika kama vile Mkristo ajikatiavyo mwenyewe, ndivyo atakavyojikata vidole vyake mwenyewe.” “Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea,” ndiyo ahadi ya Mungu kwa watu wake. Basi, na tuchukue mashaka yetu yote kwake na kusema, “Bwana, wataka nifanye nini?” Usiondoke chumbani mwako asubuhi hii bila kumwuliza Bwana.—Spurgeon.

Juni 5

Mtu mmoja . . . ambaye hakuwa ametembea kamwe . . . akamsikia Paulo akinena: ambaye . . . alipoona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema . . . Simama wima kwa miguu yako. Naye akaruka na kutembea. Matendo 14:8, 9, 10.

Palipo na imani ya kweli, italeta utii; na paitokeapo utii, sikuzote, kwa namna moja au nyingine, italeta baraka.—W. Hay Aitken.

Juni 6

Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana . . . Najua ya kuwa . . . lo lote utakalomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Martha akamwambia, Nami [58] najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yohana 11:21, 22, 23, 24.

Jihadhari, katika maombi yako, zaidi ya yote, usimwekee Mungu mipaka, si kwa kutokuamini tu, bali kwa kudhani ya kuwa unajua awezayo kufanya. Tarajia mambo yasiyotarajiwa, zaidi ya yote tuyaombayo au tuyawazayo. Kila uombeapo kwa ajili ya wengine, kwanza tulia kisha umwabudu Mungu katika utukufu wake. Fikiri juu ya awezayo kufanya, jinsi apendezwavyo kumsikia Kristo, na juu ya nafasi yako ndani ya Kristo; kisha tarajia mambo makuu.—Andrew Murray.

Juni 7

Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Wagalatia 3:27.

Si haki ya Mwokozi wetu tu, wala si uzuri wa utakatifu wake au neema za tabia yake, tunazopaswa kuvaa kama vazi. Bwana mwenyewe ndiye vazi letu. Kila Mkristo si mchukua-Kristo tu bali pia ni mvaa-Kristo. Yatupasa kuingia ndani yake kwa ushirika, kujazwa uwepo wake, na kutiwa Roho yake kiasi kwamba watu wamwone yeye watutazamapo, kama waonavyo mavazi yetu waitazamapo miili yetu.—A. J. Gordon.

Juni 8

Wewe hutaniosha miguu kamwe. Yohana 13:8.

Cho chote kinachotuzuia tusipokee baraka ambayo Mungu yu tayari kutupa si unyenyekevu, bali ni dhihaka yake. Unyenyekevu wa kweli sikuzote utahisi uhitaji wa vipimo vikubwa vya neema, nao utakamilishwa kwa kadiri ile ile ambayo kwayo neema hiyo hutolewa. Mtu mnyenyekevu kweli atatafuta kujazwa utimilifu wote wa Mungu, akijua ya kuwa ajazwapo hivyo hakuna nafasi hata kidogo ya kiburi wala ya nafsi.—George Bowen.

Juni 9

Umtwike Bwana mzigo wako, naye atakutegemeza. Zaburi 55:22.

Yeye ajitwikaye mahangaiko yake mwenyewe hujilemea mzigo mzito. Hofu ya yale yawezayo kuja, tarajio la yale yatakayokuja, tamaa ya yale yasiyokuja, na kutoweza kuyarekebisha haya yote, hayana budi kumletea mateso ya daima. Mimi nitayatwika mahangaiko yangu juu ya Mungu: Yeye ameniamuru hivyo. Hayawezi kumdhuru: Yeye aweza kuyarekebisha.—Hall.

Juni 10

Vema, mtumwa mwema na mwaminifu. . . . Wewe mtumwa mbaya na mvivu. Mathayo 25:21, 26.

Mungu hutufanya kuwajibika si kwa yale tulivyo navyo, bali kwa yale tungeweza kuwa navyo; si kwa yale tulivyo, bali kwa yale tuwezavyo kuwa.—Mark Guy Pearse.

Juni 11

Yesu akawashurutisha wanafunzi wake wapande merikebuni. Mathayo 14:22.

Yesu aliwashurutisha waende! Mtu angedhani ya kwamba kama pana wakati wowote wenye ahadi ya hakika ya kufanikiwa katika utume, ni hapa. Bila shaka, hapa, kama mahali popote, mwisho wa ushindi ungeweza kutabiriwa kwa uhakika; walakini hapa, kuliko mahali pengine popote, palikuwa na kilichoonekana kuwa kushindwa. Aliwatuma katika safari ya baharini, nao wakakutana na dhoruba kama ambayo hawakuwa wamepata kuiona.

Na niyatafakari haya, kwa maana yamekuwa hivyo kwangu, nami pia. Mara nyingine nimejihisi nikisukumwa kutenda kwa uvutano ulioonekana kuwa juu yangu—nikishurutishwa kupeleka merikebu baharini. Imani ya kwamba nilishurutishwa iliniongezea ujasiri, nami nilikuwa na hakika ya safari ya utulivu. Lakini matokeo yalikuwa kushindwa kwa nje. Utulivu ukawa dhoruba; bahari ikachafuka, pepo zikavuma, merikebu ikatupwa-tupwa katikati ya mawimbi, na shughuli yangu ikavunjika kabla haijaweza kuifikia nchi kavu.

Je, basi, ile amri yangu ya kimungu ilikuwa udanganyifu?

La; wala utume wangu haukuwa kushindwa. Yeye alinituma katika safari ile, lakini hakunituma kwa kusudi langu. Yeye alikuwa na lengo moja nami nilikuwa na lengo lingine. Lengo langu lilikuwa utulivu wa nje; lengo lake lilikuwa kukutana kwangu na dhoruba. Lengo langu lilikuwa kufikia bandari ya raha ya kimwili; lengo lake lilikuwa kunifundisha ya kuwa kuna raha hata katika bahari iliyo wazi.—George Matheson.

Juni 12

Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli. 2 Timotheo 2:15.

Kuwa na vifaa vyako tayari; Mungu atakupatia kazi.—Charles Kingsley.

Juni 13

Tokeni kati yao, mkatengwe. 2 Wakorintho 6:17.

Ijapokuwa ulimwengu wote ulikuwa mkononi mwake achague, Mungu aliwaweka watu wake wa kale mahali pa ajabu sana. Upande wa kaskazini walizingirwa na safu za milima ya theluji ya Lebanoni; jangwa tasa lilikuwa mpaka wao wa mashariki; mbali upande wa kusini palienea eneo lisilo na rutuba, lililoitwa jangwa la ukiwa lenye mngurumo; na hali bahari—ambayo wakati ule, si kama ilivyo sasa, njia kuu ya mataifa, iwezeshayo badala ya kuzuia mawasiliano—ilikuwa upande wao wa magharibi, ikivunjika kwenye ufuo uliokuwa na bandari chache na usio na mito ipitikayo na merikebu ili kuvutia hatua za biashara.

Je, hatuwezi kuona kweli kuu katika mahali penyewe ambapo Mungu aliwaweka watu wake wateule? Bila shaka yatufundisha ya kuwa ili kuwa watakatifu, au waliotakaswa, hatuna budi kuwa watu waliotengwa—tukiishi ulimwenguni, lakini si wa ulimwengu—kama mafuta, ambayo yaweza kuchanganywa, lakini hayawezi kuungana na maji.—Guthrie.

Juni 14

Mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila utakakokwenda, nami nitakurudisha tena katika nchi hii. Mwanzo 28:15.

“Pamoja nawe,” ushirika; “Nitakulinda,” ulinzi; “Nitakurudisha,” uwongozi.

Juni 15

Nimekuweka . . . uwe wokovu hata miisho ya dunia. Matendo 13:47. Nanyi mtakuwa mashahidi wangu . . . hata miisho ya dunia. Matendo 1:8.

Watu wanahoji sasa, kama ambavyo hawajapata kuhoji kamwe, kwamba je, Ukristo ndiyo kweli dini ya kweli itakayokuwa wokovu wa ulimwengu. Enyi watu wa Kikristo, ni juu yetu kutoa sehemu yetu ya jibu kwa swali hilo. Ni juu yetu, ambao ndani yetu kanisa la Kikristo kwa sasa limejionyesha kwa sehemu, kutangaza ya kuwa Ukristo, ya kwamba imani ya Kikristo, uume wa Kikristo waweza kuufanyia ulimwengu lile ambalo ulimwengu unalihitaji.

Wewe wauliza, “Mimi naweza kufanya nini?”

Waweza kutoa uzima mmoja wa Kikristo. Waweza kutoa uzima ulio mwaminifu kwa kila wajibu, ulio tayari kwa kila huduma, uliokusudia kutotenda kila dhambi, kiasi kwamba kanisa kuu la Kikristo litakuwa imara zaidi kwa sababu ya kuishi kwako ndani yake, na tatizo la ulimwengu lipate jibu, na amani fulani kuu iingie katika hali hii maskini na yenye mashaka ya ubinadamu wetu, ionapo ufunuo huo mpya wa Ukristo ulivyo.—Phillips Brooks.

Juni 16

Namjua yeye niliyemwamini. 2 Timotheo 1:12.

Kumjua Kristo binafsi ni jambo lililo hai. Kama mti utumiao kila saa kwa kukua, hustawi katika jua, huburudishwa na mvua—hata dhoruba humsukuma kushikilia zaidi mizizi yake ardhini kwa tegemeo lake. Basi, ewe moyo uliyetaabika, katika kila jaribu, sema, “Haya yaja ili nipate kumjua Bwana wangu zaidi.”—Selected.

Juni 17

Ingojeni ahadi ya Baba. Matendo 1:4. Hata ilipotimia siku ya Pentekoste, walikuwako wote mahali pamoja kwa nia moja . . . wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Matendo 2:1, 4.

Utii kwa msukumo wa kimungu huugeuza kuwa mali ya kudumu.—F. B. Meyer.

Juni 18

Nasi tumelijua tena tumeliamini pendo alilo nalo Mungu kwetu. 1 Yohana 4:16.

Siri ya kuenenda kwa ukaribu na Kristo, na kumtumikia kwa mafanikio, ni kutambua kwa ukamilifu ya kuwa sisi ni wapenzi wake. Na tuhisi tu kwamba ameuelekeza moyo wake juu yetu, kwamba anatutazama toka mbinguni kwa upendo mwororo, kwamba anaishughulikia siri ya maisha yetu kwa uangalifu na wororo, kwamba anatufuata siku baada ya siku kama mama amfuatavyo mtoto wake katika jaribio lake la kwanza la kutembea peke yake, kwamba ameuweka upendo wake juu yetu, na, hata tusipotaka, anatutimizia mapenzi yake yaliyo makuu na baraka, kwa kadiri tumruhusuvyo, ndipo hakuna kitu kiwezacho kutuvunja moyo. Mioyo yetu itawaka kwa upendo wa kuitikia. Imani yetu itaruka kuzikuta ahadi zake zenye nguvu, na dhabihu zetu zitakuwa anasa hasa za upendo kwa ajili ya yeye aliye mpenzi hivyo. Hii ndiyo iliyokuwa siri ya roho ya Yohana. “Nasi tumelijua tena tumeliamini pendo alilo nalo Mungu kwetu.” Na moyo uliojifunza haya kwa ukamilifu umeipata siri ya imani isiyo na mipaka na utumishi wenye bidii.—A. B. Simpson.

Juni 19

Ustahimili . . . kama askari mwema wa Yesu Kristo. 2 Timotheo 2:3.

Uzima si ushindi, bali ni vita. Ustahimili kitambo kidogo zaidi. Baada ya muda, kila mmoja kwa zamu yake, tutasikia mzinga wa machweo.—Selected.

Juni 20

Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Luka 14:27.

Sikuzote kuna kivuli cha msalaba kikikaa juu ya njia ya Mkristo. Je, hiyo ni sababu ya wewe kuikwepa au kutouchukua wajibu? Je, umekusudia moyoni mwako kuwa utamfuata Bwana wako kila mahali penginepo, isipokuwa apandapo njia iongozayo msalabani? Je, hiyo ndiyo dini yako? Kadiri uibadilishavyo mapema, ndivyo ilivyo bora zaidi. Dini ya Bwana Yesu Kristo ni dini ya msalaba, na tusipouchukua msalaba wetu, kamwe hatuwezi kumfuata.—W. Hay Aitken.

Juni 21

Watu hawa . . . wameupindua ulimwengu. Matendo 17:6.

Uzuri wa utulivu wa maisha matakatifu ndio uvutano wenye nguvu zaidi ulimwenguni, ukifuatiwa na uweza wa Mungu.—Pascal.

Juni 22

Ninalofanya wewe hulijui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Yohana 13:7.

Mungu ana shule kwa ajili ya watoto wake hapa duniani na mmoja wa waalimu wake walio bora ni Kukatishwa Tamaa. Rafiki yangu, wewe nami tutakapoifikia nyumba ya Baba yetu, tutatazama nyuma na kuona ya kuwa yule mwalimu mwenye sauti kali na uso mkavu, Kukatishwa Tamaa, alikuwa mmoja wa waongozaji walio bora kutuandaa kwa ajili yake. Alitupa masomo magumu; mara nyingi alitumia fimbo; mara nyingi alituongoza katika njia zenye miiba; nyakati nyingine alitutua mzigo wa anasa; lakini hilo lilitufanya tu kusafiri kwa uhuru zaidi na kwa haraka zaidi katika njia yetu ya kuelekea mbinguni. Nyakati nyingine alituongoza chini hata bondeni la uvuli wa mauti; lakini kamwe ahadi hazikusomeka kwa utamu kama zilipofumbuliwa kwa jicho la imani katika bonde lile lile. Hakuna mahali alipotuongoza mara nyingi hivyo, wala kutufundisha masomo matakatifu hivyo, kama pale msalabani pa Kristo. Ewe mwalimu mpenzi, wa zamani, mwenye mikono mikakamavu! Tutakujengea mnara bado, na kuutia taji la mashada, na kuuandika: Ibarikiwe kumbukumbu ya Kukatishwa Tamaa!—Theodore Cuyler.

Juni 23

Kama zilivyo siku zako, ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako. Kumbukumbu la Torati 33:25. Naweza kuyafanya mambo yote katika yeye anitiaye nguvu, Kristo. Wafilipi 4:13.

Hatakutwika hata mzigo mmoja usio wa lazima. Hatakudai zaidi ya ajuavyo nguvu zako ziwezavyo kubeba. Hatamwomba Petro yeyote aje kwake juu ya maji, isipokuwa atoe wakati uo huo nguvu na tegemeo juu ya mawimbi yasiyo imara. Hatakuomba uteke maji kama kisima ni kirefu mno, wala kuondoa jiwe kama ni zito mno. Lakini wala wakati uo huo hatakubali kuwa haliwezekani lile ambalo, ukiwa wakala huru na mwenye kuwajibika, liko katika uwezo wako kuliepusha. Hatalihesabu kuwa msiba wako lile lililo kosa lako.—Macduff.

Juni 24

Moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. Matendo 8:21.

Dhihaka mbaya kuliko zote ni dini iuachayo moyo bila kubadilika: dini iliyo na kila kitu isipokuwa upendo wa Kristo uliowekwa ndani ya nafsi.—F. Whitfield.

Juni 25

Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Matendo 13:2.

Tuna pembe nzuri ndogo yenye utulivu na kivuli katika shamba la mizabibu, chini kati ya zabibu changa, yenye palizi ndogo rahisi na kumwagilia maji ya kuhudumia. Kisha Bwana huja na kutuvuta kutuingiza katikati ya kazi, na kutuweka sehemu ya shamba ambapo kamwe tusingaliwaza kwenda, na kuweka vifaa vikubwa zaidi mikononi mwetu, ili tufanye mengi zaidi kwa pigo moja. Nasi twajua ya kuwa hatutoshi kwa mambo haya, na vile vifaa vyenyewe vyaonekana kuwa vizito mno kwetu, na mwangaza mkali mno na mizabibu mirefu mno. Ah! lakini je, tungezembea, turudi nyuma? Yeye asingekuwa katika pembe ya kivuli pamoja nasi sasa; kwa maana alipotupeleka nje alitutangulia, na ni kwa kumfuata kwa ukaribu zaidi tu ndipo twaweza kukaa naye.—Frances Ridley Havergal.

Juni 26

Vitu vidogo. Zekaria 4:10.

Ni maneno madogo unenayo, mawazo madogo uwazayo, mambo madogo ufanyayo au uyaachayo, dakika ndogo upoteazo au uzitumiazo kwa hekima, majaribu madogo uyakubaliayo au uyashindayo—vitu vidogo vya kila siku ndivyo vinavyofanya au kuharibu maisha yako ya wakati ujao.—Selected.

Juni 27

Mkamilike, mfarijike. 2 Wakorintho 13:11.

Kutazama tu maneno haya yatosha kutufanya tuhisi jinsi yanavyopingana. Mkamilike—hilo ni neno litupiga kwa kukata tamaa; mara moja twahisi jinsi tulivyo mbali na kiwango chetu maskini wenyewe, na, ole! jinsi tulivyo mbali zaidi na kiwango cha Mungu juu yetu. Mfarijike—ah, hilo ni tofauti sana! Hilo laonekana kusema, “Usifadhaike; usiogope. Kama huwi vile ungependa kuwa, yakupasa kushukuru kwa vile ulivyo.”

Basi swali ndilo hili—Je, haya mawili yaweza kupatanishwaje?

Ni dini ya Yesu Kristo peke yake iyapatanishayo. Yeye asimama katikati yetu, na kwa mkono wake wa kuume wa haki yake atuelekeza juu, na kusema, “Mkamilike.” Hakuna mahali pa kupumzika pungufu ya hapo. Walakini kwa mkono wake wa kushoto wa upendo wake atuzunguka, asemapo, “Ee nafsi, farijika; kwa maana ndilo nililokuja kukufanyia.”—Mark Guy Pearse.

Juni 28

Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Mathayo 5:48.

Tukitafuta msaada wa Roho Mtakatifu, na tulenge ukamilifu. Kila siku na ione dhambi fulani ikisulubiwa, vita fulani vikipiganwa, wema fulani ukifanyika, ushindi fulani ukipatikana; kila kuanguka na kufuatwe na kuinuka, na kila hatua ipatikanayo iwe, si mahali pa kupumzika, bali mwanzo mpya kwa maendeleo zaidi na ya juu zaidi.—Guthrie.

Juni 29

Laleni sasa, mpumzike. Marko 14:41.

Kamwe ile nafasi takatifu ya kukesha pamoja na Kristo haikuwarudia wanafunzi wake. Ikiisha kupotea wakati ule, ilipotea milele. Na sasa Yesu angali akitazama taabu ya nafsi yake katika ukombozi wa ulimwengu, kama ukishindwa kuwa pamoja naye ukikesha kwa ajili ya nafsi kama watu watakaopaswa kutoa hesabu, kumbuka ya kwamba nafasi hiyo kamwe haitarudi. “Kesheni, basi,” asema Bwana wako, “asije akaja ghafula, akakuta mmelala.”—A. J. Gordon.

Juni 30

Basi tusilale usingizi kama wengine. 1 Wathesalonike 5:6.

Kuna njia nyingi za kuendeleza ukesha wa Kikristo. Miongoni mwa nyingine, niwashauri Wakristo kwa nguvu wazungumze pamoja juu ya njia za Bwana. Christian na Hopeful, walipokuwa wakisafiri kuelekea Mji wa Mbinguni, walisemezana wao kwa wao:

“Ili kuzuia usingizi mahali hapa, na tuingie katika mazungumzo mema.”

Wakristo wanaojitenga na kuenenda peke yao huwa katika hatari kubwa ya kusinzia. Shikilia ushirika wa Kikristo, nawe utahifadhiwa katika ukesha kwa huo, na kuburudishwa na kutiwa moyo kufanya maendeleo ya haraka zaidi katika njia ya kwenda mbinguni.—Spurgeon.

Ukurasa 1 / 1 · 14 dakika zimebaki katika sura