Sura 34 · dakika 18 za kusoma
Unionyeshe Utukufu Wako!
"Jana niliitwa kumwona mgonjwa, mwanamke kijana aliyekuwa akiteseka vibaya mno kwa siku tatu. Hii ilikuwa hali ya kusikitisha kuliko zote nilizopata kuiona maishani mwangu. . . . Ilinibidi nimwache afe. . . . Jambo hilo lilikuwa la kutisha kiasi kwamba, ingawa mimi ni mpasuaji mzee na niliyezoea, tangu wakati huo nimefadhaishwa nalo sana. Maadamu ninaishi, kumbukumbu la tukio hilo litaninata."
Mmishonari mmoja wa China."Kama tukikataa kuwa punje za ngano ziangukazo ardhini na kufa; kama hatutaki kudhabihu matumaini yetu, wala kuhatarisha jina letu na mali na afya, wala, tuitwapo, kuacha nyumba na kukata mafungamano ya jamaa, kwa ajili ya Kristo na Injili yake, basi tutakaa peke yetu."
Thomas Gajetan Ragland, India."Si huruma tu kwa nafsi zilizokufa, bali shauku kali kwa Utukufu wa Mungu, ndiyo tuihitajiyo ili kutushikilia hata kwenye Ushindi."
Miss Lilias Trotter, Africa.SISI sote tunazifahamu hakika na takwimu zisimamiazo mambo makubwa kuliko tuyatambuavyo. Twaweza kurudia kwa wepesi kwamba wako watu karibu bilioni moja na milioni mia tano duniani, na kwamba katika hao karibu bilioni moja ni wapagani au Waislamu. Labda twaweza kuugawanya wingi huu usiofikirika katika takwimu zinazoeleweka. Twaweza kumwambia kila mtu apendaye kusikia, kwamba katika bilioni hii moja, milioni mia mbili ni Waislamu; milioni mia mbili zaidi ni Wahindu; milioni mia nne na thelathini ni Wabuddha na Wakonfusio; na zaidi ya milioni mia moja na hamsini ni wapagani.
Lakini je! tumepata kusimama na kuiacha hofu ya maneno haya ituelemee? Je! twatambua kwamba twanena juu ya nafsi zisizokufa?
Twanukuu hesabu ya mtu fulani kwamba kila siku watu elfu tisini na sita hufa pasipo Kristo. Je! tumepata kuketi saa nzima na kulifikiri jambo hilo? Je! tumelifikiri kwa nusu saa, kwa robo saa, kwa dakika tano bila kukoma? Naenda mbele zaidi, nami nakuuliza, je! umepata kuketi kimya dakika nzima moja na kuhesabu kwa mlio wa saa yako, huku nafsi baada ya nafsi ikitoka peke yake kwenda milele?
. . . Mimi nimelifanya. Ni jambo la kutisha. Kwa hesabu ndogo kuliko zote, watu sitini na sita ambao Kristo aliwafia wamekufa tangu nilipoandika neno "milele."
"Ee Mungu wangu! Mungu wangu! Watu wanaangamia, nami sijali!" . . .
Wengine sitini na sita wameondoka. Ee, mtu awezaje kukaa kimya kiasi hicho? Mauti yaonekana yakishindana mbio na mshale wa dakika wa saa yangu. Nahisi kama ningeuzuia mwendo ule wa kutisha wa mshale wa dakika. Wazunguka na kuzunguka, na kila uzungukapo, watu sitini na sita hufa.
Ndipo sasa hivi nimepata habari za kufa kwa mmoja wa hao sitini na sita. Tulimjua vema. Alikuwa mjane; hakuwa na mlinzi ye yote, na mjane asiye na mlinzi katika India yumo mahali pa hatari. Tulijua hivyo, tukajaribu kumshawishi ajikinge kwa Yesu. Alisikiliza, karibu akaamua, kisha akarudi nyuma; baadaye tukagundua sababu. Umeuona mchoro wa mtu anayenyonywa chini ya bahari na pweza; ilikuwa kama hivyo. Umewazia lile pambano la mauti; lilikuwa kama hivyo. Lakini yote yalitendeka chini ya uso wa maji, hapakuwa na cho chote kilichoonekana juu, hata labda kikatokea kiputo kikapanda taratibu na kupasuka; ilikuwa kama hivyo. Siku moja, wakati wa adhuhuri kamili, mwanamke alianguka ghafula barabarani. Mtu fulani alimchukua ndani ya nyumba, lakini alikuwa amekufa, na wale walioona mwili ule waliona alama za pambano juu yake. Maisha ya kijijini yakaendelea kama zamani; ni wachache tu waliomjua waliojua kwamba alikuwa ameuua mwili wake ili kuufunika kuuawa kwa nafsi yake. Tulikuwa tumefika kwa kuchelewa mno kwa ajili yake.
Juma lililopita nilisimama katika nyumba mahali ambapo mwingine wa hao sitini na sita alikuwa amefariki. Akiwa amejikunyata sakafuni, magoti yake yamekunjwa juu na kichwa chake juu ya magoti, mwanamke mmoja alianza kuniambia habari zake. "Alikuwa mdogo wangu wa kike. Mama yangu alitutoa kwa ndugu wawili"—naye akakoma. Nilijua ndugu hao walikuwa nani. Nilikuwa nimewaona jana—Wahindu wawili wa tabaka la juu wenye sura nzuri. Tulikuwa tumewatembelea wake zao, bila kujua. Mwanamke yule hakusema zaidi; hakuweza. Alitetemeka tu na kuuficha uso wake mikononi mwake. Jirani mmoja aliimaliza hadithi. Jambo fulani lilimwendea vibaya yule msichana. Waliita mke wa kinyozi—daktari pekee wa wanawake ajulikanaye pande hizo. Alifanya kazi yake kwa ujinga. Msichana alikufa kwa maumivu ya kutisha. Wanawake Wahindu wamezoea kuona mambo ya kutia kinyaa, lakini kifo cha msichana huyu kilikuwa cha kutisha kiasi kwamba dada yake mkubwa hajapata kupona mshtuko wa kukiona. Papo hapo aketi, waniambia, mchana kutwa, amejikunyata sakafuni, bila kunena.
Si wote wafao namna hiyo; wengine hufariki kwa utulivu sana, hakuna dhiki katika mauti yao; na wengine ni watoto wasio na hatia—ashukuriwe Mungu kwa faraja ya jambo hilo! Lakini kamwe isisahauliwe kwamba wapagani hutenda dhambi kinyume cha nuru waliyo nayo; maisha yao huwashuhudia. Wanajua kwamba wanatenda dhambi, nao wanaogopa mauti. Daktari Mkristo Mhindi, aliyekuwa akitibu katika mojawapo ya miji yetu ya Wahindu, aliniambia kwamba hakuweza kuyanena aliyoyaona na kuyasikia kando ya vitanda vya kufa vya baadhi ya wagonjwa wake.
Msichana mmoja aliingia punde tu, nami nikamwambia nilokuwa nikilifanya. Kisha nikamwonyesha ule mchoro wa Kabari; lile duara kubwa jeusi la upagani, na ule mpasuko mwembamba mweupe wa waongofu waliopatikana. Aliutazama kwa mshangao. Kisha akaufuatisha kidole chake taratibu kuzunguka lile duara, akauonyesha ule mpasuko mwembamba, machozi yake yakadondoka juu yake. "Ee, ni lazima Yesu ahisije!" akasema. "Ee, ni lazima Yesu ahisije!" Yeye ni msichana wa kijijini wa kawaida tu, amekuwa Mkristo mwaka mmoja tu; lakini kuliona lile waa jeusi kubwa kulimgusa hata ndani ya moyo wake.
Najua wako wanaojali huko kwao, lakini je! wote wanaojali, wanajali kwa kina cha kutosha? Je! wanahisi kama Yesu ahisivyo? Na kama wanahisi hivyo, je! wanawatoa walio wao? Labda wanasaidia kuwatuma wengine; lakini je! wanawatoa walio wao wenyewe?
Ee, je! kweli wanajitoa wenyewe? Sharti kuwe na kujitoa zaidi kwa nafsi zetu ikiwa ule mpasuko utapanuliwa katika lile duara. Baadhi ya wanaojali ni vijana, na maisha yote yamo mbele yao, na swali linalosonga sasa ni hili: Maisha hayo yatatumika wapi? Baadhi ni wazee mno hata hawawezi kuja, lakini wanao wale ambao wangeweza kuwatuma, laiti wangejivua kwa ajili ya Yesu.
Enyi mama na baba, je! mna huruma pamoja na Yesu? Je! mko tayari kuwa peke yenu kwa miaka michache mifupi, ili katika enzi zote za milele apate wengi zaidi wa kuwafurahia, nanyi pamoja naye? Huenda anakuja karibuni sana, na muda mfupi uliobaki, washika nafasi yetu ya mwisho hakika ya kuteseka kwa ajili yake, na huenda nafasi yetu ya mwisho ya kumshindia vito kwa taji yake. Ee, migodi ya vito ya upagani isiyofanyiwa kazi! Ee, furaha ambayo walio wake wanaikosa wakiipoteza nafasi hii moja ya mwisho!
Nyakati nyingine twadhani kwamba kama uhitaji ungeonekana wazi zaidi, jambo zaidi lingefanyika. Njia zingebuniwa; watu wawili au watatu wenye nia moja wangeishi pamoja, ili kupunguza gharama, na kumweka huru mtoto ambaye vinginevyo sharti abaki kwa ajili ya mmoja wa hao watatu. Watumishi walio ng'ambo waweza kuishi pamoja, wakiizamisha nafsi na mapendeleo yake na machukio yake kwa ajili ya lile Jambo lisimamalo kwanza. Lakini kama badiliko kama hilo haliwezekani huko kwao, jambo jingine litapangwa, ambalo kwalo wengi zaidi wataachiliwa, watakapokuwa wale wampendao Mungu wetu wanampenda vya kutosha hata kuyaweka mambo yake kwanza. "Astahili Mwana-Kondoo kupokea!" Ee, twalisema, na twaliomba! Je! twatenda kana kwamba tunalimaanisha? Enyi baba na mama, je! yeye hastahili? Enyi watoaji, mliotoa Vyote vyenu, je! hamkumwona kuwa anastahili?
"Takwimu tupu zilinilemea," akasema mmoja, alipoeleza jinsi alivyoongozwa kuja nje; "Nilishikwa na mshangao mkubwa niliposoma kwamba watu elfu ishirini na nane kwa siku katika India peke yake, huenda kufani mwao pasipo Kristo. Nami nikauliza, Je! twaliamini? Je! kweli twaliamini? Ni dawa gani ya usingizi ambayo Shetani ameiingiza katika miili yetu hata jambo hili la kutisha, la kuhuzunisha, la ajabu halitushtui kutoka usingizi wetu, na uzembe wetu wa kutisha juu ya nafsi za wanadamu?"
Kuna mto unaopita katika Wilaya hii. Wanzia katika Milima ya Western Ghauts, nao hutiririka sehemu kubwa ya mwaka ukiwa kijito kitulivu, kifupi. Lakini mvua za monsuni zizidipo kufurika vyanzo vya maji, hujaa kwa kasi ya ghafula, ya fahari; waweza kuusikia toka umbali wa maili moja.
Huko nje katika sakafu ya mto yenye mchanga zimejengwa majukwaa kadhaa marefu ya mawe, yatumiwayo na wasafiri kama mahali pa kupumzikia wakati mto umepwa. Miaka kadhaa iliyopita kikundi cha vibarua, wakiwa wamechelewa, waliamua kulala juu ya mojawapo ya majukwaa haya; kwa maana ingawa majira ya mvua yalikuwa yamewadia, mto ulikuwa umepwa sana. Lakini usiku mto ukajaa. Ukawakumba pale walipojishikilia juu ya jiwe. Ukawazungusha chini gizani hata baharini.
Hebu wazia kwamba, ukijua, kama wao wasivyojua, kwamba mvua ilikuwa imeanza kunyesha vilimani, na mto ni hakika ungejaa, ungebahatika kupita wakati vibarua hao walipokuwa wakijitayarisha kwa usiku, je! ungeweza, ungeliweza, kupita zako ukiridhika bila juhudi ya kuwaambia hivyo? Je! ungeweza, ungeliweza kwenda kitandani na kulala kwa utulivu kamili huku wanaume na wanawake hao uliowaona wangali nje katika sakafu ya mto?
Kama ungefanya hivyo, ngurumo ya mto ingekuamsha, na milele moyo wako wenyewe ungekuwa baridi kwa ubaridi ulio baridi kuliko maji ya mto, baridi kwa kuwaza wale uliothubutu kuwaacha wazame!
Waweza kusema, Huwezi kuwaona. Waweza. Mungu ameupa akili macho. Fikiri, nawe utaona. Kisha sikiliza. Ni Mungu anenaye. "Uwaokoe wanaokokotwa kwenda kufa, na wale wanaopepesuka kwa kuchinjwa uwazuie. Kama ukisema, 'Tazama, sisi hatukujua neno hili,' je! yeye apimaye mioyo hafahamu? na yeye aichungaye nafsi yako, je! hajui? naye je! hatamlipa kila mtu sawasawa na kazi yake?"
Ee, kwa kuwaza wingi wa wale wanaokokotwa kwenda kufa, na wingi wa wale wanaopepesuka kwa kuchinjwa, kwa kuwaza huzuni ya Yesu awapendaye, yatafakarini mambo haya!
Lakini si wote walioitwa kuja! Twajua hivyo. Hatulisahau. Lakini je! ni jambo lililosahauliwa kiasi hicho huko kwao hata mmishonari alazimike kulisisitiza? Lililosahauliwa kwa hakika ni kwamba shamba ni ulimwengu.
Hungependa kuiacha Uingereza tupu! Je! Uingereza ingeachwa tupu? Je! kiti kimoja tu katika benchi ya Askofu, au parokia moja tu au ukumbi mmoja wa umishonari, kingeachwa wazi daima, kama mtu akijaaye sasa angehamia mahali pale ambapo hapana ajaaye—lile pengo lililo ukingoni mwa jabali?
Lakini tuseme ingeachwa tupu, je! jambo hilo lingekuwa la kutisha kiasi hicho hatimaye? Je! hangebaki Mkristo mmoja wa kweli wa kuionyesha njia iendayo kwa Kristo? Na kama mabaya yote yangetokea, je! Biblia isingebaki bado, na uwezo wa kusoma? Je! ni lazima mtu ye yote afe pasipo kuokolewa, isipokuwa amejielekeza kujiangamiza mwenyewe? Laiti Wakristo katika Uingereza wangejua jinsi ya kupata riziki moja kwa moja toka kwa Mungu, laiti wale wasioweza kuja wangebeba jukumu la wale ambao hawajaongoka walio karibu nao, kwa nini parokia hapa na pale isingeachwa tupu kwa kitambo? Bila shaka hatupaswi kwa makusudi kuwaacha wengi mno wafe kwa njaa, kwa sababu wale walio na Mkate wa Uzima wana shauku kubwa ya vitamu-tamu. Ee, peremende za kiroho zinazotumiwa kila mwaka katika Uingereza! Mungu na ayafumbue macho yetu tuone kama tunafanya alilokusudia, na alilokusudia liendelee! Lakini watu wengine wana thamani mno hata kutupwa katika shamba la umishonari; ni watumishi wenye mafanikio makubwa hivyo, wachungaji, wainjilisti, viongozi wa mawazo. Haiwezekani kabisa waachiliwe. Fikiri hasara ya kuzika ubongo katika mchanga usiozaa! Kwa dhahiri ni hivyo, lakini je! kweli ni hivyo? Je! Mungu aliona hivyo? Tungekuwa wapi leo kama yeye angemwona Yesu kuwa na thamani mno hata kutupwa juu yetu? Je! kila saa ya ile miaka thelathini na mitatu haikuwa na thamani kuliko maisha yetu yote?
Ni fasili gani ya Mungu ya lile neno la dhahabu "mafanikio"? Yeye ayatazama Ulaya ya Kikatoliki cha Rumi, na Amerika ya Kusini ya Kirumi na ya kipagani, na Afrika na Asia ya Kiislamu na ya kipagani, na mahali pengi paliposahauliwa katika nchi nyingi kubwa. Kisha atutazama sisi, nami nashangaa afikiriaje. Ragland, Mshirika wa Chuo cha Corpus Christi, Cambridge, baada ya miaka ya hasara ya kuzika ubongo, aliandika kwamba Mungu alikuwa akimfundisha kwamba "katika mipango yote ya kuhakikisha mafanikio ulio hakika kuliko yote ni ule wa Kristo mwenyewe, kuwa punje ya ngano, ikianguka ardhini na kufa." Ikiwa kwenda ng'ambo humaanisha hivyo kwa mtu ye yote, je! ni kuomba kupita kiasi? Ndilo Bwana wetu mpendwa alilofanya.
Hili latuleta kwenye ombi jingine. Nalipata katika ile aya ichongayo kwa mikwaju miwili matokeo yote ya maisha mawili. "Kazi ya mtu ikikaa. . . . Kazi ya mtu ikiteketezwa." Matokeo halisi ya kazi ya mtu mmoja ni dhahabu, fedha, vito vya thamani; matokeo halisi ya kazi ya mtu mwingine ni miti, majani, mabua. Ni yapi yastahiliyo kutumiwa kwa maisha?
Mtumishi mwenye bidii katika fani yake maalum ya kazi anaitazama nyuma toka mahali ambapo mambo huonekana kwa ukweli zaidi, naye asema, "Mungu atusaidie sisi sote! Ni wema gani utendwao na kazi yo yote kama yangu? 'Mtu akijenga juu ya msingi huu . . . miti, majani, mabua. . . . Kazi ya mtu ikiteketezwa atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa, lakini ni kama kwa kupitia motoni!' Wingi usio na kikomo wa taabu na kazi, na yote kutoweka kama mabua na majani."
Mafanikio—yana thamani gani?
"Nilifurika kwa sifa,Lakini nikisita kwa dakika moja tu kuvuta pumzi,
Sikuweza ila kunong'ona nafsini mwangu,
'Je! ni haya tu? Yote yaliyofanyika? na yote yaliyopatikana?
Kama haya, basi, ndiyo mafanikio, ni ya kuhuzunisha zaidi
Kuliko kushindwa ko kote.'"
Ni kitu chenye uwazi kiasi gani mng'aro wa mafanikio machoni mwa mshairi aonaye wazi, na je! yampasa kumpumbaza Mkristo ambaye kwake hakuna kitu chenye thamani yo yote ila kile kidumucho? Je! hoja zilizojengwa juu ya kulinganisha kati ya mafanikio yaonekanayo ya kazi ya huko kwao na yale ya kazi ya ng'ambo yatupaswa kutuathiri kwa namna yo yote? Je! si jambo zito sana, huku kuwekwa wazi kwa utulivu na kwa dhahiri kwa ukweli uwagusao kila mmoja wetu? "Kazi ya kila mtu itafunuliwa, kwa maana ile Siku itaidhihirisha, kwa sababu itafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani." Na tutambuapo jinsi kazi yote iwezavyo kuharibika, hata iwe yaonekana kufanikiwa kiasi gani, isipokuwa ile kazi moja iliyofanywa kwa ile njia moja Mungu aikusudiayo, ee, je! haitutii moyo kutafuta kwa nia thabiti isiyokataliwa, ili kufahamu ile kazi moja ni ipi? Wazo lilo hilo latokea katika ile aya ituambiayo kwamba yale mambo hasa tunayopaswa kuyatenda yametengenezwa tangu zamani, nasi "tuliumbwa katika Kristo Yesu" ili kuyatenda. Ikiwa ni hivyo, basi je! kutenda jambo jingine lo lote kutaonekana kuwa kwa faida, tutakapotazama nyuma na kuyaona maisha kama Mungu ayaonavyo?
Yamkini yale mambo yaliyotengenezwa yamelala karibu na mkono wetu huko kwetu, lakini yamkini yamo ng'ambo. Kama yamo kwetu kutakuwa na amani tulivu katika kuyatenda huko; lakini kama yamo ng'ambo, nasi hatutaki kuja na kuyatenda?—Ee, ndipo maombi yetu yenyewe yataanguka kama yaangukavyo majani yaliyonyauka, upepo uliyatingisha ukisha kutulia, naam zaidi ya hayo, kwa maana majani yaliyonyauka yana kazi ya kufanya, bali maombi yatiwayo msukumo na upepo fulani upitao wa hisia hayafanyi cho chote, hayafanyi cho chote kwa ajili ya milele. Mungu hatasikia maombi yetu kwa ajili ya wapagani ikiwa akusudia sisi tuwe nje kati yao badala ya kukaa kwetu tukiwaombea, au ikiwa akusudia sisi tuache mwana au binti fulani, nasi twapendelea kuomba.
Bwana utuokoe na unafiki na uongo! "Ukaushe uwongo" utoke ndani yetu kama tukisema twakupenda lakini hatukutii! Je! twakaa kwetu, na kuombea umishonari hali Wewe umetuambia "Nenda"? Je! twashikilia kitu ambacho juu yake Wewe umesema, "Kifungue, ukiache kiende"? Bwana, je! sisi ni kweli kabisa ndani na nje? Bwana Mungu wa ukweli, utuokoe na uongo! Utufanye kuwa wa kweli kamilifu!
Nawageukia ninyi, ndugu zangu wa kiume na wa kike wa huko kwenu! Je! mwajua kwamba kama Mungu anawaita, nanyi mkikataa kutii hamtajua vyema jinsi ya kuvumilia yatakayotukia baadaye? Mapema au baadaye mtajua, naam mtaungua katika kila sehemu ya nafsi yenu, kwa kujua kwamba mliasi, mkaikosa nafasi yenu, mkaikosa milele. Kwa maana hiyo ndiyo sehemu ya kutisha. Ni mara chache mtu apewapo kurudi nyuma na kuiokota nafasi aliyoiacha kwa kujua. Treni ya kasi ya maisha ya mtu imepita njiapanda, wala mtu hawezi kurudi nyuma; njia zagawanyika.
"Baadhi yetu karibu tunatetemeka sasa kufikiri jinsi tulivyokaribia kubaki kwetu," aandika mmishonari. "Nawasihi, msiliache jambo hili kubwa liende ovyo. Msitembee katika kutokuwa na hakika. Msigeuzwe upande. Mtakuwa maskini zaidi milele kama mkifanya hivyo."
Yamkini huna uhakika juu ya lililo mapenzi ya Mungu kwako. U katika shaka, wewe ni mwaminifu, lakini maswali elfu yakuchanganya. Je! utamwendea Mungu kwa habari hiyo, na kupata jibu moja kwa moja?
Kama umechanganyikiwa juu ya mambo ambayo mmishonari mnyoofu aweza kuyaeleza, je! utanunua nakala ya Do Not Say, na kuisoma peke yako na Mungu? Niliache nisisitize neno lile "peke yako." "Ondoka, uende bondeni, nami nitasema nawe huko." "Palikuwa na sauti . . . waliposimama, na kuzishusha mbawa zao."
Ee, kwa kuwaza ile Siku ijayo, ambayo moto utaijaribu yote tunayoyafanya, na kweli peke yake ndiyo itakayosimama, naomba jambo hili likabiliwe kwa unyofu kabla halijawa kuchelewa mno!
Lakini hili silo ombi letu lililo na nguvu kuliko yote. Twaweza kuyarundika, ombi juu ya ombi, wala tusiimalize idadi yayo yanayosonga na kumsihi mtu kuandika. Twayapita yote, na kwenda mahali ambapo lililo na nguvu kuliko yote lasubiri: Utukufu wa Mungu wapewa mwingine. Hili ndilo ombi zito kuliko yote, ule wito wa lazima ulio mkuu kuliko yote. "Si huruma tu kwa nafsi zilizokufa, bali shauku kali kwa Utukufu wa Mungu, ndiyo tuihitajiyo ili kutushikilia hata kwenye ushindi."
"Mimi ni Bwana, ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitaipa sanamu za kuchonga sifa zangu." Lakini watu aliowafanya wamtukuze wamnyang'anya Utukufu wake, wampa mwingine; hilo, dhambi yake, aibu yake, laita kwa wito wa chini, wa ndani sana, kupitia kati ya wito wote wengine. Utukufu wa Mungu wapewa mwingine. Je! twampenda vya kutosha hata tujali? Au twapima gharama yetu binafsi, kama nafsi hizi za mbali zitakombolewa, na, tukiiona kuwa kubwa, twaacha kufikiri au kujali? "Je! si kitu kwenu, ninyi nyote mpitao njiani? Angalieni, mkaone"—"Basi wakamtwaa Yesu, wakamchukua. Naye akiwa ameuchukua msalaba wake, akatoka kwenda mahali paitwapo Fuvu la Kichwa . . . ndipo walipomsulibisha." . . . "Hii ndiyo pendo." . . . "Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu." . . . Je! tumekuwa mawe hata kupita kuhisi? Je! twaweza kusimama na kupima sasa? "Najua kwamba ni Roho peke yake, aliyeihesabu kila tone lililoanguka toka paji la uso la Kristo lililoraruliwa kuwa la thamani kuliko malango yote ya Paradiso yaliyopambwa kwa vito, awezaye kuiinua Kanisa kutoka katika kuuthamini ulimwengu wake, ule ulimwengu kama uvutiavyo tamaa zake mwenyewe za ubinafsi, hata kuuthamini ulimwengu kama uvutiavyo moyo wa Mungu." Ee Roho, njoo utuinue katika pendo hili, utuvuvie kwa pendo hili. Na tuutazame ono la Utukufu wa Mungu wetu kwa macho yaliyolitazama pendo lake!
Hatungependa kujenga ombi hata moja juu ya kitu chenye udhaifu kuliko hakika thabiti. Hisia hazitastahimili mkazo wa vuta-nikuvute halisi; lakini je! ni hakika, au sivyo, kwamba Yesu alikuhesabu wewe na mimi, na watu wengine walioko ulimwenguni, kuwa kweli tunaostahili kufia? Kama ni kweli, basi je! twampenda vya kutosha hata tujali kwa nguvu zote za nafsi zetu, kwamba leo, karibu ulimwengu mzima, Utukufu wake wapewa mwingine? Kama jambo hili halitutikisi, je! ni kwa sababu hatumpendi sana, au ni kwamba hatujapata kuomba kwa shauku ya kweli, kama Musa alivyoomba, "Nakusihi, unionyeshe utukufu wako"? Yeye aliona kidogo tu chake. "Tazama, mahali hapa panipo mimi, nawe utasimama juu ya mwamba; hata itakapokuwa utukufu wangu unapita, nitakuweka katika ufa wa mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hata nitakapokwisha kupita." Na utukufu wa Bwana ukapita, na Musa akatambua kitu fulani chake ulipopita, lakini "uso wangu hautaonekana," Na hata hivyo kidogo kile kilitosha kumtambulisha kuwa mtu aliyeishi kwa kusudi moja, aliyeng'aa katika nuru yake, aliyeungua kwa moto wake—alikuwa na wivu kwa Utukufu wa Mungu wake.
Nasi—"Nasi tuliuona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli"; nasi—sisi tumeiona "nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo."
"Utukufu wangu utakapopita . . . nitakufunika . . . uso wangu hautaonekana." "Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiutazama utukufu wa Bwana kama katika kioo, tunageuzwa"—Je! twageuzwa? Je! twafanya hivyo? Je! twajua neno lo lote juu yake kabisa? Je! tumepata kulishika hili ambalo kwalo tumeshikwa na Kristo Yesu? Je! tumepata kuliona lile Ono la Mbinguni lituvunjalo, na kutunyenyekesha hata kuisikia Sauti ya Bwana ikiuliza, "Ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?" na kututia nguvu kujibu, "Mimi hapa, nitume mimi," na kutushikilia tutii tukimsikia akisema "Nenda"?
"Nakusihi, unionyeshe utukufu wako!" Je! tutaliomba, tukilimaanisha sasa, hata upeo wenyewe? Upeo huo waweza kuwa na mambo magumu, lakini, mepesi au magumu, hapana njia nyingine ya kufika mahali ambapo maisha yetu yaweza kupokea msukumo utakaoyafanya kuwa na maana kwa milele. Nguvu ya kuchochea ni pendo la Kristo. Si pendo letu kwake tu, bali pendo lake lenyewe hasa. Ni mtiririko wenye nguvu, usiozuilika wa pendo lile tukufu uliyomfanya mmishonari wa kwanza ajimimine juu ya dhabihu na utumishi. Na furaha yake yavuma kwa ushindi, "Naam, hata kama nikimiminwa . . . nafurahi, tena nafurahi pamoja nanyi nyote!"
Naam, Utukufu wa Mungu ndilo ombi letu, lililo juu kuliko yote, lenye nguvu kuliko yote, lililo na msukumo na udumu kuliko maombi yote. Lakini ee, kwa kuwaza makutano wanaopita, kwa kuwaza Kuja kwa Bwana, kwa hakika zisizo na kikomo za uzima na mauti, mbingu na jehanamu, kwa msalaba wa Mwokozi wetu na Mateso yake, twawasihi wale wote wampendao, lakini ambao hawajayafikiri mambo haya bado, yafikirini sasa!
Na atuonyeshe ono la Utukufu, na atulete hata mwisho kabisa wa nafsi, na aiguse midomo yetu kwa kaa la moto lililowaka, na atuwashe moto tumwakie yeye, naam, tuwake kwa pendo liteketezalo kwa ajili yake, na kusudi ambalo hakuna awezaye kutugeuza toka kwalo, na shauku kali kama mwali mweupe safi, "shauku kali kwa Utukufu wa Mungu!"
Ee, shauku hii na ituteketeze! iuunguze ubinafsi utoke ndani yetu, iliunguze pendo liingie ndani yetu—kwa ajili ya Utukufu wa Mungu twaliomba, Amina.
"Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa kupokea uweza, na utajiri, na hekima, na nguvu, na heshima, na utukufu, na baraka . . . Baraka, na heshima, na utukufu, na uweza, ziwe kwake yeye."