Sura 8 · dakika 13 za kusoma
Katika Siri ya Uwepo Wake
Kwa maana fulani Mungu yu karibu nasi sikuzote. Yeye si Mungu aliyeko mbali, ahitajiye kuteremshwa kutoka mbinguni wala kupandishwa kutoka vilindini. Yu karibu, mkononi. Uwepo wake wajaza vyote vilivyoko. Kila ulimwengu, uelaeo kama kisiwa kidogo katika bahari ya anga, umejaa alama za uwepo wake, kama vile nyumba ya rafiki yako ijaavyo ushahidi mwingi wa kukaa kwake, ambao kwao wajua ya kuwa anaishi humo, ijapokuwa hukuuona uso wake. Kila ua la mfumbwe lisukumapo katika udongo wa giza; kila kimulimuli msituni; kila ndege arukaye kutoka kioto chake mbele ya miguu yako; kila kilichoko -- vyote vimejaa uwepo wa Mungu kama kile kichaka kilichowaka kwa moto wake, ambacho mbele yake Musa alivua viatu vyake miguuni akikiri ya kuwa Mungu yuko pale.
Lakini hatuutambui uwepo huo sikuzote. Mara nyingi twapitisha saa, na siku, na majjuma. Nyakati nyingine twajishughulisha na vipindi vya maombi, twaenda na kurudi kutoka nyumbani mwake, ambako ngazi ya mawasiliano imesimama; na bado kwetu yeye ni kivuli, ni jina, ni desturi, ni ndoto ya siku zilizopita.
"Laiti ningejua ni wapi ningemwona, nipate kufika hata kwenye kiti chake cha enzi! Tazama! Naenda mbele, wala hayuko; na nyuma, lakini simwoni: kushotoni, atendako kazi, lakini simtazami; ajificha kuumeni, hata siwezi kumwona."
Jinsi gani kushindwa huku kuutambua uwepo wa Mungu kunavyotofautiana na tukio lile la baraka la ukaribu wake kama walivyoupata baadhi ya watu!
Ndugu Lawrence, yule mpishi mwenye moyo mnyofu, atuambia ya kuwa kwa muda wa zaidi ya miaka sitini hakupoteza kamwe hisia ya uwepo wa Mungu, bali aliutambua alipokuwa akitimiza kazi za huduma yake ya unyenyekevu, kama vile alipokuwa akishiriki Meza Takatifu.
John Howe, katika ukurasa mtupu wa Biblia yake, aliandika maneno haya kwa Kilatini: "Asubuhi hii hasa niliamka kutoka usingizini katika ndoto ya kufurahisha na kupendeza mno, mtiririko wa ajabu na tele wa miale ya mbinguni, kutoka kile kiti kilichotukuka cha Enzi ya Mungu, ulipoonekana kupenya kifuani mwangu kilichokuwa wazi na kimekunjuliwa. Tangu wakati huo mara nyingi nimeitafakari ile ahadi ya wazi ya fadhili za pekee za Mungu, na kwa furaha mpya iliyorudiwa nimeonja utamu wake."
Je, matukio haya, yaliyojaa baraka na kutia moyo hivyo, si mfano wa lile la mwandishi wa Zaburi iliyo ndefu kuliko zote, na, kwa namna fulani, iliyo tukufu kuliko zote katika Kitabu cha Zaburi? Alikuwa akifua madini ya dhahabu ya fikira katika aya zilizofuatana zenye nguvu na uzuri wa ajabu, ghafula aonekana kuwa alitambua ya kuwa Yeye, aliyekuwa akimnena, alikuwa amekaribia, naye ainama juu yake. Hisia ya uwepo wa Mungu iliingizwa ndani ya fahamu yake ya ndani. Naye, akiinua uso uliokutanika na kuchanganyika heshima na furaha kuu, akalia, Wewe u karibu, Bwana!" (Zaburi 119:151.)
Laiti tukio kama hilo la ukaribu wa Mungu lingekuwa letu sikuzote, likitufunika kama hewa au nuru; laiti tungeweza kuhisi, kama vile Mtume mkuu alivyonena juu ya Kilima cha Mars, ya kuwa Mungu hayuko mbali, bali ndiye kile kitu ambacho ndani yake tuna uhai wetu, kama maua ya baharini yalivyo katika maziwa marefu, matulivu: -- ndipo tungefahamu maana ya Daudi aliponena juu ya kukaa nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yake, akiutazama uzuri wake, akiuliza hekaluni mwake, na kufichwa katika siri ya hema yake (Zab. 27). Ndipo, pia, tungepata ile siri ya baraka ya amani, na usafi, na nguvu.
Katika Siri ya Uwepo Wake Kuna Amani. "Ulimwenguni mtapata dhiki," alisema Bwana wetu, "lakini ndani yangu mtapata amani." Yasemekana ya kuwa mdudu fulani ana uwezo wa kujizungushia utando wa hewa, ambao ndani yake hujitumbukiza katikati ya madimbwi ya matope yaliyotuama, naye habaki bila kudhurika. Naye mwenye kuamini pia ajua ya kuwa amefungiwa ndani ya utando usioonekana wa Uwepo wa Mungu, kama barua iliyosafiri mbali ilivyo ndani ya bahasha imhifadhiyo asidhuriwe wala asichafuliwe.
"Wananikaribia wale wafuatao maovu," lakini Wewe u karibu kuliko aliye karibu kabisa, nami nakaa katika duara la ndani la uwepo wako. Milima inayonizunguka imejaa farasi na magari ya vita ya ulinzi wako. Hakuna silaha itakayofanyizwa juu yangu itakayofanikiwa, kwa maana yaweza kunifikia kwa kupitia kwako tu, nayo, ikikugusa Wewe, itageuka kando bila kudhuru. Kuwa ndani ya Mungu ni kuwa ndani ya nyumba iliyojengwa vizuri wakati dhoruba imefunguliwa kutoka kamba yake; au ndani ya patakatifu, ambapo milango yake humzuia nje mfuatiaji.
Katika Siri ya Uwepo Wake Kuna Usafi. Kule kuiona tu milima ya Alps iliyofunikwa theluji, ionekanavyo kwa mbali ng'ambo ya ziwa la Geneva, huinua na kubadilisha sura ya nafsi iliyovutwa na yenye shauku hata kuyaaibisha mambo yote maovu yatakayojisukuma katika maisha ya ndani. Uwepo wa mtoto mdogo, pamoja na usafi wake usio na hila, umejulikana kuinyang'anya tamaa silaha yake, kama vile mwali wa nuru, uangukapo katika pango lililojaa watambaao, uwatawanyavyo nyoka wenye ute. Lakini je, uwepo wako hautanitendea nini, nikipata hisia yake ya daima, na kukaa katika mahali pake pa siri? Hakika, ndani ya moyo wa moto ule, ijapokuwa mimi ni kaa jeusi la moto, nitawekwa safi, na kung'aa, na kuwaka sana!
Katika Siri ya Uwepo Wake Kuna Nguvu. Kilio changu, mchana na usiku, ni kwa ajili ya nguvu -- nguvu za kiroho. Si nguvu za akili, wala za ufasaha wa kunena, wala za uwezo wa kibinadamu. Hizi haziwezi kufaa kuzishinda safu za maovu zilizopangwa. Wasema kweli ya kuwa si kwa uwezo, wala kwa nguvu. Lakini nafsi za wanadamu zikugusazo Wewe hupata mvuto, hujazwa nguvu ya kiroho ambayo ulimwengu hauwezi kuikana wala kuipinga. Ee! Nijalie nikuguse Wewe! Nijalie nikae katika kushikamana kusikokatika nawe, ili kutoka kwako mafuriko yaliyofuatana ya nguvu ya Mungu yaingie na kupita katika roho yangu iliyotupwa wazi na yenye shauku, ikitiririka, wala isipwe kamwe, ikininua hata maisha ya huduma ya baraka, yatakayofanya jangwa lililo chini kuwa kama bustani ya Bwana.
Lakini tutapataje na kuitunzaje hisia hii ya ukaribu wa Mungu?
Je, ni lazima turudi Betheli, penye nguzo yake ya jiwe, hata Yakobo aliposema, "Hakika Bwana yumo mahali hapa"? Ah, huenda tungesimama kando yake, kwa jicho lisilotiwa mafuta, tusione ngazi, tusisikie sauti; hali yule baba wa mababa angemwona Mungu katika nyika tupu za maisha yetu, tuzikanyagazo bila heshima wala furaha.
Je, ni lazima tusafiri hata mdomo wa pango ambalo katika kivuli chake Eliya alisimama, akifurahishwa na muziki wa sauti ndogo, tulivu, iliyo tamu zaidi ikilinganishwa na radi na dhoruba? Ole! huenda tungesimama kando yake bila kuutambua Uwepo ule wa utukufu; hali Eliya, kama angekuwa hai sasa, angeutambua katika mnong'ono wa upepo, katika vitoto vitetavyo, katika mdundo wa mapigo ya moyo.
Kama tungejiweka katika hali yetu hii ya sasa kando ya Mtume Paulo alipochukuliwa hata mbingu ya tatu, yamkini tusingeona kitu ila duka la mshoni wa hema, au chumba chenye giza katika nyumba ya kupanga -- sisi tukiwa gizani, hali yeye akiwa katika furaha kuu; hali yeye angeutambua, kama angeishi tena, malaika juu ya meli zetu za mvuke, maono ndani ya mahekalu yetu, milango ifunguliwayo kuingia mbinguni katikati ya utukufu uliopunguzwa wa mbingu zetu zenye giza zaidi.
Kwa kweli, kila mahali twachukua duara letu la nuru au la giza. Mungu yumo ulimwenguni kama alivyokuwamo Henoko alipotembea pamoja naye, na Musa aliponena naye uso kwa uso. Yu radhi kuwa Uhalisi ulio hai, wenye kung'aa, wa utukufu kwetu kama alivyokuwa kwao. Lakini kosa liko kwetu. Macho yetu hayakutiwa mafuta kwa sababu mioyo yetu si mizima. Wenye moyo safi bado wamwona Mungu, na kwa wale wampendao, na kuzishika amri zake, bado hujidhihirisha kwao kama asivyojidhihirisha kwa ulimwengu. Tuache kuilaumu nyakati zetu; na tujilaumu sisi wenyewe. Sisi ndio tulioharibika, si wao.
Basi, ni hali gani ya nafsi iutambuayo kwa urahisi zaidi uwepo na ukaribu wa Mungu? Na tujitahidi kujifunza ile siri ya baraka ya kukaa daima katika siri ya Uwepo wake na kufichwa katika Hema yake (Zab. 31:20).
Basi, kumbuka, tangu mwanzo, ya kuwa wala wewe, wala ye yote wa jamii yetu, hawezi kuwa na fahamu ile ya furaha ya Uwepo wa Mungu ila kwa njia ya Yesu. Hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na wale ambao Mwana apenda kuwafunulia; wala hakuna aje kwa Baba ila kwa yeye. Pasipo Yesu Uwepo wa Mungu ni kitu cha kutisha, ambacho mashetani hujificha kutoka kwacho hata kuzimu, na wenye dhambi hushona nguo za kujifunika, au hujificha kati ya miti. Lakini ndani yake vizuizi vyote vimebomolewa, mapazia yote yamepasuka, mawingu yote yametawanyika, na mwenye kuamini aliye dhaifu kupita wote aweza kuishi, mahali Musa alipokaa, katikati ya moto, ambao mbele ya miali yake iteketezayo hakuna unajisi uwezao kusimama.
"Ni sehemu gani ya kazi ya Bwana iliyoungamana kwa ukaribu zaidi na hisia hii ya baraka ya Uwepo wa Mungu? "
Ni kwa damu ya msalaba wake wenye dhambi wanapokaribishwa. Katika kufa kwake hakuudhihirisha upendo mwororo wa Mungu tu, bali aliziondoa dhambi zetu, na kutufumia mavazi yale ya uzuri usio na doa, ambayo kwayo twakaribishwa kwa furaha katika chumba cha ndani cha Uwepo wa Mfalme. Kumbuka imesemwa, "Nitazungumza nawe kutoka juu ya kiti cha rehema." Ubao ule wa dhahabu ambao juu yake Haruni alinyunyiza damu kila alipoingia Patakatifu pa Patakatifu ulikuwa mfano wa Yesu. Yeye ndiye kiti cha kweli cha rehema. Nawe ni utakapoingia katika ushirika ulio ndani kabisa naye katika kufa kwake, na kuishi daima katika roho ya meza yake ya ukumbusho, ndipo utakapoutambua ukaribu wake kwa undani zaidi. Sasa, kama vile huko Emau, apenda kujidhihirisha katika kuumega mkate.
Na je, ndivyo hivyo tu? kwa maana nimeyasikia haya mara nyingi, na bado nashindwa kuishi katika mahali pa siri kama nitakavyo."
Ni kweli kabisa; na kwa hiyo, ili kututendea sisi lile ambalo juhudi yetu isingeweza kulitenda, Bwana wetu amepokea kutoka kwa Baba yake ahadi ya Roho Mtakatifu, ili aulete mioyoni mwetu Uwepo wenyewe wa Mungu. Fahamu ya kuwa kwa kuwa wewe u wa Kristo, yule Mfariji wa baraka ni wako. Yumo ndani yako kama alivyokuwamo ndani ya Bwana wako, na kwa kadiri uishivyo katika Roho, na kuenenda katika Roho, na kuufungua ukamilifu wa asili yako kwake, utajiona wewe mwenyewe unakuwa chumba chake cha Uwepo, kilichoangazwa kwa nuru ya utukufu wake. Nawe utambuapo ya kuwa yeye yumo ndani yako, utatambua ya kuwa wewe u ndani yake daima. Ndivyo Mtume mpendwa alivyoandika, "Katika hili twajua ya kuwa twakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa sababu ametupa katika Roho wake."
"Haya yote nayajua, na bado nashindwa kulitambua tukio hili la ajabu la kukaa kwa Roho ndani yangu; nitawezaje basi kutambua kukaa kwangu ndani yake?"
Ni kwa sababu maisha yako yana haraka mno. Hutwai muda wa kutosha kwa kutafakari na kuomba. Roho wa Mungu aliye ndani yako na Uwepo wa Mungu ulio nje yako haviwezi kutambulikana wakati hisia zimeshughulishwa na anasa, au mapigo ya moyo yaendapo upesi, au ubongo umejaa mwendo wa fikira nyingi zenye haraka. Ni maji yasimamapo ndipo huwa mangavu, na kuufunua ufuo wenye vijiwe ulio chini. Tulieni, mjue ya kuwa Mungu yumo ndani yako na kando yako! Katika utulivu wa nafsi kisichoonekana huonekana, na kile cha milele huwa halisi. Jicho lililopofushwa na jua haliwezi kuutambua uzuri wa hema lake hata litakapokuwa na muda wa kujiondolea ule mng'ao. Isipite siku yo yote pasipo kipindi chake cha kungoja kimya mbele za Mungu.
"Je, kuna masharti mengine yo yote nipasayo kuyatimiza, ili nipate kukaa katika siri ya Uwepo wake?"
Uwe safi wa moyo. Kila dhambi iruhusiwayo hufunika madirisha ya nafsi kwa matabaka mazito zaidi ya uchafu, ikififisha kuona kwa Mungu. Lakini kila kushinda juu ya unajisi na ubinafsi huyafanya macho ya kiroho kuwa mangavu, na hapo huanguka machoni, kama vile, magamba. Kwa nguvu za Roho Mtakatifu jikane nafsi, usiipe dhambi nafasi, mpinge Ibilisi, nawe utamwona Mungu.
Nafsi isiyo takatifu isingeweza kumwona Mungu ijapokuwa ingewekwa katikati ya mbingu. Lakini nafsi takatifu humwona Mungu katikati ya mambo ya kawaida ya dunia, na kila mahali huona maono yaliyo wazi. Hao wasingeweza kuwa karibu zaidi na Mungu ijapokuwa wangesimama kando ya bahari ile ya kioo. Faida yao pekee huko ingekuwa ya kuwa pazia la asili yao ya kufa na yenye dhambi likiisha kupasuliwa, maono yangekuwa ya moja kwa moja zaidi na makamilifu zaidi.
Zishike amri zake. Isiwepo hata nukta moja au herufi ndogo isiyotambulikana na isiyoshikwa. Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Musa mtumishi mwaminifu alikuwa pia mwonaji, na alinena na Mungu uso kwa uso kama mtu anenavyo na rafiki yake.
Dumu katika roho ya maombi. Nyakati nyingine maono yatakawia ili kuijaribu bidii na uthabiti wa shauku yako. Nyakati nyingine yatakuja kama mapambazuko yanavyoingia taratibu angani, na, kabla hujatambua, utajiona ukijua ya kuwa yeye yu karibu. Alikuwa na desturi ya kuingia, bila kutangazwa, katikati ya wanafunzi wake kupitia milango isiyofunguliwa. "Nyayo zako hazikujulikana."
Nyakati kama hizo twaweza kusema kwa kweli pamoja na Mtakatifu Bernard: "Hakuingia kwa macho, kwa maana uwepo wake haukuwa na alama ya rangi; wala kwa masikio, kwa maana hapakuwa na sauti; wala kwa pumzi, kwa maana hakuchanganyika na hewa; wala kwa kugusa, kwa maana hakushikika. Basi wauliza, nilijuaje ya kuwa alikuwapo. Ni kwa sababu alikuwa nguvu ihuishayo. Mara alipoingia, aliiamsha nafsi yangu iliyokuwa usingizini. Aligusa na kuuchoma moyo wangu, uliokuwa kwanza mgeni, wa jiwe, mgumu na wenye ugonjwa, hata nafsi yangu ikaweza kumhimidi Bwana, na vyote vilivyo ndani yangu vikalisifu Jina lake Takatifu."
Sitawisha desturi ya kusema na Mungu kwa sauti. Si kila mara labda, kwa sababu shauku zetu mara nyingi ni takatifu mno au za ndani mno kutiwa katika maneno. Lakini ni vyema kupata desturi ya kusema na Mungu kama na rafiki aliyepo hali ukiwa umeketi nyumbani au ukitembea njiani. Tafuta desturi ya kuzungumza mambo pamoja na Mungu -- barua zako, mipango yako, matumaini yako, makosa yako, huzuni zako na dhambi zako. Mambo huonekana kwa jinsi tofauti sana yanapoletwa katika nuru tulivu ya uwepo wake. Mtu hawezi kusema na Mungu kwa sauti kwa muda mrefu pasipo kuhisi ya kuwa yu karibu.
Ulitafakari sana neno. Hii ndiyo bustani ambamo Bwana Mungu hutembea, hekalu akaalimo, chumba cha uwepo ashikilimo baraza yake, naye hupatikana na wale wamtafutao. Ni kwa njia ya neno tulishwapo kwa Neno. Naye alisema, "Aulaye mwili wangu, na kuinywa damu yangu, hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake."
Uwe na bidii katika kazi ya Kikristo. Mahali pa maombi ni kweli mahali pa uwepo wake udhihirishwao, lakini uwepo huo ungefifia kutoka hapo kama tungebaki hapo baada ya kengele ya wajibu kuisha kutuita sisi tulioko chini. Sikuzote tutaukuta tuendapo katika kazi yetu ya lazima: "Wakutana naye afanyaye haki kwa furaha." Twendapo katika kazi zetu za kila siku malaika wa uwepo wake huja kutusalimu, na kugeuka aende kando yetu. "Enendeni," alisema Bwana; "Tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote." Si katika nyua za hekalu tu, wala katika mabonde yaliyotengwa, wala katika vyumba vya wagonjwa, bali katika mzunguko wa wajibu wa kila siku, katika mambo ya kawaida ya maisha, juu ya nchi tambarare zisizo na uhai za kuwako, twaweza kuwa daima katika siri ya uwepo wake, nasi tutaweza kusema pamoja na Eliya mbele ya Ahabu, na Gabrieli kwa Zekaria, "Nasimama mbele za Mungu " (1 Wafalme 17:1; Luka 1:19).
Sitawisha desturi ya kuutambua Uwepo wa Mungu."Heri mtu umchaguaye, na kumkaribisha kwako, apate kukaa nyuani mwako." Hakuna maisha kama haya. Kuhisi ya kuwa Mungu yu pamoja nasi; ya kuwa hatuongozi kamwe kupitia mahali palipo pembamba mno asiweze kupita naye pia; ya kuwa hatuwezi kamwe kuwa peke yetu tena, hata kwa dakika moja; ya kuwa ametuzunguka nyuma na mbele, na kutufunika kwa mkono wake; ya kuwa asingeweza kuwa karibu zaidi nasi, hata kama tungekuwa mbinguni kwenyewe. Kumpata yeye kuwa Rafiki, na Mwamuzi, na Mshauri, na Kiongozi. Kutambua ya kuwa hapatakuwapo kamwe Yeriko katika maisha yetu pasipo uwepo wa Jemadari wa jeshi la Bwana, pamoja na majeshi yale yasiyoonekana lakini yenye nguvu, ambayo mbele ya shambulio lao kuta zote sharti zianguke. Si ajabu ya kuwa watakatifu wa kale walipata ushujaa vitani waliposikia akisema, "Mimi nipo pamoja nawe; sitakupungukia kamwe wala sitakuacha."
Ondokeni hofu na huzuni na kicho cha bonde la giza! "Utanificha katika siri ya uwepo wako mbali na fahari ya mwanadamu; utanihifadhi kwa siri katika hema mbali na magombano ya ndimi."
Sura ya 8 imekamilika
Katika Siri ya Uwepo Wake