Siri ya Uongozi
Siri ya Kukaa kwa Kristo Ndani

Sura 3 · dakika 13 za kusoma

Siri ya Kukaa kwa Kristo Ndani

Yafaa kwamba kanisa kubwa kuliko yote katika mji mkuu wa Mataifa duniani liwekwe wakfu kwa mtume Paulo, kwa maana Mataifa wana deni kubwa kwake kama Mtume wa Mataifa. Ni kwake, chini ya Roho wa Mungu, tunadaiwa kufunuliwa kwa siri mbili kuu, zinazotugusa hasa sisi tulio wa Mataifa.

Ya kwanza kati ya hizi, ijapokuwa ni tukufu, hatuwezi sasa kukaa tuiongelee, ingawa ilileta mageuzi makuu ilipohubiriwa na kutetewa kwanza na Mtume mbele ya upinzani mkali kuliko yote. Hata wakati huo, Mataifa walitazamiwa kuwa Wayahudi kwanza kabla ya kuwa Wakristo, na kupitia sinagogi ili kufikia kanisa. Lakini yeye alionyesha kwamba hili halikuwa la lazima, na kwamba Mataifa walisimama sawasawa na Wayahudi kuhusu baraka za injili ‑‑ warithi pamoja, na viungo pamoja vya mwili, na washiriki pamoja wa ahadi katika Kristo Yesu kwa njia ya injili (Waefeso 3:6).

Ya pili, hata hivyo, yastahili sana kutafakariwa zaidi na sisi, kwa maana laiti tu ingetambuliwa na watoto wa Mungu, wangeanza kuishi kwa namna ya Kimungu hata kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi, na kurudia kwa kiasi kidogo maisha ya Yesu hapa duniani.

Siri hii ni kwamba Bwana Yesu yu radhi kukaa ndani ya moyo wa mtu wa Mataifa. Kwamba akae ndani ya moyo wa mtoto wa Ibrahimu ilihesabiwa kuwa tendo la ajabu la kujishusha; lakini kwamba apate makao ndani ya moyo wa mtu wa Mataifa haikusadikika. Lakini kosa hili liliondolewa mbele ya ufunuo wa kung'aa wa kweli aliopewa yule ambaye, kwa hukumu yake mwenyewe, hakustahili kuitwa Mtume, kwa sababu alikuwa amelitesa Kanisa la Mungu. Mungu aliona vema kudhihirisha kwa kupitia yeye "utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa; ndio KRISTO NDANI YENU, tumaini la utukufu" (Wakolosai 1:27).

"Rabi, unakaa wapi?" waliuliza zamani. Naye Yesu, kwa kujibu, aliwaongoza kutoka ukingo wa Yordani uliojaa watu hata kwenye hema dhaifu la matawi yaliyofumwa ambamo alikaa kwa muda. Lakini kama tukimwuliza swali hilo hilo sasa, hataonyesha kuba refu na tukufu la mbinguni, wala jengo zuri la mawe au marumaru, bali roho yenye furaha ipendayo, itumainiyo, na kumtii yeye. "Tazama," asema, " nasimama mlangoni, nabisha. Mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake." "Tutakuja," alisema, akijumlisha Baba yake pamoja naye, "na kufanya makao yetu kwake." Aliahidi kuwa ndani ya kila muumini kama mpangaji ndani ya nyumba; kama utomvu ndani ya tawi; kama damu ya uhai na nguvu ya uhai katika kila kiungo cha mwili, kijapokuwa dhaifu namna gani.

I. ‑‑ SIRI ILE.

Kristo yumo ndani ya muumini. Anakaa moyoni kwa imani, kama vile jua likaavyo ndani ya maua madogo kabisa yanayokunjua petali zake na kufunua mioyo yake mbele ya miale yake. Si kwa sababu tu wema. Si kwa sababu tunajaribu kuwa na moyo mkamilifu katika kujitoa kwetu. Si kwa sababu tunamshika kwa uthabiti wa upendo wetu. Bali kwa sababu tunaamini, na katika kuamini, tumeifungua milango na madirisha yote ya utu wetu. Naye ameingia.

Yamkini aliingia kwa utulivu hata tukashindwa kutambua kuingia kwake. Hapakuwa na mshindo wa hatua njiani. Mlio wa njuga za dhahabu chini ya vazi lake la ukuhani haukumsaliti. Aliingia taratibu juu ya mbawa za asubuhi, au kama vile ukimya ambao kwao maumbile huamka kutoka usingizi wake wa majira ya baridi na kujivika mavazi ambayo Muumba wake ameyaandaa kwa ajili yake. Lakini hii ndiyo njia ya Kristo. Hagombani, wala hapazi sauti, wala haifanyi sauti yake isikike njiani. Mwendo wake ni mwepesi hata haukanyagi kuvunja mwanzi uliopondeka, pumzi yake ni laini hata yaweza kuwasha tena cheche zinazozimika. Basi usishangae kama huwezi kutaja siku au saa ambayo Mwana wa Adamu alikuja kukaa ndani yako. Ujue tu ya kuwa amekuja. "Je! hamjijui nafsi zenu, kwamba Yesu Kristo yumo ndani yenu? Isipokuwa mmekataliwa." (2 Wakorintho 13:5.)

Ni jambo la ajabu sana. Naam; mbingu, naam mbingu za mbinguni, pamoja na nuru na utukufu wake wote, peke yake zaonekana kumstahili. Lakini hata huko hakai kwa raha zaidi kuliko akaavyo pamoja na roho iliyonyenyekea na kupondeka itumainiayo kwake tu. Katika maisha yake ya duniani, alisema kwamba Baba alikaa ndani yake kwa uhalisia hata maneno aliyoyanena na kazi alizozifanya hazikuwa zake mwenyewe, bali za Baba yake. Naye anatamani kuwa ndani yetu kama Baba yake alivyokuwa ndani yake, ili matoke ya maisha yetu yawe mifereji ambayo kwayo yeye, aliyefichwa ndani, aweze kujimwaga juu ya wanadamu.

Kwa kawaida haitambuliwi. Sivyo; ijapokuwa hilo halibatilishi ukweli wake. Twashindwa kutambua mambo mengi ndani yetu na katika maumbile yanayotuzunguka, ambayo hata hivyo ni kweli. Lakini kuna sababu inayowafanya wengi ambao utu wao hakika ni hekalu la Kristo, wabaki bila kujua uwepo wa yule Mpangaji wa ajabu akaaye ndani. Anakaa ndani sana. Chini ya uhai wa mwili, ulio kama pazia la hema; chini ya uhai wa nafsi, ambako mawazo na hisia, hukumu na fikira, tumaini na upendo, huenda huku na huko, wakihudumu kama makuhani waliovaa mavazi meupe katika mahali patakatifu; chini ya mchezo wa nuru na kivuli, azimio na nia, kumbukumbu na tumaini, kule kupwa na kujaa kusikokoma kwa mawimbi ya kujitambua, hapo, kwa njia ya Roho Mtakatifu Kristo anakaa, kama vile zamani Shekina ilivyokaa katika Patakatifu pa Patakatifu, akiwa amefunikwa sana asionekane na mwanadamu.

Ni mara chache kiasi tunapoingia katika sehemu hizi za ndani zaidi za nafsi zetu. Twaridhika kuishi maisha ya juujuu ya hisia. Twala, twanywa, twalala. Twajitoa tuzifurahie tamaa za mwili, tamaa za macho, na majivuno ya maisha. Twatimiza haja za mwili na za akili. Au twajitupa katika kufuatia maarifa na utamaduni, sayansi na sanaa. Twaingia kidogo tu katika ulimwengu wa maadili, ile hisia ya haki na batili iliyo sehemu ya maumbile ya wanadamu. Lakini tuna ujuzi mdogo mno wa kile chumba cha ndani zaidi na chenye siri zaidi cha roho. Basi hii ndiyo sababu wengi wa waaminio hawamhisi hata kidogo yule Mkazi wao wa Kimungu na wa ajabu, ambaye huifanya roho iliyozaliwa upya kuwa makao yake.

Yapasa kupokelewa kwa imani. Hapa twarudia kosa letu la kawaida kuhusu mambo ya Mungu. Twajaribu kuyahisi. Tukiyahisi, twayaamini; kama sivyo hatuyahesabu kuwa kitu. Twaugeuza mpango wa Kimungu. Twasema, hisia, IMANI, UHAKIKA. Mungu husema UHAKIKA, IMANI, hisia. Kwake hisia ni jambo dogo ‑‑ yeye hutuomba tu tuwe radhi kulipokea Neno lake mwenyewe, na kulishika kwa sababu yeye amelinena, bila kujali hata kidogo tunayoyahisi.

Naambiwa waziwazi kwamba Kristo, ijapokuwa yuko juu ya Kiti cha Enzi katika utukufu wake wa kupaa, yumo pia ndani yangu kwa Roho Mtakatifu. Nakiri sikumhisi humo. Mara nyingi katikati ya shambulio la jaribu au ukali wa dhoruba ipitayo juu ya uso wa nafsi yangu, siwezi kuutambua umbo lake wala kumsikia akisema, "Ni mimi." Lakini nathubutu kuamini kwamba yuko humo; si nje yangu, bali ndani; si kama mgeni apitaye kwa usiku mmoja, bali kama mkazi wa daima; si aliyebadilishwa na mageuzi yangu kutoka bidii hata ulegevu, kutoka kiangazi cha upendo hata baridi ya kukata tamaa, bali sikuzote asiyebadilika ni yeye yule. Nami nasema tena na tena, "Yesu, wewe upo hapa. Sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini umekuja. Jidhihirishe. Ushushe kila utawala, na mamlaka, na nguvu. Toka katika chumba chako cha siri, na umiliki yote yaliyo ndani yangu, ili yalibariki jina lako takatifu."

Katerina wa Siena wakati mmoja alitumia siku tatu katika mafungo ya faraghani, akiomba apate utimilifu na furaha kubwa zaidi ya uwepo wa Kimungu. Badala yake, ilionekana kana kwamba majeshi ya pepo wabaya walimshambulia kwa mawazo ya kufuru na mashawishi maovu. Mwishowe, nuru kuu ilionekana ikishuka kutoka juu. Mashetani wakakimbia, naye Bwana Yesu akazungumza naye. Katerina akamwuliza:

"Bwana, ulikuwa wapi moyo wangu ulipoteswa hivyo?"

"Nilikuwa moyoni mwako," akajibu.

"Bwana, wewe ni kweli ya milele," akajibu, "nami nainama kwa unyenyekevu mbele ya neno lako; lakini nawezaje kuamini kwamba ulikuwa moyoni mwangu ulipojaa mawazo ya kuchukiza namna hiyo?"

"Je, mawazo hayo yalikupa furaha au uchungu?" akauliza.

"Uchungu na huzuni kupita kiasi," ndilo jibu lake.

Ndipo Bwana akamwambia, "Ulikuwa katika taabu na huzuni kwa sababu mimi nilikuwa katikati ya moyo wako. Ni uwepo wangu uliokufanya mawazo hayo yasivumilike kwako. Kipindi nilichokuwa nimeamua kwa muda wa vita hivyo kilipokwisha, nilipeleka miale ya nuru yangu, na vivuli vya kuzimu vikaondolewa, kwa sababu haviwezi kustahimili nuru ile."

II. ‑‑ UTUKUFU WA SIRI HII.

Siri za Mungu zifunukapo, hufanya hivyo katika utukufu. Utajiri wa mzizi uliofichwa ardhini hufunuliwa katika rangi za okidi au harufu ya waridi. Uzuri uliofichika wa mwale wa nuru hufumbuliwa katika rangi saba za upinde wa mvua. Uhai mwingi, mdogo usioonekana wa bahari za kusini hulipuka kuwa mawimbi yang'aayo unapopasuliwa na tako la meli. Na kila mara ulimwengu usioonekana ulipojidhihirisha mbele ya macho ya wanadamu, umekuwa katika utukufu. Ilikuwa hivyo hasa katika Kugeuka Sura, wakati asili ya Bwana ilipopasuka kutoka kizuizi kikali alichokuwa ameifungia ndani yake na kujidhihirisha mbele ya jicho la mwanadamu. "Uso wake ukang'aa kama jua, na mavazi yake yakawa meupe kama nuru."

Basi tunapokubali uhakika wa kuwepo kwake ndani yetu, ndani zaidi kuliko sisi wenyewe, na kukifanya kuwa mojawapo ya makusudi ya maisha yetu kutumia na kukikuza, tutakuwa na hisia ya utukufu ukiyageuza maisha yetu na kuyang'arisha mambo ya kawaida, hata kuifanya dunia, pamoja na shughuli zake za kawaida kabisa, kuwa kama ukumbi wa mbinguni.

Mke wa Jonathan Edwards alikuwa amepitia mabadiliko makubwa katika uzoefu wa dini na huzuni ya mara kwa mara, hata alipofikia hatua ya kuukana ulimwengu, na kujitoa amilikiwe na kweli hizi zenye nguvu. Lakini mara tu hilo lilipotokea, mabadiliko ya ajabu yalifanyika. Alianza kupata pumziko la daima lisilokatika; amani tamu na utulivu wa nafsi; kufurahi bila kukoma katika kazi zote za mikono ya Mungu, ziwe za maumbile au za utunzaji wa kila siku; kumfikia Mungu kwa njia ya ajabu kwa maombi, kana kwamba anamwona na kuzungumza naye papo hapo; machozi yote yakafutwa; taabu zote za kwanza na huzuni za maisha zikasahauliwa, isipokuwa masikitiko kwa ajili ya dhambi zilizopita na kwa aibu iliyofanywa kwa Kristo duniani; kutenda na kuteseka kila kitu kwa ajili ya Mungu kila siku kwa hisia, na kufanya yote kwa uchangamfu, amani na furaha isiyokatika.

Utukufu wa namna hii ‑‑ ahadi ya hakika ya utukufu utakaofunuliwa ‑‑ u karibu na kila msomaji wa maneno haya atakayethubutu siku kwa siku kuhesabu kwamba Kristo anaishi ndani, naye atakuwa radhi kuzifia nguvu na misukumo ya maisha ya nafsi ili pawe na nafasi kwa maisha ya Kristo kujidhihirisha. "Nimesulubiwa pamoja na Kristo," alisema mwalimu mkuu kuliko wote wa binadamu wa sanaa hii ya Kimungu; "Kristo anaishi ndani yangu; ninaishi kwa imani katika Mwana wa Mungu."

III. ‑‑ UTAJIRI WA UTUKUFU WA SIRI HII.

Siri hii au fumbo la maisha ya Kimungu ndani ya mwanadamu linapoeleweka na kutumiwa, huyapa maisha utajiri mkubwa. Ikiwa hazina zote za hekima, maarifa, nguvu, na neema zinakaa ndani ya Yesu, naye amekuwa mkazi mpendwa na mwenye kuheshimiwa wa utu wetu, ni dhahiri kwamba nasi lazima tutajirishwe sana. Ni kama mtu maskini akiwa na rafiki tajiri wa mamilioni anayekuja kuishi naye.

Kuna utajiri wa saburi. Maisha si rahisi kwa yeyote kati yetu. Hakuna tawi liepukalo kisu cha kupogoa; hakuna kito kiepukalo gurudumu; hakuna mtoto aepukaye fimbo. Watu hututawala kikatili na kutuudhi kiasi cha kukaribia kutoweza kuvumilika. Mazingira hutuvuta hata nyuzi za mioyo yetu zikakaribia kukatika. Mfumo wetu wa mishipa unaelemewa mno na haraka na ushindani wa nyakati zetu. Kweli, tuna haja ya saburi!

Kutolegeza kamwe kujilinda; kutojiingiza kamwe katika kuwakosoa wengine kwa ukatili au bila kufikiri; kutonena kamwe neno la haraka, wala kuruhusu jibu kali; kutolalamika kamwe isipokuwa kwa Mungu; kutoruhusu kamwe mawazo magumu na yenye shaka yakae ndani ya nafsi; kuwafikiria wengine sikuzote zaidi ya nafsi; kukiona kile kipande kimoja cha buluu katika anga lililotanda mawingu; kuwa macho ili kupata udhuru kwa wale walio wakaidi na wagumu, kuvumilia maumivu na uchungu, mahitaji na majaribu ya maisha, kwa utamu, kwa unyenyekevu, kwa kutumaini; kukinywa kikombe kichungu, jicho likikaza kwenye uso wa Baba, bila kunung'unika wala kulalamika: ‑‑ hili lahitaji saburi, ambayo ustahimilivu wa kibinadamu tu usingeweza kamwe kuitoa.

Nasi hatuwezi kuishi maisha ya namna hiyo hata tutakapokuwa tumejifunza kujitumbukiza katika utajiri wa Kristo akaaye ndani. Mtume mpendwa asema juu ya kuwa mshiriki wa saburi iliyo katika Yesu (Ufunuo 1:9). Nasi na tuwe hivyo. Saburi ile ya utulivu, isiyonung'unika, isiyolaumu, iliyomfanya Mwana-Kondoo wa Mungu kuwa bubu mbele ya wakatao manyoya yake, ni yetu.

Robert Hall wakati mmoja alisikika akisema katikati ya joto la mabishano, "Nituliza, Ee Mwana-Kondoo wa Mungu!"

Lakini twaweza kwenda mbali zaidi na kusema, "Bwana Yesu, saburi yako na iinuke ndani yangu, kama chemchemi ya maji matamu katika bahari ya chumvi."

Kuna utajiri wa neema. Peke yake miongoni mwa miji mikuu ya ulimwengu, Yerusalemu haukuwa na mto. Lakini Bwana mtukufu alikuwa katikati yake, naye akawa mahali pa mito mipana na vijito, akitoa kutoka kwake mwenyewe yote ambayo mito iliipa miji, ambayo chini ya kuta zake maji ya kukaribishwa yaligusa (Isaya 32:21).

Hii ni taswira ya kile tulicho nacho, sisi tuthubutuo kutegemea kukaa kwa Bwana wetu mtukufu ndani, akiwa Mfalme, Mtoa-Sheria, na Mwokozi. Yeye huifanya neema yote iwe tele kwetu, hata tuwe na utoshelevu kwa mambo yote ya dharura, na tuweze kuzidi katika kila tendo jema. Katika nguvu zake, ziinukazo daima ndani yetu, twaweza kufanya kama wafanyavyo wale waliojaliwa vipawa vikuu vya akili na maumbile, nasi twaepuka majaribu ya kujitukuza bure na kiburi ambavyo wao wanazingirwa navyo.

Neema ya usafi na kujizuia, ya maombi ya bidii na ufahamu wa Maandiko, ya kuwapenda watu na kumwonea Mungu wivu, ya unyenyekevu na upole, ya utuwa na wema ‑‑ yote yamo ndani ya Kristo; na kama Kristo yumo ndani yetu, yote ni yetu pia. Laiti tungethubutu kuliamini hilo, na kulitumia, tukishusha ndoo ya imani ndani ya kisima kirefu cha kukaa kwa Kristo, kilichofunguliwa ndani yetu na Roho Mtakatifu!

Haiwezekani, katika mipaka hii mifupi, kulifafanua zaidi wazo hili la ajabu. Lakini laiti tungekutana na kila wito, shida, na jaribu, bila kusema, kama tufanyavyo mara nyingi, "Sitaweza kamwe kupita katika hili," bali tukisema, "Mimi siwezi; lakini Kristo yumo ndani yangu, naye aweza," tungeona kwamba majaribu yote yalikusudiwa kudhihirisha na kufunua utajiri uliofichwa ndani yetu, hata Kristo aumbwe kwa halisi ndani yetu, na maisha yake yadhihirishwe katika mwili wetu wa kufa (2 Wakorintho 4:10).

(1) Tulia kila siku kwa muda mfupi, ukiwa umeketi mbele za Mungu katika kutafakari, na umwombe Roho Mtakatifu akufunulie kweli ya kukaa kwa Kristo ndani. Mwombe Mungu aone vema kukujulisha utajiri wa utukufu wa siri hii ni nini (Wakolosai 1:27).

(2) Uheshimu utu wako kama hekalu la Bwana akaaye ndani. Kama vile mtu wa Mashariki avuavyo viatu vyake, na wa Magharibi aondoavyo kofia yake, aingiapo katika mazingira ya hekalu, vivyo hivyo uwe mwangalifu sana na chochote kitakachounajisi mwili au kuichafua nafsi. Wanyama wasilishe katika nyua za hekalu. Mwache Kristo awafukuze nje. "Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu? Hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi."

(3) Uichukie nafsi yako mwenyewe. "Mtu ye yote asipoichukia nafsi yake mwenyewe," alisema Bwana wetu, "hawezi kuwa mwanafunzi wangu" (Luka 4:26). Na neno lililotafsiriwa "maisha" ni nafsi, makao na kitovu cha maisha ya nafsi pamoja na nguvu na shughuli zake zisizotulia, uchaguzi na maamuzi yake, jitihada zake zisizokoma za kutaka kujitegemea na kuongoza. Hiki ndicho kizuizi kikuu kuliko vyote cha kuufurahia kwetu Kristo akaaye ndani. Tukipata tabia ya kusema "Hapana," si tu kwa nafsi yetu mbaya bali hata nafsi yetu njema; tukijitoa kila siku hata mautini kwa ajili ya Yesu; tukiuchukua msalaba wetu na kumfuata Bwana, ijapokuwa ni hata kaburini kwake, tutazidi kuwa na hisia ya kumilikiwa na maisha yaliyo tajiri zaidi, ya ndani zaidi, na ya Kimungu zaidi kuliko yetu wenyewe.

Sura ya 3 imekamilika

Siri ya Kukaa kwa Kristo Ndani

Ukurasa 1 / 1 · 13 dakika zimebaki katika sura