Ukaaji wa Bwana Ndani Yetu ·Unyenyekevu wa Kristo — Wokovu Wetu

Sura 7 · dakika 13 za kusoma

Unyenyekevu wa Kristo — Wokovu Wetu

Wafilipi 2:5-8.—“Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; a ambaye, ingawa alikuwa na umbo la Mungu, hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; b bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa umbo la mtumwa, c akawa ana mfano wa wanadamu. Naye alipoonekana ana umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza, akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

Wote tunaifahamu fungu hili la ajabu. Paulo anazungumza juu ya mojawapo ya mambo rahisi na ya kimatendo kabisa katika maisha ya kila siku—unyenyekevu; na kwa kuhusiana na hilo, anatuonyesha ufunuo wa ajabu wa kweli ya Mungu. Katika sura hii, tunaona Uungu wa milele wa Yesu. Alikuwa na umbo la Mungu, naye ni mmoja na Mungu. Tunaona kufanyika kwake mwili. Alishuka chini na akaonekana ana mfano wa mwanadamu. Tunaona kifo chake pamoja na upatanisho—akawa mtii hata mauti. Tunaona kutukuzwa kwake—Mungu amemtukuza sana. Tunaona utukufu wa Ufalme wake—kwamba kila goti litapigwa, na kila ulimi utamkiri. Na katika kuhusiana na nini? Je, ni somo la theolojia? Hapana. Je, ni maelezo ya Kristo ni nani? Hapana; ni kwa kuhusiana na wito rahisi na ulio wazi wa maisha ya unyenyekevu katika mahusiano yetu sisi kwa sisi.

Maisha yetu hapa duniani yameunganishwa na utukufu wote wa milele wa Uungu kama ulivyofunuliwa katika kutukuzwa kwa Yesu. Kule kumtazama Yesu, kule kumpigia Yesu goti, kunapaswa kuunganishwa kwa namna isiyoweza kutenganishwa na roho ya unyenyekevu ulio wa ndani kabisa. Fikiri juu ya unyenyekevu wa Yesu. Kwanza kabisa, unyenyekevu huo ni wokovu wetu; kisha, unyenyekevu huo ndio hasa wokovu tunaouhitaji; na tena, unyenyekevu huo ni wokovu ambao Roho Mtakatifu atatupatia.

Unyenyekevu ndio wokovu ambao Kristo anauleta. Hilo ndilo wazo letu la kwanza. Mara nyingi tunayo mawazo hafifu—naweza pia kusema ya kuwaza tu—juu ya Kristo ni nani; tunampenda nafsi ya Kristo, lakini kile kinachomfanya Kristo, kinachomfanya kuwa Kristo hasa, hicho hatukijui wala hatukipendi. Ikiwa tunampenda Kristo kuliko yote, ni lazima tuupende unyenyekevu kuliko yote, kwa maana unyenyekevu ndio asili hasa ya uzima wake na utukufu wake, na ndio wokovu anaouleta. Fikiri tu juu ya jambo hili. Ulianzia wapi? Je, kuna unyenyekevu mbinguni? Wajua ipo, kwa maana wanazitupa taji zao mbele ya kiti cha enzi cha Mungu na Mwana-Kondoo. Lakini je, kuna unyenyekevu juu ya kiti cha enzi cha Mungu? Ndiyo, ni nini kingine ila unyenyekevu wa mbinguni uliomfanya Yesu, akiwa juu ya kiti cha enzi, awe radhi kusema: “Nitashuka chini niwe mtumwa, na kufa kwa ajili ya mwanadamu; nitakwenda kuishi kama Mwana-Kondoo wa Mungu mpole na mnyenyekevu?”

Yesu alituletea unyenyekevu kutoka mbinguni. Ni unyenyekevu ndio uliomleta duniani, ama asingekuja kamwe. Kwa kufuata jambo hili, kama vile Kristo alivyofanyika mwanadamu katika unyenyekevu huu wa kimungu, ndivyo maisha yake yote yalivyoonyeshwa nao. Angeweza kuchagua umbo lingine la kujitokeza; angeweza kuja katika umbo la mfalme, lakini alichagua umbo la mtumwa. Alijifanya kuwa hana utukufu; alijifanya kuwa si kitu; alichagua umbo la mtumwa. Alisema: “Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mathayo 20:28. Nanyi mwajua, katika usiku ule wa mwisho, alitwaa nafasi ya mtumwa akajifunga taulo, akaenda kuwaosha miguu Petro na wanafunzi wengine.

Wapendwa, maisha ya Yesu hapa duniani yalikuwa maisha ya unyenyekevu ulio wa ndani kabisa. Ni jambo hili lililoyapa maisha yake thamani na uzuri wake mbele za Mungu. Kisha kifo chake—labda hamjakifikiria sana kwa kuhusiana na jambo hili—lakini kifo chake kilikuwa dhihirisho la unyenyekevu usio na kifani.

Katika waraka wake kwa Wafilipi, Paulo anataja jinsi Yesu Kristo alivyojinyenyekeza, akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Bwana wangu Kristo alitwaa nafasi ya chini wakati wote wa kutembea kwake hapa duniani; alitwaa nafasi ya chini sana alipoanza kuwaosha miguu wanafunzi; lakini alipokwenda Kalvari, alitwaa nafasi iliyo chini kuliko zote iliyoweza kupatikana katika ulimwengu wote wa Mungu, ile ya chini kabisa, naye akaacha dhambi, na laana ya dhambi, na ghadhabu ya Mungu, vimfunike. Alitwaa nafasi ya mwenye dhambi mwenye hatia, ili apate kubeba mzigo wetu, ili apate kututumikia kwa kutuokoa kutoka katika taabu yetu, ili apate kwa damu yake ya thamani kutupatia ukombozi, ili apate kwa damu ile kutuosha uchafu wetu na hatia yetu.

Tuko katika hatari ya kumfikiria Kristo, kama Mungu, kama mwanadamu, kama upatanisho, kama Mwokozi, na kama aliyetukuzwa juu ya kiti cha enzi, nasi twaunda sanamu ya Kristo, huku Kristo wa kweli, kile kilicho moyo hasa wa tabia yake, kikibaki hakijulikani. Kristo wa kweli ni nani? Ni unyenyekevu wa kimungu uliojinyenyekeza hata katika vilindi vya ndani kabisa kwa ajili ya wokovu wetu.

Unyenyekevu wa Yesu ni wokovu wetu. Twasoma, “Alijinyenyekeza… kwa hiyo Mungu amemtukuza sana.” Wafilipi 2:8-9. Siri ya kutukuzwa kwake hata kiti cha enzi ni hii: alijinyenyekeza mbele za Mungu na mwanadamu. Unyenyekevu ndiye Kristo wa Mungu, na sasa mbinguni, leo, Kristo yule, Mtu wa unyenyekevu, yuko juu ya kiti cha enzi cha Mungu. Naona nini? Naona Mwana-Kondoo amesimama, kana kwamba amechinjwa, juu ya kiti cha enzi; katika utukufu, bado ni yeye Mwana-Kondoo wa Mungu aliye mpole na mwenye upole. Unyenyekevu wake ndio alama anayoivaa huko. Mara nyingi mwatumia jina hilo—Mwana-Kondoo wa Mungu—nanyi mwalitumia kwa kuhusiana na damu ya dhabihu. Mwaimba sifa za Mwana-Kondoo, nanyi mwaweka tumaini lenu katika damu ya Mwana-Kondoo. Msifuni Mungu kwa ajili ya damu. Kamwe hamwezi kuitumainia kupita kiasi. Lakini nachelea kwamba mwasahau ya kuwa neno “Mwana-Kondoo” lapasa kumaanisha kwetu mambo mawili: lapasa kumaanisha si dhabihu tu, kumwaga damu, bali lapasa kumaanisha kwetu upole wa Mungu, aliyefanyika mwili duniani, upole wa Mungu ulioonyeshwa katika upole na wema wa Mwana-Kondoo mdogo. Lakini wokovu ambao Kristo aliuleta si wokovu utokao katika unyenyekevu tu; bali pia waongoza kwenye unyenyekevu. Ni lazima tuelewe kwamba huu si wokovu ambao Kristo aliuleta tu, bali ndio hasa wokovu ambao wewe na mimi tunauhitaji.

Ni nini chanzo cha taabu yote ya mwanadamu? Hasa ni kiburi; mwanadamu akitafuta mapenzi yake mwenyewe na utukufu wake mwenyewe.

Ndiyo, kiburi ndilo shina la kila dhambi, na hivyo Mwana-Kondoo wa Mungu huja kwetu katika kiburi chetu na kutuletea wokovu kutoka humo. Zaidi ya yote twahitaji kuokolewa kutoka katika kiburi chetu na hiari yetu wenyewe. Ni vyema kuokolewa kutoka katika dhambi za kuiba, kuua, na kila uovu mwingine; lakini mwanadamu, zaidi ya yote, ahitaji kuokolewa kutoka katika kile kilicho shina la dhambi zote, yaani hiari yake mwenyewe, na kiburi chake. Si hata mwanadamu aanzapo kuhisi kwamba huu ndio hasa wokovu anaouhitaji, ndipo aweza kweli kuelewa Kristo ni nani, na aweza kumkubali kuwa wokovu wake. Huu ndio wokovu ambao sisi kama Wakristo na waamini twauhitaji hasa. Twaijua hadithi ya kusikitisha ya Petro na Yohana; na jinsi hiari yao wenyewe na kiburi chao kilivyowaletea mambo. Hawakuhitaji kuokolewa kutoka katika kitu kingine ila nafsi zao wenyewe, na hilo ndilo somo ambalo ni lazima tujifunze tukitaka kuingia katika maisha ya pumziko.

Nasi twawezaje kuingia katika maisha hayo, na kukaa humo kifuani mwa Mwana-Kondoo wa Mungu, ikiwa kiburi kinatawala? Je, hatujasikia mara nyingi malalamiko juu ya kiasi cha kiburi kilichomo katika Kanisa la Kristo? Ni nini chanzo cha mafarakano yote, ugomvi, na wivu ambao mara nyingi hupatikana hata miongoni mwa watakatifu wa Mungu? Kwa nini mara nyingi katika familia kuna uchungu—yaweza kuwa kwa nusu saa tu, au nusu siku; lakini ni nini chanzo cha hukumu kali na maneno ya haraka? Ni nini chanzo cha kutengana kati ya marafiki? Ni nini chanzo cha kusengenyana? Ni nini chanzo cha ubinafsi na kutojali hisia za wengine? Ni hiki tu: kiburi cha mwanadamu. Hujikweza mwenyewe, na kudai haki ya kuwa na maoni na hukumu zake kama apendavyo. Wokovu tunaouhitaji kwa kweli ni unyenyekevu, kwa sababu ni kwa njia ya unyenyekevu peke yake ndipo twaweza kurudishwa katika uhusiano wetu ulio sahihi na Mungu.

“Kumngoja Mungu,”—hilo ndilo tamko pekee la kweli kwa uhusiano halisi wa kiumbe kwa Mungu; kuwa si kitu mbele za Mungu. Wazo la msingi la kiumbe kilichoumbwa na Mungu ni lipi? Ni hili: kuwa chombo ambamo aweza kumimina utimilifu wake, ambamo aweza kudhihirisha uzima wake, wema wake, nguvu zake, na upendo wake. Chombo lazima kiwe tupu kama kitajazwa, na kama tutajazwa uzima wa Mungu ni lazima tuwe tupu kabisa tusiwe na nafsi. Huu ndio utukufu wa Mungu, kwamba yeye ndiye ajazaye vitu vyote, na hasa zaidi watu wake waliokombolewa.

Kama vile huu ulivyo utukufu wa kiumbe, ndivyo huu ulivyo ukombozi pekee, na utukufu pekee wa kila nafsi iliyokombolewa, kuwa tupu na kama si kitu mbele za Mungu; kumngoja yeye, na kumwacha Mungu awe yote katika yote. Unyenyekevu unayo nafasi ya wazi karibu katika kila waraka wa Agano Jipya. Paulo asema: “Enendeni kama inavyostahili wito ule mlioitwa, kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.” Waefeso 4:1-3. Kadiri unavyomkaribia Mungu, na kadiri unavyojaa Mungu, ndivyo utakavyokuwa chini zaidi; na sawasawa mbele za Mungu na mwanadamu, utapenda kuinama chini sana. Twajua kujiamini kwa Petro kwa mapema; lakini katika nyaraka zake analitumia lugha tofauti kabisa! Aliandika humo: “Kadhalika ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jivikeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana.”

1 Petro 5:5. Alielewa, naye alithubutu kuhubiri, unyenyekevu kwa wote. Kwa kweli ndio wokovu tunaouhitaji. Ni nini kinachowazuia watu wasije katika kujisalimisha kikamili kule tunakozungumza? Ni kwamba tu hawathubutu kujiacha wenyewe, na kujitegemeza wenyewe, kwa Mungu; hawako radhi kuwa si kitu, kuyaacha matakwa yao, mapenzi yao, na heshima yao kwa Kristo.

Je, hatutaukubali wokovu ambao Yesu anautoa? Aliyaacha mapenzi yake mwenyewe; aliyaacha heshima yake mwenyewe; aliacha kujiamini kwake mwenyewe; aliishi akimtegemea Mungu kama mtumwa ambaye Baba amemtuma. Huo ndio wokovu tunaouhitaji, Roho ya unyenyekevu iliyokuwamo ndani ya Kristo. Ni nini mara nyingi kinachoisumbua mioyo yetu na amani yetu? Je, si kiburi kikitaka kuwa kitu? Na amri ya Mungu haitanguki, “Mungu huwapinga wenye kiburi, bali huwapa neema wanyenyekevu.” 1 Petro 5:5. Ni mara ngapi Yesu amelazimika kuwaambia wanafunzi wake juu ya jambo hili?

Utayaona tena na tena katika Injili maneno yale rahisi: “Kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” Mathayo 23:12. Aliwafundisha wanafunzi wake: “Bali ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu.” Mathayo 20:26. Hii ndiyo iwe kilio chetu kimoja mbele za Mungu: “Nguvu za Roho Mtakatifu na zinijilie, pamoja na unyenyekevu wa Yesu, ili nipate kutwaa nafasi ile aliyoitwaa yeye.”

Sasa laja wazo la tatu—Huu ndio wokovu ambao Roho Mtakatifu anauleta. Mwajua badiliko lililotokea katika wanafunzi wale. Na tumsifu Mungu kwa ajili yake; Roho Mtakatifu maana yake ni hii: uzima, mwelekeo, tabia, na mielekeo ya Yesu, ikishushwa toka mbinguni na kuingizwa ndani ya mioyo yetu. Huyo ndiye Roho Mtakatifu. Anazo kazi zake zenye nguvu za kuzitoa kama karama; lakini utimilifu wa Roho Mtakatifu ni huu: Yesu Kristo katika unyenyekevu wake akija kukaa ndani yetu. Kristo alipokuwa akiwafundisha wanafunzi wake, mafundisho yake yote yaweza kuwa yalisaidia kwa njia ya maandalizi, kuwavunja, kuwafanya watambue kilichokuwa kibaya, na kuamsha shauku; lakini mafundisho hayakuweza kulitimiza, na upendo wao wote kwa Yesu na shauku yao ya kumpendeza havikuweza kulitimiza hata Roho Mtakatifu alipokuja. Hilo ndilo ahadi Kristo aliyoitoa. Asema, kwa kuhusiana na kuja kwa Roho Mtakatifu: “Nitakuja kwenu.” Yohana 14:18.

Kristo aliwaambia wanafunzi wake: “Nimekuwa nanyi miaka mitatu, nanyi mmekuwa katika uhusiano wa karibu sana nami, nami nimefanya kadiri ya uwezo wangu kuifikia mioyo yenu; nimetaka kuingia mioyoni mwenu, lakini nimeshindwa; lakini msiogope, nitakuja tena. Siku ile, mtaniona, na mioyo yenu itafurahi, wala hakuna mtu atakayeiondoa furaha yenu. Nitakuja tena kukaa ndani yenu, na kuishi maisha yangu ndani yenu.” Tazama Yohana 16:22. Kristo alikwenda mbinguni ili apate nguvu ambayo hakuwa nayo hapo awali. Nayo ilikuwa nini? Ni nguvu ya kuishi ndani ya wanadamu. Mungu asifiwe kwa hili! Ni kwa sababu Yesu, yeye mnyenyekevu, Mwana-Kondoo wa Mungu, yeye mpole, mnyenyekevu na mwenye upole, alishuka katika Roho Mtakatifu ndani ya mioyo ya wanafunzi wake, ndio kiburi kilifukuzwa, na kwamba pumzi hasa ya Mbinguni ikavuma kupitia yeye katika upendo uliowafanya kuwa moyo mmoja na roho moja.

Rafiki wapendwa, Kristo ni wenu. Kristo, ajapo katika nguvu za Roho Mtakatifu, ni wenu. Je, mnamtamani kuwa naye, kuwa na Kristo Yesu aliye mkamilifu? Basi, njooni, mkaone jinsi, katikati ya tukufu za Uungu wake—kule kwake kuwa katika umbo la Mungu, na sawa na Mungu; katikati ya tukufu za kufanyika kwake mwili—kule kwake kuwa mwanadamu; katikati ya tukufu za upatanisho wake—kule kwake kuwa mtii hata mauti; na katikati ya tukufu za kutukuzwa kwake, ambao ndio utukufu mkuu na ung’aao zaidi, alivyojinyenyekeza toka Mbinguni hata chini duniani na hata msalabani.

Alijinyenyekeza ili abebe jina hilo, aonyeshe upole, na afe kifo cha Mwana-Kondoo wa Mungu.

Na sasa ni jambo gani tunalohitaji kulifanya? Twawezaje kuokolewa kwa unyenyekevu huu wa Yesu? Ni swali zito, lakini, ahsante Mungu, jibu laweza kutolewa. Kwanza, ni lazima tuutamani kuliko yote. Na tujifunze kumwomba Mungu atuokoe kutoka katika kila chembe ya kiburi, kwa maana hiki ni kitu kilicholaaniwa. Na tujifunze kuyaweka kando kwa muda mambo mengine katika maisha ya Kikristo, na kuanza kumsihi Mwana-Kondoo wa Mungu siku kwa siku, “Ee Mwana-Kondoo wa Mungu, naujua upendo wako, lakini naujua kidogo mno upole wako.” Njoo siku baada ya siku, na uweke moyo wako uegemee moyo wake, na umwambie kwa shauku kuu: “Yesu, Mwana-Kondoo wa Mungu, nipe, ee, nipe nafsi yako mwenyewe, pamoja na upole wako na unyenyekevu wako,” naye atatimiza haja ya wale wamchao. Haitoshi kuutamani na kuuombea; udai na uukubali kuwa ni wako. Unyenyekevu huu umetolewa kwako ndani ya Kristo Yesu.

Kristo ni uzima wetu. Maana yake nini? Ee, laiti Mungu angetupatia wewe na mimi maono ya maana yake. Hewa ni uzima wetu, nayo hewa iko kila mahali, imeenea kote. Twapumua bila taabu kwa sababu Mungu ametuzunguka kwa hewa, na je, hewa iko karibu nami kuliko Kristo? Jua huupatia nuru kila jani la kijani na kila unyasi, likiangaza saa kwa saa na dakika kwa dakika. Na je, jua liko karibu na unyasi kuliko Kristo alivyo karibu na nafsi ya mwanadamu? Kweli, hapana; Kristo ametuzunguka pande zote; Kristo anatusukuma tumkaribishe aingie, wala hakuna kitu mbinguni, wala duniani, wala kuzimu, kiwezacho kuizuia nuru ya Kristo isiangaze ndani ya moyo ulio tupu na wazi.

Kama madirisha ya chumba chako yangefungwa kwa vifunga, nuru isingeweza kuingia; ingekuwa nje ya jengo, ikimiminika na kumiminika juu ya vile vifunga; lakini isingeweza kuingia. Lakini yaache madirisha bila vifunga, nayo nuru itakuja, itafurahi kuingia na kukijaza chumba. Vivyo hivyo, watoto wa Mungu, Yesu, na nuru yake, Yesu na unyenyekevu wake, wako pande zote karibu nanyi, wakitamani kuingia ndani ya mioyo yenu. Njoo umtwae leo katika upole wake uliobarikiwa na wema wake. Usimwogope; yeye ni Mwana-Kondoo wa Mungu. Yeye ni mvumilivu sana kwako, ni mwenye fadhili sana, ni mpole na mwenye upendo sana.

Jipe moyo leo na umwamini Yesu aje ndani ya moyo wako na kuumiliki. Na atakapokwisha kuumiliki, kutakuwa na maisha ya siku kwa siku ya ushirika uliobarikiwa pamoja naye, nawe utahisi hitaji lililo la ndani zaidi siku zote la wakati wako wa kimya pamoja naye, na la kumwabudu na kumsujudia, na la kujitupa tu chini mbele zake katika kutokuwa na msaada na unyenyekevu, ukisema: “Yesu, mimi si kitu, na wewe ndiwe yote.” Yatakuwa maisha yaliyobarikiwa kwa sababu utakuwa na hisia ya kuwa miguuni pa Yesu. Wakati huu waweza kumdai Yesu katika unyenyekevu wake wa kimungu kuwa uzima wa nafsi yako. Je, utakubali? Je, hutaufungua moyo wako, na kusema: “Ingia; ingia?”

Njoo leo, na umtwae upya katika nguvu hii iliyobarikiwa ya unyenyekevu wake wa ajabu, na umwambie: “Ee, wewe uliyesema, ‘Jifunzeni kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu.’ Bwana wangu, najua ni kwa nini sina maisha makamilifu; ni kiburi changu, lakini leo, njoo ukae ndani ya moyo wangu. Wewe uliyewaongoza hata Petro na Yohana katika baraka ya unyenyekevu wako wa mbinguni; hutanikataa. Bwana, mimi hapa; wewe ambaye kwa unyenyekevu wako wa ajabu peke yako waweza kuokoa, ingia ndani. Ee Mwana-Kondoo wa Mungu, nakuamini wewe; umiliki moyo wangu, na ukae ndani yangu.” Utakaposema hayo, toka nje kwa utulivu, na ujitenge, ukitembea kwa upole kana kwamba unamshika Mwana-Kondoo wa Mungu moyoni mwako, na useme: “Nimempokea Mwana-Kondoo wa Mungu; yeye auweka moyo wangu kuwa jukumu lake; anavuvia unyenyekevu wake na kumtegemea Mungu ndani yangu, na hivyo ananileta kwa Mungu. Unyenyekevu wake ni uzima wangu na wokovu wangu.

Yaliyomo

Ukaaji wa Bwana Ndani Yetu Andrew Murray

Ukurasa 1 / 1 · 13 dakika zimebaki katika sura