Ukaaji wa Bwana Ndani Yetu ·Kujisalimisha Kikamili

Sura 8 · dakika 13 za kusoma

Kujisalimisha Kikamili

Mwanzo 39:1-3.—Basi Joseph alikuwa ameteremshwa mpaka Misri; na Potiphar, ofisa wa Pharaoh, jemadari wa askari walinzi, Mmisri, akamnunua kutoka mikononi mwa Waishmaeli waliokuwa wamemteremsha huko. Bwana alikuwa pamoja na Joseph, naye akawa mtu aliyefanikiwa; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake Mmisri. Bwana wake akaona ya kuwa Bwana alikuwa pamoja naye, na ya kuwa Bwana aliyafanikisha mikononi mwake yote aliyoyafanya.

Katika fungu hili tunapata somo la mfano linalotufundisha Kristo ni nini kwetu. Angalia: Joseph alikuwa mtumwa, lakini Mungu alikuwa pamoja naye kwa dhahiri hata bwana wake akaweza kuona. “Bwana wake akaona ya kuwa BWANA alikuwa pamoja naye, na ya kuwa BWANA aliyafanikisha mikononi mwake yote aliyoyafanya. Basi Joseph akapata kibali machoni pake, akamtumikia, “Mwanzo 39:3-4. Hilo lilikuwa jambo jipya. Joseph alikuwa mtumwa, lakini sasa amekuwa bwana.

“Akamweka awe msimamizi wa nyumba yake, na vyote alivyokuwa navyo akavitia mikononi mwake. Tokea wakati ule alipomweka awe msimamizi katika nyumba yake, na juu ya vyote alivyokuwa navyo, BWANA akaibariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Joseph; baraka ya BWANA ikawa juu ya vyote alivyokuwa navyo, nyumbani na shambani. Basi akaviacha vyote alivyokuwa navyo mikononi mwa Joseph; wala hakujishughulisha na neno lo lote ila chakula alichokula.” Mwanzo 39:4-6.

Tunamwona Joseph katika hali mbili ndani ya nyumba ya Potiphar: kwanza, kama mtumishi na mtumwa, mtu anayeaminiwa na kupendwa, lakini bado ni mtumishi kabisa; pili, kama bwana. Potiphar alimfanya kuwa msimamizi juu ya nyumba yake na mashamba yake, na vyote alivyokuwa navyo, hata tunasoma baadaye kwamba aliacha kila kitu mikononi mwake, wala hakujua neno lo lote ila mkate uliokuja mezani pake. Nataka kuvuta fikira zenu kwa Joseph kama mfano wa Kristo. Nyakati nyingine katika maisha ya Kikristo twanena juu ya kujisalimisha kikamili, na kwa haki, na hapa tunayo taswira nzuri ya jambo hilo lilivyo.

Kwanza, Joseph alikuwa katika nyumba ya Potiphar ili kumtumikia na kumsaidia, naye akafanya hivyo; Potiphar akajifunza kumwamini, hata akasema, “Vyote nilivyo navyo nitavitia mikononi mwake.” Basi, hivyo ndivyo hasa inavyopasa kutokea kwa Wakristo wengi. Wanamjua Kristo, wanamwamini, nao wanampenda, lakini yeye si Bwana, ni kama msaidizi tu.

Wakiwa katika taabu wanamjia, wakitenda dhambi wanamwomba msamaha katika damu yake ya thamani, wakiwa gizani wanamlilia; lakini mara nyingi sana wanaishi kwa kufuata mapenzi yao wenyewe, nao wanajitafutia msaada wao wenyewe. Lakini heri iliyoje mtu yule ajaye, na, kama Potiphar, asema, “Nitamsalimishia Yesu kila kitu!”

Wako wengi waliomkubali Kristo kuwa Bwana wao lakini bado hawajafikia kujisalimisha kwa mwisho, kwa ukamilifu, kwa vitu vyote. Enyi Wakristo, kama mwataka pumziko kamili, furaha idumuyo, nguvu za kumtumikia Mungu, oh, njoni mjifunze kwa yule Mmisri maskini asiyemjua Mungu jambo iwapasalo kutenda. Aliona ya kuwa Mungu alikuwa pamoja na Joseph, naye akasema, “Nitamkabidhi yeye nyumba yangu.” Oh, jifunzeni kutenda hivyo. Wako wengine ambao bado hawajamkubali Kristo, wengine wanaomtafuta, wakiona kiu na njaa, lakini hawajui jinsi ya kumpata.

Niwaelekeze fikira zenu kwa mawazo manne kuhusu kujisalimisha huku kwa Kristo: Kwanza, sababu zake; pili, kipimo chake; tatu, baraka yake; na mwisho, kudumu kwake. Kwanza kabisa, sababu zake. Ni nini kilichomsukuma Potiphar kufanya hivyo? Nadhani jibu ni rahisi sana: alikuwa mtumishi aliyeaminiwa wa mfalme, naye alikuwa na kazi ya mfalme ya kuitunza, na yamkini hakuweza kuitunza nyumba yake mwenyewe. Muda wake wote na fikira zake zilihitajiwa katika baraza la Pharaoh. Alikuwa na wajibu wake huko; alikuwa katika heshima kubwa, lakini nyumba yake mwenyewe ilipuuzwa. Yamkini alikuwa na wasimamizi wengine hapo awali, mtumwa mmoja aliyewekwa kuwatawala wengine, na labda huyo alikuwa si mwaminifu, au mlaghai, na kwa namna fulani nyumba yake haikuwa kama alivyoitaka.

Basi ananunua mtumwa mwingine, kama alivyofanya hapo awali, lakini katika hali hii, anaona jambo ambalo hakuwahi kuliona kamwe.

Kuna jambo lisilo la kawaida kwa mtu huyu. Anaenenda kwa unyenyekevu mwingi, anatumika kwa uaminifu na kwa upendo mwingi, na pamoja na hayo kwa mafanikio makubwa. Potiphar anaanza kuchunguza sababu ya hili na hatimaye anahitimisha kwamba Mungu yu pamoja naye.

Ni jambo kuu kuwa na mtu ambaye Mungu yu tayari kumkabidhi shughuli za mtu. Yule mpagani alilitambua hili, na kati ya uhitaji wa nyumba yake mwenyewe na kile alichokiona ndani ya Joseph, aliamua kumfanya kuwa msimamizi. Nawauliza, je, sababu hizi mbili hazisihi kwa udi mkubwa kwamba mseme: “Nitamfanya Yesu kuwa bwana juu ya nafsi yangu yote?” Nyumba yako, Mkristo, maisha yako ya kiroho, maskani, hekalu la Mungu ndani ya moyo wako,—liko katika hali gani? Je, mara nyingi si kama lile hekalu la kale, katika Yerusalemu, lililokuwa limenajisiwa na kufanywa nyumba ya biashara, na baadaye pango la wanyang’anyi? Moyo wako, uliokusudiwa kuwa makao ya Yesu, je, mara nyingi si umejaa dhambi na giza, umejaa huzuni, umejaa mashaka? Umefanya uwezavyo wote kuubadilisha, nawe umeomba msaada wa mwanadamu, na msaada wa njia mbalimbali; umetumia kila mbinu uliyoweza kuwaza ili kuurekebisha; lakini hautakuwa sawa mpaka yeye aliye wake mwenyewe aingie ndani kuchukua uongozi.

Kama kuna taabu yo yote moyoni mwako, kama uko gizani, au katika nguvu za dhambi, nakuletea Mwana wa Mungu, pamoja na ahadi kwamba ataingia ndani na kuchukua uongozi. Kama vile Potiphar alivyomchukua Joseph, je, hutamchukua Yesu?

Je, hajajithibitisha kuwa anastahili kuaminiwa? Njoo useme, “Yesu atakuwa na uongozi wote; yeye anastahili.” Usifikiri tu juu ya nguvu zake za Kimungu bali fikiri juu ya upendo wake wa ajabu; fikiri juu ya kuja kwake kutoka mbinguni ili akuokoe; fikiri juu ya kufa kwake pale Kalvari na kumwaga damu yake kwa ajili ya upendo mwingi kwako. Oh, fikiri juu ya hilo; Kristo aliye mbinguni humpenda kila mmoja aliyekabidhiwa kwake, na ambaye amemfanya kuwa mtoto wa Mungu. “Naye alivyokuwa amewapenda watu wake waliokuwa ulimwenguni, aliwapenda hata mwisho.”

Je, ni lazima nisihi kwa jina la upendo wa Yesu aliyesulubiwa; je, ni lazima niwasihi ninyi Wakristo, na kusema, Mtazameni Yesu, Mwana wa Mungu, Mkombozi wenu, na kuwaomba mmfanye kuwa msimamizi juu ya vyote? Mpeni uongozi juu ya hasira yako, mapenzi ya moyo wako, mawazo yako, nafsi yako yote, naye atajithibitisha kuwa anastahili. Joseph alikuwa kwa muda mtumwa wa kawaida tu pamoja na watumwa wengine waliokuwa wamemtumikia Pharaoh. Ole! Wakristo wengi wamemtumia Kristo kwa maendeleo na faraja yao wenyewe, kama vile mtu atumiavyo kila kitu ulimwenguni. Anawatumia baba na mama, mchungaji, fedha, na kila kitu kingine ulimwengu utakachotoa, ili kujifariji na kujifurahisha; kuna hatari katika kumtumia Kristo Yesu kwa namna iyo hiyo. Ndugu, jambo hili si sawa. Ninyi ni nyumba yake, naye ana haki ya kukaa ndani yake. Je, hamtaki kuja na kusalimisha vyote, na kusema, “Bwana Yesu, nimekufanya kuwa msimamizi juu ya vyote”?

Lakini sasa, pili, kipimo cha kujisalimisha huko. Twasoma katika mstari wa 4: “Akamweka awe msimamizi wa nyumba yake, na vyote alivyokuwa navyo akavitia mikononi mwake.” Kisha katika mstari wa 5: “Tokea wakati ule alipomweka awe msimamizi katika nyumba yake, na juu ya vyote alivyokuwa navyo”—hapo unalo mara ya pili—“BWANA akaibariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Joseph; baraka ya BWANA ikawa juu ya vyote alivyokuwa navyo”—hapo mara ya tatu. Kisha katika mstari wa 6: “Basi akaviacha vyote alivyokuwa navyo”—hapo unayo maneno mara ya nne—“mikononi mwa Joseph; wala hakujishughulisha na neno lo lote ila chakula alichokula.” Naona nini hapa? Kwamba Potiphar kwa kweli alitia kila kitu mikononi mwa Joseph. Alimfanya kuwa bwana juu ya watumwa wake. Fedha zote zilitiwa mikononi mwa Joseph, kwa maana twasoma kwamba Potiphar hakuwa na jukumu la kitu cho chote. Chakula kilipoletwa mezani, alikula, na hilo tu ndilo alilolijua juu ya yaliyokuwa yakiendelea nyumbani mwake. Je, huku si kujisalimisha kikamili?—anakabidhi kila kitu mikononi mwa Joseph. Ah, Wakristo wapendwa, nataka mjiulize: “Je, mimi nimefanya hivyo?”

Umekwisha kutoa zaidi ya sala moja ya kujiweka wakfu, nawe umekwisha kusema zaidi ya mara moja: “Yesu, vyote nilivyo navyo nakupa wewe.” Umeyasema hayo na kuyamaanisha, lakini yamkini hukutambua kikamili maana yake. Pamoja na neno ‘kujisalimisha’, siku zote yaonekana kuna maana kubwa zaidi na pana zaidi. Hatufaulu kutimiza makusudi yetu, na baadaye, twarudisha kitu hiki na kile hata tumepoteza kusudi letu la awali. Wakristo wapendwa, mruhusuni Kristo Yesu awe na vyote. Mruhusuni awe na moyo wako wote, pamoja na mapenzi yake; yeye mwenyewe hupenda, kwa upendo unaozidi ule upendo wa Jonathan. Mruhusuni awe na moyo wako wote, ukisema, “Yesu, kila nyuzi ya nafsi yangu, kila nguvu ya roho yangu, itawekwa wakfu kwako.” Naye atakubali kujisalimisha huko. Alinena neno zito: “Yakupasa, kwa kulinganisha, kumchukia kila mtu mwingine—baba yako na mama yako,” Sema hivi leo: “Bwana Yesu, upendo kwa baba na mama, kwa mke na mtoto, kwa ndugu na dada, nakuachia wewe. Nifundishe jinsi ya kukupenda. Nina shauku moja tu, nayo ni kukupenda. Nataka kuutoa moyo wangu wote ujae upendo wako.”

Lakini utakapokwisha kuutoa moyo wako, bado kuna zaidi ya kutoa. Kuna kichwa—ubongo pamoja na mawazo yake. Naamini Wakristo hawajui ni kiasi gani wanamnyang’anya Kristo kwa kusoma sana fasihi ya ulimwengu.

Mara nyingi wamejishughulisha sana na magazeti yao hata Biblia hupata nafasi ndogo mno. Oh, rafiki, nawasihi mlete nguvu hii tukufu ambayo Mungu amewapa, nguvu ya akili iwezayo kuwaza mambo ya mbinguni, ya milele, na yasiyo na kikomo, na kuiweka miguuni pa Yesu, mkisema, “Bwana Yesu, kila kipawa cha nafsi yangu nataka kukusalimishia wewe, ili unifundishe la kuwaza, na jinsi ya kuwaza, kwa ajili yako na ufalme wako.” Msifiwe Mungu, wako watu waliotoa akili zao kwa Yesu, nayo imekubaliwa naye. Na kwa habari hii, kuna maisha yangu yote ya nje. Kuna uhusiano wangu na jamii, cheo changu miongoni mwa watu, mwingiliano wangu nyumbani mwangu mwenyewe, pamoja na rafiki na jamaa; kuna fedha zangu, wakati wangu, biashara yangu; yote haya yapasa kutiwa mikononi mwa Yesu. Mtu hawezi kujua kabla baraka ya kujisalimisha huku lakini bila shaka ni baraka kweli. Njoo, kwa sababu yeye anastahili; njoo kwa sababu wajua huwezi kuyaweka mambo sawa wewe mwenyewe, na umfanye Kristo kuwa bwana juu ya vyote ulivyo navyo. Mpe Yesu baba na mama, mke na mtoto, nyumba, shamba, na fedha, vyote, nawe utaona kwamba katika kutoa vyote wavipokea tena mara mia.

Tatu, tazama baraka ya kujisalimisha kikamili. Hapa unayo maneno ya ajabu: “Tokea wakati ule alipomweka awe msimamizi katika nyumba yake, na juu ya vyote alivyokuwa navyo, BWANA akaibariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Joseph; baraka ya BWANA ikawa juu ya vyote alivyokuwa navyo, nyumbani na shambani.” Mwanzo 39:5. Nawauliza, enyi Wakristo, Ikiwa Mungu alimtendea hivi yule mpagani kwa sababu alimheshimu Joseph; ikiwa Mungu, kwa ajili ya Joseph, alimbariki yule Mmisri kwa namna hii ya ajabu, je, Mkristo hathubutu kusema: “Nikiweka maisha yangu mikononi mwa Yesu, je, nina hakika Mungu atavibariki vyote nilivyo navyo?” Oh, thubutu kusema hivyo. Potiphar alimwamini Joseph kwa moyo wote na kwa ukamilifu, na kulikuwa na ufanisi kila mahali kwa sababu Mungu alikuwa pamoja na Joseph. Rafiki wapendwa, kama mkisalimisha kila kitu, litegemeeni hilo, baraka tokea wakati ule itakuwa yenu. Kutakuwa na baraka ndani ya maisha yenu ya ndani na baraka katika maisha yenu ya nje. Alimbariki Potiphar nyumbani, shambani, na kila mahali.

Oh, Mkristo, ni baraka gani hiyo utakayoipata? Siwezi kueleza yote, lakini naweza kukuambia hili: kama utakuja kwa Kristo Yesu na kusalimisha vyote, baraka ya Mungu itakuwa juu ya vyote ulivyo navyo. Kutakuwa na baraka kwa nafsi yako mwenyewe. “Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea katika amani kamili, kwa kuwa anakutumaini.” Isaya 26:3.

Jaribu hilo; mwamini Yesu kwa kila kitu, na mkabidhi kila kitu, na baraka ya Mungu itakujilia—pumziko tamu, pumziko la imani. Vyote vimo mikononi mwa Yesu; yeye atakuongoza; atakufundisha; atatenda kazi ndani yako; atakuhifadhi; atakuwa kila kitu kwako. Ni pumziko lililobarikiwa kama nini, na uhuru kutoka jukumu na kutoka mahangaiko, kwa sababu vyote vimo mikononi mwa Yesu! Sisemi kwamba taabu na majaribu hayatakuja kamwe; bali katikati ya jaribu na taabu, utakuwa na utoshelevu kamili wa uwepo wa Yesu uwe faraja yako, msaada wako, na kiongozi chako.

Joseph aliuzwa na ndugu zake, lakini aliona Mungu ndani ya jambo hilo, naye aliridhika kabisa. Kristo alisalitiwa na Judas, alihukumiwa na Caiaphas, na kutolewa auawe na Pilate; lakini katika hayo yote, Kristo alimwona Mungu, naye aliridhika. Kabidhi maisha yako, katika hali zake zote, mikononi mwa Yesu; ukikumbuka kwamba hata nywele za kichwa chako zimehesabiwa, wala shomoro mmoja haangukii chini bila Baba kujua. Kubali sasa na useme: “Nitatia kila kitu mikononi mwa Yesu.

Mungu alimbariki Potiphar shambani; katika maisha yanayoonekana nje ya nyumba yake; na Mungu atakubariki wewe, ili, katika mwingiliano wako na watu, uweze kuwa baraka; ili kwa mwenendo wako mtakatifu, wa unyenyekevu, wa heshima, wa utulivu, uweze kuchukua faraja; ili kwa utayari wako wa upendo wa kuwa mtumishi na msaidizi kwa wote, uweze kudhihirisha Roho wa Mungu aliyoyatenda ndani yako. Oh, ndugu yangu, dada yangu, huna wazo lake,—wala mimi sina—jinsi Mungu alivyo tayari kuibariki nafsi iliyojisalimisha kabisa kwa Yesu. Mungu hawezi kufurahia kitu ila Yesu. Mungu humfurahia Yesu bila kikomo.

Mungu hutamani kutoona ndani yetu kitu ila Yesu, na kama nikiutoa moyo wangu na maisha yangu kwa Yesu, na kusema, “Mungu wangu, nataka usione ndani yangu kitu ila Yesu,” ndipo namletea Baba dhabihu iliyo yenye kukubalika kuliko zote. Oh, waaminio, njoni leo; tokeni katika taabu zenu zote, jitihada zenu zote za nafsi, kujiamini kwenu, na mruhusuni Mwana wa Mungu aliyebarikiwa achukue umiliki.

Niwaelekeze fikira zenu, na mwisho, kwa kudumu kwa kujisalimisha huku. Nataka kukazia hili—kwa sababu katika hali nyingi kujisalimisha hakudumu. Wengine huondoka, na kwa muda huwa na furaha na shangwe nyingi, lakini punde huanza kupungua, na katika majuma machache au labda miezi kwapotea yote. Wengine wasiokupoteza kabisa, hulalamika kwa huzuni nyakati nyingine, kwamba huondoka na kurudi tena. Husema: “Maisha yangu yamebarikiwa sana tangu kujisalimisha kule nilikokufanya kwa Mungu, lakini hayakuwa daima katika kiwango kile kile.” Potiphar alifanya nini? Twasoma katika mstari wa 4: “Akamweka awe msimamizi wa nyumba yake, na vyote alivyokuwa navyo akavitia mikononi mwake” Neno rahisi kama nini! Aliliacha hapo.

Watoto wa Mungu, kama mtafika tu mahali pale na kusema, “Kwa milele yote nayaacha mikononi mwa Yesu,” mtaona ni baraka iliyoje. Potiphar aliona sasa kwamba angeweza kuifanya kazi ya mfalme kwa mikono miwili na moyo usiogawanyika. Ningeweza kujaribu kumwokoa mtu anayezama kwa kushika imara mahali fulani kwa mkono mmoja, huku nikimnyoshea yule mtu mkono mwingine, lakini ni jambo kuu kwa mtu kuweza kunyosha mikono yote miwili, na mtu huyo ndiye yule aliyeacha vyote kwa Yesu—maisha yake yote ya ndani, mahangaiko yake yote na taabu zake, na amejitoa mwenyewe kabisa kuyafanya mapenzi ya Mungu.

Je, utaliacha hapo? Ni lazima nisisitize hili kwa sababu najua majaribu yatakuja. Jaribu mojawapo litakuwa kwamba hisia ulizokuwa nazo katika tendo lako la kujisalimisha zitatoweka; hazitakuwa nyangavu hivyo.

Jingine ni kwamba mazingira yatakujaribu. Mpendwa, majaribu yatakuja; Mungu ayakusudia kwa faida yako.

Kila jaribu hukuletea baraka. Lielewe hilo. Jifunze somo la kutoa kila kitu kwa Yesu, na kumwacha Yesu achukue uongozi wa kila kitu. Acha vyote kwa Yesu. Usidhani kwamba kwa kujisalimisha leo au siku yo yote, hata kuwe na nguvu kiasi gani, hata kuwe na uwezo kiasi gani, mambo yatajiweka sawa yenyewe. Wahitaji kila asubuhi upya, Mungu akuamshapo usingizini, kuutia moyo wako, maisha yako, nyumba yako, na biashara yako, mikononi mwa Yesu. Mngoje yeye, ikibidi, kwa kimya, au kwa maombi, hata akupe uhakikisho, “Mwanangu, kwa leo yote ni salama; nachukua uongozi.” Na asubuhi kwa asubuhi atakufanyia upya baraka, na asubuhi kwa asubuhi utatoka katika wakati wako wa kimya ukiwa na fahamu, “Leo nimekuwa na ushirika na Mfalme wangu, na yote ni sawa.” Yesu amechukua uongozi. Na hivyo, siku kwa siku, waweza kuwa na neema ya kuacha vyote mikononi mwa Yesu.

Kwa kuhitimisha, niseme na makundi mawili. Ziko nyakati moyo wako unapokuwa hauna raha; ziko nyakati unapoogopa kufa.

Kwa waaminio waliokwisha kufanya hivyo hapo awali, na wanaotamani kwa shauku isiyoelezeka kufanya hivyo kwa ukamilifu na kwa utimilifu,—Mtoto wa Mungu, waweza kufanya hivyo, kwa maana Roho Mtakatifu ameteremshwa kutoka Mbinguni kwa kusudi hili moja, kumtukuza Yesu; kumtukuza Yesu ndani ya moyo wako, kwa kukuwezesha kuona jinsi Yesu awezavyo kuumiliki kikamili moyo wote; kumtukuza Yesu kwa kumleta ndani ya maisha yako hasa, ili maisha yako yote yaweze kung’aa kwa utukufu wa Yesu. Kwa kulitegemea hilo, Baba atakupa kwa njia ya Roho Mtakatifu, kama uko tayari. Oh, njoo, na mwingiliano wako na Mungu ukusanywe katika sala rahisi na jibu—“Mungu wangu, kadiri utakavyotaka kunichukua ili nijazwe Kristo, utapata leo.” “Mwanangu, kadiri ya Kristo ambaye moyo wako watamani kuwa naye, utapata; kwa maana ni furaha yangu kwamba Mwanangu awe katika mioyo ya watoto wangu.”

Yaliyomo

Ukaaji wa Bwana Ndani Yetu Andrew Murray

Ukurasa 1 / 1 · 13 dakika zimebaki katika sura