Sura 6 · dakika 15 za kusoma
Kristo Uzima Wetu
Wakolosai 3:4.—Kristo aliye uzima wenu.
Swali moja linaloibuka katika kila akili ni hili: “Ninawezaje kuishi maisha yale ya kumtumaini Mungu kikamili?” Wengi hawaijui jibu sahihi wala jibu kamili. Ni hili: “Kristo lazima aishi maisha hayo ndani yangu.” Hicho ndicho alichokuwa mwanadamu kwa ajili yake; ili akiwa mwanadamu aishi maisha ya kumtumaini Mungu, na hivyo kutuonyesha jinsi itupasavyo kuishi. Alipokwisha kufanya hivyo hapa duniani, alikwenda mbinguni, ili afanye zaidi ya kutuonyesha tu, atupe, na kuishi ndani yetu maisha hayo ya kumtumaini. Ni tunapoelewa maisha ya Kristo ni nini na jinsi yanavyokuwa yetu, ndipo tutakapokuwa tayari kutamani na kumwomba yeye aishi maisha hayo yeye mwenyewe ndani yetu. Tutakapokwisha kuona kwanza uzima ni nini, ndipo tutakapoelewa jinsi anavyoweza kwa kweli kutumiliki, na kutufanya kama yeye mwenyewe. Napenda hasa kuelekeza fikira kwenye swali hilo la kwanza. Nataka kuweka mbele yenu maisha ya Kristo kama alivyoyaishi, ili tupate kuelewa ni nini alichonacho kwa ajili yetu na tunachoweza kutazamia kutoka kwake.
Kristo Yesu aliishi maisha hapa duniani ambayo anatarajia sisi tuyaige. Mara nyingi tunasema kwamba twatamani kuwa kama Kristo. Twachunguza tabia za umbile lake, twafuata nyayo zake, na kuomba neema ya kuwa kama yeye, na hata hivyo, kwa namna fulani, twafaulu kidogo mno. Na kwa nini? Kwa sababu twataka kuchuma tunda hali mzizi haupo. Kama kweli twataka kuelewa maana ya kumwiga Kristo, ni lazima twende kwenye kile kilichokuwa mzizi hasa wa maisha yake mbele za Mungu. Yalikuwa maisha ya kutegemea kabisa, kutumaini kabisa, na kujisalimisha kabisa, na hata tutakapokuwa kitu kimoja naye katika lile lililo kanuni ya maisha yake, ni bure kutafuta huku au huko kunakili neema za maisha hayo.
Katika hadithi ya Injili, twapata mambo makuu matano ya umuhimu wa pekee; kuzaliwa, maisha hapa duniani, kifo, ufufuo, na kupaa. Katika haya tunacho kile ambacho mwandishi mmoja wa zamani amekiita “mwenendo wa Yesu Kristo;” mwenendo ambao kwao alikuwa kile alicho leo—Mfalme wetu aliyetukuzwa na uzima wetu. Katika mwenendo huu wote wa uzima, ni lazima tufanywe kama yeye. Tazama la kwanza. Twasemaje juu ya kuzaliwa kwake? Ni hili: Aliupokea uzima wake kutoka kwa Mungu. Namna gani juu ya maisha yake hapa duniani? Aliishi maisha hayo kwa kumtegemea Mungu. Juu ya kifo chake? Aliutoa uzima wake kwa Mungu. Juu ya ufufuo wake? Alifufuliwa katika wafu na Mungu. Na juu ya kupaa kwake? Anaishi uzima wake katika utukufu pamoja na Mungu.
Kwanza, aliupokea uzima wake kutoka kwa Mungu. Na kwa nini ni jambo la maana kwamba tuutazame huo? Kwa sababu Kristo Yesu alikuwa na kitovu cha maisha yake yote katika huo. Alisema: “Baba amenituma;” “Baba ampenda Mwana, naye amempa vitu vyote mkononi mwake;” “Kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake.” Yohana 5:26. Kristo aliupokea kama uzima wake mwenyewe, kama vile Mungu alivyo na uzima wake nafsini mwake. Na hata hivyo, wakati wote ulikuwa uzima uliotolewa na kupokewa. “Kwa sababu Baba Mwenyezi ameutoa uzima huu kwangu, Mwana wa Adamu duniani, naweza kumtegemea Mungu kuudumisha na kunipitisha katika yote.” Na hilo ndilo somo la kwanza tunalolihitaji. Twahitaji kulitafakari mara nyingi, kuomba, kufikiri, na kungoja mbele za Mungu hata mioyo yetu ifunguke kwenye ufahamu ule wa ajabu kwamba Mungu wa milele ana uzima wa kimungu ndani yetu ambao hauwezi kuwapo isipokuwa kwa njia yake. Naamini Mungu ameutoa uzima wake ulio na mizizi ndani yake. Nahisi ni lazima udumishwe naye.
Mara nyingi twadhani kwamba Mungu ametupa uzima ambao sasa ni wetu wenyewe, uzima wa kiroho ambao sisi ndio tunaopaswa kuusimamia; kisha twalalamika kwamba hatuwezi kuutunza sawasawa. Si ajabu. Ni lazima tujifunze kuishi, kujifunze kuishi kama Yesu alivyoishi. Nina hazina niliyopewa na Mungu katika chombo hiki cha udongo. Nina nuru ya kumjua utukufu wa Mungu katika uso wa Kristo. Nina uzima wa Mwana wa Mungu ndani yangu, uzima niliopewa na Mungu mwenyewe, nao waweza kudumishwa na Mungu mwenyewe tu ninapoishi katika ushirika naye.
Mtume Paulo atufundisha nini katika Warumi 6; mahali ambapo ndipo kwanza ametuambia kwamba ni lazima tujihesabu kuwa wafu kwa dhambi, na hai kwa Mungu katika Kristo Yesu? Aendelea mara moja kusema: “Jitoeni kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa” Warumi 6:13. Mara ngapi Mkristo husikia maneno mazito juu ya kuwa kwake hai kwa Mungu, na kupaswa kwake kujihesabu kuwa amekufa kweli kwa dhambi, na hai kwa Mungu katika Kristo! Hajui la kufanya; mara hutafuta huku na huku: “Ninawezaje kuutunza, kifo hiki na uzima huu?” Sikiliza asemayo Paulo. Wakati ule ujihesabupo kuwa umekufa kwa dhambi na hai kwa Mungu, nenda na uzima huo kwa Mungu mwenyewe, jitoe kama uliye hai katika wafu, na umwambie Mungu: “Bwana, umenipa uzima huu. Wewe peke yako waweza kuutunza. Naukuletea. Siwezi kuufahamu wote. Sifahamu vyema nilichonacho, lakini naja kwa Mungu ili akamilishe kile alichokianza.” Ili niishi kama Kristo, ni lazima nijitambue kila dakika kwamba uzima wangu umetoka kwa Mungu, na yeye peke yake aweza kuudumisha.
Kisha, pili, Kristo aliyaishije maisha yake katika ile miaka thelathini na mitatu aliyotembea humu duniani? Aliyaishi kwa kumtegemea Mungu. Mwajua jinsi asemavyo daima: “Amin, amin, nawaambia, Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe, ila lile amponalo Baba analitenda.” Yohana 5:19. Alingoja bila kukoma mafundisho, amri, na uongozi wa Baba. Aliomba nguvu kutoka kwa Baba. Lolote alilolitenda, alilitenda kwa jina la Baba. Yeye, Mwana wa Mungu, alihisi uhitaji wa maombi mengi, wa maombi ya kudumu, wa kushusha kutoka mbinguni na kudumisha maisha ya ushirika na Mungu katika maombi.
Twasikia mengi juu ya kumtumaini Mungu. Jambo lililobarikiwa mno! Nasi twaweza kusema: “Ah, hicho ndicho nikitakacho,” nasi twaweza kuisahau siri hasa ya yote,—kwamba Mungu, katika Kristo, ni lazima atende yote ndani yetu. Simhitaji Mungu kama shabaha ya kumtumaini tu, bali ni lazima niwe na Kristo ndani yangu nguvu ya kutumaini; ni lazima aishi maisha yake mwenyewe ya kutumaini ndani yangu.
Kumbuka ile hadithi juu ya mwiba katika mwili, katika 2 Wakorintho 12, na ufikiri maana yake. Alikuwa katika hatari ya kujitukuza mwenyewe, na Bwana aliyebarikiwa akaja kumnyenyekeza na kumfundisha. Kama tutaingia katika pumziko la imani, na kukaa humo; kama tutaishi maisha ya ushindi katika nchi ya Kanaani, ni lazima yaanzie hapa.
Ni lazima tuvunjwe kutoka katika kujiamini kwote na kujifunza kama Kristo kumtegemea Mungu kabisa na bila kukoma. Kuna kazi kubwa zaidi ya kufanywa katika hilo kuliko labda tunavyojua. Ni lazima tuvunjwe, na mazoea ya roho zetu lazima yawe ya kutokoma: “Mimi si kitu; Mungu ni yote. Siwezi kutembea mbele za Mungu kama inipasavyo hata saa moja isipokuwa Mungu akiutunza uzima aliounipa.”
Ni suluhisho lililobarikiwa jinsi gani Mungu alitupalo kwa maswali yetu yote na magumu yetu asemapo: “Mwanangu, Kristo ameyapitia yote kwa ajili yako. Kristo ameumba asili mpya iwezayo kumtumaini Mungu, na Kristo aliye Hai mbinguni ataishi ndani yako, na kukuwezesha kuishi maisha hayo ya kutumaini.” Ndiyo sababu Paulo alisema: “Na tunao uthabiti kama huu kwa njia ya Kristo kwa Mungu,” 2 Wakorintho 3:4. Ina maana gani hiyo? Je, ina maana kwa njia ya Kristo kama mpatanishi au mwombezi tu? Kweli, sivyo. Ina maana zaidi sana; kwa njia ya Kristo akaaye ndani yetu na kutuwezesha kumtumaini Mungu kama yeye alivyomtumaini.
Kisha huja, tatu, kifo cha Kristo. Chatufundisha nini juu ya uhusiano wa Kristo na Baba? Chatufunulia mojawapo ya masomo yaliyo na kina zaidi na mazito zaidi ya maisha ya Kristo, somo ambalo Kanisa la Kristo hulielewa kidogo mno. Twajua kifo cha Kristo maana yake nini kama upatanisho, nasi hatuwezi kamwe kukazia kupita kiasi ule ubadilishano uliobarikiwa na kumwaga damu, ambako kwako ukombozi ulipatikana kwa ajili yetu. Lakini na tukumbuke, hiyo ni nusu tu ya maana ya kifo chake.
Nusu ile nyingine ni hii: kadiri Kristo alivyokuwa mbadala wangu, aliyekufa kwa ajili yangu, ni kwa kadiri iyo hiyo yeye ni kichwa changu, ambaye ndani yake, na pamoja naye, mimi ninakufa; na kama vile aishivyo kwa ajili yangu, ili aombe, vivyo hivyo aishi ndani yangu, ili atekeleze na kuyakamilisha maisha yake. Na kama nataka kujua ni maisha gani hayo atakayoyaishi ndani yangu, ni lazima nikitazame kifo chake.
Kwa kifo chake, alithibitisha kwamba aliumiliki uzima ili tu auhifadhi, na kuutumia, kwa ajili ya Mungu. Hata kikomo cha mwisho kabisa; bila kivuli cha ubaguzi wa dakika moja, aliishi kwa ajili ya Mungu,—kila dakika, kila mahali, aliushika uzima kwa ajili ya Mungu wake tu. Na hivyo, kama mtu ataka kuishi maisha ya kutumaini kikamili, ni lazima kuwe na kujisalimisha kikamili kwa uzima wake, na mapenzi yake, hata mpaka kifoni kabisa. Ni lazima awe radhi kwenda hatua zote pamoja na Yesu, hata mpaka Kalvari.
Akiwa na umri wa miaka kumi na miwili, Yesu alisema (Rejea katika Luka 2:49): “Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?”
na tena alipokuja Yordani ili abatizwe: “Ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote.” Mathayo 3:15.
Katika maisha yake yote, alisema: “Chakula changu ndicho hiki, niyafanye mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake.” Yohana 4:34 “Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako.” Na katika uchungu wa Gethsemane, maneno yake yalikuwa: “Si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.” Luka 22:42. Mtu fulani husema: “Kwa kweli natamani kuishi maisha ya kutumaini kikamili; natamani kumwacha Kristo aishi ndani yangu; nina shauku ya kufikia ufahamu wa Kristo utakaonipa uhakika kwamba Kristo atakaa ndani yangu milele; nataka kufikia hakika kamili kwamba Kristo, Yoshua wangu, atanihifadhi katika nchi ya ushindi.” Ni kitu gani kinachohitajika kwa hilo? Jibu langu ni: “Jihadhari usije ukamtwaa Kristo wa uongo, Kristo wa kuwaziwa, Kristo wa nusu.” Na Kristo aliye kamili ni nani? Kristo aliye kamili ni yule mtu aliyesema, “Naacha vitu vyote hata kufa ili Mungu atukuzwe. Sina wazo; sina haja; nisingeishi hata dakika isipokuwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu.” Wasema mara moja, “Ni Mkristo yupi awezaye kufikia hilo?” Usiulize swali hilo, bali uliza, “Je, Kristo amelifikia, na je, Kristo aahidi kuishi ndani yangu?” Mpokee katika utimilifu wake na umwache akufundishe ni kiasi gani awezacho kukufikisha na acho awezacho kutenda ndani yako.
Usiweke masharti wala vigezo juu ya kushindwa, bali jitupe juu ya, jisalimishe kwa Kristo huyu aliyeishi maisha yale ya kujisalimisha kabisa kwa Mungu ili apate kuandaa asili mpya ambayo angeweza kukupa nawe na ndani yake apate kukufanya kama yeye mwenyewe. Ndipo utakapokuwa katika njia ambayo kwayo aweza kukuongoza mbele hata kwenye uzoefu uliobarikiwa na kumiliki kile awezacho kukutendea. Kristo Yesu alikuja ulimwenguni na amri kutoka kwa Baba kwamba auweke uhai wake, naye aliishi na wazo lile moja kifuani mwake maisha yake yote. Wazo lile moja lipasalo kuwa katika moyo wa kila mwamini ni hili: “Mimi niko katika kifo pamoja na Kristo; nimejitoa kabisa, bila kubadilika, ili kumngoja Mungu, ili Mungu apate kutimiza kusudi lake na utukufu wake ndani yangu dakika kwa dakika.”
Ni wachache wanaoufikia ushindi na furaha na uzoefu kamili mara moja. Lakini hili waweza kulifanya: Chukua mtazamo ulio sahihi na unapomtazama Yesu na kile alichokuwa, sema: “Baba, umenifanya mshiriki wa asili ya kimungu, mshiriki wa Kristo. Ni katika maisha ya Kristo yaliyotolewa kwako hata kufa, katika nguvu zake na ukaaji wake wa ndani, katika mfano wake, ndipo natamani kuyaishi maisha yangu mbele zako.”
Kifo ni jambo zito, jambo la kutisha. Bustanini, kilimgharimu Kristo uchungu mkuu kufa kifo kile, wala si ajabu kwamba si rahisi kwetu. Lakini twakubali kwa hiari tunapokwisha kuijua siri; katika kifo peke yake, uzima wa Mungu utakuja; katika kifo, mna heri isiyoelezeka. Ni hili lililomfanya Paulo awe radhi kuichukua hukumu ya kifo ndani yake mwenyewe; alimjua Mungu ayafufuaye maiti. Hukumu ya kifo iko juu ya kila kitu kilicho cha asili. Lakini je, tuko radhi kuikubali, je, twaipenda? na je, sisi si badala yake tunajaribu kuikimbia hukumu au kuisahau? Hatuamini kikamili kwamba hukumu ya kifo iko juu yetu. Kila kilicho cha asili lazima kife. Mwombe Mungu akufanye uwe radhi kuamini kwa moyo wako kwamba kufa pamoja na Kristo ndiyo njia pekee ya kuishi ndani yake. Wauliza, “Lakini je, ni lazima basi kuwe ni kufa kila siku?” Ndiyo, mpendwa; Yesu aliishi kila siku katika kutazamia msalaba, nasi, katika nguvu za maisha yake ya ushindi, tukifanywa kufanana na kifo chake, ni lazima tufurahi kila siku katika kushuka pamoja naye kuingia kifoni.
Chukua kielelezo. Chukua mwaloni wa ukuaji wa miaka mia. Mwaloni ule ulizaliwaje? Kaburini. Chembe ilipandwa ardhini, na kaburi likafanywa kwa ajili yake ili chembe ipate kufa. Ilikufa na kutoweka; ikashusha mizizi chini, na kutoa machipuko juu, na sasa mti ule umesimama kwa miaka mia. Umesimama wapi? Kaburini mwake; wakati wote katika kaburi lile lile ambamo chembe ilikufa; umesimama pale ukinyoosha mizizi yake ndani zaidi na zaidi katika ardhi ile ambamo kaburi lake lilifanywa, na hata hivyo, wakati wote, ingawa ulisimama katika kaburi lile lile ambamo ulikuwa umekufa, umekuwa ukiendelea kuwa mrefu zaidi, na wenye nguvu zaidi, na mpana zaidi, na mzuri zaidi. Na matunda yote uliyopata kuyazaa, na majani yote yaliyoupamba mwaka baada ya mwaka, uliyadaiwa kwa kaburi lile ambamo mizizi yake imetupwa na kuhifadhiwa. Vivyo hivyo, Kristo anadaiwa kila kitu kwa kifo chake na kaburi lake. Nasi, pia, twadaiwa kila kitu kwa kaburi lile la Yesu. Ee! na tuishi kila siku tukiwa na mizizi katika kifo cha Yesu. Usiogope, bali sema: “Kwa mapenzi yangu mwenyewe nitakufa; kwa hekima ya wanadamu, na nguvu za wanadamu, na kwa ulimwengu, nitakufa; kwa maana ni katika kaburi la Bwana wangu ndipo uzima wake una mwanzo wake, na nguvu zake na utukufu wake”.
Hili latuleta kwenye wazo letu lifuatalo. Kwanza, Kristo aliupokea uzima kutoka kwa Baba; pili, Kristo aliuishi kwa kumtegemea Baba; tatu, Kristo aliutoa katika kifo kwa Baba; na sasa, nne, Kristo aliupokea tena akifufuliwa na Baba, kwa nguvu za utukufu wa Baba. Ee, maana ya kina ya ufufuo wa Kristo! Kristo alifanya nini alipokufa? Alishuka katika giza na hali ya kutokuwa na msaada kabisa ya kifo.
Aliutoa uzima uliokuwa bila dhambi; uzima uliotolewa na Mungu; uzima uliokuwa mzuri na wa thamani; naye akasema, “Nitautia mikononi mwa Baba yangu ikiwa autaka;” alifanya hivyo, naye alikuwa pale kaburini akimngoja Mungu ayafanye mapenzi yake; na kwa sababu alimheshimu Mungu hata kikomo cha mwisho katika hali yake ya kutokuwa na msaada, Mungu alimwinua hata kikomo cha mwisho kabisa cha utukufu na nguvu. Kristo hakupoteza kitu kwa kuutoa uzima wake katika kifo kwa Baba. Na hivyo, kama wataka utukufu na uzima wa Mungu ukujie, ni katika kaburi la kutokuwa na msaada kabisa ndipo uzima ule wa utukufu utakapozaliwa. Yesu alifufuliwa katika wafu, na nguvu ile ya ufufuo, kwa neema ya Mungu, yaweza na itatenda ndani yetu. Mtu asitazamie kuishi maisha yaliyo sawa hata aishi maisha kamili ya ufufuo katika nguvu za Yesu.
Niseme kwa namna nyingine maana ya ufufuo huu. Kristo alikuwa na uzima mkamilifu, uliotolewa na Mungu. Baba alisema: “Je, utaniachia uzima huo? Je, utaachana nao kwa amri yangu?” Naye akaachana nao, lakini Mungu akamrudishia katika uzima wa pili ulio na utukufu mara elfu kumi kuliko uzima ule wa kidunia. Ndivyo Mungu atakavyomtendea kila mmoja wetu akubaliye kwa hiari kuachana na uzima wake. Je, umepata kuielewa? Yesu alizaliwa mara mbili.
Mara ya kwanza alizaliwa Bethlehemu. Kule kulikuwa kuzaliwa katika uzima wa udhaifu. Lakini mara ya pili, alizaliwa kutoka kaburini; yeye ni “mzaliwa wa kwanza katika wafu.” Wakolosai 1:18. Kwa sababu aliutoa uzima aliokuwa nao kwa kuzaliwa kwake kwa kwanza, Mungu alimpa uzima wa kuzaliwa kwa pili, katika utukufu wa mbinguni na kiti cha enzi cha Mungu.
Wakristo, hivyo ndivyo hasa tunavyopaswa kufanya.
Mtu aweza kuwa Mkristo mwenye bidii; mtu aweza kuwa mtenda kazi aliyefanikiwa; aweza kuwa Mkristo aliyekuwa na kiasi cha ukuaji na kuendelea mbele; lakini kama hajaingia utimilifu huu wa baraka, basi ahitaji kufikia uzoefu wa pili na wenye kina zaidi wa nguvu ya Mungu ya kuokoa; ahitaji, kama vile Mungu alivyomtoa kutoka Misri, kupitia Bahari ya Shamu, kufikia mahali ambapo Mungu ampitisha kupitia Yordani hata Kanaani. Mpendwa, tumebatizwa katika kifo cha Kristo. Ni kama tusemavyo: “Nimekuwa na maisha yaliyobarikiwa sana, nami nimekuwa na uzoefu mwingi uliobarikiwa, na Mungu amenitendea mambo mengi.” Kabla Kristo hajapata maisha yake ya pumziko na ushindi juu ya kiti cha enzi, ilimpasa kufa na kutoa yote. Fanya vivyo hivyo nawe, nawe utashiriki ushindi wake na utukufu wake. Ni tumfuatapo Yesu katika kifo chake, ndipo ufufuo wake, na nguvu, na furaha vitakuwa vyetu.
Kisha huja jambo letu la mwisho. Hatua ya tano katika njia yake ya ajabu ilikuwa: Aliinuliwa juu ili awe pamoja na Baba milele. Kwa sababu alijinyenyekeza, kwa hiyo Mungu alimwadhimisha mno (Wafilipi 2:9). Uzuri na heri ya kuadhimishwa huko kwa Yesu vipatikanapo wapi? Kwa nafsi yake ushirika mkamilifu na Baba; kwa wengine kushiriki katika nguvu za uweza wote wa Mungu. Ndiyo, hilo lilikuwa tunda la kifo chake. Maandiko yaahidi si kwamba Mungu tu, katika maisha ya ufufuo, atatupa furaha, na amani ipitayo akili zote, ushindi juu ya dhambi, na pumziko katika Mungu, bali atatubatiza kwa Roho Mtakatifu; au, kwa maneno mengine, atatujaza Roho Mtakatifu.
Yesu aliinuliwa hata kiti cha enzi cha mbinguni, ili apate kupokea huko kutoka kwa Baba Roho katika udhihirisho wake mpya, wa kimungu, ili amwagwe katika utimilifu wake. Na tunapoyafikia maisha ya ufufuo, maisha yaliyo katika imani yake yeye aliye kitu kimoja nasi, na aketiye juu ya kiti cha enzi—tunapoyafikia hayo, sisi pia twaweza kuwa washiriki wa ushirika na Kristo Yesu maadamu akaapo daima katika uwepo wa Mungu, na Roho Mtakatifu atatujaza, ili atende ndani yetu, na kutoka kwetu, kwa namna ambayo hatujapata kuijua bado.
Yesu aliupata uzima huu wa kimungu kwa kumtegemea Baba kabisa maisha yake yote, akimtegemea hata chini kabisa kifoni. Yesu aliupata uzima ule katika utukufu kamili wa Roho ili amwagwe, kwa kujitoa mwenyewe katika utii na kujisalimisha kwa Mungu peke yake, na kumwacha Mungu hata kaburini atende nguvu zake kuu; na Kristo huyo huyo ataishi maisha yake ndani yako na yangu. Ee, siri hii! Ee, utukufu huu! Naam, ee, hakika ya kimungu. Yesu Kristo anakusudia kuyaishi maisha hayo ndani yako na yangu. Wadhaniaje, je, hatupaswi kujinyenyekeza mbele za Mungu? Je, tumekuwa Wakristo miaka mingi hivi, na kutambua kidogo mno cha vile tulivyo? Mimi ni chombo kilichotengwa, kilichosafishwa, kilichomwagwa, kilichowekwa wakfu; nikisimama tu, nikingoja kila dakika Mungu, katika Kristo, kwa Roho Mtakatifu, atende ndani yangu kadiri ya utakatifu na uzima wa Mwana wake kadiri impendezavyo.
Hata Kanisa la Kristo litakaposhuka kuingia katika kaburi la kudhalilishwa, na kuungama, na aibu; hata Kanisa la Kristo litakapojilaza katika mavumbi kabisa mbele za Mungu, na kumngoja Mungu afanye jambo jipya, na jambo la ajabu, jambo lipitalo maumbile, katika kuliinua juu, litabaki dhaifu katika juhudi zake zote za kuushinda ulimwengu. Ndani ya Kanisa mna uvuguvugu ulioje, kupenda ulimwengu kulioje, kutotii kulioje, dhambi iliyoje!
Twawezaje kamwe kupigana vita hivi, au kukabiliana na magumu haya? Jibu ni: Kristo, yeye Aliyefufuka, yeye Aliyevikwa taji, yeye Mwenyezi, ni lazima aje, na kuishi ndani ya viungo mmoja mmoja. Lakini hatuwezi kulitazamia hili isipokuwa tufe pamoja naye. Nilitaja mti uliokua mrefu na mzuri hivyo, wenye mizizi yake kila siku kwa miaka mia katika kaburi ambamo chembe ilikufa. Mungu atufundishe kumngoja ili apate kutenda ndani yetu yote aliyoyatenda katika Mwana wake, hata Kristo Yesu apate kuumbwa ndani yetu! Amina!