Sura 2 · dakika 13 za kusoma
Maisha ya Nafsi
“Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.” Mathayo 16:24.
Katika mstari wa 13, twasoma kwamba Yesu, huko Kaisaria-Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” Walipojibu, akawauliza, “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” Na katika mstari wa 16, Petro akajibu na kusema, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Yesu akajibu na kumwambia katika mistari ifuatayo: “Heri wewe Simoni Bar-Yona! Kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Kisha katika mstari wa 21, twasoma jinsi Yesu alivyoanza kuwaeleza wanafunzi wake habari za kifo chake kilichokuwa kikikaribia; na katika mstari wa 22 jinsi Petro alivyoanza kumkemea, akisema, “Hasha, Bwana! Halitakupata kamwe jambo hili.” Lakini akageuka na kumwambia Petro katika mstari ufuatao, “Nenda nyuma yangu, Shetani! U kikwazo kwangu. Kwa maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.” Mara nyingi twasikia habari za maisha ya maafikiano, nalo swali huja: ni nini kilicho katika shina lake?
Ni sababu gani hata Wakristo wengi hivi wanapoteza maisha yao katika utumwa wa kutisha wa ulimwengu, badala ya kuishi katika udhihirisho na fursa na utukufu wa Mungu? Na labda swali jingine latujia: Yaweza kuwa sababu gani kwamba tuonapo jambo ni baya na kulishindania, hatuwezi kulishinda? Yaweza kuwa sababu gani kwamba tumeomba mara mia na kuweka nadhiri, na bado tungali hapa tukiishi maisha ya mchanganyiko, yaliyogawanyika, ya moyo nusu? Kwa maswali hayo mawili, kuna jibu moja: ni nafsi iliyo shina la tatizo lote.
Na kwa hiyo, mtu akiniuliza, “Nitawezaje kuondokana na maisha haya ya maafikiano?” jibu halitakuwa, “Ni lazima ufanye hili, au lile, au jambo lingine,” bali jibu litakuwa, “Maisha mapya kutoka juu, maisha ya Kristo, ni lazima yashike mahali pa maisha ya nafsi; ndipo tutakapokuwa washindi.
Sikuzote twaanza kutoka nje kwenda ndani; na tufanye vivyo hapa; na tuutafakari kutoka katika maneno haya ya andiko lile neno moja, “nafsi.” Yesu alimwambia Petro: “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.” Mathayo 16:24. Hiyo ndiyo alama ya mwanafunzi; hiyo ndiyo siri ya maisha ya Kikristo—jikane nafsi na yote yatakuwa sawa. Angalia kwamba Petro alikuwa mwamini, tena mwamini aliyefundishwa na Roho Mtakatifu. Alikuwa ametoa jibu lililompendeza Kristo ajabu: “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Usidhani kwamba jambo hilo lilikuwa la kawaida ya ajabu. Sisi twalijifunza katika katekisimu zetu; Petro hakujifunza hivyo; naye Kristo aliona kwamba Roho Mtakatifu wa Baba alikuwa amemfundisha, akasema: “Heri wewe Simoni Bar-Yona!”
Lakini angalia jinsi mtu wa kimwili angali na nguvu ndani ya Petro.
Kristo hunena juu ya msalaba wake; aliweza kufahamu habari za utukufu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”
Mathayo 16:16. Lakini, kuna jambo fulani kuhusu msalaba na kifo ambalo hakuweza kulifahamu, naye kwa kujiamini nafsi yake akathubutu kusema, “Bwana, hilo halitakuwa kamwe.” Mathayo 16:22. Naye Kristo ilimbidi kumkemea: “Nenda nyuma yangu, Shetani! U kikwazo kwangu. Kwa maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” Mathayo 16:23.
Kristo akaendelea kusema, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.” Mathayo 16:24. Na tukae juu ya neno hili moja, “nafsi.” Ni kwa kadiri tu tunavyojifunza kujua nafsi ni nini ndipo tunavyojua kwa kweli kilicho katika shina la kushindwa kwetu kote, na tunakuwa tayari kwenda kwa Kristo kwa ajili ya ukombozi.
Na tuutafakari, kwanza kabisa, tabia ya maisha haya ya nafsi, kisha tutaje baadhi ya kazi zake, kisha tuulize swali: “Twawezaje kukombolewa kutoka kwake?” Nafsi ni ile nguvu ambayo kwayo Mungu ameumba na kumjalia kila kiumbe mwenye akili. Nafsi ndiyo kitovu chenyewe cha kiumbe kilichoumbwa. Na kwa nini Mungu aliwapa malaika au mwanadamu nafsi?
Kusudi la nafsi hii lilikuwa kwamba tuilete kama chombo kitupu kwa Mungu; ili yeye aweke ndani yake uzima wake.
Mungu alinipa uwezo wa kujiamulia mwenyewe ili nipate kuileta nafsi hii kila siku na kusema: “Ee Mungu, itende kazi ndani yake; nakutolea wewe.” Mungu alitaka chombo ambamo aweze kumimina utimilifu wake wa kimungu wa uzuri, hekima, na nguvu. Aliumba ulimwengu, jua, mwezi, nyota, miti, maua, na majani, ambavyo vyote vyaonyesha utajiri wa hekima yake, uzuri, na wema. Lakini vyafanya hivyo bila kujua vitendavyo.
Kisha Mungu aliwaumba malaika wenye nafsi na utashi, ili aone kama watakuja na kujitoa kwake kwa hiari kama vyombo kwake ili aweze kuvijaza. Lakini ole! wote hawakufanya hivyo. Alikuwako mmoja aliyekuwa mkuu wa jeshi kubwa, naye akaanza kujitazama mwenyewe, kufikiri juu ya nguvu za ajabu ambazo Mungu alikuwa amemjalia, na kujifurahia mwenyewe. Akaanza kufikiri: “Je, kiumbe kama mimi ni lazima daima nibaki kumtegemea Mungu?” Akajitukuza mwenyewe, kiburi kikajidhihirisha katika kujitenga na Mungu, na wakati uo huo, akawa, badala ya malaika mbinguni, ibilisi kuzimu. Nafsi iliyomwelekea Mungu ni utukufu wa kumruhusu Muumba ajidhihirishe ndani yetu. Nafsi iliyojiepusha na Mungu ni giza lenyewe na moto wa jehanamu.
Sisi sote twaijua hadithi ya kutisha ya yaliyotokea baadaye; Mungu alimuumba mwanadamu, naye Shetani akaja katika umbo la nyoka na kumjaribu Hawa kwa wazo la kuwa kama Mungu, kuwa na nafsi inayojitegemea, akijua mema na mabaya. Na alipokuwa akisema naye, akampulizia ndani yake, katika maneno hayo, sumu yenyewe na kiburi chenyewe cha jehanamu. Roho yake mwenyewe mbaya, sumu yenyewe ya jehanamu, iliingia katika wanadamu, nayo ni nafsi hii iliyolaaniwa tuliyoirithi kutoka kwa wazazi wetu wa kwanza. Ilikuwa ni nafsi hiyo iliyouharibu na kuuletea uangamivu ulimwengu huu, na yote yaliyokuwako ya dhambi, na ya giza, na ya taabu, na ya masikitiko; na yote yatakayokuwako katika zama zisizohesabika za milele kuzimu, hayatakuwa kitu ila utawala wa nafsi, laana ya nafsi, ikimtenga mwanadamu na kumgeuza ampe Mungu wake kisogo. Na kama tutakuwa na kufahamu kikamili kile Kristo atakachotufanyia, na kuwa washiriki wa wokovu kamili, ni lazima tujifunze kuijua, kuichukia, na kuiacha kabisa nafsi hii iliyolaaniwa.
Basi, kazi za nafsi ni zipi? Ningeweza kutaja nyingi, lakini na tuchukue maneno rahisi kabisa ambayo twayatumia daima: utashi wa nafsi, kujiamini nafsi, na kujitukuza nafsi. Utashi wa nafsi, kujipendeza nafsi, ndiyo dhambi kubwa ya mwanadamu, nayo iko katika shina la maafikiano yote na ulimwengu ambayo ni uangamivu wa wengi mno. Watu hawawezi kufahamu kwa nini wasijipendeze wenyewe na kufanya mapenzi yao wenyewe. Wakristo kadhaa hawajapata kamwe kulishika wazo kwamba Mkristo ni mtu ambaye hapaswi kamwe kuutafuta utashi wake mwenyewe bali sikuzote kuyatafuta mapenzi ya Mungu, kama mtu ambaye roho ile ile ya Kristo yakaa ndani yake. “Bwana, naja niyafanye mapenzi yako, Ee Mungu wangu!” Twawaona Wakristo wakijipendeza wenyewe kwa njia elfu, na hata hivyo wakijaribu kuwa na furaha, wema, na manufaa, nao hawajui kwamba katika shina la yote hayo ni utashi wa nafsi unaowaibia baraka.
Enyi Wakristo, yatazameni maisha yenu wenyewe katika nuru ya maneno ya Yesu. Je, mwaona humo utashi wa nafsi, kujipendeza nafsi?
Kumbukeni hili: kila mara mnapojipendeza wenyewe, mnamkana Yesu. Ni mojawapo ya mawili. Ni lazima umpendeze yeye peke yake, na kuikana nafsi, au ni lazima ujipendeze mwenyewe na kumkana yeye. Kisha yafuata kujiamini nafsi, kujitumainia nafsi, jitihada za nafsi, na kujitegemea nafsi. Ni nini kilichomwongoza Petro kumkana Yesu? Kristo alikuwa amemwonya; kwa nini hakuuchukua onyo? Kujiamini nafsi. Alikuwa na hakika hivi: “Bwana, nakupenda. Kwa miaka mitatu nimekufuata. Bwana, nakana kwamba jambo hilo laweza kuwa kamwe. Mimi ni tayari kwenda gerezani na kuufia.” Kilikuwa ni kujiamini nafsi tu.
Watu wameniuliza mara nyingi, “Ni sababu gani ninashindwa? Natamani kwa bidii hivi, nami naomba kwa moyo hivi, kuishi katika mapenzi ya Mungu.” Nalo jibu langu kwa kawaida ni, “Ni kwa sababu tu unajitumainia mwenyewe.” Wao hunijibu: “La, sivyo; najua mimi si mwema, tena najua kwamba Mungu yu radhi kunilinda, nami nauweka tumaini langu katika Yesu.” Lakini najibu, “La, ndugu yangu; la; kama ungemtumaini Mungu na Yesu, usingeweza kuanguka, bali unajitumainia mwenyewe.” Na tuamini kwamba sababu ya kila kushindwa katika maisha ya Kikristo si kitu ila hiki. Naitumainia nafsi hii iliyolaaniwa, badala ya kumtumaini Yesu. Naitumainia nguvu yangu mwenyewe, badala ya nguvu za Mungu Mwenyezi. Na ndiyo sababu Kristo asema, “Nafsi hii ni lazima ikanwe”.
Kuna kujitukuza nafsi, umbo lingine la kazi za nafsi. Ahaa, kuna kiburi na wivu kiasi gani katika ulimwengu wa Kikristo; kuna uchoyo kiasi gani wa kile watu wasemacho juu yetu au wanachotufikiri; kuna tamaa kiasi gani ya sifa za wanadamu na kuwapendeza wanadamu, badala ya kuishi sikuzote mbele za uso wa Mungu, kwa wazo hili moja: “Je, mimi nampendeza yeye?” Kristo alisema, “Mwawezaje kuamini, ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamuutafuti?” Yohana 5:44. Kupokeana heshima ninyi kwa ninyi hufanya maisha ya imani yasiwezekane kabisa. Nafsi hii ilianzia jehanamu, ilitutenga na Mungu, ni mdanganyifu aliyelaaniwa atupotoshaye mbali na Yesu. Sasa laja jambo la tatu. Twapaswa kufanya nini ili kuiondoa?
Yesu atujibu katika maneno ya andiko letu: “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.” Mathayo 16:24. Liangalie vema. Ni lazima nijikane mwenyewe na kumchukua Yesu mwenyewe kuwa uzima wangu, ni lazima nichague. Kuna maisha mawili, maisha ya nafsi, na maisha ya Kristo; ni lazima nichague mojawapo ya hayo mawili. “Nifuate,” asema Bwana wetu, “nifanye mimi kuwa sheria ya kuwako kwako, kanuni ya mwenendo wako; nipe moyo wako wote; nifuate, nami nitatunza yote.” Ee rafiki, ni mabadilishano ya dhati kuwekewa mbele yetu; kuja na, tukiona hatari ya nafsi hii, pamoja na kiburi chake na uovu wake, kujitupa mbele za Mwana wa Mungu, na kusema, “Nayakana maisha yangu mwenyewe, nayachukua maisha yako yawe yangu.”
Sababu ya Wakristo kuomba na kuomba ili maisha ya Kristo yaingie ndani yao, bila mafanikio, ni kwamba maisha ya nafsi hayajakanwa. Wauliza, “Nitawezaje kuondokana na maisha haya ya nafsi?” Waijua ile mithali: yule mtu aliyekaa nyumbani hata mtu mmoja mwenye nguvu alipoingia na kumtupa nje. Ndipo mahali pale palipambwa na kufagiwa, lakini palikuwa tupu, naye akarudi na roho wengine saba wabaya kuliko yeye. Mathayo 12:43-45. Ni Kristo mwenyewe tu aingiaye awezaye kuitupa nje nafsi, na kuizuia nafsi isiingie. Nafsi hii itakaa nasi hata mwisho kabisa. Mkumbuke mtume Paulo; alikuwa ameiona njozi ya mbinguni, na asije akajitukuza mwenyewe, mwiba katika mwili ulitumwa ili kumnyenyekeza. Kulikuwa na mwelekeo wa kujitukuza mwenyewe, uliokuwa wa asili, nao ungemshinda, lakini Kristo alimwokoa kutoka kwao kwa uangalizi wake wa uaminifu kwa mtumishi wake mpendwa.
Yesu Kristo aweza, kwa neema yake ya kimungu, kuizuia nguvu ya nafsi isijidhihirishe kamwe au kupata kushinda; Yesu Kristo yu radhi kuwa uzima wa roho; Yesu Kristo yu radhi kutufundisha hivyo kumfuata, na kuwa na moyo na maisha yaliyomwelekea yeye peke yake, hata kwamba yeye atakuwa daima na sikuzote nuru ya roho zetu.
Ndipo tunapofikia yale asemayo mtume Paulo: “Si mimi tena ninayeishi, bali Kristo yu hai ndani yangu.” Kweli hizo mbili zaenda pamoja. Kwanza “Si mimi tena,” kisha, “bali Kristo yu hai ndani yangu.” Wagalatia 2:20. Mtazame Petro tena.
Kristo alimwambia, “Na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.” Mathayo 16:24.
Yesu akamwongoza mpaka Gethsemane, na huko Petro akashindwa, kwa maana alilala hapo alipopaswa kuwa macho, akikesha na kuomba; Akamwongoza mbele kuelekea Kalvari, mpaka mahali ambapo Petro alimkana. Je, huo ulikuwa uongozi wa Kristo? Msifuni Mungu, ndiyo, ulikuwa. Roho Mtakatifu alikuwa bado hajaja katika nguvu zake; Petro alikuwa bado mtu wa kimwili; roho ikitaka, lakini isiweze kushinda; mwili dhaifu. Kristo alifanya nini? Alimwongoza Petro mbele hata alipovunjika moyo katika kujidhili kabisa nafsi, na kunyenyekezwa katika vilindi vya huzuni. Yesu akamwongoza mbele, kupita kaburini, kwa kupitia Ufufuo, hata Pentekoste, naye Roho Mtakatifu akaja, na katika Roho Mtakatifu Kristo pamoja na uzima wake wa kimungu akaja, na ndipo ikawa, “Kristo yu hai ndani yangu.”
Kuna njia moja tu ya kukombolewa kutoka katika maisha haya ya nafsi. Ni lazima tumfuate Kristo, tuielekeze mioyo yetu kwake, tuzisikilize mafundisho yake, na tujitoe kila siku ili apate kuwa yote kwetu, na kwa nguvu ya Kristo, kuikana nafsi kutakuwa hali halisi yenye baraka isiyokoma. Kamwe hata kwa saa moja simtazamii Mkristo kufikia hatua ambayo aweza kusema, “Sina nafsi ya kukana;” wala kamwe hata kwa dakika moja ambayo aweza kusema, “Sihitaji kuikana nafsi.” La, ushirika huu na msalaba wa Kristo utakuwa kuikana nafsi bila kukoma kila saa na kila dakika kwa neema ya Mungu. Hakuna mahali ambapo pana ukombozi kamili kutoka katika nguvu ya nafsi hii yenye dhambi.
Twapaswa kusulubiwa pamoja na Kristo Yesu. Twapaswa kuishi pamoja naye kama wale ambao hawajapata kamwe kubatizwa katika kifo chake. Fikiri juu ya hilo! Kristo hakuwa na nafsi yenye dhambi, lakini alikuwa na nafsi na nafsi hiyo aliitoa kweli kweli hata mautini. Katika Gethsemane, alisema, “Si mapenzi yangu” Luka 22:42. Nafsi hiyo isiyo na dhambi aliitoa hata mautini ili apate kuipokea tena kutoka kaburini kutoka kwa Mungu, ikiwa imefufuliwa na kutukuzwa. Je, twaweza kutazamia kwenda mbinguni kwa njia yo yote nyingine zaidi ya ile aliyoiendea yeye? Angalia! kumbuka kwamba Kristo alishuka mpaka mautini na kaburini, nayo ni katika kifo cha nafsi, kumfuata Yesu hata mwisho kabisa, ndipo ukombozi na uzima vitakapokuja.
Na sasa, ni faida gani tunayopaswa kuipata kutokana na somo hili la Bwana? Somo la kwanza litakuwa kwamba twapaswa kuchukua wakati na kujinyenyekeza mbele za Mungu, katika wazo la nafsi hii ni nini ndani yetu; kuihesabia nafsi kila dhambi, kila upungufu, kila kushindwa, na yote yaliyokuwa aibu kwa Mungu, kisha kusema, “Bwana, hiki ndicho nilicho;” kisha na tumruhusu Yesu Kristo mbarikiwa kuyashika kabisa uongozi wa maisha yetu, katika imani kwamba uzima wake waweza kuwa wetu.
Usidhani kwamba ni jambo rahisi kuondokana na nafsi. Katika mkutano wa kujitoa, ni rahisi kuweka nadhiri, kutoa sala, na kufanya tendo la kujisalimisha, lakini kama kilivyokuwa cha dhati kifo cha Kristo pale Kalvari, kutoa kwake maisha yake ya nafsi isiyo na dhambi kwa Mungu; ni lazima kiwe cha dhati vivyo hivyo kati yetu na Mungu wetu—kuitoa nafsi hata mautini.
Nguvu ya kifo cha Kristo ni lazima ije kutenda kazi ndani yetu kila siku. Ee, fikiri tofauti iliyoje kati ya Petro yule mwenye utashi wa nafsi, na Yesu akitoa utashi wake kwa Mungu! Tofauti iliyoje kati ya kujitukuza nafsi kule kwa Petro, na unyenyekevu wa ndani wa Mwana-Kondoo wa Mungu, mpole na mnyenyekevu wa moyo mbele za Mungu na mwanadamu! Tofauti iliyoje kati ya kujiamini nafsi kule kwa Petro, na kutegemea kwa ndani kwa Yesu kwa Baba, aliposema: “Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe.”
Twaitwa kuishi maisha ya Kristo, naye Kristo huja kuishi maisha yake ndani yetu, lakini jambo moja ni lazima litangulie kutokea; ni lazima tujifunze kuichukia nafsi hii na kuikana. Kama Petro alivyomkana Kristo, sisi pia ni lazima tuseme ikane nafsi, ili Kristo Yesu apate kuwa yote katika yote. Na tujinyenyekeze katika wazo la nafsi hii imetutenda nini na jinsi ilivyomvunjia heshima Yesu; na tuombe kwa bidii sana: “Bwana, kwa nuru yako, uifichue nafsi hii; twakuomba uifichue kwetu. Yafumbue macho yetu, ili tupate kuona iliyoyatenda, na kwamba ndiyo kizuizi pekee kilichokuwa kikiturudisha nyuma.”
Na tuombe hivyo kwa bidii, kisha na tumngoje Mungu hata tutakapojitoa mbali na mazoezi yetu yote ya kidini, na mbali na uzoefu wetu wote wa kidini, na mbali na baraka zetu zote, hata tutakapomkaribia Mungu, kwa sala hii moja: “Ee Bwana Mungu, nafsi ilimgeuza malaika mkuu kuwa ibilisi, na nafsi iliwaangamiza wazazi wangu wa kwanza na kuwatoa Paradiso na kuwaingiza gizani na taabuni, na nafsi imekuwa uangamivu wa maisha yangu na sababu ya kila kushindwa; ee, uifichue kwangu.” Na ndipo yaja yale mabadilishano yenye baraka, kwamba mtu anafanywa kuwa radhi na kuweza kusema: “Mwingine ataniishia maisha, mwingine ataishi pamoja nami, mwingine atanifanyia yote,” Hakuna kingine kitakachofaa. Ikane nafsi; jitwike msalaba, ufe pamoja na Yesu; mfuate yeye peke yake.
Yeye na atupe neema ya kufahamu, kupokea, na kuishi maisha ya Kristo.