Mafundisho ya Msingi ya Imani ya Kikristo
Je, Kuna Jehanamu Halisi?

Sura 15 · dakika 21 za kusoma · dakika 27 za kusikiliza

Je, Kuna Jehanamu Halisi?

“Itampasa jehanum ya moto.”—Mathayo 5:22.

Somo langu ni “Je, Kuna Jehanamu Halisi?” Laiti mambo nitakayowahubiria yasingekuwa kweli. Mungu naye anatamani vivyo hivyo, “Bwana huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba” (2 Petro 3:9). Lakini Mungu ametuumba kwa mfano wake mwenyewe, tukiwa na asili ya kimaadili, na uwezo wa kujiamulia, na uwezo wa kuchagua; na wanadamu, wakitaka, wanaweza kuchagua giza badala ya nuru. Wanaweza kuchagua kuukanyaga chini ya miguu upendo wa Mungu uokoao. Wanaweza kuchagua kumkataa Yule aliyejeruhiwa kwa makosa yao, akachubuliwa kwa maovu yao, na ambaye adhabu ya amani yao iliwekwa juu yake; na wengine watachagua hivyo. Nasikitika kwamba watachagua hivyo. Ningekuwa radhi kufa ili kuwaokoa. Bwana Yesu alikufa kweli ili kuwaokoa. Lakini wanamdharau. Basi mambo haya nitakayoyanena usiku huu ni kweli, nami nitayahubiri ili mpate kuyajua, na ili mpate kuyahakikisha. Nitahubiri habari za jehanamu ili kuwazuia wengi wenu iwezekanavyo wasiende huko.

Je, Kuna Jehanamu Halisi? Karibu watu wote wenye akili wanaoamini kwamba kuna maisha yajayo kabisa, wanaamini kwamba wanaume na wanawake wanaotenda dhambi katika maisha haya, na kufa bila kutubu na bila kuokolewa, wataadhibiwa, angalau kwa kiasi fulani, katika maisha yale yajayo. Wanaamini kwamba ye yote atendaye dhambi hana budi kuteseka, na kwamba mateso yanayoletwa na dhambi hayataishia katika maisha haya ya sasa. Lakini, ingawa karibu watu wote wenye akili wanaoamini maisha yajayo wanaamini kwamba kuna adhabu ijayo ya namna fulani, wapo wengi wasioamini jehanamu halisi, yaani, mahali pa mateso ya kutisha yasiyoneneka. Je, kuna jehanamu? Je, kuna mahali ambapo wanaume na wanawake wasiotubu watakwenda wakati fulani baada ya kufa, na kuteseka kwa maumivu makali yanayopita mbali yale ambayo mtu ye yote huyapata hapa duniani? Wengine husema, “ndiyo,” kuna jehanamu. Wengi, hata wakiwemo wahubiri si wachache wanaodhaniwa kuwa wa imani sahihi, husema, “Hapana, jehanamu pekee ni jehanamu ya ndani iliyomo moyoni mwa mtu.” Tutalimalizaje swali hili? Tutajuaje ni nani aliye sahihi? Hatuwezi kulimaliza kama wengine wanavyojaribu kulimaliza, kwa “kuhesabu vichwa.” Walio wengi si sikuzote walio sahihi. Hasa ni kweli kwamba walio wengi si sikuzote walio sahihi katika sayansi, na katika falsafa, na katika theolojia. Kile ambacho wanasayansi walio wengi walikiamini kwa uthabiti karne moja iliyopita, wanasayansi walio wengi leo hukicheka. Kile ambacho wanafalsafa walio wengi walikiamini hapo zamani, wanafalsafa walio wengi leo hukiona kuwa upuuzi mtupu. Basi walio wengi hawawezi kuwa sahihi sikuzote. Na kwa hiyo hatuwezi kulimaliza swali hili kwa kuuliza walio wengi wanaamini nini.

Hatuwezi kulimaliza swali hili kwa kufikiri juu ya kile ambacho Mungu, kwa kuwa ndiye Mungu, lazima atende; kwa maana mwanadamu, mwenye mipaka na mpumbavu, awezaje kuhukumu kile ambacho Mungu aliye mtakatifu pasipo mipaka na mwenye hekima pasipo mipaka angetenda? Mwanadamu haonekani kuwa mpumbavu zaidi kuliko anapojaribu kufikiri na kufikia hitimisho juu ya kile ambacho Mungu asiye na mipaka lazima atende. Hoja hizi zote kuhusu jehanamu zinazojengwa juu ya kufikiri kile ambacho Mungu lazima atende, au asitende, ni za kipumbavu. Mtoto wa miaka saba hawezi kufikiri bila kukosea juu ya kile ambacho mtu mwenye hekima na mwema wa miaka hamsini atatenda; sembuse viumbe duni vya mavumbini (kama mimi na wewe tulivyo, kama walivyo wanafalsafa na wanatheolojia wasomi kuliko wote) kuweza kufikiri bila kukosea juu ya kile ambacho Mungu mwenye hekima pasipo mipaka na mtakatifu pasipo mipaka lazima atende. Hata hivyo, leo ni rahisi zaidi sana kuamini jehanamu halisi, tena jehanamu ya milele, kwa mtazamo wa kufikiri tu, kuliko ilivyokuwa miaka mitatu na nusu iliyopita. Lakini hata hivyo, hatuwezi kulimaliza swali la kama kuna jehanamu halisi kwa kufikiri, hata leo, juu ya kile ambacho Mungu, kwa kuwa ndiye Mungu, lazima atende.

Ipo njia moja tu ya kulimaliza swali hili kwa usahihi, nayo ni kuiendea Biblia na kujua inasema nini, na kusimama imara bila kusita juu ya hilo. Tumeona katika jioni hizi tatu za Jumapili zilizopita kwamba Biblia, pasipo swali lo lote la haki, ni neno la Mungu; basi lo lote ambalo Biblia inasema juu ya jambo hili, au juu ya jambo jingine lo lote, ni kweli na ni hakika. Hasa ni kweli kwamba hatuna budi kuiendea Biblia na kujua inasema nini kuhusu adhabu ijayo na raha ijayo. Yote tunayoyajua juu ya wakati ujao ni yale ambayo Biblia inatuambia. Kufikiri kote juu ya wakati ujao nje ya yale ambayo Biblia inatuambia ni kubahatisha tu; ni kupoteza wakati. Hatujui lo lote juu ya mbinguni ila yale ambayo Biblia inatuambia, wala hatujui lo lote juu ya jehanamu ila yale ambayo Biblia inatuambia. Katika jambo kama hili, wakia moja ya ufunuo wa Mungu ina thamani kuliko tani elfu za makisio ya wanadamu. Swali lote ni hili: Biblia inasema nini juu ya jehanamu? Lakini ingawa tunaitegemea Biblia peke yake kabisa, Biblia inafunua waziwazi yote tunayohitaji kujua. Biblia inatuambia mengi juu ya mbinguni, na inatuambia mengi zaidi juu ya jehanamu; tena ni jambo la kuvutia kwamba Bwana Yesu mwenyewe, ambaye mamlaka yake wengi wako tayari kuyakubali ingawa hawayakubali mamlaka ya sehemu nyingine za Biblia, ndiye anayetuambia mengi zaidi juu ya jehanamu, na kwa uwazi zaidi juu ya jehanamu. Kwa kweli, yote nitakayowaonyesha ni yale ambayo Bwana Yesu mwenyewe anasema juu ya jambo hili.

I. JEHANAMU NA KUZIMU SI KITU KIMOJA

Kwanza kabisa, ili kuisafisha njia kwa ajili ya kujifunza yale ambayo Yesu anasema juu ya jambo hili, naomba niwavute mawazo yenu kwa ukweli kwamba jehanamu na kuzimu (Hades) si kitu kimoja. Kuna mahali pengi katika Authorised Version tunapolikuta neno “Hell” (jehanamu), lakini neno hilo halimo katika Revised Version, bali neno “Hades” limewekwa badala ya neno “Hell.” Revised Version iko sahihi katika jambo hilo, kama ajuavyo kila msomi wa Kiyunani. Kuzimu si jehanamu. “Hades” ni neno la Kiyunani linalolingana na neno la Kiebrania la Agano la Kale “Sheol.” Neno hili la Kiebrania “Sheol” mara nyingi limetafsiriwa katika Authorised Version ya Agano la Kale kwa neno la Kiingereza “Grave” (kaburi). Halipaswi kamwe kutafsiriwa hivyo, kwa kuwa kamwe halimaanishi “kaburi.” Nimejitaabisha kuchunguza kila fungu ambamo neno hili la Kiebrania limetumika, na hakuna hata mahali pamoja ambapo linamaanisha “kaburi.” Lipo neno jingine kabisa la Kiebrania linaloweza kutafsiriwa hivyo ipasavyo. “Sheol,” au “Hades” ya Agano Jipya, maana yake ni mahali pa roho za waliokufa. Sheol (au kuzimu), kabla ya kuja, maisha, kifo, ufufuo, na kupaa kwa Bwana wetu, palikuwa mahali walipokwenda roho zote za wafu, wema kwa wabaya. Kabla ya kupaa kwa Kristo, ndani ya kuzimu palikuwa na Paradiso, mahali pa wafu waliobarikiwa, na Tartaros, mahali pa wafu waovu. Alipopaa, Kristo aliimwaga Paradiso ya kuzimu, akaichukua pamoja naye juu Mbinguni, kama tunavyosoma katika Waefeso 4:8, “Alipopaa juu aliteka mateka, akawapa wanadamu vipawa.” Kabla Kristo hajapaa, Paradiso ilikuwa chini; sasa iko juu. Kristo alimwambia yule mwivi aliyetubu pale msalabani, “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi,” naye Yesu mwenyewe alitufundisha kwamba alishuka “katika moyo wa nchi” (Mathayo 12:40), na yule mwivi aliyekuwa akifa alishuka pamoja naye katika Paradiso hii iliyo chini ya ardhi. Nadhani Yesu mwenyewe alikwenda pia katika sehemu ile ya kuzimu walimokuwa roho zilizopotea (1 Petro 3:18-20), lakini hiyo ni habari nyingine ambayo tutaitafakari baadaye. Lililo muhimu sasa ni kwamba yule mwivi aliyetubu, aliyekuwa akifa, alishuka chini Paradisoni; lakini baada ya kupaa kwa Bwana, Paulo alipokwenda Paradiso, “alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu, mpaka Peponi” (2 Wakorintho 12:2-4). Hakuna wafu waliobarikiwa walioachwa sasa kuzimuni, na hatimaye “mauti” na “kuzimu,” yaani, wote waliokufa ambao bado hawajafufuliwa, au kunyakuliwa juu kuingia katika Paradiso ya mbinguni, wote ambao bado wamo kuzimuni, “watatupwa katika lile ziwa la moto” (Ufunuo 20:14). “Ziwa la moto” hili, ambamo mauti na kuzimu vitatupwa, ndilo jehanamu ya kweli na ya mwisho.

II. KUTAKUWAKO JEHANAMU HALISI

Tukiisha kuisafisha njia kwa kuondoa dhana potofu iliyoenea sana katika akili za watu leo, kwamba kuzimu na jehanamu ni kitu kimoja, sasa na tuseme baadaye kwamba kutakuwako jehanamu. Biblia inasema hivyo. Yesu anasema katika Mathayo 5:22, “lakini mimi nawaambia, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimwambia ndugu yake, Raka, itampasa baraza; na mtu akimwambia, Wewe mpumbavu, itampasa jehanum ya moto.” Katika mstari wa 29 wa sura iyo hiyo Bwana Yesu anasema: “Na jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee, wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.” Na katika mstari wa 30 anasema: “Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee, wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum.” Twasoma tena yale aliyoyasema Bwana wetu Yesu katika Marko 9:45-48, “na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni heri kwako kuingia katika uzima u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili ukatupwa katika jehanum. Na jicho lako likikukosesha, liondoe; ni heri kwako kuingia katika ufalme wa Mungu u chongo, kuliko kuwa na macho mawili ukatupwa katika jehanum; ambapo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.” Mtu mmoja aweza kusema kwamba maneno haya ya Bwana wetu ni ya kitamathali. Hakuna hata dokezo dogo kabisa kwamba ni ya kitamathali. Muktadha wote unapinga yachukuliwe kuwa ya kitamathali. Ni kweli ni kosa kufasiri lugha ya kitamathali kana kwamba ni halisi, lakini vile vile haina msingi wa haki, na ni kosa vile vile, kufasiri lugha halisi kana kwamba ni ya kitamathali. Bila shaka, neno “Gehenna,” linalotafsiriwa “jehanamu,” limetokana na bonde la Hinomu, ambako zamani za kale dhabihu za wanadamu zilitolewa; lakini matumizi ya neno hilo ni halisi katika Agano Jipya lote, ingawa asili yake ni ya kitamathali. Maneno mengi yaliyo ya kitamathali kwa asili yake ni halisi katika matumizi yake, na maana ya maneno kamwe haiamuliwi kwa asili yake, bali kwa matumizi. Kwa mfano, neno letu “eclipse” (kupatwa kwa jua au mwezi) ni tamathali ya usemi. Kwa mujibu wa tamathali hiyo ni kuacha, au kupungua, au kuzimia kwa mwezi au jua, cho chote kati ya hivyo kinachopatwa. Lakini ingawa ni la kitamathali kwa asili yake, matumizi yake ya kawaida ni halisi. Matumizi yote katika Agano Jipya ya “Gehenna” au “jehanamu” ni halisi. Neno lililotafsiriwa hapa “jehanamu” linapatikana mara kumi na mbili katika Agano Jipya; mara kumi na moja kati ya hizo kumi na mbili linatumiwa na Bwana wetu Yesu mwenyewe, naye hulitumia sikuzote, kama katika mafungu niliyoyasoma hivi punde, kwa maana ya jehanamu halisi. Kama hakuna jehanamu halisi, basi Bwana wetu Yesu alikuwa ama mpumbavu ama mdanganyifu. Kwa hakika alikusudia kuwapa watu wazo kwamba kulikuwa na jehanamu halisi. Hakuna shaka juu ya hilo, ikiwa tunayaendea maneno yake ili kujua maana yake ya kawaida ni nini. Kama hakuna jehanamu halisi, basi ama Yesu alidhani kwamba ipo wakati haikuwepo, na hivyo alikuwa mpumbavu; ama alijua kwamba haikuwepo, lakini akajaribu kuwafanya watu wadhani kwamba ipo, na hivyo alikuwa mdanganyifu. Hakuna njia nyingine ila ama kuamini kwamba kuna jehanamu halisi, ama kuamini kwamba Yesu wa Nazareti, Bwana wetu na Mwokozi wetu, alikuwa mpumbavu au mdanganyifu. Najua kwamba Yesu hakuwa mpumbavu. Najua kwamba yeye alikuwa Mwana pekee wa Mungu, kwamba ndani yake ulikaa utimilifu wote wa Uungu kwa jinsi ya kimwili, kwamba yeye na Baba ni umoja, kwamba watu wote wamheshimu Mwana kama wanavyomheshimu Baba. Najua kwamba alinena maneno yenyewe ya Mungu; kwa hiyo najua kwamba kuna jehanamu halisi, kwa maana yeye alisema hivyo. Zaidi ya hayo, inafaa kuangaliwa kwamba maneno mengi haya juu ya jehanamu niliyowasomea usiku huu yametoka katika Mahubiri ya Mlimani, sehemu ile moja ya Biblia ambayo karibu watu wote hudai kuiamini. Wapo wengi wasemao kwamba hawana hakika juu ya Biblia kwa ujumla wake, lakini wanayakubali Mahubiri ya Mlimani. Haya basi, mafungu haya kwa sehemu kubwa yametoka katika Mahubiri ya Mlimani. Ama uikubali sehemu hii ya Mahubiri ya Mlimani, ama uyatupilie mbali yote kama maneno ya mpumbavu au ya mdanganyifu. Hakuna msimamo mwingine uwezekanao kwa mtu ye yote aliye radhi kuyafikiri mambo mpaka mwisho wake.

III. JE, MOTO WA JEHANAMU NI MOTO HALISI?

Swali linalofuata linalotukabili ni hili: Je, moto wa jehanamu unaotajwa katika baadhi ya mafungu tuliyoyasoma ni moto halisi? Hili si swali la msingi kama lile swali, Je, kuna jehanamu halisi? Lakini hata hivyo ni swali muhimu, nami naamini kwamba swali hilo linajibiwa waziwazi katika Biblia, tena linajibiwa waziwazi na Yesu Kristo mwenyewe. Tukigeukia tena fungu lile ambalo tumekwisha kulitaja, Mathayo 5:22, twasoma: “Lakini mimi nawaambia, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimwambia ndugu yake, Raka, itampasa baraza; na mtu akimwambia, Wewe mpumbavu, itampasa jehanum ya moto.” Haya ni maneno ya Kristo mwenyewe. Haneni tu habari za jehanamu, bali za “jehanum ya moto,” na hili nalo limetoka katika Mahubiri ya Mlimani. Katika Mathayo 18:9 Bwana Yesu anasema tena, “Na jicho lako likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe; ni heri kwako kuingia katika uzima u chongo, kuliko kuwa na macho mawili ukatupwa katika jehanum ya moto.” Na tena katika Marko 9:43-49, fungu lililosomwa dakika chache zilizopita, twasoma, “Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni heri kwako kuingia katika uzima u kilema, kuliko kuwa na mikono miwili kwenda zako jehanum, katika moto usiozimika. Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni heri kwako kuingia katika uzima u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili ukatupwa katika jehanum. Na jicho lako likikukosesha, liondoe; ni heri kwako kuingia katika ufalme wa Mungu u chongo, kuliko kuwa na macho mawili ukatupwa katika jehanum; ambapo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.” Hapa tena wengine waweza kusema kwamba moto huo ni wa kitamathali. Geukia Mathayo 13:30, 41, 42, twasoma maneno haya: “Viacheni vyote vikue pamoja hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.” Basi hapa tunao mfano, nasi tunazo tamathali; na kama hili lingekuwa ndilo pekee tulilo nalo, pangekuwa na sababu ya kusema kwamba moto huo ni wa kitamathali, kama vile mambo mengine katika mstari huo yalivyo ya kitamathali. Lakini katika mstari wa 41 na wa 42 wa sura iyo hiyo twasoma, “Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake vitu vyote vikosesho, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwa na kilio na kusaga meno.” Hapa tunayo fasiri ya mfano huo. Basi katika mifano, kama ilivyokwisha kusemwa, tunazo tamathali, lakini katika fasiri ya mifano tunayo mambo halisi yanayowakilishwa na tamathali hizo; nasi tunaona waziwazi kwamba hapa, katika fasiri kama vile katika mfano wenyewe, tunao moto. Kila kitu kingine katika mfano huo kimefasiriwa, kila kipengele cha mfano isipokuwa moto; lakini moto huo unabaki kuwa moto katika fasiri ya mfano kama vile katika mfano wenyewe. Tunakuta jambo lilo hilo katika mfano mwingine, katika mistari ya 47 hadi 50, mfano wa juya lililotupwa baharini. Hapa pia, katika fasiri ya mfano kama vile katika mfano wenyewe, tunao moto. Kila tamathali nyingine ya mfano huo imefasiriwa kwa jambo halisi inalowakilisha, lakini katika fasiri ya mfano tunao “moto.” Kwa nuru ya mambo haya hatuwezi kuukana moto halisi wa jehanamu bila kuivunja kila kanuni ya busara ya ufasiri. Zaidi ya hayo, twasoma katika Ufunuo 20:15 kwamba katika hukumu ya kile kiti kikubwa cheupe cha enzi, “na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.” Hakuna kitu katika muktadha wote kinachodokeza tamathali. Na katika sura ya 21, mstari wa 8, twasoma: “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti; hii ndiyo mauti ya pili.”

Kumbukeni zaidi ya hayo kwamba waovu katika ulimwengu wa milele si roho tu zisizo na miili. Hili liko wazi katika Agano la Kale na katika Agano Jipya pia. Twasoma katika Danieli 12:2: “Na wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, na wengine wapate aibu na kudharauliwa milele.” Basi neno hili linasema “hao walalao katika mavumbi ya nchi.” Roho huondoka kwenda kuzimu. Ni mwili unaobomoka kuwa mavumbi, na ni mwili utakaofufuliwa. Katika Agano Jipya, katika Yohana 5:28, 29, Bwana wetu ameandikwa akisema: “Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa inakuja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake, nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima; na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.” Basi si roho za watu zilizomo makaburini, bali ni miili ya watu; na fungu hili linafundisha ufufuo wa miili, ya wema na ya waovu pia. Katika 1 Wakorintho 15:22 twasoma, “Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.” Anachokizungumzia Paulo katika sura hii yote ni ufufuo wa mwili, si kutokufa kwa roho tu, nasi tunaambiwa hapa waziwazi kwamba kila mtoto wa Adamu hupata ufufuo wa mwili wake katika Kristo.

Zaidi ya hayo, katika Mathayo 5:30 Yesu anasema: “Mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee, wala mwili wako mzima usiende jehanum.” Hapa, kwa maneno yaliyo wazi kuliko yote yawezekanayo, mwili unatajwa kuwa unaingia jehanamu; na kwa namna iyo hiyo katika Mathayo 10:28, Bwana Yesu anasema: “Msiwaogope wale waiuao mwili, bali roho hawawezi kuiua; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” Kutokana na maneno haya yaliyo wazi na dhahiri ya Bwana wetu, ni wazi kama mchana kwamba katika maisha yajayo tutakuwa na miili, na kwamba miili ya waliopotea itakuwa na nafasi katika jehanamu halisi ya moto, jehanamu ya kimwili. Ingawa mateso ya mwili katika moto wa jehanamu si sura ya kutisha kuliko zote ya jehanamu, ingawa maumivu ya akili, yaani, maumivu ya majuto, maumivu ya aibu, na maumivu ya kukata tamaa, ni mabaya zaidi, mabaya zaidi pasipo kipimo; hata hivyo mateso ya kimwili, mateso ya kimwili ambayo maumivu yo yote ya duniani si kitu yakilinganishwa nayo, ni sura mojawapo ya jehanamu.

IV. JE, ZIWA LA MOTO NI MAHALI PA MATESO YANAYOHISIWA KWA UFAHAMU, AU NI MAHALI PA KUANGAMIZWA KABISA, YAANI, MAHALI PA KUTOKUWAPO, AU NI MAHALI PA KUWAPO BILA UFAHAMU?

Limebaki swali jingine moja la kujibiwa, nalo ni hili: je, ziwa la moto ni mahali pa mateso yanayohisiwa kwa ufahamu, au ni mahali pa kuangamizwa kabisa, yaani, mahali pa kutokuwapo, au ni mahali pa kuwapo bila ufahamu? Wapo wanaoamini jehanamu halisi, lakini hawaamini kwamba wale watakaotupwa humo wataendelea kuteseka humo kwa ufahamu kwa muda mrefu wo wote. Wanashikilia ama kwamba wale wanaopelekwa jehanamu huangamizwa kabisa, ama kwamba wanaendelea kuwapo humo katika hali isiyo na ufahamu. Bila shaka, hii nayo ingekuwa jehanamu ya milele, na adhabu ya milele; lakini je, hiyo ndiyo jehanamu inayofundishwa katika Biblia? Je, ziwa la moto ni mahali pa mateso yanayoendelea kuhisiwa kwa ufahamu, au ni mahali pa kuwapo bila ufahamu? Katika kulijibu swali hili, naomba niwavute mawazo yenu kwa ukweli kwamba adhabu ya waovu inatajwa katika Biblia mara nyingi zaidi kuwa “Mauti” na “Maangamizi.” Maneno haya yana maana gani katika matumizi ya Biblia?

1. Hebu tuangalie kwanza matumizi ya Biblia ya neno “Mauti.” Wengi hutuambia, tena na tena, kwamba mauti maana yake ni kutokuwapo, au angalau kuwapo bila ufahamu, na kwa hiyo hiyo ndiyo maana yake lazima iwe katika mafungu ambamo inatajwa kuwa adhabu ijayo ya wasiotubu. Lakini je, “mauti” kama inavyotumika katika Biblia maana yake ni ama kuwapo bila ufahamu, ama kuangamizwa kabisa? Angalia kwanza 1 Timotheo 5:6; hapa twasoma, “Bali yeye aishiye kwa anasa amekufa, ingawa yu hai.” Mauti hapa kwa hakika haimaanishi kutokuwapo, wala kuwapo bila ufahamu. Mwanamke aishiye kwa anasa bado yupo, tena kwa hakika yupo kwa ufahamu, lakini “amekufa.” Mauti maana yake ni kuwapo kwa namna potofu, si kutokuwapo. Ni kinyume hasa cha uzima, na uzima katika matumizi ya Agano Jipya haumaanishi kuwapo tu; maana yake ni kuwapo kwa namna iliyo sahihi, kuwapo kama Mungu, kuwapo kwa utakatifu. Maana yake ni kukwezwa, na kutukuzwa, na kufanywa kuwa kama Mungu kwa kuwapo kwetu; na mauti maana yake ni kinyume hasa cha hayo: maana yake ni kuwapo kwa namna potofu, kuwapo kulikoshushwa hadhi, kuvunjika, aibu, fedheha na kukata tamaa kwa kuwapo huko. Kwa namna iyo hiyo tunaambiwa katika Waefeso 2:1 kwamba wanadamu, mpaka watakapohuishwa, yaani, kufanywa hai, kwa nguvu za Mungu, ni “wafu kwa sababu ya makosa na dhambi.” Basi ni wazi kabisa kwamba mauti haimaanishi kutokuwapo, wala kuwapo bila ufahamu. Lakini lenye kuthibitisha zaidi kuliko hili ni ukweli kwamba Mungu mwenyewe ameieleza maana ya mauti kwa usahihi mkubwa na kwa ukamilifu katika Ufunuo 21:8: “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti; hii ndiyo mauti ya pili.” Hapa tunaambiwa waziwazi kabisa kwamba “mauti” ambayo ni matokeo ya mwisho ya kudumu katika dhambi na kutokuamini, ni fungu katika mahali pa mateso, yaani, ziwa la moto. Kwamba ziwa hili la moto ni mahali pa mateso yanayohisiwa kwa ufahamu kunawekwa wazi katika sura iliyotangulia, Ufunuo 20:10, ambapo tunaambiwa kwamba “na yule Ibilisi mwenye kuwadanganya akatupwa katika lile ziwa la moto na kiberiti, walimo yule mnyama na yule nabii wa uongo; nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.” Yule mnyama na yule nabii wa uongo walikuwa wamekwisha kukaa huko miaka elfu moja wakati Ibilisi alipotupwa katika ziwa la moto, nao walikuwa wakiteswa kwa ufahamu, bila pumziko.

2. Sasa hebu tuangalie maana ya “Maangamizi” katika Agano Jipya. Tunaambiwa na mkondo fulani wa fikra za kidini kwamba “maangamizi” maana yake ni maangamizi. Naam, “maangamizi” maana yake ni maangamizi; lakini maangamizi maana yake ni nini? Wanasema maana yake ni kuangamizwa kabisa, au kukoma kuwapo; lakini neno la Kiyunani linalotafsiriwa hivyo kamwe halina maana hiyo katika Biblia, wala hata nje ya Biblia. Katika kamusi bora kuliko zote zilizopo za Kiyunani na Kiingereza ya Agano Jipya, yaani tafsiri ya Thayer ya kazi kuu ya Grimm, tunaambiwa kwamba kitu kinaposemwa “kupotea” (na kitenzi ambacho kutokana nacho limetokea lile nomino linalotafsiriwa kwa kawaida “maangamizi” na “uharibifu” ndicho kinachotafsiriwa “kupotea”), haimaanishwi kwamba kinakoma kuwapo, bali kwamba “kimeharibiwa kiasi kwamba hakitumikii tena kazi ile kilichokusudiwa.” Zaidi ya hayo, hapa tena Mungu amekuwa mwangalifu kueleza maana ya maneno yake. Yeye mwenyewe ametupa katika Biblia maana ya “maangamizi.” Twasoma katika Ufunuo 17:8, 11: “Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko; naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu, naye aenda kwenye uharibifu. Nao wakaao juu ya nchi watastaajabu . . . Na yule mnyama aliyekuwako, naye hayuko, yeye ndiye wa nane, naye ni wa wale saba, naye aenda zake kwenye uharibifu.” Hapa tunaambiwa kwamba mnyama huenda “kwenye uharibifu.” Neno lililotafsiriwa hapa “uharibifu” ni neno lilo hilo hasa ambalo mahali pengine limetafsiriwa “maangamizi,” nalo lingepaswa kutafsiriwa hivyo hapa; ama sivyo, mahali pengine pale lingepaswa kutafsiriwa, kama hapa, “uharibifu.” Basi tukiweza kujua mnyama anaingia katika nini, ndipo tutakapojua hasa “maangamizi” maana yake ni nini, kwa maana tunaambiwa kwamba yeye aenda “kwenye maangamizi.” Katika sura ya 19 ya Ufunuo, mstari wa 20, tunaambiwa hasa mnyama huenda wapi: “Yule mnyama akakamatwa, na pamoja naye yule nabii wa uongo aliyefanya zile ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya wale walioipokea chapa ya yule mnyama, na wale walioisujudu sanamu yake; wote wawili wakatupwa wangali hai ndani ya lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.” Sasa tukitazama mbele katika sura inayofuata, mstari wa 10, ambao nimekwisha kuunukuu, twasoma: “Na yule Ibilisi mwenye kuwadanganya akatupwa katika lile ziwa la moto na kiberiti, walimo yule mnyama na yule nabii wa uongo; nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.” Tukiyaweka mafungu haya pamoja tunaona kwamba mnyama aenda “kwenye maangamizi,” na maangamizi anamoingia ni mahali katika ziwa liwakalo moto na kiberiti, ambamo kwa miaka elfu moja yumo katika mateso yanayohisiwa kwa ufahamu, na ambamo, baada ya ile miaka elfu kwisha, bado yumo humo na bado anateswa. Basi “maangamizi” yameelezwa waziwazi katika Agano Jipya kwa namna ile ile ambayo “mauti” imeelezwa, yaani, kuwa hali ya viumbe walio mahali pa mateso yanayohisiwa kwa ufahamu.

Tena katika Ufunuo 14:10, 11, twasoma kuhusu wale wamsujuduo mnyama na sanamu yake na kuipokea chapa yake katika vipaji vya nyuso zao au katika mikono yao: “Yeye naye atakunywa katika mvinyo wa ghadhabu ya Mungu, iliyotengenezwa bila kuchanganywa na maji katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo; na moshi wa maumivu yao hupanda juu milele na milele; wala hawana raha mchana na usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, wala mtu ye yote aipokeaye chapa ya jina lake.” Biblia inaweka wazi kama lugha iwezavyo kuweka wazi kwamba ziwa la moto ambamo “ye yote asiyeandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo” hutupwa, ni mahali pa mateso yanayoendelea, yanayohisiwa kwa ufahamu. Hakuna njia ya kuyakwepa mafundisho yaliyo wazi ya Neno la Mungu, isipokuwa tuzitupilie mbali Biblia zetu na kuyadharau mafundisho ya Mitume na mafundisho ya Yesu Kristo mwenyewe.

Jumapili ijayo usiku tutalichukua swali, Je, Adhabu Ijayo ni ya Milele? Lakini hatuna budi kuishia hapa usiku huu. Sherman alisema, “Vita ni jehanamu.” Bila shaka, kwa maana ile aliyoikusudia Sherman, hili ni kweli. Ni kweli zaidi sana kuhusu vita vya leo kuliko ilivyokuwa katika hatua mbaya kuliko zote na zisizo na udhuru kabisa za Vita vyetu vya Wenyewe kwa Wenyewe—Libby na Andersonville, kwa mfano, kwa upande wa Kusini, na ule mwendo wa jeshi kupitia Georgia kwa upande wa Kaskazini. Lakini hata vita vya leo, kama vinavyoendeshwa na Ujerumani katika ukatili wake wote wa kutisha, si jehanamu. Jehanamu ni ya kutisha pasipo kulinganishwa kuliko vita vinavyopiganwa sasa huko Ulaya; na jehanamu hii ya kutisha tuliyokuwa tukijifunza habari zake usiku huu ndiyo hatima ya baadhi yenu hapa katika chumba hiki, msipotubu upesi na kumpokea Bwana Yesu Kristo. Mambo mengine ya kutisha juu ya jehanamu tutayachukua Jumapili ijayo usiku, lakini tumekwisha kuona ya kutosha kumfanya kila Mkristo wa kweli aazimie kufanya kazi kwa nguvu zake zote ili kuwaokoa wengine na jehanamu hii ya kutisha. Tena tumeona ya kutosha kumfanya kila mtu mnyoofu na mwenye busara aliye hapa usiku huu aazimie kuikwepa jehanamu hii ya kutisha kwa gharama yo yote.