Sura 3 · dakika 10 za kusoma
Maisha Hayo Yafafanuliwa
Katika sura yangu iliyopita, nilijaribu kutatua swali la kama maisha ya juu zaidi ya Kikristo yana msingi katika Maandiko. Ni afadhali nayaeleze kuwa ni “maisha yaliyofichwa pamoja na Kristo katika Mungu.” Kwa hiyo sasa, naliona swali hilo limekwisha tatuliwa. Maandiko huwaahidia wale wamwaminio Yesu maisha ya pumziko kamili. Yatakuwa ushindi wa daima, unaopita hali ya kawaida ya Mkristo. Yanamwonyesha Mwokozi awezaye kutuokoa na nguvu za dhambi zetu, kama vile atuokoavyo na hatia yake.
Jambo linalofuata la kuzingatia ni hili: maisha haya yaliyofichwa ni nini hasa. Yanatofautianaje na hali nyingine za Kikristo? Yana maana ya kumwachia Bwana ayasimamie mambo yetu na kuichukua mizigo yetu, badala ya sisi kujaribu kufanya yote wenyewe. Wakristo wengi ni kama mtu aliyekuwa akijikokota barabarani chini ya mzigo mzito. Gari la kukokotwa likamfikia, naye mwendeshaji kwa wema akajitolea kumsaidia. Akakubali toleo hilo kwa furaha kubwa. Lakini alipokwisha kaa, mzigo wake ukamwelemea. Bado alikuwa ameubeba mabegani mwake. “Mbona hushushi mzigo wako?” akauliza yule mwendeshaji mwenye moyo wa huruma. “Ee!” akajibu yule mtu, “Nahisi ni jambo kubwa mno kukuomba unichukue mimi, wala nisingeweza kuwaza kukuachia uchukue na mzigo wangu pia.”
Wakristo, ambao wamejikabidhi kwa Bwana Yesu, bado wanaichukua mizigo yao. Mara nyingi wanachoka na kulemewa katika safari yao. Kwa neno “mizigo,” namaanisha kila kinachotutaabisha, kiwe cha rohoni au cha ulimwengu huu.
Namaanisha, kwanza kabisa, sisi wenyewe. Mzigo mkubwa kuliko yote tunaopaswa kuubeba maishani ni nafsi yetu. Jambo gumu kuliko yote tunalopaswa kulisimamia ni nafsi yetu. Maisha yetu ya kila siku, hisia zetu, na kasoro na tamaa zetu za pekee ndizo zinazotutaabisha kuliko yote.
Mara nyingi vinatuingiza katika utumwa na giza.
Basi, katika kuiweka chini mizigo yako, wa kwanza unayepaswa kumwondoa ni wewe mwenyewe. Ni lazima umkabidhi Mungu nafsi yako ya ndani. Hii inatia ndani majaribu yako, tabia yako, na hisia zako. Kisha, viache hapo. Yeye ndiye aliyekuumba, kwa hiyo anakuelewa na anajua jinsi ya kukusimamia, nawe ni lazima umtumaini kufanya hivyo.
Mwambie, “Tazama, Bwana, najisalimisha kwako. Nimejaribu kwa kila njia niliyoweza kuiwaza kujisimamia mwenyewe na kujifanya kuwa vile ninavyojua ninavyopaswa kuwa, lakini nimeshindwa daima.
Sasa naikabidhi kwako. Uimiliki nafsi yangu yote. Fanya kazi ndani yangu mapenzi yako yote mema. Niumbe na kunifinyanga niwe chombo kama kinavyokupendeza. Najiacha mikononi mwako. Naamini kwamba, kama ulivyoahidi, utanifanya chombo cha heshima yako. “Kilichotakaswa, kinachofaa kwa matumizi ya Bwana, na kimewekwa tayari kwa kila kazi njema.” Sasa, ni lazima upumzike, ukimtumaini kabisa. Kisha, ni lazima uweke chini kila mzigo mwingine. Afya yako, sifa yako, kazi ya Kikristo, nyumba, watoto, biashara, na watumishi. Kila kitu kinachokuhusu, cha ndani au cha nje.
Wakristo huzikabidhi nafsi zao kwa Bwana kwa ajili ya umilele daima. Wanajua, bila shaka yo yote, kwamba hawawezi kujilinda wenyewe. Lakini, mambo ya maisha haya wanayaweka katika ulinzi wao wenyewe. Wanajaribu kuyachukua wakiwa na hisia isiyokiriwa. Ni jambo kubwa kumwomba Bwana ayachukue, nao hawawezi kuwaza kumwomba achukue na mizigo yao pia.
Nilimjua mwanamke mmoja Mkristo aliyekuwa na mzigo mzito sana wa mambo ya ulimwengu huu. Ulimnyima usingizi wake na hamu yake ya chakula, na kulikuwa na hatari ya afya yake kudhoofika chini yake. Siku moja, ulihisiwa kuwa mzito hasa. Akaona kijitabu kidogo kilichoitwa “Imani ya Hannah” juu ya meza karibu naye.” Akivutwa na kichwa chake, akakichukua akaanza kusoma. Hakujua kwamba kingeleta mapinduzi katika uzoefu wake wote. Hadithi ilihusu mwanamke maskini aliyekuwa amevumilia huzuni kubwa.
Wakati mmoja, alimweleza mgeni mmoja mwenye huruma historia ya maisha yake. Mwishoni, yule mgeni akasema, “Ee, Hannah, sioni jinsi ulivyoweza kuvumilia huzuni kubwa kiasi hicho!” “Sikuivumilia,” likawa jibu la haraka. “Bwana aliivumilia kwa niaba yangu.” “Ndiyo,” akasema yule mgeni. “Hiyo ndiyo njia iliyo sawa.” “Ni lazima uyapeleke matatizo yako kwa Bwana.”
“Ndiyo,” akajibu Hannah. “Lakini, ni lazima tufanye zaidi; ni lazima tuyaache huko. Watu wengi,” akaendelea, “huipeleka mizigo yao kwake, lakini wanairudisha tena. Wanabaki na wasiwasi na huzuni kama zamani.” Bali mimi naichukua yangu, na kuiacha kwake, nami naondoka na kuisahau. Na kama wasiwasi ukirudi, naupeleka kwake tena. Nafanya hivi mara kwa mara, hata ninaposahau wasiwasi wangu na kuwa katika pumziko kamili.”
Rafiki yangu aligusika sana na mpango huu, akaazimia kuujaribu. Hakuweza kubadili maisha yake. Basi, akayapeleka kwa Bwana. Akayakabidhi kwake. Kisha, akaamini kwamba ameyapokea. Akaacha wasiwasi na mahangaiko yake yote kwake. Mahangaiko yake yalirudi mara nyingi. Akayarudisha tena. Basi, ingawa mambo yalibaki kama yalivyokuwa, nafsi yake ilipata amani kamili. Alihisi kwamba amepata siri iliyobarikiwa. Tangu wakati huo, akajaribu kutochukua tena kamwe mizigo yake mwenyewe wala kujisimamia jambo lo lote. Siri hiyo ilifanya maajabu katika mambo yake ya nje. Ilikuwa na nguvu zaidi hata katika mambo yake ya ndani, ambayo yalikuwa magumu zaidi kusimamiwa.
Alijitoa nafsi yake yote kwa Bwana. Alimtumaini kwa vyote alivyokuwa navyo. Basi, akaacha kuhangaika. Maisha yake yakawa ya furaha, kwa maana alikuwa wake. Na haya ndiyo yaliyokuwa maisha ya juu zaidi ya Kikristo! Ilikuwa siri rahisi sana aliyoigundua.
Ni hii tu. Mtu aweza kuitii amri ya Mungu katika maneno haya: “ Msijisumbue kwa neno lo lote, bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. “Wafilipi 4:6. Kama mtu angeitii, matokeo yake yangekuwa, kulingana na ile ahadi, kwamba “amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Kuna zaidi ya kusema kuhusu maisha haya yaliyofichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Yapo mambo mengi kuhusu yale ambayo Bwana Yesu huwatendea wale wanaojisalimisha kwake. Kiini cha jambo kiko hapa. Nafsi ijuayo siri hii ina ufunguo.
Utaifungua hazina ya Mungu. Natumaini nimekufanya uyatamani sana maisha haya yaliyobarikiwa.
Je, hungependa kuiondoa mizigo yako? Je, hutamani kukabidhi usimamizi wa nafsi yako isiyoweza kusimamiwa mikononi mwa yule awezaye kukusimamia? Je, hukuchoka? Je, pumziko ninalolisema halionekani tamu kwako? Je, unakumbuka lile pumziko lenye furaha uliohisi baada ya siku ya kuchosha, kabla ya kwenda kulala? Jinsi ilivyokuwa ya kupendeza kulegeza kila musuli. Kuuachia mwili wangu uwe katika utulivu na starehe kamili. Mkazo wa siku ulikuwa umekoma kwa saa chache angalau, na wafanya kazi walikuwa wameitupilia mbali kazi ya siku. Hukuhitaji tena kuinua kichwa kinachouma au mgongo uliochoka. Uliutumaini kitanda kabisa. Kilikushikilia bila kujitaabisha kwa lo lote. Ulipumzika. Lakini tuseme ungalikuwa umetilia shaka nguvu ya kitanda chako. Nawe ukaogopa kwamba kingeanguka na kukudondosha sakafuni. Je, ungeliweza kupumzika hapo? Je, kila musuli usingelikaza ili ujishikilie mwenyewe? Je, uchovu usingelikuwa mkubwa kuliko kama usingelikwenda kitandani kamwe?
Mfano huu na ukufundishe maana ya kupumzika katika Bwana. Nafsi zenu na zilale juu ya mapenzi yake matamu, kama vile miili yenu ilalavyo vitandani mwenu usiku. Legeza kila mkazo na uweke chini kila mzigo.
Acha starehe na faraja yote. Amini kwamba, akikushikilia yeye, uko salama. Kazi yako pekee ni kupumzika. Fungu lake ni kukutegemeza, naye hawezi kushindwa. Au, chukua mfano mwingine, ambao Bwana wetu ameuthibitisha: ule wa maisha ya mtoto, akasema, “Akamwita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, ‘Amin, nawaambia, msipoongoka na kuwa kama vitoto vidogo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.” Mathayo 18:2-3 Basi, tabia za mtoto mdogo ni zipi, naye huishije? Huishi kwa imani, na tabia yake kuu ni kutokujishughulisha. Maisha yake ni tumaini moja refu tangu mwisho wa mwaka hata mwisho wa mwaka. Huwatumaini wazazi wake, walezi wake, na walimu wake. Hata huwatumaini watu wasiostahili, kwa sababu ya moyo wake wa kuamini. Na tumaini lake hupokea jibu la ukarimu. Hajiandalii cho chote, lakini hupokea kila kitu. Hafanyi mipango kwa ajili ya kesho. Lakini, maisha yake yamepangwa. Njia zake hujifungua mbele yake kadiri anavyozifikia, saa kwa saa, siku kwa siku. Huingia na kutoka nyumbani mwa baba yake kwa uhuru na wepesi.
Huzifurahia hazina zake, bila kutumia cho chote kuzipata.
Tauni yaweza kupita katika njia za mji wake, lakini yeye haiangalii. Njaa, moto, na vita vyaweza kuwaka kumzunguka. Lakini, chini ya uangalizi wa baba yake, hupumzika katika amani kamili. Huishi katika wakati wa sasa, akiyapokea maisha kama yajavyo. Wakati mmoja nilitembelea nyumba moja ya utajiri iliyokuwa na mtoto pekee wa kupanga. Alipokea upendo na uangalizi wote ambao mioyo na uwezo wa wanadamu ungeweza kutoa. Nikimtazama mtoto huyo akikimbia ndani na nje, siku kwa siku, niliona picha ya hali yetu ya ajabu tukiwa watoto katika nyumba ya Baba yetu. Mtoto huyo alikuwa huru na mwepesi wa moyo, akiwa na kutojali kwa furaha kwa utoto.
Nikawaza, “Kama kuna jambo ambalo lingewahuzunisha wapendwa wake, lingekuwa ni kumwona mtoto huyu akijihangaikia nafsi yake.”
Je, si zaidi sana moyo wenye upendo wa Mungu wetu unavyopaswa kuhuzunika kwa mahangaiko ya watoto wake? Nilielewa sababu iliyomfanya Bwana wetu asisitize, “Msijisumbukie nafsi zenu.” Ni nani anayetunzwa vema kuliko wote katika kila nyumba?
Je, si watoto wadogo? Naye aliye mdogo kuliko wote, yule mtoto mchanga asiye na msaada, je, hapokei fungu kubwa kuliko wote? Mwandishi mmoja wa siku za karibuni alisema kwamba mtoto mchanga “hafanyi kazi, wala hasokoti; wala mtu humlisha, humvika, humpenda, na kumfurahia.” Hakuna afurahiaye ndani yake kuliko yeye mwenyewe.
Basi, maisha haya ya imani, ambayo ninayaandikia, yana msingi katika hili: kuwa mtoto katika nyumba ya Baba.
Mtu anaposema hivi, amesema ya kutosha. Yaweza kuyageuza maisha yote yaliyochoka na kulemewa kuwa maisha ya baraka na pumziko.
Ujasiri usio na wasiwasi wa watoto wenu wadogo na uwafundishe jinsi ya kuwa pamoja na Mungu. Huwapendeza na kuiteka mioyo yenu. Jiacheni wenyewe mikononi mwake. “Msijisumbue kwa neno lo lote, bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itailinda mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Wafilipi 4:6-7. Angalia neno ‘lo lote’ katika fungu lililotangulia. Linahusisha kila sababu iwezekanayo ya wasiwasi, ya ndani na ya nje pia. Mara nyingi tunahisi kubanwa kuamini kwamba ni wajibu wetu kuhangaikia mambo fulani.
Tutawaza, “ni sawa kuacha wasiwasi wote. Katika mambo ya kiroho, wasiwasi ni kosa. Lakini ni lazima tuhangaikie mambo fulani. Ingekuwa dhambi kutofanya hivyo. Ni lazima tuwahangaikie watoto wetu, wale tuwapendao, kanisa letu, kweli, na biashara yetu.” Ingeonyesha upungufu mkubwa wa hisia iliyo sawa kutohangaikia mambo kama haya.” Au, twaweza kuwaza, “Ndiyo, ni sawa kumtumaini Bwana na wapendwa wetu na mambo yetu. Lakini tunapaswa kuhangaikia maisha yetu ya ndani, imani yetu, majaribu yetu, na dhambi zetu. Tusipofanya hivyo, yatapuuzwa.”
Twapata jibu la mawazo kama hayo, na la mengine yote yanayofanana nayo, katika andiko letu: “Kwa sababu hiyo nawaambia, Msisumbukie maisha yenu, mtakula nini au mtakunywa nini; wala miili yenu, mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?
Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je, si bora kupita hao? Ni nani kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata saa moja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti; nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo na kesho hutupwa kalibuni, je, hatawavika ninyi zaidi, enyi wa imani haba? Kwa hiyo msisumbuke, mkisema, ‘Tule nini?’ au ‘Tunywe nini?’ au ‘tuvae nini?’’ Mathayo 6:25-31 “Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
Bali utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.
“Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.” Katika Mathayo 6:32-34, Bwana wetu anaonyesha maana ya kuishi bila wasiwasi, kwa kutuambia tuwatazame ndege wa angani na maua ya mashamba, kama mfano wa aina ya maisha angetaka tuishi. Ni lazima, bila wasiwasi wala hofu, tuwe kama ndege na maua. Ndege hufurahia uangalizi wa Mungu na hupokea chakula. Maua hukua katika jua lake. Shomoro na waseme nasi: “Mimi ni shomoro mdogo, ndege wa hali ya chini. Uhai wangu una thamani ndogo, lakini Bwana mpendwa hunijali. Sina ghala wala hazina. Sipandi wala sivuni. Hunipa fungu la shomoro, lakini kamwe mbegu ya kuweka akiba. “Najua kuna shomoro wengi. Watu huwaona kila mahali ulimwenguni. Lakini Baba yetu wa mbinguni hujua mmoja wetu aangukapo chini. “Ingawa tu wadogo, hatusahauliki kamwe. Ingawa tu dhaifu, hatuogopi kamwe. Kwa maana twajua Bwana mpendwa hulinda uhai wa viumbe alivyoviumba. “Naruka juu ya miti minene zaidi na kutua juu ya matawi mengi.” Sina ramani wala dira, lakini sipotezi njia yangu kamwe.”
Nakunja bawa langu wakati wa magharibi, po pote niwezapo kuwa. Baba huwa akiangalia daima. Hakuna dhara litakalonipata. Mimi ni shomoro mdogo tu, ndege wa hali ya chini. Lakini najua Baba ananipenda. Je, ninyi mna imani ndogo kuliko sisi?”