Siri ya Mkristo ya Maisha ya Furaha ·Jinsi ya Kuingia

Sura 4 · dakika 11 za kusoma

Jinsi ya Kuingia

Nimejaribu kulitatua swali la uhalali wa kimaandiko wa uzoefu wa maisha haya ya kumtumaini Mungu kikamilifu. Pia nimeonyesha kidogo maisha hayo ni nini. Jambo linalofuata ni jinsi ya kuyafikia na kuyaishi. Kwanza kabisa, ningesema kwamba hatupaswi kuyaangalia maisha haya yaliyobarikiwa kwa namna yo yote kama kitu tunachokifikia kwa juhudi, bali kama kipawa tunachokipokea. Hatuwezi kukistahili, hatuwezi kukwea hadi kwake, hatuwezi kukishinda; hatuwezi kufanya lo lote isipokuwa kukiomba na kukipokea. Ni kipawa cha Mungu katika Kristo Yesu. Na pale kitu kilipo kipawa, njia pekee iliyobaki kwa mpokeaji ni kukichukua na kumshukuru mtoaji. Kamwe hatusemi juu ya kipawa, “Tazama nilichokifikia,” na kujivuna kwa ustadi wetu wa kukipata. Badala yake, twasema, “Tazama alichonipa mtoaji,” nasi twajivuna kwa upendo na ukarimu wa mtoaji.

Na kila kitu katika wokovu wetu ni kipawa. Tangu mwanzo hadi mwisho, Mungu ndiye mtoaji nasi ndio wapokeaji. Ahadi zilizo tajiri kuliko zote si kwa ajili ya wale wafanyao mambo makuu. Ni kwa ajili ya wale “wapokeao wingi wa neema, na kipawa cha haki.” Ili kuyajua maisha haya ya ndani, nafsi lazima iwe tayari kupokea. Lazima itambue kabisa kwamba yatakuwa kipawa cha Mungu katika Kristo Yesu. Hatuwezi kuyapata kwa juhudi wala matendo yetu wenyewe. Jambo hili litafanya mambo yawe rahisi zaidi. Swali pekee lililobaki ni nani atakayekipokea kipawa hiki kutoka kwa Mungu, na jinsi ya kukikubali. Ningejibu kwamba huwapa tu wale nafsi ambazo zimejiweka wakfu kikamilifu. Yakupasa kukipokea kwa imani.

Kujiweka wakfu ndilo jambo la kwanza. Si kwa maana yo yote ya kisheria, wala kwa kununua au kukistahili. Bali, ni kuondoa vizuizi na kumruhusu Mungu akitoe. Ili kutengeneza chombo kizuri kutoka kwa bonge la udongo, mfinyanzi lazima awe na mamlaka kamili juu yake. Lazima libaki tulivu mikononi mwake. Ili kuifanya nafsi kuwa chombo cha heshima ya Mungu, lazima iwe “imetakaswa, ikafaa kwa matumizi ya Bwana, imewekwa tayari kwa kila tendo jema.” Lazima ijisalimishe kabisa kwake na kubaki tulivu mikononi mwake. Jambo hili ni dhahiri tangu mtazamo wa kwanza.

Wakati mmoja nilijaribu kumweleza daktari mmoja wa hospitali maana na umuhimu wa kujiweka wakfu. Lakini, alionekana kushindwa kuelewa. Hatimaye, nikamwambia, “Tuseme, katika mzunguko wako, wakutana na mtu anayekusihi umponye. Lakini, hatakuambia dalili zake zote wala kutumia dawa zako.

Angesema, ‘Niko tayari kufuata maagizo yako katika mambo mengine, kadiri yanavyoonekana mema kwangu. Lakini, katika mambo mengine, napendelea kufuata maamuzi yangu mwenyewe.’ Ungefanyaje?” niliuliza.

“Kufanya!” alijibu kwa hasira, “kufanya! Ningemwacha mara moja mtu kama huyo ajitunze mwenyewe. “Bila shaka,” aliongeza. “Nisingeweza kumfanyia lo lote. Ni lazima atii maagizo yangu.” “Basi, wagonjwa lazima watii madaktari ili wapone?” “Kutii kabisa!” lilikuwa jibu lake la msisitizo. “Na huo ndio kujiweka wakfu,” niliendelea. “Mungu lazima awe na shauri zima, bila kubakiza cho chote. Maagizo yake lazima yafuatwe kabisa.” “Naliona,” alishangaa, -- “naliona! Nami nitalifanya. Mungu lazima awe na njia yake mwenyewe kwangu tangu sasa.”

Wengine waweza kudhani “kujitoa” ni neno bora zaidi. Lakini lo lote tulitumialo, tunamaanisha kujisalimisha kabisa kwa Mungu. Twampa roho yetu, nafsi yetu, na mwili wetu. Twataka atende nasi apendavyo. Tunamaanisha kwamba lugha ya nafsi yetu katika mambo yote iseme, “Mapenzi yako yatimizwe. “Tunamaanisha kuacha kila chaguo.

Tunamaanisha maisha ya utii usioepukika. Kwa nafsi isiyomjua Mungu, jambo hili laweza kuonekana gumu. Lakini kwa wale wamjuao, ni maisha yenye furaha na pumziko kuliko yote. Yeye ni Baba yetu. Anatupenda na anajua lililo bora. Kwa hiyo, mapenzi yake ndilo jambo lililobarikiwa kuliko yote liwezalo kutujia, hali zo zote ziwe. Sielewi ni jinsi gani Shetani amefanikiwa kuyapofusha macho ya Kanisa juu ya ukweli huu. Lakini yaonekana watoto wa Mungu huyaogopa mapenzi yake kuliko kitu cho chote. Mapenzi yake mazuri, yanayopendeza yamaanisha mema tu kwa nafsi zao. Yaleta fadhili, huruma nyororo, na baraka kuu.

Natamani ningeweza tu kumwonyesha kila mtu utamu usiopimika wa mapenzi ya Mungu. Mbinguni ni mahali pa raha isiyo na kikomo. Mapenzi yake hutimizwa huko kikamilifu. Maisha yetu hushiriki raha hii kadiri mapenzi yake yanavyotimizwa ndani yake.

Anatupenda, anatupenda, na mapenzi ya upendo daima ni baraka kwa mpendwa wake. Baadhi yetu twaujua upendo.

Kama tungeweza, tungewabariki wapendwa wetu. Tungewamiminia yote yaliyo mema na mazuri maishani kama tungekuwa na uwezo wa kutimiza tamaa yetu kwa ajili yao.

Na kama hii ndiyo njia ya upendo kwetu sisi, si zaidi sana ni lazima iwe hivyo kwa Mungu wetu, aliye upendo wenyewe.

Kama tungeweza kuona, hata kwa kitambo kimoja, kina cha upendo wake, tungekimbilia kuyakumbatia mapenzi yake kama hazina yetu kuu kuliko zote. Tungejisalimisha kwayo, tukiwa tumejaa shangwe na shukrani kwa pendeleo kama hilo.

Wakristo wengi huamini kwamba Baba yao aliye mbinguni anataka kuwafanya wenye taabu na kuwaondolea baraka zao.

Hudhani, nafsi maskini, kwamba wakishikilia utashi wao wenyewe, waweza kumzuia asifanye hivyo. Naona haya kuyaandika maneno haya, na bado ni lazima tukabiliane na jambo la kweli linalofanya mamia ya maisha kuwa yenye mashaka.

Bibi mmoja Mkristo, akihisi hivi, alimweleza rafiki jinsi ilivyokuwa vigumu kusema, “Mapenzi yako yatimizwe,” na jinsi alivyoogopa kuyafanya. Alikuwa mama wa mtoto mmoja tu mdogo wa kiume, aliyekuwa mrithi wa utajiri mkubwa, na kipenzi cha moyo wake. Baada ya kueleza taabu zake, rafiki yake akasema, “Itakuwaje kama Charley wako mdogo akikukimbilia kesho?” Asema, ‘Mama, nimeamua kukuruhusu uwe na njia yako kwangu tangu sasa.’

Nitakutii daima. “Nataka ufanye unaloliona kuwa bora zaidi kwangu.”

Najua unanipenda, nami nitautumaini upendo wako. Ungehisije kwake? Je, ungejiambia mwenyewe, ‘Ahaa, sasa nitapata nafasi ya kumfanya Charley mwenye taabu?

Nitaziondoa anasa zake zote, na kuyajaza maisha yake kila jambo gumu na lisilopendeza niwezalo kulipata. Nitamlazimisha afanye mambo magumu kuliko yote. Kisha, nitampa amri za kila aina zisizowezekana.” “Lo, hapana, hapana, hapana!” alishangaa yule mama mwenye hasira. “Wajua nisingefanya hivyo. Ningemkumbatia moyoni mwangu na kumfunika kwa busu. Ningeyajaza maisha yake vitu vitamu, vilivyo bora kuliko vyote.” “Je, wewe ni mpole na mwenye upendo kuliko Mungu?” aliuliza rafiki yake. “Ahaa, hapana,” lilikuwa jibu. “Naona kosa langu. Sitaogopa kusema ‘Mapenzi yako yatimizwe,’ kwa Baba yangu wa Mbinguni, kuliko ningetaka Charley wangu aogope kuisema kwangu.””

Bora na tamu zaidi kuliko afya, au rafiki, au fedha, au umaarufu, au starehe, au ufanisi, ni mapenzi yanayostahili kupendwa ya Mungu wetu. Huangaza masaa ya giza kwa taji la nuru ya kimungu. Humwaga jua angavu juu ya njia zilizo na huzuni kuliko zote. Daima hutawala yule aliyeyafanya kuwa ufalme wake; wala hakuna lo lote liwezalo kumwendea vibaya. Pendeleo tukufu linafunguka mbele yako. Hatua ya kwanza ya kuingia maisha yaliyofichwa pamoja na Kristo katika Mungu ni kujiweka wakfu kikamilifu. Siwezi kukuacha uyaangalie kama dai gumu na kali. Ni lazima uyafanye kwa shangwe, shukrani, na hamu. Ni lazima uingie katika kile ninachokiita upande wa pendeleo wa kujiweka wakfu. Nakuhakikishia, kutokana na uzoefu uliobarikiwa, ni mahali penye furaha zaidi utakapopata kamwe.

Imani ndilo jambo linalofuata. Imani ni ya lazima kwa kupokea kipawa cho chote. Rafiki zetu waweza kutupa kitu kizima kabisa, lakini hatukimiliki hadi tuamini kwamba wametupa nasi tukidai kuwa chetu. Jambo hili ni kweli hasa kwa vipawa vilivyo vya kiakili au vya kiroho tu. Mwingine aweza kutupenda bila kikomo. Lakini, hadi tuamini, kamwe hakiwi chetu. Nadhani Wakristo wengi hulijua jambo hili kuhusu msamaha wao.

Wanajua kwamba kuhubiriwa kwa msamaha wa dhambi wa Yesu kungeweza kuendelea milele. Lakini, kamwe usingekuwa wao hadi wamedai msamaha huo. Iliwapasa kuuamini kwanza. Lakini, katika kuishi maisha ya Kikristo, hulisahau jambo hili. Hudhani kwamba, wakiisha kuokolewa kwa imani, sasa yawapasa kuishi kwa matendo. Badala ya kuendelea kupokea, sasa yawapasa kuanza kutenda. Jambo hili hufanya tangazo letu kwamba maisha yaliyofichwa pamoja na Kristo katika Mungu yanaingiwa kwa imani, lionekane kutokueleweka kabisa kwao.

Na hata hivyo imetangazwa waziwazi, kwamba “kama mlivyompokea Kristo Yesu Bwana, endeleeni kuenenda ndani yake.” Tulimpokea kwa imani, na kwa imani peke yake; hivyo yatupasa kuenenda ndani yake kwa imani, na kwa imani peke yake. Imani yetu katika maisha haya yaliyofichwa ni ile ile imani iliyotuhamisha kutoka ufalme wa giza kuja kwa Mwana wa Mungu. Ila hutegemea kitu tofauti. Wakati ule tuliamini kwamba Yesu alikuwa Mwokozi wetu kutoka hatia ya dhambi. Imani yetu ikaifanya iwe hivyo. Sasa, yatupasa kuamini kwamba yeye ni Mwokozi wetu kutoka nguvu ya dhambi. Imani yetu itaifanya iwe hivyo. Tulimtumaini kwa ajili ya kuhesabiwa haki kwetu, nako kukawa kwetu. Sasa, yatupasa kumtumaini kwa ajili ya utakaso wetu, nao utakuwa wetu pia. Wakati ule tulimpokea kama Mwokozi wakati ujao kutoka adhabu za dhambi zetu. Sasa, yatupasa kumpokea kama Mwokozi wa wakati huu kutoka utumwa wa dhambi zetu.

Wakati ule alikuwa Mkombozi wetu, sasa atakuwa Uzima wetu. Wakati ule alitupandisha kutoka shimoni. Sasa, atatuketisha katika ulimwengu wa roho pamoja naye mwenyewe. Namaanisha haya kwa msingi wa ushahidi wa uzoefu na wa vitendo pia.

Najua, kwa upande wa theolojia na wa kisheria, kwamba kila mwamini ana kila kitu wakati wa kuongoka. Lakini kwa upande wa uzoefu, hakuna kilicho chake hadi kwa imani akidai kuwa chake. “ Kila mahali litakalokanyaga wayo wa mguu wenu nimewapa ninyi, kama nilivyomwahidi Musa. “Yoshua 1:3. “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni katika ulimwengu wa roho, ndani ya Kristo,”Waefeso 1:3. Lakini, hadi tuwe na imani ndani yake, si vyetu. “Kwa kadiri ya imani yenu,” daima ndiyo mpaka na kanuni.

Lakini imani hii ninayoisema lazima iwe imani ya sasa. Hakuna imani ambayo watu huitumia katika hali ya wakati ujao iwezayo kuwa na thamani yo yote. Mtu aweza kuamini milele kwamba wakati fulani ujao dhambi zake zitasamehewa, wala kamwe hatapata amani. Yampasa kuifikia imani ya sasa, na kusema kwa imani, “Dhambi zangu sasa zimesamehewa,” kabla ya kuweza kuishi maisha mapya. Vivyo hivyo, hakuna imani itafutayo ukombozi ujao kutoka dhambini itakayoiongoza nafsi kuingia maisha tunayoyaeleza. Adui hufurahia imani hii ya wakati ujao. Anajua kwamba haina nguvu ya kufikia matokeo yo yote.

Lakini hutetemeka na kukimbia mwamini adaipo kuwa huru kutoka nguvu yake. Kwa kifupi: ili kuingia maisha haya yaliyobarikiwa ya pumziko na ushindi, ni lazima uchukue hatua mbili. Kwanza, jisalimishe yote.

Pili, uwe na imani kamili.

Taabu zako ziwe zipi, hatua hizi mbili zitakusaidia. Ukizichukua, na kushikamana nazo, zitakuongoza kwenye maisha bora zaidi ya Kikristo. Waweza kuwa na hakika ya jambo hili. Ukiweka kando kila kitu kingine, na kukazia fikira mambo haya mawili, maendeleo yako yatakuwa ya haraka. Utaifikia bandari inayotamaniwa na nafsi yako mapema kuliko unavyofikiri sasa kuwa yawezekana.

Je, ni lazima niziseme tena hatua hizo, ili pasiwe na kosa? Wewe ni mtoto wa Mungu, na wataamani kumpendeza.

Wampenda Mwokozi wako mpendwa, nawe umechoka na kuchoshwa na dhambi inayomhuzunisha. Watamani mtu wa kukuokoa kutoka nguvu yake. Yote uliyoyajaribu yameshindwa. Katika kukata tamaa, sasa wajiuliza kama, kama watu hawa wenye furaha wasemavyo, Bwana aweza na atakuokoa. Wajua moyoni mwako kwamba aweza. Kukuokoa kutoka adui zako wote ndilo kusudi lake.

Basi mtumaini. Mkabidhi shauri lako. Jisalimishe kila kitu kingine na uamini kwamba atalichukua. Ukijua yeye ni nani na aliyoyasema, dai kwamba anakupa wokovu kamili sasa. Mwanzoni, uliamini kwamba alikuweka huru kutoka hatia ya dhambi kwa sababu alisema hivyo. Sasa, amini kwamba anakuweka huru kutoka nguvu ya dhambi kwa sababu anasema hivyo. Acha imani yako sasa ishike nguvu mpya katika Kristo. Umemtumaini kama Mwokozi wako aliyekufa, sasa mtumaini kama Mwokozi wako aliye hai. Kama vile alivyokuja kukuokoa kutoka adhabu ijayo, je, hakuja pia kukuokoa kutoka utumwa wa sasa? Kama alivyokuja kuzibeba dhambi zako kwa ajili yako, amekuja kuishi maisha yake ndani yako.

Huna nguvu kabisa katika pande zote mbili. Ungeweza kujiondolea dhambi zako mwenyewe kwa juhudi ile ile. Kama vile ambavyo ungeweza sasa kufikia haki ya vitendo. Kristo, na Kristo peke yake, ni lazima akufanyie yote mawili.

Sehemu yako ni kumpa yeye jambo hilo, kisha kuamini kwamba analitenda.

Bibi mmoja ambaye sasa ni mashuhuri, akiwa katika giza kuu, alitafuta kuingia. Alimwambia rafiki aliyekuwa akijaribu kumsaidia, “Nyote mwasema, ‘Jisalimishe, na uamini.’ Lakini mimi sijui jinsi gani.” Natamani ungeifanya tu kwa sauti, ili nipate kuona jinsi uifanyavyo.” Je, ni lazima niifanye kwa sauti kwa ajili yako?

“Bwana Yesu, waweza na utaniokoa kutoka masumbufu na taabu zote za maisha yangu ya Kikristo. Ulikufa ili kuniweka huru, si wakati ujao, bali sasa na hapa.” wewe una nguvu kuliko Shetani. Waweza kunilinda, hata katika udhaifu wangu, nisianguke katika mitego yake au kumtii. Nami, Bwana, nakwenda kukutumaini unilinde. Nimejaribu kudumisha utulivu wangu, nami nimeshindwa, nikapata pigo kubwa. Sina msaada kabisa; kwa hiyo, nitakutumaini sasa. Nitajitoa kwako; sibakizi cho chote. Mwili, nafsi, na roho, najitoa mimi mwenyewe, bonge la udongo lisilofaa. Nifanye kuwa cho chote upendo wako na hekima yako vitakachochagua. Na sasa, mimi ni wako.

Wakubali ninachokitoa. Nguvu yako imeuchukua moyo wangu dhaifu, mpumbavu. Umeanza kutenda kazi ndani yangu, kutaka kwangu na kutenda kwangu, kwa kulitimiza kusudi lako jema. Nakutumaini kabisa, nami nakutumaini sasa! Je, unaogopa kuchukua hatua hii? Je, yaonekana ya ghafula mno, kama vile kuruka gizani? Je, hujui kwamba hatua za imani daima “huanguka juu ya utupu unaoonekana, lakini hukuta mwamba ulio chini”? Mtu mmoja, aliyepaswa kushuka kisimani kwa kamba, aligundua, kwa hofu yake, alipokuwa amefika mbali chini, kwamba ilikuwa fupi mno. Alikuwa amefika mwisho wake, na bado alikuwa, kwa kadirio lake, karibu futi thelathini kutoka chini ya kisima. Hakujua la kufanya. Alikosa nguvu au ustadi wa kupanda kamba, na kuiachilia kungemvunja vipande vipande.

Mikono yake ilianza kulegea. Aliamua kuiachilia na kukutana na hatima yake. Alijisalimisha kwa maangamizi, na kuilegeza mikono yake. Akaanguka! Hadi chini ya kisima ilikuwa -- inchi tatu! Kama miguu yako itakapougusa “mwamba ulio chini,” ni lazima uache kila unachokishikilia na kudondokea ndani ya Mungu. Kwa maana, hakuna njia nyingine.

Na kuifanya sasa kwaweza kukuokoa miezi na hata miaka ya taabu na uchovu. Katika ngome zote za kale za Uingereza kulikuwa na mahali palipoitwa ngome-ndani. Palikuwa mahali imara na palilindwa vizuri kuliko pote pa ngome. Palificha wanyonge na wasio na msaada wakati wa hatari. Kama ungekuwa mwanamke mwoga, asiye na msaada katika ngome iliyozingirwa, ungethubutu kujificha humo?

Je, ungeogopa kuifanya? Je, ni lazima tuogope kujificha katika nguvu ya ulinzi ya Mlinzi wetu wa Kimungu?

Yeye hasinzii wala halali. Ameahidi kutulinda katika kutoka kwetu na kuingia kwetu, sasa na hata milele.

Yaliyomo

Siri ya Mkristo ya Maisha ya Furaha Hannah Whitall Smith

Ukurasa 1 / 1 · 11 dakika zimebaki katika sura