Sura 2 · dakika 14 za kusoma
Maisha Haya Katika Maandiko
Ninapoukaribia mtaala huu wa maisha ya kweli ya Kikristo, yale maisha yaliyofichwa pamoja na Kristo katika Mungu, mawazo mengi mno yanashindania kunena hata karibu ninakosa la kusema. Nitaanzia wapi? Ni jambo gani lililo muhimu zaidi la kusema? Nitawafanyaje watu wasome na kuamini? Mada hii ni tukufu mno, nayo maneno ya wanadamu yaonekana kuwa hayana nguvu kabisa! Lakini kuna jambo ninalolazimika kulisema. Ni lazima mtu aiseme siri hii.
Kwa maana ni siri ya ushindi ule uushindao ulimwengu, ukombozi ule ulioahidiwa kutoka kwa adui zetu wote, ambao kila mtoto wa Mungu huutamani na kuuombea, lakini ambao mara nyingi na kwa jumla waonekana kuwaponyoka mikononi mwao.
Mungu na anijalie kuisema hivyo. Nataraji kila mwamini asomaye kitabu hiki ataiona kweli iliyo katika Yesu.
Nao na wayapate maisha haya matukufu kwa ajili yao wenyewe. Nina hakika kwamba kila nafsi iliyoongoka huutamani ushindi na pumziko. Wengi huhisi, nyakati fulani, kwamba ni haki yao ya kuzaliwa nayo. Je, hamwezi kukumbuka, baadhi yenu, ule ukelele wa ushindi ambao nafsi zenu zilipiga mlipoanza kwanza kumfahamu Bwana Yesu, na kupata mwonekano wa nguvu zake kuu za kuokoa? Jinsi mlivyokuwa na hakika ya ushindi wakati ule! Jinsi ilivyoonekana rahisi, kuwa washindi zaidi ya washindi, kwa yeye aliyewapenda. Chini ya uongozi wa Jemadari ambaye hakuwahi kushindwa vitani, mngewezaje kuota kushindwa?
Na bado, kwa wengi wenu, jinsi lilivyokuwa tofauti tukio lenu halisi. Ushindi umetokea, lakini ni mchache na wa kupita upesi, na kushindwa ni kwingi na kwa maafa. Hamkuishi kama mnavyohisi watoto wa Mungu wapaswavyo kuishi. Kumekuwa na kupumzika katika kuielewa kweli waziwazi, bila kusonga mbele. Kuelekea nguvu na uhai wake. Kumekuwa na kufurahia maarifa ya mambo yaliyoshuhudiwa katika Maandiko, bila kuyatambua kwa uhalisia mambo yenyewe, yakionjwa nafsini. Watu humwamini Kristo, humzungumzia, na kumtumikia, lakini hawamjui yeye kuwa ndiye uhai halisi kabisa wa nafsi, akikaa humo milele, na kujidhihirisha humo daima katika uzuri wake.
Mmempata Yesu kuwa Mwokozi wenu na Bwana wenu, nanyi mmejaribu kumtumikia na kuiendeleza kazi ya ufalme wake. Mmeyachunguza Maandiko Matakatifu kwa bidii kubwa na mmekusanya kweli nyingi za thamani kutoka humo, ambazo mmejitahidi kwa uaminifu kuzitenda, lakini pamoja na maarifa yenu yote na shughuli zenu zote katika utumishi wa Bwana, nafsi zenu zina njaa kimyakimya, nanyi mnalia tena na tena kwa ajili ya ule mkate na maji ya uzima mliyoyaona yakiahidiwa katika Maandiko kwa waaminio wote.
Katika vilindi vya mioyo yenu, mnajua kwamba tukio lenu si tukio la Kimaandiko; kwamba, kama asemavyo mwandishi mmoja wa zamani, dini yenu ni “ni maneno matupu ukilinganisha na yale ambayo Wakristo wa kwanza waliyafurahia, waliyamiliki, na kuishi ndani yake.” Nazo nafsi zenu zimezama ndani yenu, huku siku baada ya siku, na mwaka baada ya mwaka, maono yenu ya awali ya ushindi yakizidi kufifia zaidi na zaidi, nanyi mmejilazimisha kutulia katika imani ile kwamba jambo bora zaidi mwezalo kutarajia kutoka katika dini yenu ni maisha ya kushindwa na kushinda kwa kupokezana; saa moja mkitenda dhambi, na inayofuata mkitubu; na kuanza tena, ili tu kushindwa tena, na kutubu tena.
Je, ndiyo yote hayo? Je, Bwana Yesu alikuwa na haya tu akilini mwake alipoutoa uhai wake wa thamani ili kuwakomboa kutoka katika utumwa wenu mchungu na wa kikatili wa dhambi? Je, alijikusudia mwenyewe ukombozi huu wa nusunusu tu?
Je, alikusudia kuwaacha hivyo mkihangaika chini ya utambuzi wenye uchovu wa kushindwa na kukata tamaa? Je, aliogopa kwamba ushindi wa kudumu ungemvunjia heshima na kuliletea aibu jina lake?
Alipoyatoa matamko yale kuhusu kuja kwake na kazi ambayo angeifanya. Je, yalimaanisha tu yale mliyoyaonja? Je, kulikuwa na akiba iliyofichwa katika kila ahadi iliyokusudiwa kuinyima utimilifu wake kamili? Je, kila ahadi ilikuwa na akiba iliyolenga kuinyima utimilifu wake kamili? Je, “kutuokoa kutoka mikononi mwa adui zetu” kulimaanisha wachache wao tu? Je, “kutuwezesha kushinda daima” kulimaanisha nyakati fulani tu, au je, kuwa “washindi zaidi ya washindi kwa yeye aliyetupenda” kulimaanisha kushindwa na kufeli daima?
La, la, mara elfu la! Mungu aweza kuokoa kabisa kabisa, naye amekusudia kufanya hivyo. Ahadi yake, iliyothibitishwa kwa kiapo chake, ilikuwa kwamba “atatujalia sisi, ya kwamba, tukiokolewa mikononi mwa adui zetu, tumtumikie pasipo hofu, katika utakatifu na haki mbele zake, siku zote za maisha yetu.” Ni kazi kuu kuifanya, lakini Mkombozi wetu aweza kuifanya. Alikuja kuziangamiza kazi za ibilisi, nasi je, twathubutu kuota hata kwa kitambo kwamba hana uwezo au hana nia ya kutimiza makusudi yake mwenyewe?
Basi, tangu mwanzo kabisa, tulieni juu ya jambo hili moja, kwamba Bwana aweza kuwaokoa kikamilifu, sasa, katika maisha haya, kutoka katika nguvu na utawala wa dhambi, na kuwatoa kabisa mikononi mwa adui zenu. Kama hamdhani kwamba yuaweza, chunguzeni Biblia yenu, na kukusanya pamoja kila tangazo au tamko kuhusu makusudi na shabaha ya kifo chake msalabani. Mtashangaa kuona jinsi yalivyo tele.
Kila mahali na sikuzote, kazi yake yasemwa kuwa ni kutuokoa kutoka katika dhambi zetu, kutoka katika utumwa wetu, kutoka katika unajisi wetu; wala hakuna dokezo lolote litolewalo popote kwamba ukombozi huu ungekuwa ni ule wa kadiri na wa nusunusu tu ambao Kanisa hujaribu daima kuridhika nao.
Ngoja niwapeni maandiko machache kuhusu jambo hili. Malaika wa Bwana alipomtokea Yusufu katika ndoto, na kutangaza kuzaliwa kunakokuja kwa Mwokozi, alisema, “Nawe utamwita jina lake Yesu, kwa maana yeye atawaokoa watu wake na dhambi zao. “Zakaria alipokuwa “amejazwa Roho Mtakatifu” wakati wa kuzaliwa kwa mwanawe, na “akatoa unabii,” alitangaza kwamba Mungu alikuwa amewajilia watu wake ili kutimiza ile ahadi na kiapo alichokuwa amewaapia, ambayo ahadi ilikuwa, “Kwamba atatujalia sisi, ya kwamba, tukiokolewa mikononi mwa adui zetu, tumtumikie pasipo hofu, katika utakatifu na haki mbele zake, siku zote za maisha yetu.”
Petro alipokuwa akihubiri katika ukumbi wa Hekalu kwa Wayahudi waliostaajabu, alisema, “Kwenu ninyi kwanza, Mungu, akiisha kumfufua Mwanawe Yesu, alimtuma awabariki kwa kumgeuza kila mmoja wenu na maovu yake. “Paulo alipokuwa akiliambia kanisa la Efeso ile kweli ya ajabu kwamba Kristo aliwapenda sana hata akajitoa mwenyewe kwa ajili yao, aliendelea kutangaza, kwamba kusudi lake kwa kufanya hivyo lilikuwa, “ili alitakase na kulisafisha kwa kuosha kwa maji katika neno, apate kujiletea kanisa tukufu, lisilo na doa wala kunyanzi wala neno lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na waa.”
Paulo alipokuwa akitaka kumfundisha Tito, mwanawe hasa katika imani ya wote, kuhusu neema ya Mungu, alitangaza kwamba shabaha ya neema hiyo ni kutufundisha utauwa katika ulimwengu huu uliopo”; na aongeza, kuwa ndiyo sababu ya jambo hili, kwamba Kristo “alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu ili atukomboe na maovu yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wenye juhudi katika matendo mema.” Petro alipokuwa akimhimiza Mkristo, ambaye alikuwa akimwandikia, mwenendo mtakatifu na wa mfano wa Kristo, awaambia kwamba “kwa ajili ya hili mliitwa, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yetu, akiwaachia kielelezo mfuate nyayo zake: yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake”; na aongeza, “yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tukiwa tumekufa kwa dhambi, tuishi kwa haki; ambaye kwa kupigwa kwake mliponywa.”
Paulo alipokuwa akilinganisha katika Waefeso mwenendo unaomfaa Mkristo, na mwenendo wa asiyeamini, awawekea mbele yao ile kweli iliyo katika Yesu kuwa ni hii, “kwamba mvue, kwa habari ya mwenendo wenu wa kwanza.
utu ule wa kale mwovu, sawasawa na, na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu kwa kuvua tamaa zenye kudanganya.
na mvae utu ule mpya, ulioumbwa na Mungu, wenye haki na utakatifu wa kweli. “Na alipokuwa, katika Warumi 6, akijibu milele lile swali kuhusu kudumu katika dhambi, na kuonyesha jinsi lilivyokuwa geni kabisa kwa roho na shabaha yote ya wokovu wa Yesu.
Aleta hoja ya kifo chetu cha kisheria na ufufuo pamoja na Kristo kuwa ni hoja isiyoweza kujibiwa kwa ukombozi wetu wa vitendo kutoka humo, na kusema, “La hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? Au hamjui ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, ili kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.”(Warumi 6:2-3) Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti, ili kama Kristo alivyofufuliwa katika wafu kwa utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama tumeungana naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaungana naye katika mfano wa ufufuo wake. Tukijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulubishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena. (Warumi 6:4-6) Wakristo wapendwa, je, mtaupokea ushuhuda wa Maandiko kuhusu jambo hili? Maswali yale yale yaliyolisumbua Kanisa siku za Paulo ndiyo yanayolisumbua sasa: kwanza, “Je, tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi?” Na pili, “Je, twaibatilisha sheria kwa njia ya imani?” Je, jibu letu kwa haya halitakuwa lile la Paulo lenye mkazo, “Hasha”; na madai yake ya ushindi kwamba badala ya kuibatilisha “twaithibitisha sheria”; na kwamba “neno lisilowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili wenye dhambi, na kwa ajili ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili: ili sisi tusioenenda kwa kufuata mwili, bali kwa kufuata Roho, tuutimize uadilifu wa sheria.
Je, twaweza kudhani hata kwa kitambo kwamba Mungu mtakatifu, achukiaye dhambi ndani ya mwenye dhambi, yu radhi kuivumilia ndani ya Mkristo, na kwamba amepanga hata mpango wa wokovu kwa namna iwafanyayo wale waliookolewa wasiweze kuiona hatia ya dhambi wala kupata ukombozi kutoka katika nguvu zake.
Dkt. Chalmers atoa kauli iliyo dhahiri, “Ni lazima tuiondoe kabisa fedheha ile iitwayo dhambi. “Ile nyumba kuu ya kiroho ambayo Uungu hufurahia juu yake, Utawala wa ajabu, kweli, kwa dhambi kuwa yenye kuchukiza mno kwa Mungu hata kuwaweka chini ya mauti wote waliokuwa nayo, na bado wanapokubaliwa tena, uzima wakubali kwamba mtu aruhusiwe dhambi hata chini ya mauti.
Kile kilichokuwa hapo awali shabaha ya kisasi cha kuangamiza sasa kiwe shabaha ya uvumilivu unaotegemezwa na kulindwa.
Kwa kuwa sasa wameiondoa adhabu, je, wadhani kwamba Mungu asiyebadilika ameweza kuiacha chuki yake juu ya dhambi, hata kwamba mwanadamu, mwanadamu aliyeharibika na kukombolewa, sasa aweze kwa kudumu kujifurahisha chini ya mpango mpya katika kile kile kilichomwangamiza chini ya mpango wa kale? Je, Mungu aliyeipenda haki na kuuchukia uovu miaka elfu sita iliyopita, hana upendo ule ule kwa haki na chuki ile ile kwa uovu hata sasa?
Sasa navuta hewa ya fadhili zenye upendo kutoka Mbinguni, nami naweza kuenenda mbele za Mungu kwa amani na neema; je, nitajaribu tena muungano usiopatana wa kanuni mbili zenye kupingana kama ule wa Mungu anayekubali na mwenye dhambi anayedumu? Sisi, tuliookolewa kutoka maafa mabaya jinsi hii, tutawezaje kudumu katika kile kilichotutia humo hapo kwanza? Msalaba wa Kristo, kwa pigo lile lile lenye nguvu na maamuzi ambalo kwalo uliuondoa mbali nasi ule laana ya dhambi, kwa hakika pia waondoa mbali juu yetu nguvu zake na upendo wake.”
Wala si Dkt. Chalmers peke yake, bali watu wengine wengi watakatifu wa kizazi chake na wa kizazi chetu, pamoja na wa vizazi vilivyopita zamani, wameungana katika kutangaza kwamba ukombozi uliotimizwa kwa ajili yetu na Bwana wetu Yesu Kristo msalabani pale Kalvari ni ukombozi kutoka katika nguvu ya dhambi vilevile kama kutoka katika hatia yake, na kwamba yeye aweza kuwaokoa kabisa kabisa wote wamjiao Mungu kwa yeye. Mtu mmoja wa dini wa kale wa ajabu wa karne ya kumi na saba asema: “Hakuna kitu kilicho kinyume cha Mungu kama dhambi, wala Mungu hataivumilia dhambi kuitawala sikuzote kito chake bora, yaani mwanadamu.
Tunapoutafakari ukomo usio na mwisho wa nguvu ya Mungu ya kuangamiza kile kilicho kinyume chake, ni nani awezaye kuamini kwamba ni lazima ibilisi asimame na kushinda sikuzote? Halikubaliani wala halipatani na imani ya kweli kwa watu kuwa Wakristo, na bado kuamini kwamba Kristo, Mwana wa milele wa Mungu, ambaye amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani, ataivumilia dhambi na ibilisi kuwa na utawala juu yao. “Lakini mtasema hakuna mtu kwa nguvu zake zote awezaye kujikomboa mwenyewe, wala hakuna mtu awezaye kuishi pasipo dhambi. Tutasema, Amina, kwa hilo. Lakini watu wakituambia kwamba nguvu ya Mungu itusaidiapo na kutukomboa kutoka katika dhambi, kama hatuwezi kutimiza hili, basi fundisho hili hatuwezi kuliondoa; wala situmaini ninyi nanyi.
“Je, ungelikubaliana nalo kama ningekuambia kwamba Mungu hutoa nguvu zake kufanya jambo kama hilo, lakini ibilisi humzuia? Kwamba Mungu hawezi kulifanya kwa sababu ibilisi halipendi? Kwamba hakuna awezaye kuwa huru na dhambi kwa sababu ibilisi ana nguvu kiasi hicho ndani yao hata Mungu hawezi kumtoa? Fundisho hili ni la kusikitisha, lakini ni nani ambaye hajalihubiri? Lasema, kwa maneno dhahiri, kwamba, ijapokuwa Mungu huingiza nguvu zake, haiwezekani, kwa sababu ibilisi ameiotesha dhambi kiasi hicho kama mwanadamu. Je, mwanadamu si kiumbe cha Mungu, na je, hawezi kumfanya upya, na kuitoa dhambi ndani yake? Kama mkisema mwanadamu huiotesha dhambi, nakubali, lakini si kwa kiwango kilekile.
Yesu Kristo ameingia kwa kina ndani ya mzizi wa asili ya mwanadamu hata amepokea nguvu za kumwangamiza ibilisi na kazi zake, na kumrejesha na kumkomboa mwanadamu katika haki na utakatifu. Ama sivyo ni uongo kwamba ‘aweza kuwaokoa kabisa kabisa wote wamjiao Mungu kwa yeye.’ Yatupasa kuitupa Biblia kama tukisema kwamba Mungu hawezi kumtoa mwanadamu katika dhambi.
“Twajua,” aendelea kusema, “rafiki zetu wanapokuwa utumwani, kama vile Uturuki, au mahali penginepo, hulipa fedha zetu kwa ukombozi wao; lakini hatutalipa fedha zetu kama wangaliwaweka bado katika minyororo yao.
Je, mtu yeyote hangalijiona amedanganywa kulipa hivyo? Angalisemwa kuwa amefanya mapatano ya ukombozi wao kwa fedha nyingi.
Je, ajikomboe mwenyewe na kuitwa mateka aliyekombolewa, lakini bado avae minyororo yake? Kwa muda gani? Maadamu ana siku ya kuishi. “Haya ni kwa ajili ya miili, lakini sasa nazungumza habari za nafsi. Ni lazima nimfanye Kristo kwangu.
.ukombozi, na aniokoe kutoka utumwani. Je, mimi ni mfungwa mahali popote? Ndiyo, yeye atendaye dhambi, alisema Kristo, ni mtumwa wa dhambi, ni mtumwa wa dhambi. Kama umetenda dhambi, wewe ni mtumwa, mateka ampasaye kukombolewa kutoka utumwani.
Ni nani atakayelipa bei kwa ajili yangu? Mimi ni maskini; sina kitu; siwezi kujikomboa mwenyewe; ni nani atakayelipa bei kwa ajili yangu? Yupo mmoja aliyelipa bei kwa ajili yangu. Hilo ni jema; hii ni habari njema, basi nataraji nitatoka utumwani mwangu. Jina lake ni nani? Je, aitwaye Mkombozi? Basi, natarajia faida ya ukombozi wangu, na kwamba nitatoka utumwani mwangu. La, wasema wao, ni lazima udumu katika dhambi maadamu unaishi.
Nini! Je, hatutajikomboa kamwe wenyewe? Je, moyo huu wenye ukaidi na utashi huu wenye upotovu ni lazima udumu sikuzote?
Je, niwe mwamini, na bado nisiwe na imani ifikiayo utakaso na maisha matakatifu? Je, hakuna ushindi wa kupatikana, hakuna kuupata ushindi juu ya dhambi? Je, ni lazima inishinde maadamu ninaishi? Basi, ni Mkombozi wa namna gani huyu, au nina faida gani katika maisha haya, ya ukombozi wangu?”
Ungeweza kunukuu vipande vinavyofanana kutoka kwa Marshall, Romaine, na wengine wengi vinavyoonyesha kwamba fundisho hili si geni katika Kanisa, ingawa huenda limesahaulika sana na kizazi cha sasa cha waaminio.
Ni ile ile hadithi ya kale iliyojaza kwa nyimbo za ushindi maisha ya kila siku ya watakatifu wengi wa Mungu katika enzi zote; na sasa, twaitangaza upya kwa furaha isiyoelezeka ya nafsi zilizochoka na kulemewa. Basi usiikatae, msomaji mpendwa, hata utakapofanya uchunguzi wa kina kwa njia ya maombi.
Yachunguze Maandiko upate kuona kama mambo haya ndivyo yalivyo. Mwombe Mungu awafumbue macho ya ufahamu wenu kwa Roho wake mpate kujua “ na ni ukuu gani usiopimika wa uweza wake kwetu sisi tuaminio, kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uwezo wake. Ambao aliutenda katika Kristo alipomfufua katika wafu na kumketisha mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho, ”(Waefeso 1:19-20), Na mtakapoanza kupata mwonekano hafifu wa nguvu hizi, jifunzeni kuyaacha kabisa udhaifu wenu wenyewe, na, mkiweka shauri lenu mikononi mwake, mtumainini yeye awaokoe.
Katika Zaburi 8:6, andiko latuambia kwamba Mungu alimfanya mwanadamu “atawale kazi za mikono yako; umeweka vitu vyote chini ya miguu yake,.” Utimilifu wa jambo hili u katika 2 Wakorintho 2:14, ambapo mtume apaza sauti, “Lakini Mungu na ashukuriwe, ambaye katika Kristo hutuongoza daima katika msafara wa ushindi, na kwa kupitia sisi hueneza harufu nzuri ya kumjua yeye kila mahali.”
Kama mtengenezaji wa mashine angetangaza kwamba ameitengeneza ili itimize kusudi fulani, na ikiwa alipoijaribu ingeshindwa kutimiza kusudi hilo, sote tungesema juu ya mtengenezaji huyo kwamba ni mlaghai.
Basi hatutathubutu kudhani kwamba haiwezekani kwa kiumbe ambacho Mungu amekiumba, kutimiza kusudi lililotangazwa ambalo kwa ajili yake kiliumbwa. Hasa Maandiko yalipojaa kauli kwamba Kristo ameliwezesha jambo hilo. Kitu pekee kiwezacho kuzuia ni kiumbe chenyewe kushindwa kutenda kwa upatano na mipango ya Muumba wake, na kama upungufu huu wa upatano waweza kuondolewa, basi Mungu aweza kutenda kazi.
Kristo alikuja ili alete upatanisho kati ya Mungu na mwanadamu, ambao ungemfanya iwezekane Mungu kutenda kazi ndani ya mwanadamu kutaka na kutenda kwa kulitimiza kusudi lake jema.
Kwa hiyo na tuwe na moyo mkuu; kwa maana kazi ambayo Kristo ameiingia anaweza na yu radhi kuitimiza. Basi na “tufuate nyayo za imani ya baba yetu Ibrahimu,” ambaye “hakusita katika ahadi ya Mungu kwa kutokuamini; bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; akijua hakika ya kwamba yeye aliyeahidi aweza kutimiza hilo pia.”