Sura 1 · dakika 11 za kusoma
Upande wa Mungu na Upande wa Mwanadamu
Katika kuzungumzia maisha na mwenendo wa imani, nataka kushughulikia kutoelewana kwa kawaida ambako mara nyingi huzuia ufahamu ulio wazi wa somo hili. Kutoelewana huku hutokana na tabia ya kukazia upande mmoja tu wa jambo bila kuuzingatia upande mwingine. Matokeo yake, watu mara nyingi huona mtazamo ulioelezwa vizuri wa upande mmoja lakini hupuuza uwiano upatikanao kwa kuangalia pande zote mbili pamoja. Haishangazi kwamba jambo hili laweza kusababisha mtazamo uliopotoka wa jambo zima.
Somo hili lina pande mbili zenye nguvu na tofauti, na, kama masomo mengine yote, haliwezi kueleweka kikamilifu isipokuwa pande hizi zote mbili zishikiliwe machoni daima. Bila shaka namaanisha upande wa Mungu na upande wa mwanadamu; au, kwa maneno mengine, sehemu ya Mungu katika kazi ya utakaso, na sehemu ya mwanadamu. Pande hizi ni tofauti sana, tena zinazoonekana kuwa kinyume. Lakini hazipingani. Ila, kwa mtazamaji wa juu juu, nyakati nyingine huonekana kana kwamba zinapingana.
Jambo hili nilielezewa kwa namna ya kushangaza siku si nyingi zilizopita. Waalimu wawili wa maisha haya ya juu zaidi ya Kikristo walifanya mikutano mahali pamoja, kwa nyakati zilizopishana. Mmoja alinena tu juu ya sehemu ya Mungu katika kazi, na mwingine alikazia tu sehemu ya mwanadamu. Walikuwa na uelewano mkamilifu wao kwa wao. Walijua kwamba kila mmoja alifundisha upande tofauti wa ukweli mmoja mkuu. Sehemu kubwa ya wasikilizaji wao pia walielewa jambo hili. Lakini, ilikuwa tofauti kwa baadhi ya wasikilizaji. Mwanamke mmoja alisema, kwa mkanganyiko mkubwa, “Siwezi kuelewa jambo hili hata kidogo.” Wahubiri wawili wanajaribu kufundisha ukweli uleule. Hata hivyo, waonekana kupingana wao kwa wao.”
Nilihisi mkanganyiko wake. Huwasumbua watafutaji wengi wanyoofu wa ukweli. Tuseme marafiki wawili watembelee jengo maarufu, kisha warudi nyumbani kulieleza. Mmoja ameuona upande wa kaskazini tu, na mwingine upande wa kusini tu.
Wa kwanza asema, “Walilijenga jengo kwa namna fulani, nalo lina ghorofa na mapambo fulani na fulani.” “La, hasha!” asema yule mwingine, akimkatiza. “Umekosea kabisa. Mimi nililiona jengo.
Walilijenga kwa namna tofauti kabisa.
Mapambo yake na ghorofa zake vilikuwa hivi na hivi.” Yaelekea mabishano makali yangetokea juu ya maelezo yao.
Kisha, marafiki hao wawili wangegundua kwamba walikuwa wameeleza pande tofauti za jengo. Kila mmoja angepatana mara moja.
Nataka kuwa wazi juu ya pande hizo mbili katika jambo hili. Kukazia upande mmoja, bila kuuona mwingine, kutazua mitazamo ya uongo juu ya ukweli. Kwa kifupi, ningesema kwamba sehemu ya mwanadamu ni kuamini na sehemu ya Mungu ni kutenda kazi. Majukumu haya mawili ni tofauti, lakini si lazima yagongane.
Namaanisha hivi. Yampasa mtu fulani kufanya kazi fulani. Mungu atatuokoa kutoka katika nguvu ya dhambi naye atatufanya wakamilifu katika kila kazi njema ili kutenda mapenzi yake. “Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiutazama utukufu wa Bwana kama katika kioo, tunageuzwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kutoka kwa Bwana aliye Roho.” (2 Wakorintho 3:18). Ni lazima tujigeuze kwa kuzifanya upya nia zetu. Ndipo tutakapoweza kuyathibitisha mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kukubalika, na makamilifu. Kazi halisi yapasa kutendwa ndani yetu na juu yetu. Ni lazima tuzishinde dhambi zituzingazo. Ni lazima tuzishinde tabia mbaya. Ni lazima tu’oe mielekeo na hisia zisizofaa. Ni lazima tusitawishe tabia na hisia takatifu.
Mabadiliko ya hakika yapasa kutokea. Basi angalau ndivyo Biblia inavyofundisha. Sasa lazima mtu fulani afanye jambo hili.
Ama sisi wenyewe tulifanye, au mwingine atufanyie. Wengi wetu tulijaribu kulifanya sisi wenyewe mwanzoni, tukashindwa. Kisha, tukajifunza kutokana na Maandiko na uzoefu wetu wenyewe kwamba hatuwezi kulifanya.
Lakini, Bwana Yesu Kristo alikuja kulifanya. Atawafanyia wote wanaomtumaini kikamilifu.
Basi katika hali hizi, ni ipi sehemu ya mwamini, na ni ipi sehemu ya Bwana? Mwamini aweza kuamini tu. Bwana, ambaye humtumaini, hufanya kazi aliyokabidhiwa. Kuamini na kutenda ni mambo yaliyo kinyume, na mara nyingi yanayopingana. Lakini, je, yanapingana katika jambo hili? Ni dhahiri sivyo, kwa sababu pande mbili tofauti zahusika. Ni ukinzani kusema kwamba upande mmoja katika shughuli ulikabidhi jambo lake kwa mwingine, lakini yeye mwenyewe akalishughulikia. Bali, tusemapo kwamba upande mmoja waumtumaini mwingine katika shughuli, na huyo mwingine akalifanya, twatoa kauli rahisi, yenye upatano.
Hatutoi tatizo gumu. Katika maisha haya ya juu zaidi, sehemu ya mwanadamu ni kuamini, na ya Mungu ni kulifanya jambo alilokabidhiwa. Mhubiri, akinena kwa niaba ya mwanadamu, aweza kuzungumza tu juu ya kujisalimisha na kuamini. Ndilo tu awezalo mwanadamu kufanya. Sote twakubaliana juu ya hili. Hata hivyo, wahubiri kama hao mara nyingi hukosolewa. Maneno yao yadokeza kuwa hakuna sehemu nyingine. Basi, twaamini tu. Na kilio hutokea kwamba fundisho hili la imani laondoa hali halisi zote. Nafsi zaambiwa ziamini, na basi ndiyo hiyo. Kisha huketi katika aina fulani ya kiti cha starehe cha kidini, wakiota ndoto maisha yasiyo na matokeo halisi.
Kutoelewa huku, bila shaka, hutokana na kushindwa kuwasiliana. Ama mhubiri alipuuza kueleza, au msikilizaji alishindwa kusikia, upande ule mwingine wa jambo. Nao ni huu, kwamba tuaminipo, Bwana hutenda kazi. Yeye hufanya mengi, si sisi. Kuamini kwetu huleta matokeo. Bwana wetu hulishughulikia lile tulilomkabidhi naye hulitimiza. Sisi hatutendi, bali yeye hutenda. Jambo hili hufanya kazi yake iwe na matokeo zaidi.
Kitendawili juu ya kuhubiri imani hutoweka jambo hili likiwa wazi. Lakini wakosoaji humlenga mhubiri anayekazia mtazamo wa Mungu kwa sababu nyingine. Yeye hanenei juu ya kuamini, kwa maana sehemu ya Bwana si kuamini, bali ni kutenda kazi. Bwana hulifanya jambo alilokabidhiwa. Yeye huiadibisha na kuizoeza nafsi kwa mazoezi ya ndani na maongozi ya nje.
Huvitumia vyote vya hekima yake na upendo wake katika kuisafisha na kuitakasa nafsi hiyo.
Huyafanya maisha yote ya mtu na hali zake vitumike kwa kusudi moja: kumkuza katika neema na kumfanya afanane na Kristo, saa kwa saa.
Humpitisha katika mchakato wa kubadilishwa, kama hali yake inavyohitaji. Huyafanya kuwa halisi na ya kujaribiwa yale matokeo ambayo nafsi imeyaamini. Kwa mfano, tumethubutu, kulingana na agizo lililo katika Warumi 6:11 “Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi, bali mlio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu.” kwa imani kujihesabu kuwa tumekufa kwa dhambi. Bwana hulifanya jambo hili kuwa halisi. Hutuongoza hata ushindi juu ya nafsi kwa nidhamu yake ya kila siku, ya maongozi yake. Kujihesabu kwetu kwaweza kupatikana tu kwa sababu Mungu hukufanya kuwa halisi.
Hata hivyo, mhubiri anayekazia upande huu wa vitendo hushtakiwa kuwa hana imani. Husemwa kwamba anahimiza utakaso wa taratibu kwa matendo na kwamba anatoa kazi isiyowezekana.
Basi, utakaso ni hatua ya ghafula ya imani na pia ni mchakato wa taratibu wa matendo. Sisi twauona kuwa hatua; Mungu auona kuwa mchakato. Kwa hatua ya imani, twaingia ndani ya Kristo; kwa mchakato, twafanywa tumkulie yeye katika mambo yote.
Kwa hatua ya imani, twamtumaini yule Mfinyanzi wa Kimungu. Kwa mchakato wa taratibu, hutufanya kuwa chombo kwa heshima yake, kifaacho kwa matumizi yake, na kilicho tayari kwa kila kazi njema. Ili kutoa mfano: nitamweleza mwanafunzi mpya jinsi ya kugeuza bonge la udongo liwe chombo kizuri. Kwanza namweleza sehemu ya udongo katika jambo hili. Nilisemalo ni hili tu: mfinyanzi huuweka udongo mikononi mwake. Kisha udongo hulala bila kutenda, ukijitiisha kwa kila mzunguko na mgeuzo wake.
Kwa kweli hakuna jingine liwezalo kusemwa juu ya sehemu ya udongo. Lakini je, msikilizaji wangu aweza kubisha kutokana na hili kwamba hakuna jingine litendwalo, kwa sababu nasema kuwa hiki ndicho tu udongo uwezacho kufanya? Kama ni msikilizaji mwenye akili, hataota kufanya hivyo, bali atasema, “Naelewa. Hivi ndivyo udongo unavyopaswa kufanya; lakini mfinyanzi apaswa kufanya nini?” “Aha,” najibu, “sasa twafika kwenye sehemu iliyo muhimu. Mfinyanzi huutwaa udongo ulioachwa na kuanza kuufanyia kazi. Huuumba kulingana na mapenzi yake mwenyewe. Huukanda na kuufanyia kazi, huuchana vipande na kuuunganisha tena pamoja, huutia maji kisha huuacha ukauke.
Nyakati fulani huufanyia kazi kwa masaa mengi. Nyakati nyingine, huuweka kando kwa siku nyingi wala hauugusi. Kisha, aishapo kuulainisha kikamilifu, huendelea kuufanya uwe chombo alichokipanga. Huuzungusha juu ya gurudumu, huutengeneza, na kuulainisha. Kisha, huukausha juani. Baadaye, huuoka katika tanuru. Mwishowe, huutoa nje ya karakana yake, chombo kwa heshima yake na kifaacho kwa matumizi yake.” Je, sasa msikilizaji wangu atasema kwamba najipinga mwenyewe?
Nilikuwa nimesema kwamba udongo hauwezi kufanya lo lote ila kulala bila kutenda mikononi mwa mfinyanzi. Sasa, nauagiza kufanya kazi kubwa. Kujifanya wenyewe kuwa chombo cha namna hiyo ni kazi isiyowezekana. Hakika sivyo.
Ataona kwamba, nilipokuwa nikinena juu ya sehemu ya udongo, sasa nanena juu ya sehemu ya mfinyanzi. Haya mawili ni kinyume, lakini si yenye kupingana. Udongo haupasi kufanya kazi ya mfinyanzi, bali kuiitikia. Upatano kati ya mafundisho haya mawili, yanayoonekana kupingana, hauwezi kukosewa. Ni nini kiwezacho kusemwa juu ya sehemu ya mwanadamu katika kazi hii kubwa? Yampasa kujisalimisha na kuamini bila kusita.
Lakini, kwa upande wa Mungu wa jambo hili, ni nini kiwezacho kusemwa juu ya njia nyingi za ajabu ambazo kwazo huikamilisha kazi aliyokabidhiwa? Ni hapa ndipo kukua kunapoingia. Bonge la udongo halingekua kamwe kuwa chombo kizuri kama lingebaki katika shimo la udongo kwa maelfu ya miaka. Lakini mara liwekwapo mikononi mwa mfinyanzi stadi, na, chini ya uundaji wake, hukua kwa haraka kuwa chombo kwa heshima yake. Vivyo hivyo, Mfinyanzi wa Mbinguni huibadilisha nafsi iliyoachwa. Roho huibadilisha toka utukufu hata utukufu iwe mfano wa Bwana.
Umechukua hatua ya imani. Umejiweka kikamilifu mikononi mwake. Sasa, yakupasa kutazamia kwamba ataanza kutenda kazi. Njia yake ya kukamilisha lile ulilomkabidhi yaweza kutofautiana na yako.
Lakini yeye anajua, nawe yakupasa kuridhika. Nilimjua mwanamke mmoja. Alikuwa ameingia katika maisha haya ya imani kwa kumwagwa kukubwa kwa Roho na mafuriko ya ajabu ya nuru na furaha. Bila shaka alidhani kwamba haya yalikuwa maandalizi kwa ajili ya utumishi fulani mkuu. Alitazamia kutumwa katika shamba la mavuno la Bwana. Badala ya haya, mumewe punde alipoteza fedha zake zote. Alijifungia nyumbani mwake kufanya kazi za nyumbani zisizo na mwisho. Jambo hili halikumwachia muda wala nguvu kwa kazi yo yote ya injili.
Aliikubali nidhamu ile. Kisha akajitoa kufagia, kufuta vumbi, kuoka, na kushona. Angalifanya vivyo hivyo kuhubiri, kuomba, au kuandika kwa ajili ya Bwana. Kupitia mazoezi haya, alimfanya kuwa chombo “kifaacho kwa matumizi ya Bwana, kilichotayarishwa kwa kila kazi njema.” Mwanamke mwingine, aliyekuja katika imani chini ya hali zilizofanana, alitazamia kutumwa kufanya kazi fulani kubwa. Badala yake, alifungiwa pamoja na wapwa wawili wagonjwa wenye kinyongo ili kuwauguza, kuwafariji, na kuwafurahisha mchana kutwa.
Tofauti na yule mwanamke wa kwanza, huyu hakuyakubali mazoezi. Alizidi kutotulia na kukasirika. Mwishowe, aliasi. Alipoteza baraka zake zote na kutumbukia katika hali ya taabu ya baridi. Mwanzoni alikuwa ameelewa sehemu yake katika kuamini. Lakini, kwa kutoijua njia ya Kimungu ya kufanya hivyo, alijiondoa kutoka mikononi mwa Mfinyanzi wa Mbinguni. Gurudumu likakiharibu chombo.
Naamini vyombo vingi vimeharibiwa vivyo hivyo kwa sababu ya kukosa kuyaelewa mambo haya.
Uzoefu wa Kikristo hukomaa kadiri ya muda. Ni kazi ya Roho Mtakatifu wa Mungu. Nguvu yake hutubadilisha na kutusaidia kukua ndani ya Kristo katika mambo yote. Twaweza kufikia ukomavu huu tu kwa kujitoa kwa kazi yake yenye uweza. Lakini, Maandiko huwahimiza waamini wote kutafuta utakaso wa sasa. Utakaso huo haupatikani katika ukomavu wa kukua, bali katika usafi wa moyo. Huu waweza kuwa mkamilifu kwa mtoto mchanga ndani ya Kristo kama ulivyo kwa mwamini mkongwe.
Bonge la udongo, mara liingiapo chini ya mkono wa mfinyanzi, ni, kila saa ya mchakato, sawasawa na vile mfinyanzi apendavyo liwe. Kwa hiyo, humpendeza. Lakini liko mbali sana na kukomaa kuwa chombo alichokusudia kukifanya wakati ujao. Mtoto mchanga aweza kuwa mkamilifu. Aweza kumpendeza mama yake. Lakini, si vile atakavyo yeye awe atakapokomaa.
Tofaa la mwezi wa Juni ni tofaa kamili kwa Juni. Ni tofaa lililo bora zaidi ambalo Juni laweza kulizaa. Lakini, ni tofauti sana na tofaa la mwezi wa Oktoba. Hilo ni tofaa lililokamilishwa. Kazi za Mungu ni kamili katika kila hatua ya kukua kwake. Kazi za mwanadamu hazikamiliki kamwe hata ziwe kamili kwa kila jinsi. Katika maisha haya ya utakaso, twadai hili tu: Kwa hatua ya imani, twajiweka mikononi mwa Bwana. Twamtumaini afanye ndani yetu mapenzi yake yote mema. Kwa imani, yatupasa kujiweka pale.
Hii ndiyo sehemu yetu katika jambo hili. Kwa kufanya hivyo, sisi, kwa maana ya Kimaandiko, twampendeza Mungu. Yaweza kuhitaji miaka ya mazoezi ili kutukomaza tuwe chombo, kifaacho kwa heshima yake na kwa kila kazi njema. Sehemu yetu ni kuamini; ni yake yeye kuyafikia matokeo. Tufanyapo sehemu yetu, yeye hakosi kamwe kufanya yake, kwa maana hakuna mtu aliyewahi kumtumaini Bwana akaaibika.
Usiogope kwamba ukiamini au ukiwaambia wengine waamini, jambo litakomea hapo. Kuamini ni mwanzo tu na msingi. Tuaminipo, Bwana hutenda kazi. Kazi yake ni sehemu muhimu. Na hili laeleza ule mkanganyiko wa kuonekana ambao huwatatiza wengi. Wao husema, “Kwa pumzi moja watuambia tusifanye lo lote ila kuamini, na kwa pumzi inayofuata watuambia tufanye mambo yasiyowezekana. Mwawezaje kupatanisha kauli zenye kupingana namna hiyo?”
Yatupasa kuzipatanisha. Ni kama kupatanisha kauli juu ya msumeno katika karakana ya seremala. Twasema, wakati mmoja, kwamba msumeno umekata gogo. Kisha, twatangaza kwamba seremala ndiye aliyefanya hivyo. Msumeno ni chombo kitumiwacho, nguvu itumiayo msumeno ni ya seremala. Vivyo hivyo, twajitoa kwa Mungu. Pia twaitoa miili yetu kwake iwe silaha za haki. Twaona kwamba yeye hutenda kazi ndani yetu, kutaka na kutenda kwa kulitimiza kusudi lake jema. Twaweza kusema pamoja na Paulo, “Nalifanya kazi; lakini si mimi, bali neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami.”
Kwa maana yatupasa kuwa kazi ya mikono yake, si yetu wenyewe. Kwa maana sisi tu kazi ya mikono yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu kwa ajili ya matendo mema, ambayo Mungu aliyatengeneza tangu zamani ili tuenende nayo. (Waefeso 2:10). Mungu peke yake, aliyetuumba, ndiye awezaye kutuumba upya. Yeye peke yake ndiye aelewaye “kazi ya mikono yake mwenyewe.” Kila jaribio la kujiumba wenyewe hukiharibu chombo. Hakuna nafsi iwezayo kupata utimilifu wake ulio wa juu zaidi ila kwa kazi yake. Yeye “afanyaye mambo yote kwa shauri la mapenzi yake.”
Bila shaka, nitakazia upande wa mwanadamu katika jambo hili. Ninaandika kwa ajili ya wanadamu. Natumaini kuwafundisha waamini jinsi ya kutimiza sehemu yao ya kazi hii kubwa. Lakini nataka lieleweke wazi. Kama nisingeamini kazi ya Mungu, nisingeandika hata neno moja la kitabu hiki.