Sura 14 · dakika 12 za kusoma
Mashaka
Wakristo wengi ni watumwa wa tabia ya kutia shaka. Hakuna mlevi aliyepata kufungwa kabisa kwa minyororo ya tabia yake ya kuangamiza kuliko wanavyofungwa wao na minyororo hiyo. Maisha yao yote ya Kikristo ni vita vya daima. Jeshi la mashaka linavizia ili kushambulia kila linapopata nafasi. Maisha yao ni ya taabu. Mashaka yao huzuia manufaa yao na kuvunja ushirika wao na Mungu.
Kuingia kwa nafsi katika maisha ya imani, ambayo kitabu hiki kinaeleza, mara nyingi hufukuza mashaka. Lakini, nyakati fulani hurudi tena. Yanaweza kusababisha kujikwaa na kukata tamaa. Hayawezi kumrudisha kabisa mwamini katika jangwa lile la huzuni.
Sisi sote, bila shaka, twakumbuka mchanganyiko ule wa kitoto wa mvuto na hofu katika hadithi ile. Ilihusu kufungwa kwa Mkristo katika Ngome ya Mashaka na yule jitu ovu Kata Tamaa. Tulifurahi mno alipookoka kutoka katika malango yale makubwa na yule jeuri katili. Hatukushuku wakati ule kwamba tungefungwa na jitu lilo hilo, katika ngome ile ile. Lakini nahofia kwamba kwa kila mshiriki wa Kanisa la Kristo limekuwapo angalau tukio moja kama hilo. Kama halingali bichi akilini mwenu, tafadhali soma tena habari ile. Waweza kukuta humo mambo yaliyokupata wewe mwenyewe. Yalikuwa magumu sana kuvumilia na yenye huzuni kuyakumbuka.
Ni jambo la ajabu kwamba watu waitwao Waaminio wapaswa kukiri mashaka kama hayo. Jina lao ladokeza kwamba sifa yao pekee ni kuamini. Ni tabia iliyoenea kiasi kwamba, kama Kanisa lingepewa jina jipya, “Wenye Mashaka” ndilo lingekuwa jina pekee lililofaa. Wakristo wengi wamekubaliana na mashaka yao. Wanayaona kuwa ugonjwa wenye maumivu usioepukika.
Wapaswa kujitolea kwalo kama sehemu ya adabu ya maisha. Hulalamikia mashaka yao kama vile mtu awezavyo kulalamikia maumivu na uchungu wake. Wanataka kuonwa kama “kisa cha kuvutia” cha jaribu adimu, kinachohitaji huruma nyingi na uangalifu mkuu.
Hili mara nyingi ni kweli kwa waaminio. Wanatamani kuishi kwa imani nao wamechukua hatua nyingi kuelekea huko. Yamkini wamepoteza mashaka yao ya zamani. Hapo kwanza yaliwatesa. Walijiuliza kama dhambi zao zimesamehewa na kama wangefika Mbinguni. Lakini, bado wana shaka. Wamehamisha tu tabia hiyo kwenye ngazi ya juu zaidi. Wanasema, huenda, “Naam, naamini dhambi zangu zimesamehewa, nami ni mtoto wa Mungu kwa imani katika Yesu Kristo. Sithubutu kutia shaka juu ya hili tena.
Lakini kisha, na “lakini kisha” hili lajumuisha mashaka juu ya kila ahadi ambayo Baba yetu amewaahidia watoto wake.
Wanapigana nayo, wakikataa kuamini hata wapate uthibitisho ulio bora wa ukweli wake kuliko neno la Mungu.
Wanashangaa kwa nini waweza kutembea katika giza kama hilo. Wanajiona kuwa wafia dini. Wanaugua chini ya mapambano ya kiroho ya kipekee wanayolazimika kuvumilia. Mapambano ya kiroho! Ingekuwa afadhali zaidi wangeitwa uasi wa kiroho! Vita vyetu vipaswa kuwa vita vya imani, na wakati ule tutiapo shaka, vita vyetu vyakoma na uasi wetu waanza.
Natamani kutoa, kama yawezekana, pingamizi moja kali dhidi ya jambo hili lote. Ningeweza vilevile kuungana na malalamiko ya mlevi. Ningeweza vilevile kuomba pamoja naye apate neema ya kuvumilia anasa yake ya kuangamiza. Ni upumbavu kama vile kuzifariji nafsi zilizofungwa kwa malalamiko yao dhaifu. Siwezi kufanya jingine ila kuzitangazia ukombozi mkamilifu ambao Bwana Yesu Kristo anao kwa ajili yao. Nawasihi, nawaomba, na kuwaamuru, kwa nafsi yangu yote, waukubali nao wawe huru. Wala kwa kitambo kimoja singesikiliza udhuru wao wa kukata tamaa. Yakupasa uwe huru, waweza kuwa huru, na lazima uwe huru!
Je, utathubutu kuniambia kwamba ni lazima isiyoepukika kwa Mungu kutiwa shaka na watoto wake?
Je, ni lazima isiyoepukika kwa watoto wako kukutia wewe shaka? Je, ungevumilia mashaka yao hata saa moja? Je, ungemhurumia mwanao kama angesema, “Baba, siwezi kuliamini neno lako, siwezi kuutumaini upendo wako”? Je, ungemwona kuwa kisa cha kuvutia? Nakumbuka mara moja nikaona hasira ya mama mmoja niliyemjua, ikichochewa hata vilindi vyake kwa shaka kidogo iliyotoka kwa mmoja wa watoto wake. Alikuwa amewaleta wasichana wawili wadogo nyumbani kwangu ili awaache huku akifanya shughuli fulani. Mmoja wao, kwa uhakika wa furaha wa kitoto, alijikabidhi kwa chumba changu cha watoto. Alipata anasa zote humo. Aliimba na kucheza hata mama yake aliporudi.
Yule mwingine, kwa tahadhari isiyofaa ya utu uzima, aliketi peke yake pembeni. Alijiuliza kama mama yake angekumbuka kurudi kumchukua. Aliogopa kusahauliwa. Alifikiri mama yake angefurahi kumwondoa, kwa kuwa alikuwa msichana mtukutu. Mwishowe, alijiingiza katika wazimu kamili wa kukata tamaa. Sitausahau kwa urahisi mtazamo wa uso wa mama yule. Ilikuwa baada ya msichana wake mdogo aliyekuwa akilia kurudi na kumwambia lililokuwako. Huzuni, upendo uliojeruhiwa, hasira, na huruma, vyote vilishindana kwa ushindi. Lakini hasira ilishinda, nami nashuku kama msichana yule mdogo alipata kushughulikiwa kwa nguvu hivyo kabla. Tukio lile limekuja mbele yangu mara mia tangu wakati ule. Limenifundisha kwa kina. Limenilazimisha kukataa mashaka juu ya upendo wa Baba yangu wa Mbinguni. Mashaka hayo yamepiga kelele mlangoni pa moyo wangu ili kuingia.
Nimesadiki kwamba, kwa wengi, kutia shaka ni anasa. Kujinyima anasa hiyo kungekuwa kujikana kugumu kuliko yote wanayoyajua. Ni anasa ambayo, kama anasa nyingine zote, huleta matokeo ya huzuni. Huenda, ukiona huzuni iliyoisababisha katika maisha yako mwenyewe ya Kikristo, ukajaribiwa kusema, Ya kusikitisha! Hii si anasa kwangu, bali ni jaribu la kutisha tu.” Lakini simama kwa kitambo. Jaribu kuiacha, nawe hivi karibuni utagundua kama ni anasa au sivyo. Je, mashaka yako hayaji kwako kama kikundi cha rafiki? Wanahurumia taabu zako nao wanataka kukufariji.
Je, si anasa kuketi nao, kuwakaribisha, na kusikiliza hoja zao? Kuungana nao katika kutoa pole? Je, isingekuwa kujikana kugeuka kwa uthabiti mbali nao, na kukataa kusikia neno lo lote wawezalo kusema?
Kama hujui, jaribu ujionee. Je, hujapata kamwe kufurahia anasa ya mawazo makali dhidi ya wale waliokukosea? Je, hujapata kamwe kujua furaha ya kutafakari ukatili wao? Ya kuchunguza uovu wao? Ya kuwazia kila namna ya mambo mabaya yasiyofurahisha juu yao? Kwa hakika kumekufanya uwe mwenye taabu. Lakini, ni namna ya taabu yenye kuvutia ambayo huwezi kuiacha kwa urahisi. Na kama vile hivi ndivyo ilivyo anasa ya kutia shaka. Mambo yamekwenda vibaya kwako katika maisha yako.
Mipango ya Mungu ni ya fumbo. Majaribu ni ya ajabu. Kisa chako chaonekana cha kipekee. Ni jambo gani lingekuwa la kawaida zaidi kuliko kukata shauri kwamba, kwa sababu fulani, Mungu amekuacha? Kwamba hakupendi wewe na hajali hali yako njema? Na jinsi imani ilivyo na nguvu kwamba wewe u mwovu mno hata Yeye asiweze kukujali, au mgumu mno hata Yeye asiweze kukuongoza?
Humlaumu Yeye wala humshtaki kwa udhalimu. Wahisi kwamba wastahili kutojaliwa na kukataliwa kwake kwa sababu ya kutostahili kwako. Hila hii yakuwezesha kujitia shaka wewe mwenyewe huku ukijifanya mnyenyekevu.
Lakini unajifurahisha katika mawazo makali, mabaya juu ya Bwana wako, kama vile ulivyofanya juu ya adui wa kibinadamu.
Yeye asema kwamba hakuja kuokoa wenye haki, bali wenye dhambi. Udhambi wako na kutostahili kwako ndio dai lako bora zaidi la upendo na uangalifu wake.
Yule mwana-kondoo maskini aliyetangatanga na kupotea nyikani angeweza kusema, “Mchungaji hanipendi, hanijali, wala hanikumbuki, kwa sababu nimepotea.” Anawapenda na kuwajali tu wana-kondoo wasiotangatanga kamwe.” Vivyo hivyo mgonjwa angeweza kusema, “Tabibu hatakuja kuniona, wala hatanipa dawa yo yote, kwa sababu mimi ni mgonjwa. Anawajali na kuwatembelea tu watu wenye afya.” Yesu asema, “ Wenye afya hawana haja ya tabibu, bali walio wagonjwa.”(Mathayo 9:12) Na tena asema, “Ni nani kwenu mwenye kondoo mia, akipotewa na mmoja wao, asiyewaacha wale tisini na tisa nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi. Na afikapo nyumbani, huwaita rafiki zake na jirani zake, akiwaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimempata kondoo wangu aliyepotea.”(Luka 15:4-6) Mawazo yo yote juu yake yanayotofautiana na maneno yake mwenyewe ni mawazo makali. Kujifurahisha katika hayo ni vibaya zaidi sana kuliko kujifurahisha katika mawazo makali juu ya rafiki au adui ye yote wa duniani. Tangu mwanzo hata mwisho wa maisha yako ya Kikristo ni dhambi sikuzote kujifurahisha katika mashaka. Mashaka yote yatoka kwa Ibilisi, nayo sikuzote si kweli. Na njia pekee ya kuyakabili ni kwa kukanusha kwa moja kwa moja na kwa msisitizo. Na hili lanileta kwenye sehemu ya vitendo ya somo lote, jinsi ya kupata ukombozi kutoka katika tabia hii ya kuangamiza. Jibu langu lingekuwa kwamba ukombozi kutoka katika hili hauwezi kupatikana kwa njia nyingine yo yote ila ukombozi kutoka katika dhambi nyingine yo yote. Wapatikana katika Bwana na katika Yeye peke yake. Yakupasa kumkabidhi Yeye kutia shaka kwako, kama ulivyojifunza kukabidhi majaribu yako mengine. Yakupasa kufanya vile vile unavyofanya na hasira yako, au kiburi chako.
Yakupasa kumkabidhi Bwana.
Naamini dawa pekee ni kuweka nadhiri dhidi yake. Kama vile ungemhimiza mlevi afanye dhidi ya kileo. Mtumaini Bwana peke yake akuweke imara.
Kama dhambi nyingine yo yote, ngome yake i katika utashi. Yakupasa kujisalimisha utashi wako wa kutia shaka, kama vile ungefanya kwa jaribu jingine lo lote. Mungu sikuzote humiliki utashi uliojisalimisha. Kama tukisema hatutatia shaka na kumkabidhi Yeye kiini chetu, Roho wake atatenda kazi ndani yetu. Tutalindwa tusitie shaka kwa nguvu zake kuu. Tatizo ni kwamba, nafsi mara nyingi haijisalimishi kikamilifu. Hujihifadhia uhuru kidogo wa kutia shaka, ikiuona kuwa wa lazima nyakati fulani. “Sitaki kutia shaka tena,” tutasema, au, “Nataraji sitatia shaka.” Lakini, ni vigumu kusema, “Sitatia shaka tena.””
Lakini hakuna kujisalimisha kwenye matokeo hata kufike kiwango cha kusema, “Sitatia”. Uhuru wa kutia shaka lazima uachwe milele. Nayo nafsi lazima ikubali maisha yenye kuendelea ya kutumaini kusikoepukika. Nadhani, mara nyingi ni lazima kukomesha shaka hii. Lazima tufikie uamuzi juu yake. Naamini ni lazima kabisa katika kisa cha mwenye shaka kama ilivyo katika kisa cha mlevi. Haitafaa kuiacha kidogo kidogo. Kanuni ya kujiepusha kabisa ndiyo pekee yenye matokeo hapa. Ikiisha kujisalimishwa, nafsi lazima ipumzike kabisa katika Bwana kwa ukombozi katika kila jaribu. Lazima iinue ngao ya imani wakati ule shambulio lijapo. Lazima ikabidhi dokezo la kwanza kabisa la shaka kwa Bwana, na lazima imwambie adui alimalize jambo hilo pamoja na Yeye.
Lazima ikatae kuisikiliza shaka hata kitambo kimoja. Ijapoonekana yenye mantiki au unyenyekevu kiasi gani, nafsi lazima iseme, “Sithubutu kutia shaka; lazima nitumaini.” Bwana ni mwema, NAYE ANANIPENDA. Yesu ananiokoa; ananiokoa sasa.” Maneno yale matatu madogo, yakirudiwarudiwa tena na tena, — “Yesu ananiokoa, Yesu ananiokoa,” — yatalishinda jeshi kubwa kabisa la mashaka lililopata kuishambulia nafsi. Nimelijaribu mara zisizohesabika, wala sijapata kuliona likishindwa. Usisimame kubishana jambo hilo na mashaka yako, wala usijaribu kuthibitisha kwamba si sahihi. Usiyajali kamwe; yatendee kwa dharau iliyo kuu. Wafunge mlango wako usoni pao, na ukanushe kwa msisitizo kila neno wanalokuambia. Toa fungu fulani la “Imeandikwa,” nalo ulitupe nyuma yao. Mtazame Yesu moja kwa moja, na umwambie kwamba unamtumaini, na kwamba unakusudia kumtumaini. Waache mashaka yapige kelele kadiri yawezavyo, hayawezi kukudhuru kama hutayaruhusu kuingia.
Yaweza kuonekana kana kwamba unawafungia mlango rafiki zako wa dhati. Moyo wako utayatamani mashaka yako kuliko wana wa Israeli walivyozitamani sufuria za nyama za Misri. Lakini jikane mwenyewe; jitwike msalaba wako katika jambo hili. Kwa kutokuwa na huruma katae kusikiliza hata neno moja. Jeshi kamili la mashaka lilingoja kuamka kwangu na kupiga kelele mlangoni pangu ili kuingia. Hakuna kilichoonekana halisi wala kweli. Zaidi ya yote, ilionekana haiwezekani kwamba mimi — mwenye taabu na mnyonge — ningeweza kuwa lengo la upendo, uangalifu, au utambuzi wa Bwana. Laiti ningeweza kuyaruhusu mashaka haya kuingia. Kama ningeweza kuyaalika yaketi na kujifanya nyumbani, ingekuwa anasa kiasi gani! Lakini miaka iliyopita, niliweka nadhiri dhidi ya kutia shaka. Ningekuwa tayari kuvunja nadhiri yangu dhidi ya kileo kwa haraka kama vile ningevunja hii.
Sikuthubutu kukubali shaka ya kwanza. Niliinua ngao yangu ya imani wakati ule nilipoyaona mawazo haya. Nilimpa Bwana wangu jeshi langu lote alishinde. Kisha, nikaendelea kusema, “Bwana ananipenda kweli.” Yeye ni Mwokozi wangu wa sasa na mkamilifu; Yesu ananiokoa, Yesu ananiokoa sasa!”
Ushindi ulikuwa kamili. Adui aliingia kama mafuriko. Lakini Bwana aliinua bendera dhidi yake.
Alishindwa akakimbizwa. Nafsi yangu yaimba wimbo wa Musa na wana wa Israeli. Wasema, “ Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia BWANA wimbo huu, wakisema, Nitamwimbia BWANA, kwa maana ametukuka sana; farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.” (Kutoka 15:1) “BWANA ni nguvu zangu na wimbo wangu, naye amekuwa wokovu wangu; huyu ndiye Mungu wangu, nami nitamsifu; Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza. BWANA ni shujaa wa vita; BWANA ndilo jina lake. ”(Kutoka 15:2-3). Itakusaidia kupinga mashambulizi ya jaribu hili la kutia shaka, kuona wazi kwamba kutia shaka ni dhambi. Lamwasi moja kwa moja Bwana wetu, atuamuruye, “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga” (Yohana 14:27) Biblia kila mahali yatuamuru kutumaini, pasipo vighairi. Wakati na nafasi vingenishinda kutaja hata sehemu ya mia moja ya haya. Lakini hakuna awezaye kusoma Zaburi bila kusadikishwa. Mtu atumainiye pasipo kuuliza ndiye pekee ampendezaye na kukubaliwa na Mungu. “Uchokozi” wa Israeli ulikuwa kwamba hawakutumaini; “Lakini waliendelea kutenda dhambi juu yake, wakimwasi Aliye juu jangwani. Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao, kwa kutaka chakula kwa ajili ya tamaa yao. Naam, walinena juu ya Mungu, wakisema, “Je! Mungu aweza kuandaa meza jangwani? Aliupiga mwamba, maji yakatoka, vijito vikafurika. Je! Aweza kutoa mkate pia? Aweza kuwapatia watu wake nyama? “Kwa hiyo, Bwana aliposikia, alighadhibika; moto ukawaka juu ya Yakobo, hasira ikapanda juu ya Israeli; kwa sababu hawakumwamini Mungu, wala hawakuutumainia wokovu wake.” (Zaburi 78:17-22.)
Kwa upande mwingine, Isaya asema juu ya wale watumainio, “Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. “(Isaya 26:3) Hakuna kitunguzacho kama shaka ya rafiki. Nimesadiki, hakuna kimhuzunishacho Mungu kuliko shaka yetu.
Mmoja wa watoto wangu, ambaye sasa yuko na Bwana, aliniambia jioni moja nilipomlaza kitandani, “Naam, mama, nimepatwa na shaka yangu ya kwanza.”” “Ee, Ray,” nikasema, “Ilikuwa nini?” “Kwani,” akajibu, “Shetani alinijia akaniambia nisiiamini Biblia, kwa maana haikuwa na neno moja la kweli ndani yake.” “Nawe ulimwambia nini?”
Niliuliza. “Ee,” akajibu, kwa ushindi, “Nilimwambia tu, Shetani, nitaiamini. Ndivyo hivyo!” Nilifurahishwa na ufahamu wa kiroho wa mtoto. Alijua jinsi ya kukabili mashaka. Nilimtia moyo, nikimweleza kwamba mashaka yote na vunja-moyo vyote vyatoka kwa adui. Yeye ni mwongo, kwa hiyo usimsikilize kamwe.
Usiku uliofuata, nilikuwa nimesahau yote kuhusu jambo hilo. Kwa hiyo, nilishangaa aliponiambia, nilipokuwa nikimlaza, “Naam, mama, Shetani amekuwa akijaribu tena.”” “Ee, Ray mpenzi wangu!” nikapaaza sauti kwa hofu, “alikuambia nini wakati huu?” “Naam,” akajibu, “aliniambia tu kwamba mimi ni msichana mtukutu hivi kwamba Yesu asingeweza kunipenda. Ilikuwa upumbavu kufikiri kwamba anipenda.”” “Nawe uliitika nini wakati huu?” niliuliza. “Ee!” akajibu, “Nilimtazama tu kwa hasira nikasema, Shetani, funga kinywa chako!” Kisha akaongeza, kwa tabasamu, “Hawezi kunifanya nisiwe na furaha hata kidogo.” Vita kuu kuliko hivi hakuna nafsi iliyopata kupigana kama mtoto huyu mdogo alivyofanya, wala hakuna ushindi mkuu zaidi uliopata kushindwa!
Ee nafsi yenye shaka mpendwa, nenda ukafanye vivyo hivyo; na ushindi kama huo utakuwa wako. Uwekapo chini kitabu hiki chukua kalamu yako na uandike azimio lako la kutotia shaka kamwe tena. Lifanye kuwa muamala halisi kati ya nafsi yako na Bwana. Achilia mbali uhuru wako wa kutia shaka milele. Weka utashi wako katika jambo hili upande wa Bwana, na umtumaini akulinde usianguke. Mwambie juu ya udhaifu wako na mashaka yako.
Adui yako amekufanya usiwe na msaada. Mkabidhi Yeye vita vyote. Mwambie kwamba hutatia shaka tena.
Kisha, endelea kumkazia macho Yesu.
Geuka mbali na nafsi yako na mashaka yako. Shikamana na imani yako, kwa maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu.
Ukikaa na uhakika hata mwisho, utakuwa, kwa yeye akupendaye, zaidi ya mshindi katika jambo hili.