Siri ya Mkristo ya Maisha ya Furaha ·Kushindwa

Sura 13 · dakika 16 za kusoma

Kushindwa

Kichwa chenyewe cha sura hii huenda kikawashtua baadhi. “Kushindwa,” watasema; “tulidhani hakuna kushindwa katika maisha haya ya imani!” Kwa hili ningejibu kwamba haipaswi kuwako, wala si lazima kuwako; lakini, kwa uhalisia, nyakati nyingine kunako. Nasi ni lazima tushughulike na hali halisi, wala si na nadharia. Hakuna mwalimu wa maisha haya ya ndani asemaye kwamba hatuwezi kutenda dhambi. Wao husisitiza tu kwamba si lazima tutende. Nafasi ya ushindi wa daima sasa yawezekana. Ni wachache wanaokana kwamba, nyakati nyingine, wamekubali kushindwa na majaribu.

Bila shaka, ninaponena juu ya dhambi hapa, namaanisha dhambi inayojulikana, ya kufahamu. Sigusi dhambi za kutokujua.

Wala sijadili ile inayoitwa dhambi isiyoepukika ya asili yetu. Zote mbili zimefunikwa na upatanisho, wala hazivurugi ushirika wetu na Mungu. Sina hamu wala uwezo wa kujadili mafundisho ya dhambi. Nitawaachia wanateolojia jambo hilo. Nitanena tu juu ya uzoefu wa mwamini. Nataka iwe wazi kwamba nitarejea tu kwa yale yaliyo ndani ya utambuzi wetu. Basi, kutoelewana juu ya jambo hili la dhambi inayojulikana ni hatari kwa maisha ya juu zaidi ya Kikristo. Mwamini, anayeamini yu katika njia kuu ya utakatifu, aweza kushtukizwa na kuingia dhambini. Ndipo hujaribiwa ama kukata tamaa, ama kuficha dhambi yake. Ili kuhifadhi fundisho, aweza kuiita “udhaifu” na kukataa kuwa mnyofu.

Kila mojawapo ya njia hizi ni yenye kuangamiza sawasawa ukuaji wo wote wa kweli na maendeleo katika maisha ya utakatifu. Ni lazima tuikabili kweli hii yenye kuhuzunisha. Ni lazima tuiite kwa jina lake na kutafuta, kama tuwezavyo, chanzo chake na tiba yake. Maisha haya ya umoja na Mungu yadai unyofu wa hali ya juu kwake yeye na kwetu wenyewe. Dhambi ingevuruga ushirika kwa muda mfupi tu. Lakini, uongo wo wote pamoja nayo bila shaka ungeuharibu. Kushindwa kwa ghafula si sababu ya kukata tamaa na kuacha yote kama yaliyopotea. Wala uadilifu wa fundisho letu hauguswi nako. Hatuhubiri hali, bali mwenendo. Njia kuu ya utakatifu si mahali, bali ni njia. Utakaso si kitu cha kupatikana katika hatua fulani ya uzoefu wetu na kumilikiwa milele. Ni maisha ya kuishiwa siku kwa siku na saa kwa saa.

Twaweza kuiacha njia kwa muda mfupi. Lakini kutanga-tanga kwetu hakuifuti. Twaweza kurudi upesi. Katika maisha haya ya imani, twaweza kushindwa nyakati nyingine. Kushindwa huku ni kwenye kuhuzunisha na kwa kuomboleza. Lakini, kukikabiliwa vyema, hakuhitaji kuvuruga tumaini letu kamili katika Mungu. Hakupaswi kukatiza ushirika wetu wenye furaha pamoja naye kwa muda mrefu.

Jambo kuu ni kurudi kwa Mungu papo hapo. Dhambi yetu si sababu ya kuacha kuamini, bali ni hoja isiyoweza kujibiwa ya kwa nini yatupasa kuamini kwa ukamilifu zaidi kuliko wakati wo wote. Hata kiwe nini chanzo cha kushindwa kwetu, kukata tamaa hakusaidii. Mtoto anayejifunza kutembea aweza kukata tamaa baada ya kuanguka. Aweza kukataa kujaribu tena. Mwamini, anayejifunza kuishi kwa imani, hana budi asikate tamaa kwa sababu ametenda dhambi. Njia pekee katika visa vyote viwili ni kuinuka mara moja na kujaribu tena. Baada ya kushindwa kwa msiba.

“Ndipo Yoshua akararua mavazi yake, akaanguka chini kifudifudi mbele ya sanduku la Bwana hata jioni, yeye na wazee wa Israeli; nao wakatia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, “Ole wangu, Ee Bwana MUNGU, mbona umewavusha kabisa watu hawa ng’ambo ya Yordani, ili kututia mikononi mwa Waamori, wapate kutuangamiza? Laiti tungaliridhika kukaa ng’ambo ya pili ya Yordani! Ee Bwana, niseme nini, iwapo Israeli wamewapa adui zao migongo yao? Kwa maana Wakanaani na wenyeji wote wa nchi watasikia habari hii, nao watatuzunguka pande zote na kulikatilia mbali jina letu katika dunia. Nawe utalitendea nini jina lako kuu?”(Yoshua 7:6-9) Kilio hiki cha kukata tamaa kilikuwaje! Nako kwarudiwa na wana wengi wa Mungu leo hii. Mioyo yao huyeyuka, kama maji, kwa sababu ya kushindwa. Hulia, “Naye Yoshua akasema, ‘Ole wangu, Bwana MUNGU, mbona umewavusha kabisa watu hawa ng’ambo ya Yordani — ili kututia mikononi mwa Waamori, wapate kutuangamiza?

Laiti tungaliridhika, na kukaa upande wa pili wa Yordani!” Wao hutabiri kushindwa zaidi na hata kushindwa mikononi mwa adui zao. Bila shaka, Yoshua alifikiri, kama tufikirivyo sasa. Baada ya kushindwa namna hiyo, kukata tamaa na kukosa matumaini kulionekana kuwa jibu pekee salama. Lakini Mungu alifikiri vinginevyo. “Bwana akamwambia Yoshua, “Inuka! Mbona umelala hivi kifudifudi? “ Hawakupaswa kujisalimisha kwa kukata tamaa, hata kungeonekana kwa unyenyekevu kiasi gani. Ni lazima wauikabili uovu na kuuondoa. Ni lazima “wajitakase” mara moja.”

“Inukeni, watakaseni watu,” siku zote ndiyo amri ya Mungu. “Lala chini ukate tamaa” siku zote ndilo jaribu la adui. Twahisi ni ujuvi, hata ni ufidhuli, kwenda kwa Bwana papo hapo baada ya kutenda dhambi juu yake. Twahisi twapaswa kuteseka kwa matokeo ya dhambi zetu kwa kitambo na kustahimili dhamiri zetu zenye hatia. Twashindwa kuamini kwamba Bwana angependa kutukaribisha tena katika ushirika wake wa upendo. Hapo kwanza msichana mdogo alinieleza hisia hii, kwa unyofu wa kitoto wa moyo mweupe. Aliuliza kama Bwana Yesu husamehe dhambi zetu daima tukimwomba. Nikasema, “Ndiyo, bila shaka husamehe.””

“Mara ile ile” alirudia, kwa shaka. “Ndiyo,” nikajibu, “dakika ile ile tuombayo, hutusamehe.”

“Vyema,” alisema kwa makini, “siwezi kuamini hilo. Ningedhani angetufanya tujisikie masikitiko kwa siku mbili au tatu kwanza. Kisha ningedhani angetufanya tumwombe mara nyingi sana, na kwa namna nzuri kabisa pia, wala si kwa maneno ya kawaida tu. Naamini ndivyo afanyavyo. Si lazima ujaribu kunifanya nidhani kwamba hunisamehe mara moja, hata Biblia iseme nini.”

Alisema tu yale wanayoyafikiri Wakristo wengi. Lililo baya zaidi, wengi hutenda kadiri yake. Majuto yao sasa huwatenga na Mungu zaidi kuliko dhambi yao ingavyofanya.

Ni kinyume kabisa cha jinsi tunavyotaka watoto wetu watende, hata nastaajabu tulipataje kuwaza wazo kama hilo juu ya Mungu. Mama huhuzunika mtoto wake mkorofi anapoenda zake peke yake katika kukata tamaa. Hutia shaka utayari wake wa kusamehe. Lakini, moyo wake humkaribisha mpenzi anayemkimbilia na kuomba msamaha!

Bila shaka, Mungu wetu aliujua upendo huu aliposema, “Rudini, enyi watoto wenye kuasi; nitawaponya kuasi kwenu.

Tazama, twakuja kwako, kwa maana wewe ndiwe Bwana, Mungu wetu.”(Yeremia 3:22) Dakika ile ile idhihirishayo dhambi, yapaswa kudhihirisha msamaha. Hili ni muhimu kwa mwenendo thabiti katika njia takatifu. Hapa, hatuwezi kuvumilia dakika moja ya kutengwa na Mungu. Twaweza kuiendea njia hii tu kwa kumtazama Yesu, kila dakika. Tukiondoa macho yetu kwake ili kuona dhambi na udhaifu wetu, tutaiacha njia mara moja. Mwamini, anayeamini yu katika njia hii, hana budi amkimbilie Bwana ikiwa dhambi yamshinda. Hana budi atende kadiri ya (1 Yohana 1:9) “Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” Hana budi asifiche dhambi yake na kutafuta kuiponya kwa udhuru, wala kuisukuma nje ya kumbukumbu yake kwa kupita kwa wakati. Bali hana budi atende kama walivyofanya wana wa Israeli. Hana budi ainuke “asubuhi na mapema,” na “akimbie” hata pale kilipofichwa kile kitu kiovu. Kisha, hana budi akitwae kutoka mahali kilipofichwa na kukiweka “mbele za Bwana.”

Hana budi aiungame dhambi yake. Kisha hana budi aipige kwa mawe, aiteketeze, na kuiondoa. Kisha, hana budi ainue chungu kikubwa cha mawe kuificha milele. Hana budi, papo hapo, aamini kwamba Mungu yuko. Hana budi aamini, kadiri ya neno lake, kwamba Mungu ni mwaminifu na wa haki hata amsamehe dhambi yake, na kwamba hufanya hivyo kweli. Hana budi pia aamini kwamba Mungu humsafisha na udhalimu wote. Hana budi, kwa imani, adai msamaha na usafisho wa mara moja. Kisha, hana budi aamini kuliko wakati wo wote.

Mara tu dhambi ya Israeli ilipofunuliwa na kuondolewa, neno la Mungu likaja. Lilikuwa ujumbe wa kutia moyo sana: “Bwana akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usifadhaike. Twaa watu wote wa vita pamoja nawe, ukainuke, uende Ai. Tazama, nimemtia mkononi mwako mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake.”(Yoshua 8:1) Ujasiri wetu ni lazima uinuke juu kuliko wakati wo wote. Ni lazima tumtumaini Bwana zaidi. Ndipo, uweza wake mkuu waweza kutenda kazi ndani yetu kulitimiza kusudi lake. Zaidi ya hayo, ni lazima tuisahau dhambi yetu mara tu ikiisha kuungamwa na kusamehewa. Ni lazima tusiiwazie, na kuichunguza, na kujifurahisha katika anasa ya huzuni na majuto. Ni lazima tusiifanye sanamu, kisha kuzunguka na kuitazama. Hilo lingeifanya kuwa mlima uufichao Mungu wetu mbele yetu. Ni lazima tufuate mfano wa Paulo. Ni lazima “tukiyasahau yaliyo nyuma, na kuyakazia yaliyo mbele.” Kisha, ni lazima “tukaze mwendo, tuifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.””

Ningependa kuleta mifano miwili yenye kutofautiana ya mambo haya. Mmoja alikuwa Mkristo mwenye bidii. Alikuwa mtendakazi hodari kanisani. Kwa miezi kadhaa, alikuwa amefurahia wokovu kamili. Kwa ghafula alishindwa na jaribu la kumtenda ndugu vibaya. Alidhani haiwezekani kutenda dhambi tena. Basi, alikata tamaa sana. Akaamua kwamba alikuwa amekosea. Hakuwahi kutumaini kweli kweli. Kukata tamaa kwake kukakua na kuwa kukosa matumaini kabisa. Akaamua kwamba hakuwahi kuzaliwa mara ya pili, akajitoa kama aliyepotea. Alitumia miaka mitatu katika taabu. Alizidi kujitenga na Mungu na kuanguka katika dhambi moja baada ya nyingine. Maisha yake yakawa laana kwake mwenyewe na kwa waliomzunguka.

Afya yake ilishindwa chini ya mzigo huo wa kutisha. Hofu zikatokea juu ya akili yake. Mwishoni mwa miaka mitatu, alikutana na bibi mmoja Mkristo, aliyeielewa kweli juu ya dhambi ambayo nilikuwa nikijaribu kuieleza. Baada ya maongezi mafupi, alifahamu tatizo lake. Akasema, “Ulitenda dhambi katika tendo hilo, bila shaka. Usijaribu kulitolea udhuru.”

Lakini je, hujawahi kuiungama kwa Bwana na kumwomba akusamehe?” “Kuiungama!” Akapaza sauti, “Sikufanya lo lote ila kuiungama. Nimemsihi Mungu anisamehe kwa miaka hii mitatu ya kutisha.” “Nawe hukuwahi kuamini kwamba alikusamehe?” aliuliza bibi yule. “La,” akasema mtu maskini yule, “ningewezaje, kwa maana sikuwahi kuhisi kana kwamba alifanya hivyo?” “Lakini ikiwa amesema anakusamehe, je, hilo lisingetosha kama vile wewe kulihisi?”

“Naam, ndiyo,” akajibu mtu yule, “ikiwa Mungu amesema hivyo, bila shaka ningeamini.” “Vyema sana, amesema hivyo,” lilikuwa jibu la bibi yule, akaigeukia aya tuliyoitwaa hapo juu. “Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.”(1 Yohana 1:9) akaisoma kwa sauti. “Sasa,” akaendelea, “kwa miaka mitatu umekuwa ukiiungama dhambi yako. Wakati huo wote, kumbukumbu ya Mungu imetangaza kwamba yeye ni mwaminifu na wa haki hata akusamehe na kukusafisha. Lakini, hujaamini hata mara moja.”

Umekuwa ukimfanya ‘Mungu kuwa mwongo’ wakati huu wote kwa kukataa kuamini ushuhuda wake.”

Mtu maskini yule aliliona jambo lote. Alishangaa na kushtuka. Bibi yule alipopendekeza wapige magoti, alitii kama mtu aliye katika kizunguzungu. Alitaka aungame dhambi zake zilizopita na kudai, papo hapo, msamaha na usafisho. Lakini tokeo lilikuwa tukufu. Katika muda mfupi, nuru ikaingia, naye akapasuka kwa sifa kwa ukombozi wa ajabu. Katika dakika tatu, roho yake, kwa imani, ilivuka safari ndefu na yenye kuchosha ya miaka mitatu. Alijikuta akipumzika ndani ya Yesu, akifurahi katika wokovu wake kamili.

Mfano wa pili ulikuwa wa bibi mmoja Mkristo. Alikuwa katika wokovu kwa muda wa majuma mawili hivi. Alikuwa na uzoefu mzuri, wenye ushindi. Kwa ghafula, mwishoni mwa muda huo, alishindwa na mpasuko mkali wa hasira. Kwa dakika moja, gharika ya kukata tamaa ikaifunika roho yake. Adui akasema, “Tazama, sasa, hilo laonyesha yote yalikuwa kosa. Bila shaka, umedanganywa juu ya jambo lote, wala hukuingia kamwe katika maisha ya kumtumaini Mungu kikamilifu.

Waweza vile vile kuacha. Huwezi kujiweka wakfu wala kujitumaini zaidi ya vile ulivyofanya wakati huu. Basi, ni dhahiri maisha haya ya utakatifu si kwa ajili yako!” Mawazo haya yalipita akilini mwake kwa dakika moja. Lakini alikuwa amefundishwa vyema katika njia za Mungu. Basi, akasema, “Ndiyo, nimetenda dhambi, nalo ni jambo la kuhuzunisha sana.” Lakini Biblia husema ya kwamba tukiziungama dhambi zetu, Mungu atatusamehe. Yeye ni mwaminifu na wa haki. Naye atatusafisha pia na udhalimu wote. Naamini atafanya hivyo.” Hakukawia. Bado akiwaka kwa hasira, alikimbia, hakutembea, kuingia chumbani ili awe peke yake. Akipiga magoti kando ya kitanda, akasema, “Bwana, naiungama dhambi yangu.” Nimetenda dhambi, hata sasa hivi natenda dhambi.

Naichukia, lakini siwezi kujiondolea. Naiungama kwa aibu na fadhaa ya uso mbele za Mungu. Na sasa naamini kwamba, kadiri ya neno lako, wewe wasamehe nawe wasafisha.” Aliyasema kwa sauti, kwa maana msukosuko wa ndani ulikuwa mkubwa mno usiweze kunenwa ndani. Maneno “wewe wasamehe nawe wasafisha” yalipopita midomoni mwake, ukombozi ukaja. Bwana akasema, “Akaamka, akaukemea upepo, akauambia ule bahari, ‘Nyamaza, utulie!” Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu,” (Marko 4:39) kukawa shwari kuu. Gharika ya nuru na furaha ikaifunika roho yake, adui akakimbia, naye akawa mshindi kupita kiasi kwa yeye aliyempenda. Ilikuwa imechukua dakika tano tu, dhambi na tiba yake. Sasa, miguu yake ikakanyaga imara kuliko wakati wo wote katika njia kuu iliyobarikiwa ya utakatifu. Basi, bonde la Akori likawa mlango wa matumaini. Aliimba wimbo wake wa ukombozi, kwa maana ya ndani zaidi: “Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu, wakisema, ‘Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; farasi na mpanda farasi amewatupa baharini” (Kutoka 15:1) Katika kila shida, tiba pekee ni kumtumaini Bwana. Kama hili ndilo tuwezalo tu kufanya, je, si afadhali kulifanya mara moja? Mara nyingi nimesimamishwa ghafula na swali, “Basi, niwezaje kufanya lo lote ila kutumaini?” Niliona mara moja upumbavu wa kutafuta ukombozi kwa njia nyingine yo yote. Nilifikiri, “Itanibidi kutumaini mwishoni. Basi, kwa nini nisifanye hivyo sasa?” Tumeingia katika maisha ya imani. Tukishindwa, kupona kwetu pekee ni lazima kuwe ongezeko la imani, wala si upungufu.

Kila kushindwa, kama kutatokea, na kukusukume kwa Bwana. Jitoe kwake na umtumaini kabisa. Ingawa ni kwenye kuhuzunisha, kushindwa huku hakutakomesha pumziko lako wala ushirika wako mtamu pamoja naye. Nimeonyesha njia ya kukwepa kushindwa. Sasa, nataka kujadili visababishi vya kushindwa katika maisha haya ya wokovu kamili.

Visababishi havimo katika nguvu za jaribu, udhaifu wetu wenyewe, au, zaidi ya yote, upungufu wo wote katika uweza wa Mwokozi wetu au utayari wake wa kutuokoa. Ahadi kwa Israeli ilikuwa thabiti, “Hapatakuwa na mtu ataleweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako. Kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja nawe. Sitakupungukia wala sitakuacha.” (Yoshua 1:5). Nayo ahadi kwetu ni thabiti vile vile, “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu. Lakini Mungu ni mwaminifu, ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo, bali pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.” (1 Wakorintho 10:13) Basi wanaume wapata elfu tatu wakakwea kutoka kwa watu wale. Nao wakakimbia mbele ya watu wa Ai. Haikuwa nguvu ya adui wao, wala Mungu hakuwapungukia. Kushindwa kwao kulikuwa na chanzo kingine, ambacho Bwana akitangaza: “Israeli wametenda dhambi. Naam, wamenihalifu agano langu niliyowaamuru.

Wamekitwaa kitu kilicholaaniwa. Naam, wameiba, tena wamejifanya kama si wao, wamekiweka pamoja na vitu vyao wenyewe.”

“Basi, wana wa Israeli hawakuweza kusimama mbele ya adui zao. Waliwapa adui zao migongo yao.”” Ulikuwa uovu uliofichwa uliowashinda. Chini sana ya nchi, ndani ya hema katika jeshi lile kubwa, kulikuwa na kitu ambacho Mungu alikuwa na neno nacho.

Kitu hiki kilichofichwa kikalifanya jeshi lote kuwa dhaifu mbele ya adui zao. “Israeli, kuna kitu kibaya katikati yako. Huwezi kusimama mbele ya adui zako hata utakapokiondoa.””

Fundisho ndilo hili: Uovu wo wote uliofichwa mioyoni mwetu, hata uwe mdogo kiasi gani, utatufanya tuanguke mbele ya adui zetu. Uchungu wo wote uliotunzwa, hukumu kali, au ulegevu katika kumtii Bwana utayadhoofisha maisha yetu ya kiroho. Vivyo hivyo tabia au mazingira yo yote yenye shaka. Huenda tumeuficha uovu mioyoni mwetu.

Huenda tumeufunika, tukikataa kuuona. Lakini, twaufahamu kwa siri.

Twaweza kuupuuza na kutangaza tumaini letu kamili. Twaweza kuwa na bidii zaidi katika wajibu wetu wa kidini. Twaweza kuona kweli na uzuri zaidi katika maisha ya imani. Twaweza kuonekana tumeshinda, kwetu wenyewe na kwa wengine pia.

Lakini, twaweza kupatwa na kushindwa kuchungu. Twaweza kustaajabu, kuuliza, kukata tamaa, na kuomba. Lakini, hakuna litakalosaidia hata kile kitu kilicholaaniwa kitakapochimbuliwa, kiletwe nuruni, na kuwekwa mbele za Mungu. Ikiwa mwamini anayeishi maisha ya ndani ameshindwa, hana budi atafute chanzo. Si nguvu ya adui. Ni upungufu uliofichwa wa kujitoa katika kiini chake.

Maumivu ya kichwa si ugonjwa, bali ni dalili yake. Uko katika sehemu nyingine ya mwili. Vivyo hivyo, katika Mkristo, dhambi ni dalili tu. Yafunua uovu ambao yamkini upo katika sehemu nyingine ya nafsi yake.

Nyakati nyingine, mtu aweza kuficha uovu hata katika kile ambacho, kwa mtazamo wa haraka, chaonekana kuwa chema. Nyuma ya tamaa kubwa ya kweli, kwaweza kuwa na mwelekeo wa kuhukumu au kupendelea maoni yetu wenyewe. Uaminifu wa Kikristo ulio wazi waweza kuficha kutokuwapo kwa upendo wa Kikristo. Chini ya utunzaji unaoonekana wa haki wa mambo yetu, twaweza kuficha ukosefu mkubwa wa kumtumaini Mungu. Kiongozi wetu mbarikiwa, Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu, yuko. Kwa siri hutufunulia mambo haya. Hufanya hivyo kwa mishtuko midogo na maumivu ya dhamiri. Basi, twaachwa bila udhuru. Ni rahisi kupuuza sauti yake ya upole. Twajishawishi kwamba yote ni sawa. Hili litaficha uovu wa kuangamiza katikati yetu, ukisababisha kushindwa kusikotarajiwa.

Mfano bora wa jambo hili ulinipata hapo kwanza katika utunzaji wangu wa nyumba. Nilihamia nyumba mpya. Nilipoikagua kwa utayari, nilikuta pipa safi sana la kandi ndani ya ghala la chini. Lilikuwa limefungwa pande zote mbili. Nilisita kama nilitwae kutoka ghalani na kulifungua. Lilionekana tupu na zuri. Basi, niliamua kuliacha, kwa kuwa ingekuwa kazi nyingi kulipandisha ngazi. Sikujisikia raha kabisa, lakini niliweka kando shaka zangu na kuliacha. Kila majira ya kuchipua na ya kupukutika, wakati wa kusafisha nyumba, ningelikumbuka pipa lile. Mshtuko wa dhamiri yangu ya kike ya nyumbani ukanisumbua. Sikuweza kupumzika katika nyumba iliyosafishwa kikamilifu wakati bado halijafunguliwa. Kwa maana nilijuaje kwamba halikuficha uovu fulani chini ya sura yake nzuri?

Hata hivyo, nilizituliza shaka zangu. Niliogopa taabu ya kulichunguza. Kwa miaka miwili au mitatu, pipa lile lisiloonekana kuwa na madhara likakaa ghalani mwangu. Kisha, kwa namna isiyoeleweka kabisa, nondo wakaanza kuijaza nyumba yangu. Nilitumia kila tahadhari iwezekanayo dhidi yao na kufanya kila jitihada kuwaangamiza, lakini bure. Waliongezeka upesi na kutisha kuharibu kila kitu nilichokuwa nacho.

Nilishuku mazulia yangu ndiyo chanzo, nikayasafisha kabisa. Nilishuku kuna kitu kibaya na samani zangu, basi nikazitengeneza upya. Nilishuku mambo ya kila namna yasiyowezekana.

Mwishowe, wazo la pipa likaniangazia. Nikaliletesha kutoka ghalani, na kichwa chake kikagongwa hata kikafunguka.

Nadhani ni salama kusema kwamba maelfu ya nondo walimwagika nje. Yule aliyekaa hapo kabla lazima aliacha kitu fulani kilichozaa nondo. Hiki ndicho kilichokuwa chanzo cha taabu yangu yote.

Sasa naamini kwamba tabia au anasa fulani, jambo fulani salama na dogo, hutusababishia mishtuko midogo ya dhamiri. Halijachunguzwa vyema chini ya jicho la Mungu litafutalo. Nadhani lipo mzizini mwa kushindwa kwingi katika maisha haya ya juu zaidi. Si yote yamejitoa. Pembe fulani ya siri yashikwa imefungwa dhidi ya kuingia kwa Bwana. Na kwa hiyo, hatuwezi kusimama mbele ya adui zetu, bali twajikuta tumepigwa chini mbele yao.

Ili kuzuia kushindwa, au kupata chanzo chake kama tutashindwa, ni lazima tuweke maombi haya mbele yetu: “Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu; unijaribu, uyajue mawazo yangu; nawe uone kama iko njia iliyo mbaya ndani yangu, ukaniongoze katika njia ya milele.””

Kwaweza kuwa na kitu chenye kudanganya sana katika mateso yetu juu ya kushindwa kwetu. Twaweza kudhani twakaza fikira juu ya utukufu wa Mungu. Lakini, roho zetu zaweza kutaabishwa na nafsi peke yake. Sisi si watakatifu kama tulivyodhani. Ugunduzi huu waumiza kujipenda kwetu. Fadhaa yetu yaweza kuwa kosa kubwa zaidi kuliko lile kosa la kwanza. Njia pekee salama ya kuchukulia kushindwa kwetu ni kuepuka kujihesabia haki au kujihukumu wenyewe.

Badala yake, yatupasa kukuweka kwa utulivu mbele za Bwana. Yatupasa kukutazama kwa amani na kwa upendo.

Waandishi wa kale wa fumbo husema kwamba kumgeukia Mungu kwa unyenyekevu na amani hutusaidia zaidi kuliko kujuta kwa kutanga-tanga kwetu kutoka kwake. “Uwe mwaminifu tu,” husema. “Mgeukie yeye tu, dakika ile uonapo dhambi yako. Uwepo wake utakuweka huru kutoka mitego iliyokunasa.” Kujitazama nafsi yako hukuzamisha zaidi katika matope, kwa maana matope haya hayakuwa lo lote ila nafsi; hali kumtazama Mungu kwa unyofu kwaweza kuutuliza na kuufariji moyo wako.

Mwishowe, tusisahau kamwe, hata kiwe nini kushindwa kwetu. Bwana Yesu aweza, kama ilivyotangazwa, kutuokoa na adui zetu. Ndipo, twaweza “Ili sisi, tukiisha kuokolewa mikononi mwa adui zetu, tumtumikie pasipo hofu, katika utakatifu na haki mbele zake siku zetu zote.”(Luka 1:74-75). Na tuombe, kila mmoja wetu, mchana na usiku: “Umzuie mtumishi wako, asije akatenda dhambi za kiburi; nazo zisinitawale.”(Zaburi 19:13). “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”(Matendo 1:8). Ni lazima tuwe wanyofu hivyo mikononi mwake, na kumtumaini. Ndipo yeye atakapo“awakamilishe katika kila kazi njema, ili mpate kuyafanya mapenzi yake, akitenda ndani yetu yapendezayo mbele zake, kwa njia ya Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele. Amina.” (Waebrania 13:21)

Yaliyomo

Siri ya Mkristo ya Maisha ya Furaha Hannah Whitall Smith

Ukurasa 1 / 1 · 16 dakika zimebaki katika sura