Sura 12 · dakika 12 za kusoma
Kuhusu Majaribu
Makosa makubwa sana hufanywa kuhusu majaribu katika maisha haya ya imani. Kwanza, watu hutazamia kwamba, baada ya nafsi kupumzika katika Mungu, majaribu yatakoma. Huamini kuwa wokovu ulioahidiwa ni ukombozi kutoka katika majaribu na kutoka katika kujaribiwa vilevile. Wanapomkuta Mkanaani bado yumo nchini, na kuona miji mikubwa yenye kuta, hukata tamaa. Hudhani kwamba lazima wamepotea njia, na kwamba hii haiwezi kuwa ile nchi ya kweli baada ya yote.
Kisha, kwa kukosea, huyaona majaribu kuwa ni dhambi. Hujilaumu wenyewe kwa ajili yake, kumbe ni kosa la adui.
Jambo hili huleta hukumu na kukata tamaa. Likiendelea, huishia katika dhambi. Adui humfanya nafsi iliyokata tamaa kuwa mawindo rahisi; hata mara nyingi tunaanguka kwa sababu ya hofu ile ile ya kuwa tumeanguka. Ili kuondoa shida ile ya kwanza, ni lazima nirejee kwenye Maandiko. Yanasema kuwa maisha ya Mkristo ni vita vya daima. Pia yanasema kwamba, hasa tunapokuwa tumeketishwa mahali pa mbinguni ndani ya Kristo Yesu, ni lazima tushindane na adui wa kiroho waliopo huko.
Nguvu na ustadi wao wa kutujaribu lazima uwe mkubwa mno kuliko wowote tuliopata kukutana nao.
Kwa kawaida majaribu huongezeka nguvu mara kumi baada ya kuanza maisha ya ndani, badala ya kupungua. Nguvu zao zisitufanye kutia shaka kwamba tumepata mahali pale pa kweli pa kukaa. Majaribu makali kwa kawaida ni ishara ya neema kubwa, wala si ya neema ndogo. Waisraeli walipotoka Misri mara ya kwanza, Bwana hakuwaongoza kupitia nchi ya Wafilisti, ile njia ya karibu zaidi. Mungu alisema, “Ikawa, Farao alipowaacha watu waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ingawa ilikuwa karibu; kwa maana Mungu alisema, “Watu wasije wakabadili nia yao wonapo vita, wakarudi Misri.” Lakini, walipojifunza kumtumaini, aliwaruhusu adui zao wawashambulie. Katika safari yao ya jangwani, walikutana na adui wachache na kupigana vita vichache. Katika ile nchi, walikabiliana na mataifa saba makubwa na wafalme thelathini na mmoja. Iliwapasa kuiteka miji yenye kuta na kuwashinda majitu.
Wasingaliweza kupigana na Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi mpaka walipokwisha kuingia katika nchi yao. Majaribu yako, Mkristo mpendwa, yaweza kuthibitisha kwamba u katika ile nchi unayotaka kuingia. Ni ya pekee kwa nchi ile. Kamwe usiyaache majaribu yako yakufanye utie shaka kwamba u katika pale “mahali pa mbinguni” palipoahidiwa.
Kosa la pili si rahisi hivyo kulishughulikia. Ni karibu bure kusema kwamba jaribu si dhambi. Lakini, taabu nyingi hutokana na kutolielewa jambo hili. Dokezo lenyewe la uovu laonekana kama laleta unajisi pamoja nalo. Kwa kuwa mtenda-kazi yule mwovu hatambuliki, ile nafsi maskini iliyojaribiwa huhofu kwamba lazima iwe mbaya sana, na mbali na Mungu, kwa kuwa imekuwa na mawazo kama hayo. Ni kama vile mwizi angeingia kwa nguvu nyumbani mwa mtu ili kuiba.
Mwenye nyumba alipoanza kumpinga, yule mwizi akamshtaki yeye kuwa ndiye mwizi. Ni hila ya werevu ya adui ili kututega.
Huja na kutunong’oneza mawazo maovu: mashaka, makufuru, wivu, husuda, na kiburi. Kisha husema, “Lo, ni lazima uwe mwovu kiasi gani hata uwaze mambo kama haya!” Ni dhahiri kwamba humwamini Bwana. Kama ungalimwamini, mambo haya yasingaliingia moyoni mwako. Hoja hii yaonekana kama ni ya kweli, hivyo ile nafsi huikubali.
Ndipo huhisi kuhukumiwa na kukata tamaa. Kutoka hapo, ni rahisi kuanguka katika dhambi. Mojawapo ya mambo yenye kuangamiza zaidi katika maisha ya imani ni kukata tamaa.
Mojawapo ya yenye kusaidia zaidi ni uchangamfu. Mtu mmoja mwenye hekima alisema kwamba, katika kuyashinda majaribu, uchangamfu ndio ufunguo. Ndilo jambo la kwanza, la pili, na la tatu. Ni lazima tutazamie kushinda. Ndiyo sababu Bwana alimwambia Yoshua mara nyingi, “Je, sikukuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike, kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako ” (Yoshua 1:9). Na ndiyo sababu pia atwambia sisi, “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga” (Yohana 14:27) .
Nguvu ya jaribu iko katika kuzimia kwa mioyo yetu wenyewe. Adui analijua hili. Sikuzote hujaribu kutuvunja moyo mwanzoni mwa mashambulizi yake, kama awezavyo.
Wakati mwingine, twahisi kuvunjika moyo. Twadhani ni huzuni ya haki na machukizo juu ya nafsi zetu kwa kuwa tumejaribiwa. Kumbe kwa kweli ni aibu. Twaona haya kwa sababu kwa siri tulijipongeza wenyewe. Tuliamini kwamba ladha zetu zilikuwa safi mno na kutengwa kwetu na ulimwengu kulikuwa kamili mno hata mambo kama hayo yasingeweza kutujaribu. Tulitazamia kitu fulani kutoka kwetu wenyewe. Twakata tamaa kukiona kimekosekana.
Kwa hiyo, twavunjika moyo. Aibu hii na kukata tamaa huku ni kubaya kuliko lile jaribu lenyewe. Yaonekana kama ni ya unyenyekevu, kumbe hutokana tu na kujipenda kulikojeruhiwa.
Unyenyekevu wa kweli waweza kuvumilia kuona udhaifu na upumbavu wake wenyewe ukifunuliwa. Haukutazamia kamwe kitu chochote kutoka kwake wenyewe. Wajua kwamba tumaini lake pekee ni lazima liwe katika Mungu. Hivyo, badala ya kuivunja nafsi moyo isitumaini, huisukuma iingie katika kutumaini kwa ndani zaidi na kwa ukamilifu zaidi. Lakini unyenyekevu wa uongo, uzaliwao na nafsi, huitumbukiza nafsi katika kukata tamaa. Huisukuma iingie katika ile dhambi yenyewe iichukiayo sana. Nakumbuka mara moja niliposikia fumbo lililonionyesha jambo hili kwa ajabu. Shetani aliwakusanya pamoja watumishi wake katika baraza ili washauriane jinsi wawezavyo kumfanya mtu mwema atende dhambi. Pepo mmoja mbaya akainuka akasema, “Nitamfanya atende dhambi.” “Utafanyaje?” akauliza Shetani. “Nitaweka mbele yake anasa za dhambi,” ndilo lilikuwa jibu; “Nitamwambia juu ya furaha zake na thawabu tajiri zitokazo kwake.” “Aa,” akasema Shetani, “hilo halitafaa; ameshalijaribu, na anajua vema kuliko hivyo.”
Ndipo pepo mwingine akainuka akasema, “Nitamfanya atende dhambi.”
“Utafanyaje?” akauliza Shetani. “Nitamwambia juu ya maumivu na huzuni za wema. Nitamwonyesha kwamba wema hauna furaha, wala hauleti thawabu.” “Aa, la!” akapaza sauti Shetani, “Hilo halitafaa hata kidogo.
Ameshalijaribu. Anajua, ‘njia za hekima ni njia za kupendeza, na mapito yake yote ni amani.’ Mwingine akasema, Nitamfanya atende dhambi. Nawe utafanyaje? Akauliza Shetani, tena. Nitaivunja nafsi yake moyo, ndilo lilikuwa jibu fupi. Aa, hilo litafaa,” akalia Shetani, “hilo litafaa! Sasa tutamshinda.” Nao wakamshinda. Mwandishi mmoja wa zamani asema, kukata tamaa kote hutoka kwa ibilisi. Ningetamani kila Mkristo alikumbuke hili na alitunze kama kito cha mfukoni. Ni lazima tuikimbie hali ya kukata tamaa kama tuikimbiavyo dhambi. Lakini hili haliwezekani ikiwa tunashindwa kumtambua mtenda-kazi wa kweli aliye katika jaribu. Kwa maana kama majaribu ni kosa letu wenyewe, hatuwezi kujizuia kukata tamaa. Lakini si kosa letu.
Biblia inasema, “Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, ambayo Mungu aliwaahidia wampendao. ”(Yakobo 1:12) Yatuhimiza “tuhesabu kuwa ni furaha tupu tunapoangukia katika majaribu mbalimbali.” Basi, jaribu haliwezi kuwa dhambi. Si dhambi kusikia minong’ono miovu ndani ya nafsi zetu kuliko ilivyo kusikia matukano ya watu waovu tunapopita njiani. Dhambi huja, katika hali zote mbili, tu kwa kusimama kwetu na kujiunga pamoja nao. Ikiwa, mawazo maovu yajapo, twayaacha mara moja, kama tuachavyo maneno maovu, na kutoyajali, hatutendi dhambi. Lakini tukiyachukua mbele akilini mwetu, na kuyavirisha chini ya ndimi zetu, na kukaa nayo kwa nusu-idhini ya utashi wetu kuwa ni ya kweli, ndipo twatenda dhambi.
Twaweza kushawishiwa na uovu mara elfu kwa siku bila dhambi, wala hatuwezi kujizuia mishawisho hii. Lakini adui akiweza kutufanya tudhani kuwa majaribu yake ni dhambi yetu, atakuwa ameshinda nusu ya vita. Ndipo huenda akashinda kabisa.
Bibi mmoja mpendwa alikuja kwangu wakati mmoja akiwa katika giza kuu, kwa sababu tu ya kutolielewa jambo hili. Alikuwa mwenye furaha sana katika imani yake kwa muda. Alikuwa huru mbali na majaribu, akadhani kwamba hatajaribiwa kamwe tena. Lakini ghafula namna ya ajabu sana ya jaribu ilimshambulia, iliyomtia hofu kuu. Aligundua kwamba mara aanzapo kuomba, mawazo ya kutisha ya kila aina yangefurika akilini mwake. Alikuwa ameishi maisha yaliyohifadhiwa sana, yasiyo na hatia. Mawazo haya yalimwonekana ya kutisha sana, hata akahisi lazima awe mmoja wa waovu kati ya wenye dhambi kuwa nayo. Alianza kwa kudhani kwamba asingaliweza kuingia katika lile pumziko la imani. Akaishia kwa kukata shauri kwamba hakuzaliwa mara ya pili kamwe.
Nafsi yake ilikuwa katika uchungu mkuu wa taabu.
Nilimwambia kwamba mawazo haya ya kutisha yalikuwa kazi ya adui. Alimjia mara aliapopiga magoti katika maombi na kuijaza akili yake nayo. Hakuwa na lawama juu yake hata kidogo. Asingeweza kujizuia zaidi ya vile angeweza kujizuia kusikia mtu mwovu akikufuru mbele yake. Nilimsihi ayaone kama yatokayo kwa adui. Asijilaumu wala asijivunje moyo. Badala yake, amgeukie Yesu na kumkabidhi Yeye. Nilimwonyesha jinsi adui alivyokuwa amepata faida kubwa kiasi gani. Yalimfanya adhani kuwa mawazo haya ni yake mwenyewe. Jambo hili lilimhukumu na kumvunja moyo. Nilimhakikishia kwamba angeshinda upesi kama angeyapuuza. Angepaswa kuyapa kisogo na kumtazama Bwana.
Aliishika ile kweli, na wakati uliofuata mawazo haya yalipokuja alimwambia adui, “Sasa nimekugundua. Ni wewe unayenidokezea mawazo haya ya kutisha, nami nayachukia, wala sitakuwa na shughuli nayo. Bwana ndiye Mwokozi wangu; nyapeleke kwake, ukayamalize mbele za uso wake.”
Adui aliyetatanishwa, akiisha kugunduliwa, akakimbia kwa fadhaa. Nafsi yake ilikombolewa kikamilifu.
Jambo jingine pia. Adui anajua kwamba Mkristo akiona dokezo la uovu kuwa ni lake, atalikataa. Atafanya hivyo upesi zaidi kuliko kama lingeonekana kuwa ni dokezo la akili yake mwenyewe. Kama Shetani angeanza kila jaribu kwa kusema, “Mimi ni Shetani, adui yako; nimekuja kukufanya utende dhambi,” yaelekea tungempinga. Yampasa kujificha ili kuzifanya chambo zake ziwe za kuvutia. Ushindi wetu utakuwa rahisi zaidi kama hatuachi kuzijua hila zake. Ni lazima tumtambue anapokaribia mara ya kwanza. Pia twafanya kosa kuhusu majaribu. Twadhani kwamba muda wote unaotumika kupigana nayo umepotea bure. Saa hupita, nasi twaonekana kama hatujapiga hatua yoyote, kwa sababu tumezidiwa na majaribu. Lakini, huenda tukawa tumemtumikia Mungu kwa kweli zaidi katika saa hizi kuliko nyakati zetu zilizo huru zaidi, tulipokabili majaribu machache.
Kwa kweli jaribu ni hasira ya ibilisi juu ya Mungu, kuliko juu yetu sisi. Hawezi kumgusa Mwokozi wetu.
Lakini, aweza kumjeruhi Yeye kwa kutushinda sisi. Uharibifu wetu wamhusu tu kwa kadiri unavyofanya hivi. Hivyo, twapigana vita vya Bwana wetu tunapoyapinga majaribu. Katika hali hizi, saa moja ina thamani ya siku nzima. Twasoma, “Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, ambayo Mungu aliwaahidia wampendao .”(Yakobo 1:12). Nina hakika hii yamaanisha kustahimili kuendelea kwake na kujirudia kwake mara kwa mara.
Hakuna kitu kinacholeza neema ya saburi kama kustahimili jaribu. Na, hakuna kitu kinachoisukuma nafsi imtegemee Bwana Yesu kama hilo. Na hatimaye, hakuna kitu kiletacho utukufu zaidi kwa Bwana wetu kuliko kujaribiwa kwa imani yetu, kuja kwa njia ya majaribu mengi. Yasemekana kuwa ni ya thamani kuliko dhahabu, ijapokuwa hujaribiwa kwa moto. Sisi, tustahimilio jaribu, tutapokea thawabu. Ndiyo “ile taji ya uzima” ambayo Bwana amewaahidia wampendao Yeye.”
Haishangazi kwamba Roho Mtakatifu ahimiza mwanzoni mwa Kitabu cha Yakobo: “ Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu, bila kupungukiwa na neno lo lote. ”(Yakobo 1:2) Jaribu ni chombo cha Mungu cha kutimiza ukamilifu wetu. Hivyo, silaha za adui mwenyewe hugeuzwa dhidi yake. Twaona kwamba mambo yote, hata majaribu, yaweza kuwafanyia mema wale wampendao Mungu.
Ili kuyapinga majaribu, sina haja ya kuwaambia wasikilizaji wangu: ni kwa imani. Kwa maana hii, bila shaka, ndiyo msingi ambao juu yake maisha yote ya ndani hukaa. Kauli-mbiu yetu moja kuu ni siku zote, “Sisi si kitu, na Kristo ni kila kitu.” Na daima na kila mahali tumeanza kusimama, na kutembea, na kushinda, na kuishi kwa imani. Tumeugundua unyonge wetu wenyewe. Hatuwezi kujisaidia wenyewe. Kwa hiyo, njia yetu pekee ni kulikabidhi jaribu kwa Bwana wetu na kumtumaini alishinde kwa ajili yetu.
Lakini tunapolitia mikononi mwake, ni lazima tuliache pale. Ni lazima tujikabidhi kwake kwa ajili ya ushindi kama tulivyofanya kwa ajili ya wokovu. Ni lazima atufanyie yote katika jambo moja, kikamilifu kama katika lile lingine. Ilikuwa imani tu wakati ule, na ni lazima iwe imani tu sasa.
Bwana hufanya miujiza katika kuyashinda majaribu ya wale wanaomtumaini. Maelfu waweza kulishuhudia hili. Lakini siwezi kulipanua jambo hili sasa. Nililenga kuonyesha jaribu katika mwanga wake wa kweli, si kueleza kwa kina njia ya kulishinda. Nataka kuzikomboa nafsi njema, zenye uaminifu, kutoka utumwani. Zitategwa kama zitachanganya jaribu na dhambi. Ni lazima zielewe asili ya kweli ya jaribu na matumizi yake. Nataka wajue kwamba majaribu ni ya muhimu sana kwa ukuaji wa nafsi zetu. Yawe yatoka wapi, Mungu huyatumia kujenga ndani yetu neema za tabia ambazo vinginevyo zingekosekana.
Popote palipo na jaribu, hapo pia yupo Mungu, akiisimamia na kuiongoza nguvu yake. “Ulikuwa wapi, Bwana, wakati nilipokuwa nikijaribiwa?” akalia yule mtakatifu wa jangwani. “Karibu nawe, mwanangu, wakati wote,” ndilo lilikuwa jibu la upole. Majaribu hutujaribu. Hatufai kitu kama hatujaribiwi. Huikuza nguvu yetu ya kiroho na ujasiri na maarifa, na kukua kwetu ndilo jambo pekee ambalo Mungu hulililia.
Ingekuwa na kina kidogo namna gani hali yetu yote ya kiroho kama isingekuwa majaribu? “Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, ambayo Mungu aliwaahidia wampendao.” Hii “taji ya uzima” itakuwa na thamani ya kustahili taabu zote na ustahimilivu wote unaogharimu kuipata; pasipo hayo, isingeweza kupatikana.
Mwanamke mmoja mgonjwa aliwahi kununua kifukofuko cha kiwavi. Kilikuwa na kipepeo kizuri sana chenye mabawa ya fahari. Alitumaini kukiona kikitoka katika kifukofuko chumbani mwake. Alikitazama kwa hamu kadiri majira ya machipuko yalivyokaribia.
Hatimaye, alifurahi kukiona kile kipepeo kikianza kutoka. Lakini kilionekana kuwa na taabu kuu. Kilisukuma, na kujikaza, na kudhamiria. Kilipiga hatua ndogo sana hata akakata shauri kwamba lazima kihitaji msaada. Kwa mkasi mwembamba, alikata ile kamba iliyokaza mdomo wa kifukofuko.
Mara moja kifukofuko kilifunguka wazi, na kile kipepeo kikatoka bila taabu nyingine yoyote. Alijipongeza mwenyewe kwa mafanikio ya jaribio lake. Lakini, kulikuwa na jambo lisilo sawa na kile kipepeo.
Kilikuwa kimetoka chote katika kifukofuko, ni kweli. Lakini, mabawa yake makubwa yalikuwa bila uhai na bila rangi. Yalijikokota nyuma yake, mzigo usiofaa. Kwa siku chache kiliishi maisha ya taabu na ya ugonjwa, kisha kikafa, bila kuinua kamwe mabawa yake yasiyo na nguvu. Yule bibi alikata tamaa sana wala hakuweza kulielewa. Lakini alipomhadithia mtaalamu wa maumbile jambo hilo, alimwambia kwamba yote yalikuwa kosa lake mwenyewe. Kwamba ni ule msukumo na ule mdhamirio wenyewe uliohitajika ili kupeleka maji ya uhai katika mishipa ya mabawa. Wema wake uliopotoka wa kufupisha ile taabu ulikuwa umeyaacha mabawa bila uhai na bila rangi.
Hivyo, mabawa yetu ya kiroho yanahitaji ile taabu ya kuyapinga majaribu. Kutuokoa nayo kungedhoofisha nguvu ya nafsi zetu ya “kupaa juu kwa mbawa kama tai.” Pia kungetunyima “ile taji ya uzima” waliyoahidiwa wale wastahimilio.