Sura 8 · dakika 29 za kusoma
Salini Bila Kukoma
“Kuomba bila kukoma.”—1 Wathesalonike 5:17.
MAHALI PA ANDIKO LETU ni pa kufikirisha sana. Angalia yale yanayolitangulia. Yanakuja mara tu baada ya agizo, “Furahini sikuzote;” kana kwamba amri hiyo ilimshtua kidogo msomaji, ikamfanya aulize, “Nawezaje kufurahi daima?” na kwa hiyo, mtume aliongeza jibu, “Salini daima.” Kadiri ya kuomba zaidi ndivyo furaha izidivyo. Maombi hutoa mfereji kwa huzuni zilizofungwa ndani ya nafsi, huzuni hizo humwagika, na badala yake vijito vya furaha takatifu humiminika moyoni. Wakati huohuo, kadiri ya furaha zaidi ndivyo maombi yazidivyo; moyo unapokuwa katika hali ya utulivu, na umejaa furaha katika Bwana, ndipo pia utakapohakikisha kumkaribia Bwana katika ibada. Furaha takatifu na maombi hutendeana na kuitikiana.
Lakini angalia, ni nini kinachofuata andiko mara moja: “Shukuruni kwa kila jambo.” Furaha na maombi vinapooana, mzaliwa wao wa kwanza ni shukrani. Tunapofurahi katika Mungu kwa ajili ya tulivyo navyo, na kumwomba kwa imani atupe zaidi, ndipo nafsi zetu humshukuru, katika kuvifurahia tulivyo navyo na katika kutarajia yale yatakayokuja. Maandiko hayo matatu ni picha tatu zinazoandamana, zinazowakilisha maisha ya Mkristo wa kweli; mchoro wa katikati ndio kiungo kinachounganisha vile vilivyo kila upande. Maagizo haya matatu ni pambo la neema shingoni mwa kila mwamini; yavaeni kila mmoja wenu, kwa utukufu na kwa uzuri; “Furahini sikuzote;” “Kuomba bila kukoma;” “shukuruni kwa kila jambo.”
Lakini hatuwezi kutumia muda wowote kuutafakari muktadha, bali ni lazima tuendelee hadi agizo lililo mbele yetu. Andiko letu ingawa ni fupi mno, limejaa ajabu, nasi tutalizungumza chini ya vichwa vifuatavyo. Tutauliza na kujibu maswali manne. Maneno haya yanadokeza nini? Pili, Yanamaanisha nini hasa? Tatu, Tutayatii jinsi gani? Na, nne, Kwa nini SISI hasa tuyatii?
I. MANENO HAYA YANADOKEZA NINI? “Kuomba bila kukoma.” Je, hayadokezi kwamba matumizi ya sauti si kipengele cha lazima katika maombi? Ingekuwa jambo lisilofaa kabisa, hata kama ingewezekana kwetu kuendelea kuomba kwa sauti bila kukoma. Bila shaka hapangekuwapo nafasi ya kuhubiri na kusikiliza, ya kubadilishana mazungumzo ya kirafiki, ya biashara, wala ya wajibu mwingine wowote wa maisha; huku ghasia ya sauti nyingi kiasi hicho ikiwakumbusha majirani zetu ibada ya Baali kuliko ile ya Sayuni. Haikuwa kamwe kusudi la Bwana Yesu kwamba makoo yetu, mapafu, na ndimi zetu vifanye kazi milele. Kwa kuwa tunapaswa kuomba bila kukoma, na hata hivyo hatungeweza kuomba kwa sauti bila kukoma, ni dhahiri kwamba lugha inayosikika si ya lazima katika maombi. Twaweza kunena maneno elfu yanayoonekana kuwa maombi, na hata hivyo tusiombe kamwe; kwa upande mwingine, twaweza kumlilia Mungu masikioni mwake kwa nguvu kabisa, na hata hivyo tusinene neno lolote. Katika kitabu cha Kutoka Mungu anaonyeshwa akimwambia Musa, “Mbona unanililia mimi?” Na hata hivyo haikuandikwa kwamba Musa alikuwa ametamka hata silabi moja wakati ule. Ni kweli kwamba matumizi ya sauti mara nyingi husaidia maombi. Mimi binafsi, naona kwamba naweza kuomba vizuri zaidi nikiwa peke yangu ikiwa naweza kuisikia sauti yangu mwenyewe; wakati huohuo si jambo la lazima, haliingii hata kidogo katika kukubalika, uhalisia, wala nguvu ya maombi. Kimya ni vazi linalofaa kwa ibada kama vazi lolote ambalo lugha yaweza kulifuma.
Ni dhahiri vivyo hivyo kwamba mkao wa maombi si wa umuhimu mkubwa, kwa maana kama ingekuwa lazima tuombe tukiwa tumepiga magoti tusingeweza kuomba bila kukoma; mkao ungekuwa wenye maumivu na madhara. Muumba wetu ametupa miguu kwa kusudi gani, kama hataki tusimame juu yake kamwe? Kama angalikusudia tuwe magotini bila kukoma, angeliuumba mwili kwa namna nyingine, wala asingelitupa urefu huo usio wa lazima wa viungo. Ni vyema kuomba kwa magoti; ni mkao unaofaa sana; ni ule unaoonyesha unyenyekevu, na unyenyekevu unapohisiwa kweli, kupiga magoti ni ishara ya asili na nzuri yake, lakini, wakati huohuo, watu wema wameomba wakiwa wamelala kifudifudi, wameomba wakiwa wameketi, wameomba wakiwa wamesimama, wameomba katika mkao wowote, na mkao hauingii katika kiini cha maombi. Msikubali kutiwa utumwani na wale ambao kwao goti lililopigwa lahesabiwa kuwa la maana zaidi kuliko moyo uliopondeka.
Ni dhahiri pia, kutokana na andiko, kwamba mahali si pa lazima katika maombi, kwa maana kama pangekuwapo mahali fulani patakatifu tu ambapo maombi hukubalika, nasi ni lazima tuombe bila kukoma, makanisa yetu yangepaswa kuwa makubwa mno, ili tuweze kuishi humo daima, na yangepaswa kuwa na mipango yote inayohitajiwa kwa makazi ya wanadamu. Kama ni kweli kwamba kuna utakatifu fulani upande huu wa ukuta wa matofali kuliko ulivyo upande wa pili wake, kama ni kweli kwamba hewa safi huipeperusha neema, na kwamba ili tukubalike zaidi tunahitaji matao yaliyopindwa, nguzo, njia za kanisani, madhabahuni, na mabawa ya jengo, basi kwaherini, enyi vichochoro vya kijani, na bustani nzuri, na misitu ya kupendeza, kwa maana tangu sasa ni lazima, bila kukoma, tukae mahali ambapo harufu yenu nzuri na uburudisho wenu haviwezi kutufikia kamwe. Lakini haya ni ya kipuuzi; kwa hiyo nahitimisha kwamba kuhudhuria mahali fulani hususa hakuna uhusiano wowote, au hakuna mwingi, na maombi; na hitimisho kama hilo lapatana na neno la Paulo juu ya Kilima cha Mars, “Mungu aliyeuumba ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, kwa kuwa yeye ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono.”
“Kuomba bila kukoma.” Agizo hilo kwa pigo moja huipindua fikira ya nyakati fulani ambazo ndani yake maombi hukubalika zaidi au huwa ya kufaa zaidi kuliko nyakati nyingine. Kama ninapaswa kuomba bila kukoma, basi kila nukta lazima iwe inayofaa kwa maombi, wala hakuna dakika moja isiyo takatifu katika saa, wala saa moja isiyokubalika katika siku, wala siku moja isiyotakaswa katika mwaka. Bwana hakuweka juma fulani kwa ajili ya maombi, bali majuma yote yapaswa kuwa majuma ya maombi; wala hakusema kwamba saa moja ya siku hukubalika zaidi kuliko nyingine. Nyakati zote zinafaa sawasawa kwa dua, ni takatifu sawasawa, hukubalika sawasawa mbele za Mungu, ama sivyo tusingeambiwa kuomba bila kukoma. Ni vyema kuwa na nyakati zenu za maombi; ni vyema kutenga majira kwa ajili ya dua za pekee—hatuna shaka juu ya hilo; lakini kamwe hatuna budi kutokuruhusu jambo hili lizae ushirikina kwamba kuna saa fulani takatifu ya maombi asubuhi, saa inayokubalika hususa kwa maombi jioni, na wakati mtakatifu wa maombi katika majira fulani ya mwaka. Popote tumtafutapo Bwana kwa mioyo ya kweli hupatikana kwetu; wakati wowote tumliliapo hutusikia. Kila mahali ni ardhi takatifu kwa moyo uliotakaswa, na kila siku ni siku takatifu kwa mtu mtakatifu. Tangu Januari hadi Desemba kalenda haina tarehe hata moja ambayo ndani yake maombi yamekatazwa. Siku zote ni siku za baraka, ziwe za Sabato au za kazi, zote ni nyakati zinazokubalika kwa maombi. Basi ni dhahiri, kutokana na andiko, kwamba sauti, mkao, mahali, wakati—hakuna hata kimojawapo kinachoingia katika kiini cha maombi, ama sivyo, katika hali hii, tungeamriwa kutenda jambo lisilowezekana, ambalo tuna hakika kabisa kwamba si kwa mtindo wa Bwana Mungu wetu.
Kuna jambo jingine moja linalodokezwa katika andiko, yaani, kwamba Mkristo hana haki ya kuingia mahali popote ambapo asingeweza kuendelea kuomba. Kuomba bila kukoma? Basi kamwe sitakuwa mahali ambapo nisingeweza kuomba bila kukoma. Kwa hiyo, tafrija nyingi za kidunia, bila kuzitaja moja moja, zaweza kuhukumiwa na kulaaniwa papo hapo. Watu fulani huamini maombi yaliyotengenezwa tayari, yaliyokatwa na kukaushwa kwa ajili ya hafla zote, na, wakati huohuo, huamini kwamba watu wamezaliwa upya katika ubatizo ingawa maisha yao si ya Kikristo hata kidogo; je, hawapaswi kuandaa maombi kwa ajili ya hali zote ambazo ndani yake hawa, wana na binti wapendwao waliozaliwa upya lakini wasio na neema wa kanisa lao, wanapatikana? Kwa mfano, sala ya kicho kwa ajili ya mkuu kijana au mtu mashuhuri, ambaye yu karibu kwenda kwenye mashindano ya kupiga risasi, ili asamehewe kwa ukatili wake kwa njiwa hao maskini ambao wamejeruhiwa vibaya tu na kuachwa kudumu katika taabu; kadhalika sala kwa ajili ya bwana mwenye dini na aliyezaliwa upya anayekwenda kwenye mbio za farasi, na sala kwa ajili ya vijana waliopokea neema ya kipaimara, wanapokwenda kwenye ukumbi wa michezo kutazama mchezo wenye shaka sana. Je, sala hizo za pekee hazingeweza kutengenezwa kwa agizo? Wewe wachukizwa na wazo hilo. Basi, usiwe na uhusiano wowote na kile ambacho huwezi kumwomba Mungu abariki; usiwe na uhusiano nacho, kwa maana kama Mungu hawezi kukibariki, waweza kuwa na hakika kwamba ibilisi amekilaani. Kila jambo lililo halali kwako kulitenda waweza kulitakasa kwa maombi; na hili na liwe kipimo na jaribio la hakika kwako: ikiwa unahisi kwamba lingekuwa ni tusi kwa fahari ya mbingu wewe kumwomba Bwana abariki kile kinachopendekezwa kwako, basi jitenge na kitu hicho kisicho kitakatifu. Kama Mungu hakubali, wala wewe usiwe na ushirika nacho.
Mambo haya yanadokezwa waziwazi katika agizo, “Kuomba bila kukoma.”
II. Lakini sasa, JAMBO HILI LAMAANISHA NINI HASA? Ikiwa halimaanishi kwamba tunapaswa kuwa magotini daima, wala kusema maombi daima, wala kuwa kanisani au mkutanoni daima, na halimaanishi kwamba tunapaswa kuihesabu siku yoyote kuwa haifai kwa kuomba, basi ni nini? Maneno hayo yamaanisha, kwanza, pendeleo; pili, agizo—“Kuomba bila kukoma.” Bwana wetu Yesu Kristo katika maneno haya anakuhakikishia kwamba waweza kuomba bila kukoma. Hakuna wakati ambao hatuwezi kuomba. Hapa umepewa ruhusa ya kukikaribia kiti cha rehema utakapo, kwa maana pazia la mahali Patakatifu Zaidi limepasuka vipande viwili tangu juu hata chini, na kufikia kwetu kiti cha rehema hakubishaniwi wala hakuwezi kubishaniwa. Wafalme hufanya mikutano yao ya kupokea wageni katika siku fulani zilizowekwa, ndipo watumishi wa mahakama zao hukubaliwa kuingia; lakini Mfalme wa wafalme ana mkutano wa kupokea usiokoma. Mfalme ambaye jumba lake la kifalme lilikuwa Shushani hangeruhusu yeyote amkaribie asipomtuma kumwita, lakini Mfalme wa wafalme amewaita watu wake wote, nao waweza kuja nyakati zote. Waliuawa wale walioingia kwa mfalme Ahasuero, isipokuwa awanyoshee fimbo yake ya ufalme; lakini Mfalme wetu kamwe haiondoi fimbo yake, imenyoshwa daima, na kila atakaye kumjia aweza kuja sasa, na kuja wakati wowote. Miongoni mwa Waajemi walikuwako wachache wa waheshimiwa waliokuwa na haki ya pekee na ya hususa ya kuonana na mfalme wakati wowote waliopenda. Basi, kile kilichokuwa haki ya pekee ya wachache sana na ya wakuu sana, ndicho pendeleo la kila mtoto wa Mungu. Aweza kuingia kwa Mfalme nyakati zote. Kiwango cha usiku wa manane si kuchelewa mno kwa Mungu; kupambazuka kwa asubuhi, wakati mwanga wa kwanza wa kijivu uonekanapo, si mapema mno kwa Aliye Juu; wakati wa adhuhuri hana shughuli nyingi mno; na jioni ikusanyikapo hachoki na maombi ya watoto wake. “Kuomba bila kukoma,” ni, kama nikilisoma sawasawa, ni ruhusa tamu na ya thamani sana kwa mwamini kuumimina moyo wake nyakati zote mbele za Bwana. Nasikia sauti yake ndogo ya utulivu ikisema, “Njoo kwenye kiti cha rehema, Ee mwanangu, wakati wowote utakao; njoo kwenye hazina ya neema wakati wowote utamaniyo.”
“Malango yenye furaha ya neema ya injili
Yasimama wazi usiku na mchana.”
Milango ya hekalu la upendo wa Mungu haitafungwa. Hakuna kitu chochote kiwezacho kuweka kizuizi kati ya nafsi iombayo na Mungu wake. Njia ya malaika na ya maombi i wazi daima. Na tuipeleke tu njiwa ya maombi, nasi twaweza kuwa na hakika kwamba atatururudia akiwa na tawi la mzeituni la amani kinywani mwake. Sikuzote Bwana huyaangalia madua ya watumishi wake, naye angoja ili awafadhili.
Hata hivyo, bado ni agizo, “Kuomba bila kukoma.” Nalo lamaanisha nini? Lamaanisha kweli kuu ambayo siwezi kuiwasilisha kwenu vizuri kwa maneno machache, na kwa hiyo, ni lazima nijaribu kuidhihirisha chini ya vidokezo vinne au vitano.
Lamaanisha, kwanza, usiache kamwe maombi. Kamwe kwa sababu wala kwa hoja yoyote usikome kuomba. Usidhani kwamba yakupasa kuomba mpaka uokolewe, kisha waweza kuacha. Kwa wale ambao dhambi zao zimesamehewa maombi ni ya lazima kabisa kama yalivyo kwa wale wanaoomboleza chini ya hisia ya dhambi. “Kuomba bila kukoma,” kwa maana ili udumu katika neema ni lazima udumu katika maombi. Ukija kuwa mwenye uzoefu katika neema na kutajirishwa kwa maarifa mengi ya kiroho, usiwaze kamwe kuyazuia maombi kwa sababu ya vipawa na neema zako. “Kuomba bila kukoma,” ama sivyo ua lako litanyauka na tunda lako la kiroho halitaiva kamwe. Dumu katika maombi hata dakika ya mwisho ya maisha yako.
“Maadamu waishi lazima Wakristo waombe,
Kwa maana ni maadamu waombapo ndipo waishipo.”
Kama tupumuavyo bila kukoma, ndivyo yatupasavyo kuomba bila kukoma. Kama vile hakuna kufikia kwa lolote maishani, la afya, wala la nguvu, wala la uhodari wa misuli, kuwezako kumweka mtu nje ya lazima ya kupumua, ndivyo hakuna hali ya kukua kiroho au kuendelea katika neema itakayomruhusu mtu kuachana na maombi.
“Na tuombe! maisha yetu ni kuomba;
Maombi pamoja na wakati peke yao yaweza kukoma:
Ndipo mbinguni, tukiyatii mapenzi ya Mungu,
Uhai ni sifa na amani kamili.”
Kamwe usiache kuomba, hata kama Shetani angekushawishi kwamba ni bure wewe kumlilia Mungu. Omba mbele ya meno yake; “kuomba bila kukoma.” Ikiwa kwa muda mbingu zimekuwa kama shaba na maombi yako yanavuma tu kama radi juu ya kichwa chako, endelea kuomba; ikiwa mwezi baada ya mwezi maombi yako yaonekana kuwa yamepotea, wala hujajaliwa jibu lolote, bado endelea kumkaribia Bwana. Usikiache kiti cha rehema kwa sababu yoyote ile. Ikiwa ni jambo jema ambalo umekuwa ukiliomba, nawe una hakika kwamba ni kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu, kama maono yakikawia yangoje, omba, lia, sihi, shindana, tahayari mpaka upate kile unachokiombea. Ikiwa moyo wako u baridi katika maombi, usiyazuie maombi mpaka moyo wako upate joto, bali iombee nafsi yako mpaka ipate joto kwa msaada wa Roho abarikiwaye milele asaidiaye udhaifu wetu. Ikiwa chuma ni cha moto basi kifue, na kama ni baridi kifue mpaka ukipe joto. Kamwe usikome kuomba kwa aina yoyote ya sababu au hoja. Ikiwa mwanafalsafa atakuambia kwamba kila tukio limewekwa tayari, na kwa hiyo, maombi hayawezi kabisa kubadili kitu chochote, na, kwa sababu hiyo, ni lazima yawe upumbavu; hata hivyo, kama huwezi kumjibu nawe umetatizika kidogo, endelea na dua zako bila kujali yote hayo. Hakuna tatizo gumu kuhusu umeng'enyaji lingekuzuia kula, kwa maana matokeo yake huhalalisha tendo; vivyo hivyo hakuna ubishi wowote ungetufanya tukome kuomba, kwa maana mafanikio yake ya hakika hutupendekezea. Wajua yale ambayo Mungu wako amekuambia, na kama huwezi kujibu kila ugumu ambao mwanadamu aweza kuupendekeza, azimu kuyatii mapenzi ya Mungu, na bado “Kuomba bila kukoma.” Kamwe, kamwe, kamwe usiukane mazoea ya maombi, wala ujasiri wako katika nguvu yake.
Maana ya pili ni hii. Kamwe usisitishe utoaji wa kawaida wa maombi. Ukiwa Mkristo mwenye kukesha, utakuwa na nyakati zako za ibada ya kila siku, zisizowekwa kwa ushirikina, bali kwa urahisi wako na ukumbusho; kama vile Daudi, mara tatu kwa siku, na kama mtakatifu mwingine, mara saba kwa siku, alivyomtafuta Bwana: sasa hakikisha kudumisha maombi haya ya kila siku bila kukatiza. Shauri hili halitakusanya wigo wote wa andiko, sidai kwamba linakusanya; ninalitaja tu sasa kuwa nyongeza kwa mawazo mengine. “Kuomba bila kukoma;” yaani, kamwe usiache maombi ya asubuhi, wala maombi ya jioni, wala maombi ya adhuhuri ikiwa hayo yamekuwa desturi yako. Ukibadili saa na nyakati, kama waweza, bado dumisha zoea la kujitenga, kutafakari, na kuomba kwa nyakati zinazorudi kwa ukawaida. Waweza kusemwa kuwa unadumu katika maombi ikiwa ibada zako za kawaida zinadumishwa. Ingekuwa sawa kabisa kwangu kusema kwamba namjua mtu aliyekuwa akiomba-omba daima tangu nilipokuja Londoni. Sidhani kama nimewahi kupita mahali asimamapo bila kumwona hapo. Ni mtu kipofu, na husimama karibu na kanisa. Kwa kadiri kumbukumbu langu linavyonitumikia amekuwa akiomba-omba bila kukoma; bila shaka hakuomba-omba alipokuwa amelala, hakuomba-omba alipokwenda nyumbani chakulani, wala hamkunielewa kwamba nilidai jambo la kipuuzi kiasi hicho niliposema kwamba amekuwa akiomba-omba bila kukoma kwa miaka mingi. Na hivyo, ikiwa katika nyakati zile ambazo yakupasa kujitenga na kazi zako za kawaida, unaendelea kwa bidii kuomba-omba katika kiti cha enzi cha rehema, yaweza kusemwa juu yako kwa usahihi wa kadiri kwamba unaomba bila kukoma. Ingawa saa zote ni sawa kwangu, naona ni faida kukutana na Mungu katika vipindi vilivyowekwa, kwa maana hivyo vyaonekana kwangu kama kuzungusha kwa saa ya ukutani. Saa ile ipaswa kwenda mchana kutwa, lakini kuna wakati wa kuizungusha; na kile kipindi kidogo cha pekee tunachokitenga na kukizungushia uzio kwa ushirika na Mungu wetu, chaonekana kutuzungusha kwa ajili ya sehemu iliyobaki ya siku. Kwa hiyo, kama ungependa kuomba bila kukoma, dumu katika kutoa dhabihu ya asubuhi na ya jioni, na iwe kwako amri ya daima, kwamba nyakati zako za maombi hazivunjwi.
Hilo, hata hivyo, ni msaada tu, kwa maana ni lazima niongeze, tatu, kati ya nyakati hizi za ibada, jitahidi kuwa mwingi katika maombi ya haraka-haraka. Wakati mikono yako ina shughuli na dunia, iache mioyo yenu ingali ikizungumza na Mungu; si kwa sentensi ishirini kwa wakati mmoja, kwa maana muda kama huo waweza kutopatana na wito wako, bali kwa sentensi zilizovunjika na vielezi. Ni kosa sikuzote kumtolea Mungu wajibu mmoja uliochafuliwa kwa damu ya mwingine, na hilo ndilo tungelifanya kama tungeliharibu kusoma au kazi kwa kukimbia kwenda kuomba kila saa; lakini twaweza, bila hili, kuziacha sentensi fupifupi zipande mbinguni, naam, na twaweza kupiga kilio juu, na maneno pekee, kama vile “Ah,” au “Oh,” au “Laiti;” au, bila maneno twaweza kuomba kwa kuinua jicho juu au kwa kuugua kwa moyo. Yeye aombaye bila kukoma hutumia mishale midogo mingi na maguruneti ya mkono ya tamaa ya kimungu, ambayo huyatupa kila nafasi ipatikanapo. Wakati mwingine ataivukuta tanuru ya tamaa zake ipate joto kubwa katika maombi ya kawaida, na kwa sababu hiyo nyakati nyingine, cheche zitaendelea kupanda mbinguni kwa namna ya maneno mafupi, na mitazamo, na tamaa.
Nne, kama tungependa kuomba bila kukoma, ni lazima tuwe daima katika roho ya maombi. Moyo wetu, uliofanywa upya na Roho Mtakatifu, lazima uwe kama sindano yenye sumaku, ambayo daima ina mwelekeo kuelekea ncha ya dunia. Haielekei sikuzote kwa ncha ile, waweza kuigeuza kando kama utakavyo; katika meli ya chuma huonyesha mikengeuko mikubwa, katika hali zote si sahihi kabisa; lakini ukiiweka kidole chako kwenye sindano ile na kuilazimisha izunguke hata mashariki, huna budi ila kuuondoa msukumo, na papo hapo hurudi tena kwa ncha yake ipendayo. Basi acha moyo wako utiwe sumaku kwa maombi, ili kwamba kama kidole cha wajibu kikiugeuza mbali na tendo la moja kwa moja la maombi, ingaliweko tamaa ya shauku ya maombi katika nafsi yako, na mara utakapoweza kufanya hivyo, moyo wako urejee kwenye kazi yake ipendayo. Kama manukato yalivyo ndani ya maua hata wakati hayamwagi harufu yake nzuri katika upepo, ndivyo iache maombi yalale mioyoni mwenu.
Lakini, labda, maana ya mwisho nitakayoitoa ina kweli ya andiko iliyo nyingi zaidi ndani yake, yaani hii: Acha matendo yako yote yapatane na maombi yako, na kwa hakika yawe ni mwendelezo wa maombi yako. Kama ninapaswa kuomba bila kukoma, haiwezi kumaanisha kwamba nipaswa kuwa daima katika tendo la ibada ya moja kwa moja; kwa maana akili ya mwanadamu, kama ilivyoumbwa kwa sasa, yahitaji shughuli za namna mbalimbali, wala isingeweza, bila kutokeza wazimu au upumbavu, kuendelea daima katika kutenda kazi moja. Kwa hiyo ni lazima tubadili modus au namna ya utendaji ikiwa tutaendelea bila kukoma katika maombi. Ni lazima tuyafuatilie maombi yetu, lakini tulifanye kwa namna nyingine. Chukua mfano. Asubuhi ya leo nilimwomba Mungu awaamshe watu wake kupenda maombi; vema sana; nilipokuja katika nyumba hii nafsi yangu iliendelea kupaza, “Ee Bwana, waamshe watoto wako kupenda maombi.” Sasa, wakati ninawahubiria ninyi na kulenga jambo lilo hilo, je, siombi? Je, mahubiri yangu si mwendelezo wa maombi yangu, kwa maana natamani na kulenga jambo lilo hilo? Je, si kuendelea kuomba tunapotumia njia zilizo bora katika kupata kile tunachokiombea? Je, huoni jambo langu? Yeye aombaye kwa ajili ya viumbe wenzake, kisha akatafuta hali yao njema, angali akiomba. Kwa maana hii kuna kweli katika ubeti ule wa kale.
“Aombaye vyema ni yeye apendaye vyema
Mtu, na ndege, na mnyama pia.”
Kupenda ni kuomba. Kama natafuta katika maombi hali njema ya kiumbe mwenzangu, kisha nikaenda na kujaribu kuiendeleza, kwa vitendo ninaiombea hali yake njema katika matendo yangu. Kama natafuta, kama inipasavyo, utukufu wa Mungu kuliko kila kitu, basi kama matendo yangu yote yamekusudiwa kuelekea utukufu wa Mungu, ninaendelea kuomba, ingawa huenda nisiombe kwa mawazo yangu wala kwa midomo yangu. Ee, laiti maisha yetu yote yangekuwa maombi. Yaweza kuwa hivyo. Kwaweza kuwako kuomba bila kukoma mbele za Bwana, ingawa kwaweza kuwako vituo vingi katika kile ambacho wengi wa watu wangekiita maombi. Basi omba bila kukoma, ndugu yangu. Acha maisha yako yote yawe ni kuomba. Ukibadili mbinu, usibadili lengo; bali endelea kuabudu, endelea kusujudu. Hii nadhani ndiyo maana ya andiko letu—kamwe usiache kabisa maombi; usisitishe utoaji wa kawaida wa maombi; uwe mwingi katika maombi ya bidii, uwe daima katika roho ya maombi, na acha maisha yako yote yapatane na maombi yako, na yawe sehemu yake.
III. TWAWEZAJE KUYATII MANENO HAYA? Kwanza, na tujitahidi kadiri tuwezavyo kuvizuia vikwazo vyote vya dhambi. “Kuomba bila kukoma.” Basi ikiwa haiwezekani kuwa katika tendo la maombi daima, angalau na tuwe katika tendo hilo kadiri iwezekanavyo; na tuvizuie vile vikwazo nilivyovitaja mwanzoni mwa hotuba yangu, vikwazo vinavyosababishwa na dhambi yetu wenyewe. Na tujitahidi kujiepusha, kadiri tuwezavyo, na kila kitu na chochote ndani yetu, au kinachotuzunguka, kingezuia wingi wetu katika dua. Nasi pia na tujiepushe na vikwazo vitokanavyo na dhambi za wengine. Je, wengine wanatukataza kuomba? Tusiogope hasira yao. Mkumbukeni Danieli, ambaye wakati alipokuwa chini ya adhabu ya kutupwa katika tundu la simba, hata hivyo alifungua dirisha lake kuelekea Yerusalemu, na kuomba mara saba kwa siku kama alivyokuwa amefanya tangu zamani. Chini ya vitisho vyovyote, na kwa rushwa yoyote, tusikome kamwe kuomba. Faraghani na tuombe daima, na ikiwa wajibu watuita kufanya hivyo mahali ambapo wengine wanatuona, na tuyaogope hivyo sana macho ya Mungu hata tusithubutu kuyaogopa macho ya mwanadamu.
Kisha na tuepuke vikwazo vyote visivyo vya lazima vya kila namna kwa maombi yetu. Kama tunajua kwamba jambo lolote, ambalo twaweza kuliepuka, lina mwelekeo wa kusumbua roho ya maombi ndani yetu, na tuliepuke kwa bidii. Na tujaribu, kadiri iwezekanavyo, tusipoteze mkondo katika maombi. Kusudi la Shetani litakuwa ni kuiondoa akili, kuiangusha nje ya njia, kuligeuza lengo lake, lakini na tuazimu mbele za Mungu, hatutakengeuka na kuacha kumfuata kwa bidii. Sir Thomas Abney kwa miaka mingi alikuwa akitenda maombi ya jamaa kwa ukawaida; alichaguliwa kuwa Meya Mkuu wa Londoni, na usiku wa uchaguzi wake ilimpasa kuhudhuria karamu, lakini wakati ulipofika wa kuwaita jamaa yake pamoja kwa maombi, akiwa hana nia ya kuwa Farisayo wala ya kuacha zoea lake, aliwaomba radhi wageni kwa namna hii—alisema alikuwa na miadi ya maana na rafiki mpendwa sana, nao wangempa radhi kwa dakika chache. Ilikuwa kweli kabisa, rafiki yake mpendwa zaidi alikuwa Bwana Yesu, na maombi ya jamaa yalikuwa miadi ya maana; na hivyo alijitenga kwa muda kuelekea madhabahu ya jamaa, na kwa jambo hilo aliomba bila kukoma. Wakati mwingine twaruhusu mambo mema kuyakatiza maombi yetu, na hivyo kuyafanya kuwa mabaya. Bibi Rowe aeleza katika mojawapo ya barua zake, kwamba kama mitume kumi na wawili wangekuwa wakihubiri katika mji aliokaa naye asingeweza kuwasikia tena kamwe, kama ungekuwa wakati wake wa ibada ya faragha, asingehongwa kutoka chumba chake cha ndani kwa tumaini la kuwasikia. Sina hakika ila kwamba angeliweza kuchukua wakati mwingine kwa ibada zake za faragha, na hivyo kufurahia mapendeleo yote mawili, lakini wakati huohuo, tukidhani kwamba ilimpasa apoteze maombi na kupata mahubiri tu badala yake, nakubaliana naye, ingekuwa ni kubadilishana dhahabu kwa fedha. Angefaidika zaidi katika kuomba kuliko angavyofaidika katika kusikiliza, kwa maana kuomba ndicho mwisho wa mahubiri. Mahubiri ni bua tu la ngano, bali kuomba ni chembe ya dhahabu yenyewe, na yeye aipataye ndiye aliye na kilicho bora.
Wakati mwingine twadhani tumeshughulika mno tusiweze kuomba. Hilo pia ni kosa kubwa, kwa maana kuomba ni kuokoa wakati. Wakumbuka neno la Lutheri, “Nina mengi ya kufanya leo hata sitalimaliza kwa maombi ya chini ya saa tatu.” Hakuwa amezoea kuchukua muda mwingi kiasi hicho kwa maombi katika siku za kawaida, lakini kwa kuwa ile ilikuwa siku ya shughuli nyingi, ilimbidi awe na ushirika zaidi na Mungu wake. Lakini, labda, shughuli zetu huanza mapema, na kwa hiyo twasema, “Nitawezaje kuwa peke yangu na Mungu katika maombi?” Yasemwa juu ya Sir Henry Havelock kwamba kila asubuhi wakati msafara ulipoanza saa sita, yeye daima aliamka saa nne, ili asikose wakati wake wa kusoma Maandiko na ushirika na Mungu wake. Kama hatuna wakati ni lazima tuutengeneze, kwa maana kama Mungu ametupa wakati kwa wajibu wa daraja la pili, ni lazima atupewe wakati kwa ule wa daraja la kwanza, na kumkaribia yeye ni wajibu wa daraja la kwanza, wala hatuna budi kuacha kitu chochote kiuweke kando. Hakuna haja halisi ya kutoa dhabihu wajibu wowote, tuna wakati wa kutosha kwa yote kama hatuko wavivu; na, kwa kweli, mmoja utausaidia mwingine badala ya kugongana nao. Edward Payson alipokuwa mwanafunzi Chuoni, aliona alikuwa na mengi ya kufanya kuhudhuria masomo yake na kujiandaa kwa mitihani, hata asingeweza kutumia muda kama upasavyo katika maombi ya faragha; lakini, mwishowe, alipoamka na hisia kwamba alikuwa akirudi nyuma katika mambo ya kimungu kwa sababu ya mazoea yake, alichukua muda upasao kwa ibada, naye adai katika shajara yake kwamba alifanya mengi zaidi katika masomo yake katika juma moja baada ya kutumia muda na Mungu katika maombi, kuliko alivyokuwa amefanya katika miezi kumi na miwili iliyotangulia. Mungu aweza kuzidisha uwezo wetu wa kutumia wakati. Kama tukimpa Bwana haki yake, tutakuwa na wa kutosha kwa makusudi yote ya lazima. Katika jambo hili tafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa. Miadi yenu mingine itakwenda vyema kama hamtaisahau miadi yenu na Mungu.
Ni lazima, wapendwa marafiki, ili tuombe bila kukoma, tupambane na uzembe katika maombi. Naamini kwamba hakuna mtu apendaye maombi mpaka Roho Mtakatifu amemfundisha utamu na thamani yake. Kama umewahi kuomba bila kukoma utaomba bila kukoma. Watu wasiopenda kuomba lazima wawe wageni kwa furaha yake ya siri. Maombi yanapokuwa tendo la kimekanika, wala hamna nafsi ndani yake, ni utumwa na uchovu; lakini yanapokuwa kweli maombi yaliyo hai, na mtu aombapo kwa sababu ni Mkristo wala hawezi kujizuia kuomba, aombapo njiani, aombapo katika biashara yake, aombapo nyumbani, aombapo shambani, wakati nafsi yake yote imejaa maombi, ndipo hawezi kuwa na maombi mengi mno. Hatakuwa nyuma katika maombi yeye akutanaye na Yesu ndani yake, bali yeye asiyemjua yule Mpendwa atayahesabu kuwa kazi ngumu ya kuchosha.
Na tuepuke, zaidi ya vitu vyote, ulegevu na kutojali katika maombi. Ee, ni jambo la kutisha kwamba tuweze kuitukana fahari ya mbingu kwa maneno ambayo moyo wetu umeondoka. Ni lazima, ee roho yangu, ni lazima nikufundishe hili, kwamba lazima uwe na ushirika na Mungu, na kama katika maombi yako husemi na Mungu, utaendelea kuomba hata usemapo. Usiondoke kwenye kiti cha rehema hata uwe umeomba.
Ndugu mpendwa, sema na nafsi yako, hivi—“hapa nimekuja kwenye kiti cha enzi cha neema kumwabudu Mungu na kutafuta baraka yake, wala sitaondoka hata nilifanye hili; sitainuka kutoka magotini mwangu, kwa sababu nimetumia dakika zangu za kawaida, bali hapa nitaomba hata niipate baraka.” Shetani mara nyingi ataacha kushawishi anapokukuta hivyo ukiwa imara katika maombi. Ndugu zangu, twahitaji kuamshwa. Mazoea ya kawaida hutuzidia. Twaingia katika mtindo wa farasi wa kinu—kuzunguka, na kuzunguka, na kuzunguka kinu. Mungu na atuokoe na hili. Ni lenye kufisha. Mtu aweza kuomba miaka ishirini kwa ukawaida, kwa kadiri ya wakati, na kwa kadiri ya namna, wala asiwe ameomba hata chembe moja ya maombi katika kipindi chote. Kuugua kumoja kwa kweli kulikochotwa moyoni kwafaa kuliko sala milioni moja, pumzi moja iliyo hai kutoka nafsi yenye neema yafaa kuliko sala elfu kumi. Na tuwekwe macho kwa neema ya Mungu, tukiomba bila kukoma.
Nasi ni lazima tuwe waangalifu, ndugu wapendwa, tena, kama tungependa kutimiza wajibu huu, kwamba tupambane na chochote kama kukata tamaa ya kusikiwa. Kama hatujasikiwa baada ya mara sita ni lazima, kama Eliya, tuende tena mara saba; kama Petro wetu yumo gerezani, na kanisa limemwomba Mungu amfungue, naye angali amefungwa minyororo katika gereza la ndani, na tuendelee kuomba, kwa maana siku moja kati ya hizi Petro atagonga langoni. Uwe mwenye kudumu, lango la mbingu halifunguki kwa kila kugonga kwa mkimbiaji. Gonga, na gonga, na gonga tena; na uongeze kwa kugonga kwako na kwa kuomba kwako kutafuta, wala usiridhike hata upate jibu la kweli.
Kamwe usikome kuomba kwa sababu ya kujiona; jihadhari na hilo. Hisi, Ee Mkristo, kwamba wahitaji kuomba daima. Usiseme, “Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sihitaji kitu.” Wewe kwa asili bado u uchi, na maskini, na wa kuhurumiwa; kwa hiyo, dumu katika maombi, na ununue kwa Bwana dhahabu iliyo safi, na mavazi safi, ili upate kuwa tajiri, na kuvikwa kwa kufaa.
Hivyo nimejaribu kuweka mbele yenu, wapendwa, jinsi kwa kupinga kujiona na kukata tamaa, uzembe na ulegevu, na kwa kujaribu kuweka kando vikwazo vyote vya dhambi na vinginevyo, twaweza kuomba bila kukoma.
IV. Sasa, kwa ufupi sana, mahali pa mwisho, KWA NINI TUYATII AGIZO HILI? Bila shaka twapaswa kuyatii kwa sababu lina mamlaka ya Mungu; lakini, zaidi ya hayo, twapaswa kulizingatia kwa sababu Bwana daima anastahili kuabudiwa. Maombi ni njia ya kuabudu; kwa hiyo, endelea daima kumtolea Muumba wako, Mhifadhi wako, Mkombozi wako, Baba yako, heshima ya maombi yako. Kwa Mfalme kama huyo tusiwe walegevu katika kutoa heshima. Na tumlipe ushuru wa sifa daima. Sikuzote na tulitukuze na kulibariki jina lake. Adui zake wanamlaani; sisi na tumbariki bila kukoma. Zaidi ya hayo, ndugu zangu, roho ya upendo iliyo ndani yetu bila shaka hutusukuma kumkaribia Mungu bila kukoma. Kristo ni mume wetu. Je, bibi arusi ni mwaminifu kwa nadhiri zake za ndoa ikiwa hajali kuwa na mpendwa wake? Mungu ni Baba yetu. Ni mtoto wa namna gani asiyetamani kupanda goti la baba yake na kupokea tabasamu kutoka uso wa baba yake? Kama wewe na mimi tunaweza kuishi siku baada ya siku na juma baada ya juma bila kitu chochote kama ushirika na Mungu, upendo wa Mungu wakaaje ndani yetu? “Kuomba bila kukoma,” kwa sababu Bwana kamwe hakomi kukupenda, kamwe hakomi kukubariki, wala kamwe hakomi kukuhesabu kuwa mtoto wake.
“Kuomba bila kukoma,” kwa maana wahitaji baraka juu ya kazi yote unayoifanya. Je, ni kazi ya kawaida? “Bwana asipoijenga nyumba, waijengao wafanya kazi bure.” Je, ni biashara? Ni bure kuamka mapema na kukesha, na kula chakula cha taabu, kwa maana pasipo Mungu huwezi kufanikiwa. Umefundishwa kusema, “Utupe leo riziki yetu ya kila siku,”—ni maombi yaliyovuviwa kwa ajili ya mambo ya kidunia. Ee, takasa mambo yako ya kidunia kwa maombi. Na, kama umejishughulisha katika utumishi wa Mungu, kuna kazi gani ambayo ndani yake waweza kutumaini mafanikio pasipo baraka yake? Kufundisha vijana, kuhubiri injili, kugawa vijitabu, kuwafundisha wasiojua, je, hayo yote hayahitaji baraka yake? Ni nini hayo kama fadhili hiyo ikinyimwa? Kwa hiyo, omba, maadamu unafanya kazi.
Wewe u daima katika hatari ya kushawishiwa; hakuna nafasi maishani ambayo ndani yake usiweze kushambuliwa na adui. “Kuomba bila kukoma,” kwa hiyo. Mtu aendaye katika njia yenye giza ambako ajua kwamba kuna adui, kama ni lazima awe peke yake naye ana upanga pamoja naye, huuchukua ukiwa umefutwa alani mkononi mwake, ili kuwajulisha wanyang'anyi kwamba yu tayari kwao. Vivyo hivyo, Mkristo, omba bila kukoma; chukua upanga wako mkononi mwako, tikisa silaha ile yenye nguvu ya maombi-yote ambayo Bunyan anaisema. Kamwe usiuweke alani; utakata hata deraya za chuma. Huna haja ya kumwogopa adui yeyote kama waweza tu kuomba. Kama unavyoshawishiwa bila kukoma, ndivyo omba bila kukoma.
Wahitaji kuomba daima, kwa maana daima wahitaji kitu fulani. Katika hali yoyote huwezi kuwa tajiri kiasi cha kutohitaji kitu kutoka kwa Mungu wako. Haiwezekani kwako kusema, “Ninavyo vitu vyote,” au, ikiwa waweza, unavyo katika Kristo peke yake, na kutoka kwa Kristo ni lazima uendelee kuvitafuta. Kama ulivyo daima katika uhitaji, ndivyo omba daima langoni pa rehema. Zaidi ya hayo, baraka daima zinakungoja. Malaika wako tayari na fadhili usizozijua, nawe huna budi ila kuomba nawe upate. Ee, kama ungeweza kuona kile kingeweza kupatikana kwa kuomba usingekuwa mlegevu kiasi hicho. Baraka za mbingu zisizo na thamani ambazo bado zimewekwa kando, ee, laiti ungetambua kwamba zinakungoja tu wewe uombe, usingesita kwa dakika moja. Mtu ajuaye kwamba kilimo chake ni chenye faida, na kwamba shamba lake huzaa kwa wingi, atafurahi kupanda eneo pana zaidi la ardhi mwaka mwingine; na yeye ajuaye kwamba Mungu hujibu maombi, naye yu tayari bado kuyajibu, atafumbua kinywa chake zaidi ili Mungu akijaze.
Endeleeni kuomba, ndugu zangu, kwa maana hata kama wewe mwenyewe usingehitaji maombi kuna wengine wahitajio—kuna wanaokufa, wagonjwa, maskini, wasiojua, wanaorudi nyuma, wanaokufuru, wapagani walioko nyumbani, na wapagani walioko ng'ambo. “Kuomba bila kukoma,” kwa maana adui hufanya kazi bila kukoma, na hata sasa ufalme haujaufikia Sayuni. Kamwe hutaweza kusema, “Niliacha kuomba, kwa maana sikuwa na kitu cha kuombea.” Upande huu wa mbingu shabaha za maombi ni nyingi kama nyota za angani.
Na, sasa, nilisema ningesema neno kuhusu kwa nini SISI twapaswa kuomba hususa, na hilo litafunga hubiri hili. Wapendwa marafiki, kanisa hili lapaswa kuomba bila kukoma. Katika miaka iliyopita tumekuwa mashuhuri kwa maombi. Kama kuna kanisa lililoomba wakati wowote ni kanisa hili. Ningeweza kuona makosa mengi kwa baadhi ya wanaozuia maombi, lakini hata hivyo ni lazima niseme mbele za Mungu kwamba najua na nahisi kwamba yamekuwako maombi yaliyo hai katika kanisa hili kwa miaka mingi, na kwa hiyo ndiyo maana tumepata miaka mingi ya amani na ufanisi. Hatujakosa kitu kwa sababu hatujakosa maombi. Sina shaka tungeweza kupata mengi zaidi kama tungeomba zaidi; hata hivyo maombi yamekuwa na nguvu sana hapa. Sasa, ndugu zangu, tuseme msingekuwa na mchungaji, tuseme mhubiri amekuondokeni, na kwamba kitambaa cheusi juu ya mimbari hii hakikuwa kwa ajili ya mzee wa kanisa aliyekufa bali kwa ajili ya mhubiri mwenyewe, mngeomba, sivyo? Je, hamtaniombea basi wakati ningali hai? Kama mngemwombea mwingine aje, je, hamtaniombea wakati nikiwa hapa? Natamani kuutimiza wajibu wangu mbele yenu machoni pa Mungu kwa bidii yote, lakini siwezi bila maombi yenu; na kama nikiwa nimekuondokeni, mngepaza kuugua kwingi, nanyi mngeomba kwa maombi mpate mrithi, niombeeni wakati ningali pamoja nanyi. Wapendwa, mmemwombea mchungaji kwa bidii sana alipokuwa mgonjwa, maombi yenu yamekuwa faraja yake na uponyaji wake; je, hamtamwombea sasa akiwa anaweza kuhubiri injili, ili afya yake itakaswe kwa utumishi wa Mungu, na huduma ya kweli iwe na nguvu katika kuvuta nafsi? Nawaomba jambo hili, nadhani ningeweza kulidai kwenu. Nawasihi kweli, ndugu zangu, tuombeeni.
Tuseme tena, ndugu wapendwa, kusingekuwa na waongofu katikati yetu, je, hamngeomba? Na kwa kuwa kuna waongofu wengi sana, je, hiyo iwe sababu ya kuacha? Je, tutamwabudu Mungu kidogo zaidi kwa sababu anatupa zaidi? Badala ya maombi mamoja ambayo yangepanda kama kusingekuwa na waongofu, yapaswa kuwako kumi sasa kwa kuwa anaendelea kutenda wokovu katikati yetu.
Tuseme tungekuwa tumegawanyika, na tukawa na migawanyiko mingi, na wivu, na magombano, je, walio waaminifu wasingeomba kwa uchungu wa roho? Je, hamtaomba kwa kuwa hakuna migawanyiko, na kuna upendo mwingi wa Kikristo? Hakika, nasema tena, hamtamtendea Mungu vibaya zaidi kwa sababu anawatendea vyema zaidi. Hilo lingekuwa upumbavu kweli kweli.
Tuseme tungekuwa tumezungukwa leo na majeshi ya watesi, na kwamba uzushi kila mahali ungeingia katikati yetu na kutudhuru, je, hamngeomba, ninyi mpendao Bwana? Na sasa kwa kuwa twaishi katika siku za amani, na uzushi, ingawa unazunguka-zunguka, umezuiwa nje ya zizi letu, je, hamtafanya ushirika na Bwana zaidi sana? Nitasema kwa mara ya tatu, je, tutaomba kidogo zaidi kwa sababu Mungu anatupa zaidi? Ee la, bali kadiri alivyo mwema kwetu ndivyo zaidi na tumsujudie na kulitukuza jina lake.
Sasa hivi twahitaji kuomba, kwa maana wengine wanapoa, na kugeukia dhambi zao za zamani. Twahitaji kuomba, kwa maana tunafanya mengi kwa ajili ya Kristo. Kila wakala uko katika kazi kamili. Twataka baraka kuu juu ya jitihada kuu. Tumepata matokeo kutoka kwa maombi ambayo yangeweza kumfanya mtu masikio yake yaziize ambaye angesikia habari zake kwa mara ya kwanza: historia yetu kama kanisa haijakuwa ya pili hata kwa historia ya kitume yenyewe: tumeuona mkono wa Mungu ukifunuliwa machoni pa watu wote, na hata miisho ya dunia ushuhuda wa mimbari hii umeenea, na maelfu wamempata Mwokozi—yote katika kujibu maombi mengi. Basi omba, bila kukoma. Ee kanisa lililo katika Tabenakulo, shika sana ulicho nacho, mtu asiitwae taji yako. Ee, endelea kuwa kanisa liombalo ili sisi kwa pamoja; tutakaposimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, mchungaji na watu, tusishtakiwe kuwa hatuombi, wala kuwa walegevu katika kazi ya Bwana. Natumaini kwa bidii yote haya yataielekeza siku ya kesho ya maombi kuwa ya bidii na ya nguvu zaidi; lakini zaidi bado naomba kwamba nyakati zote sisi sote tuwe wenye moto, wa mara kwa mara, wa papo hapo, na wa kudumu katika maombi; tukiomba katika Roho Mtakatifu, kwa jina la Yesu.
SEHEMU YA MAANDIKO ILIYOSOMWA KABLA YA HUBIRI—1 Wathesalonike 4:13-18 na 5.