Sura 7 · dakika 29 za kusoma
Kusali katika Roho Mtakatifu
“Mkisali katika Roho Mtakatifu.” Yuda 1:20.
MANENO haya yamo katika fungu ambamo Mtume anaonyesha tofauti iliyopo kati ya wasiomcha Mungu na wamchao. Wasiomcha Mungu wanadhihaki, wakinena maneno makuu ya majivuno na kuandama tamaa zao mbaya, hali wenye haki wanajijenga katika imani yao iliyo takatifu kabisa, na kujilinda katika upendo wa Mungu. Wasiomcha Mungu wanaonyesha sumu ya mioyo yao kwa kuomboleza na kunung'unika, hali wenye haki wanadhihirisha kanuni mpya iliyomo ndani yao kwa “kusali katika Roho Mtakatifu.” Mtu asiyemcha Mungu huchukua uchungu kinywani mwake, hali midomo ya Mkristo hudondoza asali safi ya ibada. Kama vile buibui inavyosemekana kupata sumu katika maua yale yale ambayo nyuki hufyonza asali, ndivyo waovu wanavyoyatumia vibaya kwa dhambi rehema zile zile ambazo wamchao Mungu huzitumia kwa utukufu wa Mungu.
Kama vile nuru ilivyo mbali na giza, na uzima na mauti, ndivyo Mwaminio anavyotofautiana na asiyemcha Mungu. Na tuitunze tofauti hii ikiwa hai machoni petu. Wakati waovu wanavyozidi kuwa waovu, na tuzidi kuwa watakatifu, wenye kusali zaidi, na wacha Mungu zaidi, tukisema pamoja na Yoshua mzee mwema, “Wengine na wafanye watakavyo, lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Bwana.” Angalia ya kwamba andiko hili linakuja katika utaratibu fulani ndani ya muktadha wake. Wenye haki wanaelezwa, kwanza kabisa, kuwa wanajijenga katika imani yao iliyo takatifu kabisa. Imani ndiyo Neema ya kwanza ya Mungu, shina la utauwa, msingi wa utakatifu, mapambazuko ya kumcha Mungu—kwa hili ndipo uangalifu wa kwanza upasa kutolewa.
Lakini hatuna budi tusikawie katika kanuni za kwanza. Mbele ndiko safari yetu! Basi, ni nini kifuatacho nyuma ya imani? Ni yupi mzaliwa wa kwanza wa imani? Mzabibu wa imani unapokuwa na nguvu na kuzaa matunda ya utakatifu, ni kipi kishada cha kwanza kilichoiva? Je, si maombi—“kusali katika Roho Mtakatifu”? Mtu asiye na maombi hana imani, naye mtu aliye na imani tele karibuni atakuwa na dua tele. Imani mama, na maombi mtoto, mara chache hutengana. Imani huyachukua Maombi mikononi mwake, na Maombi huyavuta uhai kifuani mwa Imani. Kujengwa katika imani huleta bidii katika dua. Eliya kwanza aonyesha imani yake mbele ya makuhani wa Baali, kisha astaafu kushindana na Mungu juu ya Karmeli.
Litafiti andiko letu kwa makini na uone ni nini kifuatacho baada ya “kusali katika Roho Mtakatifu.” “Jilindeni katika upendo wa Mungu.” Baada ya maombi hufuata hisia ya kudumu ya upendo wa Mungu kwetu na kufurika kwa upendo wetu kumwelekea Mungu. Maombi hujenga madhabahu na kupanga dhabihu na kuni kwa utaratibu, kisha Upendo, kama kuhani, huleta moto mtakatifu kutoka Mbinguni na kuiwasha sadaka! Imani, kama tulivyosema, ndiyo shina la Neema. Maombi ni bua la yungiyungi, na upendo ni ua lisilo na doa. Imani humwona Mwokozi, maombi humfuata nyumbani, bali upendo huvunja kibweta cha marhamu ya thamani na kuimimina kichwani pake.
Lakini kuna hatua nyingine ipitayo hata furaha takatifu za upendo! Yasalia jiwe la juu kabisa la kuikamilisha jengo—nalo ni kuamini kwa kutazamia—“mkitazamia rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo hata uzima wa milele.” Tumaini lenye kuona mbali hupanda ngazi ambayo Imani imeijenga, na kupiga magoti ya Maombi hutazama kupitia dirisha ambalo Upendo amelifungua, na kumwona Bwana Yesu Kristo akija katika utukufu wake na kuwapa watu wake wote uzima wa milele utakaokuwa fungu lao. Basi, ona thamani ya maombi kama ishara ya kuwa na imani, na kama kivuli kitangulizacho na kutegemeza nguvu na kukua kwa upendo.
Tukija moja kwa moja kwenye andiko, twaona ya kuwa Mtume anena juu ya maombi, lakini anataja aina moja tu ya kusali. Yakitazamwa kwa jicho fulani, maombi ni ya namna nyingi. Nadhani hakuna maombi mawili ya kweli kutoka kwa watu wawili mbalimbali yawezayo kufanana kabisa. Mafundi wa sanaa hawapendi kuzidisha mchoro uleule—wapendelea kutoa mawazo mapya kila mara washikapo kalamu. Na hivyo ndivyo Fundi Mkuu wa sanaa, Roho Mtakatifu, aliye Mtungaji wa maombi, hazoei kutoa maombi mawili yatakayofanana kabisa juu ya vibao vya mioyo ya watu wake.
Maombi yaweza kugawanywa katika tabaka mbalimbali. Kuna maombi ya kuepusha ambayo kwayo twaomba ghadhabu ya Mungu iondoke, na kumsihi ageuze hasira yake kali, aondoe fimbo yake, na kuutia upanga wake alani. Maombi ya kuepusha yapasa kutolewa nyakati zote wakati msiba unapohofiwa, na dhambi ilipomtia Bwana wivu. Kisha kuna maombi ya kusihi ambayo kwayo twasihi baraka na kuomba rehema kutoka mkono wa ukarimu wa Mungu, na kumsihi Baba yetu wa mbinguni atupatie mahitaji yetu kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu ndani ya Kristo Yesu. Kuna maombi yaliyo ya nafsi ambayo mwombaji husihi hasa kwa ajili yake mwenyewe. Na kuna dua zilizo za maombezi, ambazo, kama Ibrahimu, mwombaji huombea Sodoma, au husihi kwamba Ishmaeli aishi mbele za Mungu.
Maombi haya kwa ajili ya wengine yapasa kuongezwa kadiri ile ile ya maombi kwa ajili yetu wenyewe, tusije tukakifanya Kiti cha Rehema kuwa mahali pa kuonyesha ubinafsi wa kiroho. Maombi yaweza kuwa ya hadhara au ya faragha, ya kunena au ya moyoni, marefu au ya haraka. Maombi yaweza kukolezwa kwa kuungama, au kutiwa manukato kwa shukrani. Yaweza kuimbwa kwa muziki, au kuliliwa kwa kuugua. Kadiri yalivyo maua ya kiangazi, ndivyo zilivyo aina za maombi! Lakini ingawa maombi ni ya tabaka hizi mbalimbali, kuna jambo moja ambalo kwalo yote ni kitu kimoja kama yanakubalika kwa Mungu—lazima yawe, kila moja lao, “katika Roho Mtakatifu.”
Maombi yale yasiyo katika Roho Mtakatifu yamo katika mwili. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili, nasi twaambiwa ya kwamba walio katika mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Yote yatokayo katika asili yetu iliyoharibika yamechafuliwa na kuharibiwa, wala hayawezi kukubalika kwa Mungu aliye mtakatifu kabisa. Kama mbingu hazikuwa safi machoni pake, yatakubalikaje kwake maombi yale yaliyozaliwa na nchi? Mbegu ya ibada yenye kukubalika lazima itoke katika ghala la Mbinguni. Ni maombi yale tu yatokayo kwa Mungu yawezayo kwenda kwa Mungu! Njiwa atapeleka barua tu kwenye kitundu alikotoka, na vivyo hivyo maombi yatarudi Mbinguni kama yalitoka Mbinguni. Ni lazima tuzirudishe mishale ya Bwana kwake.
Shauku ile aiandikayo juu ya moyo wetu itausukuma moyo wake na kuteremsha baraka, lakini tamaa za mwili hazina nguvu kwake. Nikiwa na shauku ya kuisisitiza Kweli hii kuu ya Mungu katika nia za Ndugu zangu wa kiume na wa kike asubuhi hii, nitayatumia maneno machache ya andiko hili kwa njia tano.
I. Kwanza tutalitumia andiko kama TANURU la kuyapima maombi yetu. Nawasihi, jichunguzeni kwa uangalifu mkali! Litumieni andiko kama chombo cha kusafishia, tanuru, jiwe la kupimia au kalibu ya kutambulia kama maombi yenu yamekuwa ya kweli au sivyo! Huu ndio mtihani—je, kweli kweli yamekuwa—“kusali katika Roho Mtakatifu”? Ndugu zangu, hatuna haja ya kuwahukumu wale wasalio maombi yasiyoeleweka, maombi kwa lugha ya kigeni, maombi wasiyoyafahamu. Twajua bila mjadala wa dakika moja juu ya swali hili ya kuwa maombi yasiyoeleweka hayawezi kuwa maombi katika Roho, kwa maana hata roho ya mtu mwenyewe haiingii ndani yake—basi Roho wa Mungu awezaje kuwamo?
Maneno ya fumbo au maneno ya Kilatini ya makuhani hayawezi kupanda mbele za Mungu na kukubalika! Basi, na tuweke hukumu yetu kwa ajili yetu wenyewe. Huenda wapo waliohudhuria ambao tangu utoto wao wamezoea kutumia sala ya kukariri. Labda usingethubutu kutoka kwenda kazini kwako mchana bila kuwa umeikariri sala hiyo kando ya kitanda. Ungeogopa kulala usiku bila kuyapitia maneno uliyojiwekea kuyakariri. Rafiki zangu wapendwa, je, naweza kuwaulizeni swali—mtajaribu kulijibu kwa unyofu? Je, mmesali katika Roho Mtakatifu? Je, Roho Mtakatifu amekuwa na sehemu yoyote katika sala hiyo? Je, kweli amewafanya kuihisi mioyoni mwenu? Je, si yamkini ya kuwa mmemdhihaki Mungu kwa sauti ya heshima juu ya ulimi usio na fikira? Je, si yamkini ya kuwa kutokana na namna ya ovyo ambavyo mtu huja kukariri sala ijulikanayo huenda hapana moyo wowote ndani yake—wala chembe ya unyofu?
Je, Mungu hachukii dhabihu pale moyo usipopatikana? Lingekuwa jambo la huzuni kama tungekuwa tumeziongeza dhambi zetu kwa maombi yetu! Lingekuwa jambo la masikitiko makubwa kama ingedhihirika ya kwamba tulipopiga magoti katika kile tulichodhania kuwa ni ibada ya Mungu, kumbe tulikuwa tukimtukana Mungu wa Mbinguni kwa kunena maneno yasiyoweza ila kuwa chukizo kwake kwa sababu mioyo yetu haikwenda pamoja na midomo yetu! Na tuwe na hakika ya kuwa kama kwa miaka sabini tumefanya ibada zetu kwa ukamilifu kwa kutumia kitabu, au sala ile tuliyoijifunza, huenda, miaka hiyo sabini yote, hatukusali hata mara moja! Na muda huo wote huenda tulikuwa tukiishi mbele za Mungu maisha ya kutokumcha, yasiyo na maombi, kwa sababu hatukumwabudu Mungu, aliye Roho, katika roho na kweli, wala hatukusali kamwe katika Roho Mtakatifu! Jihukumuni wenyewe, Ndugu zangu, msije mkahukumiwa!
Lakini je, hawapo wengine miongoni mwetu ambao hawakupata kutumia sala iliyoandikwa? Ambao tangu utoto wetu wa mwanzo tumeziepuka na hata kuzichukia sala za kukariri, lakini hata hivyo tuna sababu njema ya kuyapima maombi yetu kama walivyo wengine? Tumetamka maneno ya papo kwa papo, na matamko hayo ya papo kwa papo yalihitaji mazoezi kidogo ya akili, uangalifu kidogo—lakini bado huenda tulikuwa bila moyo ndani yake. Nadhani twajua vyema ya kuwa twaweza kuingia katika mazoea kama hayo ya maombi ya papo kwa papo hata yasiwe na tofauti kubwa, au hata kidogo, na kama tungekariri kile tulichojifunza. Yaweza kupatikana ufasaha kama huo kwa mazoezi hata usemi wa mtu ukatiririka kwa dakika tano au kumi, au robo saa, na hali moyo waweza kuwa unatangatanga katika ubatili au umetuama katika kutojali! Mwili waweza kuwa magotini, bali roho ikiwa juu ya mabawa yake mbali na Kiti cha Rehema.
Na tuchunguze ni kwa kadiri gani maombi yetu ya hadhara yamekuwa katika Roho Mtakatifu. Mhubiri asimamaye hapa amwomba Mungu amchunguze katika jambo hilo. Kama ametimiza kazi ya maombi ya hadhara kwa sababu tu ni wajibu wake rasmi kuongoza ibada za kusanyiko, ana mengi ya kutolea hesabu mbele za Mungu—kuongoza ibada za umati huu mkubwa bila kuutafuta msaada wa Roho Mtakatifu si dhambi ndogo! Na yatasemwaje juu ya maombi kwenye Mikutano ya Maombi? Je, mengi yao si maneno matupu? Ingekuwa afadhali kama rafiki zetu wasingesema kabisa kuliko kusema katika mwili!
Nina hakika ya kuwa maombi pekee ambayo msikiaji mcha Mungu aweza kuungana nayo, na yanayokubalika kwa Mungu, ni yale yaliyo kweli maombi ya moyoni—maombi ya nafsi, kwa hakika—maombi ambayo Roho Mtakatifu hutusukuma kuyasali. Mengine yote ni kuupiga upepo na kupoteza wakati bure. Ndugu zangu, namshukuru Mungu kwa kuwa wapo wengi wenu katika ushirika na Kanisa hili mliojaliwa kipawa cha maombi, nami natamani kila mshiriki wa kila Kanisa la Kikristo angeweza kusali hadharani. Yawapasa nyote kujaribu kufanya hivyo, wala asiache mtu yeyote wenu ila iwapo yamekuwa jambo lisilowezekana kabisa. Lakini ee, Ndugu zangu msalio hadharani, je, isiwe wakati mwingine kwenu kama ilivyo kwa wengine wetu—kutumia kipawa na si kufurika kwa Neema ya Mungu? Na kama ni hivyo, mwombeni Bwana awasamehe maombi kama hayo na kuwawezesha kumngojea katika nguvu za Roho Mtakatifu.
Tusisahau kuyachunguza maombi yetu yaliyo ya faragha zaidi, dua zetu kwenye madhabahu ya jamaa, na zaidi ya yote, maombi yetu katika kile chumba kidogo tulichokiweka wakfu kwa ushirika na Mungu. Ee Ndugu zangu, tungeweza kabisa kuyachukia maombi yetu tungaliona jinsi yalivyo duni! Zipo nyakati ambapo ni jambo tamu na lililobarikiwa kuzishika pembe za madhabahu na kuhisi ya kuwa damu inyunyizayo madhabahu imekunyunyiza wewe—ya kuwa umenena na Mungu nawe umeshinda! Ee ni jambo lililobarikiwa kumshika Malaika wa Agano, na kushindana naye hata saa baada ya saa, ukisema, “Sitakuacha uende, usiponibariki”! Lakini nachelea kuwa haya si mambo ya kudumu. Twaweza kuyasema kuwa ni ziara za malaika, chache na za mbalimbali.
Njooni, Ndugu zangu, yatieni maombi yenu katika kalibu hii ya “kusali katika Roho Mtakatifu.” Mtatia ndani madini mengi, lakini yatatoka dhahabu safi kidogo. Njooni myaweke maombi yenu juu ya sakafu hii ya kupuria, na kuyapura kwa andiko hili, “kusali katika Roho Mtakatifu.” Na ee, kutakuwako majani makavu na makapi kiasi gani, na nafaka iliyopepetwa vyema kiasi kidogo namna gani! Njooni mtazame kupitia dirisha hili mashamba ya ibada zetu, yaliyofunikwa na miiba, na michongoma, na mibaruti—jangwa la matendo ya nje tu! Na kilo kile kipande kidogo, kilichozungushiwa Neema, ambacho Mungu Roho Mtakatifu mwenyewe amekisafisha, na kukilima, na kukipanda—ambako matunda ya maombi yametolewa hata ukamilifu!
Baba yetu wa mbinguni na atufundishe kuwa wanyenyekevu mbele zake tunapotafakari jinsi ilivyo kidogo hata ya mambo yetu yaliyo mema kabisa yatakayostahimili mtihani wa macho yake yachunguzayo, na wale wetu tulio watakatifu wake na tumjie upya, na kumwomba atujaze Roho wake, na kutukubali katika Mwana wake!
II. Baadaye tutalitumia andiko kama DAWA YA KUBURUDISHA. Ni fikira ya kufurahisha sana kwa nia ya Mkristo ya kuwa Mungu huwaangalia watu wake wala haketi kama mtazamaji asiyejali migogoro na taabu zao. Kwa mfano, hutuangalia kwa makini katika maombi yetu. Ajua ya kuwa maombi, ingawa yangepasa kuwa jambo rahisi kuliko yote duniani, si hivyo. Ajua ya kuwa sisi tuliokosea hatuoni daima kuwa rahisi kumkaribia katika roho ya kweli ya dua, naye ajua hili kwa huruma ya kujishusha. Huo ni mstari wa thamani kwa mioyo ile iliyo dhaifu sana na iliyovunjika, “Yeye anaijua hali yetu; anakumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.” Na ule mwingine, “Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.”
Huzitambua dhaifu zetu na kushindwa kwetu katika kazi ya dua. Humwona mtoto wake aangukapo ajaribupo kutembea, na kuyaona machozi ambayo kwayo huililia udhaifu wake. “Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake yako wazi kusikia kilio chao.” Fikira tamu zaidi yasalia katika andiko, yaani, ya kuwa akiisha kuyafikiri makosa yetu haya, ambayo mengi yao ni ya dhambi, Bwana wetu hana hasira nasi kwa ajili yake. Na badala ya kugeuka na kuwa na ghadhabu, husukumwa kutuhurumia na kutupenda. Badala ya kusema, “Kama huwezi kusali, hutapata. Kama huna
Neema ya kutosha hata kuomba ipasavyo, nitakufungia malango ya rehema.” La, hubuni njia za kuwaleta vilema na waliofukuzwa mbele zake! Huwafundisha wajinga jinsi ya kusali na kuwatia nguvu wanyonge kwa nguvu zake mwenyewe!
Katika hili pia hufanya maajabu, kwa maana njia ambazo kwazo huusaidia udhaifu wetu zapasa kustaajabiwa mno. Msaada huo haupatikani katika kitabu wala katika kuamriwa maneno fulani mahali fulani palipowekwa wakfu, bali katika msaada wa kujishusha wa Mungu mwenyewe, kwa maana ni nani anayenenwa katika andiko ila Mungu? Roho Mtakatifu, Nafsi ya tatu ya Utatu unaostahili kuabudiwa, huusaidia udhaifu wetu, akituombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa! Ni alama ya kujishusha kwa ajabu ya kuwa Mungu si kwamba ayajibu maombi yetu tu yatolewapo, bali hutuombea maombi yetu! Ya kuwa Mfalme amwambie mwombaji, “Lete shauri lako mbele yangu nami nitakupa haja yako,” ni wema. Lakini yeye kusema, “Nitakuwa mwandishi wako. Nitakuandikia ombi lako. Nitalitia katika maneno yafaayo na kutumia vifungu vinavyofaa ili ombi lako lipangwe kwa namna ya kukubalika”—huu ni wema uliopita kiasi!
Na hivi ndivyo hasa Roho Mtakatifu anavyotutendea sisi wana wa watu maskini, wajinga, wenye kuyumbayumba, wanyonge. Nayapasa kuelewa kutokana na usemi, “kusali katika Roho Mtakatifu,” ya kuwa Roho Mtakatifu yu radhi kweli kunisaidia kusali—ya kuwa ataniambia jinsi ya kusali! Na ya kuwa nifikapo mahali ambapo nimesita nisiweze kuzieleza shauku zangu, atatokea katika shida yangu na kuniombea ndani yangu kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Yesu katika uchungu wake alitiwa nguvu na malaika—wewe utasaidiwa na Mungu mwenyewe! Haruni na Huri waliishika mikono ya Musa, bali Roho Mtakatifu mwenyewe huusaidia udhaifu wako!
Ndugu zangu wapendwa katika Kristo, wazo hili halihitaji kupambwa kwa maneno ya ufasaha! Lipokee kama kipande cha dhahabu ya Ofiri na ulithamini. Halina thamani, lililopita thamani yote. Mungu mwenyewe, Roho Mtakatifu, hujishusha kukusaidia uwapo magotini, na ijapokuwa huwezi kuunganisha maneno mawili pamoja katika usemi wa kawaida kwa watu, hata hivyo atakusaidia kunena na Mungu! Ee, na kama pale Kiti cha Rehema utashindwa maneno, hutashindwa uhalisia, kwa maana moyo wako utashinda. Mungu hahitaji maneno. Kamwe hayasomi maombi yetu kwa kadiri ya matamko ya nje, bali kwa kadiri ya kuugua kwa ndani. Huitambua shauku, kutamani, kuugua, na kulia.
Kumbuka ya kuwa upande wa nje wa maombi ni ganda tu—upande wa ndani wa maombi ndio kiini na asili yake ya kweli. Kama maombi yakipeperushwa Mbinguni katika wimbo wa umati, pamoja na mvumo wa muziki mtukufu, hayakubaliki kwa Mungu hata chembe zaidi ya yanapoliliwa kwa kilio kichungu cha uchungu kutoka roho iliyo ukiwa. Kilio hicho kilicho na mvurugano mno masikioni mwa wanadamu ni muziki masikioni mwa Mungu—
“Kwake kuna muziki katika kuugua, Na uzuri katika chozi.” Angalia jambo hili, basi, ukafarijike.
III. Andiko laweza tena kutumika kama RAMANI ya kutuongoza katika njia ya maombi. Hapa nitahitaji kunena kwa urefu zaidi. Kusali jinsi gani? Kwa kitabu? Bila kitabu? Hadharani? Faragha? Njiani? Nyumbani? Ukiwa magotini? Ukiwa umesimama? Ukiwa umeketi? Ukipiga magoti? Hakuna lililonenwa juu ya haya! Namna ya kukaa, mahali, na wakati vyote vimeachwa wazi. Hakuna kanuni ila moja—“katika Roho Mtakatifu.”
Hilo ni la lazima kabisa. Likipatikana, hakuna jambo jingine lenye maana hata chembe. Kama ni kusali katika Roho Mtakatifu, mengine yote yaweza kuwa kama utakavyo. Kusali katika Roho Mtakatifu maana yake ni nini? Neno hilo laweza kutafsiriwa, “kwa Roho Mtakatifu,” au, “kupitia Roho Mtakatifu,” sawa na, “katika Roho Mtakatifu.” Na kifungu hicho maana yake, kwanza, ni kusali katika nguvu za Roho Mtakatifu. Nia ya kimwili haijui neno lolote juu ya hili. Ingekuwa sawa nijieleze kwa Kiholanzi kama kwa Kiingereza juu ya jambo hili kwa mtu asiyezaliwa mara ya pili. Lakini watu waliozaliwa mara ya pili walio wa Roho na kuishi katika ulimwengu wa Roho wanajua mawasiliano yaliyopo kati ya roho zao na Roho Mtakatifu ambaye sasa akaaye katikati ya Kanisa la Mungu.
Twajua ya kuwa Roho wa Mungu, bila kutumia sauti, hunena mioyoni mwetu. Twajua ya kuwa bila tamko liwezalo kusikiwa na masikio aweza kuifanya nafsi yetu kujua uwepo wake na kufahamu maana yake. Hutupitisha kivuli cha kiroho cha uvutano wake juu yetu, akiipaka rangi mawazo yetu na hisia zetu kwa kadiri ya kusudi na mapenzi yake mwenyewe. Ni ukweli mkuu wa kiroho ambao Mkristo aujua kwa hakika ya kuwa Roho Mtakatifu, Roho wa Mungu, ana shughuli za mara kwa mara na nia za kiroho na huwapa nguvu zake. Roho yetu iliyozaliwa upya ina kiasi fulani cha nguvu ndani yake, lakini nguvu hizo hazidhihirishwi kamwe kikamilifu wala kuvutwa nje ila Roho wa Mungu aihuishapo roho yetu na kuisisimua ifanye kazi.
Roho yetu husali, lakini ni kwa sababu imefunikwa na kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu. Siwezi kwa sasa kujieleza, lakini nakusudia hivi, ya kuwa kama mimi, kama mtu, ningeweza kwenda kwenye Kiti cha Enzi cha Neema na kusali tu kama asili yangu ya kimwili ingesali, maombi hayo yasingekubalika. Lakini niendapo kwenye Kiti cha Rehema na asili yangu mpya isalipo kama Roho Mtakatifu anavyoniwezesha kusali, ndipo maombi yangu yatafanikiwa kwa Mungu. Kama nikitenda mbele za Mungu pale kiti cha enzi kile ambacho mwili na damu vyaweza kutenda wala si zaidi, sikutenda neno—kwa maana kile kilicho cha mwili bado hakipandi juu kupita mwili.
Lakini kama, katika kuja mbele ya Kiti cha Enzi cha Neema ya mbinguni, Roho wa milele wa Mungu akinena na nafsi yangu na kuiinua kutoka usawa uliokufa wa ubinadamu ulioanguka. Na kama akiiinua ijazwe nguvu ya Uungu—kama Roho huyo yumo ndani yangu kama chemchemi ya maji yabubujikayo hata uzima wa milele, kama nikiipokea nuru na nguvu ile ya Uungu ya Roho Mtakatifu—na kama katika nguvu zake nikimkaribia Mungu kwa bidii, maombi yangu lazima yatashinda kwa Mungu! Nguvu hizi zaweza kumilikiwa na kila Mkristo. Mungu na azijalie kwa watu wake wote sasa, wapate kusali wote katika Roho!
Hiyo, nadhani, ni maana moja ya andiko—kusali katika nguvu za Roho. Bila shaka maana kuu ya andiko ni kusali katika Roho kuhusu jambo la kuomba. Hatujui daima tuombee nini, na, Ndugu zangu, kama tungejizuia kusali kwa dakika chache hata tulipojua, ingekuwa kanuni njema na yenye hekima. Zoea tulilotumbukia, katika kusali kwa papo kwa papo, la kusali sikuzote moja kwa moja kile tunachokiomba—bila kusita hata dakika moja tuwaze kile tutakachoomba—ni jambo lenye kudhuru sana roho ya maombi. Ningependa, niwapo peke yangu, kuchukua dakika chache kufikiri kile nitakachomwomba Mungu, maana la sivyo yaonekana kwangu kama kutafuta mahojiano na mmojawapo wa maafisa wa Serikali ili kuomba jambo ambalo huenda likatujia wakati ule ule.
Ungependaje kupata mahojiano na Bwana Derby, kisha ghafula uwaze ni jambo gani ulilokuja kwa ajili yake? Hakika akili ya kawaida ingesema, Ngoja kwanza hata uwe umelipanga shauri lako akilini mwako, na ndipo utakapojua wewe mwenyewe waziwazi ni kitu gani unachokitaka, utaweza kuomba kile unachohitaji. Je, hatupasi kumngojea Mungu katika maombi, tukimwomba atufunulie ni mambo gani yale ambayo kwayo twapasa kumsihi? Jihadhari na maombi ya kubahatisha! Kamwe usifanye dua kwa ovyo. Njoo kwenye Kiti cha Enzi cha Neema ukifahamu kwa akili ni kitu gani unachohitaji.
Ni vyema kwetu katika maombi Roho Mtakatifu aiongozapo nia. Je, watu wote wa kiroho hawajui hili, ya kuwa wajihisi wamefungwa kuhusu mambo fulani, na huru upande mwingine tu? Basi na wamtii Roho Mtakatifu na kusali kama aelekezavyo, kwa maana ajua ombi letu lipasavyo kuwa. Naam, ni nini basi? Ndugu zangu wapendwa, ombeni kile ambacho Mungu Roho awasukumapo kukiombea, nanyi iweni wepesi sana kuhisi uvutano wa Roho Mtakatifu. Napenda tashbihi aliyoitumia Thomas Shillitoe katika Maisha yake, aliposema ya kuwa alitamani nia yake mwenyewe iwe kama chelezo juu ya maji, ikitambua kila mwendo wa Roho wa Mungu. Ingekuwa vyema kuwa mwepesi hivyo kuhisi Roho wa Mungu hata pumzi yake iliyo hafifu kabisa iwe na uwezo wa kusababisha mtetemeko juu ya bahari ya nafsi yetu na kuifanya iende kama Roho apendavyo.
Tumefika hali ya juu ya utakaso Mungu Roho na roho yetu ya ndani vinapopatana kwa ukamilifu. Na tuongozwe kuingia hali hiyo iliyobarikiwa isiyoelezeka! Hatusali vema tukiwaza ni kitu gani tunachokitaka na tunachokitamani, kisha tukakiomba kwa ukaidi wa ubinafsi. Twasali vema tunapokubaliana na kile kilicho nia ya Roho, na kunena kama atusukumavyo kunena. Hakika tutatajirishwa kwa mema tunapongojea jambo lenyewe la dua zetu tulipokee lote kwake. Bwana, utufundishe kusali! Tia mawazo katika nia zetu, shauku ndani ya mioyo yetu, na maneno yenyewe midomoni mwetu, kama ni mapenzi yako, ili maombi yetu yote yawe kusali katika Roho wala si katika mwili.
Sehemu kuu ya kusali katika Roho lazima isiwe katika nguvu za Roho tu, au katika Roho kutufundisha jambo la kuomba, bali katika Roho kutusaidia katika namna. Angalieni, Ndugu zangu, njia nyingi zilizopo za kusali ambazo ni chukizo kwa Mungu—ziangalieni na kuziepuka! Kuna namna moja tu ya kusali ambayo Bwana huikubali. Mnajua ni ipi. Nitazieleza kwa ufupi sifa zake. Yeye ajaye kwa Mungu lazima akumbuke ya kuwa “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli, kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.” Jambo la kwanza kabisa la lazima katika maombi ni kusali katika kweli, wala hatusali katika kweli ila Roho wa Mungu aiongozapo nia zetu za ubatili kuingia katika unyofu na uhalisia wa ibada.
Kusali katika kweli ndio huku—si kutumia usemi mtupu wa maombi, bali kukusudia tunavyosema. Ni moyo kufanya juhudi na Mungu na kujaa shauku kali. Nawe utapata wapi namna hiyo ya maombi ila katika mtu wa kiroho, asukumwapo na Roho Mtakatifu? Mtu wa kimwili, kama ni mpumbavu vya kutosha, aweza kuimba sala. Mtu wa kimwili aweza “kusoma ibada,” na “kutimiza wajibu” sawa na mtu mwingine yeyote awezaye kusoma kitabu, lakini yeye hasali! Hakuna ombi liwezalo kutoka kwake. Ni mtu wa kiroho peke yake awezaye kuugua na kutamani, na kulia katika moyo wake wa ndani kabisa, na katika chumba cha nafsi yake mbele za Mungu—lakini hatafanya hivyo ila Roho wa Kweli amwongozapo kwa unyofu kuingia katika siri ya maombi ya moyoni.
Kusali katika Roho Mtakatifu ni kusali kwa bidii. Maombi ya baridi, Ndugu zangu, humwomba Bwana asiyasikie! Wale wasiosihi kwa bidii, hawasihi kabisa. Ni sawa kunena juu ya moto usiovuguvugu kama kunena juu ya maombi yasiyovuguvugu! Ni lazima yawe ya moto mkali. Maombi ya kweli huchomwa kama kwa chuma cha moto ndani ya nafsi ya mtu, kisha hutoka katika nafsi ya mtu kama makaa ya mrentendele yenye joto kali mno. Maombi kama hayo hakuna awezaye kuyatoa ila Roho Mtakatifu. Nimesikia toka mahali hapa maombi ambayo kamwe siwezi kuyasahau, wala nyie hamtayasahau kamwe.
Mwezi wa Januari na Februari uliopita zilikuwako nyakati ambapo baadhi ya Ndugu zetu walisaidiwa kusali kwa nguvu kubwa hata tukainamishwa katika unyenyekevu, na baadaye tukainuliwa juu kama juu ya mabawa ya tai katika nguvu za dua! Kuna namna ya kusali kwa nguvu ambapo mtu aonekana kuzishika nguzo za lango la Mbinguni, kama Samsoni alivyozishika nguzo za hekalu, na aonekana kana kwamba angevuta yote yamwangukie yeye mwenyewe kuliko kuikosa baraka. Ni jambo la ushujaa kwa moyo kuweka nadhiri, “Sitakuacha uende, usiponibariki.” Hiyo ndiyo kusali katika Roho Mtakatifu. Na tufundishwe ustadi wa kutoa maombi ya bidii yenye matokeo!
Baada ya hilo, ni lazima katika maombi tusali kwa kudumu. Kila mtu aweza kupiga mbio kwa kasi kwa muda mfupi, lakini kudumu hivyo maili baada ya maili—hapo ndipo penye vita! Na hivyo, roho fulani zenye moto zaweza kusali kwa bidii kubwa mara kwa mara, lakini kudumu katika maombi—ni nani atakayefanya hili ila Roho wa Mungu amtegemezapo? Roho za wanadamu hulegea na kuchoka. Mwendo wa ibada ya kimwili tu ni kama mwendo wa konokono ayeyukaye atambaapo. Nia za kimwili huendelea mbele na ibada yao hupungua kidogo kidogo na kupungua kwa masikitiko, wakilia, “Ni uchovu ulioje!” Lakini Roho Mtakatifu amjazapo mtu na kumwongoza aingie katika maombi, hukusanya nguvu aendeleapo—na huongezeka bidii hata Mungu akawiapo kujibu! Kadiri lango linavyoendelea kufungwa ndivyo azidivyo kuupiga mlango kwa nguvu hata avume katika maombi yake! Na kadiri Malaika anavyokawia, ndivyo azidivyo kuamua ya kuwa akimshika kwa mshiko wa kufa hatamwacha kamwe aende bila baraka.
Kuzuri machoni pa Mungu ni kudumu kwenye machozi lakini kusikoshindwa. Yesu hufurahi kushikwa na yule asemaye, “Siwezi kupokea Hapana kuwa jibu, baraka hii sharti niipate, kwa maana umeiahidi nawe umenifundisha kuiomba, wala sitasadiki ya kuwa waweza kujikana mwenyewe.” Hakika ni lazima tuwe na Roho Mtakatifu atusaidie kusali hivi. Tukisali katika Roho tutakuwa na hakika ya kusali katika hali takatifu ya nia. Ndugu zangu, je, huwahi kuvurugwa akilini mwenu? “Ee,” wasema, “najiuliza ni lini ambapo sivurugwi.” Nathubutu kusema ya kuwa mmeingia nyumbani humu mkiwa na mizigo, na hali njiani mlikuwa mkisema, “Hii ni Jumapili iliyobarikiwa, nahisi nina uwepo wa Mungu.”
Kisha mchambaji fulani mjinga akakutana nawe kwenye ngazi na kukueleza hadithi ya bure iliyokuvuruga. Waweza hata kuketi hapa kimya, kisha kumbukumbu la mtoto aliyeko nyumbani, au kumbukumbu la kile alichosema mtu fulani majuma sita yaliyopita likaitatiza nia yako hata usiweze kusali. Lakini Roho Mtakatifu ajapo, huchukua mjeledi wa kamba ndogo na kuwafukuza wanunuzi na wachuuzi hawa nje ya hekalu na kuliacha wazi kwa ajili ya Mungu. Na ndipo waweza kuja na nia takatifu, ya ibada, iliyokazwa na kutulizwa katika lengo lako kuu la kumkaribia Mungu. Huku ndiko kumkaribia katika Roho. Ee laiti tungekuwa na zaidi ya ibada hii iliyobarikiwa, isiyosumbuliwa!
Lakini nisingeweza kumaliza maelezo ya kusali katika Roho kama nisingesema ya kuwa maana yake ni kusali kwa unyenyekevu, kwa maana Roho Mtakatifu hatuvimbishi kamwe kwa kiburi. Yeye ndiye Roho ainayeihakikisha dhambi na hivyo hutuinamisha katika toba na moyo uliovunjika. Ni lazima tusali mbele za Mungu kama yule mtoza ushuru mnyenyekevu, ama sivyo hatutatoka kamwe tumehesabiwa haki kama alivyotoka yeye. Hatutaimba kamwe Gloria in Excelsis ila tumsalipo Mungu De Profundis—toka vilindini ni lazima tulie, ama sivyo hatutauona kamwe utukufu ulio juu! Maombi ya kweli lazima yawe maombi ya upendo kama ni kusali katika Roho Mtakatifu. Maombi yapaswa kutiwa manukato ya upendo, kulowekwa katika upendo—upendo kwa watakatifu wenzetu, na upendo kwa Kristo. Zaidi ya hayo, lazima yawe maombi yaliyojaa imani. Maombi ya bidii yenye matokeo ya mtu hushinda tu kadiri amwaminivyo Mungu, naye Roho Mtakatifu ndiye Mtungaji wa imani ndani yetu, naye huilea na kuitia nguvu ili tusali tukiziamini ahadi za Mungu.
Ee laiti mchanganyiko huu uliobarikiwa wa Neema bora, zisizo na thamani na tamu kama vikolezo vya mfanyabiashara, ungekuwa wenye harufu nzuri ndani yetu kwa sababu nguvu za Roho Mtakatifu zimemwagwa mioyoni mwetu! Wakati wanishinda, kwa hiyo sina budi niache maelezo kamili ya kusali katika Roho Mtakatifu ni nini, lakini nataraji mtakuwa nayo na hivyo kuyaelewa.
IV. Nne, nitalitumia andiko kama KERUBI kutangaza kufanikiwa kwetu katika maombi. Kusali katika Roho—maneno yaliyobarikiwa! Basi kwa maombi kama hayo ni hakika kabisa ya kuwa lazima nitafanikiwa na Mungu katika maombi. Kama maombi yangu yangekuwa maombi yangu mwenyewe, huenda nisingekuwa na hakika hivyo. Lakini kama maombi niyanenayo ni maombi ya Mungu mwenyewe yaliyoandikwa juu ya nafsi yangu, Mungu daima yu Mmoja pamoja na nafsi yake—na kile aandikacho juu ya moyo kimeandikwa hapo tu kwa sababu kimeandikwa katika makusudi yake.
Yasemwa na mwanateolojia mmoja wa zamani ya kuwa maombi ni kivuli cha Uweza wa yote. Mapenzi yetu, Mungu Roho Mtakatifu ayavutapo, ni kiashiria cha mapenzi ya Mungu. Watu wa Mungu wasalipo, ni kwa sababu baraka inakuja na maombi yao ni kivuli cha baraka ijayo! Iweni na hakika ya hili, Ndugu zangu, Mungu kamwe hakujikana mwenyewe! Kamwe hakupingana mahali pamoja na kile alichosema mahali pengine. Wewe nami twaweza kujipinga wenyewe, si kwa uwongo tu, bali hata kwa udhaifu.
Huenda tusiweze kulisimamia neno letu, na twaweza kusahau tuliyosema—na hivyo mahali pengine twaweza kusema jambo linalolipinga—lakini Mungu si dhaifu kwa kumbukumbu, wala si mwenye kubadilika kwa mapenzi. Alichoahidi jana hukitimiza leo. Alichosema mahali pamoja, hulitangaza mahali pengine. Basi kama Mungu akisema moyoni mwangu, “Mwombee fulani,” ni kwa sababu amelisema katika kitabu cha maagizo yake. Kule kuandika kwa Roho wa Mungu moyoni sikuzote hupatana na kule kuandikwa kwa majaliwa katika kitabu cha kusudi la Mungu la milele. Iweni na hakika ya kuwa hamwezi ila kufanikiwa mtakapokuwa mmeiweka nafsi yenu kama karatasi mbele za Bwana na kumwomba aandike juu yake! Ndipo si tena maombi yenu wenyewe, tu, bali ni Roho anayewaombea ndani yenu kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu.
Wakati kama huo huna haja ya kusema, “Nataraji Mungu atayajibu maombi.” Atafanya hivyo—amejifunga kufanya hivyo. Ni namna ya kutokuamini kusema, “Sijui kama Bwana ni mwaminifu kwa ahadi yake au sivyo, lakini nataraji yu hivyo.” Yeye ni kweli! Mungu na awe kweli na kila mtu mwongo. Ee, kama wengi wenu mngemjaribu kama baadhi yetu tulivyolazimika kufanya, mngelazimika kuinua mikono yenu kwa mshangao, na kusema, “Kweli, lolote lisilo hakika, ni hakika ya kuwa Mungu, aketiye katika mbingu zilizo juu kabisa, huyasikiliza malalamiko ya watu wake, na kuwapa kwa kadiri ya haja ya mioyo yao.” Kama Roho akikufundisha kusali, ni hakika kama vile mara mbili mbili ni nne ya kuwa Mungu atakupa unachokitafuta.
V. Kisha nitalitumia andiko kama hitimisho kama GARI la kuzipeleka nafsi zetu wenyewe mbele katika zoezi la kupendeza la maombi. Zoezi tulilogawiwa leo na kesho ni lile la kusali katika Roho. Ndugu zangu, ni jambo la kupendeza kwa baadhi yetu kuamini ya kuwa Roho wa Mungu ndiye Mtungaji wa wimbi kuu la maombi linalovunjika sasa juu ya Makanisa tuliyo yetu. Halikuwa la kubuni au kupanga kwetu, bali lilikuwa mwendo wa Roho Mtakatifu wa Mungu juu ya Ndugu wachache waliotamani kutumia siku moja katika maombi ya dhati na kupata baraka kubwa hivyo ndani yake hata hawakuweza ila kuwaeleza wengine!
Basi, wengine wakasukumwa wenyewe, na bila neno la upinzani au tofauti ya maoni wote wakasema, “Amina. Na sisi pia tukutane pamoja kwa maombi.” Roho ya fadhili za kindugu, umoja, na upendo ilipewa kwa dhehebu letu, kisha roho ya shauku ya dhati ya kuteremsha baraka kutoka kwa Mungu. Tumejua wakati ambapo haikuwa hivyo. Tumejua wakati ambapo siku ya kufunga na kusali, kama isingedharauliwa, kwa vyovyote isingethaminiwa kama itakavyothaminiwa sasa. Tu wa moyo mmoja katika jambo hili nami najua kutokana na mawasiliano na watu wengi wa Kikristo ya kuwa watu wengi wa Mungu tayari wahisi kana kwamba wamo katika maombi kwa namna ya pekee—kana kwamba si juhudi sasa kusali, bali kana kwamba ni pumzi yao yenyewe sasa kuvuta nje shauku za kutamani uamsho wa watakatifu na kuvunwa kwa wenye dhambi.
Ndugu wa Kanisa hili, mmekuwa na uwepo wa Mungu. Kwa miaka mingi mmejaliwa wingi wa “kusali katika Roho Mtakatifu,” na kuona kwa macho yenu wenyewe mambo makuu ambayo Mungu ameyatenda kwa kuyajibu maombi. Je, mmoja wenu atarudi nyuma sasa? Je, atakuwako mtu mmoja leo au kesho ambaye hatakuwa na bidii katika maombi? Je, mtu mmoja, au hata mtoto mmoja aliye katika ushirika na Kanisa hili, atakuwa mvuguvugu katika maombi? Ningesema, Usimtende Bwana dhambi kwa kujizuia kwenda juu kwenye Kiti cha Rehema pamoja na Ndugu zako. Usimchukize Bwana hata akakunyima baraka kwa sababu unajinyima mwenyewe kuungana katika zoezi hilo.
Rafiki zangu wapendwa, ilikuwa walipokuwa wamekutana wote kwa nia moja mahali pamoja ndipo ghafula waliposikia sauti kama ya upepo wa nguvu ukivuma. Hatuwezi kuwa wote mahali pamoja, lakini, kwa vyovyote, na tuwe wote kwa nia moja. Nini? Je, wasema huna cha kuombea? Nini? Hakuna watoto wasioongoka, hakuna rafiki wasiookoka, hakuna jirani ambao bado wamo gizani? Nini? Kuishi London na usiwaombee wenye dhambi? Waishi wapi? Je, ni katika jangwa fulani kubwa, katikati ya “kivuli fulani kilichoenea bila mpaka,” ambapo tetesi za dhambi na za ujinga hazikuwahi kufika sikioni mwako? La, waishi katikati ya mamilioni ya watu wasiomcha Mungu! Mamilioni wanaomdharau Mungu aliyewaumba! Mamilioni wanaoidharau Injili ya Kristo!
Mamilioni, si maelfu! Sikia neno hilo uone kama waweza kueleza maana yake! Mamilioni wanaoishi bila Mungu na bila tumaini, na wanateremkia Jehanamu! Tuna, katika ufalme wote pia, maovu ya hatari yanayoenea. Je, yanipasa kuwakumbusha daima juu yake? Kutokuamini kukiwa kumevaa kilemba cha askofu, na Upapa ukinyakua nafasi ya Uprotestanti! Mnashambuliwa na mbwa mwitu na simba, nyoka na dubu! Kila namna ya uovu inakuja mbele kulishambulia
Kanisa. Msisali? Kama hamsali, je, niseme, Na mpate adhabu kwa uzembe wenu? La, sithubutu hata kidogo kunena kana kwamba naomba ole uwapate, lakini ole utawajia, mtegemee hilo! Kama mimi sitalisema, lakini Mungu atalisema saa hii ya sasa. “Ilaanini Merozi, asema Bwana, kwa sababu hawakuja kumsaidia Bwana, kumsaidia Bwana juu ya walio hodari.”
Hatuwaombi kutoa katika mali yenu katika jambo hili. Kama tungefanya hivyo, Bwana Yesu ana haki juu yake, nanyi mngempa kwa hiari. Wala hatuwaombi nyote leo kuhubiri. Kama tungefanya hivyo, baadhi yenu mngesamehewa kwa kukosa uwezo. Lakini twadai maombi yenu, wala hatuna budi kunyimwa! Hamwezi kusali? Basi je, hamna neema, hamna Kristo, hamna tumaini, mmepotea, nami sitawaomba kuungana nasi! Bali nawaomba kwanza mwende kwa Mungu kwa ajili yenu wenyewe. Na kama u Mkristo waweza kusali. Umaskini hakukufanyi maskini katika maombi. Kukosa elimu hakuna haja kukuzuie ukiwa magotini. Kukosa cheo na hadhi katika jamii hakutakuwa kizuizi kwako ushughulikapo na Mungu asikiaye mtu maskini aliapo na kumjibu kwa ukarimu wa Neema ya Mungu!
Ndugu zangu, kama mwampenda Kristo, kama mmewahi kuhisi upendo wake ukimwagwa moyoni mwenu. Kama mmeoshwa katika damu yake. Kama mmeokolewa na ghadhabu kwa njia yake. Kama ninyi ni viumbe vipya ndani yake. Kama mwataraji kuuona uso wake kwa kukubalika mwishoni, ningeliweza kuwawekea jambo hili kama sharti! Lakini nawasisitizia kama sihi ya kindugu—unganeni nasi katika kusali katika Roho Mtakatifu! Je, mmoja atarudi nyuma? Basi jihadhari, kama ukikataa kuungana na Ndugu zako katika maombi, usije wakati uchaguapo kulia ukajikuta umebanwa na kufungwa gerezani! Jihadhari, usije kwa kukataa kusali sasa, ambapo Roho wa Mungu amekuja, baadaye ukajihisi umenyimwa uwepo wa faraja wa Roho Mtakatifu na kuuona utamu wa ibada umeondoka kwako.
Bwana na alete baraka. Sharti aiteremshe—mioyo yetu itavunjika kama hataifanya! Twahisi ya kuwa inakuja. Tumeishika ahadi. Tumemsihi Yehova! Tumeisihi damu ya Yesu! Twaisihi sasa! Twakusudia kudumu katika kusihi huko hata baraka ije, nasi twaweza kuitumainia ya kuwa manyunyu ya mbinguni yatashuka karibuni! Hakuiambia mbegu ya Yakobo, “Nitafuteni uso wangu bure.” Ndugu zangu, iweni na matumaini, na tuungane kwa nia moja katika kusali katika Roho Mtakatifu!
Bwana na awabariki, Rafiki wapendwa, katika jambo hili kwa ajili ya Yesu.