Nguvu Kuu katika Maombi ·Omba Nawe Utapata

Sura 5 · dakika 30 za kusoma

Omba Nawe Utapata

“Mwatamani, wala hamna kitu; mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata; mwafanya vita na kupigana, lakini hamna kitu, kwa sababu hamwombi. Mwaomba wala hampati, kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” Yakobo 4:2,3.

MANENO haya yenye nguvu na yatufae kwa mafundisho ya Roho Mtakatifu. Mwanadamu ni kiumbe kilichojaa mahitaji, kisichotulia kamwe; kwa hiyo, moyo wake umejaa tamaa. Sidhani ya kwamba yupo mtu asiye na tamaa nyingi za namna moja au nyingine. Mwanadamu ni kama yule nyamachetezo wa bahari mwenye vipapatio vingi vinavyowinda chakula majini daima; au kama mimea fulani itoayo vikonyo, ikitafuta cha kujikwezea juu. Mshairi asema, “Mwanadamu hafikii kamwe, bali sikuzote hutamani kubarikiwa.” Huelekeza chombo chake kwenye bandari aidhaniyo kuwa yake, lakini, hata sasa, bado atupwatupwa juu ya mawimbi. Siku moja katika hizi atumaini kuiona furaha ya moyo wake, naye aendelea kutamani, akiwa na matumaini mengi au machache.

Jambo hili lawahusu watu walio wabaya kabisa na watu walio wema kabisa vivyo hivyo. Katika watu wabaya, tamaa hugeuka kuwa tamaa mbaya—hutamani yaliyo ya ubinafsi, ya kimwili na, kwa hiyo, maovu. Mkondo wa tamaa zao huelekea kwa nguvu upande usiofaa. Tamaa hizi mbaya, mara nyingi, huwa kali mno—humfanya mtu kuwa mtumwa wao. Hutawala akili yake; humchochea afanye jeuri—hufanya vita na kupigana—labda huua kihalisi. Machoni pa Mungu, ahesabuye hasira kuwa uuaji, mtu huyu huua mara nyingi. Nguvu za tamaa zake ni kubwa kiasi kwamba huitwa shauku kali. Na shauku hizi zikichochewa kabisa, ndipo mtu, mwenyewe, hujitahidi kwa juhudi kubwa, hata ufalme wa shetani hupatwa na jeuri, nao wenye jeuri hujitwalia kwa nguvu!

Wakati huohuo, katika watu wenye neema pia zimo tamaa. Kuwanyang'anya watakatifu tamaa zao kungewadhuru sana, kwa maana kwa hizo huinuka kutoka katika nafsi zao za chini. Tamaa za wenye neema huelekea vitu vilivyo bora—vitu safi na vya amani, vinavyostahili sifa na kuinua. Hutamani Utukufu wa Mungu, kwa hiyo, tamaa zao huchipuka kutoka nia zilizo za juu kuliko zile ziwashazo akili isiyofanywa upya. Tamaa za namna hii katika watu Wakristo mara nyingi huwa za bidii na za nguvu sana. Ndivyo zipasavyo kuwa sikuzote. Tamaa hizo zizaliwazo na Roho wa Mungu huitikisa asili iliyofanywa upya, ikiisisimua na kuichochea, na kumfanya mtu augue na kuwa katika uchungu na utungu hata aweze kupata kile ambacho Mungu amemfundisha kukitamani. Tamaa mbaya za waovu na tamaa takatifu za wenye haki zina njia zao za kutafuta kutosheka. Tamaa mbaya za waovu hujidhihirisha katika ugomvi—huua na hutamani kuwa na mapigano yake, nayo hufanya vita. Bali, kwa upande mwingine, tamaa ya wenye haki, iongozwapo vema, huishika njia iliyo kali zaidi sana ili kutimiza kusudi lake, kwa maana hujieleza katika maombi ya bidii na ya kudumu. Mtu mcha Mungu, ajaapo tamaa, huomba na kupokea mikononi mwa Mungu.

Wakati huu, kwa msaada wa Mungu, nitajaribu kudhihirisha kutokana na andiko letu, kwanza, umaskini wa kutamani—“Mwatamani, wala hamna kitu.” Pili, kwa huzuni nitaonyesha umaskini wa Wakristo wengi wanaojidai, katika mambo ya kiroho, hasa katika hali yao ya Kikanisa—nao hutamani wala hawapati. Tatu, tutanena, kwa kuhitimisha, juu ya utajiri ambao tamaa takatifu zitalipwa, tukitumia tu njia zilizo sahihi. Tukiomba tutapokea.

Kwanza, tafakarini UMASKINI WA KUTAMANI—“Mwatamani, wala hamna kitu.” Tamaa za mwili, hata ziwe na nguvu kiasi gani, mara nyingi hazipati kile zinachokitafuta. Kama linenavyo andiko, “Mwatamani kuwa na kitu, wala hamwezi kupata.” Mtu hutamani kuwa na furaha, lakini hana. Hutamani sana kuwa mkuu, lakini huzidi kuwa duni kila siku. Hutumaini hiki na kile adhaniacho kuwa kitamridhisha, lakini hajaridhika bado. Yeye ni kama bahari ichafukayo isiyoweza kutulia. Kwa njia moja au nyingine, maisha yake ni kukatishwa tamaa. Hujitaabisha kama vile ndani ya moto wenyewe, lakini tokeo lake ni ubatili na kujitaabisha roho. Yawezaje kuwa vinginevyo? Tukipanda upepo, je! Hatutavuna tufani na si kitu kingine?

Au, kama, labda, tamaa kali za mtu mwenye bidii, mwenye vipawa, avumiliaye zampa kile akitafutacho, lakini haraka jinsi gani huipoteza! Anacho hali ya kwamba hana. Kufuatia ni kazi ngumu, bali kumiliki ni ndoto. Hukaa kula na tazama! Karamu hunyakuliwa, kikombe hutoweka kikiwa midomoni pake! Hushinda ili kupoteza! Hujenga, na msingi wake wa mchanga huteleza chini ya mnara wake, na juhudi zake huwa magofu. Yule aliyeziteka falme, alikufa hali hakuridhika juu ya mwamba wa upweke katikati ya bahari, na yule aliyeuhuisha ufalme wake, alianguka asisimame tena kamwe. Kama vile mtango wa Yona ulivyonyauka usiku mmoja, ndivyo falme zilivyoanguka ghafla, na wakuu wao wamekufa uhamishoni. Kile watu wapatacho kwa vita na mapigano ni milki ya kukodishwa kwa muda mfupi—kupata huko ni kwa muda hivi kwamba lingali kweli, “hutamani, wala hawana.”

Au kama watu kama hao wana vipawa na nguvu za kutosha kuyashika waliyoyashinda, lakini kwa maana nyingine hawana wanapokuwa nayo, kwa maana furaha waliyoitazamia ndani yake haimo. Huchuma tunda, nalo huwa moja la yale matunda ya Bahari ya Chumvi yageukayo majivu mkononi. Mtu ni tajiri, lakini Mungu humwondolea uwezo wa kufurahia utajiri wake. Kwa tamaa zake na vita vyake mtu mfisadi, mwishowe, hupata shabaha ya matamanio yake na, baada ya kutosheka kwa muda kidogo, huchukia kile alichokitamani kwa shauku hivyo! Huitamani ile anasa idanganyayo, huinyakua na kuiponda kwa mkono wake wa hamu!

Mtazame yule mvulana akiwinda kipepeo kirukacho ua hata ua huku akikifuatia kwa hamu. Mwishowe kimefikika, naye kwa kofia yake hukiangusha chini! Lakini achukuapo mabaki maskini, hukikuta kile kipepeo chenye rangi kimeharibiwa na kile kitendo kilichokishinda! Vivyo hivyo yaweza kunenwa juu ya wingi wa wana wa watu—“Mwatamani, wala hamna kitu.” Umaskini wao umeonyeshwa kwa namna tatu. “Mwaua na kutamani kuwa na kitu, wala hamwezi kupata,” “Hamna kitu, kwa sababu hamwombi.” “Mwaomba wala hampati, kwa sababu mwaomba vibaya.” Watamaniao wakishindwa, si kwa sababu hawakuanza kazi kuyapata makusudi yao, kwa maana, kwa kadiri ya asili yao, walitumia njia zilizo za matendo zaidi zilizo mikononi mwao, tena wakazitumia kwa hamu!

Kwa kadiri ya nia ya mwili, njia pekee ya kupata kitu ni kukipigania, naye Yakobo huliweka hili kuwa sababu ya mapigano yote. “Vita na mapigano kati yenu vyatoka wapi? Je! Havitoki katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu?” Hii ndiyo namna ya juhudi tusomayo habari zake, “Mwafanya vita na kupigana, lakini hamna kitu.” Watu hushikilia namna hii ya kutenda tangu kizazi hata kizazi. Mtu akitaka kuendelea katika dunia hii, waniambia, sharti ashindane na jirani zake, na kuwasukuma kutoka mahali pao pazuri. Haimpasi kujali jinsi wao watakavyofanikiwa, bali sharti aangalie faida yake mwenyewe na kujihadhari apande juu, hata awakanyage wengi kiasi gani. Hawezi kutumaini kuendelea akimpenda jirani yake kama nafsi yake! Ni pigano la haki, na kila mtu sharti ajiangalie mwenyewe!

Je! Mwadhani ninadhihaki? Yamkini, lakini nimesikia maneno ya namna hii kutoka kwa watu waliomaanisha. Basi hujiingiza katika kupigana, na kupigana huko mara nyingi hushinda, kwa maana, kwa kadiri ya andiko, “mwaua”—yaani, hupigana hata wamwangushe adui wao, na huo ndio mwisho wake. Ni watu wenye nguvu nyingi, wana-simba wawezao kutoka na kurarua mawindo yao vipandevipande, lakini, wasemwa juu yao, ya kwamba “hutindikiwa na kuona njaa.” Bali wamngojeao Bwana hawatapungukiwa na kitu chema chochote, hali watamaniao hawa hawana kizuizi katika juhudi zao za kufikia shabaha yao! Hawaachi lolote, huua na hutamani kuwa na kitu.

Zaidi ya hayo, hupigana kwa uvumilivu mwingi, kwa maana andiko lasema, “Mwafanya vita na kupigana.” Basi, vita ni mwendelezo wa tendo la kupigana, ukilirefusha kutoka mapambano hata mapambano na kuliendesha kwa kanuni za ufundi wa jeshi hata ushindi upatikane. Wingi wa watu wanaishi kwa ajili ya nafsi zao, wakishindana huku na kupigana huko, wakijipigania wenyewe kwa uvumilivu mkuu. Hawana hiari nyingi juu ya jinsi watakavyoifanya. Dhamiri hairuhusiwi kuingilia mambo yao, bali shauri la zamani lavuma masikioni mwao, “Pata fedha! Pata fedha kwa haki, kama uwezavyo, lakini kwa njia yoyote pata fedha.” Haidhuru ijapokuwa mwili na roho vinaharibiwa na wengine wanagharikishwa kwa taabu—endelea kupigana—kwa maana hakuna kuondoka katika vita hivi! Ukitaka kushinda, sharti upigane—na kila kitu ni halali vitani!

Basi hukusanya majeshi yao, hushindana na wenzao, huifanya vita ya maisha kuwa kali na kali zaidi, huufukuza upendo na kuuita wororo upumbavu—na bado, pamoja na hila zao zote, hawaupati mwisho wa maisha kwa maana yoyote ya kweli. Yakobo asema vema, “Mwaua na kutamani kuwa na kitu, wala hamwezi kupata; mwafanya vita na kupigana, lakini hamna kitu.” Watu walioshikilia sana makusudi yao ya ubinafsi wasipofaulu, huenda wakasikia ya kwamba sababu ya kutofaulu kwao ni “Kwa sababu hamwombi.” Basi, je! Kufaulu kwapatikana kwa kuomba? Ndivyo andiko laonekana kudokeza—na ndivyo wenye haki waonavyo. Kwa nini mtu huyu mwenye tamaa kali hajiingizi katika kuomba? Sababu ni, kwanza, kwa kuwa ni kinyume cha maumbile kwa mtu wa asili kusali—ni kama vile kumtazamia aruke!

Huidharau fikira ya kusihi. “Kusali?” asema. “La, nataka kuwa kazini. Siwezi kupoteza wakati kwa ibada; maombi hayana faida ya matendo. Nataka kupigania njia yangu. Wakati mnaposali, mimi nitakuwa nimemshinda mpinzani wangu. Naenda nyumbani kwangu kwa hesabu na kuwaacha ninyi na Biblia zenu na maombi yenu.” Hana nia ya kumwomba Mungu. Hutangaza ya kwamba hakuna aombaye ila wanafiki wenye maneno matupu, hivyo akiungama ya kwamba kama angesali, angekuwa mnafiki mwenye maneno matupu! Kwake yeye, kusali kwake ni kwa namna nyingine kabisa, na ole wao waingiao katika makucha yake! Watagundua ya kwamba kwake yeye, biashara ni biashara, tena biashara kali kabisa. Hatainama kamwe kusali, ana kiburi mno. Kumtegemea Mungu hakuelewi—kujitegemea mwenyewe ndilo neno lake! Nafsi ndiye mungu wake, na kwa mungu wake huutazamia ufanisi!

Ana kiburi kiasi kwamba hujihesabu kuwa Riziki yake mwenyewe! Mkono wake wa kuume na mkono wake wenye bidii vitampatia ushindi. Awapo mpole sana katika maoni yake, hukiri ya kwamba ijapokuwa hasali, lakini yamkini mna wema fulani ndani yake, kwa maana hutuliza akili za watu na kuwafanya wawe na raha zaidi. Lakini kuhusu jibu lolote kuja kutokana na maombi, huicheka fikira hiyo na kunena kwa hekima ya kifalsafa na ya kitheolojia juu ya upumbavu wa kudhania ya kwamba Mungu hubadili mwenendo wake kwa heshima ya maombi ya wanaume na wanawake. “Ni upuuzi,” asema, “upuuzi kabisa!” Kwa hiyo, katika hekima yake mwenyewe iliyo kuu, hurudi kwenye kupigana kwake na vita vyake, kwa maana kwa njia hizo atumaini kufikia mwisho wake. Lakini hapati!

Historia yote ya wanadamu huonyesha kushindwa kwa tamaa mbaya kupata shabaha yake. Kwa muda mtu wa mwili huendelea kupigana na kufanya vita, lakini, baada ya kitambo, hubadili nia yake, kwa maana ni mgonjwa, au ameogopa. Kusudi lake ni lilelile, lakini kama haliwezi kutimizwa kwa njia moja, atajaribu njia nyingine. Kama sharti aombe, vema, ataomba—atakuwa mtu wa dini na kujitendea mema kwa njia hiyo. Hukuta ya kwamba watu fulani wa dini hufanikiwa duniani, na ya kwamba hata Wakristo walio wanyofu si wapumbavu hata kidogo katika biashara na, kwa hiyo, atajaribu mpango wao. Na sasa huja chini ya lawama ya tatu ya andiko letu—“Mwaomba wala hampati.” Ni sababu gani mtu aliye mtumwa wa tamaa zake hapati haja yake, hata aombapo?

Sababu ni kwa kuwa kuomba kwake ni jambo la kufuata desturi tu. Moyo wake haumo katika ibada yake. Hununua kitabu chenye vitu viitwavyo, “kanuni za sala,” naye huzirudia hizi, kwa maana kurudia ni rahisi kuliko kusali wala hakudai fikira! Sina pingamizi mkitumia kanuni ya sala kama mkisali nayo, lakini nawajua wengi sana wasiosali nayo, bali huikariri tu ile kanuni. Fikirini yangetokea nini katika jamaa zetu kama, badala ya watoto wetu kunena nasi waziwazi wanapokuwa na hitaji lolote, wangefikiri sikuzote ya kwamba sharti waende maktabani na kutafuta kanuni ya sala na kutusomea! Bila shaka hisia yote ya nyumbani na upendo vingekoma! Maisha yangeenda katika minyororo! Nyumba yetu ingekuwa kama shule ya bweni, au kambi ya askari—na yote yangekuwa gwaride na desturi—badala ya macho yenye furaha yakitazama juu kwa tumaini la upendo katika macho ya wapendwa yafurahiayo kuitika!

Watu wengi wa kiroho hutumia kanuni, lakini watu wa mwili ni hakika kwamba watafanya hivyo, kwa maana huishia katika kanuni. Sala ya mtu huyu ni kuomba vibaya kwa sababu ni kwa ajili ya nafsi yake peke yake. Hutaka kufanikiwa ili ajifurahishe mwenyewe. Hutaka kuwa mkuu ili tu asifiwe—sala yake huanza na kuishia na nafsi. Angalieni aibu ya sala kama hiyo hata kama ni ya kunyofu. Mtu asalipo hivyo, humwomba Mungu awe mtumishi wake na kutosheleza tamaa zake. La, baya zaidi ya hilo! Hutaka Mungu ajiunge naye katika kutumikia tamaa zake mbaya! Yeye atatosheleza tamaa zake mbaya, na Mungu atakuja kumsaidia kuzitosheleza! Sala ya namna hii ni ya kufuru, lakini kiasi kikubwa chake hutolewa, nayo ni lazima iwe mojawapo ya mambo yamkasirishayo Mungu zaidi ambayo Mbingu iliyapata kuyaona!

La, kama mtu atataka kuishi kwa ajili ya nafsi yake na tamaa zake, na afanye hivyo, na kadiri anavyozidi kujitenga na Mungu ndivyo atakavyokuwa na mpatano zaidi. Asiseme kwa mdomo Sala ya Bwana kana kwamba Mungu ni baba yake, wala asilikokote jina takatifu la Kristo ili atakase choyo chake, wala asiuombe uweza uliobarikiwa wa Roho kuhusiana na kujitukuza kwake mwenyewe au tamaa yake ya ubinafsi! Akifanya hivyo, hatakuwa katika hali njema kuliko alivyokuwa mwanzo—ataomba, wala hatakuwa na kitu. Kuomba kwake kutakosa kwa sababu huomba vibaya, ili avitumie kwa tamaa zake. Kama tamaa zenu ni matamanio ya asili iliyoanguka; kama tamaa zenu huanza na kuishia na nafsi yenu, na kama mwisho mkuu mnaoishi kwa ajili yake si kumtukuza Mungu, bali kujitukuza wenyewe, basi mwaweza kupigana, lakini hamtakuwa na kitu!

Mwaweza kuamka mapema na kukesha, lakini hakuna cha thamani kitakachopatikana kwa hilo! Kumbukeni jinsi Bwana alivyonena katika Zaburi ya 37—“Uache hasira, ukaache ghadhabu; usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya. Kwa maana bado kitambo kidogo, na mtu mwovu hatakuwapo; naam, utapaangalia kwa bidii mahali pake, wala hatakuwapo. Bali wenye upole watairithi nchi; watajifurahisha kwa wingi wa amani.”

Basi yatosha hayo juu ya umaskini wa kutamani.

II. Pili, sasa nina mbele yangu shughuli nzito, nayo ni, kuonyesha JINSI MAKANISA YA KIKRISTO YANAVYOWEZA KUPATWA NA UMASKINI WA KIROHO hata nayo, “yatamani kuwa na kitu, wala hayawezi kupata.” Bila shaka Mkristo hutafuta vitu vilivyo bora kuliko vya mtu wa dunia, la sivyo asingestahili jina hilo hata kidogo. Angalau, kwa madai, shabaha yake ni kupata utajiri wa kweli na kumtukuza Mungu katika roho na kweli. Naam, lakini tazameni, Ndugu wapendwa, si Makanisa yote yapatayo yanayoyatamani. Yatupasa kulalamika, si huku na huko, bali katika mahali pengi, juu ya Makanisa yaliyo karibu kulala usingizi na yanayozidi kupungua taratibu.

Bila shaka hupata udhuru. Idadi ya watu inapungua, au mahali pengine pa ibada panawavuta watu. Sikuzote kuna udhuru ulio tayari mtu ahitajipo. Lakini bado, jambo lasimama—ibada ya hadhara imekaribia kuachwa mahali fulani, huduma haina nguvu ya kukusanya watu—na wale wanaohudhuria hawaridhiki au hawajali. Katika Makanisa kama hayo hakuna waongofu. Kama wangeongezewa nusu dazani kwa mwaka, wangehitaji kuimba “Wimbo wa Haleluya”! Lakini kuhusu kumleta maelfu kwa Kristo, kwa siri huogopa ya kwamba jambo hili lingekuwa lisilotamanika, kwa maana lingeweza kuleta mchafuko—nao ni wenye adabu kiasi kwamba huogopa jambo lolote la namna hiyo!

Kutofanya lolote na kuwaacha watu wahukumiwe adhabu ni, kwa hukumu yao, jambo linalofaa na la heshima. Lakini kuwa hai na kuwa na bidii ni hali ya hatari, kwa maana lingeweza kuongoza kwenye ushabiki na kukosa adabu! Wanaogopa hasa jambo lolote lililo kama “kutafuta hisia kali.” Neno hilo lenye sura mbaya hulitia mbele yetu kama vile Wachina wajaribuvyo kuwaogofya adui zao kwa kupaka sura za kutisha juu ya ngao zao! Msilijali neno hilo la kutisha—halitamdhuru mtu yeyote! Makanisa haya “hayana kitu,” kwa maana hakuna Kweli ya Mungu inayoenezwa kwa bidii yao; hakuna dhambi inayopigwa; hakuna utakatifu unaokuzwa; hakuna lolote lifanywalo ambalo kwalo Mungu hutukuzwa. Na sababu yake ni nini?

Kwanza, hata miongoni mwa wanaojidai kuwa Wakristo huenda pakawa na kufuatia vitu vinavyotamanika kwa njia isiyo sahihi. “Mwafanya vita na kupigana, lakini hamna kitu.” Je! Makanisa hayakufikiri kufanikiwa kwa kushindana na Makanisa mengine? Katika mahali fulani pa ibada wana mtu mwerevu sana—sisi nasi sharti tupate mtu mwerevu! Kwa kweli, sharti awe mwerevu kidogo kuliko shujaa wa jirani yetu. Hilo ndilo jambo—mtu mwerevu! Ole wangu, kwamba tuishi katika zama ambazo twanena juu ya watu werevu katika kuhubiri Injili ya Yesu Kristo! Ole, kwamba huduma hii takatifu idhaniwe kutegemea werevu wa kibinadamu! Makanisa yameshindana kila moja na jingine katika ujenzi, katika muziki, katika mavazi na katika hadhi ya kijamii. Viongozi hudhania ya kwamba ili kufaulu sharti wawe na kitu kilicho kizuri zaidi, chenye sanaa zaidi, au cha gharama zaidi kuliko jirani zao—kwa hiyo hujenga majengo ya kigothiki ambamo sauti ya mhudumu hupanda katikati ya mbao wala haisikiki vema kamwe—au sivyo hununua kinanda chenye kila kizuizi ila kile cha sauti kamili!

Maoni yaonekana kuenea kotekote ya kwamba mna Neema tele katika kinanda. Kumwomba Mungu kwa kinu cha upepo, kama Watartari, kungekuwa upumbavu mkubwa! Lakini kumsifu Mungu kwa upepo upitao katika mfululizo wa mirija ni jambo linalofaa mno! Sijapata kuona tofauti hiyo wala sioni sasa. Kinanda au bila kinanda si, sasa, ndilo swali, bali nanena juu ya matukio ambamo mashine hizi husimikwa kama jambo la ushindani. Je! Si kusudi la wengi kufaulu kwa jengo lililo zuri zaidi, muziki ulio bora zaidi na huduma iliyo na werevu zaidi kuliko wengine? Je! Si jambo la ushindani kama vile sura ya duka na dirisha lililopambwa vilivyo kwa wafanyabiashara wa nguo? Je! Hii ndiyo njia ambayo kwayo Ufalme wa Mungu utakua kati yetu?

Katika baadhi ya matukio mna kiasi cha uchungu katika ushindani. Si jambo la kupendeza kwa akili ndogo kuona Makanisa mengine yakifanikiwa kuliko yao. Yamkini wao ni wenye bidii kuliko sisi na wanaifanya kazi ya Mungu vema zaidi, lakini sisi twaelekea mno kuwatazama kwa jicho la wivu—na sisi, kwa uwazi, tungependelea wasiendelee vizuri hivyo. Je! Mwadhani Andiko lasema bure, “Roho akaaye ndani yetu hututamani hata kuona wivu?” Kama tungeweza kuona machafuko kati yao, hata wavunjike na kuuawa kikanisa, hatungefurahi. La hasha! Lakini pia tusingepatwa na huzuni yoyote ya kufisha! Katika Makanisa fulani roho mbaya hukaa. Sileti mashtaka ya matukano, kwa hiyo, sinena zaidi ila hili—Mungu hatabariki kamwe njia kama hizo na roho kama hiyo—wale wanaozikubali watatamani kuwa na kitu, lakini hawatapata kamwe.

Wakati huohuo, ni sababu gani hawapati baraka? Andiko lasema, “Kwa sababu hamwombi.” Naogopa kuna Makanisa yasiyoomba. Maombi ya kila namna yamepuuzwa mno. Maombi ya faragha yaachwa yafifie. Nitaliweka mbele ya dhamiri ya kila mtu kuhusu kadiri maombi ya siri yanavyotimizwa na kiasi cha ushirika na Mungu kilichopo kwa siri miongoni mwa washiriki wa Makanisa yetu. Bila shaka kuwako kwake kwa afya ni jambo la lazima kwa ufanisi wa Kanisa. Kuhusu maombi ya jamaa ni rahisi zaidi kuhukumu, kwa maana twaweza kuyaona. Naogopa ya kwamba siku hizi wengi wameyaacha kabisa maombi ya jamaa. Nawasihi msiwaige!

Ningependa nyote mngekuwa na nia moja na yule kibarua Mskoti aliyepata kazi katika nyumba ya mkulima tajiri aliyejulikana kulipa vema. Rafiki zake wote walimwonea wivu kwamba alikwenda kuishi katika utumishi kama huo. Baada ya muda mfupi alirudi kijijini kwao. Na walipomwuliza kwa nini aliacha kazi yake, akajibu ya kwamba, “hakuweza kuishi katika nyumba isiyo na paa.” Nyumba isiyo na maombi ni nyumba isiyo na paa! Hatuwezi kutazamia baraka juu ya Makanisa yetu kama hatuna baraka juu ya jamaa zetu! Kuhusu maombi ya kusanyiko, kukutana pamoja katika kile tuitacho Mikutano yetu ya Maombi—je! Hakuna kupungua? Katika matukio mengi Mkutano wa Maombi hudharauliwa na kutazamwa chini kama mkusanyiko wa daraja la pili. Wako washiriki wa Makanisa wasiohudhuria kamwe, wala haichomi dhamiri zao ya kwamba wanakaa mbali.

Baadhi ya makutaniko huchanganya Mkutano wa Maombi na hotuba, ili kufanya ibada moja tu kwa juma. Siku moja nilisoma udhuru wa haya yote—husemwa ya kwamba watu ni afadhali wakiwa nyumbani, wakishughulikia mambo ya jamaa. Haya ni maneno matupu! Ni nani miongoni mwetu atakaye watu wapuuze mambo yao ya nyumbani? Itaonekana ya kwamba wanaoyashughulikia vema mambo yao wenyewe ni wale walio na bidii kupanga kila kitu kwa utaratibu, ili waweze kutoka kwenda kwenye makusanyiko ya ibada. Kupuuza Nyumba ya Mungu mara nyingi ni ishara ya kupuuza nyumba zao wenyewe! Hawawaleti watoto wao kwa Kristo, nasadiki, kwani wangewalea hata waje kwenye ibada. Vyovyote iwavyo, maombi ya Kanisa hupima ufanisi wake. Tukiyazuia maombi twaizuia baraka.

Ufanisi wetu wa kweli kama Makanisa waweza kupatikana tu kwa kuuomba kwa Bwana. Je! Hatuko tayari kujirekebisha na kujisahihisha katika jambo hili? Laiti saa ya utungu wa Sayuni ingekuja, ambapo uchungu wa maombi utausukuma mwili mzima wa waaminifu! Lakini baadhi hujibu, “Kuna Mikutano ya Maombi nasi twaomba baraka, lakini bado haiji.” Je! Maelezo hayapatikani katika sehemu ile nyingine ya andiko, “Hamna kitu, kwa sababu mwaomba vibaya”? Mikutano ya Maombi ipatapo kuwa desturi tu; Ndugu wasimamapo na kupoteza wakati kwa hotuba zao ndefu badala ya kunena na Mungu kwa maneno ya bidii na yawakayo; kusipokuwa na kutazamia baraka—maombi yapokuwa baridi na yenye kuganda—ndipo hakuna kitakachotokana nayo. Yeye asaliye pasipo bidii hasali kabisa! Hatuwezi kushirikiana na Mungu, aliye moto ulao, kama hakuna moto katika maombi yetu!

Maombi mengi hukosa lengo lake kwa sababu hakuna imani ndani yake. Maombi yaliyojaa shaka ni maombi ya kukataliwa. Fikirini ya kwamba mlimwandikia rafiki na kusema, “Rafiki Mpendwa, nina taabu kubwa, kwa hiyo nakuambia, na kukuomba msaada kwa kuwa yaonekana vema kufanya hivyo. Lakini ijapokuwa naandika hivi, sina imani ya kwamba utanipelekea msaada wowote. Kwa kweli, ningeshangaa sana kama ungefanya hivyo, na ningelisema kuwa ni ajabu kubwa.” Je! Mwadhani mtapata msaada? Ningesema rafiki yenu angekuwa na busara ya kutosha kutambua tumaini dogo mlilo nalo kwake, naye angejibu ya kwamba, kwa kuwa hamkutazamia kitu chochote, hangewashangaza. Maoni yenu juu ya ukarimu wake ni ya chini kiasi kwamba haoni kuwa amewajibika kujitaabisha kwa ajili yenu. Maombi yapokuwa ya namna hiyo hamwezi kustaajabu tukiwa “hatuna kitu, kwa sababu twaomba vibaya.”

Zaidi ya hayo, kama kuomba kwetu, hata kuwe na bidii na imani kiasi gani, ni kuomba tu ili Kanisa letu lifanikiwe kwa sababu twataka kujisifu katika ufanisi wake—kama twataka kuona dhehebu letu likiongezeka sana na heshima yake ikiboreshwa, ili tushiriki heshima zake—basi tamaa zetu si kitu ila tamaa mbaya, baada ya yote! Je! Yawezekana wana wa Mungu waonyeshe mashindano yaleyale, wivu na tamaa za makuu kama watu wa dunia? Je! Kazi ya dini iwe jambo la ushindani na mashindano? Ah, basi, maombi yanayotafuta kufaulu hayatakubalika mbele ya Kiti cha Rehema! Mungu hatatusikia, bali atatuamuru tuondoke, kwa maana hajali maombi ambayo nafsi ndiyo shabaha yake. “Hamna kitu, kwa sababu hamwombi, au kwa sababu mwaomba vibaya.”

' III. Tatu, nina kazi ya kupendeza zaidi sana ya kufanya, nayo ni kudokeza juu ya UTAJIRI UNAONGOJEA MATUMIZI YA NJIA ZILIZO SAHIHI, yaani, ya kumwomba Mungu kwa halali. Nawaalika mtie fikira zenu za dhati sana katika jambo hili, kwa maana ni la muhimu mno. Na tazamio langu la kwanza ni hili—ni ndogo mno, baada ya yote, hitaji hili ambalo Mungu hutudai. Kuomba? Ni jambo dogo kabisa awezalo kututazamia, wala si zaidi ya tunavyowadai kwa kawaida wale wanaohitaji msaada kutoka kwetu! Twamtazamia maskini aombe, na kama hafanyi hivyo, twaweka lawama ya upungufu wake juu yake mwenyewe. Kama Mungu atatoa kwa kuombwa nasi tukabaki maskini, ni nani wa kulaumiwa? Je! Lawama hii si nzito mno? Je! Haionekani kana kwamba hatuko sawa na Mungu, hata hatujinyenyekezi hata kuomba fadhili kwake? Bila shaka, ni lazima uwepo, mioyoni mwetu, uadui uliojificha juu yake, la sivyo, badala ya kuwa hitaji lisilopendeza, lingehesabiwa kuwa furaha kubwa!

Lakini, Ndugu, tupende tusipende, kumbukeni, kuomba ndiyo kanuni ya Ufalme. “Ombeni, nanyi mtapata.” Ni kanuni ambayo haitabadilishwa kamwe kwa mtu yeyote. Bwana wetu Yesu Kristo ndiye Ndugu mkubwa wa

jamaa, lakini Mungu hakumlegezea kanuni hiyo! Kumbukeni andiko hili—Yehova amwambia Mwanawe mwenyewe, “Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, na miisho ya dunia kuwa milki yako.” Ikiwa Mwana wa Mungu aliye wa kifalme na wa Kimungu hawezi kusamehewa kanuni ya kuomba, ili apate, mimi na wewe hatuwezi kutazamia kanuni hiyo ilegezwe kwa faida yetu!

Kwa nini iwe hivyo? Ni sababu gani iwezayo kutolewa ya kwamba tusamehewe maombi? Ni hoja gani iwezayo kuwapo ya kwamba tunyimwe pendeleo hili na kuokolewa na ulazima wa kusihi? Mimi sioni hata moja—je! Wewe waona? Mungu atambariki Eliya na kunyesha mvua juu ya Israeli, lakini Eliya sharti aiombee. Kama taifa lililochaguliwa litafanikiwa, Samweli sharti aliombee. Kama Wayahudi watakombolewa, Danieli sharti aombe maombezi. Mungu atambariki Paulo, na mataifa yataongolewa kwa kupitia yeye, lakini Paulo sharti aombe! Naye aliomba, bila kukoma—Nyaraka zake huonyesha ya kwamba hakutazamia kitu chochote ila kwa kukiombea. Kama mwaweza kuwa na kila kitu kwa kuomba na hakuna kitu pasipo kuomba, nawasihi mwone jinsi maombi yalivyo ya lazima kabisa! Nami nawasihi mzidi ndani yake.

Zaidi ya hayo, ni wazi hata kwa mwenye kufikiri kwa juujuu zaidi ya kwamba viko vitu fulani vya lazima kwa Kanisa la Mungu ambavyo hatuwezi kuvipata ila kwa maombi. Waweza kumpata yule mtu mwerevu niliyesema juu yake—labda kadiri unavyopunguza kumwombea, ndivyo iwavyo bora zaidi! Na Kanisa lile jipya, na kinanda kile kipya, na kwaya waweza kuvipata pia pasipo maombi—lakini huwezi kupata upako wa mbinguni—kipawa cha Mungu hakinunuliwi kwa fedha! Baadhi ya washiriki wa Kanisa katika kijiji cha zamani cha Amerika walidhani ya kwamba wangeinua kusanyiko kwa kutundika taa nzuri sana ya kioo katika Nyumba ya Mkutano. Watu walinena juu ya taa hii ya kioo na baadhi walikwenda kuiona—lakini nuru yake ilififia upesi.

Waweza kununua kila namna ya samani za kikanisa! Waweza kununua kila aina ya rangi, shaba, kitani chembamba, buluu, nyekundu na kitani safi—pamoja na filimbi, vinubi, mabaragumu, vinanda na kila namna ya muziki—waweza kuvipata bila maombi. Kwa kweli, ingekuwa dharau kuomba juu ya takataka kama hizo! Lakini huwezi kumpata Roho Mtakatifu bila maombi. “Yeye huvuma apendako.” Hataletwa karibu kwa mtaratibu wowote au mbinu iliyo mikononi mwetu bila kuomba. Hakuna njia za kimitambo zitakazoziba pengo la kutokuwepo kwake! Kama Roho Mtakatifu hayupo, ni faida gani ya yule mtu wenu mwerevu? Je! Kutakuwa na yeyote atakayeongolewa? Je! Nafsi yoyote itafarijiwa? Je! Wana wa Mungu wowote watafanywa upya katika uzima wa kiroho bila Roho Mtakatifu? Wala huwezi kupata ushirika na Mungu bila maombi. Yeye asiyetaka kusali, hawezi kuwa na ushirika na Mungu. Zaidi ya hayo, hakuna ushirika halisi wa kiroho wa Kanisa na washiriki wake wenyewe maombi yasimamishwapo. Maombi sharti yawe katika tendo, la sivyo baraka zile zilizo za lazima kabisa kwa ufanisi wa Kanisa haziwezi kamwe kulijia. Maombi ni mlango mkuu wa baraka ya kiroho, na ukiufunga, waizuia fadhili nje.

Ndugu wapendwa, je! Hamdhani ya kwamba kuomba huku, ambako Mungu hutaka, ni pendeleo kubwa mno? Fikirini kwamba pangetangazwa amri ya kuwa hampaswi kusali—hilo lingekuwa dhiki, kweli kweli! Kama maombi yangekatiza, badala ya kuongeza mkondo wa baraka, lingekuwa msiba wa kusikitisha. Je! Mmepata kuona bubu aliye chini ya msisimko mkali, au anayeteseka maumivu makali na, kwa hiyo, ana hamu ya kunena? Ni jambo la kutisha kuliona! Uso hupindika, mwili hutikiswa vibaya—bubu hujigalagaza na kujitaabisha katika dhiki kali. Kila kiungo hupinda kwa tamaa ya kuusaidia ulimi, lakini hauwezi kuvunja vifungo vyake! Sauti tupu hutoka kifuani na kigugumizi cha maneno yasiyofaa huamsha usikivu, ijapokuwa hayawezi kufika hata kwenye kueleweka. Kiumbe maskini kimo katika maumivu yasiyoelezeka!

Fikirini kwamba tungekuwa, katika asili yetu ya kiroho, tumejaa tamaa kali na bado mabubu kuhusu ulimi wa maombi? Nadhani lingekuwa mojawapo ya mateso mabaya kabisa yawezayo kutupata! Tungekuwa vilema vibaya na waliokatwakatwa viungo—na uchungu wetu ungetuzidi nguvu! Jina lake libarikiwe, Bwana huamuru njia ya kunena na kuuamuru moyo wetu uneme kwake! Wapendwa, ni lazima tusali—yaonekana kwangu kwamba lapasa liwe jambo la kwanza tunalowaza kufanya tunapokuwa katika hitaji. Kama watu wangekuwa sawa na Mungu na kumpenda kweli, wangesali kwa maumbile kama wapumuavyo! Natumaini baadhi yetu wako sawa na Mungu wala hawahitaji kusukumwa kwenye maombi, kwa maana yamekuwa hulka ya asili yetu.

Rafiki yangu aliniambia, jana, hadithi ya mvulana mdogo Mjerumani—hadithi ambayo mchungaji wake alipenda kuisimulia. Mtoto mpendwa mdogo alimwamini Mungu wake na kufurahia maombi. Mwalimu wake wa shule alikuwa amewahimiza wanafunzi kufika shuleni kwa wakati, na mtoto huyu sikuzote alijitahidi kuwa hivyo. Lakini baba yake na mama yake walikuwa watu wa polepole na, asubuhi moja, kwa kosa lao, peke yao, alitoka mlangoni sawasawa saa ilipopiga wakati wa shule kufunguliwa. Rafiki mmoja, aliyekuwa amesimama karibu, alimsikia yule mdogo akilia, “Ee Mungu mpendwa, tafadhali nijalie niwahi shuleni.” Ilimgusa yule aliyesikiliza ya kwamba kwa mara hii, maombi hayangeweza kusikiwa, kwa maana mtoto alikuwa na mwendo mfupi kiasi mbele yake na saa ilikuwa tayari imefika. Alitaka kujua matokeo.

Basi ikawa asubuhi ile ya kwamba mwalimu, alipojaribu kufungua mlango wa nyumba ya shule, aliuzungusha ufunguo upande usiofaa wala hakuweza kuusogeza komeo. Ilibidi watume kumwita fundi wa kufuli aufungue mlango. Kwa hiyo kukawa na kucheleweshwa, na sawasawa mlango

ulipofunguliwa, rafiki yetu mdogo aliingia pamoja na wengine, wote kwa wakati mzuri! Mungu ana njia nyingi za kutimiza tamaa zilizo sawa. Ilikuwa jambo la kawaida kabisa kwamba, badala ya kulia na kunung'unika, mtoto aliyempenda Mungu kweli anene naye juu ya taabu yake. Je! Isiwe jambo la kawaida kwako na kwangu, papo hapo na mara moja, kumwambia Bwana huzuni zetu na kuomba msaada? Je! Hii isiwe njia ya kwanza tukimbiliayo? Ole, kwa kadiri ya Maandiko na kwa kuchunguza—na, nasikitika kuongeza—kwa kadiri ya uzoefu, maombi mara nyingi ni jambo la mwisho!

Mtazameni mtu mgonjwa katika Zaburi ya 107. Rafiki humletea vyakula mbalimbali, lakini nafsi yake huchukia kila namna ya chakula. Matabibu hufanya wawezalo kumponya, lakini huzidi kuwa mbaya na mbaya zaidi, na kukaribia malango ya mauti— “Ndipo humlilia Bwana katika taabu zao.” Lililowekwa mwisho ndilo lililopaswa kuwa la kwanza! “Mwiteni tabibu. Mwandalieni chakula. Mfungeni katika nguo za sufu!” Yote ni mema kabisa, lakini ni lini mtamwomba Mungu? Mungu ataitwa hali itakapokuwa ya kukata tamaa! Watazameni mabaharia walioelezwa katika Zaburi ileile. Meli imekaribia kuvunjika. “Hupanda mbinguni, hushuka tena vilindini; nafsi yao huyeyuka kwa sababu ya taabu.” Bado hufanya wawezayo yote kuyapinga mawimbi. Lakini “wanapoyumbayumba na kupepesuka kama mlevi, na akili zao zote zikawaishia; ndipo humlilia Bwana katika taabu zao.”

Ee, naam; Mungu hutafutwa tunaposukumwa pembeni na kuwa tayari kuangamia! Na ni rehema iliyoje kwamba husikia maombi ya kuchelewa namna hiyo na kuwaokoa wasihio kutoka katika taabu zao! Lakini je! Ipasa kuwa hivyo kwako na kwangu, na kwa Makanisa ya Kristo? Je! Msukumo wa kwanza wa Kanisa lililopungua usipaswi kuwa, “Na tuombe mchana na usiku hata Bwana atujilie. Na tukutane pamoja kwa nia moja mahali pamoja wala tusitengane hata baraka itushukie”? Je! Mwajua, Ndugu, ni mambo makuu kiasi gani yawezayo kupatikana kwa kuomba? Je! Mmepata kulifikiria? Je! Halikuchochei kusali kwa bidii? Mbingu yote yakaa mbele ya mkono wa yule aombaye! Ahadi zote za Mungu ni tajiri na zisizoisha—na kutimizwa kwake kwapatikana kwa maombi!

Yesu asema, “Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu,” naye Paulo asema, “Vitu vyote ni vyenu, nanyi ni wa Kristo.” Ni nani asingesali hali vitu vyote vimekabidhiwa kwetu hivyo? Naam, na ahadi zilizotolewa kwanza kwa watu maalum zote hutolewa kwetu ikiwa twajua jinsi ya kuziombea katika maombi. Israeli walipita katika Bahari ya Shamu enzi za kale, lakini twasoma katika Zaburi ya 66, “Huko tulimfurahia.” Yakobo peke yake ndiye aliyekuwapo Penieli, lakini Hosea asema, “Huko alisema nasi.” Paulo ataka kutupa ahadi kuu kwa nyakati za hitaji, naye anukuu kutoka Agano la Kale, “Kwa maana amesema, Sitakuacha kamwe wala sitakupungukia kamwe.” Paulo aliipata wapi hiyo? Ndio uthibitisho ambao Bwana alimpa Yoshua—“Sitakuacha kamwe wala sitakupungukia kamwe.”

Bila shaka ahadi ilikuwa kwa ajili ya Yoshua peke yake! La, ni kwa ajili yetu! “Hakuna Andiko lipatalo kufasiriwa kwa nafsi ya mtu peke yake.” Andiko lote ni letu. Tazameni jinsi Mungu anavyomtokea Sulemani usiku na kusema, “Omba nitakupa nini.” Sulemani aomba hekima. “Ee, huyo ni Sulemani,” mwasema. Sikilizeni!—“Mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu.” Mungu alimpa Sulemani utajiri na umaarufu pia kwa nyongeza! Je! Hilo si la Sulemani peke yake? La, kwa maana hunenwa juu ya hekima ya kweli, “Wingi wa siku u katika mkono wake wa kuume; na katika mkono wake wa kushoto utajiri na heshima”—na je! Hili si kama sana maneno ya Mwokozi wetu, “Utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa”? Hivyo, mwaona, ahadi za Bwana zina timizo nyingi, nazo zinangoja kumimina hazina zake katika paja la maombi! Je! Hili haliyainui maombi hata daraja la juu, hali Mungu yu radhi kurudia habari za maisha ya watakatifu wake ndani yetu, akingoja kufanya neema, na kututwika baraka zake?

Nitataja Kweli nyingine ya Mungu ipasayo kutufanya tusali, nayo ni ya kwamba, tukiomba, Mungu atatupa zaidi sana ya tuombavyo. Ibrahimu alimwomba Mungu kwamba Ishmaeli aishi mbele zake. Aliwaza, “Bila shaka huyu ndiye uzao ulioahidiwa: siwezi kutazamia ya kwamba Sara atazaa mtoto katika uzee wake. Mungu ameniahidi uzao, na bila shaka ni lazima awe huyu mtoto wa Hagari. Ee laiti Ishmaeli angeishi mbele zako.” Mungu alimjalia hilo, naye akampa Isaka pia, na baraka zote za Agano! Yupo Yakobo. Hupiga magoti kusali na kumwomba Bwana ampe mkate wa kula na nguo za kuvaa. Lakini Mungu wake alimpa nini? Aliporudi Betheli, alikuwa na makundi mawili, maelfu ya kondoo na ngamia, na utajiri mwingi! Mungu alikuwa amemsikia na kufanya kwa wingi kupita kiasi zaidi ya alivyoomba!

Hunenwa juu ya Daudi, “Mfalme alikuomba uhai, ukampa; naam, wingi wa siku,” naam, ukampa si wingi wa siku tu, bali na kiti cha enzi kwa wanawe vizazi vyote, hata Daudi alipoingia na kuketi mbele za Bwana, akishindwa na wema wa Bwana. “Vema,” mwasema, “lakini je! Hilo ni kweli kwa maombi ya Agano Jipya? “Naam, ni hivyo kwa waombao wa Agano Jipya, wakiwa watakatifu au wenye dhambi! Walimletea Kristo mtu, mwenye ugonjwa wa kupooza, na kumwomba amponye. Naye akasema, “Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.” Hakuwa ameomba hilo, sivyo? La, lakini Mungu hutoa vitu vikuu kuliko tuombavyo!

Sikilizeni maombi ya unyenyekevu ya yule mwivi maskini aliyekuwa akifa, “Bwana, unikumbuke utakapoingia katika Ufalme wako.” Yesu ajibu, “Leo hivi utakuwa pamoja nami peponi”! Hakuwa amewaza heshima kama hiyo!

Hata hadithi ya yule Mpotevu hutufundisha hili. Aliazimu kusema, “Sistahili kuitwa mwana wako; nifanye kama mmoja wa watumishi wako wa mshahara.” Jibu ni nini? “Huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye yu hai tena: leteni vazi lililo bora, mkamvike; tieni pete mkononi mwake, na viatu miguuni mwake.” Mara upatapo hali ya mwombaji nawe utapata usichokiomba kamwe wala usichowaza kukipokea! Andiko mara nyingi hunukuliwa vibaya—“Mungu aweza kufanya mambo ya ajabu mno kupita yote tuwezayo kuomba, au hata kuwaza.” Tungeweza kuomba, kama tungekuwa na busara zaidi na imani zaidi, kwa vitu vilivyo vikuu kabisa, lakini Mungu yu radhi kutupa kupita kiasi zaidi ya tuombavyo!

Wakati huu naamini ya kwamba Kanisa la Mungu lingeweza kupata baraka zisizowazika kama lingekuwa tayari, sasa, kusali. Je! Mmepata kuiona ile picha ya ajabu katika sura ya 8 ya Ufunuo? Yastahili kutazamwa kwa makini. Sitajaribu kuieleza, katika muktadha wake, bali nitaielekeza tu ile picha kama inavyoning'inia ukutani peke yake. Someni—“Alipoifungua muhuri ya saba, kukawa kimya mbinguni kama nusu saa.” Kimya mbinguni!? Hazikuwapo nyimbo za sifa, wala hallelujah, wala malaika hakutikisa bawa! Kimya mbinguni!? Je! Mwaweza kuwaza? Na tazameni! Mwaona malaika saba wamesimama mbele za Mungu, nao hupewa baragumu saba. Hapo hungoja, baragumu mkononi, lakini hakuna sauti! Hakuna hata noti moja ya shangwe au ya onyo katika kipindi ambacho kilikuwa kirefu vya kutosha kuchochea hisia hai, lakini kifupi vya kutosha kuzuia kukosa saburi.

Kimya kisichovunjika, kirefu, cha kutisha, kilitawala mbinguni! Tendo limesimamishwa mbinguni, kitovu cha shughuli zote. “Kisha malaika mwingine akaja, akasimama mbele ya madhabahu, mwenye chetezo cha dhahabu.” Hapo asimama, lakini hakuna sadaka itolewayo—kila kitu kimefikia kusimama tuli. Ni nini kiwezacho kukiweka katika mwendo? “Akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi.” Maombi hutolewa pamoja na ustahili wa Bwana Yesu! Basi, tazameni litakalotokea—“Na moshi wa ule uvumba, uliokuja pamoja na maombi ya watakatifu, ukapanda mbele za Mungu kutoka mkononi mwa malaika.” Huo ndio ufunguo wa jambo lote!

Sasa mtaona—malaika aanza kutenda kazi—huchukua chetezo, hukijaza moto wa madhabahuni na kukitupa chini juu ya nchi, “kukawa na sauti, na ngurumo, na umeme, na tetemeko la nchi.” “Na wale malaika saba wenye baragumu saba wakajifanya tayari wapige baragumu.” Kila kitu chasonga sasa! Mara maombi ya watakatifu yalipochanganywa na uvumba wa ustahili wa milele wa Kristo na kuanza kupanda kama moshi kutoka madhabahuni, ndipo maombi yalipofanyika yenye nguvu! Yakaanguka makaa yaliyo hai kati ya wana wa watu, hali malaika wa Riziki ya Kimungu, waliokuwa wamesimama tuli, hapo mbele, wakapiga ngurumo zao, na mapenzi ya Bwana yakatimizwa! Ndivyo ilivyo hali ya mambo mbinguni, kwa kadiri fulani, hata leo hii. Leteni hapa uvumba! Leteni hapa maombi ya watakatifu! Yawasheni moto kwa ustahili wa Kristo, na juu ya madhabahu ya dhahabu na yatoe moshi mbele za Aliye Juu! Ndipo tutakapomwona Bwana akitenda kazi, na mapenzi yake yatatimizwa duniani kama mbinguni! Mungu na apeleke baraka yake pamoja na maneno haya, kwa ajili ya Kristo. Amina.

Yaliyomo

Nguvu Kuu katika Maombi Charles H. Spurgeon

Ukurasa 1 / 1 · 30 dakika zimebaki katika sura