Sura 3 · dakika 29 za kusoma
Ufunguo wa Dhahabu wa Maombi
“Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.” Yeremia 33:3.
BAADHI ya kazi zilizosomeka zaidi duniani zanukia mafuta ya taa ya usiku wa manane. Lakini vitabu na maneno ya watu yaliyo ya kiroho zaidi na yenye faraja zaidi kwa kawaida huwa na harufu ya unyevunyevu wa gerezani. Ningeweza kutaja mifano mingi—Msafiri wa John Bunyan waweza kutosha badala ya mia nyingine. Na andiko hili letu jema, lililojaa ukungu na baridi ya gereza alimolala Yeremia, hata hivyo lina mng’ao na uzuri ambao huenda lisingekuwa nao kamwe kama lisingelikuja kama neno la kutia moyo kwa mfungwa wa Bwana aliyefungwa katika ua wa gereza.
Watu wa Mungu sikuzote, katika hali yao mbaya kabisa, wamekigundua kilicho bora zaidi cha Mungu wao. Yeye ni mwema nyakati zote, lakini aonekana kuwa katika ubora wake wa hali ya juu wakati wao wako katika hali yao mbaya kabisa. “Uliwezaje kuvumilia kifungo chako kirefu vizuri hivyo?” mtu mmoja alimwuliza Landgrave wa Hesse aliyekuwa amefungwa kwa sababu ya kushikamana kwake na kanuni za Matengenezo. Akajibu, “Faraja za Kimungu za wafia-dini zilikuwa pamoja nami.”
Bila shaka kuna faraja iliyo na kina zaidi, iliyo na nguvu zaidi kuliko nyingine yoyote ambayo Mungu huiweka akiba kwa ajili ya wale ambao, wakiwa mashahidi wake waaminifu, wanapaswa kuvumilia dhiki kubwa mno itokanayo na uadui wa mwanadamu. Kuna mianga ya ajabu ya angani kwa ajili ya ukanda ulio na baridi kali. Na nyota hung’aa katika mbingu za kaskazini kwa fahari isiyo ya kawaida. Rutherford alikuwa na msemo wa kipekee kwamba alipotupwa katika vyumba vya chini vya mateso, alikumbuka kwamba Mfalme mkuu sikuzote aliweka mvinyo wake humo, naye akaanza mara moja kutafuta chupa za mvinyo na kunywa ile “mivinyo iliyokaa juu ya urojorojo, iliyosafishwa vema.”
Wale wazamiao katika bahari ya mateso huleta lulu adimu. Mnajua, enyi wenzangu katika mateso, kwamba ndivyo ilivyo. Ninyi ambao mifupa yenu imekaribia kutokeza nje ya ngozi kwa kulala muda mrefu juu ya kitanda cha uchovu. Ninyi mlioona mali zenu za kidunia zikichukuliwa mbali nanyi hata mkakaribia kufikia ufukara. Ninyi mliokwenda kaburini mara hizi saba, hata mkaogopa kwamba rafiki yenu wa mwisho wa kidunia angechukuliwa mbali na Mauti isiyo na huruma. Nyote mmethibitisha kwamba yeye ni Mungu mwaminifu, na kwamba kadiri dhiki zenu zizidivyo, ndivyo na faraja zenu zizidivyo kwa Kristo Yesu!
Ombi langu, katika kulichukua andiko hili asubuhi hii, ni kwamba wafungwa wengine wa Bwana wapate kunenewa ahadi yake yenye furaha mioyoni mwao! Kwamba ninyi mliofungwa msioweza kutoka nje kwa sababu ya uzito wa roho uliopo sasa mpate kumsikia akisema, kama kwa mnong’ono mwororo masikioni mwenu na mioyoni mwenu, “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.”
Andiko hili lenyewe lajigawa katika sehemu tatu tofauti za Kweli ya Mungu. Juu ya hizi na tuseme kadiri tuwezeshwavyo na Mungu Roho Mtakatifu. Kwanza, maombi yaliyoamriwa—“Niite.” Pili, jibu lililoahidiwa—“Nami nitakuitikia.” Tatu, imani iliyotiwa moyo—“Nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.”
I. Kichwa cha kwanza ni MAOMBI YALIYOAMRIWA. Hatushauriwi na kupendekezewa tu kusali, bali twaamriwa kusali. Huku ni kujishusha kukuu. Hospitali hujengwa—yaonwa yatosha kwamba wagonjwa wapewe ruhusa ya kuingia bure watakapoitafuta. Lakini hakuna amri ya baraza itolewayo kwamba mtu ni lazima aingie malango yake. Jiko la kupikia supu huandaliwa vema wakati wa kilele cha baridi. Tangazo hutolewa kwamba walio maskini waweza kupokea chakula wakiliomba. Lakini hakuna afikiriaye kupitisha Sheria ya Bunge iwalazimishayo maskini kuja na kungoja mlangoni ili wapokee sadaka.
Yaonekana yatosha kukitoa bila kutoa amri ya aina yoyote kwamba watu wakikubali. Lakini ni ajabu kiasi gani upumbavu wa mwanadamu, kwa upande mmoja, umfanyao kuhitaji amri ili awe na huruma kwa nafsi yake mwenyewe! Na ni ajabu kiasi gani kujishusha kwa Mungu wetu mwenye neema kwa upande mwingine—kwamba hutoa amri ya upendo ambayo pasipo hiyo hakuna mwanadamu aliyezaliwa na Adamu ambaye angeshiriki karamu ya Injili, bali angependelea kufa njaa kuliko kuja! Katika jambo la maombi ndivyo hasa ilivyo. Watu wa Mungu mwenyewe wanahitaji amri ya kusali, la sivyo wasingeipokea.
Kwa nini hivi? Kwa sababu, Rafiki wapendwa, twaelekea sana kushikwa na mashambulizi ya kupenda dunia, kama kwa kweli hiyo si hali yetu ya kawaida. Hatusahau kula—hatusahau kufungua vipande vya duka—hatusahau kuwa na bidii katika biashara—hatusahau kwenda vitandani mwetu kupumzika—lakini mara nyingi twasahau kushindana na Mungu katika maombi, na kutumia, kama tupasavyo kutumia, nyakati ndefu katika ushirika uliowekwa wakfu pamoja na Baba yetu na Mungu wetu. Kwa waumini wengi mno daftari la biashara ni zito kiasi kwamba huwezi kulisogeza! Na Biblia, iwakilishayo ibada yao, ni ndogo kiasi kwamba waweza karibu kuiweka katika mfuko wa fulana yako.
Saa nyingi kwa ajili ya dunia! Dakika chache kwa ajili ya Kristo! Dunia hupata bora yetu, na chumba chetu cha maombi mabaki ya wakati wetu. Twaipa nguvu zetu na ubichi wetu njia za mamona, na uchovu wetu njia za Mungu. Kwa hiyo ndipo twahitaji kuamriwa kushughulikia tendo lilo hilo ambalo lingepasa kuwa furaha yetu kuu, kama vile lilivyo pendeleo letu la juu kuliko yote kulitenda—kukutana na Mungu wetu! “Niite,” yeye asema, kwa maana yeye ajua kwamba twaelekea kusahau kumwita Mungu.
“Wataka nini, ewe Mlala-usingizi? Ondoka, umwite Mungu wako,” ni himizo litakikanalo nasi kama vile lilivyotakikana na Yona katika dhoruba. Yeye afahamu jinsi tunavyokuwa na mioyo mizito, wakati mwingine, tukiwa chini ya hisia ya dhambi. Shetani atwambia, “Kwa nini usali? Wawezaje kutumaini kushinda? Wasema bure, 'Nitaondoka na kwenda kwa Baba yangu,' kwa maana hustahili kuwa mmoja wa watumishi wake wa mshahara! Wawezaje kuuona uso wa Mfalme baada ya kumfanyia hila? Utathubutuje kuikaribia madhabahu wakati wewe mwenyewe umeitia unajisi, na dhabihu ambayo ungeileta hapo ni chafu maskini?”
Enyi Ndugu wa kiume na wa kike, ni vema kwetu kwamba twaamriwa kusali, la sivyo katika nyakati za uzito huenda tungeacha! Mungu akiniamuru, ingawa sistahili, nitatambaa hadi kwenye kiti cha miguu cha Neema ya Kimungu. Na kwa kuwa asema, “Salini bila kukoma,” ijapokuwa maneno yananishinda na moyo wangu wenyewe utatangatanga, hata hivyo bado nitatamka kwa kigugumizi matamanio ya nafsi yangu yenye njaa na kusema, “Ee Mungu, angalau nifundishe kusali, unisaidie nishinde nawe.”
Je, hatuamriwi kusali, pia, kwa sababu ya kutokuamini kwetu kwa mara kwa mara? Kutokuamini kwanong’ona, “Kuna faida gani ukimtafuta Bwana juu ya jambo fulani na fulani? Hii ni hali iliyo nje kabisa ya orodha ya mambo yale ambayo Mungu ameingilia kati, na kwa hiyo, (asema ibilisi), kama ungekuwa katika hali nyingine yoyote ungeweza kuutegemea mkono wa Mungu wenye nguvu. Lakini hapa maombi yako hayatakufaa. Ama ni jambo dogo mno, au limehusiana mno na mambo ya wakati huu, au sivyo ni jambo ambalo umetenda dhambi mno ndani yake, au sivyo ni jambo lililo juu mno, gumu mno, lililotatanika mno—huna haki ya kulipeleka hilo mbele za Mungu!” Ndivyo apendekezavyo yule Pepo mchafu wa Jehanamu.
Kwa hiyo pameandikwa kama agizo la kila siku lifaalo kwa kila hali ambayo Mkristo aweza kutupwa ndani yake, “Niite.” “Niite. Je, u mgonjwa? Wataka kuponywa? Nililie mimi, kwa maana mimi ni Tabibu Mkuu. Je, Riziki yakusumbua? Je, unahofu kwamba hutaweza kuandaa mambo ya haki machoni pa wanadamu? Niite! Je, watoto wako wakukasirisha? Je, unahisi kile kilicho kikali kuliko jino la nyoka—mtoto asiye na shukrani? Niite! Je, huzuni zako ni ndogo, lakini zenye maumivu, kama ncha ndogo na michomo ya miiba? Niite! Je, mzigo wako ni mzito kana kwamba ungevunja mgongo wako chini ya uzito wake? Niite! Umtwike Bwana mzigo wako, naye atakutegemeza! Hatamwacha kamwe mwenye haki aondoshwe.”
Bondeni—mlimani—juu ya mwamba usio na kitu—katika bahari ya chumvi! Ukiwa umezama chini ya mawimbi na kuinuliwa punde juu ya vilele vya mawimbi—katika tanuru wakati makaa yanapowaka—katika malango ya mauti wakati mataya ya Jehanamu yangejifungia juu yako—usikome, kwa maana amri hukuambia milele, “Niite.” Maombi bado yana nguvu, na ni lazima yashinde na Mungu ili kukuletea ukombozi wako. Hizi ni baadhi ya sababu kwa nini pendeleo la kusihi katika Maandiko Matakatifu limenenwa pia kuwa ni wajibu—kuna nyingi zaidi—lakini hizi zitatosha asubuhi hii.
Hatuna budi tusiiache sehemu yetu ya kwanza hata tuwe tumetoa maelezo mengine. Yatupasa kufurahi sana kwamba Mungu ametupatia amri hii katika Neno lake ili iwe ya hakika na ya kudumu. Waweza kuyageukia mafungu hamsini ambamo agizo lilo hilo linenwa. Sisomi mara kwa mara katika Maandiko, “Usiue.” “Usitamani.” Mara mbili Sheria imetolewa, lakini mara nyingi nasoma maagizo ya Injili, kwa maana ikiwa Sheria imetolewa mara mbili, Injili imetolewa mara sabini mara saba. Kwa kila agizo nisiloweza kulishika kwa sababu ya kuwa dhaifu kwa njia ya mwili, napata maagizo elfu ambayo ni matamu na yenye kupendeza kwangu kuyashika kwa sababu ya nguvu ya Roho Mtakatifu akaaye ndani ya watoto wa Mungu!
Na amri hii ya kusali husisitizwa tena na tena. Huenda ikawa zoezi lifaalo kwa baadhi yenu kugundua ni mara ngapi katika Maandiko mnaambiwa msali. Mtashangaa kuona ni mara ngapi maneno kama haya yanatolewa—“Uniite siku ya mateso; nitakuokoa.” “Enyi watu, mimimineni mioyo yenu mbele zake.”
“Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana. Mwiteni, maadamu yu karibu.” “Ombeni, nanyi mtapewa. Tafuteni, nanyi mtaona. Bisheni, nanyi mtafunguliwa.” “Kesheni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni.” “Salini bila kukoma.” “Na tukikaribie kiti cha enzi cha neema kwa ujasiri.” “Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi.” “Dumuni katika kuomba.”
Sina haja ya kuzidisha mahali ambapo nisingeweza kamwe kumaliza. Nachagua mawili au matatu kutoka katika mfuko huu mkuu wa lulu. Njoo, Mkristo, hupaswi kamwe kutia shaka kama una haki ya kusali—hupaswi kamwe kuuliza, “Je, naruhusiwa kuja mbele za uwepo wake?” Ukiwa na amri nyingi hivyo, (na amri za Mungu zote ni ahadi na zote ni uwezeshaji), waweza kukikaribia kiti cha enzi cha neema kwa ujasiri kwa njia mpya iliyo hai kupitia pazia lililopasuka. Lakini kuna nyakati ambazo Mungu hawaamuru watu wake kusali katika Biblia tu—bali pia huwaamuru kusali moja kwa moja kwa misukumo ya Roho wake Mtakatifu.
Ninyi mjuao maisha ya ndani mnanielewa mara moja. Mnahisi ghafla, huenda katikati ya shughuli, wazo lisukumalo kwamba ni lazima mjitenge ili kusali. Yamkini hamzingatii sana mwelekeo huo mwanzoni, lakini waja tena na tena na tena—“Jitenge, ukasali!” Nagundua kwamba katika jambo la maombi mimi mwenyewe ni kama gurudumu la maji lililoendeshwa na maji, likwendalo vizuri kunapokuwa na maji tele, lakini lizungukalo kwa nguvu kidogo mno kijito kinapopungua. Au, kama meli irukayo juu ya mawimbi ikitandaza matanga yake yote upepo unapokuwa mzuri, lakini ambayo ni lazima igeuke-geuke kwa taabu nyingi kunapokuwa na kidogo tu cha upepo mwema.
Sasa yanigusa kwamba kila mara Bwana wetu akupapo mwelekeo wa pekee wa kusali, unapaswa kuongeza bidii yako maradufu. Yakupasa kusali sikuzote wala usikate tamaa—lakini akupapo shauku ya pekee ya maombi na ukahisi ustadi na furaha ya kipekee ndani yake, unayo, zaidi ya amri ile ifungayo daima, amri nyingine ipasayo kukulazimisha kwenye utii wa furaha. Nyakati kama hizo nadhani twaweza kusimama katika hali ya Daudi ambaye Bwana alimwambia, “Utakaposikia sauti ya kwenda juu ya vilele vya miforsadi, ndipo utakapojihimiza.”
Kule kwenda juu ya vilele vya miforsadi huenda kulikuwa ni nyayo za malaika waliokuwa wakiharakisha kumsaidia Daudi, na ndipo Daudi angewapiga Wafilisti. Na wakati rehema za Mungu zinapokuja, nyayo zake ni tamaa zetu za kusali. Na tamaa zetu za kusali zapaswa kuwa mara moja ni ishara kwamba wakati uliowekwa wa kuihurumia Sayuni umefika. Panda kwa wingi sasa, kwa maana waweza kupanda katika tumaini! Lima kwa furaha sasa, kwa maana mavuno yako ni ya hakika! Shindana sasa, Yakobo, kwa maana u karibu kufanywa mkuu ushindaye, na jina lako litaitwa Israeli! Sasa ndio wakati wako, enyi wafanya-biashara wa kiroho! Soko liko juu, fanyeni biashara nyingi—faida yenu itakuwa kubwa. Angalieni kwamba mnautumia vema saa ya dhahabu na kuvuna mavuno yenu jua liking’aa.
Tunapofurahia matembeleo kutoka juu twapaswa kuwa wa kudumu kwa namna ya pekee katika maombi. Na kama wajibu mwingine usio na msukumo mkubwa ungepaswa kupewa nafasi ya kwanza kwa kitambo, haitakuwa kosa nasi hatutapata hasara—kwa maana Mungu anapotuamuru kusali kwa namna ya pekee kwa maonyo ya Roho wake, ndipo twapaswa kujihimiza katika maombi.
II. Sasa na tuchukue kichwa cha pili—JIBU LILILOAHIDIWA. Hatupaswi kuvumilia hata dakika moja wazo la kutisha na la kuhuzunisha kwamba Mungu hatajibu maombi! Asili yake, kama ilivyodhihirishwa katika Kristo Yesu, yalidai hilo. Amejidhihirisha katika Injili kuwa Mungu wa upendo, ajaaye neema na kweli. Naye awezaje kukataa kuwasaidia wale viumbe vyake ambao kwa unyenyekevu, kwa njia yake mwenyewe aliyoiweka, wanautafuta uso wake na fadhili zake? Wakati baraza la wazee wa Athene pindi moja lilipoona ni afadhali kukutana pamoja hewani wazi, walipokuwa wameketi katika mashauriano yao, shomoro, akifukuzwa na mwewe, akaruka kuelekea barazani.
Akiwa amebanwa sana na ndege huyo mla-nyama, akatafuta hifadhi kifuani mwa mmoja wa wale wazee. Yeye, akiwa mtu wa tabia mbaya na ya kikatili, akamtoa yule ndege kifuani mwake, akamgonga chini na hivyo akamwua. Papo hapo baraza zima likainuka kwa ghasia na bila sauti hata moja ya kupinga, wakamhukumu afe, kwa kuwa hastahili kuwa na kiti barazani pamoja nao, wala kuitwa Mwathene, kama asingempa msaada kiumbe kilichomtumaini. Je, twaweza kudhani kwamba Mungu wa Mbinguni, ambaye asili yake ni upendo, angeng’oa kifuani mwake yule njiwa maskini apapatikaye ambaye huukimbia tai wa Haki na kuukimbilia kifua cha Rehema yake?
Je, atatupa mwaliko wa kuutafuta uso wake, na tutakapo, kama ajuavyo, kwa tetemeko kubwa la hofu, hata hivyo tukajipa ujasiri wa kutosha kuukimbilia kifua chake—je, atakuwa dhalimu na asiye na neema kiasi cha kusahau kukisikia kilio chetu na kutuitikia? Tusimfikirie kwa ukali hivyo Mungu wa Mbinguni! Na tukumbuke tena Tabia yake kuu vilevile na Asili yake. Namaanisha Tabia ile aliyojipatia kwa matendo yake ya Neema yaliyopita. Fikirini, Ndugu zangu, ile onyesho moja la ukarimu wa ajabu—kama ningetaja elfu nisingeweza kutoa kielelezo bora zaidi cha Tabia ya Mungu kuliko tendo hilo moja—“Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote.” Na si hitimisho langu tu, bali ni hitimisho lililovuviwa la Mtume—“Atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?”
Ikiwa Bwana hakukataa kuisikiliza sauti yangu nilipokuwa mwenye dhambi mwenye hatia na adui, awezaje kukipuuza kilio changu sasa, hali nimehesabiwa haki na kuokolewa? Imekuwaje kwamba aliisikia sauti ya taabu yangu wakati moyo wangu haukuijua wala haukutaka kutafuta nafuu, ikiwa baada ya yote hatanisikia sasa nilivyo mtoto wake, rafiki yake? Vidonda vitiririkavyo vya Yesu ni dhamana za hakika za maombi kuitikiwa. George Herbert aonyesha katika ule ushairi wake wa kipekee, “Mfuko,” Mwokozi akisema—
“Kama unacho cho chote cha kupeleka au kuandika (Sina mfuko, lakini hapa pana nafasi) Kwa mikono na machoni pa Baba yangu, (Niamini) kitawasili salama. Kwamba nitayazingatia uyakabidhiyo Tazama, waweza kukiweka karibu sana na Moyo wangu, Au kama baadaye yeyote wa rafiki Atanitumia kwa jinsi hii, mlango Utakuwa bado wazi; kile atumacho Nitakiwasilisha na kitu zaidi kidogo Si kwa hasara yake.”
Bila shaka, wazo la George Herbert lilikuwa kwamba Upatanisho wenyewe ulikuwa dhamana kwamba maombi ni lazima yasikiwe—kwamba lile jeraha kubwa lililotobolewa karibu na moyo wa Mwokozi lililoruhusu nuru kuingia hata vilindini mwa moyo wa Uungu—lilikuwa uthibitisho kwamba yeye aketiye Mbinguni angekisikia kilio cha watu wake! Waisoma vibaya Kalvari ikiwa wadhani kwamba maombi hayana faida. Lakini, Wapendwa, tunayo ahadi ya Bwana mwenyewe juu ya jambo hilo, naye ni Mungu asiyeweza kusema uongo—“Uniite siku ya mateso, nami nitakuitikia.” Je, hakusema, “Lo lote mtakaloliomba katika sala, aminini ya kwamba mmelipokea, nanyi mtakuwa nalo”? Kwa kweli hatuwezi kusali, tusipoiamini fundisho hili—“kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.”
Na kama tunayo swali lo lote kabisa juu ya kama maombi yetu yatasikiwa, twafanana na yeye asitasitaye—“kwa maana yeye asitasitaye ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku. Mtu huyo asidhani ya kwamba atapokea kitu kwa Bwana.” Zaidi ya hayo, si lazima, lakini bado laweza kuimarisha hoja tukiongeza kwamba uzoefu wetu wenyewe hutuongoza kuamini kwamba Mungu atajibu maombi. Sipaswi kunena kwa niaba yenu, lakini naweza kunena kwa niaba yangu mwenyewe. Kama kuna jambo lo lote nijualo, jambo lo lote nililo na hakika nalo zaidi ya shaka yote, ni kwamba pumzi ya maombi haitumiki bure kamwe. Kama hakuna mtu mwingine hapa awezaye kulisema, mimi nathubutu kulisema, nami najua kwamba naweza kulithibitisha.
Kuongoka kwangu mwenyewe ni tunda la maombi—marefu, ya upendo, ya bidii, ya kudumu. Wazazi waliniombea! Mungu alizisikia sala zao na hapa niko naihubiri Injili. Tangu wakati huo nimejaribu mambo fulani yaliyokuwa mbali zaidi ya uwezo wangu, kama nilivyodhani. Lakini sijashindwa kamwe, kwa sababu nimejitupa juu ya Bwana. Mnajua kama Kanisa kwamba sijasita kujiruhusu kuwa na mawazo makubwa ya yale tuwezayo kumfanyia Mungu. Nasi tumefanikisha yote tuliyokusudia. Nimeutafuta msaada wa Mungu na uwezeshaji na saada katika shughuli zangu zote nyingi! Na ijapokuwa siwezi kusimulia hapa hadithi ya maisha yangu ya faragha katika kazi ya Mungu, hata hivyo kama ingeandikwa ingekuwa uthibitisho udumuo kwamba yuko Mungu ajibuye maombi!
Amezisikia sala zangu, si mara moja moja, wala si mara moja au mbili, bali mara nyingi mno hata imekuwa desturi kwangu kutandaza shauri langu mbele za Mungu nikiwa na hakika kamili kwamba cho chote nimwombacho Mungu, atanipa. Sasa si “huenda,” wala si uwezekano—najua kwamba Bwana wangu ananijibu, wala sithubutu kutia shaka! Kwa hakika ingekuwa upumbavu kama ningefanya hivyo. Kama nilivyo na hakika kwamba kiasi fulani cha nguvu ya kaninya kitainua uzito, ndivyo najua kwamba kiasi fulani cha maombi kitapata cho chote kutoka kwa Mungu. Kama wingu la mvua liletavyo manyunyu, ndivyo maombi yaletavyo baraka. Kama majira ya machipuko yatawanyavyo maua, ndivyo kusihi kuhakikishavyo rehema. Katika kazi zote mna faida, lakini zaidi ya yote katika kazi ya maombezi—nina hakika ya hili—kwa maana nimeivuna.
Kama niutumainivyo fedha ya malkia nami sijashindwa kamwe kununua nikitakacho ninapotoa fedha taslimu, ndivyo naziamini ahadi za Mungu nami nakusudia kufanya hivyo hata nitakapokuta kwamba ataniambia mara moja tu kwamba ni sarafu bandia zisizofaa kufanyia biashara katika soko la Mbinguni. Lakini kwa nini niseme? Enyi Ndugu, nyote mnajua ndani ya nafsi zenu wenyewe kwamba Mungu husikia maombi! Kama hamjui, basi Ukristo wenu uko wapi? Dini yenu iko wapi? Mtahitaji kujifunza ni yapi mambo ya kwanza ya Kweli ya Mungu, kwa maana watakatifu wote, wachanga au wazee, waliweka kuwa jambo la hakika kwamba yeye husikia maombi!
Lakini, kumbuka kwamba maombi sikuzote yapasa kutolewa kwa kunyenyekea mapenzi ya Mungu. Tunaposema, “Mungu husikia maombi,” hatukusudii kwa hilo kwamba sikuzote hutupa hasa kile tuombacho. Bali twamaanisha hili—kwamba hutupa kile kilicho bora kwetu. Na kwamba kama hatutupi rehema tuiombayo kwa fedha, hututunuku kwa dhahabu. Kama hauondoi mwiba katika mwili, hata hivyo asema, “Neema yangu yakutosha,” na hilo huwa sawa mwishoni. Lord Bolingbroke alimwambia Countess wa Huntingdon, “Sielewi, Bibi mheshimiwa, jinsi uwezavyo kuonyesha kwamba maombi ya bidii yaweza kupatana na kunyenyekea mapenzi ya Kimungu.”
“Bwana wangu,” akasema, “hilo ni jambo lisilo na ugumu. Kama ningekuwa mtumishi wa mfalme fulani mkarimu naye akanipa ruhusa kumwomba fadhili yo yote nitakayo, ningehakikisha kuiweka hivi, 'Je, Mfalme atakuwa radhi kwa neema kunipa fadhili fulani na fulani—lakini wakati huohuo, ingawa naitamani sana, kama ingempunguzia Mfalme heshima yake kwa namna yo yote, au kama katika hukumu ya Mfalme ingeonekana afadhali nisiipate fadhili hii, nitaridhika vivyo hivyo kwenda pasipo hiyo kama kuipokea.' Basi waona ningeweza kutoa dua kwa bidii na hata hivyo ningeweza kwa unyenyekevu kuiacha mikononi mwa mfalme.”
Ndivyo ilivyo kwa Mungu. Kamwe hatutoi maombi bila kuingiza kifungu kile, ama katika roho au katika maneno, “Walakini, si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Mapenzi yako yatimizwe, si yangu.” Twaweza kusali pasipo neno “kama tu pale tunapokuwa na hakika kabisa kwamba mapenzi yetu ni lazima yawe mapenzi ya Mungu, kwa sababu mapenzi ya Mungu ni mapenzi yetu kikamilifu. Mshairi aliyesingiziwa sana amesema vema—“Mwanadamu, yaangalie maombi yako kama kusudi la upendo kwa nafsi yako. Iheshimu Riziki iliyoyaongoza kama kielelezo cha nia njema ya Mungu. Ndivyo utakavyosali sawasawa na maneno yako yatakubaliwa. Pia, katika kuwasihia wengine, shukuru kwa ukamilifu wa maombi yako. Kwa maana kama u tayari kuomba, Bwana yu tayari zaidi kutoa. Chumvi huihifadhi bahari, na watakatifu huitegemeza dunia. Maombi yao ndizo nguzo elfu zishikiliazo dari ya Asili.
“Amin, saa moja bila maombi, itokayo katika akili fulani ya kidunia, ingekuwa laana katika kalenda ya wakati, doa la weusi wa giza. Yamkini ile siku ya kutisha ambapo dunia ni lazima itikisike hata magofuni, itakuwa ni ile isiyong’arishwa na maombi—je, atakuta imani juu ya nchi? Kwa maana kuna uangalizi wa rehema, kama ulivyo wa hekima na nguvu na njia. Wala hakuna baraka moja itolewayo bila kuombwa kutoka katika hazina ya wema—na moyo wa ukarimu wa yule Aliyeko, ambaye kumtegemea ni furaha, hauzuii kamwe ukarimu, maadamu mtu wake asali. Naam, omba utakalo, hata kwenye kiti cha enzi cha pili Mbinguni, ni lako, kwako uliyewekewa. Hakuna kikomo cha maombi—lakini ukiacha kuomba, tetemeka, ewe kiumbe uliyejisimamisha mwenyewe, kwa maana nguvu zako zimekatwa kama zilivyokuwa za Samsoni—na saa ya maangamizi yako imefika.”
III. Nafika kwenye jambo letu la tatu, ambalo nadhani limejaa kitia-moyo kwa wale wote wanaotenda sanaa takatifu ya maombi—KITIA-MOYO KWA IMANI. “Nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.” Na tuseme tu kwamba haya yalinenwa awali kwa Nabii aliyekuwa gerezani, na kwa hiyo yanahusika, kwanza kabisa, na kila mwalimu na, kwa kweli, kwa kuwa kila mwalimu ni lazima awe mwanafunzi, yana uhusiano na kila mwanafunzi wa Kweli ya Kimungu.
Njia iliyo bora ambayo kwayo nabii na mwalimu na mwanafunzi waweza kuzijua Kweli za Mungu zilizowekwa akiba—Kweli za juu zaidi na za fumbo zaidi za Mungu—ni kwa kumngoja Mungu katika maombi. Nilitambua kwa namna ya pekee sana jana nilipokuwa nikisoma Kitabu cha Nabii Danieli, jinsi Danieli alivyoligundua ndoto ya Nebukadneza. Waaguzi, wachawi, wanajimu wa Wakaldayo walitoa vitabu vyao vya ajabu na vyombo vyao vyenye sura ya ajabu, wakaanza kunung’unika maneno yao ya uchawi na kila aina ya maombi ya kifumbo, lakini wote walishindwa.
Danieli alifanya nini? Alijiweka katika maombi, na kwa kuwa alijua kwamba maombi ya kundi la watu walioungana yana nguvu zaidi kuliko maombi ya mtu mmoja, twaona kwamba Danieli aliwaita pamoja ndugu zake na kuwaamuru waungane naye katika maombi ya bidii ili Mungu apendezwe katika rehema zake zisizo na mwisho kuufunua ule maono. “Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari Hanania, na Mishaeli, na Azaria, wenzake; ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni katika habari ya siri hiyo; Danieli na wenzake wasije wakaangamizwa pamoja na wenye hekima wengine wa Babeli.”
Na kwa habari ya Yohana, aliyekuwa Danieli wa Agano Jipya, wakumbuka aliona kitabu katika mkono wa kuume wa yeye aliyeketi juu ya Kiti cha Enzi—kitabu kilichotiwa muhuri wa mihuri saba ambacho hakuna aliyeonekana kustahili kukifungua wala kukitazama. Yohana alifanya nini? Kitabu kilifunguliwa punde na Simba wa Kabila la Yuda aliyekuwa ameshinda kukifungua kitabu. Lakini imeandikwa, kwanza, kabla kitabu hakijafunguliwa, “Nikalia sana.” Naam, na machozi ya Yohana ambayo yalikuwa maombi yake ya majimaji, yalikuwa, kwa upande wake, funguo takatifu ambazo kwazo kile kitabu kilichokunjwa kilifunguliwa.
Ndugu katika huduma, ninyi mlio walimu katika shule ya Jumapili na nyote mlio wanafunzi katika chuo cha Kristo Yesu, nawasihi kumbukeni kwamba maombi ndiyo njia yenu bora ya kujifunza—kama Danieli mtaielewa ndoto na tafsiri yake mtakapokuwa mmemtafuta Mungu. Na kama Yohana mtaiona mihuri saba ya Kweli ya thamani ya Mungu ikifunguliwa baada ya kulia sana. “Naam, ukiita busara, na kupaza sauti yako upate ufahamu; ukiutafuta kama fedha, na kuutafuta kama hazina zilizositirika: ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, na kupata kumjua Mungu.”
Mawe hayavunjwi ila kwa kutumia nyundo kwa bidii. Naye avunjaye mawe kwa kawaida hupiga magoti. Tumia nyundo ya bidii na uache magoti ya maombi nayo yatumike, wala hakuna fundisho lolote gumu kama jiwe katika Ufunuo ambalo ni la kukufaa kulielewa ambalo halitasambaratika vipande-vipande chini ya zoezi la maombi na imani. “Bene orasse est bene studuisse” lilikuwa neno la hekima la Luther ambalo limenukuliwa mara nyingi mno hata twathubutu kulidokeza tu. “Kuwa umesali vema ni kuwa umejifunza vema.”
Waweza kupenya kwa nguvu kupitia kila kitu kwa nguvu ya maombi. Mawazo na hoja yaweza kuwa kama vibanio vya chuma viwezavyo kufungua njia kuingia katika Kweli ya Mungu. Lakini maombi ndio mtambo uufunguao kwa nguvu ule sanduku la chuma la siri takatifu ili tupate kuifikia hazina iliyofichwa humo kwa ajili ya wale wawezao kupenya kwa nguvu kuifikia. Ufalme wa Mbinguni bado wapatwa na nguvu, nao wenye nguvu wauteka kwa nguvu. Angalia kwamba wafanya kazi sikuzote kwa chombo chenye nguvu cha maombi, wala hakuna kitakachoweza kusimama dhidi yako.
Lakini, hatuna budi tusiishie hapo. Tumelitumia andiko kwa hali moja tu—linaweza kutumika kwa hali mia. Twachagua nyingine. Mtakatifu aweza kutazamia kugundua uzoefu wenye kina zaidi na kujua zaidi ya maisha ya juu ya kiroho kwa kuwa mwingi katika maombi. Kuna tafsiri mbalimbali za andiko langu. Toleo moja lasema, “Nami nitakuonyesha mambo makubwa, yaliyo na ngome, usiyoyajua.” Nyingine yasoma, “Mambo makubwa yaliyowekwa akiba, usiyoyajua.” Basi maendeleo yote ya maisha ya kiroho hayapatikani kwa urahisi sawasawa. Kuna hali za kawaida na hisia za toba na imani na furaha na tumaini ambazo hufurahiwa na jamaa nzima—lakini kuna ulimwengu wa juu wa furaha kuu, wa ushirika na muungano wa fahamu na Kristo—ambao uko mbali sana na kuwa maskani ya kawaida ya Waaminio.
Waaminio wote wamwona Kristo, lakini Waaminio wote hawatii vidole vyao katika alama za misumari, wala hawatii mkono wao ubavuni mwake. Hatuna pendeleo la juu la Yohana la kuegemea kifua cha Yesu, wala la Paulo la kunyakuliwa hadi Mbingu ya tatu. Katika safina ya wokovu twapata ghorofa ya chini, ya pili na ya tatu. Wote wamo ndani ya safina, lakini wote hawamo katika ghorofa ile ile. Wakristo wengi, kwa habari ya mto wa uzoefu, wamefika vifundoni tu. Wengine wameukanyaga hata mkondo umefika magotini. Wachache wauona ukiwa kifuani. Na wachache—lo, wachache kiasi gani!—wauona kuwa mto wa kuogelea, ambao chini yake hawawezi kuufikia.
Ndugu zangu, kuna vilele katika ujuzi wa kimajaribio wa mambo ya Mungu ambavyo jicho la tai la ufahamu na fikira za kifalsafa halijawahi kuviona. Na kuna njia za siri ambazo mwana-simba wa akili na busara haujajifunza bado kuzipita. Mungu peke yake aweza kutuchukua huko, lakini gari lile analotupandisha juu, na farasi wa moto ambao kwao gari hilo huvutwa, ni MAOMBI yenye kushinda. Maombi yenye kushinda huyashinda Mungu wa Rehema. “Kwa nguvu zake alishindana na Mungu; naam, alishindana na malaika, akashinda; akalia, akamsihi; alimwona huko Betheli, na huko akasema nasi.” Maombi yenye kushinda humchukua Mkristo hadi Karmeli na kumwezesha kuzifunika Mbingu kwa mawingu ya baraka na dunia kwa mafuriko ya rehema.
Maombi yenye kushinda humwinua Mkristo juu hadi Pisga na kumwonyesha urithi uliowekwa akiba. Naam, nayo humpandisha hadi Tabori na kumgeuza sura, hata katika mfano wa Bwana wake, kama alivyo yeye, ndivyo tulivyo sisi! Katika dunia hii, kama ungetaka kufikia jambo lililo juu zaidi ya uzoefu wa kawaida wa kutambaa, mwelekee ule Mwamba ulio juu kuliko wewe, na utazame kwa jicho la imani kupitia madirisha ya maombi ya kudumu. Kukua katika uzoefu basi, ni lazima kuwe na maombi mengi.
Ni lazima muwe na saburi nami huku nikilitumia andiko hili kwa hali mbili au tatu zaidi. Ni kweli hakika kwa yule ateswaye chini ya jaribu—akimngoja Mungu katika maombi atapokea ukombozi mkubwa zaidi kuliko alivyowahi kuota— “mambo makubwa, magumu usiyoyajua.” Huu hapa ushuhuda wa Yeremia—“Ulikaribia siku ile nilipokuita; ukasema, Usiogope. Ee Bwana, umezitetea nafsi yangu; umeukomboa uhai wangu.” Na wa Daudi ni ule ule—“Nalimwita Bwana katika shida; Bwana akaniitikia, akaniweka mahali panapo nafasi... Nitakushukuru, kwa maana umeniitikia, umekuwa wokovu wangu.”
Na tena—“Ndipo walipomlilia Bwana katika dhiki zao, naye akawaokoa na shida zao. Akawaongoza kwa njia iliyonyoka, wapate kufika mji wa kukaa.” “Mume wangu amekufa,” akasema yule mwanamke maskini, “na mdai wangu amekuja kuwatwaa wanangu wawili kuwa watumwa.” Alitumaini kwamba huenda Eliya angesema, “Madeni yako ni yapi? Nitayalipa.” Badala ya hayo, akaizidisha mafuta yake hata imeandikwa, “Nenda ukalipe madeni yako, na”— lile “na” lilikuwa nini?—“ukae wewe na wanao kwa mabaki.” Mara nyingi hivyo itatokea kwamba Mungu hatawasaidia watu wake tu kupitia mahali penye matope pa njia ili wapate kusimama tu upande wa pili wa dimbwi—bali atawaleta salama mbali katika safari.
Hiyo ilikuwa miujiza ya ajabu, wakati katikati ya dhoruba, Yesu Kristo alikuja akitembea juu ya bahari! Wanafunzi wakampokea ndani ya mashua na si tu kwamba bahari ikatulia, bali imeandikwa, “Mara ile mashua ikafika nchi ile waliyokuwa wakiiendea.” Hiyo ilikuwa rehema zaidi ya vile walivyoomba. Wakati mwingine nawasikia mkisali na kutumia nukuu isiyo katika Biblia—“Yeye aweza kufanya mno ya ajabu kupita yote tuwezayo kuomba au hata kufikiri.” Haikuandikwa hivyo katika Biblia. Sijui tunaloweza kuomba au tunaloweza kufikiri. Bali imesemwa, “Yeye aweza kufanya mno ya ajabu kupita yote tuombayo au tufikiriyo.”
Basi, Rafiki wapendwa, tunapokuwa katika jaribu kuu, na tuseme tu, “Sasa nimo gerezani. Kama Yeremia nitaomba kama alivyoomba yeye, kwa maana ninayo amri ya Mungu ya kufanya hivyo. Nami nitatazamia kama yeye, nikingoja ya kuwa atanionyesha rehema zilizowekwa akiba nisizozijua kabisa sasa.” Hatawaleta watu wake kupitia vita tu, akizifunika vichwa vyao humo, bali atawaleta nje na mabango yakipepea ili kugawa nyara pamoja na wenye nguvu na kudai fungu lao pamoja na hodari! Tazamieni mambo makuu kutoka kwa Mungu atoaye ahadi kuu kama hizi!
Tena, huku hapa ni kitia-moyo kwa mfanya kazi. Wengi wenu mnamfanyia Kristo jambo fulani. Nafurahi kuweza kusema hivi, nikijua kwamba siwarairai. Rafiki zangu wapendwa, mngojeni Mungu sana katika maombi nanyi mnayo ahadi kwamba atawafanyia mambo makubwa zaidi kuliko myajuayo. Hatujui ni kiasi gani cha uwezo wa kufaa kilichomo ndani yetu. Ule mfupa wa taya wa punda ulaolala pale juu ya nchi—waweza kufanya nini? Hakuna ajuaye uwezalo kufanya. Waingia mikononi mwa Samsoni—usiloweza kufanya ni lipi? Hakuna ajuaye usiloweza kufanya sasa kwa kuwa Samsoni ndiye auushikaye! Na wewe, Rafiki, mara nyingi umejidhania kuwa wa kudharauliwa kama ule mfupa nawe umesema, “Naweza kufanya nini?” Naam, lakini Kristo, kwa Roho wake, akikushika—usiloweza kufanya ni lipi?
Kwa kweli waweza kuyatumia maneno ya Paulo na kusema, “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Lakini, usitegemee maombi bila juhudi. Katika shule fulani alikuwepo msichana mmoja aliyemjua Bwana. Alikuwa mtoto mwenye neema sana, mwenye moyo mnyofu, mwenye kuamini. Kama kawaida, Neema ya Kimungu ilijidhihirisha ndani ya mtoto kadiri ya hali ya mtoto. Masomo yake sikuzote yalisemwa vizuri kuliko ya yeyote darasani. Msichana mwingine alimwambia, “Imekuwaje masomo yako sikuzote yasemwa vizuri hivyo?” “Namwomba Mungu anisaidie,” akasema, “kujifunza somo langu.” “Vema,” akawaza yule mwingine, “basi nami nitafanya vivyo hivyo.” Asubuhi iliyofuata aliposimama darasani hakujua lolote. Na alipokuwa katika aibu akamlalamikia yule mwingine, “Nilimwomba Mungu anisaidie kujifunza somo langu wala sijui lolote juu yake. Kuna faida gani ya maombi?”
“Lakini je, uliketi ukajaribu kulijifunza?” “La, hasha,” akasema, “sikukitazama kitabu kamwe.” “Aha, basi,” akasema yule mwingine, “nilimwomba Mungu anisaidie kujifunza somo langu—lakini kisha nikaketi kulisoma kwa bidii nami nikaendelea nalo hata nikalijua vema nami nikalijifunza kwa urahisi, kwa sababu shauku yangu ya bidii, niliyokuwa nimemweleza Mungu, ilikuwa, nisaidie kuwa na bidii katika kujitahidi kutimiza wajibu wangu.” Ndivyo ilivyo kwa baadhi wafikao kwenye Mikutano ya Maombi na kusali kisha wanakunja mikono yao na kwenda zao wakitumaini kwamba kazi ya Mungu itaendelea. Kama yule mwanamke mweusi aliyeimba, “Ruka mbali, ewe Injili yenye nguvu,” lakini bila kutia hata senti sahaniani—hata rafiki yake akamgusa na kusema, “Lakini itawezaje kuruka kama hutaipa mabawa ya kurukia?”
Wako wengi waonekanao kuwa hodari sana katika maombi, wa ajabu katika kusihi! Lakini kisha wamtaka Mungu afanye yale wawezayo kufanya wenyewe na kwa hiyo Mungu hawafanyii lolote kabisa. “Nitamwacha ngamia wangu bila kufungwa,” alisema Mwarabu mmoja pindi moja kwa Mahomet, “na kuitumainia riziki.” “Mfunge,” akasema Mahomet, “kisha uitumainie riziki.” Basi ninyi msemao, “Nitasali na kuikabidhi Kanisa langu, au darasa langu, au kazi yangu kwa wema wa Mungu,” afadhali muisikie sauti ya Uzoefu na Hekima isemayo, “Fanya uwezavyo. Fanya kazi kana kwamba yote yategemea juhudi yako—kana kwamba lengo lako mwenyewe lingeleta wokovu wako. Na utakapokuwa umefanya yote, jitupe juu yake ambaye pasipo yeye ni bure kuamka mapema na kukesha hata usiku na kula chakula cha taabu. Naye akikufanikisha, mpe yeye sifa.”
Sitawachelewesha dakika nyingi zaidi, lakini nataka kuonyesha kwamba ahadi hii yapasa kuthibitika kuwa yenye faida kwa kuwafariji wale walio waombezi kwa ajili ya wengine. Ninyi mnaomwita Mungu awaokoe watoto wenu, awabariki jirani zenu, awakumbuke waume zenu au wake zenu kwa rehema mwaweza kupata faraja kutokana na hili! “Nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.” Mhudumu mmoja mashuhuri wa karne iliyopita, Bwana Bailey mmoja, alikuwa mtoto wa mama mcha-Mungu. Mama huyu alikuwa amekaribia kuacha kumwombea mume wake aliyekuwa mtu wa tabia isiyomcha Mungu kabisa na mtesaji mkali.
Mama alimwombea mtoto wake, na alipokuwa bado na umri wa miaka kumi na moja au kumi na miwili, rehema ya milele ilikutana naye. Mtoto huyo alifundishwa kwa utamu mwingi katika mambo ya ufalme wa Mungu hata mama akamwomba—naye kwa muda akafanya hivyo sikuzote—aongoze maombi ya jamaa nyumbani. Asubuhi na jioni huyu mdogo alikifungua Biblia. Na ijapokuwa baba hangekubali kusimama kwa ajili ya maombi ya jamaa, hata hivyo pindi moja alikuwa na hamu kidogo ya kujua, “ni namna gani mtoto angelimaliza jambo hilo,” hivyo akasimama upande wa pili wa mlango na Mungu akabariki maombi ya mtoto wake mwenyewe aliye chini ya miaka kumi na mitatu hata akaongoka!
Akasema mama, “Ningeweza vema kulisoma andiko langu kwa machozi yatiririkayo na kusema, 'Naam, Bwana, umenionyesha mambo makubwa, magumu nisiyoyajua! Hukumwokoa mwanangu tu, bali kupitia mwanangu umemleta mume wangu kwenye Kweli.” Huwezi kubuni jinsi Mungu atakavyokubariki sana! Nenda tu ukasimame mlangoni pake—huwezi kujua kilichowekwa akiba kwa ajili yako. Usipoomba kabisa, hutapata lolote. Lakini ukiomba huenda asikupe tu, kwa kusema, mifupa na nyama iliyobaki, bali aweza kumwambia mtumishi mezani pake, “Twaa nyama ile tamu ukamwandalie yule mtu maskini.”
Ruthu alienda kuokota. Alitazamia kupata masuke machache mazuri—lakini Boazi akasema, “Mwacheni aokote hata katikati ya miganda, wala msimkemee.” Tena akamwambia, “Wakati wa chakula njoo hapa ule mkate, ukachovye tonge lako katika siki.” Alipata mume mahali ambapo alitazamia kupata konzi ya shayiri tu. Vivyo hivyo katika kuwaombea wengine, Mungu aweza kutupa rehema kiasi kwamba tutastaajabishwa nazo kwa kuwa tulitazamia kidogo tu. Sikieni yale yaliyonenwa juu ya Ayubu, mkajifunze funzo lake, “Bwana akasema, Mtumishi wangu Ayubu atawaombeeni; kwa maana yeye nitamkubali; nisije nikawatenda sawasawa na upumbavu wenu; kwa kuwa hamkusema yaliyo sawa katika habari zangu, kama mtumishi wangu Ayubu... Bwana akaugeuza uteka wa Ayubu, alipowaombea rafiki zake; naye Bwana akamwongezea Ayubu vitu vyote alivyokuwa navyo mara mbili.”
Sasa, neno hili la kumalizia. Baadhi yenu ni watafutao kuongoka kwenu wenyewe. Mungu amewahuisha kwa maombi mazito juu ya nafsi zenu wenyewe. Hamridhiki kwenda Jehanamu. Mwataka Mbingu. Mwataka kuoshwa katika damu ya thamani—mwataka uzima wa milele. Rafiki wapendwa, nawasihi lichukueni andiko hili—Mungu mwenyewe alinena kwenu—“Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.” Mara moja mchukueni Mungu kwa Neno lake. Rudini nyumbani—ingieni chumbani mwenu na kufunga mlango na kumjaribu!
Kijana wa kiume, nasema, Mjaribu Bwana! Kijana wa kike, mthibitishe—tazama kama yeye ni kweli au sivyo! Ikiwa Mungu ni kweli, huwezi kutafuta rehema mkononi mwake kupitia Yesu Kristo na kupata jibu la kukataa. Ni lazima—kwa maana ahadi yake mwenyewe na Tabia yake vinamfunga kwa hilo—alifungue lango la Rehema kwako wewe ubishaye kwa moyo wako wote! Mungu akusaidie, ukimwamini Kristo Yesu, kumlilia Mungu kwa sauti, na jibu lake la amani liko njiani tayari kuja kukulaki! Utamsikia akisema, “Dhambi zako zilizo nyingi zimesamehewa zote.” Bwana akubariki kwa ajili ya upendo wake. Amina.
[MAELEZO—Katika hubiri iliyotangulia, tulipokuwa tukikashifu kosa la “kutoungama dhambi kwa Waaminio,” tuliwahusisha kimakosa uzushi huo mbaya na Ndugu wa Plymouth. Tangu wakati huo tumejifunza kwamba wale watu tuliowarejelea wamefukuzwa katika jumuiya hiyo na kwa hiyo twatamani kuiondolea lawama jumuiya hiyo kwa kosa ambalo hawana hatia nalo. Twasikitika kutoa shtaka hili, kwa kuwa ni mbali na nia yetu kunena vibaya juu ya yeyote, lakini hatukuwa tukijua juu ya kufukuzwa kwa wale watu wenye hatia.]