Nguvu Kuu katika Maombi ·Maombi, Dawa ya Masumbufu

Sura 12 · dakika 29 za kusoma

Maombi, Dawa ya Masumbufu

“Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu kwa njia ya Kristo Yesu.” Wafilipi 4:6, 7.

Tuna kipawa cha kufikiria mambo yajayo, lakini, kama vipawa vyetu vyote, kimepotoshwa, na mara nyingi kinatumiwa vibaya. Ni jambo jema mtu awe na uangalifu mtakatifu na kuyatilia maanani mambo yote ya maisha yake, lakini, ole, ni rahisi sana kuubadilisha uangalifu huo kuwa usumbufu usio mtakatifu na kujaribu kuinyakua kutoka mkononi mwa Mungu ile huduma ya riziki ambayo ni yake, wala si yetu. Mara ngapi Luther alipenda kuzungumza juu ya ndege na jinsi Mungu anavyowatunza! Alipojaa masumbufu yake, alikuwa akiwaonea wivu ndege daima kwa sababu waliishi maisha huru na yenye furaha kiasi hicho. Anazungumza juu ya Daktari Shomoro, Daktari Kurumbizi na wengine waliokuwa wakija kuzungumza na Daktari Luther na kumwambia mambo mengi mema! Mnajua, ndugu zangu wanaume na wanawake, ndege walioko huko nje uwanjani, wakitunzwa na Mungu, hufanikiwa kuliko sana wale wanaotunzwa na mwanadamu. Msichana mdogo wa London, aliyekuwa amekwenda mashambani, aliwahi kusema, “Tazama, mama, ndege huyo mdogo maskini. Hana tundu lo lote!” Jambo hilo lisingenionekana kuwa hasara yo yote kwa ndege huyo—na kama wewe nami tungekuwa bila tundu letu, na sanduku la mbegu, na bilauri ya maji, isingekuwa hasara kubwa kama tungeachiliwa katika uhuru wa utukufu wa maisha ya kumtegemea Mungu kwa unyenyekevu!

Ni tundu lile la tumaini la kimwili na sanduku lile la mbegu ambalo tunajitaabisha daima kulijaza, ndilo lifanyalo wasiwasi wa maisha haya ya kufa. Lakini yeye aliye na neema ya kukunjua mabawa yake na kuruka mbali—na kuingia katika uwanja wazi wa kumtumaini Mungu—aweza kuimba mchana kutwa na kuwa daima na wimbo huu—

“Ewe mwanadamu, acha taabu na huzuni; Mungu huandaa kwa ajili ya kesho.”

Basi, hapa ndipo fundisho la andiko—“Msijisumbue kwa neno lo lote.” Neno hili, “kujisumbua,” katika lugha ya kale halikumaanisha sawasawa kama linavyomaanisha leo. Angalau linanibebea maana tofauti na ile waliyokuwa nayo wale waliolitafsiri. Ningesema kwamba yatupasa kuwa waangalifu. “Kuwa mwangalifu” ni somo jema kwa vijana na watu wachanga wanapoanza maisha, lakini, kwa maana ile ambayo neno “kujaa masumbufu” lilieleweka wakati wa watafsiri, hatupaswi kujisumbua, yaani, kujaa masumbufu. Andiko lamaanisha, msiwe na wasiwasi—msifikiri daima juu ya mahitaji ya maisha haya ya kufa. Nitalisoma tena, nikilinyoosha neno kidogo, ndipo mtaipata maana yake—“Msijaze masumbufu kwa neno lo lote.” Laiti Mungu angetufundisha jinsi ya kuepuka uovu uliokatazwa hapa, na kuishi kwa ule utulivu mtakatifu ulio uzuri hasa wa maisha ya Kikristo—wakati masumbufu yetu yote yametupwa kwa Mungu, nasi twaweza kufurahi na kushangilia katika uangalizi wake wa riziki juu yetu!

“Ee,” mtu fulani asema, “siwezi kuacha kujisumbua.” Basi, somo la usiku huu ni kukusaidia uache kujisumbua au kuwa na wasiwasi na, kwanza, fikiri, hapa, mbadala wa masumbufu. Msijisumbue kwa neno lo lote, bali salini kwa kila neno—huo ndio mbadala wa masumbufu, “kusali na kuomba.” Pili, angalia tabia ya pekee ya maombi haya yatakayokuwa mbadala wa wasiwasi—“Katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Kisha nataraji tutabaki na dakika chache za kufikiri athari tamu ya maombi haya—“Amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu kwa njia ya Kristo Yesu.”

I. Basi, kuanza, hapa ndipo, kwanza, MBADALA WA MASUMBUFU AU WASIWASI.

Nadhani ni kweli kwa wengi wetu kwamba masumbufu yetu ni mengi. Ukishakuwa mwenye kujisumbua, mwenye wasiwasi, mwenye kunung'unika, hutaweza kamwe kuyahesabu masumbufu yako, ijapokuwa waweza kuzihesabu nywele za kichwa chako. Na masumbufu huelekea kuongezeka kwa

wale walio na masumbufu tele na utakapokuwa umejaa masumbufu kadiri uwezavyo kufikiri, ni hakika utakuwa na mavuno mengine ya masumbufu yakiota pande zote kukuzunguka. Kujiachilia katika tabia hii mbaya ya wasiwasi hupelekea wasiwasi kutawala maisha, hata maisha yasistahili kuishiwa kwa sababu ya masumbufu tuliyo nayo juu yake. Masumbufu ni mengi na, kwa hiyo, maombi yenu na yawe mengi vilevile. Geuza kila lililo sumbufu liwe ombi. Masumbufu yenu na yawe malighafi ya maombi yenu na, kama vile wataalamu wa kale walivyotumaini kugeuza takataka kuwa dhahabu, ndivyo nawe, kwa ustadi mtakatifu, wageuza kweli lile ambalo kwa asili lingekuwa sumbufu liwe hazina ya kiroho katika umbo la ombi! Batiza kila wasiwasi katika jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu—na hivyo ulifanye kuwa baraka!

Je, una sumbufu la kupata? Jihadhari lisije likakupata wewe! Je, wataka kupata faida? Angalia usije ukapoteza zaidi ya unavyopata kwa faida zako. Nakusihi, usiwe na sumbufu la kupata zaidi ya lile uthubutulo kuligeuza kuwa ombi! Usitamani kuwa na kile usichothubutu kumwomba Mungu akupe. Pima tamaa zako kwa kipimo cha kiroho nawe hivyo utahifadhiwa na kila kitu kama tamaa mbaya. Masumbufu huwajia wengi kutokana na hasara zao—hupoteza walichokipata. Naam, huu ni ulimwengu ambao ndani yake kuna mwelekeo wa kupoteza. Maji hupwa baada ya kujaa na majira ya baridi huponda maua ya kiangazi. Usistaajabu ukipoteza kama watu wengine wapotezavyo, bali omba juu ya hasara zako. Enenda kwa Mungu nazo—na badala ya kunung'unika, zifanye kuwa nafasi ya kumngoja Bwana na kusema—“Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na lihimidiwe. Nionyeshe ni kwa nini unashindana nami, na umwokoe mtumishi wako, nakusihi, nisije nikakulalamikia kamwe, lo lote utakaloniruhusu kupoteza!”

Labda wasema kwamba sumbufu lako halihusu kupata wala kupoteza, bali chakula chako cha kila siku. Ee, basi, una ahadi kwa ajili ya hilo, wajua! Bwana amesema, “Nawe utakaa katika nchi, na kwa hakika utalishwa.” Anakupa faraja tamu asemapo kwamba huyavika majani ya kondeni—je, hatawavika ninyi zaidi sana, enyi wa imani haba? Na Bwana Yesu anakuagiza uwaangalie ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani, na Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Basi, enenda kwa Mungu wako na masumbufu yako yote! Kama una jamaa kubwa, mapato haba na taabu nyingi kuunganisha ncha mbili, na kuandaa mambo ya adili machoni pa watu wote, una visababu vingi vya kubisha hodi mlangoni pa Mungu—sababu nyingi zaidi za kuonekana mara kwa mara katika kiti cha enzi cha neema! Nakusihi, uvitumie kwa faida. Najihisi huru kumwendea rafiki ninapokuwa kweli na shughuli naye—nawe waweza kuwa na ujasiri wa kumwendea Mungu wakati mahitaji yanapokusonga. Badala ya kujisumbua kwa jambo lo lote kwa wasiwasi, ligeuze mara moja liwe sababu ya kusali upya.

“Ee,” mmoja asema, “lakini nimechanganyikiwa. Sijui nifanye nini.” Basi, ndugu mpendwa, hakika yakupasa kusali usipoweza kutambua kama ni njia ya mkono wa kuume, au ya kushoto, au kwenda moja kwa moja, au kama yakupasa kurudi nyuma! Naam, ukiwa katika ukungu mzito hata usiweze kuiona taa iliyo karibu, ndipo wakati wa kusali. Njia itakuwa wazi mbele yako ghafula. Mara nyingi imenibidi kujaribu mpango huu mwenyewe—nami nashuhudia kwamba nilipojitegemea mwenyewe, nilikuwa mpumbavu mkubwa mno! Lakini nilipomtumaini Mungu, ndipo aliponiongoza moja kwa moja katika njia iliyo sawa, wala hapakuwa na kosa lo lote! Naamini kwamba watoto wa Mungu mara nyingi hukosea zaidi katika mambo rahisi kuliko katika mambo magumu. Mnajua ilivyokuwa kwa Israeli, wale Wagibeoni walipokuja, na viatu na mavazi yao ya kuukuu, na kuonyesha mkate uliokuwa na ukungu, waliousema waliutwaa mbichi kutoka matanuru yao. Wana wa Israeli walidhani, “Jambo hili liko wazi. Watu hawa ni wageni, wametoka nchi ya mbali, basi twaweza kufanya agano nao.” Walikuwa na hakika kwamba ushahidi wa macho yao ulithibitisha kuwa hawa si Wakanaani, kwa hiyo hawakutaka shauri kwa Mungu! Jambo lote lilionekana wazi kiasi hata wakafanya agano na Wagibeoni, jambo lililokuwa taabu kwao daima baadaye! Kama tungependa, katika kila neno, kumwendea Mungu kwa maombi, machanganyiko yetu yasingetuingiza katika makosa zaidi ya yale ya urahisi wetu—na katika mambo rahisi na magumu tungeongozwa na Aliye Juu.

Labda rafiki mwingine asema, “Lakini ninafikiri juu ya wakati ujao.” Ndivyo? Basi, kwanza, naomba nikuulize una uhusiano gani na wakati ujao? Wajua siku moja itazaa nini? Umekuwa ukifikiri utakavyokuwa utakapokuwa mzee, lakini una hakika kwamba utawahi kuwa mzee? Nilimjua mwanamke mmoja Mkristo aliyekuwa akijisumbua juu ya jinsi atakavyozikwa. Swali hilo halikunisumbua kamwe na kuna mambo mengine mengi ambayo hatuna haja ya kujisumbua juu yake. Sikuzote waweza kupata fimbo ya kumpiga mbwa na, ukihitaji sumbufu, kwa kawaida waweza kupata sumbufu la kuzipiga roho zenu wenyewe! Lakini hiyo ni kazi duni kwa ye yote wenu. Badala ya kufanya hivyo, geuza kila lililoweza kuwa jambo la masumbufu liwe jambo la maombi. Haitakuwa muda mrefu kabla ya kuwa na jambo la masumbufu, kwa hiyo hutakaa muda mrefu bila jambo la maombi. Lifute neno lile, “masumbufu,” na uandike tu mahali pake neno hili, “maombi”—ndipo, ijapokuwa masumbufu yako ni mengi, maombi yako nayo yatakuwa mengi.

Angalia, tena, ndugu wapendwa, kwamba masumbufu yasiyofaa ni kuingilia mamlaka ya Mungu. Ni kujifanya wewe baba wa nyumba badala ya kuwa mtoto—ni kujifanya wewe bwana badala ya kuwa mtumishi ambaye bwana wake humpa posho lake. Basi, kama, badala ya kufanya hivyo, utageuza masumbufu kuwa maombi, hapatakuwa na kuingilia, kwa maana waweza kumwendea Mungu kwa maombi bila kushtakiwa kwa kujidai. Yeye anakualika usali. La, hapa, kwa mtumishi wake, anakuagiza, “katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Tena, masumbufu hayatufai kitu, nayo hutuletea hasara kubwa. Kama ungejisumbua muda utakao, hungeweza kujiongezea hata inchi moja kimo, wala kuota unywele mwingine kichwani mwako, wala kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi! Ndivyo Mwokozi atuambiavyo naye auliza, ikiwa masumbufu yanashindwa katika mambo madogo kama hayo, masumbufu yaweza kufanya nini katika mambo makubwa zaidi ya riziki? Hayawezi kufanya lo lote! Mkulima mmoja alisimama shambani mwake na kusema, “Sijui litakalotupata sisi sote. Ngano itaharibika kama mvua hii itaendelea. Hatutakuwa na mavuno yo yote isipokuwa tupate hali ya hewa nzuri.” Alitembea huku na huku, akikung'uta mikono yake, akijisumbua na kuifanya nyumba yake yote isiwe na raha. Wala hakutoa hata mwanga mmoja wa jua kwa wasiwasi wake wote—hakuweza kupeperusha lo lote la mawingu kwa maneno yake yote ya uchungu, wala hakuweza kuzuia tone moja la mvua kwa manung'uniko yake yote.

Basi, kuna faida gani kuendelea kuutafuna moyo wako mwenyewe, hali huwezi kupata kitu kwa hilo? Zaidi ya hayo, kunadhoofisha uwezo wetu wa kujisaidia na hasa uwezo wetu wa kumtukuza Mungu. Moyo uliojaa masumbufu hutuzuia tusihukumu sawasawa katika mambo mengi. Mara nyingi nimetumia mfano huu (sijui ulio bora zaidi) wa kutwaa darubini, tukiipulizia pumzi ya moto ya wasiwasi wetu, tukiiweka jichoni petu kisha tukisema kwamba hatuwezi kuona kitu ila mawingu! Bila shaka hatuwezi, wala hatutaweza kamwe maadamu tunaipulizia. Kama tungekuwa watulivu, wenye amani, wenye kujimiliki na wenye kumilikiwa na Mungu, tungefanya jambo lililo sawa. Tungekuwa, kama tusemavyo, “makini kabisa,” wakati wa taabu. Mtu aliye na Uwepo wa Mungu aweza kutazamia kuwa na utimamu wa akili. Tukisahau kusali, je, wastaajabu kwamba sote tunapapatika na kujisumbua, nasi tunafanya jambo la kwanza lijalo akilini mwetu—ambalo kwa kawaida ni jambo baya kuliko yote—badala ya kungoja hata tuone litakalofanyika kisha tulifanye kwa kutumaini na kuamini kama mbele za Mungu? Masumbufu, au wasiwasi, ni yenye kudhuru, lakini ukigeuza tu masumbufu haya kuwa maombi, ndipo kila wasiwasi utakuwa faida kwako.

Maombi ni malighafi ya ajabu ya kujenga jengo la kiroho. Sisi wenyewe twajengwa kwa maombi. Twakua katika neema kwa maombi na kama tutamwendea Mungu kila dakika kwa dua, tutakuwa Wakristo wanaokua haraka! Nilimwambia mtu mmoja asubuhi hii, “Niombee, ni wakati wa haja,” naye akajibu, “Sikufanya jambo jingine tangu nilipoamka.” Nimewaomba wengine kadhaa vivyo hivyo nao wamesema wamekuwa wakiniombea. Nilifurahi sana, si kwa ajili yangu tu, mimi niliyepata faida kutoka maombi yao, bali kwa ajili yao, kwa sababu ni hakika watakua kwa hilo! Ndege wadogo wanapoendelea kupapatika mabawa yao, wanajifunza kuruka. Mishipa itakuwa na nguvu zaidi na ndege wataondoka kiotani karibuni. Kupapatika huko kwa mabawa yao ni mafunzo—na kujaribu kusali—kuugua, kuhema, kulia kwa roho yenye maombi, ndiko, chenyewe, baraka! Basi, acha tabia hii yenye kudhuru ya wasiwasi na uishike tabia hii yenye kutajirisha ya maombi! Tazama jinsi utakavyopata faida maradufu—kwanza, kwa kuepuka hasara, na pili, kwa kupata kile kitakachokufaidi wewe na wengine pia!

Tena, masumbufu ni matokeo ya kusahau ukaribu wa Kristo kwetu. Je, mliona jinsi maneno yanayozunguka andiko yasemavyo? “Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote.” Bwana Yesu Kristo ameahidi kuja tena naye aweza kuja usiku huu. Wakati wo wote aweza kutokea! Basi Paulo aandika, “Bwana yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Ee, laiti tungeweza kusimama juu ya nchi hii kama juu ya kivuli kitupu! Laiti tungeweza kuishi kama wale watakaomaliza karibuni maisha haya maskini yapitayo! Kama tungeshika kila kitu cha dunia kwa mkono uliolegea sana, ndipo tusingejisumbua, wala kuwa na wasiwasi, wala kunung'unika—bali tungeanza kusali, kwa maana hivyo tungeushika ulio halisi, na ulio imara, na kukanyaga miguu yetu juu ya usioonekana, ambao, hatimaye, ni wa milele! Ee, ndugu wapendwa, andiko hili, ambalo nimewasomea tena na tena, sasa na lidondoke mioyoni mwenu kama changarawe iangukavyo katika ziwa la mlimani na, liingiapo, na lifanye miduara ya faraja juu ya uso wenyewe wa nafsi yenu!

II. Sasa yatupasa kuliangalia andiko kwa ukaribu zaidi kidogo ili tuone, mahali pa pili, TABIA YA PEKEE YA MAOMBI HAYA. Ni maombi ya namna gani yatakayotupunguzia masumbufu?

Basi, kwanza, ni maombi yanayohusu kila kitu. “Katika kila neno” “haja zenu na zijulikane na Mungu.” Waweza kusali juu ya jambo dogo kuliko yote na juu ya jambo kubwa kuliko yote—waweza kusali si kwa ajili ya Roho Mtakatifu tu, bali waweza kusali kwa ajili ya jozi mpya ya viatu. Waweza kumwendea Mungu juu ya mkate ulao, maji unywayo, vazi uvaalo na kumwomba juu ya kila kitu. Usiweke mstari useme, “Hata hapa ndipo iwe chini ya uangalizi wa Mungu.” Lo, basi, utafanya nini na sehemu iliyobaki ya maisha? Je, hiyo iishiwe chini ya donda-ndugu la aina fulani ya kutokumcha Mungu? La hasha! Ee, laiti tungeishi ndani ya Mungu kwa habari ya nafsi yetu yote, kwa maana nafsi yetu ni namna ambayo hatuwezi kuigawanya! Mwili wetu, roho na nafsi ni kitu kimoja, na maadamu Mungu anatuacha katika ulimwengu huu nasi tuna mahitaji yatokanayo na hali ya miili yetu,

yatupasa kuyaleta mahitaji ya miili yetu mbele za Mungu kwa maombi. Nawe utaona kwamba Mungu mkuu atakusikia katika mambo haya. Usiseme kwamba ni madogo mno hata asiyaangalie—kila kitu ni kidogo kikilinganishwa naye! Nifikiripo jinsi alivyo Mungu mkuu, yaonekana kwangu kwamba ulimwengu huu wetu mdogo maskini ni chembe moja tu isiyo na maana ya mchanga ufuoni pa ulimwengu wote—wala haustahili kuangaliwa kamwe. Dunia yote ni kidoto tu katika ulimwengu mkuu wa Uumbaji na, ikiwa Mungu anajishusha kuiangalia, aweza vilevile kuinama chini kidogo zaidi na kutuangalia sisi! Naye hufanya hivyo, kwa maana asema, “Hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.” Kwa hiyo, katika kila neno haja zenu na zijulikane na Mungu.

Namna ya maombi yatuokoayo na masumbufu ni maombi yanayorudiwarudiwa—“Katika kila neno kwa kusali na kuomba.” Mwombe Mungu kisha uombe tena—“kwa kusali na kuomba.” Kama Bwana hakujibu mara ya kwanza, uwe na shukrani nyingi kwamba una sababu njema ya kusali tena! Kama hakukujalia haja yako mara ya pili, amini kwamba anakupenda sana hata anataka kuisikia sauti yako tena! Na kama akikuweka ungoje hata umemwendea mara saba, jiambie mwenyewe, “Sasa najua kwamba namwabudu Mungu wa Eliya, kwa maana Mungu wa Eliya alimwacha aende, tena, mara saba kabla ya baraka kutolewa.” Ihesabu kuwa heshima kuruhusiwa kushindana na Malaika wa Mungu! Ndivyo Mungu awafanyavyo wakuu wake! Yakobo asingekuwa Israeli kamwe kama angepata baraka kutoka kwa Malaika kwa kuomba mara ya kwanza—bali ilipombidi kuendelea kushindana hata akashinda, ndipo alipokuwa mkuu pamoja na Mungu! Maombi yaangamizayo masumbufu ni maombi yanayoendelea na kudumu.

Tena, ni maombi yenye akili—“Haja zenu na zijulikane na Mungu.” Nilisikia habari za Mwislamu aliyetumia, nadhani, saa sita katika maombi kila siku na, ili asije akalala alipokuwa melini, alisimama wima na akawa na kamba tu iliyotandwa mbele, ili aweze kuiegemea. Naye akilala, angeanguka. Nia yake ilikuwa kuendelea saa sita na kile alichokiita maombi. “Basi,” nilimwuliza mmoja aliyemjua, na aliyekuwa amemwona melini mwake mtoni Nile, “Yalikuwa maombi ya namna gani?” “Kumbe,” rafiki yangu akajibu, “aliendelea kurudia, 'Hakuna mungu ila Mungu, na Muhammadi ni nabii wa Mungu,' jambo lilo hilo tena, na tena, na tena.” Nikasema, “Je, aliomba kitu?” “La, hasha!” “Je, alikuwa akimsihi Mungu ampe kitu?” “La, aliendelea tu na kurudiarudia huko kwa maneno fulani, kama vile mchawi awezavyo kurudia uganga.”

Je, wadhani kuna kitu katika namna hiyo ya kusali? Ukipiga magoti na kurudia tu kanuni fulani, itakuwa mdomo tu wa maneno. Mungu ana shughuli gani na maombi ya namna hiyo? “Haja zenu na zijulikane na Mungu.” Hayo ndiyo maombi ya kweli! Mungu anajua haja zenu ni nini, lakini yakupasa kumwomba kana kwamba hajui. Yakupasa kuzijulisha haja zako, si kwa sababu Bwana hajui, bali, labda, kwa sababu wewe hujui. Nawe utakapokuwa umezijulisha haja zako kwake, kama andiko likuambiavyo, utakuwa umezijulisha waziwazi zaidi kwako mwenyewe. Utakapokuwa umeomba kwa akili, ukijua ulichokiomba, na kujua kwa nini umekiomba, labda utasimama na kujiambia mwenyewe, “La, sitaomba haja hiyo baada ya yote.” Nyakati fulani, utakapoendelea kusali kwa kile Mungu asichokupa, yaweza kuwa itaingia moyoni mwako hakika kwamba huko katika njia iliyo sawa na tokeo hilo la maombi yako litakufaidi, lenyewe, na kuwa baraka kwako.

Lakini yakupasa kusali huku ukizijulisha haja zako kwa Mungu. Yaani, kwa maneno ya wazi, sema unachohitaji, kwa maana haya ndiyo maombi ya kweli. Jitenge peke yako na umwambie Bwana unachohitaji—mimina moyo wako mbele zake. Usidhani kwamba Mungu anahitaji lugha yo yote nzuri! La, huna haja ya kukimbilia juu ghorofani kuchukua kitabu chako cha maombi, na kufungua sala iliyoandikwa—utakaa muda mrefu kabla ya kupata sala iliyoandikwa itakayokufaa kama unaomba kweli! Omba unachohitaji kama vile ungemwambia mama yako au rafiki yako mpendwa kuliko wote haja yako. Mwendee Mungu kwa namna hiyo, kwa maana hayo ndiyo maombi halisi, na hiyo ndiyo namna ya maombi yatakayoyafukuza masumbufu yako.

Basi, ndugu wapendwa, tena, namna ya maombi yaletayo uhuru toka masumbufu ni ushirika na Mungu. Kama hujasema na Mungu, hujaomba kweli. Mtoto mdogo amejulikana (nadhani watoto wenu wamefanya hivyo) kwenda na kuweka barua chini kwenye wavu wa mfereji wa maji na, bila shaka, hapakuwa kamwe na jibu la barua iliyotumwa namna hiyo. Kama barua haiwekwi katika sanduku la posta, ili imwendee yule iliyoandikwa kwake, ina faida gani? Vivyo hivyo, maombi ni mawasiliano halisi na Mungu. Yakupasa kutambua kwamba yeye yuko na kwamba yeye ni mwenye kuwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii, ama sivyo huwezi kusali. Yampasa kuwa halisi kwako, halisi aliye hai, nawe wapaswa kuamini kwamba yeye husikia maombi, kisha yakupasa kusema naye na kuamini kwamba umeipata haja uiombayo kwake—na hivyo utaipata. Hajawahi kamwe kushindwa kuyaheshimu maombi ya imani. Aweza kukuweka ungoje kwa muda, lakini kukawia si kukataa, naye mara nyingi amejibu ombi lililoomba fedha kwa kutoa dhahabu! Aweza kuwa amekataa hazina ya kidunia, lakini ametoa utajiri wa mbinguni wa thamani mara elfu kumi zaidi—na mwombaji ameridhika kupita kiasi kwa badiliko hilo! “Haja zenu na zijulikane na Mungu.”

Najua ufanyalo unapokuwa katika taabu—wamwendea jirani yako, lakini jirani yako hataki kukuona mara nyingi hivyo kwa shughuli kama hizo. Yamkini wamwendea ndugu yako, lakini kuna andiko likuonyalo usiingie nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako. Waweza kumwendea rafiki mara nyingi mno unapokuwa na dhiki—aweza kufurahi sana kukuona hata asikiapo unalolitaka! Lakini ukimwendea Mungu wako, hatakupa kamwe uso wa baridi. Hatasema kamwe kwamba waja mara nyingi mno. Kinyume chake, atakukemea hata kwa sababu humwendei mara nyingi vya kutosha!

Kuna neno moja nililoliruka, sasa hivi, kwa sababu nilitaka kuliacha kwa maelezo yangu ya mwisho juu ya jambo hili—“Kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Basi hilo lamaanisha nini? Lamaanisha kwamba namna ya maombi yaangamizayo masumbufu ni maombi yaombayo kwa uchangamfu, kwa furaha, kwa shukrani. “Bwana, mimi ni maskini. Niache nikuhimidi kwa ajili ya umaskini wangu kisha, Ee Bwana, je, hutanijazia mahitaji yangu yote?” Hiyo ndiyo namna ya kusali. “Bwana, mimi ni mgonjwa. Nakuhimidi kwa mateso haya, kwa maana nina hakika yana maana ya jambo jema kwangu. Sasa uridhie kuniponya, nakusihi!” “Bwana, mimi ni katika taabu kubwa, lakini nakusifu kwa ajili ya taabu, kwa maana najua ina baraka ndani yake ijapokuwa bahasha ina ukingo mweusi! Bwana, nisaidie nipite katika taabu yangu!” Hiyo ndiyo namna ya maombi yaangamizayo masumbufu—“kuomba, pamoja na kushukuru.” Changanya vitu hivi viwili vyema! Kipimo kimoja—la, vipimo viwili vya maombi—kusali na kuomba, kisha kipimo kimoja cha kushukuru! Visugue pamoja navyo vitakuwa dawa ya baraka ya masumbufu. Bwana na atufundishe kuufanya ustadi huu mtakatifu wa mfamasia!

III. Namalizia kwa jambo hili la tatu, ATHARI TAMU YA MAOMBI HAYA—“Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu kwa njia ya Kristo Yesu.”

Kama ukiweza kusali kwa namna hii, badala ya kujiachilia katika wasiwasi mbaya, tokeo litakuwa kwamba amani isiyo ya kawaida itaingia moyoni na nia yako. Isiyo ya kawaida, kwa maana itakuwa “amani ya Mungu.” Amani ya Mungu ni nini? Ni utulivu usiotibuliwa wa Mungu aliye na furaha isiyo na mwisho, ni ukimya wa milele wa Mungu aliyeridhika kabisa! Hii itaumiliki moyo na nia yako. Angalia jinsi Paulo aielezavyo—“Amani ya Mungu, ipitayo akili zote.” Watu wengine hawataielewa. Hawataweza kufahamu jinsi uwezavyo kuwa mtulivu hivyo. Zaidi ya hayo, hutaweza kuwaeleza, kwa maana kama inapita akili zote, kwa hakika inapita usemi wote! Na lililo la ajabu zaidi—wewe mwenyewe hutaielewa!

Itakuwa amani ambayo kwako haitapimika wala kupimwa kina chake. Mmoja wa mashahidi alipokaribia kuchomwa moto kwa ajili ya Kristo, alimwambia hakimu aliyekuwa akiamuru kuwasha rundo, “Je, utakuja kuweka mkono wako juu ya moyo wangu? “Hakimu akafanya hivyo. “Je, unapiga kwa haraka?” akauliza shahidi. “Je, ninaonyesha dalili yo yote ya hofu?” “La,” akasema hakimu. “Sasa weka mkono wako juu ya moyo wako mwenyewe uone kama wewe si mwenye mshtuko zaidi yangu.” Mfikirie mtu huyo wa Mungu, ambaye, asubuhi ile aliyopaswa kuchomwa moto, alikuwa amelala usingizi mzito hata ilibidi wamtikise ili wamwamshe—ilimbidi aamke ili achomwe moto! Na ijapokuwa alijua kwamba ndivyo itakavyokuwa, alikuwa na tumaini kubwa hivyo katika Mungu hata akalala usingizi mtamu. Hii ndiyo “amani ya Mungu, ipitayo akili zote.” Katika mateso yale ya kale ya Diokletiani, mashahidi walipoingia uwanjani ili wararuliwe na wanyama wakali—mmoja alipowekwa katika kiti cha chuma chekundu cha moto, mwingine alipopakwa asali ili aumwe hata afe na nyigu na nyuki—hawakutetemeka kamwe!

Mfikirie mtu huyo hodari aliyewekwa juu ya chuma cha kuchomea ili aokwe hata afe, aliyewaambia watesi wake, “Mmeniiva upande mmoja. Sasa nigeuzeni upande wa pili.” Kwa nini amani hii katika hali kama hizo? Ilikuwa “amani ya Mungu, ipitayo akili zote.” Hatuna lazima ya kuteseka namna hiyo, siku hizi, lakini kama ikiwahi kufikia jambo kama hilo, ni ajabu amani ambayo Mkristo huifurahia! Baada ya kuwako dhoruba kuu, Bwana alisimama katika omo la chombo na kuiambia pepo, “Nyamaza, utulie.” Nasi twasoma, “kukawa shwari kuu.” Je, umewahi kuhisi hili? Utalihisi usiku huu kama umejifunza ustadi huu mtakatifu wa kuzijulisha haja zako kwa Mungu katika kila neno na amani ya Mungu ipitayo akili zote inahifadhi mioyo yenu na nia zenu kwa njia ya Kristo Yesu.

Amani hii ya baraka huhifadhi mioyo na nia zetu—ni amani yenye kulinda. Neno la Kiyunani ladokeza jeshi la ulinzi. Je, si jambo la ajabu kwamba neno la kijeshi limetumika hapa na kwamba ni amani inayotenda kama mlinzi wa moyo na nia? Ni amani ya Mungu itakayomlinda mtoto wa Mungu—mfano wa ajabu lakini mzuri! Nimesikia kwamba hofu ndiye mtunza-nyumba wa Mkristo. Basi, hofu yaweza kuwa mlinzi mzuri wa kuzuia mbwa wasiingie, lakini haina kabati lililojaa! Bali amani, ijapoonekana udhaifu, ndiyo asili ya nguvu na, iwapo inalinda, pia inatulisha na kutujazia mahitaji yetu yote.

Pia ni amani inayotuunganisha na Yesu—“Amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu.” Yaani, hisia zenu na mawazo yenu, tamaa zenu na akili zenu—moyo wenu—ili usiogope.

Nia yenu, ili isijue namna yo yote ya mchanganyiko—“amani ya Mungu itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu kwa njia ya Kristo Yesu.” Yote ni, “kwa njia ya Kristo Yesu” na, kwa hiyo, ni tamu na ya thamani maradufu kwetu!

Ee wasikilizaji wangu wapendwa, baadhi yenu mnaingia humu usiku wa Alhamisi nanyi hamjui lo lote juu ya amani hii ya Mungu na, labda, mnashangaa kwa nini sisi watu wa Kikristo tunaifanyia dini yetu fujo kiasi hicho! Ee, kama mngejua, labda, mngeifanyia fujo zaidi kuliko sisi, kwa maana kama kusingekuwa na uzima ujao—nasi twajua kwamba upo—hata hivyo tabia ile ya baraka ya kumwendea Mungu kwa maombi na kumtwika masumbufu yetu yote hutusaidia kuishi kwa furaha kuu, hata katika maisha haya! Hatuamini katika mambo ya kidunia peke yake, lakini kama tungeamini, kusingekuwa na maandalizi ya maisha ya kidunia kama haya ya kuishi kwa ajili ya Mungu na kuishi ndani ya Mungu! Kama una mungu wa uongo nawe waenda tu Kanisani au Kikanisani na kuchukua kitabu chako cha maombi au kitabu chako cha nyimbo, na, kwa hiyo, wadhani u Mkristo, unajidanganya mwenyewe! Lakini kama una Mungu aliye hai nawe una ushirika halisi naye na daima, kama desturi, waishi chini ya kivuli cha mabawa ya Mwenyezi, ndipo utafurahia amani itakayowastaajabisha wengine na kukufanya wewe mwenyewe ushangae pia, naam, “amani ya Mungu, ipitayo akili zote.” Mungu na akujalie, wasikilizaji wangu wapendwa, kwa ajili ya Kristo! Amina.

MAELEZO NA C. H. SPURGEON: Wafilipi 4

Mstari 1. Basi, ndugu zangu wapendwa na kutamaniwa, furaha yangu na taji yangu, simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu. Mnajua kwamba Kanisa la Filipi lilikuwa la thamani sana moyoni mwa Mtume. Hangeweza kamwe kusahau wakati ule alipomwomba Mungu pamoja na Sila na wale wanawake kando ya mto na baadaye walipoomba na kuimba sifa kwa Mungu gerezani, wafungwa walipowasikia. Lidia na nyumba yake na yule mlinzi wa gereza wa Filipi walikuwa miongoni mwa malimbuko ya kazi ya Paulo huko Filipi na sikuzote kulikuwa na upendo wa ndani sana kati yake na washirika wa Kanisa mahali pale. Wao walimjali naye aliwajali. Mara mbili katika mstari huu mmoja awaita “wapendwa.” Asema kwamba “aliwatamani, alitamani kuja kuwaona uso kwa uso, alitamani wawe na furaha katika Bwana kwa daraja lililo juu kabisa. Basi asema, “ndugu zangu wapendwa na kutamaniwa, furaha yangu.” Ilikuwa furaha kwake, hata, kuwafikiri kama watoto wake wa kiroho na hasa kuona jinsi walivyojiendesha kwa namna ya utauwa na ukarimu. Naam, na anawaita “taji” yake—shada alilolishinda katika mashindano ya kiroho! Waongofu wa Mkristo ni furaha yake, hapa, nao watakuwa taji yake milele mbinguni. Paulo aliwaagiza hawa Wafilipi, “simameni imara katika Bwana.” Laonekana jambo rahisi sana kusimama imara, lakini wale wanaojaribu kufanya hivyo wanajua ni kazi ngumu kiasi gani.

2. Namsihi Euodia, namsihi na Sintike, wawe na nia moja katika Bwana. Ni wanawake wawili tu waliokuwa wamekosana, lakini Mtume ana shauku kubwa hivyo ya umoja mkamilifu hata anaweka “namsihi” kwa kila mmoja wao. Hasemi ni yupi aliyekuwa sahihi na yupi aliyekosea, bali angependa wawe “na nia moja katika Bwana.” Tofauti ndogo, hata kati ya washirika wasiojulikana wa Kanisa, zaweza kuzuia kazi ya Roho wa Mungu. Roho Mtakatifu ni kama njiwa—na njiwa hupenda mahali penye utulivu—hawaji mahali penye kelele na ugomvi. Ee, na tusitawishe upendo sisi kwa sisi! Na kama katika jambo lo lote tumetofautiana wakati wo wote, na tudhani kwamba twamsikia Paulo akisema, usiku huu, “Namsihi Euodia, nami namsihi Sintike, wawe na nia moja katika Bwana.” Patanani, ndugu zangu wa kike! Patanani, ndugu zangu wa kiume! Ugomvi wo wote ulivyo, umalizeni na, “iweni na nia moja katika Bwana.” Mkinunuliwe kwa damu ile ile ya thamani, mkivikwa haki ile ile kamilifu, mkiwa njiani kwenda Mbinguni pale pale, “iweni na nia moja katika Bwana.”

3. Nami nakuomba wewe pia, mfanyakazi mwenzangu wa kweli, uwasaidie wanawake hao waliojitaabisha pamoja nami katika Injili, pamoja na Klementi, na wafanyakazi wenzangu wengine, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima. Hatujui ni nani huyu “mfanyakazi mwenzangu wa kweli.” Yamkini alikuwa Epafradito aliyeipeleka Waraka huu Filipi. Ye yote aliyekuwa, alikuwa mtu aliyefanya kazi pamoja na Paulo bega kwa bega. Kama maksai wawili wakivaa nira ile ile na bado wasipatane, wanafanyiana taabu sana. Kama mmoja akijaribu kulala chini na mwingine ataka kusimama, au kama mmoja aendapo mbio kuliko mwingine, nira inakuwa yenye kuudhi maradufu. Paulo anazungumza juu ya mtu fulani hapa kama aliyekuwa “mfanyakazi mwenzake wa kweli”—naye amwambia, “Uwasaidie wanawake hao waliojitaabisha pamoja nami katika Injili.”

Ni mahali bora kiasi gani wanawake wameshika sikuzote katika utumishi wa Bwana Yesu Kristo na hapa Paulo anasema juu yao kama waliojitaabisha pamoja naye katika Injili! Bila shaka Lidia lazima alikuwa mmoja wa hao. “Pamoja na Klementi, na wafanyakazi wenzangu wengine, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima.” Kwa mujibu wa wafafanuzi fulani wenye elimu, jina la mtu laweza kuwa katika kitabu cha uzima kwa muda, lakini laweza kuondolewa. Kama fundisho lao ni kweli, kitabu hicho kitakuwa kimekwaruzwa na kutiwa madoa sana. Namshukuru Mungu kwamba siamini kitabu cho chote kama hicho! Kama Bwana Yesu Kristo ameliandika jina langu katika kitabu cha uzima, katika daftari kuu la jamaa ya waliokombolewa, nawapinga mashetani wote wa Kuzimu kamwe kulifutisha!

4. Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini. Kama wawahi kufurahi katika Bwana, waweza kufurahi katika Bwana sikuzote, kwa maana yeye ni yeye yule sikuzote, na mwenye neema sikuzote! Kuna sababu ya kufurahi katika Mungu wakati mmoja kama wakati mwingine, kwa kuwa habadiliki kamwe.

5. Upole wenu na ujulikane na watu wote. Neno hili, “upole,” katika Kiyunani, ni neno gumu sana kulitafsiri. Halimaanishi kiasi kwa maana ile ambayo watu wengine hulitumia neno hilo, kwa maana wanalifanya, kama nidhaniavyo, karibu neno lililolaaniwa. “Upole wenu”—wema wenu, ukubalifu wenu, uvumilivu wenu—“na ujulikane na watu wote.” Ndiyo maana yake. Msisukume haki zenu wenyewe mbali mno—simameni kabla ya kile mngeweza kudai kwa haki na mnapohisi, wakati wo wote, hasira kidogo, jizuieni—jishikeni, vumilieni na stahimilini. Msiende mbali kama mwezavyo, wala mbali kama wengine wadhanivyo kwamba yawapasa, katika kutetea haki zenu wenyewe. Wema wenu, ukubalifu wenu, na ujulikane na watu wote.

5. Bwana yu karibu. Kristo anakuja—kwa nini unajisumbua? Bwana yu karibu nawe akusaidie—kwa nini una wasiwasi kupita kiasi? Kwa nini unachukuliwa hivyo na jaribu la sasa lililo la muda? “Bwana yu karibu.”

6. Msijisumbue kwa neno lo lote. Msijisumbue kwa wasiwasi kwa neno lo lote! Imbeni, pamoja na Faber—

“Sina masumbufu, Ee Bwana mbarikiwa, Kwa maana masumbufu yangu yote ni yako.”

6-8. Bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu kwa njia ya Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya heshima, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwako wema wo wote, na ukiwapo sifa yo yote, yatafakarini hayo. Kila jambo la namna hii lawahusu ninyi, kwa hiyo lisaidieni kadiri mwezavyo. Kuweni upande wa kila jambo laweza kuelezwa hivyo. Kama linatetea kweli, unyofu, uchaji, dini, usafi, utakatifu—kuweni upande huo. Kama liko lo lote lililo kinyume cha hili, msihusike nalo kamwe, lakini kama liko tendo lo lote ulimwenguni litakalosaidia kuendeleza mambo yaliyo ya kweli, ya heshima, ya haki, safi, yenye kupendeza na yenye sifa njema, “yatafakarini hayo,” na yatafakarini kiasi cha kuongeza uvutano wao miongoni mwa wana na binti za wanadamu!

9. Mambo yale mliyojifunza kwangu, na kuyapokea, na kuyasikia, na kuyaona kwangu, yatendeni. Ni vyema mhubiri awezapo kusema hivyo—asipolazimika kusema, “Fanyeni kama nisemavyo wala si kama nifanyavyo,” bali awezapo, kama Mtume, kusema—“mambo yale mliyojifunza, na kuyapokea, na kuyasikia, na kuyaona kwangu, yatendeni.”

9. Naye Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi. Mungu wa amani yu pamoja sikuzote na wale wampokeao Mwana wake mpendwa na wanaosaidia Injili yake. Ni mojawapo ya baraka za Waaminio wa kweli kwamba Mungu wa amani atakuwa pamoja nao daima.

10. Lakini nalifurahi katika Bwana sana, kwa kuwa sasa, hatimaye, ule uangalizi wenu kwangu umesitawi tena; ambao kweli mlikuwa nao, ila mlikosa nafasi. Paulo alikuwa gerezani Rumi na hawa Wafilipi walikuwa wametoa mchango. Nao walikuwa wamemtuma Epafradito nao ili amsaidie Mtume katika umaskini wake, basi akawaambia, “Mlinijali zamani; lakini kwa muda hamkuwa na nafasi ya kunisaidia, na sasa mmenikumbuka, tena, kwa hiyo nafurahi katika Bwana sana.”

11. Sisemi hivi kwa kuwa nina mahitaji; kwa maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo. Je, hilo si jambo bora la kujifunza? Paulo alikuwa mtu mwenye elimu nawe u vivyo hivyo, kama umejifunza somo hili! Huenda usiweze kuweka D.D., au LL.D., baada ya jina lako, lakini u mtu mwenye elimu kama waweza kusema, “Nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo.”

12. Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa. Haya ni mambo mawili makuu ya kujifunza. Wako baadhi wajuao la kwanza, lakini wasiolijua la pili. Nimewajua kadhaa wa watoto wa Mungu walioonekana mashuhuri kwa utauwa walipodhiliwa, lakini hawakuwa na maana yo yote walipopata utajiri. Hawakujua kufanikiwa—wakawa na kichwa kizito na wakubwa mno kupita kadiri yao! Haikuwa hivyo kwa Mtume, kwa maana angeweza kusema kwa kweli, “Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa.”

12. Kila mahali na katika mambo yote nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kufanikiwa na kupungukiwa. Je, hakuwa Bingwa wa Sanaa wa kweli? Alikuwa ameistadi sanaa ya kuona njaa bila kunung'unika, sanaa ya kushiba bila kujivuna, sanaa ya kupungukiwa bila kukosa saburi, sanaa ya kufanikiwa bila kuweka moyo wake katika vitu vya kidunia. Alikuwa, kweli, Bingwa wa Sanaa wa daraja la juu kabisa!

13. Nayaweza mambo yote—Hilo laonekana kama kujisifu, sivyo? Malizia sentensi.

14. Katika yeye anitiaye nguvu. Hapa hakuna kujisifu kusikofaa, kwa maana Paulo angeweza kuyafanya mambo yote kwa nguvu za Kristo zilizo kuu! Imesemwa vyema kwamba malaika hupita kwa nguvu, bali watakatifu hupita katika udhaifu wao. Tunapokuwa dhaifu kuliko wakati mwingine, na Kristo akatutia nguvu, ndipo hutokea sifa njema kuliko zote.

14-17. Lakini mlifanya vyema, kwa kushiriki nami katika dhiki yangu. Nanyi Wafilipi mnajua vilevile, ya kuwa mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna Kanisa lililoshiriki nami kwa habari ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu. Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu mara moja na tena. Si kwamba nataka kipawa; bali nataka faida izidishwe katika hesabu yenu. Ukarimu wao uliandikwa katika hesabu yao katika kitabu cha Mungu.

18, 19. Lakini ninavyo vitu vyote tena kwa wingi; nimejaa tele, nikiisha kupokea kwa mkono wa Epafradito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, dhabihu inayokubaliwa, impendezayo Mungu. Naye Mungu wangu atawajazeni kila mnachohitaji kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. Ni Mungu wa Paulo aliyewatunza Wafilipi na ni Mungu wa Paulo atakayenitunza wewe nami! “Mungu wangu,” asema Paulo, “atawajazeni kila mnachohitaji—si kama mlivyonijazia mimi, kutoka umaskini wenu, bali kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu”! Msidhani kwamba mtawahi kuumaliza utajiri wa Mungu katika utukufu, au kukausha hazina ya taifa ya kutosha kwa yote—jambo hilo haliwezekani.

20. Sasa Mungu, Baba yetu, na apewe utukufu milele na milele. Amina. Yeye anatubariki, na tumbariki yeye! Yeye anatujazia mahitaji yetu yote kwa kadiri ya utajiri wake katika utukufu—na tuutukuze utukufu wake milele na milele.

21. Msalimuni kila mtakatifu katika Kristo Yesu. Mpeni mtikiso wa mkono. Semeni, “Habari yako, ndugu yangu? Nakutakia mema.” Salamu hizi za moyoni yapasa ziwe za kawaida katika kila kusanyiko la Kikristo. Sikuzote nachukia ile heshima ya ajabu iliyopo katika mahali fulani pa ibada ambapo hakuna mtu amjuaye mwingine. Wana heshima mno hata wasiweze kufahamiana na ndugu zao. Kama u katika Kristo Yesu, fahamianeni! “Msalimuni kila mtakatifu katika Kristo Yesu.”

21, 22. Ndugu walio pamoja nami wanawasalimu. Watakatifu wote wanawasalimu, hasa wale walio wa nyumba ya Kaisari. Nadhani wengi wa hawa walikuwa watumwa tu katika nyumba ya kifalme. Yamkini walikuwako mmoja au wawili, labda, wa daraja la juu zaidi, lakini, kwa uwezekano mkubwa, Injili iliwafikia kwanza watumwa katika jumba la Kirumi, mahali pale pa machafuko ya uovu, ambapo tamaa mbaya na ukatili vilijaa. Kulikuwa na watakatifu hata pale—na Mungu bado ana baadhi ya vito vyake vikilala juu ya majalala!

23. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi nyote. Amina.

Yaliyomo

Nguvu Kuu katika Maombi Charles H. Spurgeon

Ukurasa 1 / 1 · 29 dakika zimebaki katika sura