Nguvu Kuu katika Maombi ·Nguvu ya Maombi na Furaha ya Sifa

Sura 11 · dakika 31 za kusoma

Nguvu ya Maombi na Furaha ya Sifa

“Ninyi nanyi mkisaidiana kwa kutuombea sisi, ili kwa kipawa tulichojaliwa kwa maombi ya watu wengi, watu wengi wapate kutolea shukrani kwa ajili yetu. Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa unyofu na uaminifu wa kimungu, si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu, tumeenenda katika ulimwengu, na hasa zaidi kwenu ninyi.” 2 Wakorintho 1:11,12.

MTUME Paulo alikuwa, kwa maongozi ya pekee, ameokolewa katika hatari iliyokuwa karibu sana huko Asia. Wakati wa ile ghasia kubwa katika Efeso, Demetrio na wenzake watengenezaji wa vihekalu walipoinua fujo kubwa dhidi yake, kwa sababu waliona ya kuwa kazi yao ilikuwa hatarini, uhai wa Paulo ulikuwa katika hatari kubwa. Kwa hiyo aandika, “Tulilemewa mno kupita nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi.” Mtume amhusu Mungu, peke yake, uhifadhi wake wa pekee. Na kama alikuwa akirejea pia kwa ile nafasi alipopigwa mawe na kuachwa kama amekufa, kuna ufaafu mwingi katika kumbariki kwake “Mungu awafufuaye wafu.”

Zaidi ya hayo, Mtume ahoji kutokana na jambo hili kwamba Mungu alikuwa amemwokoa hivyo zamani, na alikuwa bado msaidizi wake sasa, ya kwamba angekuwa pamoja naye pia siku zijazo. Paulo ni bingwa wa hesabu zote—imani yake sikuzote ilikuwa kikokotoo tayari—na hapa twamkuta akihesabu kwa Kanuni ya Tatu ya Mwamini. Ahoji kutoka yaliyopita hadi yaliyopo, na kutoka yaliyopo hadi mambo yatakayokuja. Fungu litangulialo maandiko yetu ni mfano wa fahari wa kufikia hitimisho la faraja kwa Kanuni ya Tatu—“Ambaye alituokoa na mauti kubwa namna hii, tena atatuokoa; ambaye kwake tumeweka tumaini letu ya kuwa atazidi kutuokoa.”

Kwa sababu Mungu wetu ni “yeye yule jana na leo na hata milele,” pendo lake katika wakati uliopita ni hakikisho lisilokosea la wema wake leo, na ni ahadi iliyo hakika sawasawa ya uaminifu wake kesho. Hali zetu ziwe zipi, njia yetu iwe na matatizo kiasi gani, na upeo wetu wa macho uwe na giza kiasi gani, tukihoji kwa kanuni ya, “Ameokoa, Anaokoa, Ataokoa,” faraja yetu haiwezi kamwe kuharibiwa. Basi jipeni moyo, enyi wazao wa Israeli mliotaabika. Kama mngekuwa na Mungu abadilikaye kushughulika naye, roho zenu zingejaa uchungu—lakini kwa sababu yeye ni, “yeye yule jana na leo na hata milele,” kila udhihirisho unaorudiwa wa neema yake wapaswa kuwafanyia iwe rahisi zaidi kumtegemea. Kila uzoefu mpya wa uaminifu wake wapaswa kuimarisha uhakika wenu katika neema yake. Roho aliyebarikiwa atufundishe kukua katika uhakika mtakatifu ndani ya Bwana wetu aliye mwaminifu daima.

Ingawa Mtume wetu alikiri hivyo mkono wa Mungu, na mkono wa Mungu peke yake, katika kuokolewa kwake, hata hivyo hakuwa mjinga kiasi cha kukana au kudharau visababu vya pili. Kinyume chake, akiisha kumsifu kwanza Mungu wa Faraja Yote, sasa akumbuka kwa shukrani maombi ya bidii ya waombezi wengi wenye upendo. Shukrani kwa Mungu kamwe isiwe kisingizio cha kukosa shukrani kwa mwanadamu. Ni kweli ya kwamba Yehova alimkinga yule Mtume wa Mataifa, lakini alifanya hivyo kwa kujibu maombi. Chombo kilichochaguliwa hakikuvunjwa kwa fimbo ya waovu, kwa maana mkono ulionyoshwa wa Mungu wa Mbinguni ulikuwa ulinzi wake—lakini mkono ule ulinyoshwa kwa sababu watu wa Korintho, na watakatifu wa Mungu kila mahali walikuwa wameshinda katika Kiti cha Enzi cha Neema kwa dua zao za pamoja.

Kwa shukrani dua zile zilizofanikiwa zatajwa katika andiko, “Ninyi nanyi mkisaidiana kwa kutuombea sisi,” naye awatamani Ndugu sasa waunganishe sifa zao pamoja na zake, “ili kwa kipawa tulichojaliwa kwa maombi ya watu wengi, watu wengi wapate kutolea shukrani kwa ajili yetu.” Aongeza ya kwamba ana haki juu ya pendo lao kwa kuwa hakuwa kama baadhi waliokuwa si waaminifu kwa amana yao, bali dhamiri yake ilikuwa safi ya kwamba alikuwa amehubiri Neno kwa unyofu na kwa uaminifu.

Tukiwa tunazungumza juu ya mambo haya, Roho atiaye mafuta na ashuke sasa kuyafanya yatunufaishe. Kwanza, tutakiri nguvu ya maombi ya pamoja. Pili, tutawachochea kwenye sifa za pamoja. Na kisha, mahali pa tatu, tutasisitiza dai letu la furaha juu yenu—dai ambalo si letu peke yetu, bali ni la watumishi wote wa Mungu wanaotumika kwa unyofu kwa ajili ya roho za watu.

I. Basi kwanza, ndugu wapendwa, ni wajibu wangu na pendeleo langu asubuhi hii KUKIRI NGUVU YA MAOMBI YA PAMOJA.

Imempendeza Mungu kufanya maombi kuwa mto ufurikao na kushangilia ambao kupitia kwake rehema zetu nyingi zilizo bora hutufikia. Ni ufunguo wa dhahabu ufunguao maghala yaliyojaa ya Yusufu wetu wa mbinguni. Yaandikwa juu ya kila rehema ya Agano, “Kwa jambo hili nitaulizwa na nyumba ya Israeli niwafanyie.” Kuna rehema zijazo bila kutafutwa, kwa maana Mungu apatikana na wale wasiomtafuta. Lakini kuna fadhili nyingine ambazo hutolewa tu kwa watu waombao, na kwa hiyo hupokea—watafutao, na kwa hiyo huona—wabishao, na kwa hiyo hupata kuingia.

Kwa nini Mungu amependezwa kutuamuru tuombe kabisa si vigumu kugundua, kwa maana maombi humtukuza Mungu, kwa kumweka mwanadamu katika hali ya unyenyekevu kuliko zote ya ibada. Kiumbe katika maombi humkiri Muumba wake kwa heshima na kumkiri kuwa ndiye mtoaji wa kila kipawa chema na kilicho kamili. Jicho huinuliwa juu ili kuutazama Utukufu wa Bwana, huku magoti yakipigwa chini nchini katika unyenyekevu wa udhaifu unaokiriwa. Ingawa maombi si namna iliyo juu kabisa ya kuabudu, ama sivyo yangeendelezwa na watakatifu Mbinguni, hata hivyo ndiyo iliyo nyenyekevu zaidi, na hivyo iliyo faafu zaidi, kuudhihirisha Utukufu wa yule Aliye Kamili kama uonwavyo na mwili na damu isiyo kamili.

Tangu ile “Baba Yetu,” ambamo twadai uhusiano, hadi kufikia, “ufalme na nguvu na utukufu,” ambavyo twavikiri kwa Mungu wa pekee wa kweli, kila sentensi ya maombi humheshimu Aliye Juu. Kuugua na machozi ya waombaji wanyenyekevu vinakubalika kwa kweli kama vile ile, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,” ya Makerubi na Maserafi isiyokoma. Kwa maana katika hakika yao yenyewe maungamo yote ya kweli ya makosa ya binafsi si kitu ila ni heshima itolewayo kwa ukamilifu usio na kikomo wa Bwana wa Majeshi. Bwana huheshimiwa zaidi kwa maombi yetu kuliko kwa moshi usiokoma wa uvumba mtakatifu wa madhabahu iliyosimama mbele ya pazia.

Zaidi ya hayo, tendo la kuomba latufundisha kutostahili kwetu, jambo ambalo si baraka ndogo kwa viumbe wenye kiburi kama sisi. Kama Mungu angetupa fadhili bila kutulazimisha kuziombea, kamwe tusingejua jinsi tulivyo maskini. Lakini maombi ya kweli ni orodha ya mahitaji, ni faharasa ya shida, ni shauri la kimaskini (in forma pauperis), ni kufunuliwa kwa vidonda vya siri, ni ufunuo wa umaskini uliofichwa. Wakati ni ombi kwa utajiri wa Mungu, ni ungamo la utupu wa kibinadamu. Naamini ya kwamba hali iliyo na afya zaidi ya Mkristo ni kuwa mtupu sikuzote—na sikuzote akimtegemea Bwana kwa ruzuku. Kuwa maskini nafsini sikuzote na tajiri katika Yesu—dhaifu kama maji binafsi—lakini mwenye nguvu kwa Mungu kutenda matendo makuu. Na kwa hiyo faida ya maombi—kwa sababu wakati unamwabudu Mungu, humweka kiumbe pale apaswapo kuwa—katika mavumbi kabisa.

Maombi yenyewe, mbali na jibu yaletayo, ni faida kubwa kwa Mkristo. Kama mkimbiaji apatavyo nguvu za mbio kwa mazoezi ya kila siku, vivyo hivyo kwa mbio kubwa ya maisha twapata nishati kwa kazi takatifu ya maombi. Maombi huotesha manyoya kwenye mabawa ya vifaranga vya tai wa Mungu ili wajifunze kupaa juu ya mawingu. Maombi hufunga viuno vya mashujaa wa Mungu na kuwapeleka vitani, mishipa yao imekazwa na misuli yao imara. Mwombaji wa bidii hutoka chumbani mwake, kama vile jua lichomozavyo katika vyumba vya mashariki, likishangilia kama shujaa kupiga mbio zake.

Maombi ni ule mkono wa Musa ulioinuliwa uwashindao Waamaleki zaidi ya upanga wa Yoshua. Ni ule mshale uliopigwa kutoka chumba cha Nabii ukitabiri kushindwa kwa Washami. Nikisemaje ya kwamba maombi humvika Mwamini sifa za Uungu, hufunga udhaifu wa kibinadamu kwa nguvu za Kimungu, hugeuza upumbavu wa kibinadamu kuwa hekima ya mbinguni, na huwapa wanadamu wenye taabu utulivu wa Mungu asiyekufa? Sijui maombi hayawezi kutenda nini! Nakushukuru, Mungu mkuu, kwa Kiti cha Rehema, kipawa kiteule cha fadhili zako za ajabu. Utusaidie kukitumia sawasawa!

Kama vile rehema nyingi zaletwavyo kutoka Mbinguni katika merikebu ya maombi, vivyo hivyo kuna fadhili nyingi zilizo teule na za pekee ambazo zaweza kuletwa kwetu tu kwa majahazi ya maombi ya pamoja. Ni mengi mema ambayo Mungu atawapa akina Eliya na akina Danieli wake walio peke yao, lakini kama wawili wenu wakikubaliana katika jambo lo lote mtakaloliomba, hakuna kikomo cha majibu ya ukarimu wa Mungu. Petro asingaliweza kutolewa gerezani kama isingalikuwa ya kwamba maombi yalifanywa bila kukoma na Kanisa lote kwa ajili yake. Pentekoste isingalikuja kama wanafunzi wote wasingalikuwa, “mahali pamoja kwa nia moja,” wakingoja kushuka kwa zile ndimi za moto. Mungu apendezwa kumpa mwombaji mmoja rehema nyingi, lakini nyakati nyingine aonekana kusema, “Nyote mtatokea mbele zangu na kuomba fadhili zangu, kwa maana sitauona uso wenu, wasipokuwapo hata ndugu zenu walio wadogo pamoja nanyi.”

Kwa nini hivi, ndugu wapendwa? Naona ya kwamba kwa njia hii Bwana wetu mwenye neema huonyesha kuithamini kwake ushirika wa watakatifu. “Naamini ushirika wa watakatifu” ni kifungu kimoja cha ile imani kuu ya Kikristo, lakini ni wachache jinsi gani waelewao. Lo, kuna kitu kama muungano wa kweli kati ya watu wa Mungu. Twaweza kuitwa kwa majina mbalimbali—

“Lakini watumishi wote wa Mfalme wetu, Mbinguni na duniani ni mmoja.”

Hatuwezi kumudu kupoteza msaada na pendo la ndugu zetu. Augustino asema, “Maskini wameumbwa kwa ajili ya matajiri, na matajiri wameumbwa kwa ajili ya maskini.” Sina shaka ila watakatifu wenye nguvu wameumbwa kwa ajili ya watakatifu dhaifu, na ya kwamba watakatifu dhaifu huwaletea baraka za pekee waliokomaa. Kuna ulinganifu katika mwili mzima—kila kiungo chadaiwa kitu na kila kiungo kingine—na mwili mzima umefungwa pamoja na kushikamanishwa kwa kile ambacho kila kiungo hukitoa. Kuna tezi fulani katika mwili wa mwanadamu ambazo mtaalamu wa anatomia haelewi vizuri. Aweza kusema juu ya ini, kwa mfano, ya kwamba latoa umajimaji wa thamani kubwa mno katika utendaji wa mwili. Lakini kuna vitoa vingine ambavyo thamani yao dhahiri hawezi kuithibitisha. Lakini, bila shaka, kama tezi hiyo ingeondolewa, mwili mzima ungeweza kuteseka kwa kiwango kikubwa.

Na hivyo, ndugu wapendwa, waweza kuwako baadhi ya Waaminio ambao twaweza kusema juu yao, “Sijui faida yao. Siwezi kueleza jema gani afanyalo Mkristo yule.” Lakini kama kiungo hicho kisicho na maana, na kionekanacho hakina faida, kingeondolewa, mwili mzima ungeweza kufanywa uteseke, mwili mzima ungeweza kuwa mgonjwa, na moyo wote ungezimia. Hii yaelekea ndiyo sababu ya kwamba baraka nyingi zenye uzito za pendo la Mbingu hutolewa tu kwa maombi ya pamoja—ili tupate kutambua faida ya mwili mzima na hivyo tulazimishwe kutambua muungano wa kweli ulio hai ambao Neema ya Mungu imefanya—na kuudumisha kila siku kati ya watu wa Mungu. Je, si wazo lenye furaha, ndugu wapendwa, ya kwamba hata mshiriki wa Kanisa aliye maskini na asiyejulikana kabisa aweza kuongeza kitu kwenye nguvu ya mwili?

Hatuwezi sote kuhubiri. Hatuwezi sote kutawala. Hatuwezi sote kutoa dhahabu na fedha—lakini sote twaweza kuchangia maombi yetu. Hakuna mtu aliyeongoka, ijapokuwa ana siku mbili au tatu tu katika Neema ya Mungu, ambaye hawezi kuomba. Hakuna dada aliye kitandani katika Yesu ambaye hawezi kuomba. Hakuna Mwamini mgonjwa, mzee, dhaifu wa akili, asiyejulikana, asiyejua kusoma, wala asiye na senti ambaye hawezi kuongeza dua zake kwenye hazina ya wote. Huu ndio utajiri wa Kanisa. Twaweka masanduku mlangoni ili tupokee sadaka zenu kwa ajili ya kazi ya Mungu—kumbukeni kuna sanduku la kiroho ndani ya Kanisa ambamo sote twapaswa kudondosha maombezi yetu ya upendo, kama katika hazina ya Bwana. Hata mjane asiye na senti zake mbili aweza kutoa sadaka yake katika hazina hii. Basi ona, ndugu wapendwa, muungano na ushirika ulioje kati ya watu wa Mungu, kwa kuwa kuna rehema fulani ambazo hutolewa tu wakati watakatifu waombapo kwa pamoja.

Jinsi gani twapaswa kuhisi kifungo hiki cha muungano! Jinsi gani twapaswa kuombeana! Jinsi gani, kila mara Kanisa likutanapo kwa dua, sote twapaswa kuifanya kuwa wajibu wetu tulioufunga kuwapo hapo! Ningetamani ya kwamba baadhi yenu ambao mko mbali na Mkutano wa Maombi kwa kisingizio kidogo cho chote mngetafakari jinsi mnavyotunyang’anya sote. Mkutano wa Maombi ni taasisi isiyokadirika thamani, uwahudumiao nguvu mikutano na huduma nyingine zote. Je, hamko wengi ambao mngeweza, kwa kubana kidogo muda wenu na kusukuma kazi zenu, kuja kati yetu mara nyingi zaidi? Na iweje mkipoteza mnunuzi mara kwa mara, je, hamdhani ya kwamba hasara hiyo ingeweza kufidiwa vema kwenu kwa faida zenu katika siku nyingine? Au isipokuwa hivyo, je, faida ya kiroho isingezidi sana kuliko hasara ndogo yo yote ya kimwili? “Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine.”

Sasa tuko tayari kwa neno lingine zaidi. Maombi haya ya pamoja yapaswa hasa kufanywa kwa ajili ya watumishi wa Mungu. Ni kwa ajili yao, hasa, ambapo maombi haya ya hadhara yamekusudiwa. Paulo ayaomba—“Ndugu, tuombeeni.” Na watumishi wote wa Mungu hadi wakati wa mwisho watakiri sikuzote ya kwamba hii ndiyo chemchemi ya siri ya nguvu yao. Maombi ya watu lazima yawe nguvu ya watumishi. Je, nijaribu kuwaonyesha kwa nini mtumishi, kuliko mtu mwingine ye yote katika Kanisa, ahitaji maombi ya bidii ya watu? Je, nafasi yake si ndiyo iliyo hatarini zaidi? Amri za Shetani kwa majeshi ya Kuzimu ni, “Msipigane na mdogo wala mkubwa, ila na watumishi wa Mungu peke yao.” Ajua kwamba akiweza mara moja kumpiga kwa moyo mmojawapo wa hawa, kutakuwa na fujo kwa jumla. Kwa maana kama shujaa amekufa, ndipo watu hukimbia.

Ni kuzunguka mbeba-bendera ambapo mapigano huwa mazito zaidi. Hapo mashoka ya vita hugonga juu ya kofia za chuma. Hapo mishale huelekezwa juu ya silaha, kwa maana adui ajua ya kwamba akiweza kuiangusha bendera, au kupasua fuvu la kichwa cha mbeba wake, atapiga pigo zito na kusababisha kukata tamaa kukubwa. Basi songeni karibu nasi, enyi watu wenye silaha! Enyi mashujaa wa msalaba mwekundu, kusanyikeni kwa ulinzi wetu, kwa maana pambano linazidi kuwa kali! Twawasihi, kama mkituchagua kwenye wadhifa wa uhudumu, simameni imara kando yetu katika mapambano yetu ya kila saa. Nilitambua nirudipo kutoka Rotterdam, tulipokuwa tukivuka kizingiti kwenye mdomo wa Maas, ambapo kwa sababu ya maji mafupi na upepo mbaya, usafiri wa majini ulikuwa hatari mno, ya kwamba amri zilitolewa—“Mikono yote juu ya sitaha!”

Basi nadhani maisha ya mtumishi ni hatari mno, hata naweza kupaza sauti vema, “Mikono yote juu ya sitaha”—kila mtu kwenye maombi! Hata mtakatifu aliye dhaifu kabisa na awe na bidii katika dua. Mtumishi, akiwa amesimama katika nafasi hatari namna hiyo, ana, zaidi ya hayo, uzito mzito wa wajibu ukimlemea. Kila mtu apaswa kuwa mlinzi wa ndugu yake kwa kadiri fulani, lakini ole wao walinzi wa Mungu wasipokuwa waaminifu, kwa maana mikononi mwao damu ya roho itatakwa. Mlangoni pao Mungu ataweka uharibifu wa watu kama hawahubiri Injili kwa ukamilifu na kwa uaminifu.

Kuna nyakati ambapo mzigo huu wa Bwana huwalemea watumishi wa Mungu hata wanapaza sauti kwa maumivu kana kwamba mioyo yao ingepasuka kwa uchungu. Nilimtazama nahodha tulipokuwa tukivuka kizingiti kile akitupa kipimo cha kina, yeye mwenyewe, baharini. Na mtu alipouliza kwa nini hakuwaacha mabaharia wafanye hivyo, alisema, “Kwa wakati huu, sasa hivi, sithubutu kumwamini mtu ye yote ila mimi mwenyewe kutupa kipimo, kwa maana hatuna zaidi ya inchi sita kati ya merikebu yetu na sakafu ya bahari.” Na, kweli, tulihisi chombo kikigusa mara moja au mbili kwa namna isiyopendeza sana. Vivyo hivyo zitakuja nyakati kwa kila mhubiri wa Injili—kama yeye ni yule apaswaye kuwa—atakapokuwa katika mashaka ya kutisha kwa ajili ya wasikilizaji wake. Hataweza kutimiza wajibu wake kwa niaba, bali lazima atumike binafsi kwa ajili ya watu—wala hata hajiamini mwenyewe kuhubiri—bali akimwomba Mungu wake msaada kwa kuwa sasa amelemewa na mzigo wa roho za watu.

Lo, tuombeeni! Kama Mungu akiwapa sisi kwenu, na kama mkikubali kipawa hicho kwa furaha kuu, msitudharau sisi wala Mungu kwa kutuacha bila senti na maskini kwa sababu maombi yenu yamezuiwa. Zaidi ya hayo, kuhifadhiwa kwa mtumishi ni mojawapo ya mambo ya maana zaidi kwa Kanisa. Waweza kumpoteza baharia kutoka merikebuni, na jambo hilo ni baya sana, kwake na kwenu pia. Lakini kama rubani angeanguka baharini, au nahodha angepigwa na ugonjwa, au mshika-usukani angesombwa na maji kutoka usukanini, ndipo chombo kitafanya nini? Kwa hiyo, ingawa maombi yapaswa kutolewa kwa ajili ya kila mtu mwingine katika Kanisa, hata hivyo kwa ajili ya mtumishi yapaswa kutolewa kwanza na zaidi ya wote, kwa sababu ya nafasi ashikayo.

Na tena, ni kiasi gani zaidi kinachotakwa kwake kuliko kwenu? Kama ninyi mnapaswa kuweka meza ya faragha kwa mafundisho ya mtu mmoja mmoja, yeye, kwa namna fulani, apaswa kuweka meza ya hadhara, karamu ya vitu vyema kwa wote wajao. Naye atafanyaje hivi ikiwa Bwana wake hampi ruzuku tele? Ninyi mnapaswa kuangaza kama taa ndani ya nyumba—mtumishi apaswa kuwa kama mnara wa taa—aonekane mbali sana kuvuka kilindi. Naye ataangazaje usiku kucha ikiwa hajanolewa na Bwana wake, na mafuta mapya kupewa kutoka Mbinguni? Ushawishi wake ni mpana kuliko wenu—kama ni kwa uovu, atakuwa mti wa sumu, wenye matawi yaenezayo sumu kwa vyote vilivyo chini ya kivuli chake. Lakini kama Mungu akimfanya kuwa nyota katika mkono wake wa kuume, mwali wake wa nuru utafariji kwa ushawishi wake mwema mataifa yote, na vipindi vyote vya wakati. Kama kuna ukweli wo wote katika haya yote, nawasihi, tupatieni kwa ukarimu na kwa kudumu msaada wa maombi yenu.

Naona ya kwamba katika lugha ya asili, neno la, “kusaidiana,” ladokeza KAZI ya bidii sana. Maombi ya baadhi ya watu hayana kazi ndani yake. Lakini maombi pekee yashindayo kwa Mungu ni maombi ya kweli ya mtu afanyaye kazi—ambapo mwombaji, kama Samsoni, hutikisa malango ya Rehema, na hufanya kazi kuyang’oa badala ya kukatazwa kuingia. Hatutaki maombi ya ncha za vidole, yagusayo tu mzigo—twahitaji maombi ya mabegani—yabebayo mzigo wa bidii, na yasiyokataliwa haja yao. Hatutaki zile hodi za haraka za kukimbia mlangoni pa rehema, ambazo wadai-imani hutoa wanapojionyesha kwenye Mikutano ya Maombi. Twaomba hodi ya mtu aliyeazimia kupata, na aliyeazimia kusimama mlangoni pa Rehema hata litakapofunguka na haja yake yote itakaposhibishwa.

Nishati, ukali, na nguvu ya mtu asiyekubali kukataliwa, bali aazimiaye kuiteka Mbingu kwa nguvu hata atakaposhinda shauku ya moyo wake—haya ndiyo maombi ambayo watumishi huyatamani kutoka kwa watu wao. Yasemekana Melankthoni alipata faraja kubwa kwa habari ya kwamba wafumaji maskini fulani, wanawake na watoto, walikuwa wamekutana pamoja kuombea Matengenezo. Naam, Melankthoni—kulikuwa na msingi thabiti wa faraja hapa. Amini, haikuwa Lutheri peke yake, bali maelfu ya watu maskini walioimba zaburi kwenye ncha ya jembe, na mamia ya wanaume na wanawake watumishi waliotoa dua, ndio waliofanya Matengenezo kuwa yale yaliyokuwa.

Twaambiwa juu ya Paulus Fagio, mwanazuoni maarufu wa Kiebrania, aliyekuwa na faida kubwa katika kuingiza Matengenezo katika nchi hii, ya kwamba mojawapo ya maombi yake ya mara kwa mara kwa wanafunzi wake wadogo lilikuwa ni kwamba wadumu katika maombi, ili Mungu apendezwe kumwaga baraka kwa kujibu maombi yao. Je, sijasema mara mia ya kwamba baraka zote ambazo Mungu ametupatia hapa, ongezeko lote la Kanisa letu, limetokana, chini ya Mungu, na dua zenu za bidii na moto? Kumekuwa na nyakati zisogezazo Mbingu katika nyumba hii na katika New Park Street. Tumekuwa na nyakati ambapo tulihisi tungeweza kufa mapema kuliko kutosikilizwa. Tulipolibeba Kanisa letu kifuani petu kama mama ambebavyo mtoto wake. Tulipohisi shauku na uchungu wa kuzaa kwa ajili ya roho za watu.

Twaweza kusema kwa kweli, tuonapo Kanisa letu likiongezeka kila siku, na makutano bado wakining’inia midomoni petu kusikiliza Neno, “Mungu amefanya nini?” Je, sasa tutakoma na maombi yetu? Je, sasa tutamwambia yule Kuhani Mkuu, “Yatosha”? Je, sasa tutanyofoa makaa yawakayo kutoka madhabahuni na kuuzima uvumba uwakao? Je, sasa tutakataa kuleta wana-kondoo wa asubuhi na jioni wa maombi na sifa kwenye dhabihu? Enyi wana wa Efraimu, mliojifunga silaha na kuchukua pinde, je, mtageuza migongo yenu siku ya vita? Gharika imegawanyika mbele yenu. Yordani imerudishwa nyuma! Je, mtakataa kupita katikati ya vilindi? Mungu, naam Mungu wenu, awatangulia. Sauti ya shangwe ya Mfalme yasikika katikati ya majeshi yenu!

Je, sasa mtakuwa waoga na kukataa kupanda na kuimiliki nchi? Je, sasa mtapoteza pendo lenu la kwanza? Je, “Ikabodi” litaandikwa mbele ya hema hili? Je, itasemwa ya kwamba Mungu amewaacha? Je, itakuja siku ambapo binti za Ufilisti watashangilia, na wana wa Shamu watashinda? Kama sivyo, rudini magotini tena, kwa nguvu zote za maombi! Kama sivyo, rudini kwenye dua zenu za bidii tena! Kama sivyo, kama hamtaki kuona mema yakiharibiwa na uovu ukishinda, shikaneni mikono tena—na kwa jina la yeye aishiye milele kutuombea—mara nyingine mshinde katika maombi ili baraka ipate kushuka tena! “Ninyi nanyi mkisaidiana kwa kutuombea sisi.”

II. Sasa lazima TUWACHOCHEE KWENYE SIFA. Sifa yapaswa sikuzote kuandama maombi yaliyojibiwa. Ukungu wa shukrani ya dunia wapaswa kupanda kama jua la pendo la Mbingu lipashavyo ardhi joto. Je, Bwana amekuwa mwenye neema kwenu, na ameutega sikio lake kwa sauti ya dua yenu? Basi msifuni maadamu mwaishi. Msimnyime wimbo yeye aliyejibu maombi yenu, na kuwapa haja ya moyo wenu. Kunyamaza juu ya rehema za Mungu ni kujiletea hatia ya kukosa shukrani kwa kutisha, na kukosa shukrani ni mojawapo ya maovu mabaya kuliko yote.

Nataraji, ndugu wapendwa, hamtatenda kwa ubaya kama wale wenye ukoma tisa, ambao baada ya kuponywa ukoma wao, hawakurudi kumpa shukrani Bwana aliyewaponya. Kusahau kumsifu Mungu ni kukataa kujinufaisha wenyewe, kwa maana sifa, kama maombi, ina faida mno kwa mtu wa kiroho. Ni zoezi tukufu na lenye afya. Kucheza, kama Daudi, mbele za Bwana, ni kuchangamsha damu katika mishipa, na kufanya mapigo ya moyo yapige kwa kasi yenye afya zaidi. Sifa hutupatia karamu kubwa, kama ile ya Sulemani, aliyempa kila mtu kipande chema cha nyama, na chupa ya divai.

Sifa ndiyo iliyo ya mbinguni kuliko wajibu wote wa Kikristo. Malaika hawaombi, lakini hawakomi kusifu mchana na usiku. Kumbariki Mungu kwa rehema zilizopokewa ni kuwanufaisha wanadamu wenzetu—“wanyenyekevu watasikia na kufurahi.” Wengine waliokuwa katika hali kama hizo watapata faraja kama twaweza kusema, “Enyi, mtukuzeni Bwana pamoja nami, na tuliadhimishe jina lake pamoja, maskini huyu alilia, na Bwana akamsikia.” Wakristo waliofungwa ndimi ni aibu ya kusikitisha kwa Kanisa. Tunao baadhi kama hao—baadhi ambao ibilisi amewaziba vinywa—na muziki wa sauti kubwa zaidi wanaotoa ni wakati wanapotafuna lijamu la ukimya wao. Ningetamani, ndugu zangu, ya kwamba katika hali zote kama hizo ulimi wa bubu upate kuimba.

Kwenda hatua moja zaidi hapa. Kama sifa ilivyo njema na yenye kupendeza, ikimbariki mwanadamu na kumtukuza Mungu, sifa ya pamoja ina sifa ya pekee kuu. Sifa ya pamoja ni kama muziki wa pamoja. Sauti ya ala moja ni tamu mno, lakini mamia ya ala, za upepo na za nyuzi, zote zikiunganishwa, ndipo kikundi cha wanamuziki hutoa wingi mtukufu wa upatano. Sifa ya Mkristo mmoja hukubaliwa mbele za Mungu kama chembe ya uvumba, lakini sifa ya wengi ni kama chetezo kilichojaa ubani ukifuka mbele za Bwana. Sifa ya pamoja ni kionjo cha Mbinguni, kwa maana katika kusanyiko lile kuu wote, pamoja, kwa moyo mmoja na sauti moja, humsifu Bwana—

“Elfu kumi mara elfu ndizo ndimi zao, lakini furaha zao zote ni moja.”

Sifa ya hadhara yapendeza sana kwa Mkristo mwenyewe. Ni mizigo mingapi ambayo imeondoa? Nina hakika nisikiapo shangwe ya sifa katika nyumba hii huupasha moyo wangu joto. Nyakati nyingine ni ya polepole kidogo kwa ladha yangu, na lazima niwahimize mwongeze mwendo wenu, ili mawimbi yavingirikayo ya sifa tukufu yaonyeshe nguvu yake yote! Lakini pamoja na vizuizi vyote, kwa moyo wangu hakuna muziki kama wenu. Rafiki zangu wa Kiholanzi humsifu Bwana kwa polepole mno hata mtu angeweza vema kusinzia, akibembelezwa na nyimbo zao zilizorefushwa. Hata pale, hata hivyo, sauti nyingi hufanya upatano mtukufu wa sifa.

Napenda kuwasikia watu wa Mungu wakiimba wanapoimba kweli, si wakati ni kuvutwa mahali fulani kati ya upatano na mvurugano. Lo, ningetamani wimbo mtakatifu, shangwe ya sifa ya juu ambamo roho ya kila mtu hupiga mpigo na ulimi wa kila mtu husikika tuni—na kila mwimbaji huhisi tamaa kuu ya kumzidi mwenzake kwa shukrani na pendo! Kuna kitu kizuri mno katika muungano wa mioyo ya kweli katika kuabudu Mungu—na mioyo hii ionyeshwapo katika wimbo—jinsi sauti zake za kuvutia zilivyo tamu. Nadhani twapaswa kuwa na Mkutano wa Sifa mara moja kwa juma. Tuna Mkutano wa Maombi kila Jumatatu, na Mkutano wa Maombi kila Jumamosi, na Mkutano wa Maombi kila asubuhi, lakini kwa nini hatuna Mkutano wa Sifa? Hakika nyakati zapaswa kutengwa kwa ajili ya ibada zinazofanyizwa na sifa tangu mwanzo hadi mwisho. Na tujaribu mpango huo mara moja.

Kama nilivyosema juu ya maombi ya pamoja, ya kwamba yapaswa kutolewa hasa kwa ajili ya watumishi, vivyo hivyo sifa ya pamoja mara nyingi yapaswa kuchukua sura ile ile. Kundi lote lapaswa kumsifu na kumbariki Mungu kwa rehema itolewayo kwa Kanisa kupitia wachungaji wake. Sikilizeni jinsi Mtume wetu asemavyo tena—“Ili kwa kipawa tulichojaliwa kwa maombi ya watu wengi, watu wengi wapate kutolea shukrani kwa ajili yetu.” Ndugu, twapaswa kumsifu Mungu kwa ajili ya watumishi wema kwamba wako hai—kwa maana wafapo kazi yao nyingi hufa pamoja nao. Ni jambo la kushangaza jinsi matengenezo yatakavyosonga mbele Lutheri na Kalvini wangali hai, na jinsi yatakavyokoma mara watengenezaji wafapo.

Roho za watu wema hazifi ila kwa maana fulani tu. Makanisa ya Mungu katika zama hizi ni kama Waisraeli katika nyakati za Waamuzi. Waamuzi walipokufa, walifuata sanamu za kuchonga tena. Na ni vivyo hivyo sasa. Mungu amwokoapo mtu, Kanisa lasitawi, lakini mtu afapo, ari ambayo aliipeperusha hata ikawa mwali huvia kati ya majivu katika visa tisa kati ya kumi, kama si tisini na tisa kati ya kila mia. Ufanisi wa Kanisa wategemea uhai wa mtumishi. Mungu aamuru hivyo ili atunyenyekeze. Kwa hiyo yapasa kuwe na shukrani kwa uhai uliohifadhiwa.

Lakini yapasa kuwe na shukrani kubwa kwa tabia iliyohifadhiwa, kwa maana lo, mtumishi aangukapo, ni fedheha iliyoje! Ndiyo, msomapo katika ripoti za polisi kisa cha kusikitisha cha Mch. Bw. fulani, aliyechagua kujiita mtumishi wa Kibaptisti, kila mtu husema, “Ni jambo la kuchukiza kama nini! Watu wa Kibaptisti lazima ni kikundi kibaya kama nini.” Basi, mpumbavu ye yote duniani aweza kujiita mtumishi wa Kibaptisti. Uhuru wetu ni kamili mno hata hakuna sheria wala mpango uliopo. Mtu ye yote awezaye kupata watu kumi na wawili wamsikilize akihubiri ni mtumishi, angalau kwao. Kwa hiyo hamwezi kudhani ila kwamba watakuwepo wanafiki fulani watakaolichukua jina hilo ili kupata sifa ya namna fulani.

Kama mtumishi wa kweli akihifadhiwa na kufanywa aushike uadilifu wake kwa nguvu, yapaswa kuwe na shukrani ya daima kwa Mungu kwa ajili yake. Kama mtumishi akihifadhiwa akiwa amejaa maudhui mema. Kama yeye ni kama kisima kibubujikacho. Kama Mungu akimpa kutoa katika hazina yake vitu vipya na vya kale ili kuwalisha watu wake, yapaswa kuwe na shukrani za moyoni. Naye akihifadhiwa akiwa mzima, kama hageukii falsafa upande mmoja, wala finyu ya mafundisho upande mwingine, yapaswa kuwe na shukrani hapo. Kama Mungu akiwapa makutano nia ya kumsikia, na zaidi ya yote, kama roho zikiongoka na watakatifu wakijengwa, yapaswa kuwe na heshima na sifa isiyokoma kwa Mungu.

Lo, sasa nazungumza juu ya jambo mnalolijua nyote, nanyi mwatikisa tu vichwa vyenu kukubali, na kudhani hakuna jambo kubwa ndani yake. Lakini kama mngefanywa kuishi Uholanzi kwa muda kidogo mngethamini upesi maneno haya. Nilipokuwa nikisafiri huko, nilikaa katika nyumba pamoja na watu watauwa—watu wa Mungu ambao ningeweza kufanya nao ushirika mtamu—ambao hawawezi kuhudhuria mahali palipokuwa mahali pao pa kuabudu zamani. Kwa nini sivyo? “Bwana,” wasema, “je, naweza kwenda mahali pa kuabudu ambapo wengi wa watumishi hukana kila Neno la Maandiko? Si wale wa Kanisa lililorekebishwa tu, bali wa kila dhehebu katika Uholanzi! Nawezaje kuwasikiliza wasaliti waapao kwa vifungu vya Kikalvini au Kilutheri, kisha huingia mimbarani na kukana uhalisi wa ufufuo, au kudai ya kwamba kupaa kwa Yesu ni fumbo la kiroho tu?”

Naona ya kwamba katika Uholanzi wako miaka hamsini mbele yetu katika ukafiri. Tutawapata upesi kama mabwana wa shule fulani ninayoijua wataruhusiwa kuongezeka. Wanachuoni wa Kiholanzi wamepiga hatua kubwa katika Neolojia, hata sasa watu wanalipenda kweli la Mungu na kuna wingi ulio tayari kulisikia. Lakini hawa wamelazimika kabisa kukataa kwenda Kanisani kabisa, wasije kwa njia yo yote wakaunga mkono mafundisho ya uzushi na ya uongo yanayohubiriwa kwao kila Jumapili.

Lo, kama Mungu angeliondoa mara moja kutoka Uingereza watumishi wahubirio Injili kwa ujasiri na kwa wazi, mngemlilia Mungu awarudishie kinara tena. Twaweza kweli kusema juu ya Uingereza—

“Pamoja na makosa yenu yote nakupenda bado.” Tunaye askofu wa kikoloni akiriye kutoamini kwake. Tunao watu wachache wa madhehebu yote wanaoteleza kimya kutoka kwenye Kweli. Lakini, ashukuriwe Mungu si kitu bado. Wao ni kama tone ndani ya ndoo ukilinganisha na Makanisa ya Kristo, na wale kati yetu wasio Wakalvini kabisa kama tungependa. Namshukuru Mungu, wako wengi wasiobisha kamwe uvuvio wa Maandiko, wala kutia shaka Kweli kuu ya kuhesabiwa haki kwa imani. Bado tumehifadhiwa kati yetu watu walio waaminifu kwa Mungu, na wahubirio Kweli yote kama ilivyo katika Yesu.

Iweni na shukrani kwa ajili ya watumishi wenu, nasema tena, kwa maana kama mngewekwa mahali ambapo baadhi ya Waaminio wako, mngemlilia Mungu wenu—“Bwana, uturudishie Manabii wako. Utupelekee njaa ya mkate au njaa ya maji, lakini usitupelekee njaa ya Neno la Mungu!”

Naomba kwa ajili yangu mwenyewe asubuhi hii, kama mtumishi wenu, shukrani zenu zichanganywe na zangu katika kumsifu Mungu kwa msaada ambao amenijalia katika kazi ngumu sana ya wiki mbili zilizopita. Sifa na iwe kwa Mungu kwa kukubaliwa alikonijalia katika nchi ile kati ya watu wa tabaka zote. Nasema kwa sifa yake wala si yangu, kwa maana hili limekuwa nadhiri kwangu, ya kwamba Mungu akinipa mavuno, sitachukua hata suke moja la nafaka lake, bali yeye atakuwa na yote. Nilikuta, katika mahali pote nilipoenda, makutano makubwa ya watu, umati usioweza kumwelewa mhubiri, lakini waliotaka kuuona uso wake, kwa sababu Mungu alikuwa amezibariki mahubiri yake yaliyotafsiriwa kwa roho zao.

Makutano wengi walinipa mkono wa fadhili za kidugu na, wakiwa na machozi machoni pao, waliomba, katika lugha ya Kiholanzi, kila baraka juu ya kichwa changu. Nilitumaini kuwahubiria watu hamsini na mamia fulani, na badala yake, walikuwepo wengi mno hata makanisa makubwa hayakuwa makubwa kupita kiasi. Hili lilinishangaza, na kunifurahisha—na kunifanya nishangilie katika Mungu—nami nawaomba mshangilie pamoja nami. Namshukuru Mungu kwa kukubaliwa alikonipa kati ya watu wa tabaka zote. Wakati maskini walipokusanyika kupeana mikono, hata karibu wanivute vipande vipande, ilimpendeza Mungu kuugusa moyo wa Malkia wa Uholanzi hata akaniita, nami kwa saa moja na robo nilipata pendeleo la kuzungumza naye juu ya mambo yaletayo amani yetu.

Sikutafuta mahojiano naye. Ilikuwa hamu yake mwenyewe. Kisha nikaiinua roho yangu kwa Mungu ili nisizungumze lo lote ila Kristo, na nimhubirie yeye lo lote ila Yesu. Na ikampendeza Bwana kunisaidia. Nami nikamwacha yule bibi mwema kabisa, bila kuepa kutangaza shauri lote la Mungu. Nilifurahishwa, kweli, kujikuta nikipokelewa kwa moyo na madhehebu yote, hata Jumamosi huko Amsterdam nilihubiri katika Kanisa la Wamennoni asubuhi, na katika Kanisa la zamani la Kiholanzi lililorekebishwa jioni. Asubuhi ya Jumapili iliyofuata katika Kanisa la Kipresbiteri la Kiingereza, na kisha tena, jioni, katika Kanisa Huru la Kiholanzi.

Nyakati nyingine niliruhusiwa kuhubiri katika makanisa makubwa, kama katika Dom Kirk huko Utrecht, na katika Peter’s Kirk, huko Leyden, bila kuwa na maskini peke yao, bali watu wa cheo na waungwana wa nchi, ambao, bila shaka, wangeweza kuelewa Kiingereza vizuri zaidi ya maskini wengi, ambao hawakuwa na nafasi ya kujifunza. Nilihisi, nilipokuwa nikitoka mji hadi mji, Bwana akinisaidia daima kuhubiri. Sikupata kamwe kujua unyumbufu wa roho namna hiyo, kuruka kwa moyo namna hiyo maishani mwangu kabla. Nami narudi, si nikiwa nimechoka na kuchakaa, ijapokuwa nikihubiri mara mbili kila siku, bali nimejaa nguvu na uhai zaidi kuliko nilipoanza kwanza!

Nampa Mungu utukufu kwa roho nyingi nilizosikia zimeongoka kupitia kusomwa kwa mahubiri yaliyochapishwa, na kwa baraka za upendo za wale waliotufuata hadi ukingoni mwa maji kwa machozi mengi, wakituambia—“Fanya bidii kuja tena kabla ya majira ya baridi,” na kutusihi mara nyingine tuhubiri Neno katika nchi ile. Yaweza kuchanganyika na haya kiasi fulani cha kujisifu. Bwana ajua kama ni hivyo au sivyo, lakini mimi silitambui. Namsifu na kumbariki jina lake, ya kwamba katika nchi ambamo mna falsafa nyingi namna hii, amenisaidia kuhubiri Kweli yake kwa unyofu namna hiyo, hata sikutamka neno kama mtaalamu wa mafundisho tu, bali nilihubiri Kristo na Kristo peke yake. Shangilieni pamoja nami, ndugu zangu wapendwa. Lazima niwafanye mshangilie ndani yake, au kama hamtaki, lazima nishangilie peke yangu, lakini mkate wangu wa sifa ni mkubwa mno nisiweze kuula wote mwenyewe.

III. Nasi twafika mwisho. Nina budi kusisitiza MADAI YA FURAHA ambayo Mtume aatoa katika mstari wa kumi na mbili, kama sababu ya KWA NINI YAPASWA KUWE NA MAOMBI NA SIFA. “Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa unyofu na uaminifu wa kimungu, si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu, tumeenenda katika ulimwengu, na hasa zaidi kwenu ninyi.”

Lo, baada ya yote, faraja ya mtu lazima itoke, karibu na wokovu uliokamilika wa Mungu, kutoka kwa ushuhuda wa dhamiri yake mwenyewe. Na kwa mtumishi, ni ushuhuda ulioje ya kwamba amehubiri Injili kwa unyofu, ambao una maana mbili—amehubiri si kwa nia mbili—akisema jambo moja na kumaanisha lingine. Naye ameuhubiri, si kama wapiga-makasia wapigavyo—wakitazama upande mmoja na kukokota mwingine—bali ameuhubiri akimaanisha aliyoyasema, akiwa na moyo mmoja, akitamani Utukufu wa Mungu na wokovu wa watu.

Na ni baraka iliyoje kuwa ameuhubiri kwa unyofu, yaani, bila maneno magumu, bila misemo iliyong’arishwa, bila kamwe kusoma madaha ya usemaji, bila kamwe kutafuta mapambo ya maneno. Ni laana iliyoje maisha ya mtu anayenajisi mimbari kwa madaha ya ufasaha! Ni yenye kukata tamaa jinsi gani kitanda chake cha kifo atakapokumbuka ya kwamba alifanya maonyesho ya uwezo wake wa usemaji badala ya mambo thabiti yaletayo kuokoa roho! Dhamiri hiyo yaweza kwa haki kutulia iwezayo kunena juu ya kuishughulikia Kweli ya Mungu kwa unyofu.

Mtume asema, pia, ya kwamba alihubiri kwa uaminifu. Yaani, aliuhubiri akiumaanisha, akiuhisi—akiuhubiri hata hakuna aliyeweza kumshtaki kuwa mwongo. Neno la Kiyunani lina kitu ndani yake cha mwanga wa jua, naye ndiye mtumishi wa kweli wa Mungu ahubiriye kile ambacho angetaka kikaangikwe katika mwanga wa jua, au ambaye mwanga wa jua huangaza moja kwa moja kupitia kwake. Naogopa ya kwamba hakuna hata mmoja wetu aliye kama kioo cheupe—wengi wetu tumepakwa rangi kidogo—lakini ana furaha yule atafutaye kuiondoa dutu ya rangi kadiri iwezekanavyo, ili nuru ya Injili iangaze moja kwa moja, safi kama itokavyo kwa Jua la Haki, kupitia kwake.

Paulo alikuwa amehubiri kwa unyofu na uaminifu. Naye aongeza, “Si kwa hekima ya mwili.” Lo, ni hadithi zilizoje nilizosikia za yale ambayo hekima ya mwili itakayoyafanya! Nami nimejifunza somo katika wiki mbili zilizopita ambalo ningetamani Uingereza ingelijifunza. Kuna shule tatu za makosa ya kitheolojia kule ng’ambo, na kila moja huruka juu ya mgongo wa mwenzake. Baadhi yao hushikilia ya kwamba mambo yote ya Maandiko ni ngano tu. Wengine wao husema ya kwamba kuna mambo mema fulani katika Biblia, ingawa mna makosa mengi. Na wengine huenda mbali zaidi, na kuitupa Biblia yote mbali kabisa kuhusu Uvuvio wake, ingawa bado huihubiri, na bado huitegemea, wakisema ya kwamba hufanya hivyo kwa ajili ya kujenga watu wa kawaida tu—wakiitegemeza tu kwa ajili ya makutano—ingawa napaswa kuongeza, kwa ajili ya kupata riziki yao pia.

Inasikitisha! Inasikitisha! Inasikitisha ya kwamba Kanisa limefikia kiwango kama hicho—lile Kanisa la zamani la Kiholanzi lililorekebishwa—kioo hasa cha Ukalvini, likisimama imara na thabiti katika vifungu vyake vya imani juu ya mafundisho yote tuyapendayo, na bado limepotea hata uhuru wa kilegevu na wa upotovu. Lo, kwa bidii iliyoje twapaswa kuikemea hekima ya mwili! Naogopa, ndugu wapendwa, ya kwamba nyakati nyingine baadhi yenu, msikiapo mtumishi, hupenda aeleze vema kabisa, nanyi mwaona kosa asipoonyesha kiasi fulani cha kipaji. Nashangaa kama hilo si dhambi? Nusu naelekea kudhani ni hivyo.

Nyakati nyingine nadhani kama hatupaswi kuangalia kidogo kila siku kipaji, na zaidi na zaidi maudhui ya Injili ihubiriwayo. Kama mtu amebarikiwa kwa uwezo wa usemaji labda tutafaidika zaidi kwake—kama hilo si udhaifu. Kama hatungekuwa afadhali kurudi kwenye siku za wavuvi tena, na kutowapa watu elimu ya namna yo yote kabisa, bali kuwatuma tu wahubiri Kweli ya Mungu kwa unyofu. Hivi, badala ya kwenda urefu wanaokwenda sasa, wakiwapa watu, sijui nini, kila aina ya elimu isiyo na faida yo yote ya duniani kwao, bali ambayo huwasaidia tu kuupotosha unyofu wa Mungu. Napenda neno lile katika andiko langu—“Si kwa hekima ya mwili.”

Na sasa naweka dai langu, kama dhamiri yangu inishuhudiavyo—naweka dai langu kwa kujisifu huku kwa Mtume wetu. Nimeihubiri Injili ya Mungu kwa unyofu. Sijui jinsi ningeweza kuihubiri kwa unyofu zaidi, wala siwezi kuitangaza kwa uaminifu zaidi. Nimeihubiri kwa uaminifu—Mpekuzi wa mioyo yote ajua hilo. Nami sikuihubiri kwa hekima ya mwili, na hiyo kwa sababu moja bora—kwamba sina yo yote—nami nimelazimika kushikamana na ushuhuda rahisi wa Bwana. Lakini kama nimefanya lo lote, limefanywa kwa neema ya Mungu.

Kama mafanikio yo yote yamepatikana, ni neema ya Mungu iliyoyafanya yote. “Na hasa zaidi kwenu ninyi.” Kwa maana ijapokuwa neno letu limekwenda hadi nchi nyingi, na ushuhuda wetu wazunguka dunia, lakini, “hasa zaidi kwenu ninyi.” Ninyi tumewaonya. Ninyi tumewasihi. Ninyi tumewahimiza. Pamoja nanyi tumesihi. Juu yenu tumelia. Kwa ajili yenu tumeomba. Kwa baadhi yenu tumekuwa mzazi wa kiroho katika Kristo. Kwa wengi wenu kama baba mlezi. Kwa wengi wenu kama mwalimu na mjengaji katika Injili. Nasi twatumaini kwa nyote kama rafiki wa kweli katika Kristo Yesu. Kwa hiyo nadai maombi yenu—yenu kuliko ya watu wengine wo wote.

Na ingawa hawatakuwa wachache watakaotukumbuka katika dua zao, nawasihi, kwa kuwa imekuwa, “hasa zaidi kwenu ninyi,” niacheni hasa niwe na maombi yenu. Wengine watasema ni ukatili hata kwangu kudhani ya kwamba hamwombi. Naam, sidhani hivyo kwa ukatili, lakini waweza kuwako baadhi wanaosahau—baadhi wanaosahau kusihi. Lo, endeleeni kuniombea bado! Kusanyiko lote halijaokoka bado. Wako baadhi wanaotusikia ambao bado hawajaongoka. Sihini na Mungu kwa ajili yao. Wako mioyo migumu ambayo bado haijavunjwa! Mwombeni Mungu aufanye nyundo upige. Na maadamu wako baadhi ambao bado hawajayeyushwa, mwombeni Mungu alifanye Neno liwe kama moto!

London hii kubwa yahitaji kuchochewa toka mwisho hata mwisho. Waombeeni watumishi wenu wote, ili Mungu awafanye kuwa hodari. Kanisa lahitaji zaidi bado ya sauti kuu ya Mungu kulizindua kutoka usingizini mwake. Mwombeni Mungu awabariki watumishi wake wote aliowatuma. Sihini naye kwa nguvu za Kimungu, ili ufalme wake upate kuja, na mapenzi yake yatimizwe duniani kama huko mbinguni.

Lo, laiti nyote mngemwamini Yesu! Kwa maana msipoamini, hamwezi kuomba wala kusifu! Lo, laiti nyote mngemwamini Yesu! Kumbukeni, hii ndiyo njia pekee ya wokovu. Mtumaini Yesu, kwa maana amwaminiye yeye hahukumiwi, bali asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana wa Mungu. Mtumaini Yesu nanyi mtaokoka. Kristo na awakubali sasa, kwa ajili ya pendo lake mwenyewe. Amina.

Yaliyomo

Nguvu Kuu katika Maombi Charles H. Spurgeon

Ukurasa 1 / 1 · 31 dakika zimebaki katika sura