Pamoja na Kristo katika Shule ya Maombi
Maisha ya Maombi

Sura 32 · dakika 8 za kusoma

Maisha ya Maombi

“Furahini sikuzote. Ombeni bila kukoma. Kwa kila jambo shukuruni.”—1 Wathesalonike 5:16, 17, 18.

BWANA wetu alinena mfano wa yule mjane na yule hakimu dhalimu ili kutufundisha kwamba imewapasa watu kuomba sikuzote, wala wasikate tamaa. Kama vile yule mjane alivyodumu katika kutafuta jambo moja maalum, mfano huo waonekana kuhusu maombi ya kudumu kwa ajili ya baraka fulani, wakati Mungu anapokawia au anapoonekana kukataa. Maneno yaliyo katika Nyaraka, yanenayo juu ya kudumu katika maombi bila kuchoka, kudumu katika kuomba na kukesha ndani yake, na kuomba sikuzote katika Roho, yaonekana zaidi kuelekeza juu ya maisha yote kuwa maisha ya maombi. Kadiri nafsi ijaavyo shauku ya kudhihirishwa kwa utukufu wa Mungu kwetu na ndani yetu, kwa kupitia sisi na pande zote zetu, pamoja na uhakika kwamba yeye husikia maombi ya watoto wake; maisha ya ndani kabisa ya nafsi hupanda juu daima kwa kutegemea na imani, kwa shauku ya kutamani na kutazamia kwa kumwamini.

Tunapofikia mwisho wa tafakari zetu haitakuwa vigumu kusema kinachohitajiwa ili kuishi maisha kama hayo ya maombi. Jambo la kwanza pasipo shaka ni kuitoa sadaka maisha yote kwa ajili ya ufalme na utukufu wa Mungu. Yeye atafutaye kuomba bila kukoma kwa sababu ataka kuwa mtu wa dini sana na mwema, hatafika huko kamwe. Ni kujisahau nafsi na kujitoa wenyewe tuishi kwa ajili ya Mungu na heshima yake ndiko kuupanuzao moyo, kunakotufundisha kuyaangalia mambo yote katika nuru ya Mungu na mapenzi yake, na ambako kwa asili hutambua katika kila kitu kinachotuzunguka uhitaji wa msaada na baraka ya Mungu, nafasi ya yeye kutukuzwa. Kwa sababu kila jambo hupimwa na kujaribiwa kwa lile jambo moja liujazalo moyo—utukufu wa Mungu, na kwa sababu nafsi imejifunza kwamba ni kile tu kilicho cha Mungu ndicho kiwezacho kweli kuwa kwake na kwa utukufu wake, maisha yote huwa ni kutazama juu, ni kulia toka moyoni kabisa, ili Mungu adhihirishe nguvu na upendo wake na hivyo kuonyesha utukufu wake. Mwamini huamka kwa kutambua kwamba yeye ni mmoja wa walinzi walio juu ya kuta za Sayuni, mmoja wa wakumbushaji wa Bwana, ambao kilio chao chamgusa kweli na kumsukuma Mfalme aliye mbinguni afanye lile ambalo lisingefanyika. Aelewa jinsi lilivyokuwa la kweli onyo la Paulo, “mkiomba sikuzote kwa sala zote na maombi katika Roho kwa ajili ya watakatifu wote na kwa ajili yangu,” na “dumuni katika kuomba, huku mkituombea na sisi pia.” Kujisahau, kuishi kwa ajili ya Mungu na ufalme wake kati ya watu, ndiyo njia ya kujifunza kuomba bila kukoma.

Maisha haya yaliyowekwa wakfu kwa Mungu lazima yaandamane na uhakika wa ndani kwamba maombi yetu yana nguvu. Tumeona jinsi Bwana wetu Mbarikiwa asivyosisitiza jambo lo lote katika masomo yake ya maombi kuliko imani kwa Baba kuwa ni Mungu ambaye kwa hakika kabisa hufanya lile tuliombalo. “Ombeni nanyi mtapata;” tegemea kwa uhakika kupata jibu, ndilo kwake mwanzo na mwisho wa mafundisho yake (linganisha Mathayo 7:8 na Yohana 16:24). Kadiri uhakika huu utushikavyo, na inavyokuwa jambo lililothibitika kwamba maombi yetu kweli yana matokeo na kwamba Mungu hufanya lile tuliombalo, hatuthubutu kupuuza matumizi ya nguvu hii ya ajabu: nafsi humgeukia Mungu kabisa, na maisha yetu huwa maombi. Twaona kwamba Bwana ahitaji na huchukua muda, kwa sababu sisi na vyote vinavyotuzunguka ni viumbe vya wakati, chini ya sheria ya kukua; lakini tukijua kwamba hakuna hata ombi moja la imani liwezalo kupotea, kwamba kuna wakati mwingine haja ya kuhifadhi na kukusanya maombi, kwamba maombi ya kudumu hayazuiliki, maombi huwa ni kuishi kwa utulivu na kwa kudumu maisha yetu ya shauku na imani mbele za Mungu wetu. Ee, tusiendelee tena kwa hoja zetu kuzipunguza na kuzidhoofisha ahadi hizo huru na za hakika za Mungu aliye hai, tukizinyang’anya nguvu zake, na sisi wenyewe uhakika ule wa ajabu zilizokusudiwa kuutia ndani yetu. Si katika Mungu, si katika mapenzi yake ya siri, si katika mipaka ya ahadi zake, bali ndani yetu, katika nafsi zetu wenyewe ndiko kilipo kizuizi; sisi si vile tunavyopaswa kuwa ili kuipata ahadi. Na tuufungue moyo wetu wote kwa maneno ya ahadi ya Mungu katika unyofu na kweli yake yote: yatatuchunguza na kutunyenyekeza; yatatuinua na kutufanya wenye furaha na nguvu. Na kwa imani ijuayo kwamba yapata yale iyaombayo, maombi si kazi wala mzigo, bali ni furaha na ushindi; huwa ni jambo la lazima na tabia ya pili.

Muungano huu wa shauku kuu na uhakika thabiti tena si kitu ila ni uhai wa Roho Mtakatifu ndani yetu. Roho Mtakatifu akaa ndani yetu, hujificha katika vilindi vya utu wetu, na huchochea shauku ya kuvitamani Visivyoonekana na vya Kimungu, kumtamani Mungu mwenyewe. Mara katika kuugua kusikoweza kutamkwa, mara katika uhakika ulio wazi na wenye ufahamu; mara katika maombi maalum na ya wazi kwa ajili ya kufunuliwa kwa Kristo kwa kina zaidi kwetu, mara katika kusihi kwa ajili ya nafsi, kazi fulani, Kanisa au ulimwengu, sikuzote na peke yake ni Roho Mtakatifu autoaye moyo umwonee Mungu kiu, utamani yeye ajulikane na kutukuzwa. Pale mtoto wa Mungu aishipo na kwenda kweli katika Roho, pale asiporidhika kubaki wa kimwili, bali atafutapo kuwa wa kiroho, katika kila jambo chombo kifaacho kwa Roho wa Kimungu kudhihirisha uhai wa Kristo na Kristo mwenyewe, hapo maisha ya maombezi yasiyokoma ya Mwana Mbarikiwa hayana budi kujidhihirisha na kujirudia katika uzoefu wetu. Kwa sababu ni Roho wa Kristo aombaye ndani yetu, maombi yetu lazima yasikiwe; kwa sababu ni sisi tuombao katika Roho, kuna haja ya muda, na saburi, na kufanya upya maombi daima, hata kila kizuizi kishindwe, na upatano kati ya Roho wa Mungu na roho zetu uwe mkamilifu.

Lakini jambo kuu tunalolihitaji kwa maisha kama hayo ya maombi yasiyokoma ni kujua kwamba Yesu hutufundisha kuomba. Tumeanza kuelewa kidogo mafundisho yake ni nini. Si kutupasha mawazo au maoni mapya, si kugundua kushindwa au kosa, si kuchochea shauku na imani, ijapokuwa hayo yote ni ya maana kiasi gani, bali ni kutuchukua na kutuingiza katika ushirika wa maisha yake mwenyewe ya maombi mbele za Baba—kwa hilo ndilo Yesu hufundisha kweli. Ni kumwona Yesu akiomba ndiko kulikowafanya wanafunzi watamani na kuomba wafundishwe kuomba. Ni imani ya Yesu aombaye daima, ambaye kwake peke yake ndiko kwenye nguvu ya kuomba, ndiyo itufundishayo kuomba kweli. Twajua kwa nini: yeye aombaye ndiye Kichwa chetu na Uhai wetu. Vyote alivyo navyo ni vyetu na hupewa kwetu tunapojitoa sisi wote kwake. Kwa damu yake hutuingiza mbele za Mungu papo hapo. Patakatifu pa ndani ndipo makao yetu, tunakaa humo. Naye akaaye karibu hivyo na Mungu, na kujua kwamba ameletwa karibu ili kuwabariki walio mbali, hana budi kuomba. Kristo hutufanya washiriki pamoja naye wa nguvu yake ya maombi na maisha yake ya maombi. Basi twaelewa kwamba lengo letu la kweli halipaswi kuwa kufanya kazi nyingi na kuwa na maombi ya kutosha ili kuiweka kazi sawa, bali kuomba sana na kisha kufanya kazi ya kutosha ili nguvu na baraka iliyopatikana katika maombi ipate njia yake kupitia sisi kwa watu. Ni Kristo aishiye daima ili kuomba, aokoaye na kutawala. Yeye hutupasha maisha yake ya maombi: huyadumisha ndani yetu tukimtumaini. Yeye ni dhamana ya kuomba kwetu bila kukoma. Naam, Kristo hufundisha kuomba kwa kuonyesha jinsi afanyavyo, kwa kulifanya ndani yetu, kwa kutuongoza tulifanye ndani yake na kama yeye. Kristo ni yote, uhai na nguvu pia kwa maisha ya maombi yasiyokoma.

Ni kuona huku, kumwona Kristo aombaye daima kuwa uhai wetu, ndiko kutuwezeshako kuomba bila kukoma. Kwa sababu ukuhani wake ni nguvu ya uhai usio na mwisho, uhai ule wa ufufuo usiofifia kamwe wala usiopungukiwa kamwe, na kwa sababu uhai wake ndio uhai wetu, kuomba bila kukoma kwaweza kuwa kwetu si kitu pungufu ila ni furaha ya uhai wa mbinguni. Hivyo Mtume asema: “Furahini sikuzote; ombeni bila kukoma; kwa kila jambo shukuruni.” Ikichukuliwa juu kati ya furaha isiyokoma na sifa isiyokoma, maombi yasiyokoma ni kudhihirika kwa nguvu ya uhai wa milele, mahali Yesu aombapo sikuzote. Muungano kati ya Mzabibu na tawi kwa hakika kabisa ni muungano wa maombi. Kufananishwa kwa juu zaidi na Kristo, kushiriki kulikobarikiwa zaidi katika utukufu wa uhai wake wa mbinguni, ni kwamba twashiriki katika kazi yake ya maombezi: yeye na sisi twaishi daima ili kuomba. Katika uzoefu wa muungano wetu naye, kuomba bila kukoma huwa jambo liwezekanalo, jambo halisi, sehemu takatifu na iliyobarikiwa zaidi ya ushirika wetu mtakatifu na uliobarikiwa na Mungu. Tuna makao yetu ndani ya pazia, mbele za Baba. Lile Baba alisemalo, twalifanya; lile Mwana alisemalo, Baba hulifanya. Kuomba bila kukoma ni kudhihirika kwa mbingu duniani kulikoshuka kwetu, kionjo cha uhai ule ambao huko hawapumziki mchana wala usiku katika wimbo wa ibada na kuabudu.

“BWANA, UTUFUNDISHE KUOMBA.”

Ee Baba yangu, kwa moyo wangu wote nakusifu kwa ajili ya maisha haya ya ajabu ya maombi yasiyokoma, ushirika usiokoma, majibu yasiyokoma, na uzoefu usiokoma wa umoja wangu na yeye aishiye daima ili kuomba. Ee Mungu wangu! nihifadhi daima nikikaa hivyo na kwenda mbele za utukufu wako, ili maombi yawe udhihirisho wa moyoni wa maisha yangu pamoja nawe.

Mwokozi Mbarikiwa! kwa moyo wangu wote nakusifu kwa kuwa ulishuka kutoka mbinguni ili kushiriki nami katika mahitaji na vilio vyangu, ili nipate kushiriki nawe katika maombezi yako yashindayo yote. Nami nakushukuru kwa kuwa umeniingiza katika shule ya maombi, ili kufundisha heri na nguvu ya maisha yaliyo maombi yote. Na zaidi ya yote, kwa kuwa umeniinua na kuniingiza katika ushirika wa maisha yako ya maombezi, ili kupitia mimi pia baraka zako zigawiwe kwa walio karibu nami.

Roho Mtakatifu! kwa heshima ya ndani nakushukuru kwa kazi yako ndani yangu. Ni kwa kupitia wewe ninainuliwa na kuingizwa katika kushiriki mawasiliano yaliyo kati ya Mwana na Baba, na hivyo naingia katika ushirika wa uhai na upendo wa Utatu Mtakatifu. Ee Roho wa Mungu! ikamilishe kazi yako ndani yangu; niingize katika muungano mkamilifu na Kristo Mwombezi wangu. Kukaa kwako ndani yangu kusikokoma na kunifanye maisha yangu kuwa ya maombezi yasiyokoma. Na hivyo maisha yangu yawe yaliyo daima kwa utukufu wa Baba na kwa baraka ya walio karibu nami. Amina.

Ukurasa 1 / 1 · 8 dakika zimebaki katika sura