Kusudi katika Maombi
Kuomba Kusiko na Maombi

Sura 10 · dakika 18 za kusoma · dakika 23 za kusikiliza

Kuomba Kusiko na Maombi

Nayatazama Injili zote nne kuwa za kweli kabisa, kwa maana ndani yake mna mng’ao wa ukuu uliotoka katika nafsi ya Yesu, ukuu ulio wa aina ya Kimungu kuliko wo wote uliopata kuonekana duniani.—Goethe

Hakuna uwezekano wala sababu ya lazima kwa kuomba kusiko na maombi, tendo lisilo na moyo, desturi isiyo na akili, mazoea yaliyokufa, tendo la haraka na la uzembe—halihalalishi kitu. Kuomba kusiko na maombi hakuna uzima, hakutoi uzima, kumekufa, hutoa pumzi ya mauti. Si shoka la vita bali kitu cha kuchezea cha mtoto, kwa ajili ya mchezo wala si kwa ajili ya utumishi. Kuomba kusiko na maombi hakufikii hata umuhimu na makusudi ya burudani. Kuomba kusiko na maombi ni mzigo tu, kizuizi katika saa ya mapambano, ya vita vikali, mwito wa kurudi nyuma wakati wa vita na ushindi.

Kwa nini hatuombi? Ni vipi vizuizi vya maombi? Hili si swali la udadisi wala la mzaha. Linagusa si jambo zima la kuomba kwetu tu, bali jambo zima la dini yetu. Dini haina budi kudhoofika kuomba kunapozuiliwa. Kile kinachozuia kuomba huizuia dini. Yeye aliye na shughuli nyingi mno hata asiweze kuomba atakuwa na shughuli nyingi mno hata asiweze kuishi maisha matakatifu.

Wajibu mwingine huwa wa kukaza na wa kumeza mtu, nao huyasukuma maombi nje. Alikufa kwa kusongwa, ndiyo ingekuwa hukumu ya mchunguzi wa vifo katika visa vingi vya maombi yaliyokufa, kama uchunguzi ungeweza kufanywa juu ya msiba huu mbaya wa kiroho. Njia hii ya kuyazuia maombi huwa ya kawaida mno, nyepesi mno, isiyo na hatia mno hata hutujia sote bila kujua. Tukiruhusu kuomba kwetu kusukumwa nje, jambo hilo litatendeka sikuzote. Shetani angependa tuache majani yaote juu ya njia iendayo chumbani mwetu mwa maombi kuliko kitu kingine cho chote. Chumba cha maombi kilichofungwa maana yake ni kwamba tumefunga duka letu kwa habari ya dini, au, lililo baya zaidi, tumefilisika na tunaiendesha dini yetu kwa jina jingine lisilo la Mungu na kwa utukufu wa mtu mwingine. Utukufu wa Mungu hupatikana katika biashara ya dini kwa kuiendesha dini hiyo kwa mtaji mkubwa wa maombi tu. Mitume walilielewa jambo hili walipotangaza kwamba wakati wao usitumike hata katika wajibu mtakatifu wa kugawa sadaka; ilikuwa lazima, walisema, wajitoe “kudumu katika kuomba, na katika huduma ya lile neno,” maombi yakiwekwa mbele nao, na huduma ya Neno ikipata ufanisi wake na uzima wake kutoka kwa maombi.

Mwenendo wa kuyazuia maombi kwa kuyasukuma nje ni rahisi, nao huenda kwa hatua zinazoendelea. Kwanza, maombi hufanywa kwa haraka. Wasiwasi na fadhaa, vinavyoharibu kabisa mazoezi yote ya ibada, huingia. Kisha muda hufupishwa, hamu ya zoezi lile hupungua. Kisha hubanwa pembeni na kutegemea vipande vya wakati ili yafanyike. Thamani yake hushuka. Wajibu huo umepoteza umuhimu wake. Hauamrishi tena heshima wala kuleta faida. Umeanguka kutoka katika makadirio, kutoka moyoni, kutoka katika mazoea, kutoka katika maisha. Tunaacha kuomba na kuacha kuishi kiroho.

Hakuna kizuizi cha mafuriko yaharibuyo ya kidunia na ya biashara na ya masumbufu, ila maombi. Kristo alimaanisha jambo hili alipotuagiza kukesha na kuomba. Hakuna kikosi cha kutangulia kuifungulia Injili njia ila maombi. Paulo alijua jambo hilo alipotangaza kwamba “usiku na mchana tukiomba sana ili tuwaone nyuso zenu, na kuutimiza upungufu wa imani yenu.” Hakuna kufikia hali ya juu ya neema bila kuomba sana, wala hakuna kudumu katika vimo vile vya juu bila kuomba kukuu. Epafra alijua jambo hili alipokuwa “akijitahidi sikuzote kwa ajili yenu katika maombi yake” kwa ajili ya Kanisa la Kolosai, “ili msimame wakamilifu na kuthibitika katika mapenzi yote ya Mungu.”

Njia pekee ya kukilinda kuomba kwetu kisizuiliwe ni kuyathamini maombi kwa thamani yake ya kweli na kuu. Yathamini kama Danieli alivyoyathamini, ambaye “alipojua ya kuwa ile hati imetiwa sahihi, aliingia nyumbani mwake; na madirisha yake yalikuwa yamefunguliwa kuelekea Yerusalemu; akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, na kushukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tangu hapo.” Yaweke maombi katika thamani za juu kama Danieli alivyofanya, juu ya cheo, heshima, raha, mali, uhai. Yaweke maombi katika mazoea kama Danieli alivyofanya. “Kama alivyokuwa akifanya tangu hapo,” kuna mengi ndani yake ya kutoa uthabiti na uaminifu katika saa ya majaribu; mengi ndani yake ya kuondoa vizuizi na kuyashinda mazingira yanayopinga.

Mojawapo ya hila za Shetani zenye ujanja kuliko zote ni kukiharibu kilicho bora kwa kilicho chema. Biashara na wajibu mwingine ni mema, lakini tumejazwa nayo kiasi kwamba yanakisukuma nje na kukiharibu kilicho bora. Maombi hulishika ngome kwa ajili ya Mungu, na kama Shetani aweza kwa njia yo yote kuyadhoofisha maombi amepata faida hata hapo, na maombi yanapokufa ngome imetwaliwa. Imetupasa kuyalinda maombi kama mlinzi mwaminifu alindavyo zamu yake, kwa uangalifu usiolala. Hatupaswi kuyaweka yakiwa na njaa nusu na dhaifu kama mtoto mchanga, bali imetupasa kuyaweka katika nguvu za jitu. Chumba chetu cha maombi kinapaswa kupata nguvu zetu zilizo mpya kuliko zote, wakati wetu ulio tulivu kuliko wote, saa zake zisizofungwa, bila kuingiliwa, bila haraka. Mahali pa faragha na wakati mwingi ndio uzima wa maombi. “Kupiga magoti mara tatu kila siku, na kusali, na kushukuru mbele za Mungu, kama tulivyokuwa tukifanya tangu hapo,” ndio moyo na nafsi yenyewe ya dini, nako huwafanya watu, kama Danieli, kuwa na “roho bora,” “wapendwa sana mbinguni.”

Ukuu wa maombi, kwa kuwa unamhusu mtu mzima, katika namna yake kali kabisa, hautimizwi bila nidhamu ya kiroho. Hili huyafanya kuwa kazi ngumu, na mbele ya juhudi hii inayodai mengi na kuteketeza, uvivu wetu wa kiroho au udhaifu wetu husimama kwa aibu.

Urahisi wa maombi, viungo vyake vya kitoto, huwa kizuizi kikubwa kwa kuomba kwa kweli. Akili huingia njiani mwa moyo. Roho ya mtoto peke yake ndiyo roho ya maombi. Si kazi ya sikukuu kumfanya mtu mzima kuwa mtoto tena. Katika wimbo, katika ushairi, katika kumbukumbu, aweza kutamani kuwa mtoto tena, lakini katika maombi hana budi kuwa mtoto tena kwa kweli. Magotini mwa mama yake, bila hila, mtamu, mwenye bidii, wa moja kwa moja, mwenye kutumaini. Bila kivuli cha shaka, bila tabia ya kukataliwa. Shauku iwakayo na kuteketeza ambayo yaweza kutamkwa kwa kilio tu. Si kazi nyepesi kuwa na roho hii ya maombi ya maisha ya kitoto.

Kama kuomba kungekuwa saa moja tu chumbani, matatizo yangeikabili na kuizuia hata saa hiyo, lakini kuomba ni maisha yote yakijiandaa kwa ajili ya chumba cha ndani. Ni vigumu jinsi gani kuifunika nyumba na biashara, mambo yote matamu na yote machungu ya maisha, kwa hali takatifu ya chumba cha ndani! Maisha matakatifu ndiyo maandalizi pekee ya maombi. Ni vigumu kuomba kama vile ilivyo vigumu kuishi maisha matakatifu. Katika jambo hili twaona ukuta wa kufukuza umejengwa kuvizunguka vyumba vyetu vya ndani; watu hawapendi kuomba kutakatifu, kwa sababu hawapendi, wala hawataki, kuishi kwa utakatifu. Montgomery anayaeleza matatizo ya kuomba kwa kweli anapotangaza utukufu na urahisi wa maombi.

Maombi ni usemi rahisi kuliko yote

Ambao midomo ya mtoto mchanga yaweza kujaribu.

Maombi ni nyimbo tukufu kuliko zote zifikazo

Kwake Mwenye Enzi aliye juu.

Huu si ushairi mzuri tu, bali ni kweli kuu kuhusu ukuu na urahisi wa maombi. Kuna matatizo makubwa katika kuzifikia nyimbo za maombi zilizoinuka, zilizo kama za malaika. Tatizo la kushuka hata kufikia urahisi wa midomo ya mtoto mchanga si dogo sana kuliko hilo.

Katika Agano la Kale maombi yanaitwa kushindana mweleka. Mapambano na ustadi, juhudi kali, ya kumaliza nguvu zote, zimo ndani yake. Katika Agano Jipya tuna maneno kujitahidi, kujibidiisha sana, kwa bidii, kufaa sana, uchungu mkuu, yote yakionyesha juhudi kali iliyotolewa, matatizo yaliyoshindwa. Sisi, katika nyimbo zetu za sifa, huimba—

“Ni vizuizi vingi namna gani tukutanavyo

Tujapo kwenye kiti cha rehema.”

Tumejifunza pia kwamba matokeo ya neema yapatikanayo kwa maombi kwa kawaida hulingana na gharama iliyotolewa katika kuviondoa vizuizi vinavyozuia ushirika wa juu wa nafsi zetu na Mungu.

Kristo alinena mfano kwa kusudi hili, kwamba imewapasa kuomba sikuzote, wala wasikate tamaa. Mfano wa yule mjane mwenye kusumbua hufundisha matatizo yaliyomo katika kuomba, jinsi yatakavyoshindwa, na matokeo ya furaha yafuatayo kuomba kwa ushujaa. Matatizo yatazuia njia iendayo chumbani mwa maombi sikuzote maadamu inabaki kuwa kweli,

“Ya kwamba Shetani hutetemeka aonapo

Mtakatifu aliye dhaifu kuliko wote akipiga magoti.”

Imani yenye ujasiri hufanywa kuwa na nguvu zaidi na safi zaidi kwa kuyashinda matatizo. Matatizo haya huyafungua tu macho ya imani yaione tuzo tukufu atakayoipata yeye ashindaye mweleka katika maombi. Watu wasikate tamaa katika shindano la maombi, bali wajitoe kwa kazi hii ya juu na takatifu, wakiyapinga matatizo yaliyo njiani, nao watapata katika matokeo yake furaha ipitayo ya malaika. Luther alisema: “Kuomba vema ni kujifunza vema.” Zaidi ya hayo, kuomba vema ni kupigana vema. Kuomba vema ni kuishi vema. Kuomba vema ni kufa vema.

Maombi ni karama adimu, si karama ya watu wote, iliyo tayari mkononi. Maombi si tunda la vipawa vya asili; ni zao la imani, la utakatifu, la tabia ya kiroho iliyo ya kina. Watu hujifunza kuomba kama wajifunzavyo kupenda. Ukamilifu katika unyofu, katika unyenyekevu, katika imani—hivi ndivyo viungo vyake vikuu. Wanaoanza tu katika neema hizi si stadi katika maombi. Maombi hayawezi kunyakuliwa na mikono isiyofundishwa; wahitimu wa shule kuu ya ustadi ya mbinguni peke yao ndio wawezao kuzigusa funguo zake nzuri kuliko zote, na kuzitoa sauti zake tamu kuliko zote, za juu kuliko zote. Malighafi bora na umaliziaji kamili vinahitajika. Mafundi wakuu wanahitajika, kwa maana vibarua tu hawawezi kuitenda kazi ya maombi.

Roho ya maombi inapaswa kuitawala roho yetu na mwenendo wetu. Roho ya chumba cha maombi haina budi kuyatawala maisha yetu, la sivyo saa ya chumbani itakuwa butu na kavu. Kuomba sikuzote rohoni; kutenda sikuzote katika roho ya kuomba; haya huyafanya maombi yetu kuwa na nguvu. Roho ya kila dakika ndiyo inayoupa nguvu ushirika wa chumba cha ndani. Ni kile tulicho nje ya chumba cha ndani kinachokipa chumba cha ndani ushindi au kukiletea kushindwa. Ikiwa roho ya ulimwengu inashinda katika saa zetu zilizo nje ya chumba cha ndani, roho ya ulimwengu itashinda katika saa zetu za chumbani, nazo zitakuwa mchezo wa kuigiza usio na maana wala faida.

Imetupasa kuishi kwa ajili ya Mungu nje ya chumba cha ndani kama tunataka kukutana na Mungu chumbani. Imetupasa kumhimidi Mungu kwa maisha ya kuomba kama tunataka kupata baraka ya Mungu chumbani. Imetupasa kuyatenda mapenzi ya Mungu katika maisha yetu kama tunataka sikio la Mungu chumbani. Imetupasa kuisikiliza sauti ya Mungu hadharani kama tunataka Mungu aisikilize sauti yetu faraghani. Mungu hana budi kuwa na mioyo yetu nje ya chumba cha ndani, kama tunataka kuwapo kwa Mungu chumbani. Kama tunataka kuwa na Mungu chumbani, Mungu hana budi kutupata nje ya chumba cha ndani. Hakuna njia ya kumwomba Mungu, ila kwa kuishi kwa ajili ya Mungu. Chumba cha ndani si mahali pa kuungama tu, bali ni saa ya ushirika mtakatifu, na ya mazungumzo ya juu na matamu, na ya maombezi makali..

Watu wangeomba vizuri zaidi kama wangeishi vizuri zaidi. Wangepata zaidi kutoka kwa Mungu kama wangeishi kwa utii zaidi na kwa kumpendeza Mungu vema. Tungekuwa na nguvu zaidi na wakati zaidi kwa kazi ya Kimungu ya maombezi kama tusingelazimika kutumia nguvu nyingi hivyo na wakati mwingi hivyo kulipa madeni ya zamani na kodi zetu tulizochelewa kulipa. Madeni yetu ya kiroho yanazidi sana mali zetu za kiroho hata wakati wetu wa chumba cha ndani hutumika kuomba hati ya kufilisika badala ya kuwa wakati wa utajiri mkuu wa kiroho kwa ajili yetu na kwa ajili ya wengine. Vyumba vyetu vya ndani vinafanana mno na tangazo lile, “Kimefungwa kwa Matengenezo.”

Yohana alisema juu ya kuomba kwa Wakristo wa kwanza, “Lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.” Twapaswa kuangalia ni maeneo gani yasiyo na mipaka yaliyofunikwa, ni vipawa gani visivyo na mipaka vilivyopokewa kwa kuomba kwao kwenye nguvu: “Lo lote”—ni pana kiasi gani eneo na upokeaji wa kuomba kwenye nguvu; zina maana kiasi gani sababu za kuweza kuomba na kujibiwa maombi. Utii, lakini zaidi ya utii tu, kuyatenda mambo yanayompendeza Mungu vema. Walikwenda vyumbani mwao wakiwa wametiwa nguvu kwa utii wao kamili na uaminifu wao wa upendo kwa Mungu katika mwenendo wao. Maisha yao hayakuwa ya kweli na ya utii tu, bali walikuwa wakifikiri juu ya mambo yaliyo juu ya utii, wakitafuta na kutenda mambo ya kumfurahisha Mungu. Watu kama hawa waweza kuja kwa hatua za shauku na nyuso zinazong’aa kukutana na Baba yao chumbani, si ili kusamehewa tu, bali ili kukubaliwa na kupokea.

Ni tofauti kubwa kama tunakuja kwa Mungu kama mhalifu au kama mtoto; ili kusamehewa au ili kukubaliwa; ili kumaliza hesabu au ili kukumbatiwa; kwa ajili ya adhabu au kwa ajili ya fadhili. Ili kuomba kwetu kuwe na nguvu hakuna budi kutegemezwa na maisha matakatifu. Jina la Kristo halina budi kuheshimiwa na maisha yetu kabla halijayaheshimu maombezi yetu. Maisha ya imani huyakamilisha maombi ya imani.

Maisha yetu hayakipi kuomba kwetu rangi tu, bali hukipa pia mwili. Kuishi vibaya huzaa kuomba vibaya. Twaomba kwa udhaifu kwa sababu twaishi kwa udhaifu. Mto wa kuomba hauwezi kupanda juu kuliko chemchemi ya kuishi. nguvu ya chumba cha ndani imeundwa kwa nishati itiririkayo kutoka katika mito ya kuishi inayokutana pamoja. Udhaifu wa kuishi hutupa uzimbe wake katika makao ya chumba cha ndani. Hatuwezi kuzungumza na Mungu kwa nguvu ikiwa hatujaishi kwa ajili ya Mungu kwa nguvu. Chumba cha ndani hakiwezi kufanywa kitakatifu kwa Mungu ikiwa maisha hayajakuwa matakatifu kwa Mungu. Neno la Mungu hukazia mwenendo wetu kuwa ndio unaokipa kuomba kwetu thamani. “Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiondoa kati yako kongwa, na kunyosha kidole, na kunena maneno ya ubatili.”

Watu wanapaswa kuomba “wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.” Twapaswa kuenenda kwa hofu wakati wa kukaa kwetu hapa ugenini kama tunataka kumwita Baba. Hatuwezi kukitenga kuomba na mwenendo. “Lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.” “Mwaomba wala hampati, kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” agizo la Kristo, “Kesheni, mwombe,” ni la kuufunika na kuulinda mwenendo ili tuje vyumbani mwetu tukiwa na nguvu yote inayopatikana kwa ulinzi wa kukesha juu ya maisha yetu.

Dini yetu huanguka mara nyingi zaidi na kwa huzuni zaidi katika mwenendo wetu. Nadharia nzuri huharibiwa na maisha mabaya. Jambo gumu kuliko yote, na pia lenye kuvutia kuliko yote, katika utauwa ni kuuishi. Kuomba kwetu huumia kwa kuishi vibaya kama vile dini yetu iumiavyo. Katika nyakati za kwanza wahubiri waliagizwa kuhubiri kwa maisha yao au wasihubiri kabisa. Vivyo hivyo Wakristo kila mahali wanapaswa kuagizwa kuomba kwa maisha yao au wasiombe kabisa. Bila shaka, maombi ya toba hukubalika. Lakini toba maana yake ni kuacha kutenda mabaya na kujifunza kutenda mema. Toba isiyozaa badiliko katika mwenendo ni ya uongo. Kuomba kusikozaa mwenendo safi ni udanganyifu. Tumeikosa kazi yote na fadhila yote ya kuomba ikiwa haunyooshi mwenendo. Ni katika asili yenyewe ya mambo kwamba hatuna budi kuacha kuomba au kuacha mwenendo mbaya. Kuomba kwa baridi, kulikokufa, kwaweza kuwako pamoja na mwenendo mbaya, lakini kuomba kwa baridi, kulikokufa, si kuomba hata kidogo machoni pa Mungu. Kuomba kwetu huendelea katika nguvu kadiri kunavyoyanyoosha maisha. Maisha yanayokua katika usafi wake na katika kujitoa kwake yatakuwa maisha ya kuomba zaidi.

Jambo la kusikitisha ni kwamba sehemu kubwa hivyo ya kuomba kwetu haina kitu kinacholengwa wala lengo. Haina kusudi. Ni kuomba kwingi kiasi gani kunakofanywa na wanaume na wanawake ambao kamwe hawakai ndani ya Kristo—kuomba kwa haraka, kuomba kutamu kulikojaa hisia, kuomba. kunakopendeza, lakini kusikotegemezwa na maisha yaliyofungamana na Kristo. Kuomba kwa kupendwa na watu! Ni kiasi gani cha kuomba huku kutokacho katika mioyo isiyotakaswa na midomo isiyo mitakatifu! Maombi huzuka chini ya mvuto wa msisimko fulani mkubwa, kwa dharura fulani inayobana, kwa kelele za watu wengi, kwa hatari fulani kubwa. Lakini masharti ya maombi hayamo. Twakimbilia mbele za Mungu na kujaribu kumfunga—kwenye shauri letu, kumwasha kwa tamaa zetu, kumsukuma—kwa hatari yetu. Mambo yote yanapaswa kuombewa—lakini kwa mikono safi, kwa kuyanyenyekea kabisa mapenzi ya Mungu na kwa kukaa ndani ya Kristo. Kuomba kusiko na maombi kwa midomo na mioyo isiyofundishwa kuomba, kwa maisha yasiyopatana na Yesu Kristo; kuomba kusiko na maombi, kulicho na umbo na mwendo wa maombi lakini kusicho na moyo halisi wa maombi, kamwe hakumsukumi Mungu kujibu. Ni juu ya kuomba kwa namna hiyo ambapo Yakobo asema: “Hamna kitu, kwa sababu hamwombi; mwaomba wala hampati, kwa sababu mwaomba vibaya.”

Maovu mawili makuu—kutokuomba, na kuomba kwa njia isiyo sahihi. Labda ovu lililo kubwa zaidi ni kuomba vibaya, kwa maana lina ndani yake sura ya wajibu uliotimizwa, ya kuomba hali hapakuwa na kuomba—udanganyifu, hila, uongo. Nyakati za kuomba kwingi kuliko zote si kwa kweli nyakati za kuomba kulikobora kuliko zote. Mafarisayo waliomba sana, lakini walisukumwa na majivuno; kuomba kwao kulikuwa ishara ya unafiki wao ambao kwa huo waliifanya nyumba ya sala ya Mungu kuwa pango la wanyang’anyi. Kwao kulikuwa kuomba katika sherehe rasmi—kwa namna ya mashine, kwa kutimiza wajibu tu, kwa kikazi, kuzuri kwa maneno, kwenye harufu nzuri ya hisia, kwenye utaratibu mzuri, kulikopokewa vema na masikio yaliyosikia, lakini kusiko na kabisa kiungo cho chote cha maombi halisi.

Masharti ya maombi yamepangwa vema na yako wazi—kukaa ndani ya Kristo; katika jina lake. Mojawapo ya mahitaji ya kwanza, ikiwa tutaushika uwezekano usio na mipaka wa maombi, ni kuondokana na kuomba kusiko na maombi. Mara nyingi kuomba huko ni kuzuri kwa maneno na kwa utendaji wake; kuna mapambo ya maombi katika namna tajiri na ya gharama, lakini kunakosa nafsi ya kuomba. Twaanguka kwa urahisi mno katika mazoea ya ibada isiyo na maombi, ya kutimiza tu ratiba.

Laiti watu wangeomba kweli katika nyakati zote na katika kila mahali wanapofanya mwendo wa kuomba! Laiti kungekuwa na mioyo mitakatifu iliyowashwa moto nyuma ya maneno haya yote mazuri na namna hizi za neema! Laiti kungekuwa sikuzote na mioyo iliyoinuliwa ndani ya watu hawa waliosimama wima wanaotamka mbele za Mungu maneno yasiyo na kasoro lakini ya bure! Laiti kungekuwa sikuzote na mioyo ya kicho iliyoinama magoti yaliyopigwa yanapotamka maneno mbele za Mungu ili kuyapendeza masikio ya wanadamu!

Hakuna kitu kitakachoulinda uzima wa maombi; nguvu zake, utamu wake, wajibu wake, uzito wake na thamani yake, kama vile kusadiki kwa kina kwamba maombi ni kumkaribia Mungu, kumsihi Mungu, kumwomba Mungu. Ndipo uhalisi utakuwamo ndani yake; kicho kitakuwamo katika mkao, mahali, na katika hewa yenyewe. Imani itavuta, itawasha na kufungua. Desturi tupu na hali ya kufa haviwezi kuishi katika makao haya ya juu ya nafsi yaliyo mazito kabisa.

Kuomba kusiko na maombi hukosa kiungo kikuu cha kuomba kwa kweli; hakujengwi juu ya shauku, nako hakuna bidii wala imani. Shauku hulitwika gari la maombi mzigo, nayo imani huendesha magurudumu yake. Kuomba kusiko na maombi hakuna mzigo, kwa sababu hakuna hisia ya kuhitaji; hakuna moto, kwa sababu hakuna maono, wala nguvu, wala mwanga wa imani. Hakuna msukumo mkuu wa kuomba, hakuna kumshika Mungu kwa mshiko usiokufa, wa kukata tamaa, “Sikuachi usiponibariki.” Hakuna kujiacha kabisa, kujipoteza katika utungu wa ombi la kukata tamaa, la kushikilia, na la kuteketeza: “Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao—na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako;” au “Nipe Uskoti, la sivyo nife.” Kuomba kusiko na maombi hakuweki kitu rehani juu ya matokeo, kwa maana hakuna kitu cha kuweka. Huja kwa mikono mitupu, kweli, lakini ni mikono iliyolegea pamoja na kuwa mitupu. Haijajifunza kamwe somo la mikono mitupu ikiung’ang’ania msalaba; somo hili kwao halina umbo wala uzuri.

Kuomba kusiko na maombi hakuna moyo katika kuomba kwake. Ukosefu wa moyo hukinyang’anya kuomba uhalisi wake, na kukifanya kuwa chombo kitupu kisichofaa. Moyo, nafsi, uzima hayana budi kuwamo katika kuomba kwetu; mbingu hazina budi kuihisi nguvu ya kilio chetu, na hazina budi kuletwa katika huruma iliyolemewa kwa ajili ya hali yetu chungu na ya uhitaji, Uhitaji unaotulemea, usio na faraja ila katika kumlilia Mungu, hauna budi kuyapa maombi yetu sauti.

Kuomba kusiko na maombi si kwa unyofu. Hakuna uaminifu moyoni mwake. Twataja kwa maneno yale tusiyoyataka moyoni. Maombi yetu hutamka kwa desturi mambo ambayo mioyo yetu haiyaonei njaa tu, bali kwa kweli haina ladha nayo kabisa. Wakati mmoja tulimsikia mhubiri mashuhuri na mtakatifu, ambaye sasa yuko mbinguni, akiwajia kwa ghafla na kwa ukali watu wa kusanyiko waliokuwa wametoka tu kuinuka kutoka katika maombi, kwa swali na kauli hii, “Mliomba nini? Kama Mungu angewashika na kuwatikisa, na kudai mwambie mliomba nini, msingeweza kumwambia, hata kama ingekuwa kuokoa maisha yenu, ombi lile lilikuwa nini lililokufa sasa hivi midomoni mwenu.” Ndivyo ilivyo sikuzote, kuomba kusiko na maombi hakuna kumbukumbu wala moyo. Umbo tupu, mchanganyiko usio na mpangilio, kitu kisicho na ladha, mchanganyiko uliotupwa pamoja kwa ajili ya sauti na kujaza nafasi, lakini usio na moyo wala lengo, ndio kuomba kusiko na maombi. Desturi kavu, utumwa wa kuchosha, kazi butu na nzito, ndio kuomba huku kusiko na maombi.

Lakini kuomba kusiko na maombi ni kubaya zaidi sana kuliko kazi au utumwa, kunakitenga kuomba na kuishi; hutamka maneno yake dhidi ya ulimwengu, lakini kwa moyo na maisha hukimbilia ulimwenguni; huombea unyenyekevu, lakini hulea kiburi; huombea kujikana nafsi, huku kikiuendekeza mwili. Hakuna kitu kinachopita kuomba kwa kweli katika matokeo ya neema, lakini ni afadhali kutokuomba kabisa kuliko kuomba maombi yasiyo na maombi, kwa maana si kitu ila kutenda dhambi, na dhambi iliyo mbaya kuliko zote ni kutenda dhambi tukiwa tumepiga magoti.

Mazoea ya kuomba ni mazoea mema, lakini kuomba kwa nguvu ya mazoea tu ni mazoea mabaya sana. Aina hii ya kuomba haikupangwa kwa utaratibu wa Mungu, wala haikuzaliwa kwa nguvu za Mungu. Si upotevu tu, upotoshaji, na udanganyifu, bali ni chemchemi izaayo sana ya kutokuamini. Kuomba kusiko na maombi hakupati matokeo. Mungu hafikiwi, nafsi haisaidiwi. Ni afadhali kutokuomba kabisa kuliko kukosa matokeo yo yote ya kuomba. Ni afadhali kwa yeye aombaye, ni afadhali kwa wengine. Watu husikia habari za matokeo makubwa ajabu yanayoweza kupatikana kwa maombi: mema yasiyo na kifani yaliyoahidiwa katika Neno la Mungu kwa maombi. Hawa watu wa kidunia wenye macho makali, au hawa wenye imani haba waoga, huiona tofauti kubwa kati ya matokeo yaliyoahidiwa na matokeo yaliyopatikana, nao kwa lazima huongozwa kuitilia shaka kweli na thamani ya jambo lile lililo kubwa hivyo kwa ahadi na duni hivyo kwa matokeo. Dini na Mungu huvunjiwa heshima, shaka na kutokuamini hutiwa nguvu kwa kuomba kwingi na kutokupata kitu.

Tofauti na hayo, ni nguvu kuu namna gani kuomba kulikojaa maombi. Maombi halisi humsaidia Mungu na mwanadamu. Ufalme wa Mungu huendelezwa kwayo. Mema makuu kuliko yote humjia mwanadamu kwayo. Maombi yaweza kufanya lo lote ambalo Mungu aweza kufanya. Jambo la kusikitisha ni kwamba hatuliamini jambo hili kama tupasavyo, wala hatulitii katika kujaribiwa.