Kusudi katika Maombi
Kulifikia Sikio la Mungu

Sura 9 · dakika 10 za kusoma · dakika 13 za kusikiliza

Kulifikia Sikio la Mungu

Iinueni mikono iliyolegea, kwa imani na maombi; yategemezeni magoti yanayoyumba. Je, mnazo siku za kufunga na kuomba? Kishambulieni kiti cha neema na kudumu humo, na rehema itashuka.—John Wesley

Imetupasa kukumbuka kwamba lengo la maombi ni sikio la Mungu. Lisipofikiwa hilo, maombi yameshindwa kabisa. Kutamkwa kwake kwaweza kuwa kumewasha hisia za ibada mioyoni mwetu, kusikiwa kwake kwaweza kuwa kumeifariji na kuitia nguvu mioyo ya wale tulioomba pamoja nao, lakini ikiwa maombi hayakuufikia moyo wa Mungu, yameshindwa katika kusudi lake kuu.

Mtu wa ibada ya desturi tupu aweza sikuzote kuomba kwa namna ya kujipendeza mwenyewe. Ana kazi gani ila kukifungua kitabu chake na kuyasoma maneno yaliyoamriwa, au kupiga goti lake na kurudia maneno yale yanayomjia kumbukumbuni au mawazoni? Kama ile Mashine ya Kuombea ya Watartari, ipe tu upepo na gurudumu, na shughuli yote imekamilika. Kupiga magoti kiasi fulani na kusema kiasi fulani, na maombi yamekwisha. Maombi ya mtu wa desturi tupu ni mema sikuzote, au tuseme, mabaya sikuzote, vilevile. Lakini mtoto wa Mungu aliye hai kamwe hatoi ombi linalompendeza yeye mwenyewe; kipimo chake kiko juu ya kile alichokifikia; hustaajabu kwamba Mungu humsikiliza, na ingawa ajua kwamba atasikiwa kwa ajili ya Kristo, hata hivyo huhesabu kuwa ni mfano wa ajabu wa rehema ya kujishusha kwamba maombi duni kama yake yaweze kamwe kuyafikia masikio ya Bwana Mungu wa majeshi.—C. H. Spurgeon

Yaweza kusemwa kwa mkazo kwamba hakuna mtakatifu mvivu aombaye. Je, aweza kuwako mtakatifu mvivu? Je, aweza kuwako mtakatifu asiyeomba? Je, kuomba kwa ulegevu hakupunguzi taji na ufalme wa utakatifu? Je, aweza kuwako askari mwoga? Je, aweza kuwako mnafiki mtakatifu? Je, yaweza kuwako maovu yenye wema? Ni hapo tu mambo hayo yatakapoletwa kuwako ndipo tutakapoweza kumpata mtakatifu asiyeomba.

Kufanya tu mwendo wa kuomba ni kazi ya kuchosha, ingawa si ngumu. Kusema sala kwa namna ya adabu na ya upole si kazi nzito. Lakini kuomba kwa kweli, kuomba hata kuzimu kuhisi pigo lile zito, kuomba hata malango ya chuma ya taabu yafunguliwe, hata milima ya vizuizi iondolewe, hata ukungu utoweke na mawingu yainuliwe, na mwanga wa jua wa siku isiyo na wingu ung’ae—hii ni kazi ngumu, lakini ni kazi ya Mungu na kazi bora ya mwanadamu. Kamwe taabu ya mkono, ya kichwa na ya moyo haikutumika bure kidogo kuliko inapotumika katika kuomba. Ni vigumu kungoja na kukaza na kuomba, bila kusikia sauti yo yote, lakini kudumu hata Mungu ajibu. Furaha ya maombi yaliyojibiwa ni furaha ya mama aliye katika utungu mtoto mwanamume anapozaliwa ulimwenguni, furaha ya mtumwa ambaye minyororo yake imekatika vipande vipande na ambaye uzima mpya na uhuru vimemjia sasa hivi.

Mtazamo wa jumla wa yale yaliyotimizwa kwa maombi unaonyesha kile tulichopoteza wakati majira ya maombi halisi yalipobadilishwa kwa kujifanya na kwa unafiki wa Kifarisayo; unaonyesha pia jinsi ilivyo kuu haja ya wanaume na wanawake watakatifu watakaojitoa kwa kuomba kwa bidii, kama Kristo alivyoomba.

Si jambo jepesi kuomba. Nyuma ya kuomba hayana budi kuwapo masharti yote ya maombi. Masharti hayo yawezekana, lakini hayanyakuliwi kwa dakika moja na wasioomba. Yaweza kuwapo sikuzote kwa walio waaminifu na watakatifu, lakini hayawezi kuwako ndani ya roho ya upuuzi, ya uzembe na ya ulegevu, wala kutimizwa nayo. Maombi hayasimami peke yake. Si tendo lililotengwa. Maombi husimama katika uhusiano wa karibu na wajibu wote wa utauwa wenye bidii. Ni matokeo ya tabia iliyoundwa kwa viungo vya imani yenye nguvu na yenye mamlaka. Maombi humheshimu Mungu, hukiri kuwako kwake, huitukuza nguvu zake, huyaabudu maongozi yake, hujipatia msaada wake. Nusu-ukanaji wa kiakili wenye dharau hupiga kelele dhidi ya ibada, kwamba haifanyi kitu ila kuomba. Lakini kuomba vizuri ni kufanya mambo yote vizuri. Ikiwa ni kweli kwamba ibada haifanyi kitu ila kuomba, basi haifanyi kitu kabisa. Kutokufanya kitu ila kuomba ni kushindwa hata kuomba, kwa maana masharti ya maombi yanayotangulia, yanayoambatana nayo, na yanayofuata si kitu kingine ila jumla ya nguvu zote zilizotiwa uhai za utauwa wa kivitendo, wenye kufanya kazi.

Uwezekano wa maombi huenda sambamba na ahadi za Mungu. Maombi hufungua njia ya kutokea kwa ahadi, huviondoa vizuizi katika njia ya kutimizwa kwake, huziweka katika hali ya kufanya kazi, na hujipatia makusudi yake ya neema. Zaidi ya hayo, maombi, kama imani, hujipatia ahadi, hupanua utendaji wake, na huongeza kipimo cha matokeo yake. Ahadi za Mungu zilikuwa kwa Ibrahimu na kwa uzao wake, lakini matumbo mengi tasa, na vizuizi vingi vidogo vilisimama katika njia ya kutimizwa kwa ahadi hizo; lakini maombi yaliviondoa vyote, yakazifanyia ahadi njia kuu, yakaongeza wepesi na upesi wa kutimizwa kwake, na kwa maombi ahadi iling’aa angavu na kamilifu katika kutimizwa kwake.

Uwezekano wa maombi waonekana katika kujiunga kwake na makusudi ya Mungu, kwa maana makusudi ya Mungu na kuomba kwa mwanadamu ni muungano wa nguvu zote zenye uweza na zenye uweza wote. Zaidi ya hayo, uwezekano wa maombi waonekana katika ukweli kwamba hubadilisha makusudi ya Mungu. Ni katika asili yenyewe ya maombi kusihi na kutoa maagizo. Maombi si kukana tu. Ni nguvu halisi itendayo. Kamwe hayaasi dhidi ya mapenzi ya Mungu, kamwe hayagongani na mapenzi hayo, lakini ni dhahiri kwamba hutafuta kubadilisha kusudi la Mungu. Kristo alisema, “Kikombe alichonipa Baba, je! Mimi nisikinywe” na bado alikuwa ameomba usiku ule ule, “Ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke.” Paulo alitafuta kubadilisha makusudi ya Mungu kuhusu mwiba katika mwili wake. Makusudi ya Mungu yalikuwa yamekazwa kuwaangamiza Israeli, na maombi ya Musa yakabadilisha makusudi ya Mungu na kuwaokoa Israeli. Katika wakati wa Waamuzi Israeli walikuwa wameasi na kuonewa sana. Walitubu na kumlilia Mungu, naye akasema: “Lakini mmeniacha mimi, na kuitumikia miungu mingine; basi sitawaokoa tena:” lakini walijinyenyekeza, wakaiondoa miungu yao ya kigeni, na Mungu, “roho yake ikahuzunika kwa sababu ya mashaka ya Israeli,” naye akawapelekea wokovu kwa mkono wa Yeftha.

Mungu alimtuma Isaya kumwambia Hezekia, “Tengeneza mambo ya nyumba yako; kwa maana utakufa, wala hutapona.” naye Hezekia akaomba, na Mungu akamtuma Isaya arudi kusema, “Nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako miaka kumi na mitano.” “Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa,” ndio ujumbe wa Mungu kwa kinywa cha Yona. Lakini Ninawi ulimlilia Mungu kwa nguvu, na “Mungu akaghairi katika habari ya mabaya aliyosema ya kwamba atawatenda; wala hakuyatenda.”

Uwezekano wa maombi waonekana katika hali mbalimbali yanazozifikia na makusudi mbalimbali yanayoyatimiza. Eliya aliomba juu ya mtoto aliyekufa, naye akahuika; Elisha alifanya vivyo hivyo; Kristo aliomba kaburini pa Lazaro, naye Lazaro akatoka. Petro alipiga magoti akaomba kando ya Dorkasi aliyekufa, naye akafumbua macho yake akaketi, na Petro akamweka hai mbele ya kundi lililokuwa na huzuni. Paulo alimwombea Publio, akamponya. Kuomba kwa Yakobo kuligeuza chuki ya kuua ya Esau kuwa mabusu ya kukumbatiana kwa upole kabisa wa kindugu. Mungu alimpa Rebeka Yakobo na Esau kwa sababu Isaka alimwombea. Yusufu alikuwa mtoto wa maombi ya Raheli. Kuomba kwa Hana kulimpa Israeli Samweli. Yohana Mbatizaji alipewa Elisabeti, ingawa alikuwa tasa na amepita umri, kwa kujibu maombi ya Zakaria. Kuomba kwa Elisha kuliwaletea Israeli njaa au mavuno; kama alivyoomba ndivyo ilivyokuwa. Kuomba kwa Ezra kulimpeleka Roho wa Mungu kwa kuhakikisha dhambi kunakovunja moyo katika mji mzima wa Yerusalemu, na kuwarudisha kwa Mungu katika machozi ya toba. Kuomba kwa Isaya kulikirudisha kivuli cha jua madaraja kumi nyuma katika madaraja ya Ahazi.

Kwa kujibu kuomba kwa Hezekia malaika aliwaua watu mia moja themanini na tano elfu wa jeshi la Senakeribu katika usiku mmoja. Kuomba kwa Danieli kulimfungulia maono ya unabii, kukamsaidia kuyasimamia mambo ya ufalme mkuu, na kukamtuma malaika kufunga vinywa vya simba. Malaika alitumwa kwa Kornelio, na Injili ikafunguliwa kupitia yeye kwa ulimwengu wa Mataifa, kwa sababu maombi yake na sadaka zake zilikuwa zimepanda mbele za Mungu, kama malaika alivyomwambia: “Maombi yako yamepanda kuwa ukumbusho mbele za Mungu.” “Nami niseme nini zaidi? Kwa maana wakati hautanitosha kuwasimulia habari za Gideoni, na Baraka, na Samsoni, na Yeftha; na Daudi, na Samweli, na manabii;” na za Paulo na Petro, na Yohana na Mitume, na kundi takatifu la watakatifu, wanamatengenezo, na mashahidi waliokufa kwa ajili ya imani, ambao kwa kuomba, “walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka makali ya upanga, walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.”

Maombi humtia Mungu katika jambo kwa nguvu ya mamlaka: “Niulizeni mambo yatakayokuja katika habari za wana wangu,” asema Mungu, “na katika habari ya kazi ya mikono yangu niagizeni.” Tumeagizwa katika Neno la Mungu “kuomba sikuzote,” “katika kila neno kwa kusali,” “mkidumu katika kuomba,” “waombe kila mahali,” “mkiomba kila wakati.” Ahadi haina mipaka kama vile amri ilivyo pana. “Yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapata,” “lo lote mtakaloomba,” “Mkiniomba neno lolote.” “Ombeni mtakalo lote, nanyi mtatendewa.” “Lo lote mtakalomwomba Baba, atawapa.” Ikiwa kuna jambo lo lote lisilomo katika “yo yote,” au lisiloonekana katika maneno “neno lolote,” basi mambo hayo yaweza kuachwa nje ya maombi. Lugha isingeweza kufunika eneo pana zaidi, wala kuyahusisha kwa ukamilifu zaidi mambo yote madogo madogo. Maneno haya ni mifano tu ya uwezekano wa maombi unaoyakumbatia mambo yote chini ya ahadi za Mungu kwa wale wanaoyatimiza masharti ya kuomba kwa haki.

Hata hivyo, mafungu haya yanatoa tu muhtasari wa jumla wa maeneo makubwa ambayo maombi huyatawala. Zaidi ya hayo, matokeo ya maombi hufika na kujipatia mema kutoka maeneo yasiyoweza kupitiwa kwa lugha wala kwa mawazo. Paulo aliimaliza lugha na mawazo katika kuomba, lakini akijua kuwa yapo mahitaji yasiyofunikwa na milki za mema zisizofikiwa, huyafunika maeneo hayo yasiyopenyeka na yasiyogunduliwa kwa ombi hili la jumla, “kwake yeye mwenye kuweza kufanya nyingi mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu.” Ahadi ni hii, “Niite, nami nitakuitikia, nitakuambia mambo makubwa, magumu, usiyoyajua.”

Yakobo atangaza kwamba “kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, kukiwa kwa bidii.” Kwafaa kiasi gani hakuweza kusema, lakini anakieleza kwa nguvu ya kuomba kwa Agano la Kale ili kuwachochea watakatifu wa Agano Jipya kuwaiga wale watu watakatifu wa zamani kwa bidii na mvuto wa kuomba kwao, na kuirudia na kuipita nguvu ya kuomba kwao. Eliya, asema, alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, naye akaomba kwa bidii mvua isinyeshe; na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.

Katika Ufunuo wa Yohana viumbe vyote vya chini vya Mungu na utawala wake wa maongozi, Kanisa na ulimwengu wa malaika, wako katika hali ya kungoja ufanisi wa maombi ya watakatifu walioko duniani ili kuyaendeleza mambo mbalimbali ya dunia na ya mbinguni. Malaika anachukua moto uliowashwa na maombi na kuutupa duniani, “kukawa na sauti, na radi, na umeme, na tetemeko la nchi.” Maombi ndiyo nguvu inayozaa mashtuko haya yote, na misukosuko, na mitetemo. “Uniombe,” asema Mungu kwa Mwanawe, na kwa Kanisa la Mwanawe, “nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, na miisho ya dunia kuwa milki yako.”

Watu waliomfanyia Mungu mambo makuu sikuzote wamekuwa hodari katika maombi, wameufahamu vema uwezekano wa maombi, na kuutumia kwa ukamilifu. Mwana wa Mungu, aliye wa kwanza wa wote na mwenye nguvu kuliko wote, ametuonyesha uwezekano wa maombi ulio na uweza wote na unaofika mbali. Paulo alikuwa hodari kwa ajili ya Mungu kwa sababu alijua jinsi ya kuzitumia, na jinsi ya kuwafanya wengine wazitumie, nguvu kuu za kiroho za maombi.

Maserafi, wanaowaka moto, wasiolala, wanaoabudu, ndio mfano wa maombi. Maombi hayazuiliki katika bidii yake, yamejitoa wakfu, wala hayachoki. Viko vizuizi vya maombi ambavyo hakuna kitu kiwezacho kuvishinda ila mwali safi na mkali. Ziko taabu na gharama na saburi ambazo hakuna kitu kiwezacho kuzistahimili ila mwali wenye nguvu kuliko yote, wenye bidii kuliko yote. Maombi yaweza kuwa ya sauti ya chini, lakini hayawezi kuwa ya sauti baridi. Maneno yake yaweza kuwa machache, lakini hayana budi kuwa ya moto. Hisia zake zaweza zisiwe za haraka ya pupa, lakini hazina budi kuwa za moto mweupe. Ni kuomba kunakofaa sana, kukiwa kwa bidii, ndiko kunakomwathiri Mungu.

Nyumba ya Mungu ni nyumba ya sala; kazi ya Mungu ni kazi ya maombi. Ni wivu kwa ajili ya nyumba ya Mungu na wivu kwa ajili ya kazi ya Mungu unaoifanya nyumba ya Mungu kuwa tukufu na kazi yake kudumu.

Vyumba vya maombi vya watakatifu vinapofungwa au kuingiwa kwa kawaida tu au kwa ubaridi, ndipo viongozi wa Kanisa huwa wa kidunia, wa kimwili, wa kupenda vitu; tabia ya kiroho hushuka hata kiwango cha chini, na huduma hufungwa na kudhoofishwa.

Maombi yanapoanguka, ulimwengu hushinda. Maombi yanapokoma Kanisa hupoteza tabia zake za Kimungu, nguvu zake za Kimungu; Kanisa humezwa na mfumo wa kidini wenye kiburi, nao ulimwengu hudhihaki udhaifu wake ulio wazi.