Sura 5 · dakika 2 za kusoma
Kuulima Roho wa Maombi
Chochote unachokilima kwa makusudi hukua!
Roho wa Maombi ni nani?
“Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu; kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” Warumi 8:26 Roho wa maombi ni Roho Mtakatifu, naye ndiye anayetuombea. Kupitia kwetu, huidumisha hali ya maombi katika maisha yetu. Kila mtu anapaswa kuwa naye! Iwe tunatambua au la, hutenda kazi kwa nguvu ndani yetu, na pasipo yeye, hakuna jambo linaloweza kufanyika kwa ukamilifu.
Tunampokea na kumkaribisha kwa shauku. Tunampokea kwa njia ile ile tuliyompokea Bwana Yesu Kristo katika maisha yetu; kwa imani. Huwezi kufanya tendo lolote ili kumpata Roho Mtakatifu, hata matendo mema hayawezi kumfanya aje wala kukujaza. Ni kwa shauku na imani.
Roho Mtakatifu ni wa ajabu kweli kweli. Ikiwa una kiu, atakutosheleza. Utajikuta ukiomba bila kukoma. Atakuongoza katika maono, mipango, na makusudi yake. Atajidhihirisha kupitia kwako katika maombi, nawe utajua kwamba yuko kazini! Kila mtu anahitaji kuwa na Roho wa maombi kwa sababu yeye ni kiongozi mkamilifu katika mambo yote.
Mtu anaweza kusema: “Nimeomba na kumkaribisha roho wa maombi ayaathiri maisha yangu, lakini sioni mabadiliko yoyote.” Nitalijibu hili kwa mfano wa mama anayetaka watoto wake wampokee Bwana Yesu na kuzaliwa mara ya pili. Anaomba watoto wake wamwone Yesu ili waweze kwenda kanisani kama familia nzima. Je, umeona tatizo linatoka wapi? Tatizo liko katika sababu/nia ya kuomba. Ni jambo la ajabu kuomba roho zije kwa Kristo, lakini ikiwa nia ni kwa ajili ya starehe ya binafsi, huacha kuwa maombi yenye nguvu kwa sababu ni ya ubinafsi. “Mwaomba wala hampati, kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.”
Yakobo 4:3. Lengo letu linapaswa kuwa katika uzima wa milele. Labda hii ndiyo sababu mtu hajaona mabadiliko yoyote hata baada ya kuomba kwa ajili ya Roho wa maombi. Unapomwombea rafiki yako, mwalimu, dada au mtu mwingine yeyote, kumbuka daima kuwa na sababu sahihi kwa kile unachokiombea.
Basi tunawezaje kuulima Roho wa Maombi? Tunawezaje kunufaika kikamilifu na Roho Mtakatifu? Tunawezaje kuukuza Roho wa Maombi?
1. Kwa kuomba kila wakati katika Roho, ukiwa na imani, na kudhihirisha kwamba unaenenda kwa imani wala si kwa kuona. Hii ina maana kwamba waweza kuyaita yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. Waweza kuiamuru hali ibadilike kwa sababu nguvu zimo ndani yako. Wewe una nguvu kuliko majeshi 10,000! Una nguvu kuliko malaria, vidonda vya tumbo, saratani, homa ya ini, fibroidi, VVU, selimundu, uvimbe, na ugonjwa au maradhi mengine yoyote. Bwana asifiwe! Omba katika Roho, funua siri kwa sababu una nguvu za kuleta mabadiliko katika maisha yako.
2. Tunaulima Roho wa maombi kwa kulitafakari Neno la Mungu. Kupitia hilo, Roho Mtakatifu aweza kuchochewa na kutufanya tuombe kwa bidii. Kadiri unavyolisoma Neno, ndivyo unavyolijua zaidi, na ikiwa waweza kukitenda kile ulichokijua, na kulitafakari daima, huwezi kamwe kukata tamaa wala kupungukiwa. Unakua siku zote kwa sababu unajilisha na kulitenda neno la Mungu, na hilo huuchochea Roho wa Maombi. Magonjwa hayawezi kustawi katika hali kama hizo, maradhi hayawezi, wala huzuni, hukumu, au wasiwasi!