Sura 4 · dakika 5 za kusoma
Kuomba Katika Roho
Sisi si wa ulimwengu huu, kwa hiyo hatuenendi kwa kanuni zake. Basi, na tuseme lugha ya uraia wetu — lugha ya Roho.
Kwanza, mwanadamu kimsingi ni roho yenye nafsi, anayeishi katika mwili wa kimwili. Mtu akiungama kwa kinywa chake kwamba Yesu ni Bwana, na kuamini moyoni mwake kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, mtu huyo ataokoka (Warumi 10:8-9). Mwanadamu huyu ndipo hutengwa na wengine. Wakorintho wa Pili 5:17 husema: “Kwa hiyo, mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya. Ya kale yamepita; tazama, yamekuwa mapya.” Anakuwa kiumbe kipya, mtu wa ajabu, mtu mwenye uzima wa Mungu, mtu ambaye hawezi kamwe kupungukiwa maishani. Kwa hili, sasa yumo katika ufalme wa Mungu, na ndipo mahali pake. Kwa hiyo inakuwa jambo la muhimu sana kwake kuijua lugha ya mahali atokako, kwa sababu inaweza kumsaidia kuendelea kufahamu yanayotokea katika Ufalme.
Mtu awezaje kuijua au kuijifunza lugha hiyo? Waweza kuuliza.
Kiumbe hiki kipya, mtu huyu wa ajabu, amepewa lugha ya roho iliyoumbwa upya. Hiyo ni kunena kwa lugha nyingine. Baadhi ya tafsiri za Biblia huieleza kwa namna tofauti na kusema kuwa ni lugha ya malaika. Lugha hii haifundishwi na wanadamu bali hutolewa na Mungu, kwa hiyo wanadamu wa kawaida hawawezi kuielewa kwa sababu ni lugha ya kimungu itokayo kwa Mungu. Je, si jambo zuri kunena lugha ambayo Mungu anaijua vyema kabisa na hata Shetani hawezi kuelewa hata neno moja? Hii ndiyo kuomba katika Roho. Ni jambo la kupendeza mno!
Tena, waweza kuuliza, nianzeje kunena lugha hii, kunena kwa lugha nyingine? Mojawapo ya majibu ni kumwomba Mungu akujaze Roho Mtakatifu, ambako huambatana na kunena kwa lugha, na katika kufanya hivyo, amini kwamba amekujibu kisha uanze kunena kwa lugha nyingine. Kama ilivyotajwa awali, usiwe na shaka. Jibu jingine ni kwa kuwekewa mikono kama inavyoonekana katika Matendo 19:6 “Hata Paulo alipowawekea mikono yake, Roho Mtakatifu akawajilia; wakaanza kunena kwa lugha na kutabiri.”
Maswali mengine yaweza kuja bado: “Je, kila muumini ni lazima anene kwa lugha, au ni kwa ajili ya wateule tu? Nini hutokea tusipoomba kwa lugha? Je, hatuna Roho Mtakatifu ikiwa hatuombi kwa lugha? Kuna faida gani ya kuomba kwa lugha?” Basi na tuingie moja kwa moja katika maelezo, sivyo?
Je, ni lazima waumini wote wanene kwa lugha?
Swali hili ni kama kuuliza kama ni lazima mtu ale chakula. Mtu aweza kula, au asile, lakini kutokula chakula kwa muda mrefu kwaweza kuudhuru mwili.
Yesu alipokuwa akiondoka kuelekea Mbinguni, alisema: “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio: kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka kwa mikono yao; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.” Marko 16:17. Hii ina maana kwamba kunena kwa lugha hakuzuiliwi kwa watu maalum; ni kwa ajili ya wote wamwaminio Bwana Yesu Kristo. Mtu yeyote asikilaumu wala kusema kuwa ni kwa ajili ya watu fulani tu. Kwa kuwa wewe ni roho na Mungu naye ni Roho, kunena lugha ya roho kwapaswa kuwa kipaumbele.
Kunena kwa lugha ni ishara kwamba mtu amejazwa Roho. Wanafunzi walikuwa wakimngojea Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste. Walikuwa mahali pamoja kwa nia moja.
Ndimi zilizogawanyika kama za moto zilikaa juu ya kila mmoja wao. Tazama Matendo 2:4. “Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”
Katika Agano la Kale, Roho Mtakatifu aliwajilia wafalme, makuhani, na waamuzi ili waweze kutimiza kazi na kuwafundisha watu wa Mungu. Hivyo kwanza alikaa juu yao kama ndimi za moto. Baadaye, aliwajaza. Lakini katika Agano Jipya, Roho Mtakatifu anakaa ndani yetu na kutufanya kuwa hekalu lake. Anakujilia ili akujaze. Ushahidi kwamba umejazwa Roho Mtakatifu ni ushahidi wa ishara ya kunena kwa lugha. Kuwa na Roho Mtakatifu na kujazwa Roho Mtakatifu si mambo yaliyo sawasawa. Wale waliojazwa Roho Mtakatifu hunena kwa lugha nyingine. Kwa hiyo, kunena kwa lugha hakuwahusu wachungaji, Maaskofu, na wainjilisti peke yao, ni kwa ajili ya kila mmoja.
Kwa nini basi unapaswa kunena kwa lugha?
1. Hukujenga “Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake, bali yeye atabiriye hulijenga kanisa.” 1 Wakorintho 14:4. Kujenga maana yake ni kuimarisha, kusimika, na kuthibitisha. Yuda 1:20 (AMP) husema: “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya [msingi wa] imani yenu iliyo takatifu kabisa [mkiendelea daima, mkiinuka kama jengo juu zaidi na zaidi], ombeni katika Roho Mtakatifu.” Hivyo anatuambia tujijenge katika imani iliyo takatifu kabisa, tukiomba katika Roho Mtakatifu. Ndivyo kuomba kwa lugha kulivyo muhimu. Unaponena kwa lugha, unajengwa, nawe unakuwa mkubwa kuliko hali unazokabiliana nazo. Ni jambo zuri, sivyo?
Je, unakabiliwa na changamoto au hali inayoonekana kutokuwa na suluhisho? Je, ni kuhusu afya yako, familia yako, jamii yako, au taifa? Una uwezo wa kuleta mabadiliko katika kila jambo linalokuhusu. Nena kwa lugha, endelea kunena kwa lugha, na mabadiliko yataletwa.
Haleluya!
2. Kunena kwa lugha kukuchaji nguvu Katika kitabu hicho hicho cha 1 Wakorintho, yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake. Neno hili pia lina maana ya kuchaji nguvu. Unaponena kwa lugha nyingine, unazalisha nguvu na uwezo.
Je, ulijichaji nguvu asubuhi? Unapokwenda darasani, jichaji nguvu. Kabla ya kwenda kanisani, jichaji nguvu. Utakapoanza kusoma, utafanya vyema kwa sababu umejichaji nguvu. Msifuni Bwana!
4. Kunena kwa lugha nyingine kukuburudisha Kama Mkristo, wakati wowote unapohisi haja ya kutulia, labda akili yako inapolemewa na jambo lolote, suala lolote, kunena kwa lugha kunakuburudisha. Mungu aweza kusema nawe, kukuongoza, na kukuletea amani wakati huo. “Kwa maana kwa midomo ya watu wa lugha ngeni na kwa ulimi mgeni Bwana atasema na watu hawa” Isaya 28:11.
5. Kunena kwa lugha kunatuwezesha kushirikiana na Roho Mtakatifu Tunaponena kwa lugha, tunanena lugha ya Roho Mtakatifu. Ni njia ya kuhusiana naye na kupokea hekima yake, ujasiri, na uthabiti. Ndiyo sababu kila mmoja anapaswa kunena kwa lugha. Unaponena kwa lugha mara kwa mara, huwezi kamwe kushindwa. Utajua la kufanya nawe utaongozwa na Mungu wa Mbingu na Nchi, akihakikisha unabaki katika njia iliyo sawa. Haleluya!