Sura 13 · dakika 8 za kusoma
Namna ya Mwandishi
KUHUSU
JINSI YA KUTUMA SEHEMU YAKE YA PILI
YA
MSAFIRI
Nenda sasa, Kitabu changu kidogo, kila mahali
Ambapo Msafiri wangu wa kwanza amekwisha onyesha uso wake:
Bisha mlangoni pao: kama mtu akiuliza, Ni nani huyo?
Ndipo ujibu wewe, Kristiana yuko hapa.
Wakikualika uingie, basi ingia wewe,
Pamoja na wavulana wako wote; kisha, kama ujuavyo,
Waeleze wao ni nani, na tokea wapi walikotoka;
Labda watawatambua kwa sura zao, au jina lao:
Lakini kama hawatambui, waulize tena kwa mara nyingine,
Kama zamani hawakumkaribisha
Mmoja Mkristo, Msafiri? Kama watasema
Naam walimkaribisha, na kufurahia njia yake;
Basi wajulishe kuwa hawa walikuwa jamaa
Zake; naam, ni mke wake na watoto wake.
Waeleze, kuwa wameacha nyumba na makao yao;
Wamekuwa Wasafiri; wanatafuta ulimwengu ujao;
Kwamba wamekutana na machungu njiani;
Kwamba wanakabiliwa na taabu usiku na mchana;
Kwamba wamekanyaga nyoka; wamepigana na mashetani;
Tena wameshinda maovu mengi;
Naam, waeleze pia juu ya wale waliofuata,
Ambao kwa kuipenda safari, walikuwa hodari na jasiri
Watetezi wa njia hiyo; na jinsi bado
Wanavyoukataa ulimwengu huu ili kutimiza mapenzi ya Baba yao.
Nenda uwaeleze pia juu ya vitu vile vitamu
Ambavyo safari humletea Msafiri.
Waache wafahamu pia, jinsi walivyo
Wapendwao na Mfalme wao, chini ya ulinzi wake;
Makao mema kama nini awaandalia;
Ijapokuwa hukutana na pepo kali na mawimbi yavimbayo,
Ni utulivu wa ajabu kama nini watakaoufurahia mwishoni,
Wao washikamanao na Bwana wao, na kwa njia zake.
Labda kwa moyo na mkono watakukumbatia
Wewe, kama walivyomkumbatia mzaliwa wangu wa kwanza; nao watakupamba
Wewe na wenzako kwa furaha na karamu,
Ionyeshayo vema, kuwa wao ni wapenzi wa Wasafiri.
Pingamizi la kwanza
Lakini itakuwaje wasiponisadiki
Kuwa mimi ni wako kweli? kwa kuwa wako baadhi
Wanaomwiga Msafiri na jina lake kwa udanganyifu,
Wakitafuta, kwa kujigeuza, kuonekana kama yeye hasa;
Na kwa njia hiyo wamejiingiza
Mikononi na nyumbani mwa watu nisiowajua.
jibu
Ni kweli, wapo waliojaribu, siku hizi, kumwiga
Msafiri wangu, wakayaweka majina yangu juu ya vyao;
Naam, wengine nusu ya jina langu, na cheo changu pia,
Wameyashona katika vitabu vyao, ili viuzike.
Lakini bado wao, kwa sura zao, hujionyesha
Kuwa si wangu, wawe wa nani wao.
Ukikutana na hao, basi njia yako pekee
Mbele yao wote, ni, kunena unenalo
Kwa lugha yako ya asili, ambayo hakuna mtu
Aitumiaye sasa, wala aiwezaye kuiga kwa urahisi.
Kama, baada ya yote, bado watakutilia shaka,
Wakidhani kuwa wewe, kama wahamaji, wazunguka,
Kwa hila mbaya ili kuinajisi nchi;
Au kwamba unatafuta kuwadanganya watu wema
Kwa mambo yasiyofaa; nitume mimi,
Nami nitashuhudia kuwa ninyi ni wasafiri;
Naam, nitashuhudia kuwa ninyi peke yenu
Ndio Wasafiri wangu, na hilo pekee latosha.
Pingamizi la pili
Lakini bado, labda, nitamuulizia yeye
Kwa wale wamtakiao maangamizi ya nafsi na mwili.
Nitafanya nini, nifikapo mlango kama huo
Kuuliza Wasafiri, nao wazidi kughadhibika?
jibu
Usijitie hofu, Kitabu changu, kwa vitisho kama hivyo
Si kitu ila hofu zisizo na msingi.
Kitabu cha Msafiri wangu kimesafiri bahari na nchi kavu,
Lakini sijapata kamwe kufahamu
Kuwa kilidharauliwa au kufukuzwa mlangoni
Na ufalme wo wote, wawe matajiri au maskini.
Katika Ufaransa na Flanders, ambako watu huuana,
Msafiri wangu huhesabiwa rafiki, na ndugu.
Katika Uholanzi, nako, husemwa, kama niambiwavyo,
Msafiri wangu kwa wengine, wa thamani kuliko dhahabu.
Watu wa nyanda za juu na Waayalandi wa porini hukubaliana
Kuwa Msafiri wangu awe rafiki yao wa karibu.
Huko New England amepandishwa hadhi hivyo,
Apokea huko upendeleo mwingi wa upendo,
Hata kunakshiwa, kuvikwa mavazi mapya, na kupambwa kwa vito,
Ili aonyeshe sura zake, na viungo vyake.
Tena zaidi: kwa uzuri kama nini Msafiri wangu atembeavyo,
Hata maelfu humwimbia na kumnena kila siku.
Ukikaribia zaidi nyumbani, itaonekana
Msafiri wangu hana sababu ya aibu wala hofu:
Mji na shamba watamkaribisha,
Kwa maneno, Karibu, Msafiri; naam, hawawezi kujizuia
Kutabasamu, Msafiri wangu akiwa karibu tu,
Au akijitokeza katika kundi lo lote.
Mashujaa hodari humkumbatia na kumpenda Msafiri wangu,
Humthamini sana, naam, humwona bora kuliko
Vitu vikubwa zaidi; naam, kwa furaha
Husema, mguu wa cheche wangu ni bora kuliko mwewe mzima.
Wanawali, na wanawake vijana pia,
Humwonyesha Msafiri wangu wema si haba;
Makasha yao, vifua vyao, na mioyo yao,
Msafiri wangu ameyapata; kwa kuwa huwapa
Vitendawili vyake vizuri kwa mahadhi yenye afya,
Vitoavyo faida maradufu ya taabu yao
Ya kusoma; naam, nadhani naweza kuthubutu
Kusema baadhi humthamini kupita dhahabu yao.
Hata watoto watembeao barabarani,
Wakikutana tu na Msafiri wangu mtakatifu,
Watamsalimu; watamtakia mema, na kusema,
Yeye ndiye kijana bora wa zama hizi.
Wale wasiomwona kamwe, hata hivyo huvutiwa
Na yale waliyoyasikia juu yake, na kutamani sana
Kuwa naye pamoja, na kumsikia akisimulia
Zile hadithi za Wasafiri azijuazo vema hivyo.
Naam, baadhi wasiompenda mwanzoni,
Bali walimwita mpumbavu na mjinga, husema ni lazima,
Sasa wamemwona na kumsikia, wamsifu
Na kwa wale wawapendao humpeleka.
Kwa hiyo, Sehemu yangu ya Pili, huhitaji kuwa
Na hofu ya kujitokeza: hakuna awezaye kukudhuru,
Miongoni mwa wamtakiao mema yule aliyetangulia;
Kwa kuwa waja nyuma na hazina ya pili
Ya vitu vizuri, vyenye utajiri, vyenye faida,
Kwa vijana, kwa wazee, kwa wayumbao, na kwa waliothibiti.
Pingamizi la tatu
Lakini wako wasemao, Hucheka kwa sauti kubwa mno
Na wengine husema, Kichwa chake ki katika wingu.
Wengine husema, Maneno yake na hadithi zake ni giza mno,
Hawajui jinsi, kwa hayo, ya kuyafikia makusudio yake.
jibu
Yaweza, nadhani, kusemwa, Vicheko vyake na vilio vyake
Vyaweza kutambuliwa kwa macho yake yenye machozi.
Baadhi ya mambo ni ya namna hiyo, hata kuufanya
Moyo wa mtu ucheke, hali moyo wake wauma:
Yakobo alipomwona Raheli wake na kondoo,
Wakati mmoja alibusu na kulia.
Ijapokuwa wengine husema, Kuna wingu kichwani mwake;
Hilo laonyesha tu kuwa hekima yake imefunikwa
Kwa mavazi yake yenyewe—na ili kuuchochea moyo
Kuyatafuta vema yale ungependa kuyapata,
Mambo yaonekanayo kufichwa katika maneno yasiyo dhahiri
Huuvutia zaidi tu moyo wa mcha-Mungu
Kuchunguza yale maneno yapasavyo kuwa nayo,
Yanenayo kwetu kwa mfumo wenye giza kama huo.
Tena najua kuwa mfano wenye giza
Huingia zaidi katika moyo utafutao,
Nao hushikamana zaidi moyoni na kichwani,
Kuliko mambo yasiyotolewa katika mifano.
Kwa hiyo, Kitabu changu, kutokati tamaa ko kote
Kusizuie safari zako. Tazama, umetumwa
Kwa rafiki, si adui; kwa rafiki watakaokupa nafasi
Wewe, wasafiri wako, na kuyakumbatia maneno yako.
Zaidi ya hayo, yale Msafiri wangu wa kwanza aliyoyaficha,
Wewe, Msafiri wangu jasiri wa pili, umeyafunua;
Yale Mkristo aliyoyafunga, akaenda zake,
Kristiana mpole huyafungua kwa ufunguo wake.
pingamizi la nne
Lakini wengine hawapendi mtindo wa wako wa kwanza:
Huuhesabu kuwa hadithi za kubuni; wautupa kama vumbi.
Nikikutana na hao, niseme nini?
Je, niwadharau kama wanivyodharau, au sivyo?
jibu
Kristiana wangu, ukikutana na hao,
Kwa vyo vyote, wasalimu kwa upendo wote;
Usiwalipe matukano kwa matukano,
Bali, wakikunja uso, nakusihi uwatabasamie:
Labda ni tabia yao, au habari mbaya fulani,
Iliyowafanya kudharau hivyo, au kujibu hivyo.
Wengine hawapendi samaki, wengine jibini, na wengine
Hawapendi rafiki zao, wala nyumba au makao yao;
Wengine hushtuka kwa nguruwe, hudharau kuku, hawapendi ndege
Zaidi ya wapendavyo kekeo au bundi.
Waache hao, Kristiana wangu, na hiari yao,
Ukawatafute wale watakaofurahi kukupata;
Usishindane kamwe, bali, kwa unyenyekevu mkuu,
Jionyeshe kwao katika sura yako ya Usafiri.
Basi nenda, Kitabu changu kidogo, ukawaonyeshe wote
Watakaokukaribisha na kukukaribu,
Yale utakayoyaficha mbali na wengine;
Na utamani yale utakayowaonyesha yabarikiwe
Kwao kwa mema, na kuwafanya wachague kuwa
Wasafiri, kwa aliye bora kuliko wewe au mimi.
Basi nenda, nasema, uwaambie watu wote wewe ni nani:
Sema, Mimi ni Kristiana; na fungu langu
Ni sasa, pamoja na wanangu wanne, kuwaeleza
Maana ya mtu kuchukua fungu la Msafiri.
Nenda pia, uwaambie wao ni nani na ni watu wa namna gani
Wanaosafiri pamoja nawe sasa;
Sema, Huyu ni jirani yangu Rehema: yeye ni mmoja
Aliyesafiri pamoja nami siku nyingi:
Njoni, mtazame uso wake wa ubikira, na kujifunza
Kupambanua kati ya wavivu na wasafiri.
Naam, na wasichana vijana wajifunze kwake kuuthamini
Ulimwengu ule ujao, kwa vyo vyote.
Wasichana wadogo warukarukao wamfuatapo Mungu,
Na kuwaacha wazee wapumbavu kwa fimbo yake,
Ni kama zile siku ambazo wadogo walipiga kelele
Hosana! wakati wazee walipodhihaki.
Kisha waeleze juu ya Mzee Mkweli, uliyemkuta
Akikanyaga nchi ya Msafiri kwa mvi zake;
Naam, waeleze jinsi mtu huyu alivyokuwa mnyofu wa moyo;
Jinsi alivyoubeba msalaba kumfuata Bwana wake mwema.
Labda kwa mtu fulani mwenye mvi, hili litafaulu
Kumpenda Kristo, na kuomboleza dhambi.
Waeleze pia, jinsi Bwana Mwenye-Hofu alivyoenda
Katika safari, na jinsi alivyoutumia wakati wake
Katika upweke, kwa hofu na vilio;
Na jinsi, mwishoni, alivyoushinda ujira wa furaha.
Alikuwa mtu mwema, ijapo alikuwa mzito rohoni;
Ni mtu mwema, naye anaurithi uzima.
Waeleze juu ya Bwana Akili-Dhaifu pia,
Ambaye hakwenda mbele, bali sikuzote nyuma.
Waonyeshe pia, jinsi alivyokaribia kuuawa,
Na jinsi Bwana Moyo-Mkuu alivyoyaokoa maisha yake.
Mtu huyu alikuwa mwaminifu wa moyo; ijapo dhaifu wa neema,
Mtu angeweza kusoma utauwa wa kweli usoni pake.
Kisha waeleze juu ya Bwana Tayari-Kuchechemea,
Mtu mwenye magongo, lakini asiye na hatia sana.
Waeleze jinsi Bwana Akili-Dhaifu na yeye
Walivyopendana, na kupatana sana katika maoni.
Na wote wajue, ijapokuwa udhaifu ulikuwa fungu lao,
Lakini nyakati nyingine mmoja aliweza kuimba, mwingine kucheza.
Usimsahau Bwana Shujaa-wa-Kweli,
Yule mtu wa ujasiri, ijapo kijana sana:
Mwambie kila mtu kuwa roho yake ilikuwa hodari mno,
Hakuna mtu aliyeweza kamwe kumgeuza nyuma;
Na jinsi Bwana Moyo-Mkuu na yeye wasivyoweza kuvumilia,
Bali kuibomoa Ngome ya Mashaka, na kumwua Kata-Tamaa!
Usimpuuze Bwana Vunjika-Moyo,
Wala Ogopa-Sana, binti yake, ijapo wamejilaza
Chini ya mavazi yaliyowafanya waonekane
(Kwa baadhi) kana kwamba Mungu wao amewaacha.
Walikwenda taratibu, lakini kwa uhakika; na, mwishoni,
Walimkuta Bwana wa Wasafiri kuwa rafiki yao.
Utakapokuwa umeuambia ulimwengu mambo haya yote,
Ndipo geuka, Kitabu changu, ukazigusa nyuzi hizi;
Ambazo, zikiguswa tu, zitatoa muziki wa namna hiyo,
Utakaomfanya kilema kucheza, na jitu kutetemeka.
Vile vitendawili vilivyofichwa kifuani mwako,
Vitoe kwa uhuru, uvifafanue; na kwa yale mengine
Ya mistari yako ya siri, na yabaki
Kwa wale ambao akili zao za wepesi zitayapata.
Sasa na Kitabu hiki kidogo kiwe baraka
Kwa wale wakipendao Kitabu hiki kidogo na mimi;
Na mnunuzi wake asiwe na sababu ya kusema,
Fedha yake imepotea tu au imetupwa bure.
Naam, na Msafiri huyu wa pili azae tunda lile
Litakalofaa moyo wa kila Msafiri mwema;
Na akishawishi baadhi, wapoteao,
Kuigeuza miguu na mioyo yao kuielekea njia iliyo sawa,