Sura 7 · dakika 7 za kusoma
Thawabu ya Kumpenda Mungu
NA TUONE ni faida gani tunayoipata kwa kumpenda Mungu. Ingawa twaweza kuiona hii kwa upungufu mkubwa kiasi gani, ni afadhali kuliko kuwa vipofu kwayo. Tumekwisha kunena (japo kwa namna isiyostahili utukufu wa Mungu, lakini kwa kadiri ya uwezo wetu) juu ya haki ya Mungu ya kupendwa nasi; sasa tutanena juu ya thawabu aliyoiambatanisha na kule kumpenda kwetu; kwa maana ijapokuwa yatupasa kumpenda Mungu bila kutegemea thawabu yo yote, hata hivyo tutalipwa kwa kuwa tumempenda. Upendo wa kweli hauwezi kuachwa bila ujira, ingawa si wenye choyo wala hautafuti mambo yake wenyewe. Upendo ni kutoka nje kwa nafsi, si mkataba; hautokani na maagano, wala haupatikani kwa maafikiano; huchipuka wenyewe katika misukumo yake, na hutufananisha nao; tena upendo wa kweli ni utoshelezo wake wenyewe. Thawabu yake i katika kile kinachopendwa nao; kwa maana cho chote kile tunachoonekana kukipenda, kama shabaha yetu ya kweli ni kitu kingine,
basi ni kile kitu kingine hasa tukipendacho, wala si kile ambacho kwacho moyo wetu hujitahidi kukifikia. Mtakatifu Paulo hakuihubiri Injili kwa ajili ya mkate wake wa kila siku, bali mkate uliomhifadhi hai ndio uliomwezesha kuihubiri Injili. Alichokipenda ni Injili, si mkate. Upendo wa kweli hautafuti thawabu, lakini unaistahili; ni hakika kabisa kwamba hakuna anayekusudia kulipia upendo, ingawa si kwamba unastahili thawabu yake tu, bali kwa yakini utaipata. Katika mambo ya daraja la chini, ni nani hao wanaochangamshwa na ahadi ya thawabu? Ni wale walegevu wasio na upendo. Je, yampata mtu ye yote kuwashawishi kwa malipo wale wanaowaka shauku ya kuruhusiwa kutumika? Hakuna ampaye mtu mwenye njaa fedha ili amshawishi ale, kama vile asivyompa mama mpole fedha ili amshawishi kumnyonyesha mtoto wake, au kumfanya mkulima wa mizabibu ailinde mizabibu yake, au mwenye nyumba aijenge upya nyumba yake iliyoanguka. Kwa kadiri ndogo zaidi ampendaye Mungu hahitaji kuhimizwa kwa ahadi ya thawabu ambayo si Mungu Mwenyewe; ingekuwa hivyo, basi angekuwa akiipenda ile thawabu, si Mungu.
Ni jambo la asili kwa kiumbe mwenye akili kutamani kile kinachomwonekana, kwa kadiri ya namna yake ya kufikiri, kuwa bora kuliko kile alicho nacho; na kutotosheka kamwe ikiwa kitu chema kinapungukiwa na ile sifa maalumu aipendayo. Akipenda uzuri, atatamani kile kinachomwonekana kizuri zaidi. Akijisifu kwa kumiliki johari ya thamani kubwa, atatamani kumiliki nyingine iliyo ya fahari zaidi; na mali yo yote awezayo kuwa nayo, tabia yake ni kutaka zaidi. Je, si jambo tuonalo kila siku, mwenye milki na utajiri usiokadirika kununua ardhi zaidi, wala hatosheki ila kwa kupanua mashamba yake? Wale wakaao katika majumba makubwa ya kifahari, je, hawajengi mapya siku zote, wakibadilisha daima, wakiifanya mviringo ile yenye pembe, na yenye pembe ile ya mviringo? Je, watu wenye vyeo vya juu hawatamani daima vya juu zaidi, wakijitahidi daima kupaa, kwa tamaa iliyo ngumu zaidi na zaidi kuituliza? Hakuna kikomo cha wasiwasi wa namna hiyo, kwa sababu, katika mambo yote ya jinsi hiyo, haiwezekani kufikia kilele kilicho chema na cha juu kabisa. Lakini si ajabu kwamba maadamu mtu aweza kuona mbele yake kitu kikubwa zaidi na kilicho kamili zaidi, hataridhika na milki yake mwenyewe ya kile kilicho kidogo na kibaya zaidi. Lililo la kipumbavu kupita maelezo yote ni hili — kutamani daima vitu ambavyo haviwezi hata kutuliza tamaa zetu, sembuse kuzitosheleza. Nini kifuatacho? Ni hili — kwamba moyo, ukijaribiwa na vivutio vingi vya udanganyifu, hujichokesha bure, hutamani daima, na hauhesabu kitu kile ulichokifurahia, ukilinganisha na kile ungependa sana kuwa nacho; nao huteswa, kwa tamaa ya kile usicho nacho, ukikosa furaha yote katika kile ulicho nacho. Mtu hawezi kuwa na vyote; kwa maana kwa kile kidogo kiwezekanacho kupatikana, sharti bei ya taabu ilipwe; nacho sharti kifurahiwe kwa kutetemeka; naam, kwa hakika yenye kuhuzunisha kwamba siku moja sharti kipotee, ijapokuwa tarehe ya siku hiyo haijulikani.
Nimeeleza mwenendo wa nia potovu inayotafuta kwa upofu wema ulio mkuu. Hufanya haraka bure, ikiwa mchezo wa ubatili wake wenyewe, ikidanganywa na uovu. Kwa nini kuutumia mchana wote katika juhudi zisizozaa matunda huku na huku, na kukamatwa na mauti bila kutoshelezwa? Katika taabu za namna hiyo wanajinasa wasiomcha Mungu, wanaotafuta huko na huko, kama wapumbavu, ili kupata matamanio ya nafsi zao. Huyatumia maisha yao katika jitihada zisizo na maana wala hawafiki katika furaha kamili; kwa maana wanavipenda vitu vilivyoumbwa, wala si Muumba, nao huvijaribu, kimoja kisha kingine, kabla ya kuota hata kumjaribu Bwana aliyeviumba vyote. Lakini, kama wangeweza kupata matamanio ya mioyo yao na kufikia kumiliki ulimwengu, bila Yeye aliye asili yake, hatimaye wangehisi, kwa sheria ile ile iliyoyaongoza maisha yao, kwamba Yeye ndiye lazima wawe naye, au kutopumzika kamwe. Wamekwenda kutoka tamaa moja hata nyingine, wakitamani sikuzote kitu bora zaidi; na sasa, wakiwa mabwana wa vyote vilivyo mbinguni na duniani, upesi wangeona vyote havitoshi, na kugundua kwamba walilazimika kumtafuta Yeye ambaye bado hayupo, sharti wamtafute Mungu Mwenyewe. Mara ukifikia kugundua hilo, mara ukimfikia Yeye,
kuna amani; haiwezekani kuvuka zaidi ya hapo. Nafsi sharti ipaze sauti: “ Ni vyema kwangu kumkaribia Mungu wangu;” au, “Ni nani niliye naye mbinguni ila Wewe? Wala duniani sitamani kitu ila Wewe?” na tena: “Wewe ndiwe Mungu wa moyo wangu, na fungu langu milele.” Hata kwa njia hii nafsi ingeishia kwa Mungu bila shaka kama ingeweza kujaribu kwa mfuatano vitu vyote vilivyo duni kuliko Yeye. Lakini maisha ni mafupi mno, na nguvu zingeishiwa katika jaribio la namna hiyo; tena idadi ya washindani ni kubwa mno. Isingewezekana kuvijaribu viumbe vyote na kuviona kuwa pungufu. Ingekuwa rahisi zaidi na yenye faida zaidi kuifanya kazi hii katika mawazo kuliko katika uhalisia. Akili zetu zimejaliwa ubidii na uwelewa zaidi kuliko mioyo yetu kwa ajili ya lengo hili hasa— kwamba zitangulie na kuuzuia moyo usijifunge na kile ambacho akili haikukiona kwanza kuwa cha kutamanika. “ Jaribuni mambo yote; lishikeni sana lililo jema.” La kwanza lipaswa kuandaa nafasi kwa la pili, ili moyo ufuate hukumu ya akili. La sivyo hakuna tumaini la “ kupanda mlima wa Bwana, na kukaa mahali pake patakatifu;” tena ni bure kuwa na akili yenye kufikiri, kama tukifanya kama wanyama wafanyavyo, na kutii hisia zetu tu, akili isiingilie kati. Wale wasioongozwa na akili, kwa kweli hupiga mbio katika shindano, lakini hupiga mbio bila nafasi ya kushinda.
Watashindaje, wakiona kwamba hawajali kwanza tuzo, bali huiweka hiyo mwisho wa yote? Watawezaje kufanya jingine ila kujinasa katika kizingamzinga kisicho na mwanzo wala mwisho? Sivyo kwa wenye haki. Wakionywa na lawama iliyoelekezwa kwa wale wakosao hivyo (kwa maana njia ni pana na yenye kukanyagwa sana iongozayo mautini), huichagua njia ya kifalme isiyogeukia kuume wala kushoto, kwa maana “ njia ya mwenye haki ni nyofu.” Huichukua njia iliyo fupi kabisa, wakiongozwa na neno lililo rahisi kama kurahisisha, liwaamuruo wasiyaangalie yale ambayo macho yao yaweza kuyaona, bali kuuza vyote na kuwapa maskini; kwa maana heri kweli maskini kama hao, na ufalme wa mbinguni ni wao. Bwana aijua njia ya wenye haki, naye aisifu. Aijua pia njia ya mwenye dhambi, ambayo ndani yake hana budi kuangamia. Wenye haki wana furaha katika umaskini wao, na matajiri hawatoshelezwi katika wingi wao; kwa maana mwenye hekima asema: “Apendaye utajiri hatavuna faida kwao.” Bali wale “wenye njaa na kiu ya haki watashibishwa.” Haki ndicho chakula chao cha lazima. Kwa habari ya vitu vya ulimwengu huu, nafsi hailishwi navyo zaidi ya mwili ulishwavyo na hewa. Kama tungemwona mtu mwenye njaa akivuta pumzi kwa kinywa kilichofunguka wazi, akinywa funda ndefu za upepo ili kuutuliza kiu chake, tungesema, Maskini mpumbavu! Ndivyo ilivyo kwa wale watafutao kuitosheleza nafsi kwa vitu vya ulimwenguni, ambavyo havifanyi ila kuivimbisha kama kwa upepo, wala haviilishi zaidi ya vitu vya kiroho vilishavyo miili yetu. “ Umhimidi Bwana, Ee nafsi yangu, yeye akushibishaye tamaa yako kwa mema.” Yeye akujaza kutokana na utimilifu wake; papo hapo akikupa tamaa yako, na kukuchochea kutaka zaidi. Yeye hutangulia, yeye hutegemeza, yeye hukujaza; yeye huwasha tamaa moyoni mwako, naye Mwenyewe ndiye Shabaha ya tamaa yote.
Nimesema kwamba sababu ya upendo wetu kwa Mungu ni Mungu Mwenyewe, nalo limesemwa vema, kwa maana Yeye ndiye sababu itendayo kazi na pia mwisho wa mwisho wa upendo wetu. Yeye ni wa namna ambayo haiwezekani kumjua na usimpende; wala kutokuwa na tumaini kwake; kwa maana, kama tusingekuwa na tumaini la kumpenda kwa ukamilifu huko mbele, upendo wetu wa sasa kwake ungekuwa si kitu. Upendo wetu huandaliwa na kulipwa na wake. Yeye kwanza hutupenda kutokana na wema wake uzidio; kisha hudai marejesho yastahiliyo ya upendo, na kuturuhusu wakati ujao matumaini yaliyo matukufu kupita yote. Yeye ni mkarimu kwa wale wamwitao, lakini hawezi kutoa kitu kilicho bora kuliko Yeye Mwenyewe. Yeye Mwenyewe ndiye mwisho wa ustahili wetu, na thawabu yetu. Yeye ni chakula cha nafsi takatifu, ukombozi wa wale ambao bado wamo utumwani. Ikiwa Bwana ni mwema kwa nafsi imtafutayo, basi Yeye ni nini kwa nafsi iliyomwona? Lakini hili laweza kuonekana la ajabu, kwamba hakuna awezaye kumtafuta Bwana ambaye hajakwisha kumwona; kwa maana mapenzi yake ni kuonwa ili azidi kutafutwa; na kutafutwa, ili aonwe kwa ukamilifu zaidi. Lakini, ijapokuwa aweza kutafutwa na kuonwa, hawezi kamwe kutanguliwa. Yeye siku zote ndiye wa kwanza; na kama tukisema: “Asubuhi maombi yangu yatakutangulia,” pamoja na hayo ni hakika kabisa kwamba maombi hayo yangekuwa baridi sana kama, Ee Mungu, uvuvio wako usingeyatangulia.
Tumekwisha kunena juu ya utimilifu wa upendo wa Mungu, sasa na tuone ni yapi mwanzo wake.