Ulazima wa Maombi
Maombi na Tabia na Mwenendo

Sura 9 · dakika 10 za kusoma · dakika 13 za kusikiliza

Maombi na Tabia na Mwenendo

“Jenerali Charles James Gordon, shujaa wa Khartoum, alikuwa askari Mkristo kweli kweli. Akiwa amezingirwa katika mji ule wa Sudani, alishikilia kwa ushujaa kwa mwaka mmoja, lakini, mwishowe, alishindwa na kuuawa. Juu ya ukumbusho wake katika Westminster Abbey yameandikwa maneno haya, ‘Aliwapa maskini fedha zake; wenye huzuni huruma yake; nchi yake maisha yake, na Mungu nafsi yake.’” — HOMER W. HODGE.

MAOMBI hutawala mwenendo, na mwenendo hufanya tabia. Mwenendo, ni kile tunachotenda; tabia, ni kile tulicho. Mwenendo ni maisha ya nje. Tabia ni maisha yasiyoonekana, yaliyofichwa ndani, lakini yanayothibitishwa na kile kinachoonekana. Mwenendo ni wa nje, unaoonekana kwa nje; tabia ni ya ndani — ikifanya kazi ndani. Katika mpango wa neema mwenendo ni mzao wa tabia. Tabia ni hali ya moyo, mwenendo ni kielelezo chake cha nje. Tabia ni mzizi wa mti, mwenendo, ni tunda linalozaa.

Maombi yanahusiana na karama zote za neema. Kwa tabia na mwenendo uhusiano wake ni ule wa msaidizi. Maombi husaidia kuisimika tabia na kuufinyanga mwenendo, na vyote viwili hutegemea maombi ili viendelee kwa mafanikio. Kunaweza kuwa na kiasi fulani cha tabia njema na mwenendo mwema bila maombi, lakini hakuwezi kuwa na kitu cho chote kama tabia halisi ya kidini na mwenendo wa Kikristo bila maombi. Maombi husaidia, pale ambapo misaada mingine yote hushindwa. Kadiri tunavyoomba zaidi, ndivyo tunavyokuwa bora zaidi, na maisha yetu safi zaidi na bora zaidi.

Mwisho na kusudi hasa la kazi ya upatanisho ya Kristo ni kuumba tabia ya kidini na kufanya mwenendo wa Kikristo.

“Ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wenye juhudi katika matendo mema.”

Katika mafundisho ya Kristo, si matendo ya hisani na matendo ya rehema tu anayoyasisitiza, bali tabia ya ndani ya kiroho. Hili linadaiwa, wala hakuna kilicho pungufu yake kitakachotosha.

Katika kujifunza Nyaraka za Paulo, liko jambo moja linalojitokeza, waziwazi na bila kukosea — msisitizo juu ya utakatifu wa moyo, na haki ya maisha. Paulo hatafuti sana kuendeleza kile kinachoitwa “kazi ya mtu binafsi,” wala wazo kuu la barua zake si matendo ya hisani. Ni hali ya moyo wa mwanadamu na kutokuwa na lawama kwa maisha ya mtu binafsi, ndiyo yanayounda uzito wa maandiko ya Mtakatifu Paulo.

Mahali pengine katika Maandiko pia, ni tabia na mwenendo vinavyopewa nafasi ya kwanza. Dini ya Kikristo hushughulika na watu wasio na tabia ya kiroho, na wasio watakatifu katika maisha, nayo hukusudia kuwabadilisha hivi kwamba wawe watakatifu moyoni na wenye haki maishani. Hukusudia kuwageuza watu wabaya kuwa watu wema; hushughulika na ubaya wa ndani, na hufanya kazi kuugeuza kuwa wema wa ndani. Na ni hapa hasa maombi yanapoingia na kuonyesha uwezo wake wa ajabu na matunda yake. Maombi huelekea mwisho huu hasa. Kwa kweli, bila maombi, hakuna badiliko kama hilo lisilo la kawaida katika tabia ya mtu linaloweza kamwe kutokea. Kwa maana badiliko kutoka ubaya hata wema halifanywi “kwa matendo ya haki tuliyoyatenda sisi,” bali kwa rehema ya Mungu, ambayo hutuokoa “kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili.” Na badiliko hili la ajabu huletwa kwa maombi ya bidii, ya kudumu, na ya uaminifu. Ukristo wo wote unaodaiwa, usioleta badiliko hili katika mioyo ya watu, ni udanganyifu na mtego.

Kazi ya maombi ni kubadilisha tabia na mwenendo wa watu, na mara zisizohesabika, badiliko hilo limefanywa kwa maombi. Hapa, maombi, kwa vyeti vyake, yamethibitisha uungu wake. Na kama vile ilivyo kazi ya maombi kuleta jambo hili, ndivyo ilivyo kazi kuu ya Kanisa kuwashika watu waovu na kuwafanya wema. Utume wake ni kubadilisha asili ya mwanadamu, kubadilisha tabia, kuathiri matendo, kuugeuza kabisa mwenendo. Kanisa linadhaniwa kuwa la haki, nalo linapaswa kujishughulisha na kuwageuza watu kuwa na haki. Kanisa ni kiwanda cha Mungu duniani, na wajibu wake wa kwanza ni kuumba na kukuza haki ya tabia. Hii ndiyo kazi yake ya kwanza kabisa. Kwanza kabisa, kazi yake si kupata washiriki, wala kukusanya hesabu kubwa, wala kulenga kupata fedha, wala kujishughulisha na matendo ya hisani na kazi za rehema, bali kuzaa haki ya tabia, na usafi wa maisha ya nje.

Kitu kilichotengenezwa huakisi na kushiriki tabia ya kiwanda kilichokitengeneza. Kanisa lenye haki, lenye kusudi la haki, hufanya watu wenye haki. Maombi huzaa usafi wa moyo na unyofu wa maisha. Hayawezi kuzaa kitu kingine. Mwenendo usio wa haki huzaliwa na kukosa maombi; viwili hivyo huenda pamoja. Maombi na kutenda dhambi haviwezi kuandamana pamoja. Kimoja, au kingine, sharti kwa lazima kikome. Wafanye watu waombe, nao wataacha kutenda dhambi, kwa sababu maombi huleta kuchukizwa na dhambi, na hufanya kazi juu ya moyo hivi kwamba kutenda maovu kunakuwa jambo la kuchukiza, na asili yote huinuliwa hata kuyatafakari kwa uchaji mambo yaliyo juu na matakatifu.

Maombi yamejengwa juu ya tabia. Jinsi tulivyo mbele za Mungu ndivyo kunavyopima uzito wetu kwake. Ilikuwa tabia ya ndani, wala si sura ya nje, ya watu kama Ibrahimu, Ayubu, Daudi, Musa na wengine wote, waliokuwa na uzito mkubwa hivyo kwa Mungu siku za kale. Na, leo, si sana maneno yetu, bali kile tulicho kwa kweli, kinachokuwa na uzito kwa Mungu. Mwenendo huathiri tabia, bila shaka, na una uzito mwingi katika kuomba kwetu. Wakati huo huo, tabia huathiri mwenendo kwa kiasi kikubwa zaidi sana, na ina mvuto ulio juu zaidi juu ya maombi. Maisha yetu ya ndani hayayapi tu maombi yetu rangi, bali na mwili pia. Maisha mabaya maana yake ni maombi mabaya na, mwishowe, kutokuomba kabisa. Tunaomba kwa udhaifu kwa sababu tunaishi kwa udhaifu. Mto wa maombi hauwezi kupanda juu kuliko chemchemi ya maisha. Nguvu ya chumba cha ndani hufanyizwa na nguvu inayotiririka kutoka mito inayokutana ya maisha. Na udhaifu wa maisha hutokana na ukosefu wa kina na udhaifu wa tabia.

Udhaifu wa maisha huonyesha unyonge na ulegevu wake katika saa za maombi. Hatuwezi kabisa kuzungumza na Mungu kwa nguvu, kwa ukaribu, na kwa uhakika, isipokuwa tunaishi kwa ajili yake, kwa uaminifu na kwa kweli. Chumba cha maombi hakiwezi kutakaswa kwa Mungu, wakati maisha ni mageni kwa amri zake na kusudi lake. Sharti tujifunze funzo hili vema — kwamba tabia ya haki na mwenendo ulio kama wa Kristo hutupa msimamo maalum na wa upendeleo katika maombi mbele za Mungu. Neno lake takatifu linatilia mkazo wa pekee sehemu ambayo mwenendo unayo katika kuyapa maombi yetu thamani, linapotangaza:

“Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa; kama ukiondoa kati yako nira, na kunyosha kidole, na kunena maneno ya ubatili.”

Uovu wa Israeli na matendo yao ya kuchukiza yalitajwa waziwazi na Isaya, kuwa sababu ya Mungu kuyageuzia mbali masikio yake na maombi yao:

“Nanyi mnyoshapo mikono yenu, nitawaficha macho yangu nisiwaone; naam, mtakapoomba maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.”

Kweli ile ile ya kusikitisha ilitangazwa na Bwana kwa kinywa cha Yeremia:

“Kwa hiyo, wewe usiwaombee watu hawa, wala usiwapazie kilio wala maombi kwa ajili yao; kwa maana sitawasikia wakati watakaponililia kwa sababu ya taabu yao.”

Hapa, imeelezwa waziwazi, kwamba mwenendo usio mtakatifu ni kizuizi cha kuomba kwa mafanikio, kama vile inavyodokezwa wazi kwamba, ili kuwa na njia kamili ya kumfikia Mungu katika maombi, sharti kuwe na kuiacha kabisa dhambi inayojulikana na iliyokusudiwa.

Tumeagizwa kuomba, “wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano,” nasi sharti tuupitishe wakati wa kukaa kwetu hapa kama wageni, katika kujiepusha kabisa na uovu, ikiwa tutalidumisha pendeleo letu la kumwita Baba. Hatuwezi, kwa njia yo yote, kutenganisha kuomba na mwenendo.

“Na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.”

Naye Yakobo anatangaza waziwazi kwamba watu huomba wala hawapokei, kwa sababu huomba vibaya, na kutafuta tu kutimiza tamaa za ubinafsi.

Agizo la Bwana wetu, “Kesheni ninyi, mwombe sikuzote,” ni la kuufunika na kuulinda mwenendo wetu wote, ili tupate kuja kwenye chumba chetu cha ndani na nguvu zake zote zimelindwa kwa ulinzi wa kukesha unaowekwa juu ya maisha yetu.

“Na jiangalieni nafsi zenu, mioyo yenu isije wakati wo wote ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya, siku ile ikawajia ghafula.”

Mara nyingi, uzoefu wa Kikristo huvunjikia juu ya mwamba wa mwenendo. Nadharia nzuri huharibiwa na maisha mabaya. Jambo gumu kuliko yote kuhusu utauwa, kama vile ndilo lenye kuvutia kuliko yote, ni kuweza kuuishi. Ni maisha ndiyo yenye uzito, na kuomba kwetu huumia, kama zinavyoumia sehemu nyingine za uzoefu wetu wa kidini, kwa sababu ya maisha mabaya.

Nyakati za kwanza wahubiri waliagizwa kuhubiri kwa maisha yao, au wasihubiri kabisa. Vivyo hivyo, leo, Wakristo, kila mahali, wangepaswa kuagizwa kuomba kwa maisha yao, au wasiombe kabisa. Mahubiri yenye nguvu kuliko yote, si yale yanayosikika kutoka mimbarani, bali yale yanayotangazwa kwa utulivu, kwa unyenyekevu na kwa uthabiti; yanayoonyesha uzuri wake nyumbani, na katika jamii. Kielelezo huhubiri hotuba yenye nguvu zaidi sana kuliko agizo. Mahubiri bora kuliko yote, hata mimbarani, ni yale yanayoimarishwa na maisha ya utauwa, ndani ya mhubiri mwenyewe. Kazi yenye nguvu kuliko zote inayofanywa na waumini vitini hutanguliwa na, na kuambatana na, utakatifu wa maisha, kujitenga na dunia, kukatana na dhambi. Baadhi ya miito yenye nguvu kuliko yote hutolewa kwa midomo iliyonyamaza — na baba wacha Mungu na mama watakatifu ambao, kandokando ya moto wa nyumbani, walimcha Mungu, walipenda kazi yake, na kila siku waliwaonyesha watoto wao na wengine waliowazunguka, uzuri na ubora wa maisha na mwenendo wa Kikristo.

Hotuba iliyoandaliwa vizuri kuliko zote, yenye ufasaha kuliko zote, yaweza kuharibiwa na kufanywa isiwe na nguvu, kwa matendo ya kutiliwa shaka ya mhubiri. Mfanyakazi wa kanisa aliye hodari kuliko wote anaweza kuiona kazi ya mikono yake ikiharibiwa na roho ya kidunia na maisha yasiyo thabiti. Watu huhubiri kwa maisha yao, si kwa maneno yao, na mahubiri hutolewa, si sana ndani ya mimbari na kutoka mimbarani, bali katika hasira, matendo, na matukio elfu na moja yanayojaa katika njia ya maisha ya kila siku.

Bila shaka, ombi la toba linakubalika kwa Mungu. Yeye hupendezwa kusikia vilio vya wenye dhambi wanaotubu. Lakini toba haihusishi tu huzuni kwa ajili ya dhambi, bali kugeuka kuacha kutenda mabaya, na kujifunza kutenda mema. Toba isiyoleta badiliko katika tabia na mwenendo, ni udanganyifu mtupu, ambao haupaswi kumdanganya mtu ye yote. Ya kale sharti yapite, yote sharti yawe mapya.

Kuomba kusikoleta fikira njema na maisha mema, ni mchezo wa kuigiza. Tumeikosa kabisa kazi ya maombi ikiwa yanashindwa kuisafisha tabia na kuunyoosha mwenendo. Tumeshindwa kabisa kuufahamu uwezo wa maombi, ikiwa hayaleti kugeuzwa kabisa kwa maisha. Kwa asili ya mambo, sharti tuache kuomba, au tuache mwenendo wetu mbaya. Kuomba kwa ubaridi na kwa desturi tu kwaweza kukaa ubavu kwa ubavu na mwenendo mbaya, lakini kuomba namna hiyo, katika makadirio ya Mungu, si kuomba kamwe. Kuomba kwetu huendelea katika nguvu, kadiri tu kunavyoyanyoosha maisha. Kukua katika usafi na katika kujitoa kwa Mungu kutaleta maisha ya maombi zaidi.

Tabia ya maisha ya ndani ni sharti la maombi yenye kufaa. Kama yalivyo maisha, ndivyo yatakavyokuwa maombi. Maisha yasiyo thabiti huzuia kuomba na hubatilisha yale maombi machache tunayoweza kuomba. Siku zote, ni “kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana.” Kwa kweli, mtu anaweza kwenda mbele zaidi na kusema kwamba ni maombi ya mwenye haki peke yake yanayofaa kitu cho chote — wakati wo wote. Kuwa na jicho kwa utukufu wa Mungu; kutawaliwa na shauku ya bidii ya kumpendeza katika njia zetu zote; kuwa na mikono iliyo na shughuli katika utumishi wake; kuwa na miguu myepesi kukimbia katika njia ya amri zake — hayo huyapa maombi uzito na mvuto na nguvu, na hutupatia kusikilizwa na Mungu. Mzigo mzito wa maisha yetu mara nyingi huivunja nguvu ya kuomba kwetu, na, si mara chache, huwa kama milango ya shaba mbele ya maombi.

Kuomba sharti kutoke katika moyo uliosafishwa, na kutolewe na kusisitizwa kwa “kuinua mikono iliyotakata.” Sharti kuimarishwe na maisha yanayokusudia, bila kukoma, kumtii Mungu, kufikia kufanana na sheria ya Mungu, na kuja katika kujitiisha kwa mapenzi ya Mungu.

Isisahauliwe, kwamba, wakati maisha ni sharti la maombi, maombi pia ni sharti la kuishi maisha ya haki. Maombi huendeleza maisha ya haki, nayo ndiyo msaada mmoja mkuu wa unyofu wa moyo na wa maisha. Tunda la maombi ya kweli ni maisha mema. Kuomba humweka yeye aombaye katika kazi kuu ya “kuutimiza wokovu wake mwenyewe kwa kuogopa na kutetemeka;” humfanya ailinde hasira yake, mazungumzo yake na mwenendo wake; humfanya “aangalie sana jinsi aenendavyo, akiukomboa wakati;” humwezesha “kuenenda kama inavyostahili wito ule alioitiwa, kwa unyenyekevu wote na upole;” humpa kichocheo cha juu cha kuendelea na safari yake ya ugenini kwa uthabiti kwa “kuiepuka kila njia mbaya, na kutembea katika ile njia njema.”

Umemaliza Maombi na Tabia na Mwenendo