Sura 12 · dakika 9 za kusoma
Unyenyekevu na Kukwezwa
“Ajinyenyekeshaye atakwezwa.” Luka 14:11, 18:14.
“Jinyenyekesheni mbele za Bwana, naye atawakweza.” Yakobo 4:10.
“Basi jinyenyekesheni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake” 1 Petro 5:6.
Jana tu niliulizwa swali hili: nitawezaje kukishinda kiburi hiki? Jibu lilikuwa rahisi.
Mambo mawili yahitajika. Fanya lile Mungu asemalo ni kazi yako: jinyenyekeshe. Mtumaini yeye kufanya lile asemalo ni kazi yake: yeye atakukweza. Amri i wazi: jinyenyekeshe. Hiyo haimaanishi kwamba ni kazi yako kukishinda na kukitoa kiburi cha asili yako, na kuunda ndani yako hali ya chini ya Yesu mtakatifu. La, hii ni kazi ya Mungu. Ndiyo asili yenyewe ya kukwezwa kule, ambako kwako yeye akuinua hata kuufikia mfano halisi wa Mwana mpendwa.
Amri hiyo maana yake ni hii: tumia kila nafasi ya kujinyenyekeza mbele za Mungu na mwanadamu. Katika imani ya neema itendayo kazi ndani yako tayari, katika uhakika wa neema zaidi kwa ushindi ujao, kwa kadiri ya nuru ambayo dhamiri huimulika kila mara juu ya kiburi cha moyo na kazi zake, na ijapokuwa kushindwa na kuanguka kote, simama kwa kudumu chini ya amri isiyobadilika: jinyenyekeshe.
Pokea kwa shukrani kila kitu Mungu akiruhusucho, kutoka ndani au nje, kutoka kwa rafiki au adui, katika asili au katika neema, kikukumbushe uhitaji wako wa kunyenyekezwa na kikusaidie kuufikia. Uuhesabu unyenyekevu kuwa kweli ndio wema ulio mama wa yote, wajibu wako wa kwanza kabisa mbele za Mungu, ulinzi wa daima wa roho, na uuelekeze moyo wako kwake kama chemchemi ya baraka zote. Ahadi ni ya Kimungu na ya hakika: ajinyenyekeshaye atakwezwa (Luka 14:11). Angalia kwamba wafanya lile jambo moja Mungu alitakalo: jinyenyekeshe. Mungu atafanya lile jambo moja aliloliahidi. Atakupa neema zaidi, naye atakukweza kwa wakati wake.
Shughuli zote za Mungu na mwanadamu zina hatua mbili. Kuna wakati wa maandalizi, ambapo amri na ahadi, na uzoefu uliochanganyika wa juhudi na kutoweza, wa kushindwa na kufaulu kwa sehemu, na kutazamia kutakatifu kwa kilicho bora zaidi, huwaamsha watu, kuwazoeza, na kuwatia nidhamu kwa hatua iliyo juu zaidi. Kisha huja wakati wa kutimizwa, ambapo imani huirithi ahadi na kufurahia kile ilichokitaabikia bure mara nyingi. Sheria hii hushika kila sehemu ya maisha ya Kikristo, na kuufuatia kila wema mmoja mmoja, kwa kuwa imesimama katika asili yenyewe ya mambo. Katika yote yahusuyo ukombozi wetu, ni lazima Mungu aanzishe.
Hilo likiisha kufanywa, ndipo zamu ya mwanadamu huja. Katika juhudi ya utii na kufikia lengo, ni lazima ajifunze kujua kutoweza kwake, na katika kujikata tamaa afe kwa nafsi yake, na hivyo afanywe tayari kupokea kwa hiari na kwa ufahamu kutoka kwa Mungu ule mwisho, ukamilisho wa kile alichokubali mwanzo wake katika ujinga. Hivyo Mungu, aliyekuwa Mwanzo kabla mwanadamu hajamjua vema wala kufahamu kikamilifu kusudi lake, hutamaniwa na kukaribishwa kama Mwisho, kama Yote katika yote. Ndivyo ilivyo pia katika kuufuatia unyenyekevu.
Kwa kila Mkristo amri huja kutoka kiti cha enzi cha Mungu mwenyewe: jinyenyekeshe. Jaribio la bidii la kusikiliza na kutii litalipwa; naam, kwa ugunduzi wenye maumivu wa mambo mawili. La kwanza: kilikuwapo kina cha kiburi kiasi gani—kutokuwa tayari kujihesabu na kuhesabiwa si kitu, kujitiisha kabisa kwa Mungu—ambacho mtu hakukijua kamwe. La pili: kuna kutoweza kwa kiasi gani katika juhudi zetu zote, na katika maombi yetu yote ya msaada wa Mungu, ili kumwangamiza mnyama huyu mbaya.
Heri mtu ajifunzaye sasa kuweka tumaini lake kwa Mungu, na kudumu, ijapokuwa nguvu yote ya kiburi ndani yake, katika matendo ya kujinyenyekeza mbele za Mungu na wanadamu. Twaijua sheria ya asili ya kibinadamu: matendo huzaa mazoea, mazoea huzaa hulka, hulka hutengeneza utashi, na utashi uliotengenezwa vema ndiyo tabia.
Sivyo tofauti katika kazi ya neema. Matendo, yakirudiwa kwa kudumu, huzaa mazoea na hulka, na hivi vikiutia nguvu utashi, yeye atendaye kazi kutaka na kutenda huja kwa uweza wake mkuu na Roho wake; na kunyenyekezwa kwa moyo wenye kiburi, ambako kwako mtakatifu mwenye toba alijitupa mara nyingi mbele za Mungu, hulipwa kwa neema zaidi ya moyo mnyenyekevu, ambamo ndani yake Roho ya Yesu imeshinda, na kuileta asili mpya hata kukomaa kwake, na yeye, aliye mpole na mnyenyekevu, sasa akaa milele. Jinyenyekesheni mbele za Bwana, naye atawakweza. Nako kukwezwa huko kuko katika nini? Utukufu wa juu kabisa wa kiumbe ni kuwa chombo tu cha kupokea na kufurahia na kuudhihirisha utukufu wa Mungu.
Chaweza kufanya hivi tu kikiwa tayari kuwa si kitu, ili Mungu awe yote. Maji hujaza mahali palipo chini kwanza. Kadiri mtu alalavyo chini na mtupu zaidi mbele za Mungu, ndivyo utiririko wa utukufu wa Kimungu utakavyokuwa wepesi na uliojaa zaidi. Kukwezwa Mungu akuahidiko si, wala hakiwezi kuwa, kitu cho chote cha nje kilicho mbali naye: yote aliyo nayo au awezayo kutoa ni yeye mwenyewe zaidi tu, akitwaa milki iliyo kamili zaidi. Kukwezwa huko si, kama tuzo la kidunia, jambo la kuchagua tu, lisilo na uhusiano wa lazima na mwenendo ulipwao. La; bali katika asili yake ni tokeo na matunda ya kujinyenyekeza kwetu. Si kitu ila kipawa cha unyenyekevu wa Kimungu ukaao ndani, kufanana namna hiyo na kuumiliki unyenyekevu wa Mwana-Kondoo wa Mungu, kunakotufanya tufae kuupokea kikamilifu ukaaji wa Mungu ndani yetu.
Ajinyenyekeshaye atakwezwa. Kwa habari ya ukweli wa maneno haya, Yesu mwenyewe ndiye uthibitisho; na kwa habari ya hakika ya kutimizwa kwake kwetu, yeye ndiye amana yake. Na tujitie nira yake na kujifunza kwake, kwa kuwa yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo. Kama tuko tayari kuinama mbele zake, kama yeye alivyoinama kwetu, ataendelea kuinama kwa kila mmoja wetu tena, nasi tutajikuta hatujafungwa naye katika nira isiyolingana.
Tuingiapo kwa kina zaidi katika ushirika wa kunyenyekezwa kwake, tukijinyenyekeza sisi wenyewe au tukistahimili kunyenyekezwa na wanadamu, twaweza kutegemea kwamba Roho ya kukwezwa kwake, “Roho wa utukufu na wa Mungu,” atatukalia juu yetu. Uwepo na nguvu ya Kristo aliyetukuzwa vitawajia wale walio na roho ya unyenyekevu.
Mungu atakapopata tena mahali pake pa haki ndani yetu, atatuinua. Utukufu wake na uwe jukumu lako katika kujinyenyekeza kwako. Yeye atafanya utukufu wako kuwa jukumu lake katika kuukamilisha unyenyekevu wako, na kukupulizia, uwe uzima wako udumuo, Roho yenyewe ya Mwana wake. Uzima wa Mungu uenezao yote ukikumiliki, hakutakuwa na kitu cha asili zaidi, wala kitamu zaidi, kuliko kuwa si kitu, pasipo wazo wala shauku ya nafsi, kwa kuwa yote yameshughulishwa naye ajazaye yote. “Basi kwa furaha nitajisifu zaidi katika udhaifu wangu, ili nguvu za Kristo zinikalie.”
Ndugu, je, hapa hatuna sababu ya kujitoa kwetu na imani yetu kufaa kidogo hivyo katika kuufuatia utakatifu? Ilikuwa kwa nafsi na nguvu yake kazi ilifanywa chini ya jina la imani; ilikuwa kwa ajili ya nafsi na furaha yake Mungu aliitwa; ilikuwa, bila kujua lakini kwa kweli, katika nafsi na utakatifu wake roho ilifurahi. Hatukujua kamwe kwamba unyenyekevu—kamili, udumuo, ulio kama wa Kristo, na kujifuta nafsi—ukienea na kutia alama maisha yetu yote na Mungu na mwanadamu, ndicho kilikuwa kipengele cha lazima kuliko vyote cha utakatifu tuliokuwa tukiutafuta.
Ni katika kumiliki Mungu peke yake ndipo najipoteza mimi mwenyewe. Kama vile ni katika urefu na upana na utukufu wa jua ndipo udogo wa kichembe kichezacho katika miali yake huonekana, vivyo hivyo unyenyekevu ni kuichukua nafasi yetu katika uwepo wa Mungu ili tusiwe kitu ila kichembe kikaacho katika mwanga wa jua wa upendo wake. Yeye atuambia: “Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu, na kuihuisha mioyo ya waliotubu.” Isaya 57:15.
Hili na liwe fungu letu! “Ee, kuwa mtupu zaidi, mnyonge zaidi, Duni, nisiyeonwa, nisiyejulikana, Na kwa Mungu chombo kitakatifu zaidi, Kijazwacho Kristo, Kristo peke yake!”
MAELEZO D Siri ya Siri: Unyenyekevu ndiyo Roho ya Maombi ya Kweli Hata roho ya moyo itakapofanywa upya, itakapomwagwa tamaa zote za kidunia, na kusimama katika njaa na kiu ya kudumu ya kumtafuta Mungu, ambayo ndiyo roho ya kweli ya maombi—hata hapo, maombi yetu yote yatakuwa, kwa kiasi fulani, kama masomo apewayo mwanafunzi; nasi tutayasema kwa sehemu kubwa kwa kuwa tu hatuthubutu kuyapuuza. Lakini usikate tamaa; pokea shauri lifuatalo, ndipo waweza kwenda kanisani bila hatari yo yote ya kazi ya midomo tu au ya unafiki, ijapokuwa pawe na wimbo au ombi ambalo lugha yake i juu kuliko moyo wako. Fanya hivi: nenda kanisani kama yule mtoza ushuru alivyokwenda hekaluni; simama kwa ndani, katika roho ya nia yako, katika hali ile aliyoionyesha kwa nje alipoinamisha macho yake, asiweze kusema ila, “Ee Mungu, uniwie radhi.” Simama bila kubadilika, angalau katika shauku yako, katika hali hii ya moyo; itaitakasa kila dua itokayo kinywani mwako; na kitu cho chote kisomwapo au kuimbwa au kuombwa kilicho juu kuliko moyo wako, ukilifanya hili kuwa nafasi ya kuzama chini zaidi katika roho ya yule mtoza ushuru, ndipo utasaidiwa na kubarikiwa sana na maombi na sifa zile zionekanazo kuwa za moyo ulio bora kuliko wako.
Hii, rafiki yangu, ni siri ya siri; itakusaidia kuvuna usipopanda, nayo itakuwa chemchemi ya daima ya neema rohoni mwako; kwa maana kila kitu kikusukumacho kwa ndani, au kikupatacho kwa nje, huwa jema halisi kwako, kikikuta au kikiamsha ndani yako hali hii ya nia ya unyenyekevu.
Kwa maana hakuna kilicho bure, wala kisicho na faida, kwa roho mnyenyekevu; husimama sikuzote katika hali ya ukuaji wa Kimungu; kila kiiangukiacho ni kama umande wa mbinguni kwake. Basi, jifungie ndani ya hali hii ya Unyenyekevu; kila jema limefungwa ndani yake; ni maji ya mbinguni yaugeuzayo moto wa roho iliyoanguka kuwa upole wa uzima wa Kimungu, nayo huumba mafuta yale ambayo kwayo upendo kwa Mungu na mwanadamu hupata mwali wake.
Basi, funikwa ndani yake sikuzote; na uwe kama vazi ufunikwalo nalo daima, na mshipi ufungwao nao; usipumue ila ndani ya na kutoka katika roho yake; usione ila kwa macho yake; usisikie ila kwa masikio yake. Uwe kanisani au nje ya kanisa, ukisikia sifa za Mungu au ukipokea maovu kutoka kwa wanadamu na ulimwengu, yote yatakuwa ni kujengwa, na kila kitu kitausaidia mbele ukuaji wako katika uzima wa Mungu (The Spirit of Prayer, Pt II, uk.
121).
OMBI KWA AJILI YA UNYENYEKEVU Nitakupa hapa kigezo kisichokosea kitakachojaribu yote hata kweli. Ni hiki: jitenge na ulimwengu na mazungumzo yote, kwa mwezi mmoja tu; usiandike, usisome, wala usibishane na nafsi yako juu ya jambo lo lote; komesha kazi zote za awali za moyo na akili yako; na, kwa nguvu zote za moyo wako, simama mwezi huu wote, kadiri uwezavyo kwa kudumu, katika namna ifuatayo ya kuomba kwa Mungu. Litoe mara kwa mara ukiwa magotini; lakini uwe umekaa, unatembea, au umesimama, uwe sikuzote ukitamani kwa ndani na kuliomba kwa bidii ombi hili moja: “Kwamba kwa wema wake mkuu angekujulisha, na kuondoa moyoni mwako, kila namna na sura na kiwango cha kiburi, kiwe kimetoka kwa pepo wabaya au asili yako iliyoharibika; na kwamba angeamsha ndani yako kina kirefu kabisa na kweli ya unyenyekevu ule uwezao kukufanya uifae nuru yake na Roho wake Mtakatifu.” Kataa kila wazo, ila la kungoja na kuomba katika jambo hili kutoka chini ya moyo wako, kwa kweli na bidii kama ya watu walio katika mateso watakavyo kuomba wakaokolewa nayo. Kama waweza na wataka kujitoa kwa kweli na unyofu kwa roho hii ya maombi, nathubutu kusema kwamba, hata kama ungekuwa na pepo wabaya mara mbili ya wale aliokuwa nao Mariamu Magdalene, wote watatolewa ndani yako, nawe utalazimika pamoja naye kulia machozi ya upendo miguuni pa Yesu mtakatifu. The Spirit of Prayer, Pt.
2, uk. 124.